Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

TUZO CHALLENGE

   


MTUNZI : WAANDISHI


“KESHANIHARIBIA maisha yangu,” Eva alisema angali amejiinamia.

“Kwani imekuwaje?” Rumi aliuliza.

Eva Mazengo alikuwa amejiinamia kwa muda mrefu. Si kujiinamia tu, bali pia, kutokwa machozi. Hakuwa na muda wa kuyafuta. Wala, hakuwaza kufanya hivyo. Kwake, yalikuwa kitu kidogo ukilinganisha na maumivu aliyokuwa nayo. Maumivu yaliyoambatana na kukata tamaa.

Rumi Dago alimtazama Eva kwa macho ya maswali. Tangu kuingia kwake ndani ya ukumbi wa semina, hakuwa amefanikiwa kumfanya Eva kumweleza kinagaubaga sababu ya kulia kwake. Hakuwa amejua uwepo wa Eva ukumbini humo. Alimtafuta kwa rununu yake pasina mafanikio. Alimpigia na kumtumia ujumbe mara kadhaa. Kwa kuwa walikuwa bado chuoni, aliwaza amtafute ukumbini humo, ama maktaba.

Eva ana nini kwani?

Swali hili lilikizonga kichwa cha Rumi tangu alipoutia mguu wake ndani ya ukumbi huo. Eva aliketi nyuma kabisa. Rumi alitembea haraka kuzipandisha ngazi katikati ya viti vilivyopangwa kama ukumbi wa sinema. Alihema juujuu huku mkono mmoja ukivibaraza viti vya mbao laini vilivyopangwa na kufungwa kwa ustadi.

“Niambie shida ni nini mpenzi wangu?” Rumi aliuliza huku akimpetipeti Eva mgongoni.

Mkono wa Rumi mgongoni kwake ulimsisimua. Ukampa afua dhidi ya maumivu aliyokuwa nayo. Ndiposa, akauinua uso wake na kumtazama Rumi. 

Rumi aliyatazama macho mekundu ya Eva akiwa na mchanganyiko wa maumivu na huruma. Maumivu ya nini sasa? Hata mwenyewe hakuwa na jibu maana hakufahamu kilichomzonga Eva. Huruma je? Ilikuwa juu ya ile hali aliyomkuta nayo.

“Ona mwenyewe,” Eva alisema huku akimpa Rumi rununu yake. Aliweka kidole chake cha shahada juu ya kioo. Mwanga ukajitokeza. Macho ya Rumi yalitekwa nadhari na nembo ya Chuo Kikuu cha Mzizima. Maandishi yalitokeza vema. Hata ufupisho wa jina la chuo, CHUKIM ulionekana uzuri kabisa.

Eva alipandisha juu maandishi kwenye kioo cha rununu yake. Alipofikia mahali alipotaka Rumi apaone, aliacha kupapasa. Macho yake yalizingatia kilichokuwepo. Ikamfanya, Rumi pia kuzingatia.

“Haiwezekani!” Rumi alisema kwa sauti iliyochanganyika mshangao na hasira. 

“Dokta kanifanyia hivi mimi kweli?” Eva aliuliza. Pengine, siyo swali. Bali, maelezo.

“Yule mzee mshenzi hivi kumbe!” 

Eva akadakia, “Bora angekuwa mshenzi, mwanaizaya kabisa!”

“Daah!”

“Hebu niambie mpenzi wangu,” Eva alisema akimtazama Rumi aliyeonesha kuwaza mbali. “Mimi nitafanyaje lakini?”

Badala ya kujibu, Rumi aliichukua rununu ya Eva. Akamwonesha ishara aingize msimbo kuifungua. Eva alifanya hivyo. Ukurasa uleule wa chuo ulionekana.

“Lakini, hili somo si unalijua?”

“Shangaa wewe, mpenzi wangu.”

“Sasa kwa nini kakufanyia hivi?” Rumi aliuliza.

Eva akajibu kwa swali, “Kwa nini kanifanyia hivi?”

“Aah, najua sababu. Ila, sikuwa nimewaza mzee yule anaweza kuamua kukuharibia binti mdogo kama wewe.”

“Kashika mpini, mie nimeshika makali,” Eva alisema kwa kulalama. Kitu chenye ncha kali kilimchomachoma moyoni. Alihisi kutetemeka na kuishiwa Nguvu.

“Zile texts zake si bado unazo? Nilisema usizifute.”

“Sasa si nilibadili simu nilipoibiwa ile nyingine.”

“Najua.”

Eva alimtazama Rumi. Hakutia neno.

Rumi akalitia, “Wazee kama hawa na wachawi wote halimoja.”

“Ujana wake alikula na nani hata ataka uzee wake ale na mimi? Wasichana wangapi amewafelisha kwa sababu wamemkataa? Hivi binti yake akifanyiwa alivyonifanyia atajisikiaje? Ipo siku Mungu atanilipia,” Eva alisema.

“Badala ya kukaa chini na kusema ipo siku Mungu atakulipia, unapaswa usimame imara na kuipigania haki yako. Mwenyezi Mungu ametujaalia uwezo wa kupambana,” Rumi alisema akimtazama Eva usoni.

“Mungu atanilipia. Karma is real.”

Rumi akadakia, “Hata kama. Mungu angetaka kila kitu tumwachie yeye, asingetujaalia uwezo wa kupambana na mazingira yetu. Huyo mzee kamwaga mboga, sasa ni zamu yako kumwaga ugali na kuzima moto kabisa.”

“Unamaanisha nini?”

“Ushahidi upo kuwa alikuwa anakutaka,” Rumi alijibu.

“Mie sitaki matatizo na mtu, mpenzi wangu.”

“Ila unataka kuendelea kufeli kwa sababu tu ya baradhuli mmoja?”

“Acha tu, honey. Mwezi Septemba siyo mbali. Nitafanya tu sup.”

“Vipi kwenye sup usipotoboa. Unataka kucarry hiyo course? Or, do you wanna compromise?”

“Kwa nini unasema nataka kucompromise?” Eva aliuliza kwa utulivu.

“Nataka kujua. Unadhani hatokusumbua tena kabla ya wewe kufanya sup? Unadhani ukifanya, utatoboa kama hujampa unachokitaka?” Rumi aliuliza.

“Labda atanionea huruma,” Eva alisema.

“Hatuishi kwa kutaka kuonewa huruma. Haya ni maisha, mpenzi wangu. Tunaishi kwa kupambana.”

“Siyo kila kitu mtu unahitaji kupambania.”

“Unakwama, mpenzi wangu,” Rumi alisema kwa tuo. “Kila kitu ni kupambana. Kwenye maisha, you don’t get what you deserve, but what you’re capable to bargain. Na kama hujui, how you bargain is a battle.”

“Hata sijakuelewa,” Eva alisema.

“Inategemea  unasikiliza kwa madhumuni gani,” Rumi alisema. “Ukinisikiliza ili unielewe utanielewa. Ukinisikiliza ili unijibu hutonielewa kamwe.”

“Mbona sasa unakuwa kama mkali?” 

“Kuna wakati unahitaji kuuona uso wangu mkavu. You’re my girlfriend. Wewe ni msichana ninayekupenda sana. Kwa moyo na akili. Sipo tayari kumwona yule bwege akikuharibia maisha yako kwa sababu tu ya tamaa zake za ngono. Haya ni mapambano. Nataka kukuona ukipambana. Nataka kukuona ukishinda.”

“Ni sawa,” Eva alisema. “Lakini, mimi sitaki tena makubwa na Dokta…”

Rumi akamkatisha, “Kwamba, unataka kumkubalia eeeh?”

“Aaah jamani, huko umefika mbali sana.”

“Nirudishe wewe karibu,” Rumi alisema kwa sauti isiyo na chembe ya masihara.

“Nisamehe kama nimekukwaza,” Eva alisema taratibu. “Unajua hili jambo linaniumiza sana.”

“Najua linakuumiza. Ulipoyaona matokeo umewasiliana na huyo mwalimu wako?”

“Hapana,” Eva alijibu. “Mimi nd’o mwenye shida. Ngoja nimpigie nimsikilize.”

Rumi hakutia neno. Alimrudishia Eva rununu yake. Akatulia akimtazama anavyoitafuta namba ya Dokta Tindo Masanga.

“Weka loudspeaker,” Rumi alisema akimtazama Eva aliyekuwa na rununu sikioni kwake.

Eva akairudisha simu mkononi na kuweka sauti.

“Habari yako?” Sauti nzito ilisikika kutoka upande wa pili.

“Salama. Shikamoo, Dokta.”

Salamu haikujibiwa. Bali, swali. “Una shida gani?”

“Dokta…” Eva alisita. Alimtazama Rumi ambaye nadhari yake ilikuwa kwenye mazungumzo.

“Unasemaje?” Dokta Masanga aliuliza kufuatia ukimya wa Eva.

“Nimefeli somo lako.”

“Cha ajabu ni nini sasa? Ulitegemea kufaulu eeh?”

Eva alikosa jibu.

Dokta Masanga akaendelea, “Ni jambo la kawaida kwa mwanafunzi mwenye kiburi na jeuri kama wewe. Kufaulu shule hakuishii darasani. Ni mkusanyiko wa mambo mengi.”

“Naomba nisaidie, Dokta.”

“Jisaidie kwanza mwenyewe.” 

Eva alikosa jibu.

“Shauri yako. Ni maisha yako mwenyewe hata hivyo.”

“Dokta, nimefeli somo lako,” Eva alisema.

“Umeshasema. By the way, hata mimi najua. You don’t need to remind me.”

Rumi alimtazama Eva huku masikio yake yakizingatia mazungumzo simuni. Eva alikifungua kinywa chake, hata maneno yasimtoke.

Ukimya wake ukavunjwa na Dokta Masanga. “Ulidhani kufaulu somo langu ni kazi rahisi eeh? Elimu ni kitu aghali sana.”

“Naelewa hivyo, Dokta.”

“Bado hujaelewa. Ukielewa utajua cha kufanya. Fikiria vizuri kabla haijawa too late to catch the train.”

Rumi alimpa ishara Eva akubali.

Akakubali, “Sawa.”

“Unajua jinsi ya kunipata. Utanipigia.”

“Sawa.”

Simu ikakatwa.

“Imekula kwake huyu bwege,” Rumi alisema akimtazama Eva aliyeonesha kuwaza mbali.

Vuta n’kuvute ya Eva na Dokta Tindo Masanga ilianza tangu mwanzoni mwa semista. Ndiyo kwanza Eva alikuwa ameingia mwaka wa pili akisoma shahada ya Sosholojia. Eva hakuwa na mazowea na mwalimu huyo wa somo la Takwimu. Alikutana naye tu darasani wakati wa kipindi. Wala, hakuwa na wazo lolote kuwa Dokta Masanga anamzingatia.

Siku moja, ikiwa ni mwezi wa pili wa semista, wanafunzi walitakiwa kufanya uwasilishaji wa swali kupitia makundi yao. Eva na wenzake wanne waliunda kundi namba nne. Hivyo, ilipowadia zamu yao, walikwenda mbele kuwasilisha.

Wakati wote wakiwa pale mbele, Dokta Masanga alimtazama Eva. Nyakati kadhaa, waligongana macho. Macho ya Dokta Masanga yalimtisha. Kila alipomtazama mwalimu huyu aliyesifika kwa kukamata wanafunzi wake wake kwenye mtihani wa kumaliza semista, ndivyo Eva alivyoupoteza uchangamfu wake.

“Hili swali hamjalifanya vizuri kama nilivyotaka,” Dokta Masanga aliwaambia mara tu walipomaliza uwasilishaji. “Shida yenu wanafunzi, hamji ofisini kwa walimu wenu kupata ushauri wa kitaaluma.”

Darasa lilikuwa kimya. Utulivu ulichangiwa na mambo mawili. Ugumu wa somo, na vilevile, ukali wa mwalimu huyo.

“Wanafunzi wa siku hizi mna shida sana. Badala ya kuwa mnakuja ili msaidiwe, mnajifanya mnajua sana kutumia Google. Mtafeli sana mkiendekeza huo ujinga.”

Darasa lilibaki tuli likimsikiliza.

Uwanja ukaendelea kuwa wake. “Group Number 4, mje ofisini kwangu mmojammoja. Sitaki msongamano.”

Kundi la akina Eva waliitikia kwa kutingisha kichwa.

Eva alikuwa mtu wa pili kwenda ofisini kwa mwalimu. Ilikuwa mara yake ya kwanza kuingia ofisini kwa mwalimu yeyote tangu aanze chuo. Alizipandisha ngazi kuelekea ghorofa ya pili ya jengo la Idara ya Sosholojia. Mwendo wake wa wastani haukumzuia kuhema kwa nguvu akizipandisha ngazi hizo. 

Pilika za wanafunzi na walimu hazikuwa haba. Hakuwa na muda wa kumzingatia yeyote. Akili yake ilikuwa juu ya nini mwalimu wao angemwambia. Suala la kuwa hawakufanya uwasilishaji mzuri lilikigonga kichwa chake. 

“Ingia.” Sauti nzito ya Dokta Masanga ilisikika kutoka ndani Eva alipogonga mlango.

Eva aliutazama mlango kabla ya kuufungua. Maandishi yaliyonakshiwa yalilinadi jina la mwalimu huyo.

“Wewe nd’o unayeitwa nani?” Ilikuwa salamu ya Dokta Masanga pale Eva alipoingia ofisini kwake.

“Naitwa Eva Mazengo.”

“Hii ni second year, na bado hampo serious na shule?”

“Hapana, Dokta.”

“Unaishi campus ama off campus?”

“Naishi campus.”

“Which block?”

“Block A.”

“Good,” Dokta Masanga alisema. Akayapotezea machoye kwenye karatasi juu ya meza kabla ya kuibuka na swali jingine. “How do you spend your weekend?”

“Huwa nawatembelea wazazi wangu.”

“Unawatembelea every weekend? That’s too much.”

“Hapana, siyo kila weekend,” Eva alijibu. “Mara mojamoja tu kama ratiba ya kusoma haijanibana.”

“Good.”

Ukimya mfupi ukatawala. Eva alikuwa angali wima, ilhali Dokta Masanga akiikodolea karatasi.

Kisha, akauinua uso wake na kumtazama Eva. “Sasa, nataka kukutana nawe on Saturday mchana.”

“Sawa, Dokta,” Eva alijibu. “Utakuwepo ofisini saa ngapi nije?”

“Siyo ofisini. What do you like?”

Eva alikosa jibu. Anapenda nini? Hakujua anapenda nini katika muktadha huo.

“Nyamachoma ama drinks?” Dokta Masanga aliuliza.

Eva akapata mwanga. “Hapana, ahsante.”

Uso wa Dokta Masanga ulibadilika. “Hapana nini?”

Woga ukamwingia Eva kidogo. Akakosa jibu.

“Hujui unapenda nini?”

Eva hakujibu.

“Nipe namba yako.”

Eva akaitaja.

“Kwa hiyo,” Dokta Masanga alisema. “Nitakupigia nikwambie tuonane wapi.”

“Sawa,” Eva alijibu. Hiyo sawa aliitoa ili kufunga mjadala.

Hadi anaondoka ofisini kwa mwalimu, hakukufanyika mazungumzo yoyote juu ya uwasilishaji wao darasani. Hakuhitaji kuwa na shahada ya uzamivu kuelewa nini azma ya mwalimu wake. 

“Siwezi kufanya huo ujinga,” Eva aliongea kwa sauti kana kwamba anamwambia mtu wakati akishuka ngazi. Akili yake ilivurugwa na hasira zilizompata.

“Dokta anakutaka huyo,” Rumi alimwambia Eva walipokutana kwenye mgahawa wa chuo kwa ajili ya chakula.

Eva alimsimulia Rumi juu ya mazungumzo yake na Dokta Masanga.

“Kuwa mwangalifu sana,” Rumi alisema.

“Mimi siwezi kukutana naye. Kwanza ikifika hiyo Jumamosi nitazima simu yangu nije kuiwasha Jumatatu asubuhi.”

“Atajua umemfanyia makusudi. Atakuundia zengwe ufeli.”

“Sasa mimi nifanyeje?”

“Nakushauri ukutane naye hiyo Jumamosi tuone anataka kufanya nini.”

“We’ Rumi wewe,” Eva alisema. “Yaani kabisa unamwambia mpenzi wako aende kwenye domo la mamba?”

“Kama ninamwamini mpenzi wangu kuwa hatetereshwi msimamo wake. I want you to play smart.”

“Aaah wapi, mi sitaki kukutana naye.”

“Mimi ninakushauri tu. Mwalimu mwenyewe anakufundisha semista moja. Baada ya miezi miwili tu kutoka sasa, umemalizana naye. Kama mimi ulinizungusha karibia mwaka nd’o ukanikubali, unashindwa nini kumpotezea muda kijanja ili semista iishe?” Rumi aliuliza.

“Ni sawa unav’osema. Ila kusema ukweli, mimi sitaki kukutana naye.”

Kama alivyomwambia mpenzi wake, Eva alikwepa kukutana na Dokta Masanga. Alianza kwa kuzima rununu yake Jumamosi asubuhi. Alikuja kuiwasha Jumapili usiku. Alikutana na ujumbe kuwa kuna namba ilimtafuta mara sita.

Namba hiyohiyo, ikamtumia ujumbe mfupi wa maandishi.

Habari yako Eva? Mbona sikupati kwenye simu? Ukipata text yangu call me. Dr.

Hakuwa na mpango wa kumjibu wala kumpigia.

Kipindi kingine cha Takwimu kilikuwa siku ya Jumanne. Eva aliwahi kwenye ukumbi wa semina. Akaketi nyuma kabisa, sambamba na rafikiye mkubwa, Zena Masamba.

“Sasa akikuuliza kwa nini ulizima simu utamwambiaje?” Zena alimwuliza.

“Jibu nitalipata hapohapo.”

“Jamani eeh.” Sauti ya kiongozi wa darasa ilisikika. Utulivu ukatawala. “Dokta Masanga amesema leo haji. Ameacha individual assignment. Inatakiwa kukusanywa kwenye kipindi chake cha Alhamisi.” 

“Afadhali haji,” Eva alisema.

“Bahati…” 

Zena alikatishwa na mwanafunzi mbele yake aliyemwuliza kiongozi wa darasa, “Eti CR, mbona Alhamisi ni keshokutwa tu, kwa nini tusipewe muda zaidi?”

Akajibiwa, “Amesema ni swali rahisi hivyo ni Alhamisi na hakuna mjadala.”

Wakati zogo likiendelea ukumbini humo, Eva aliunyanyua mkoba wake, akamshika mkono Zena. Wakatoka wameshikana mikono.

“Eva…” Sauti ilisikika nyuma yake akiwa anaingia mlango wa maktaba ya chuo.

Nguvu zilimwishia alipogeuka nyuma na kukutana uso kwa uso na Dokta Masanga. Si tu hakutarajia kukutana naye maeneo hayo, bali pia, hakujiandaa kukabiliana naye.

“Kwa nini ulinizimia simu?”

Eva alibabaika.

“Umefaidika nini sasa?”

Akajitutumua kujibu, “Sikuzima. Simu yangu ilipotea.”

“Lakini text yangu imekuwa delivered Jumapili usiku.”

Walau sasa, akili ya Eva ilifanya kazi haraka. “Nilirenew line yangu Jumapili jioni.”

“Sawa. Tuonane the coming weekend. I’ll call you.”

Dokta Masanga akaenda zake kabla Eva hajajibu.

Eva na Dokta Masanga ikawa mtafutano na mkwepano. Kila Dokta Masanga alipotaka kukutana na Eva, Eva alikataa. Na pale alipokubali, ilikuwa ahadi hewa.

“Unaniona mimi mjinga sana, eeh?” Dokta Masanga alimwuliza Eva siku moja.

“Hapana. Siyo hivyo.”

“Ila?”

“Mimi sipo tayari kutoka na wewe,” Eva aliweka bayana.

“Kunifanya mtu mzima mimi kuumizwa kichwa na mtoto wewe ni dharau ya kiwango cha juu sana,” Dokta Masanga aliongea kwa hasira.

‘Sasa si uache kunisumbua ili usiumizwe kichwa?’ Eva aliwaza.

“Unadhani wewe upo smart sana?” Dokta alimwuliza.

“Hapana.”

“Basi, siku moja tutaheshimiana.”

Suala la Dokta Masanga kuwafelisha wasichana wanaomgomea hitaji lake, sasa lilikuwa la kawaida kichwani mwa Eva. Katika kipindi hiki tangu aanze kuwaruana na Dokta Masanga, ndipo aliposikia simulizi nyingi kwa wanafunzi wenzake wa kike.

“Nasikia ana tabia ya kumkamata mtu kwenye UE,” Eva alimwambia Rumi.

Rumi akamjibu, “Kutishana tu huku ili atimize haja yake. Cha muhimu wewe piga msuli mnene. Likija paper lake hakikisha unalichana kama huna akili nzuri. Atakosa pa kukukamatia.”

Hatimaye, amekamatwa.

“Mi’ nakwambia mpenzi wangu, imekula kwake,” Rumi alisema. Walikuwa bado ndani ya ukumbi wa semina. Walau, Eva hakuwa akitokwa tena na machozi.

“Inaonekana anataka kunikamata tena nitakapofanya sup.”

Rumi aliafikiana naye. “Na ndiyo lengo lake hasa. Unaona alivyokwambia kwenye simu, anataka usalimu amri.”

“Mimi sitaki kusalimu amri kwake,” Eva alisema.

“Labda nikuulize,” Rumi alisema. “Utakuwa tayari nikitaka kumshikisha adabu?”

“Mimi naogopa mpenzi wangu,” Eva alijibu. “Kwa nini usiniache nifanye tu hiyo sup yake. Akinifelisha tena potelea mbali. Kufeli shule siyo kufeli maisha. Utu wangu una thamani kubwa kuliko degree ya kuchojolewa.”

“Utu wako una thamani ndiyo. Pamoja na yote hayo, kumbuka kuna wasichana wengi ni wahanga wa mshenzi yule. Panahitajika msichana mmoja jasiri kubutua ili kuwaokoa wasichana wenzake. Msichana huyo ni wewe hapo. Mimi nipo tayari kukupa ushirikiano wote ili kufanikisha,” Rumi alisema.

“Wewe unashauri nifanyeje?”

“Kitu pekee tunachoweza kufanya sasa,” Rumi alisema. “Ni kwa wewe kukubali kukutana naye. Halafu, from there tutajua mwelekeo ni upi. Sawasawa?”

“Ila mimi naogopa sana.”

“Woga wako ndiyo utumwa wako. Nataka uuvae ujasiri na kuushinda huo woga wako. Kwenye maisha yako, huwezi kufanikiwa kama utaendekeza woga.”

“Lakini, usisahau kuwa, kunguru mwoga huukimbiza ubawa wake na kuishi maisha marefu,” Eva alisema.

“Achana na falsafa hizo cha kutubembabemba tuendelee kuwa waoga. Nataka kuset plan ya kumtia mtengoni huyo bwege. Plan yangu itafanya kazi kama wewe utakuwa tayari.”

“Sasa si inategemea aina ya plan ili nijue kama nitakuwa tayari ama la.”

“Aina ya plan inategemea kama utakuwa tayari.”

“Kama nikikubali, itakuwaje?”

“Ndiyo nakwambia sasa.”

“Na kama nitakataa?”

“Sitokuwa na la kufanya. Zaidi, nitajiuliza juu ya nafasi yangu kwako. Nitajiuliza kama mimi ninaweza kukushauri jambo kwa nia njema na ukashaurika?”

“Hapo unanimanipulate, mpenzi wangu,” Eva alisema.

“Vyovyote unavyoweza kuita, ninachotaka ni wewe kuwa tayari.”

“Niambie sasa unaplan kufanya nini?”

“Naomba utulie kwanza. Ninahitaji kupata muda wa kutosha wa kupanga na kupangua. It’s a trial and error,” Rumi alisema.

Eva akadakia, “Sawa, tulia kisha uniambie. Ila, ukumbuke kuwa wewe ni mpenzi wangu. Ni wajibu wako kunishauri vizuri. Ingawa, ni haki yangu kukataa ushauri wowote ninaoona hautonisaidia.”

“Huu utakusaidia,” Rumi alisema. “Tena, hautokusaidia wewe peke yako tu. Utawasaidia wasichana wengi wanaonaswa kinyonge kwenye mawindo ya walimu mabazazi kama Dokta Masanga.”

“Mama yangu atanichamba sana nikimwambia nimepata sup.”

“Mama anapaswa kuelewa juu ya vita unavyopambana navyo kama mwanafunzi wa kike hapa chuoni.”

“Kuna walimu wana mambo ya ajabu sana utadhani wao hawana watoto.”

“Hakuna haja ya kulalamika,” Rumi alisema. “Sasa ni wasaa mahsusi wa mapambano.”

“Sawa.”

“Sasa,” Rumi alisema. “Wewe rudi ukapumzike. Twende nikusindikize. Kisha, mimi ninakwenda kutazama mpira baadaye kidogo. Leo nitatumia muda mwingi kuwaza namna ya kumtia adabu huyu bwege.”

“Unayemwita bwege ujue ni mwalimu.”

“Ni mwalimu ndiyo, lakini siyo mwalimu wangu. Mimi nisingependa kufundishwa na mwalimu mkora kama Dokta Masanga.”

Wakaondoka ukumbini hapo wakiwa wameshikana mikono.



Siku mbili baadaye, Eva alitoka chumbani tayari kuianza safari. Alivalia fulana ya rangi ya pinki, aliyokuwa ameichomekea kwenye sketi nyeupe, iliyoishia juu ya magoti. Miguuni alivaa raba nyeusi zenye soli nyeupe na nembo ya njano, zilizochochea mvuto wa miguu yake minene na myeupe. Mawazo yaliendelea kuutafuna ubongo wake. Bado hakuwa na hakika kama anachokwenda kukifanya ni sahihi au ni nakama kwa mustawa wa maisha yake. Alijihisi mfano wa mbuzi aliyefungwa kamba shingoni na kufuata mwelekeo wa mchungaji.

Alipotoka nje ya jengo analoishi, Block A, jua lilimpokea. Akafungua pochi yake ndogo na kuchomoa miwani ya jua na kuipachika usoni. Miwani myeusi juu ya uso mweupe ilimzidisha ung’avu. Kama vile hakuna kinachomzonga kichwani, alitembea taratibu kwa kuifuata njia inayoelekea barabara kuu, nje ya eneo la chuo. Walakini, kabla hajafika mbali, alisikia akiitwa jina kwa sauti ya juu. Alipogeuka, kwa mbali alikutanisha macho na Zena Masamba, aliyekuwa amesimama akianika nguo kwenye kamba, mkabala na jengo alilotokea.

“Wapi tena na jua lote hili?” Zena alisaili baada ya Eva kumkariba, huku akivuta kiti na kuketi mbele ya ndoo ya kufulia.

“Kwanza, imekuaje uko hapa muda huu?” Eva alirudisha swali. “Maana ulisema kuwa jana na leo ungelala kwa Faraji?”

Zena aliketi. Kisha, akavuta ndoo iliyokuwa na nguo. Akaendelea kufua huku akitikisa kichwa. “Mwenzangu, si unajua tena kazi za Faraji. Jana nilipofika tu, akapokea simu akitakiwa ajiandae kwa safari muda huohuo. Akasepa na kuniacha doro. Nikaona aheri nirudi zangu walau nifanye usafi. Enhee, unaendeleaje na Dokta Masanga?”

Eva na Zena walikutana kwa mara ya kwanza, wakiwa mwaka wa kwanza chuoni hapo. Ikatokea tu kwa mshabaha wa mazungumzo yao, wakashikana urafiki. Muda wote wakawa pamoja mithili ya ulimi na mate. Walishirikiana na kutegemeana katika kadha wa kadhalika mfano wa uta na upote. Hata kadhia nzito kama vitimbi vya Dokta Masanga, Eva alianza kumsimulia Zena kabla hata ya kumfikishia Rumi.

“Mwenzangu,” Eva alijibu na kuachia ucheko hafifu. Akavuta ndoo ndogo ya maji na kukalia. “Ndiye huyo anayenifanya niingie barabarani na jua lote hili.”

“Amekuita?”

“Bora hata angeniita,” Eva alijibu, huku akiinua mkono wake kutazama saa. “Rumi ameinunua kesi.”

Zena alikunja uso na kutengeneza mfano wa matuta katika paji la uso wake. “Kivipi?”

“Ameifikisha kesi TAKUKURU. Na sasa, mpango ni kumtia nguvuni Dokta Masanga.”

“Mungu wangu,” Zena alisema na kujitwisha mikono kichwani. “Eva, mbona mmefika mbali sana? Kwa nini hata usingeanzia kwa Dean?” 

“Mimi pia nilifikiria hivyo. Lakini Rumi akasema kesi za namna hiyo ukiwashirikisha hao ma-dean, huharibu ushahidi kwa kuwatonya wenzao, na kisha kibao kinageuka. Kila nilivyojaribu kumwonesha kuwa siko tayari kwenda TAKUKURU, alinijia juu sana, akinituhumu kuwa nina mpango wa kumkubalia Dokta. Ningefanyaje mwenzangu? Nikose vyote?”

Zena aliacha kufua, akaisukumia pembeni ndoo ya nguo. Kisha, akajifuta maji mikononi akitumia upande wa khanga. “Kuwa makini Eva, usije ukaufungua mlango usioweza kuufunga.” 

Kikapita kimya cha muda mfupi kabla ya Zena kuuliza, “So, ilikuaje mpaka mkaenda TAKUKURU?”

“Juzi usiku ulivyoondoka kwenda kwa Faraji, ndipo nikapokea simu ya Rumi, akinitaka nifike haraka pale barabarani wanapouza makaroni. Nikamkuta yuko na kaka mmoja, ambaye baadaye alinitambulisha kuwa ni afisa wa TAKUKURU, anasema alisoma na kaka yake. Akanitaka nimweleze mkasa mzima…”

“Na wewe ulivyo zuzu ukafunguka?”

“Sikuwa na namna.”

 “Lakini wewe ndiye mwenye kesi, ungeweza kukataa kusema lolote.”

 “Haikuwa rahisi unavyodhani. Tayari afisa wa TAKUKURU yuko hapo, na ameshadokezwa kisa kamili. Endapo ningejaribu kuficha ukweli katika mazingira yale, ningeonekana nimeanza kukubaliana na Dokta, nami ningejumuishwa kwenye kapu moja.”

“Enhee,” Zena akamtia moto aendelee.

“Baada ya kumsimulia huyo afisa, akaandika kila kitu kwenye notebook yake na kututaka twende ofisini kwake kesho yake asubuhi – ambayo ni jana...”

“Kwa hiyo, hivi sasa ulikuwa unakwenda wapi?” Zena akarusha swali jipya.

“Punguza wenge basi shosti, sijamaliza la kwanza unanirusha la tatu,” Eva alijibu pasi na papara. “Japo niligombana sana na Rumi kwa kitendo cha kuwaalika TAKUKURU without my consent, jana hadi tunakwenda huko, nilikupigia sana simu sikukupata. Tulipofika, tukakuta faili limekwishafunguliwa kwa yale maelezo yangu ya juzi. Nikatakiwa tu kuongezea maelezo mengine ya kushibisha upelelezi. Walipomaliza kuandika, wakanitaka nimpigie Dokta ili tupange appointment.”

“Nisikilize Eva,” Zena alidakia. “Si kwamba ninamtetea Dokta. Lakini, kumkamatisha kwa TAKUKURU naona kama ni kombora kubwa sana. Kumbuka hawa walimu ni watoto wa mjini – wana connection nyingi. Ikitokea akagundua mpango wako na akafanikiwa kukuponyoka, hapo ndo hutoboi milele. Na ikitokea akanaswa, jua walimu wote hapa chuoni watakuchukia. Zaidi ya hayo, familia yake itaingia vitani nawe. Nani atakubali wanaye washindwe kwenda shule kisa baba yao yuko jela kwa sababu ya kutengenezewa kesi? Nani atakubali kuona familia nzima ikifedheheka kwa sababu ya kesi ya ngono? Usiporogwa jiandae kupokea ugeni wa majambazi.”

“Katika mazingira hayo, ungekuwa wewe ungefanyaje?”

“Ningetafuta namna nyingine ya kumalizana na hiyo kesi. Kwanza, nisingeruhusu bwana wangu aingilie mambo yangu kwa kiwango hicho – na pengine hata asingejua kabisa. Kumbuka hawa wote ni wanaume; Dokta Masanga anachotaka ni penzi lako, na Rumi anachojaribu kufanya ni kulinda penzi lako lisipotee. Kwa Rumi, hili ni suala la wivu wa mapenzi kuliko upambanaji wa rushwa ya ngono. Trust me, endapo Rumi angelikuwa ni rafiki yako wa kawaida tu, angeliona ni aheri umkubali Dokta ili upate matokeo.”

“Kwa hiyo, ungekuwa ndo wewe ungemkubali Dokta Masanga?”

“Ukitaka uzuri, shurti udhurike,” Zena alijibu huku akibetua mdomo kwa kedi. “Kama nina uwezo wa kukabiliana na mishale toka kwa familia yake na kwa utawala wa chuo, nitapambana naye jino kwa jino.”

“Na kama huna uwezo huo?”

“Ningechukua tu maneno ya wahenga; cha mwanafuu mkufuu hu, cha mkufuu mwanafuu ha.”

“Unamaanisha nini?”

 Zena aliachia ucheko. Akajibu, “Kwamba siku zote, cha mwanafunzi, mkufunzi hula. Lakini cha mkufunzi, mwanafunzi hali. Mimi ni nani hadi nipingane na maneno ya wahenga? Unachoogopa ni nini hasa? Kwani ni sabuni hiyo kusema itakwisha!”

Eva hakuwa na haja ya kusubiri jibu la moja kwa moja. Alikwishaipata lugha ya picha, kwamba Zena anajaribu kumshajiisha apindue meza.  Alisimama, akaukamata vema mkoba wake kwa ajili ya kuondoka. “Aende huko. Wasichana wamejaa tele chuoni hapa, kwani ni lazima atoke nami!”

 “Aende wapi? Ndio amekuona wewe sasa. Panya wa msikitini hula misahafu. Kocha huwa wa kwanza kuonja burudani ya wachezaji wake; mwalimu atakula zawadi za wanafunzi; tabibu atapokea takrima ya wauguzi; na kila mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake. Ndo mfumo wa maisha,” Zena alisema na kucheka. “Anyway, kwa hiyo sasa mtaanzia wapi kumnasa? Maana hata hujanimalizia kuhusu hiyo appointment yako na Dokta.”

“Nitakumaliziaje na kila nikianza kusimulia, unadandia treni kwa mbele?”

“Aah babu eeh, kuimba kupokezana – raha ya mazungumzo kujibizana.”

“Nahisi n’shachelewa,” Eva aliinua tena mkono kutazama saa. “Natakiwa nifike TAKUKURU saa nane kamili. Saa kumi ndo appointment yangu na Dokta.”

“Yaani mnataka kumkamata leo?”

 “Kumbe je?” Eva alijibu na kuanza kuondoka. “Mchuzi wa mbwa hunywewa wa moto.”

Zena akainuka na kumsindikiza. “So, mmeshapanga pa kukutania na Dokta?”

“Yes,” Eva alijibu huku akiendelea kutembea taratibu. “Ila sikufichi shoga’angu, pamoja na ushenzi wake wote, lakini huruma inautafuna moyo wangu. Sina tu namna. Maji nimekwishayavulia nguo.”

“Mimi simhurumii hata kidogo. Nakuhurumia wewe tu. Endapo deal itabuma au akakushtukia. Yule anaweza hata kukuua.”

Zena alimsindika Eva hadi barabarani. Tayari Eva alikwishaita Uber. Hivyo, walipofika tu barabarani, haikuchukua muda mrefu, gari ikafika na Eva akajitoma ndani.

***

Eva alifika TAKUKURU na kumkuta Rumi ameketi kwenye kochi sehemu ya wageni. Rumi, aliyekuwa amevalia shati jeusi la mikono mirefu, pamoja na suruali ya kijivu, alisimama na kumlaki Eva kwa kumkumbatia.

“Pole kwa jua, mpenzi,” Rumi alisema.

“Ahh, nimeshapoa,” Eva alijibu na kuketi. “Umefika muda mrefu?”

 “Sana. Nichelewe niharibu mipango!?”

Ukimya ulitanda. Hapakuonekana mtu yeyote wala kusikika sauti yoyote. Eva aliangaza huku na kule ili kujaribu kuyazoea mazingira. Akasema, “Hivi Rumi una hakika na hiki tunachokifanya?” 

 Kabla Rumi hajajibu, sauti kavu ilisikika ikimwita kutokea ofisini. “Rumi!”

“Naam,” Rumi aliitika na kumtazama Eva. Kisha akanong’ona. “Mr. Hubiri huyo.”                        

“Ndo nani?” Eva alisaili.

“Yule afisa anayesimamia hii kesi,” Rumi alisema na kusimama. “Twende.”                                

Waliingia ofisini na kumkuta Hubiri akiwa ametuna nyuma ya meza yake pana. Walivuta viti viwili mbele ya meza na kuketi.

“Aisee karibuni sana,” Hubiri aliwakaribisha.

“Shukrani kaka,” Rumi alijibu, ilhali Eva akilazimisha tabasamu.                               

“Huyu anaitwa Mr. Bahati,” Hubiri alimtambulisha kijana mmoja aliyekuwa ameketi kwenye kochi dogo kushotoni mwake. “Tutakuwa naye kwenye kesi hii.”

Rumi na Eva waliinua nyuso zao kumtazama. Kijana mtanashati; mweupe, mrefu, aliyejazia misuli yake kimazoezi. Alivalia jinsi ya bluu na fulana nyeupe. Wakatikisiana vichwa kama ishara ya kusalimiana.                     

Hubiri aliinua mkono wake na kutazama saa. “Naona tuko nyuma ya muda. Enhe Eva, uliwasiliana tena na Dokta?”

“Ndiyo.”

“Ameshakutajia mahali pa kukutania?”

 “Ndiyo. Ni Kigamboni. Hoteli inaitwa Miami.”                                   

“Vizuri!” Hubiri alivuta droo, akachomoa kifaa kidogo mfano wa simu na kumkabidhi Eva. “Hii ni recorder. Utaificha kwenye pochi yako. Mkishaingia chumbani, utaibonyeza hapa kwenye kitufe chekundu ili kuanza kunasa sauti. Wala usiitoe kwenye mkoba – ina uwezo mkubwa wa kunasa sauti.”

“Sawa.” Eva aliikipokea recorder ile na kuisunda kwenye pochi.

“Sisi tutavamia chumbani baada ya dakika kumi tangu muingie,” Hubiri alisema. “Ukisikia tu tumegonga mlango, usimpe muda wa kujipanga. Chomoka upesi uje kufungua mlango nasi tutaingia.”

                                                                                    “Sawa.”

                                                                                        “Now, mpigie simu. Mwambie uko njiani unaelekea Kigamboni.”

                                                                                            Eva alichomoa simu mkobani. Akatafuta jina la Dokta Masanga na kumpigia.

                                                                                                “Weka loudspeaker,” Hubiri alisema.

                                                                                                    Eva akatii.

                                                                                                        “Hello, Eva!” Sauti nzito ya Dokta Masanga ilisikika upande wa pili.

                                                                                                            “Shikamoo, Dokta,” Eva alimsalimu huku akiwatembezea macho Hubiri na Rumi.

                                                                                                                “Vipi uko tayari, mtoto mzuri?” Dokta Masanga aliuliza bila kujishughulisha na shikamoo aliyopewa.

                                                                                                                    “Ndo niko njiani to Kigamboni.”

                                                                                                                        “Oops, umefika wapi?”

                                                                                                                            Eva alirudisha macho yake kwa Hubiri. Haraka Hubiri akamwashiria aseme amefika maeneo ya Ferry. Eva akasema.

                                                                                                                                “Ooh, bora hujafika mbali,” Dokta Masanga aliendelea. “Miye bado sijatoka ofisini hadi sasa. Kuna kazi ilinitinga. Kama vipi rudi tu unikute hapa ofisini kwangu then tutatoka pamoja kwa gari yangu.”

                                                                                                                                    “Anhaa, kwa hiyo, nije ofisini kwako?” Eva alirusha swali ambalo tayari jibu lake amekwishapewa, ili kuvuta muda wa kushauriana na Hubiri.

                                                                                                                                        “Yah. Njoo tu moja kwa moja ofisini.”

                                                                                                                                            Kabla Hubiri hajamwelekeza Eva kitu cha kusema, simu ikakatwa.

                                                                                                                                                Hubiri alijikuna kichwa sekunde kadhaa, kisha akamgeukia Bahati. “Unasemaje?”

                                                                                                                                                    Bahati akajibu, “Hakuna kilichoharibika. Siye tutangulieni huko Miami Hotel. Eva arudi ofisini kwa huyo Dokta. Wakishaanza kuondoka kuja hotelini, Eva atutonye, tukae tayari.”

                                                                                                                                                    “Vipi kama watachelewa kutoka ofisini, akaamua kubadilisha hoteli?” Hubiri alihoji.

                                                                                                                                                   “Hilo nalo neno,” Rumi alidakia.

                                                                                                                                                   “Sikia Bahati,” Hubiri alisema, “Wewe utatangulia Kigamboni, sisi tutakwenda na Eva hadi chuoni. Tutabaki barabarani wakati Eva akienda ofisini kwa Dokta Msanga. Watakapotoka tu Eva atatujulisha kama mwelekeo ni uleule, then, sisi tutaunga tela kwa nyuma.”

                                                                                                                                                    “Wazo zuri,” Bahati aliunga mkono.

***

Waliwasili chuoni majira ya saa kumi alasiri. Hubiri na Rumi walibaki kwenye gari, nje ya chuo. Eva aliteremka na kwenda kuingia katika viunga vya chuo. Bila ajizi, alikwenda moja kwa moja hadi jengo la Idara ya Sosholojia. Taratibu, akapandisha vidato vya ngazi kuelekea ghorofa ya pili. Korido ilimezwa na ukimya wa hali ya juu. Alitembea taratibu sakafuni kuelekea mwishoni kabisa mwa korido ambapo ndipo ilipo ofisi ya Dokta Masanga. Alipofika mlangoni, alisimama na kujitengeneza vizuri.   Aligonga mlango taratibu huku akijaribu kuifukuzia mbali hofu iliyoendelea kumchoma moyoni.

“Yes!” Sauti nzito ya Dokta Masanga ilimlaki. “You may enter.”

Alikamata kitasa cha mlango, akakizungusha taratibu na kufungua mlango. Alipoingia ofisini na kuufunga mlango kwa nyuma, alijihisi kama aliyeopolewa kwenye jiko la kuoka mikate na kutoswa kwenye jokofu. Joto lote alilotoka nalo nje lilimezwa na hewa mwanana iliyopozwa na kiyoyozi.

Dokta Masanga aliketi nyuma ya meza nadhifu ya mbao, iliyoko mwishoni kabisa mwa ofisi. Nyuma yake, shubaka kubwa la vitabu liliwambwa ukutani kiasi cha kuumithilisha mwonekano wa ofisi na ule wa maktaba ya mkoa.

“Ooh, Eva,” Dokta Masanga alisema huku akivua miwani baada ya Eva kumkaribia mezani. Akamwashirikia kwa mkono wa kulia. “Karibu kitini.”

Mbele ya meza palikuwa na kiti kidogo cha mbao, na pembeni kidogo, palikuwa na kochi dogo la mbao lililoegeshwa ukutani.

“Ahsante,” Eva alijibu na kuvuta kiti kidogo mbele ya meza. Alipoketi, akamsalimu. “Shikamoo, Dokta.”

“Inaonekana nje kuna jua kali,” Dokta Masanga alijisemesha, huku akiondoa macho yake kwa Eva, na kuchungulia nje kupitia dirisha la vioo liliko kuliani mwake. “Sijatoka muda mrefu. Utakunywa kinywaji gani?”

“Ahsante Dokta,” Eva alijibu huku akikwepesha macho yake. “Niko vizuri tu.”

“Okay. Kuna kazi ilinitinga muda mrefu. Ila nimekwishaimaliza. Sasa, ninayetaka kumkabidhi hapokei simu. Huyo ndo ananiweka hapa muda wote. Ungekunywa hata maji basi.”

“Usijali, Dokta.” Eva alijibu huku uso ameuinamisha chini.

“Lakini huonekani kuwa na furaha, Eva,” Dokta Masanga alisema hali ya kuwa amemkazia macho. “Mapenzi ni furaha ya moyo na raha ya mwili. Ndo maana yakaitwa mapenzi, yaani upendo. Hatupaswi kuwa kama maadui…”

“Lakini Dokta somo lako nililifanya vizuri sana,” Eva alisema kwa sauti ya unyonge. “Sikupaswa kufanyiwa vile kabisa.”

Dokta Masanga alitabasamu. Akavuta kiti mbele, karibu zaidi na meza. Akamshika Eva mikono yake na kuivuta mezani. Akasema huku akimpapasa viganjani, “Nilishakwambia, Eva. Kufaulu kwako kunategemea kalamu yangu, na si akili yako. Lakini kufeli kwako kutatokana na ujinga wako mwenyewe. Sasa, ujinga si lazima iwe ni wa kutokuelewa maswali kwenye mtihani, bali hata kutokuelewa mbinu za ndani na nje ya uwanja. Ulipaswa kujifunza utundu wa kufaulu mtihani kabla ya kuufanya. Lakini si kitu, hayo yamekwishapita. Sasa utafaulu. Sawa mtoto mzuri?”

Eva aliinamisha macho yake mezani. Akaupachika mguu wa kulia juu ya ule wa kushoto. Sketi yake fupi ilizidi kupanda juu na kuacha sehemu kubwa ya mapaja yake meupe ikionekana. Kisha akatikisa kichwa kuafiki.

Dokta Masanga alimwachia Eva mikono yake. Akasimama. Kisha, akatembea taratibu kuelekea mlangoni. Akaufunga mlango na kurejea mezani. Alipofika, akasimama nyuma ya Eva na kumwekea mikono mabegani. Akasema, “Sikia Eva. Japo tumekwishaelewana, na kwamba tulipanga kukutana leo, lakini sipendi kukuona ukiwa na simanzi usoni. Sikusudii kukudhalilisha hata kidogo. Kadri tutakavyoendelea kuwa pamoja unaweza kunipima zaidi. Ikiwa utaona nakufaa tunaweza kuendelea kuwa pamoja, na ikiwa tutashindwana basi kila mmoja ataendelee na hamsini zake bila mawaa yoyote. Sawa?”

Eva alitikisa tena kichwa kuafiki.

“Very good,” Dokta Masanga alisema, huku akishusha mikono yake taratibu hadi kifuani kwa Eva, na kuanza kutalii eneo hilo. “Akili ni uwezo wa kutembea juu ya mayai bila kuyapasua…inahitaji mtu mjanja kama wewe kufanya hivyo.”

Mapigo ya moyo yalianza kukishambulia kifua cha Eva. Akaanza kupumua juujuu kama aliyekimbizwa na mbwa. Baada ya dakika chache za utalii, kwa ustadi wa hali ya juu, Dokta Masanga aliikamata fulana ya Eva na kuivuta taratibu hadi ikachomoka katika sketi aliyokuwa amechomekea. Kitovu pamoja na sehemu ya tumbo vikabaki wazi.

Kufikia hapo, uzalendo ukamshinda Eva. Akainua mikono yake ili kumshika Dokta Msanga akidhamiria kumzuia. Akafunua kinywa kusema, “Lakini Dokta…”

“Evaaa, what are you doing?” Dokta Masanga alimwinamia Eva na kumbusu shingoni. “Si umesema umenielewa? Sasa mbona unataka kuharibu tena?”

Pamoja na kwamba tayari Eva alikwishakuwa chini ya milki yake, lakini bado Dokta Masanga aliendelea kumraghibisha kwa maneno laini ya tashiwishi.

Ooh, my God, nifanyeje sasa? Eva alijiuliza kichwani.

Dokta Masanga aliendelea kuipandisha fulana ya Eva hadi juu ya matiti yake. Kisha, akiwa bado amemwinamia, kwa kutumia mikono yake, akaendelea na utalii sehemu ya tumbo na kifua. Na kwa kutumia ulimi, akaenda kutalii ndani ya masikio yake. Haikuchukua muda, bila zohali wala papara, akamalizia kumvua fulana pasi na kukutana na pingamizi.

Dokta Msanga alilegeza tai yake, akafungua kishikizo cha juu cha shati lake na kulivua. Akamnyanyua Eva kitini, wote wakiwa vifua wazi, na kwenda naye moja kwa moja kochini.

“Lakini Dokta…humu ni ofisini…si sehemu salama...”

“Nimeshafunga mlango. Hakuna anayeweza kuingia wala kutusikia. It’s between you and me,” Dokta Masanga alimnong’oneza sikioni. “You help me to relax and the exam is all yours.”

Makubaliano yalikuwa ni kumpitia Dokta Masanga ofisini ili watoke pamoja kwenda hotelini. Lakini kwa kuwa mazingira hayakuruhusu kutoka, hivyo, Dokta Masanga akaamua kuianzisha safari mumo humo ofisini. Sasa, Eva asingizie nini ilhali hicho ndicho kilichofanya wakapanga miadi siku hiyo? Asingizie kushikwa na tumbo la ukubwa? Angeulizwa alikuja kufanya nini. Kila wazo lililompitikia kichwani lilikosa mantiki.

‘Akikushitukia anaweza hata kukuua!’ maneno ya Zena yalipita kama mwangwi kichwani mwa Eva. Akaanza kujionya mwenyewe kuwa, endapo atalazimisha kubumba visingizio visivyo na mantiki, basi pengine Dokta angeshitukia mpango wake.

Eva akiwa bado anapambana na fikra zake, Dokta Masanga aliendelea kufanya utalii maungoni mwake. Tahamaki, sehemu kubwa ya miili yao, walibaki watupu. Hapo sasa, hofu ya Eva haikuwa tena juu ya kukutana kimwili na Dokta, bali wasiwasi wake ulikuwa ni kwa akina Rumi na yule afisa wa TAKUKURU waliobaki wakimsubiri barabarani – wangeweza kuamua kumfuata baada ya kuona kimya cha muda mrefu. Hakuwa na namna ya kumhadhari Dokta Masanga. Katika mazingira kama hayo, ndipo lisilo budi hutendwa. Akakubali kukata pua ili kuunga wajihi.  Kochi likawa uwanja. Mbaya zaidi, hapakuwa na kinga yoyote uwanjani hapo.

Baada ya takribani dakika tano tu, Dokta Masanga aliteremka mlimani, na kwenda kuketi kwenye mkono wa kochi ilhali Eva angali amejilaza papo hapo kochini. Uso wa Eva ulijaa fadhaa na izara. Kila alipofumba macho, aliona taswira ya Rumi akiwa ameketi ndani ya gari pamoja na afisa wa TAKUKURU, wakimsubiri yeye na Dokta Masanga watoke ili kuelekea Miami Hotel. Hawakutanabahi kwamba, Miami Hotel ni mumo humo ofisini kwa Dokta Masanga.

Maswali yaliendelea kupita kichwani mwa Eva, endapo aendelee kushiriki mpango wa kumkatamatisha Dokta Masanga au amnusurishe ili kusubiri kufaulishwa mtihani?

Hakuwa na muda wa kuyatafutia majibu maswali hayo. Akainuka kochini na kuvaa nguo zake ili kuondoka.



Nje ya lango la kuingilia Chuo Kikuu cha Mzizima, gari dogo Toyota Spacio, rangi ya fedha, liliegeshwa karibu na barabara, mwishoni mwa jengo pana la ghorofa moja lililo mkabala na chuo. Jengo hilo lilikuwa na maduka pamoja na mgahawa mdogo eneo la chini huku  ofisi mbalimbali zikiwa eneo la juu. 

Alasiri hiyo, barabara ya lami iliyotenganisha majengo haya mawili haikuwa na pilikapilika nyingi. Hata ile ingia toka katika majengo haya ilikuwa ya kuhesabika. Kulikuwa na utulivu uliomfanya yeyote aliyetaka kufuatilia chochote, toka kona yoyote, ajione yu mwenye nyota ya jaha. 

Mle garini, Rumi na yule afisa wa TAKUKURU walitulia humo kama mzigo uliosahaulika uvunguni. Licha ya wote kuketi viti vya mbele, Hubiri akiwa kwenye usukani, hawakutazamana seuze kusemezana. 

Ghafla tu, soga za mikakati na vicheko vilivyotamalaki njia nzima, vilichanja mbuga na kutokomea kusikojulikana. Kukawa na ukimya mzito uliwaokumbatia dakika mbili tatu za mwanzo, tangu Eva alipowaacha eneo lile na kuelekea ofisini kwa Dokta Masanga. 

Katikati ya ule ukimya, walilipepesa macho ya kuvizia. Hubiri aliwaza namna atakavyomchezesha yosayosa na kumtia pingu mtuhumiwa wake. Kadhalika, Rumi aliukokotoa mpaka uzito wa ngumi atakayomkandika huyo mgoni wake. 

Muda ule, Eva alipoteremka na kuchapua hatua kulifuata geti la kuingilia chuoni, Rumi alimtazama mahabuba wake kwa mahaba na huruma.  Ilikuwa kama kumsalimisha ndama wake mdomoni mwa chatu kwa mikono yake. 

Akili ilimpa ujasiri wa kujipa subira ilhali nafsi yake ikimsusia kutulia. Angetulia vipi na msimamo wa Eva bado ulimtia jakamoyo? Mzozano uliozuka baada ya kumpatia Eva taarifa ya kesi yake kufika TAKUKURU, ulimtia wivu. Wivu uliomchonyota nusu ya kukitoboa kifua na kuambaa hewani mithili ya moshi. 

Hofu ya Eva ilijidhihirisha zaidi, hakutaka yafike mbali. Walakini, yasiyofika mbali huwa ni yale yaliyokatwa makali. Makali ya nani? Yake yeye aliyeyavalia kibwaya au yake yule anayewapigia manyanga. 

Alikosa majibu, akajikuta tu anabweta.  

“Leo ndo kiama chako bwege wewe!” alinong’ona kwa sauti ya kichwani. Pasi kujua, hata sauti yake mwenyewe ilimsaliti na kutokea mdomoni. 

Hubiri aliyekuwa amemaliza kuzungumza na simu, aliuitikia haraka ule mnong’ono wa Rumi. Alimtegea sikio, pengine kwa kudhani Rumi alikuwa akisemazana naye. 

Aliyesikilizwa alitikisa kichwa kulia kushoto. Aliitazama saa yake ya mkononi kwa mara nyingine tena. Subira aliyojivika ilianza kumvuka polepole.

Pamoja na kuutazama muda mara chungu nzima, bado hakuwa na yakini na muda uliokwishakatika. Mshawasha aliokuwa nao ulimfanya ajihisi tayari alikuwa amekwishazitafuna saa dazeni. Waama, alikiri nafsini, urefu wa siku si muda.

“Mbona hawatokezei sasa?” Rumi aliuliza akiinamisha shingo na kuchungulia tena kule getini huku akiweweseka. “Labda tumpigie simu?” 

“Hapana, inaweza kuharibu.”

“Au niwafwate nini?” Rumi alidakia. Mkono ukigusa kitufe cha kufungulia mlango. Umakini wake wote ulikuwa kule getini. 

“Subiri kwanza, una uhakika Eva hakumshirikisha yeyote zaidi yako?” 

Swali hilo ndilo lililofanikiwa kumfanya Rumi amtazame Hubiri. Alimgeukia akiwa ameyakodoa macho kwa upana aliojaaliwa. Kisha, taratibu aliyaondoa macho usoni pa Hubiri na kuyaelekeza tena kule getini. 

Awamu hii, alilitazama lile geti la chuo kama lango la kuzimu. Sentensi zilizofuata baada ya lile swali, zilipita masikioni mwa Rumi kama hatua za minyato. 

Hakuzisikia na kama alizisikia hakuzielewa. Hamaki ilimfanya afanye pupa kuufungua mlango wa gari na kuteremka.

‘Anakwenda wapi tena huyu, Aaah!’ Hubiri alihamanika akiubamiza usukani.

Hakusubiri manyunyu yawe rasharasha, naye alichomoka garini chapuchapu. Ikawa kama watu wawili wanaofukuzana kimyakimya kuelekea kule getini. Hata hivyo, mbio zao zilisimama ghafla. 

Wote wawili walimwona Eva kupitia nondo nyembamba zilizoshikamana na nembo ya chuo na kuumba lango maridadi la kuingilia chuoni hapo. Alikuwa akija kwa mwendo wa haraka. Mwendo ambao uliwafikishia hisia mchanganyiko. Haukuwa mwendo wa mtu mwenye utulivu kichwani. Zaidi, alikuwa peke yake. 

Rumi aligeuka nyuma kutazama alikotoka. Hakuwa na uhakika kama uamuzi wa kuchomoka garini ulikuwa sahihi. Hubiri, aliyekuwa hatua takribani 15 toka aliposimama Rumi, naye kimuyemuye kilimtafuna.

Eva alipolikaribia zaidi geti, Rumi alipiga hatua kurudi nyuma. Hatua moja iliyozaa nyingine. Mwishowe, aligeuka na kuanza kurejea kule walikoegesha gari lao. Hubiri aliyekuwa amekwishaingia garini, aliibebanisha mikono kichwani wakati akiwatazama Rumi na Eva kwa awamu, kadiri walivyojongea kulifuata gari.

Uwepo wa Eva peke yake nyuma ya Rumi kulimbainishia kuwa hali haikuwa shwari.  Samaki alikuwa amekitema chambo.  

Eva alipojitoma garini. Rumi alimsaili, “Imekuwaje?”

“A..a..amekataa kuongozana nami.” Sauti yake ilikosa tafsiri rasmi.

“Kiaje? Si alishakubali mnaenda wapi kule sijui.” 

“Amekataa kuongozana nami!! Hujanisikia?” Eva alilirudia jibu lake kwa sauti ya juu yenye msisitizo.

“Sasa unanifokea ama?” Rumi aliyekuwa amepachika kichwa katikati ya viti vya mbele, alimuwakia Eva kule nyuma. Hakuona mantiki ya Eva kumpandishia sauti namna ile. 

“Sijakufokea Rumi, nimekwambia amekataa.” Eva alinyong'onyea. 

“Amekataaje? Au imekuwaje?” Rumi alizidi kumbananisha.

“Tunaweza kuondoka eneo hili? Nimeshachoka mimi,” Eva aliyefumbata mikono kifuani kwa kuipishanisha alizungumza akitazama pembeni.

Alihema kiasi cha kifua chake kuonekana wazi kikiinuka na kushuka. 

“Siamini unanijibu kuwa umechoshwa na mambo haya wakati kama huu, hivi uko serious mpenzi? After everything I’ve…” 

“Tunaweza kuondoka hapa?” Eva alimkatiza, akazungumza akimtazama Hubiri kisogoni.  

“Kwa hiyo unaona ninachokuuliza mimi ni upuuzi, si ndiyo?” Rumi bado hakuwa amekubaliana na kilichotokea.

Eva hakumjibu. Aliyahofia majibu yake yaliyomjia kwa wakati ule. Alijizuia mno kutojibizana na Rumi. Kosa moja, goli moja. Hakutaka kujifunga goli la pili.

Mchanganyiko wa hisia za hofu, soni, hasira na majuto ulijipika asteaste na kumtolea bokoboko lililomkaba kooni. Waama, lisingepita hata kwa juisi ya machozi. 

“Kwa hiyo hujamrekodi chochote?” Rumi alihisi kukata tamaa.

“Si tulikubaliana ningerekodi akifika chumbani?” Eva alijitetea, akijua wazi akili ya kurekodi chochote hakuwa nayo. Shambulizi alilofanyiwa lilikimbia na uwezo wake wa kufikiri. 

Eva alikikumbuka kile kifaa cha kunasia sauti alichopewa kule ofisini, na yeye kukisunda mkobani. Alikitoa na kumkabidhi Hubiri.  Hakikuwa na maana tena. Wakati akikitoa, aliikumbuka miwani yake. Aliupekua mkoba wake kwa papara na kujipapasa bila kuiona. 

Mungu wangu, itakuwa imebaki kule!

Alimeza mate kwa taabu. Rumi naye, alikirudisha kichwa mbele kwa dakika moja tu, na iliyofuata alimgeukia tena Eva. “Labda, kuna mtu mwingine ulimshirikisha jambo hili?”

Kwa yote yaliyotokea ndani ya muda mfupi uliopita, Eva alihitaji utulivu kidogo aweze kuyatafakari. Rumi hakuonekana kumpatia nafasi hiyo. Ikiwa ni yeye pia ndiye aliyemshinikiza kuwinda asichoweza kukiua, mwishowe kimemrudia na kumwuma. 

Hubiri na Rumi walipoukazia usaili. Eva aliangua kilio.

“Eva...Eva!” Rumi aliita kwa wahka.

Aliteremka toka kule mbele na kuja kuketi kiti cha nyuma. 

“Niambie nini shida mpenzi? Eva!” Rumi alimtikisa akijaribu kumfanya mpenzi wake amtazame usoni.

Hubiri aliingilia kati, “Mwache kwanza, ana hasira sana. Alijua leo ndiyo mwisho wa haya yote. Haya mambo huwa si rahisi kihivyo hasa kwa mtu kama Dokta Masanga. Kuna wakati inabidi utege na kutegua hadi atakaponasa. Ustahimilivu unahitajika aisee!” 

“Sikiliza mpenzi wangu, sikiliza basi,” Rumi alimbembeleza.

Alijaribu tena kuyashika mashavu ya Eva ili wapate kutazamana. Ujasiri wa kumtazama Rumi usoni hakuwa nao. Eva aliuficha uso wake kifuani pa Rumi wakati akiendelea kuomboleza. 

“Tutampata tu, atanasa tu mtegoni mpenzi, tuliza hasira,” Rumi alisaganisha magego kwa jazba, hali akitoa maneno ya matumaini. Aliumia kumwona mpenzi wake akiwa katika hali ile. 

Hubiri aliliondoa gari na kuliingiza barabarani. Njiani, aliwasiliana na Bahati aliyetangulia kule Miami Hotel, Kigamboni. 

***

Usingizi wa mang’amung’amu uliomjia alfajiri baada ya mkesha wa mawazo, ndiyo uliomfanya Eva ashindwe hata kuusikia mlio wa simu iliyokuwa juu ya meza, ikichajiwa. Ilipoanza kuita kwa mara ya nne, Eva alitoka katika ile hali ya kuukorota usingizi kifudifudi na kupapasa chini ya mto. 

Alikikosa alichokuwa anakitafuta. Akasonya. Mlio wa simu usiopumzika hata sekunde ulimkera. Mpigaji naye aliikazia dhamira yake kana kwamba alikuwa na haraka ya kununua dakika za uhai wa nyongeza.

Eva alijiinua na kutupa shuka kando. Akateremsha miguu sakafuni. Aliitazama simu yake mezani bila papara. Ilinyamaza kwa sekunde chache na kuanza tena kuita. Naye kama mlevi, alijiinua akiyumba na kuifuata pale mezani. 

Jina la mpigaji lilimfanya atabasamu kizembe. Alikuwa Zena.

Akaichomoa simu kutoka kwenye chaji na kuipokea.

“Hebu fungua mlango kabla sijaung’olea mbali, kulala gani huko?” Sauti kali ya Zena ilimfanya aiweke simu mbali na sikio lake. 

Aliufuata mlango, akaufungua.

“Nimedamka hivi kwa ajili yako ujue, yaani nimepiga simu kiama, hupokei. Haya kimetokea nini?” Zena alitupa mikono hewani, akielekea kujiegemeza kwenye ile meza iliyotazamana na kitanda cha double decker. 

Eva alishusha pumzi. Alimtazama Zena bila mshawasha wa kumweleza yaliyojiri. Lakini, kwa namna Zena alivyomtazama yeye, ni dhahiri angemkaba hadi ayatapike.

Mawazo haya yalimfanya atamani kucheka wakati akijiondosha kichovu pale mlangoni na kuirejesha simu kwenye chaji.

“Mambo ni mazito shosti,” Eva alitamka akiiegesha mikono yake kiunoni. Kichwa kikilala upande.

“Enhe! Imeshindikana au imekuwaje? Maana nilisubiri jana grupu la chuo liwake moto kwa mapicha ya uchi ya mzee baba, hola! Nikajaza bando la wiki Instagram kunogile, hola! Haya vipi tena?” Zena alimeza mate kwa shauku.  

Vile alivyokuwa akiongea kishabiki, changanya na wanja alioupaka kwa haraka; wanja uliofanya jicho moja lionekane kuwa juu kuliko lingine, alimfanya Eva acheke kwa sauti ya mguno. 

“Haikuwa rahisi, ameukwepa mtego.” Eva alinyanyua bega moja juu na kulishusha.

“Kaukwepajekwepaje? Hebu nipe stori vizuri.” Zena aliweka mikono kiunoni.  

Eva hakusema neno.

“Kama namwona vile Rumi na maafisa wake walivyolegea kama ndevu za mahindi.” Akacheka. “Nilikwambiaje? Hawa walimu watoto wa mjini. We’ ukamwamini aliyekuja mjini kwa hisani ya bodi ya mikopo. Na usipoangalia, utabembea na sup hilo hadi mwaka wa mwisho.” 

Eva hakumjibu. Kulikuwa na mengi ya kumweleza. Zena alikuwa mtu pekee ambaye alitaraji asingemficha jambo lolote. Ila, ghafla tu, nafsi iliingia uzito. Ni kama vile aliyaonea aibu na kinyaa yote yalitokea ofisini kwa Dokta Masanga. 

Kwamba amelabuliwa, kijungu kilikuwa kimepakuliwa. Kirahisi, kuliko urahisi wenyewe. Akiri mbele ya Zena kuwa, kwa ulimi wa Dokta sikioni, na mawazo tele kichwani, alijikuta tu akimkabidhi Dokta kijungu akikoroge atakavyo. Naye, akakikoroga kikakorogeka.

Amba! Kwa majitwezo aliyoanza nayo, ilikuwa muhali kuyakiri yote haya kwa Zena. Angechekwa hata na mijusi ya mle ndani.

Hivyo, alimsimulia Zena ya tangia ofisini kule TAKUKURU. Kisha, akaufuta mkanda na kuingiza vipande vya uongo na ukweli kuificha izara yake. Akamalizia na kipande cha Rumi kumrejesha pale Block A akiwa na hasira za mkizi. 

“Kwa hiyo, bado mnataka kuyachimba msoweza kuyafukia? Haya! Ila kama kaukwepa mtego, basi muwe makini zaidi. Nilishakuonya. Mwambie Rumi atulie kidogo kwanza. Atakuponza.” 

Ushauri aliopewa na Zena ulikuwa sawa kidogo na ule waliopewa jana yake na Hubiri. Alipokuwa akiwashusha sehemu anayoishi Rumi. Aliwaambia, ilihitajika mipango zaidi ya hii waliyofanya. Hivyo, wakakubaliana kumsubiria Dokta Masanga alianzishe tena, wamnase. 

Wakati Rumi akisubiria sakata liwive, Eva alikuwa akitafuta namna ya kumwaminisha Rumi kuwa Dokta Masanga alikuwa ameacha kumsumbua. Zilihitajika sababu zisizoacha mashaka hata kidogo. 

Uongo uliovishwa imani na kupendeza ulipaswa kuandaliwa. Rumi alikwishamhoji kama alipata kumwambia mtu mwingine kuhusu jambo lao. Eva akamhakikishia hakukuwa na mwingine. Alihofia kumwingiza Zena matatani.

Hilo la kuutafuta uongo, lilimtafuna Eva pengine kuliko hata usumbufu aliokuwa akiupata.

***

Wiki moja baada ya lile tukio lao ofisini, Dokta Masanga alikuwa kimya. Hakujishughulisha tena na Eva, hata pale walipopishana kila mtu akiwa kwenye hamsini zake. 

Ukimya wa Dokta Masanga ulimtesa Eva. 

Yumkini, alitamani kupokea walau meseji yenye kumhakikishia hakuwa vitani tena. Pengine, kuhakikishiwa kuwa alama za mtihani aliofelishwa zingekaa kwenye mstari.  Yasijekuwa ya wali deni, mchuzi karadha. 

Wiki ya pili ilipokatika bila neno, Eva aliamua kujiongeza, kwa kujiaminisha kuwa sasa hakuwa na deni tena na Dokta Masanga. Akajitahidi kuishawishi nafsi yake kusonga mbele, huku akiutafuta ule uongo wa kuendelea kumtulizia Rumi. 

Rumi ambaye sakata la Dokta Masanga kwake, mkoko ulikuwa umealika maua, alikuwa akiisubiri kwa hamu siku ya kumwadabisha.

 *** 

“Bado niko chuoni na Zena, nitakupigia baadaye mpenzi wangu. Au njoo basi,” Eva alizungumza na Rumi akiwa ameibana simu kwa bega la kulia ilhali mikono yake ikijaribu kuzipanga karatasi na kuzibana pamoja.

Zilikuwa karatasi za kazi iliyokuwa inatakiwa kukamilishwa na kukusanywa siku hiyo, muda huo wa saa kumi na moja kasoro, jioni. Ya kwake, alikwishaikamilisha kitambo. Iliyokuwa mikononi mwake ilikuwa kazi ya Zena. Wakati akizungumza na Rumi, Zena alifika akitweta.

“Yule mbabu anataka kufunga ofisi yake. Hebu tupeleke tu hivi hivi,” 

Zena aliongea kwa sauti, asijali mwenzake alikuwa akizungumza simuni. Eva alikata simu na kumpa umakini rafiki yake.

“Karatasi zingine umeshazipata?” 

“Nizipate wapi, nimeokota hizi, we unganisha hapo tukakusanye.” Zena alimkabidhi Eva karatasi alizofika nazo.

“Mbona hizi zinaanzia ukurasa wa 12 wakati hapa mwisho ni… khe! na hizi mbona maandishi yamegeuka juu chini?” 

“Yule babu atafunga ofisi bwana, hizo kurasa zitajiongeza mbele kwa mbele. Twende.” Zena alizikwapua karatasi zote alizokuwa nazo Eva na kuanza kutoka nje ya ukumbi wa semina.  Eva aliibeba mikoba yao na kumfuata nyuma mbiombio.  

Walikwenda  moja kwa moja mpaka lilipo jengo la Idara ya Sosholojia. Eva alibaki ghorofa ya chini wakati Zena akipandisha ngazi kwa mwendo wa mchakamchaka.

Tangu alipotoka ofisini kwa Dokta Masanga alasiri ile, hakupita tena karibu na jengo hili hata kwa bahati mbaya. Kusimama hapo akimsubiri Zena, kulimrejeshea kumbukumbu  alizokuwa akiendelea kupambana nazo kimyakimya.

 Simu yake iliyoanza kuita ndiyo iliyomtoa mawazoni. Aliitoa mkobani na kuileta usoni. Jina lililosomeka juu ya kioo cha simu, lilimfanya azungushe shingo mithili ya mtu mwenye degedege. Aliangaza kwa kasi ya ajabu akiutafuta uwepo wa mpigaji eneo lile. 

Simu ile ilimtia kiwewe. Aliiacha iite mpaka alipokatika 

yenyewe.

Aliposikia hatua za mtu kwenye ngazi, alikurupuka na kuzifuata ngazi kwa haraka. Pengine, alitumaini kukutana na Zena akiteremka baada ya kukabidhi kazi. Alitaka kumshika mkono na kumuhimiza kuondoka eneo lile kwa kasi ya mchomoko wa risasi. 

Lahaula! Huko alikoelekea ndiko alikogongana uso kwa uso na Dokta Masanga aliyekuwa na simu sikioni. Ni wakati huo, Eva naye alitambua simu aliyokuwa nayo mkononi ilikuwa imeanza kuita tena. Mpigaji akiwa yuleyule aliyesimama mbele yake.

“Kumbe upo hapa! Nina bahati nawe. Tunaweza kuongea, right now?” Dokta Masanga aliuliza, akiitoa simu sikioni. 

“But, siko hapa kwa ajili ya kuonana nawe,” Eva alijitutumua. Macho yake yakimtazama Dokta Masanga na kuzitazama zile ngazi zilizoelekea juu. Ngazi zilizokuwa nyuma ya mwanaume huyo.  

“Nakusubiri ofisini.” 

“Siwezi kuja.”

“Huwezi au hutaki?”

“Niko na rafiki yangu, nisingependa anitilie shaka na…” 

“Zena Masamba?” 

Dokta Masanga alitabasamu alipoushuhudia mshangao uliotanda usoni pa Eva baada ya kumtajia kwa ukamilifu jina la rafiki yake.

 ‘Mungu wangu nisaidie,’ sauti ya kichwani mwake iliumba kibwagizo kilichojirudia mara kadhaa. 

“Unataka tuzungumzie hapa?” Swali la Dokta Masanga lilienda sambamba na kusikika kwa sauti za hatua za mtu anayeteremka ngazi. Walikaa kimya mpaka pale Zena alipowafikia. 

Kama mtu aliyeelewa kuwa hakuhitajika kuwa pale, Zena alimsalimia Dokta Masanga, kisha akauchukua mkoba wake toka mikononi mwa Eva. Kimyakimya, aliambaa akimwacha mwenzake apambane na hali yake.

Kwa unyonge, Eva alivikwea vidato vya ngazi akimfuata mwenyeji wake mithili ya mbwa mdomoni mwa chatu. Kama ilivyo ada, hali ya hewa mororo ilimpokea ofisini mle.  Unyonge aliokuwa nao, ulimsimamisha mbali kidogo na lile kochi lililomkirimu nafasi ya kutetea maksi zake. 

“Come on, Eva! Unataka tuzungumze ukiwa mbali kote huko?”

“Niambie ulichoniitia, niondoke.”

Kwa kujua kuwa Eva asingesogea pasipo yeye kumfuata, Dokta Masanga aliinuka toka kitini alikokuwa ameshajipweteka. Alimfuata Eva pale aliposimama. Mkono wake wa kushoto ulinyooka na kiganja chake kutua ukutani. Mkono wake wa kuume ulikifuata kidevu cha Eva na kukishika. Alikipandisha juu taratibu na kuuinua uso wake. Wakatazamana pasipo tendo lingine lolote kupita kati yao. 

“Eva,” Dokta Masanga aliita kwa tuo. 

Eva alibung’aa asijue kama aitike ama la.

“Bado nakuhitaji,” Dokta Masanga alisema.  Sauti yake iliyojaa huba lenye mamlaka ilipenya taratibu mithili ya dawa imiminwayo kuyapooza maumivu. Macho yake yaliyokuwa nyuma ya lenzi za miwani yalifumba na kufumbua katika namna ambayo ingeweza kuushawishi moyo wa mtazamwaji kujitenga na kifua.

Eva alihisi kubanwa. Akajitoa karibu na Dokta Masanga. Akaenda kusimama karibu na lile kochi. 

“Ulipomaliza haja zako hukuzungumza nami,” Eva alisema, katikati ya wahka na hasira.

“Kwa sababu uliniacha nikiwa sijielewi.” Dokta Masanga alimfuata pale alipokimbilia.

“Ulipata ulichokuwa unakitaka, now what else do you want from me?”

“You! Wewe! Nakutaka wewe.” 

“Kwa nini unanifanyia hivi lakini?” Eva aliuliza kwa sauti hafifu.

“Siyo mimi, ni hisia nilizonazo juu yako Eva.” Dokta Masanga alimkaribia zaidi.

Eva akababaika. Kuna kitu kilimkaba tena kooni. Hakuelewa kama ni hasira au uchungu. “Dokta, kuna wanawake wangapi hapa chuoni?”

“Macho yangu yamekuona wewe.” 

Eva alijiinamia kwa sekunde kadhaa. Alipokiinua kichwa chake, alimkabili.

“Nilivua utu wangu kutetea kitu kilicho haki yangu. Hiki unachotaka sasa kiko nje ya uwezo wangu. Kwa nini usikubaliane na ukweli kuwa siwezi kukupa moyo wangu?” 

Maneno ya Eva, yalifika kama mshale wa moto kifuani pa Dokta Masanga. Pengine, hakutarajia baada ya yote kutokea, Eva angeendelea kuwa msumbufu.

Kwa muda aliokaa kimya baada ya kushughulishana na Eva, Dokta Masanga alijiuliza mara kadhaa, ni kwa nini Eva aliendelea kumjia akilini tena na tena. Hamu ya kuendelea kummiliki ilimjia. Hakuona pingamizi katika hilo. Kuyasikia maneno makali kutoka kwa Eva, kulimuumiza. Kulimkera.

“Pengine, kuna mtu anayesababisha usinione kama mwanaume anayekufaa” 

Eva alimtolea macho, mapigo ya moyo yakianza kumwenda mbio.

“Maybe, you’re in love with me ila hujalijua hilo.” 

Eva alianza kuhisi anazungumza na kichaa.  Akapayuka, “naondoka, mimi na wewe hatudaiani kitu. Hizo hisia zako siyo zangu.”

Alijaribu kumpita Dokta Masanga na kuufuata mlango. Hakuzuiliwa. Aliufungua mlango na kuubamiza nyuma yake. Aliziteremsha ngazi kwa mwendo wa haraka. Yumkini, hakutaka kuonekana maeneo yale muda kama ule, akiwa peke yake.

Alipoifikia ghorofa ya chini, simu yake ilitoa mlio wa kuingia kwa ujumbe. Akaifungua huku akiendelea kutembea kwa haraka. Ulikuwa ujumbe wa Rumi ukimjulisha juu ya uwepo wake kwenye mgahawa wa chuo kama walivyoahidiana simuni. Mgahawa ambao haukuwa mbali na jengo aliloliacha.

Aliijibu haraka kuwa yu karibu kufika eneo hilo. Kabla hajairudisha simu mkobani. Ujumbe mwingine uliingia. Akaufungua kwa pupa. 

Nakusubiri hapa ofisini now, au kesho Bwana Rumi Dago naye aanze kupokea salamu zangu. Nina miwani yako hapa. Don't play smart with me.

Eva alisimama ghafla. Mkono uliokuwa na simu ulianza kutetemeka kupita maelezo. Alifumba macho, akauruhusu mdomo wake umsaidie kupumua. 



Ikirai iliyoingia simuni ilimvuruga zaidi. Makwapa yalilowa jasho, akahisi tone la haja ndogo likidondoka kwenye nguo yake ya ndani. Hakuelewa dhamira ya Dokta Masanga.

Huu ujumbe una maana gani? Aliihoji akili yake kana kwamba ilisaidiana kuandika ujumbe na mwonja tamu yake.

Aliganda mithili ya kinyago kilichokosa mteja dukani. Alijikuta akisahau kuwa Rumi alikuwa mgahawani akimsubiri. Alijitahidi kujizuia asilie, lakini alishitukia michirizi ya machozi ukibarizi sehemu ya chini ya mboni zake. Akayapangusa na kuvuta kamasi.

Akaingia kwenye uwanja wa kuandika ujumbe kwenye rununu yake. Hakujua cha kuandika. Akaandika na kufuta si chini ya mara tano. Hatimaye, akaandika na kutuma: 

Una maana gani?

Hakujua kama alichofanya ni sahihi au la. Hakutaka kumtibua zaidi Dokta Masanga. Alihofia kukosa pwani na bara. 

Baada ya sekunde chache, simu yake ilifanya mtetemo. Vidole vilimtetemeka kama mtu anayetunga uzi kwenye tundu la sindano gizani. Alivuta pumzi yenye sauti iliyopoteza matumaini. Akaufungua ujumbe.

Mbona hufiki?

Ni Rumi.

Haraka, Eva akaujibu ujumbe ule: 

Nakuja. Niliingia washroom.

Huku akihisi kufungwa mawe miguuni, Eva alijaribu kupiga hatua za haraka mithili ya askari jeshi aliye kwenye gwaride la mwendo wa haraka.

Alipofika mgahawani haikumchukua muda, akamwona Rumi, aliyekuwa na simu mkononi. Akaondoa mlio kwenye simu yake.  Akaumba tabasamu bandia. Akamsogelea. 

“Hello,” alimsalimu, huku akiibwaga pochi yake ya hudhurungi pamoja na simu juu ya meza ya mbao iliyovishwa kapeti chakavu.

Akavuta kiti na kuketi. 

Rumi aliinua uso na kumtazama pasina kutia neno. Akaiweka simu mezani na kuvitenga viwiko vyake mezani. Sura yake ilifadhaika mitihili ya ndugu anayesubiri taarifa za mgonjwa aliyepo chumba cha wangonjwa mahututi.

Siku zote, Rumi alipomwona Eva basi alichangamka kama samaki aliyekatwa shombo kwa ndimu. Siku hii ilikuwa ni tofauti kabisa kwake. Alishindwa kabisa kuzificha hisia zake. Eva alilitambua hilo.

“Kuna tatizo?” Eva alihoji huku akitupia macho kwenye simu yake, akitaraji kupokea ujumbe kutoka kwa Dokta Masanga.  

“Kuna jambo unanificha Eva,” Rumi alisema, huku akiondoa viganja vyake mashavuni. “Ni lini umeanza kunidanganya?”

Eva alichezesha ulimi mdomoni kama mtoto mdogo aliyewashwa mapengo yaliyoanza kuota meno. Hakujua ajibu nini. Swali lilisukwa mfano wa fumbo. Kama Rumi amejua kuwa kuna kitu amefichwa, yumkini kitu hicho ni kitendo alichofanya na Dokta Masanga ofisini. Eva alitaka kuipangua hoja hiyo, lakini hoja nyingine ikapita kichwani mwake, kwamba, huenda Rumi amejua tu kuwa muda ule Eva alitoka ofisini kwa Dokta Masanga. Ikamlazimu kupiga kimya. Aliposhindwa kutazamana na Rumi, akainamisha kichwa chini kwa sekunde kadhaa. Alipoinua uso, machozi yalionekana kutota machoni pake. Alipojaribu kuyazuia kwa kufumbo macho, ndipo yakatumbuka na kutengeneza mfereji mashavuni.

“Sina ninachokuficha, Rumi,” Eva alijibu kwa sauti ya chini, yenye kukwaruza.

“Una hakika?”

“Unahisi kuna jambo nakuficha?”

“Ndiyo.”

Mungu wangu! Amegundua jambo huyu? Eva aliwaza. Hakuongeza neno. Akabaki amemtumbulia macho Rumi.

Rumi akaendelea, “Kwa nini hutaki kuniambia mtu uliyeongea naye jambo hili?” 

Eva alishusha pumzi mithili ya mpiga mbizi aliyeibua kichwa toka kwenye maji yenye kina kirefu. Swali la Rumi lilimpunguzia kihoro moyoni. Walau, alihisi kashfa kubwa haikuwa imegundulika.

“Nikujibu mara ngapi?” Eva alijikaza kutoa sauti. “Na kwa nini unishuku mimi tu? Una hakika wewe pia hujamweleza mtu yeyote?”

“Mimi naelewa hatari ya hili jambo. Siwezi kumwambia mtu yeyote.”

“Sasa ni nani asiyeelewa hatari hiyo? Mimi ni mtu mzima kama wewe. Jifunze kunisikiliza na kunielewa.”

Rumi alipandisha mabega yake juu. Akaingiza mkono kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake na kuchomoa pochi. Akatoa pesa na kurudisha pochi mfukoni. Akamwita mhudumu aliyekuwa akipita jirani. Akampatia pesa na kusema, “Pesa ya juisi na…” Akarudisha macho yake kwa Eva. “Utakunywa nini?”

“Hapana. Sinywi chchote.” Eva alimtazama mhudumu na kufanya tabasamu hafifu usoni. “Ahsante.”

Rumi alirudisha macho kwa mhudumu. “Niongeze maji. Yasiwe ya baridi sana.”

Baada ya mhudumu kuondoka, Rumi akaendelea, “Dokta alikutafuta tena?”

“Anitafutie nini?”

Rumi alipigwa butwaa. Majibu ya Eva yalimshangaza. Haikuwa kawaida yake kumjibu kwa ghadhabu namna ile.

“Kwani siku zote amekuwa akikutafuta kwa jambo gani?” Rumi aliongeza. 

“Angenitafuta ningekwambia.”

“Nina hofu kubwa juu yako. Majibu yako ni kama ya mwanasiasa anayehama chama, jinsi unavyoonesha kila dalili za kukwepa utekelezaji wa mikakati yetu.”

Eva alitupia tena macho kwenye kioo cha simu yake. Hakuona ujumbe wowote. Akamtazama Rumi kwa sekunde kadhaa. “Hivi huniamini?”

“Sijasema kama sikuamini, bali maelezo yako yamepindapinda kama kona za Nyang'oro. Una jambo hutaki kuniweka wazi, mpenzi.”

Mhudumu akaweka chupa ya maji mezani.

Rumi alinyamaza na Eva akapiga kimya.

Mtungo wa maswali ulizidi kujirefusha kichwani mwa Rumi. Kila jibu lilitengeneza matawi kadhaa ya maswali mapya. Ni dhahiri utata wote wa Eva ni katika kutafuta kuficha jambo, na kwamba haoneshi tena ari ya kumkamata Dokta Masanga. Kwa nini amefikia hatua hiyo? Kipindi walichokuwa kwenye mahusiano, kilimtosha Rumi kumsoma Eva na kumjua tabia.

Baada ya kimya kirefu, Eva aliburuza kiti kwa nyuma na kuinuka. Akakwapua pochi yake juu ya meza na kuondoka. Rumi akabaki akimtazama kwa nyuma. Hakuamini namna Eva alivyobadilika.

Eva aliamua kuondoka kama ishara ya kukwazwa na Rumi ilhali akitambua fika ni kweli alitenda uovu. Alihofia kuendelea kubaki pale mezani kumfanya Rumi azidi kudadisi ukweli wa mambo, kitu ambacho kingemfanya anase mtegoni. Akiwa njiani, aliendelea kuisikia sauti ya Rumi kichwani mwake: “Kwa nini hutaki kuniambia mtu uliyeongea naye jambo hili?”

Japo aliendelea na msimamo wake uleule, lakini moyoni, alitambua yupo aliyemwambia kuhusu Dokta Masanga. Mtu huyo ni Zena. Kumfikiria Zena kukaanza kubadili mawazo yake.

Kuna uwezekano Zena alinizunguka? Eva alijiuliza kichwani.

Eva anatambua Zena hampendi pia Dokta Masanga. Hakuwa na majibu ya kumfanya amtuhumu Eva kumgeuka kwa mtu asiyemkubali. Pamoja na hayo, tayari taa nyekundu ilianza kumulika kichwani mwake. 

****

Saa kumi na mbili jioni, walianza kurudi hosteli. Vyumba vilianza kuchangamka kwa soga na michapo ya hapa na pale. Sauti hafifu za redio zilizofunguliwa kisirisiri zilinogesha zaidi. Kwa baadhi ya vyumba, waliishi wanafunzi wannewanne, na vyumba vingine walifika mpaka wanane. Vyumba vichache tu chuo kizima, waliishi wawili. Eva alibahatika kuishi kwenye moja ya vyumba hivyo. Kila jengo moja la hosteli lilikuwa na vyumba vinane, ingawa kuna majengo mengine yalikuwa kama bwalo kwa ukubwa yakigawanywisha vyumba.

Meza moja kubwa na takribani viti vinne vichakavu vilipangwa kwa kutazamana. Juu ya meza, upande wa kushoto, kulikuwa na jagi la umeme, vikombe vya chai, kibobo cha sukari, pamoja na boksi la majani ya chai. Upande wa kulia, yalizagaa madaftari pamoja na vitabu.

Kutoka katika kitanda cha juu, kati ya viwili vilivyopandana, upande wa kushoto mwa chumba, Zena aliyekua amelala fofofo aliendelea kukoroma kama mashine ya kukoboa nafaka. Sauti ya kukoroma ilikoma ghafla baada ya kuvutwa mguu wa kulia na mtu aliyekuwa amesimama sakafuni. Akiwa bado na mawenge ya usingizi, alikurupuka na kukaa kitako. Akakutanisha macho yake na Eva. 

“Kuna nini tena?”

Eva alimtazama Zena bila kusema neno.

“Mbona sikuelewi?”

“Naomba tuzungumze.”

Pamoja na Eva kujaribu kuficha ghadhabu zake moyoni lakini uso wake ulimsaliti. Zena alihisi uwepo wa balaa. Akashuka kitandani kwa kutumia ngazi ndogo ambazo hutumika kukwea juu ya kitanda. 

“Nakuja,” Eva alisema na kutoka nje.

Alikwenda bafuni na kunawa uso kwa maji ya baridi. Akarudi chumbani huku akijifuta maji kwa upande wa khanga aliyoifunga kifuani. Akavuta kiti kwenye meza na kuketi.

“Haya hebu niambie, ikawaje kuyabeba mambo ninayoteta nawe, na kwenda kuyabwaga huko nje?”

“Ishia hapo hapo!” Zena alinyoosha mkono wa kulia kumnyamazisha Eva. “Nimebwaga nje jambo gani?”

“Umeongea nini na Dokta Masanga?”

Zena alibaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa. Kisha akacheka kwa dharau. “Tangu lini mimi na Dokta Masanga tukawa na mazungumzo?”

“Nani aliyemdokeza kuwa tunakwenda kumkamata?”

“Mungu wangu! Ina maana amejua?” Zena alirusha swali.

“Mimi nakuuliza wewe, nawe unaniuliza mimi tena?”

 “Naapa kwa jina la Mungu, sijazungumza na mtu yeyote kuhusu issue yako.”

Ikawa zamu ya Eva kuachia cheko la kebehi huku akibetua mdomo wake upande. “Zena, usinifanye miye mtoto. Lile jambo sikumwambia mtu yeyote zaidi yako. Unadhani Dokta aliota ndotoni?” 

“Nakuhakikishia sijamwambia mtu, Eva. Nimwambie mtu kwa manufaa gani? Vitu vingapi navijua kuhusu wewe na sijawahi kunyanyua kinywa changu kuvisema? Kama niliweza kumficha kabisa Rumi, kuhusu yule jamaa’ko wa first year, uliyelala naye siku ile tupotoka club usiku, nitakuwa chizi kama nitakwenda kuyazagaza haya ambayo unapambania maisha yako.”

Eva alinywea baada ya kukumbushwa moja ya kadhia alizopata kuhifadhiwa na Zena. Ilitokea miezi kadhaa nyuma, ambapo wakiwa muziki usiku, Eva alikutana na huyo kijana aliyekuwa anammendea kwa muda mrefu. Siku hiyo akanasa. Ilikuwa ni baada ya kupata chupa kadhaa za pombe, akajikuta akikubali kuondoka naye na kwenda kulala nje ya hosteli alikopanga kijana huyo.

“Hata mimi nina yako mengi tu nayajua, na sijawahi kuyaeneza kwa mtu yeyote,” Eva alisema akiwa ameishiwa hoja.

“Basi nd’o hivyo, hakuna aliyeyasema ya mwenziye.”

“Hapana, Zena. Kwa hili, hapana. Swali langu ni moja tu, amejuaje?”

“Nilikukanya, Eva, uwe makini. Nilikwambia hawa watu wanajuana na wengi. Wanaweza kutonywa na watu hata usiowategemea. Unadhani Dokta hawezi kuwa na watu hukohuko TAKUKURU? Hebu kwanza niambie, amejuaje?”

“Unaniuliza tena mimi?” Eva alisaili kwa mshangao. “Laiti ungejua madhara ya kitendo ulichokifanya-sawa tutaoneshana.”

Eva aliondoka eneo lile. Akafungua mlango na kutoka nje. 

Zena alibaki amebung’aa macho huku mikono ameiweka kiuononi. 

****

Pilika za wanafunzi kwenye korido zilikuwa nyingi. Wengi walitembea kwa vikundi kuanzia watu wawili hadi watano. Walicheka na kupiga soga za kila aina ambazo rika moja likikutana husogoa. 

Eva alivaa sketi fupi usawa wa magoti. Kitambaa cha shifoni ya waridi iliyopoza ilinoga zaidi na blauzi rangi nyeusi ya maua myeupe aliyochomekea. Rangi ya mkanda wa kahawia ulienda sambamba na viatu vya middle hills. Akaonekana maridadi zaidi.  

Alichagua moja ya vimbweta kilichokuwa wazi. Akaketi. Alipeleka akili yake mbele na nyuma. Alishindwa kuingia darasani siku hiyo. Alilala usingizi wa mang’amung’amu. Alichokuwa anasubiri ni kupambazuke tu, saa za jioni aende kwa Dokta Masanga. Hakuwa na uamuzi mwingine wa kufanya zaidi ya huo. “Sina budi,” Eva alisema kwa sauti. 

Wakati ni ukuta, muda ukawadia.

“Ngo ngo ngo.” Vidole vya Eva viligonga na kutoa sauti. 

“Karibu, pita ndani.”

Eva alinyooka mpaka kwenye meza ya alipoketi hasimu wake. Hakusubiri kukaribishwa kiti, akakivuta na kuketi.  

Dokta Masanga alikuwa kimya. Hakusema neno. Akaendelea kuandika kwenye tarakilishi yake. 

Eva akahangaika kama kuku aliyelazimika kutaga juu ya sakafu. Hakujua aanze kuuliza kuhusu ujumbe au amwambie nimekuja. Akaikumbuka kauli, 'Mpe Rumi salamu zangu.'  Aliyapeleka macho juu na chini kama mtu afanyaye hesabu ngumu kwa kutumia kichwa.

Kimya cha dakika mbili kilizibuliwa na sauti ya kikohozi kikavu cha Dokta Masanga. Akachukua chupa ndogo ya maji iliyokuwa pembeni ya meza. Aliifungua na kuweka mdomoni.

Ni kama alikusudia kuipa mateso ya fikra akili ya Eva. Hakika alifanikiwa. Eva alihisi Dokta Masanga alijua mpango wake wa kumkamatisha TAKUKURU. Na ndiyo maana akaambiwa afikishe salamu kwa Rumi. Kama amejua basi nitakataa, Eva aliwaza, akiangalia maji yalivyoshuka kwenye koo la Dokta Masanga.

"Samahani kwa kukuweka mrembo," Dokta Masanga alisema akiweka chupa ya maji pembeni. "Umefanya uamuzi wa busara kuja."

"Sawa, lakini jana ulimtaja Rumi," Eva alisema kwa tuo na kuendelea, "Sijajua Rumi anaingiaje kwenye hili."

"Mbona una haraka, mrembo?" 

Aliinuka kwenye kiti na kuzungusha funguo iliyopachikwa ndani ya kitasa. Akamsogelea Eva na kunyanyua kitanga cha mkono wake na kukibusu.

 "Najua kuhusu Rumi, ulifikisha salamu zangu?"  

Eva akawa dhaifu kupitiliza. Akabaki ameunyosha mkono kama dada aliyesubiri kuvishwa pete ya uchumba, kasoro yeye hakulivaa tasabasamu.

Kauli ya Dokta Masanga ikamvuruga zaidi. Alihisi homoni ya adrenali ikimwagika na kumnyong'onyeza viungo vyake.

"Nina mapenzi ya dhati kwako, Eva." Dokta Masanga alisema kwa sauti nzito iliyosheheni ushawishi.

"Rumi-"

Alizunguka na kuvuta kiti, na kuketi wakitazamana. Akaingiza mkono ndani ya sketi ya Eva na kuyaminyaminya taratibu mapaja kama mteja achaguaye parachichi sokoni.

Eva alitulia tuli mithili ya swala aliyeng'atwa na simba kooni. Hakufurukuta. Akasubiri bomu kumlipukia. 

Eva aliwaza kauli itakayofuatia ni: Ulidhani utaweza kunizunguka wewe na Rumi wako? 

"Najua kama…najua," Dokta Masanga alishikwa na kigugumizi kwani mkono wake ulifika mbali zaidi. Maneno yakamtoka. "Rumi ni mpenzi wako."

Eva alishusha pumzi za aina mbili. Ya kwanza kwa kauli aliyoisikia kumbe hakujua mpango wao.  La pili, mhemko alioupata kwa mkono uliokuwa bado ndani ya sketi.

Akajikaza na kunyanyua mdomo ambao ulikua mzito utadhani samaki aliyenaswa kwenye chambo. "Nina mpenzi, ndiyo. Hiyo ni sababu tosha ya kuachana na huu mchezo."

"Mimi sijali kuhusu Rumi. Wala sikuzui kuendelea naye."

"Una maana gani?"

"Endelea na Rumi, huku na mimi utaendelea kunipa. Ondoa shaka. Kwa vile nakupenda." 

Aliingiza mkono wa pili. Akaminya sehemu za mapaja zilizotuna kwa kukaa. Akamwinua Eva ambaye alifuata kila alichofanyiwa kama roboti iliyosetiwa. Akamwinamisha kwenye meza na kumshusha nguo ya ndani mpaka usawa wa miguu. Akafungua mkanda wa suruali yake na kuiteremsha kidogo. Akafanya zoezi la sebene isiyo na watazamaji. Dakika tatu hazikuzidi sebene kufika kaditama, akagugumia na kutoa sauti kama ya kuku mwenye mdondo.

Hakujali kama sebene lile wote walifurahia au la! Alimradi alijua kucheza peke yake, hayo mengine hayakumhusu. Eva akapandisha nguo yake ya ndani ambayo ilitatuka kidogo kwa kuvutwa kwa pupa. Akaichomekea sketi yake vizuri, na kuokota pochi ambayo ilikuwa sakafuni.

Dokta Masanga alikwishavaa. Akamalizia maji kwenye chupa yake. Akamtazama Eva kwa jicho la mahaba. 

"Wewe ni mtamu sana." Akauendea mlango na kufungua. "Nifurahishe, nami nitakurahisha hapa chuoni."

Eva akajutia kwa kitendo chake cha kuliwa mara ya pili na Dokta Masanga. Akauma meno kwa hasira. 

"Kwani dokta, hapa si tumemalizana?" Eva alihoji kwa sauti ya kitetemeshi. "Sipo tayari kuendelea na mchezo huu."

"Ebo! Unakuwa mgumu kuelewa.” Aliachia tabasamu iliyomchefua, Eva. “Sikiliza huu mfano: Mimi ni kama simba na wewe ni kama swala. Na chuo ni manyasi. Mimi lazima nile nyama ya swala, wewe lazima ule nyasi. Swala asipokula nyasi, ina maana simba atakosa kitoweo. Na sehemu ya malisho anayotumia swala, simba nd’o mfalme wa mbuga. Kwa hiyo, kama unataka kuacha, labda uhame chuo." 

Akavuta kiti na kuketi. "Sijui umenielewa?"

Eva alinyanyuka kwa hasira na kuondoka. Alikuwa ameyavulia nguo maji ya chumvi, alipokoga yakamwachia alama na utamu tamu wa chumvi ambao hakujua atautoaje. 

Alijichukia kwa maumuzi ambayo asingeweza kurudi nyuma. Alihisi harufu ya jasho la Dokta Masanga kwenye mwili wake. Mama yake aliwahi kumwambia, 'Mwili wako ni hekalu. Sio kila mtu anaruhusiwa kuingia. Inatakiwa uheshimu hilo.' Kumbukizi hizo zikamtia hatia ya kuyasaliti maneno ya mama yake aliyoyaishi muda mrefu. Na vilevile, kujisaliti mwenyewe. Pale binadamu anapojisaliti mwenye huchukua uamuzi gani? Alijiuliza. 

Eva alijiaminisha ile ni siri ya wao wawili tu. Hakuna mtu mwingine aliyeijua. Suala la Dokta Masanga kujua uhusiano wake na Rumi likamvuruga. Alijuaje? Ni swali ambalo alipaswa kumwuliza Dokta Masanga. Angeulizaje ilhali muda anasemeshwa alipumua kwa mdomo? 

Eva aliwaza huku akitembea kuelekea msalani, 'Habari ya mimi na Rumi hapana shaka baadhi ya watu wanajua. Nani sasa amemwambia Dokta Masanga? Kama Dokta Masanga ameweza kujua kuhusu hilo basi anauwezo wa kujua mengi zaidi.'

Aliyapita madarasa na kuingia msalani karibu na geti la kutokea chuo. Akaminya maji yaliyopita kwenye bomba. Kuna hali ya mashaka ikamkumba. Aliweka kidole chake. Alihisi kuteleza. Ni ada kuiona hali hiyo pale anapokuwa kwenye siku za hatari. 

“Hapana, hapana,” Eva alilalama kwa takriri.




Baada ya Eva kuinuka na kuondoka kwa kisirani pale mgahawani, Rumi alibaki akiukodolea macho mgongo wa yule mpenzi wake huku akihisi kitu kama rojo la mshumaa kikitambaa juu ya moyo wake.

Hakuelewa. Kile alichofanya Eva hakikumwingia akilini. Na kilichofanikiwa kuingia, hakikumtosha. Badala yake, kiliacha ombwe kubwa ambalo akili yake makini ilihitaji kujitawanya zaidi ili kulijaza ufahamu, apate kuelewa kilichokuwa kinatokea.

Tabia ya Eva ilikuwa imebadilika sana tangu siku ile waliyokosa kumnasa Dokta Masanga. Aliamini kitendo cha Dokta Masanga kukataa kuongozana na Eva hadi kule Miami Hotel siku ile, kilimaanisha alijua alitegewa mtego. 

Nani kamtonya?

Hakutaka kubaki sana kwenye hili. Akili yake ikarudi kwa Eva. 

Kawaje, Eva?

Alishusha pumzi ndefu. Akapiga funda jingine la maji. Akajilazimisha kufikiri bila mhemko. Halikuwa jambo rahisi. Kilichokuwa kikijijenga kwenye hisia zake wakati ule hakutaka kabisa kukipa ubia na akili yake. Wala, hakutaka kufikiria kitakachozaliwa kwenye ubia huo, iwapo ataruhusu utokee.

Akajikita kuichambua tabia ya Eva. 

Maneno three stories yalimgonga akilini. Yamekuwa yakimgonga tangu wamalize mazungumzo yao na Eva siku ile alipotoka ofisini kwa Dokta Masanga. Na leo, yameigonga tena akili yake wakati akijaribu kumsaili mpenzi wake, na majibu aliyotoa kabla hajamsusia meza. Jambo ambalo hajawahi kumfanyia hata siku moja hapo kabla. 

Three Stories.

Maneno haya yalitoka kwenye somo la ziada kwenye kozi yake pale chuoni. Critical Conversations, yaani 'Maongezi Magumu' haikuwa kozi ya msingi wala ya lazima kuisoma pale chuoni, ila ilikuwa inaongeza pointi za ziada kwenye mtihani. Siyo wanafunzi wengi walioichagua kozi hii. Yeye aliichagua. Hakuwahi kutarajia kuona uhalisia wa kile alichokuwa akikisoma kwenye kozi ile kabla ya mtanziko huu uliochipua kati yake na Eva.

Mwalimu wao aliwafundisha, kwenye maongezi magumu siku zote wajaribu kutafuta moja kati ya hadithi tatu kutoka kwa mtu unayejadiliana naye. Ukishajua anaangukia kwenye hadithi gani, basi utaujua msimamo wake kwenye suala mnaloongelea. Na ukiujua msimamo wake, utajua uupeleke vipi mjadala wenu kwa maslahi yako.

Akauma midomo.

Alizikumbuka wazi wazi hizo hadithi tatu kichwani mwake. 

The Villain Story, yaani Hadithi ya adui.

The Victim Story, yaani Hadithi ya mhanga.

The Helpless Story, yaani Hadithi ya asiye na namna. 

Kila moja ilikuwa ina tafsiri mahsusi kwenye msimamo wa mtu unayejadiliana naye au unayefanya naye mazungumzo. 

Tabia ya Eva inamuweka kwenye hadithi gani? Alijiuliza, kisha akatafakari zaidi, 'Hadithi ya adui ni pale mtu anapoamua kumlaumu kila mtu isipokuwa yeye mwenyewe kwenye suala lililopo mezani. Yaani yeye hana kosa lolote bali ni mtu mwingine ndiye mwenye makosa, mtu mwingine ndiye adui (villain), na sio yeye.  Hata kama kiuhalisia na yeye alikuwa ana mchango kwenye suala lililopo.'

Alikumbuka jinsi Eva alivyomkaripia pale alipoulizwa kwa nini hakumrekodi Dokta Masanga kule ofisini kwake, “Si tulikubaliana ningerekodi akifika chumbani?”

Kwa maana nyingine, Eva alikuwa anaeleza hilo halikuwa kosa lake, bali la Dokta Masanga kwa kutompeleka Miami Hotel ili akamrekodi.

Anakwepa kitu? Alijiuliza. 

Akajiuliza tena, Hadithi ya mhanga, je? 

Akakunja uso. Hii ni pale ambapo mtu anapoamua kuonesha kuwa kila mtu anamwonea yeye bila sababu. Yeye ndiye mnyonge aliyeonewa.

Akamung’unya mdomo.

Akaifikiria hadithi ya asiye na namna. 'Huwa pale mtu anapoamua kulaumu suala lililopo mezani kwenye mfumo au mwenendo wa mambo nje ya uwezo wake. Kama sheria inakataza watu kuoa au kuolewa chini ya umri fulani, basi hakuna la kufanya zaidi ya kukubaliana tu na hali hiyo. Jibu rahisi kwa watu wa namna hii ni, mikono yangu imefungwa na sheria. Sina namna.'

Akaguna.

Ni wapi Eva anaangukia? 

Akili ilianza kumwelekeza kwenye jibu alililokuwa analitafuta.

“Oyaa dogo, kuna mitihani zaidi ya hii ya hapa chuoni huko duniani! Usiwaze saaana!” Sauti ilimgutusha.

“Ah, mambo vipi kaka?” Alijilazimisha kutabasamu huku akimsalimu yule jamaa aliyemsemesha.

Jamaa akamcheka. “Poa tu mwana. Usiwaze sana b'ana...mitihani ya chuo ni rahisi kuliko ya maisha."

Rumi alibaki akimtazama yule jamaa aliyeendelea na safari yake kuelekea nje ya mgahawa, mkononi mwake akiwa amebeba chakula kwenye kibebeo cha plastiki. Kitu kikamgonga akilini kuhusu yule jamaa.

“Eeh, bradha Juli!” alimwita huku akiinuka.

Juli alisimama na kugeuka .“Unasemaje dogo?”

“Na…naomba kukuuliza kidogo...” Rumi alisema akimfuata. 

Juli akawa anamfuata huku akimwashiria akae tu pale kitini.

Wakaketi wakitazamana.

Julius Kamili alikuwa na umri mkubwa kuliko wanafunzi wote darasani kwao. Na, alikuwa ana uelewa mkubwa wa masomo. Alikuwa amerudia kozi ile kwa mwaka mmoja, ikiwa baada ya kukaa nje ya masomo kwa mwaka mwingine mmoja kabla ya hapo. Kimsingi, asingetakiwa kuendelea kuwa pale chuoni akisoma na wao kipindi kile, iwapo angemaliza masomo yake kwa wakati.

Kisa chake kilikuwa kikinong'onwa kwenye makundi mbali mbali ya kujisomea pale chuoni.

“Okay Rumi, whats up?” aliuliza.

Rumi hakujua aanzie wapi. Alipomwita alikuwa amehemkwa na kilichokuwa kikipita kichwani mwake wakati ule, na sasa aliona kuwa hilo halikuwa jambo la busara.

“Aah… hivi… ni kweli kuwa ulirudia mwaka kutokana na sakata la kugombea mwanamke?” Swali liliponyoka. Sivyo kwa namna aliyoikusudia. Dakika hiyohiyo alijutia. Si swali ambalo yeye angependa kuulizwa.

Julius alicheka kwa fadhaa huku akitazama pembeni na kutikisa kichwa kwa masikitiko.

“Mi’ n’lidhani unawaza kilichokuleta chuoni, kumbe unawaza porojo za chuoni?” aliuliza huku bado akitabasamu. Hakuonesha kuchukia. 

Rumi akajipa ujasiri. “Noo! Of course sikuwa nimekaa hapa kuwaza hayo, ila limenijia tu hili swali baada ya kukuona.”

“Kwa nini unataka kujua?”

“Look bro, sorry kama nimekukwaza. Sikupaswa kukupotezea muda wako juu ya hili...”

“To the contrary, hili ni suala ninalopenda kuliongelea anytime!”

“Oh? Okay...kwa hiyo...”

“Nataka tu kujua ni kwa nini umeona ni muhimu uniulize juu ya hili...na kwa nini sasa.”

“Aam, nataka niandike research yangu kuhusiana na suala la rushwa za ngono vyuoni, na nilihisi labda suala lako—”

Julius alimkata kauli kwa kicheko kikubwa.

Rumi akamtupia swali kwa macho kuhusu kicheko kile.

“Tafuta topic nyingine mdogo wangu! Hutapata mwalimu yeyote wa kukusimamia kwenye hiyo topic nakwambia!” 

“Kwa nini?”

Julius alimtazama kama vile alikuwa mwehu. “Hilo ni la kuuliza? Hapo unapiga ikulu wewe! Unadhani kuna mwalimu atakayetaka utafiti huo uingie kwenye kumbukumbu na makabrasha ya CHUKIM? Niulize mimi.” 

Rumi akajiweka sawa kitini akimtazama Julius aliyeongea kwa hamasa. Akamtupia swali, “Kivipi bro? Hiyo ndiyo sababu ya wewe kusimamishwa chuo na kurudia mwaka baadaye?”

Julius akaachia sauti ya nusu mguno, nusu kicheko. “Hapa rushwa ya ngono ndio mahala pake dogo,” 

Rumi alihisi mapigo ya moyo yakianza kushindana kasi.

“Hawa madokta?” Julius alimwandalia jibu kwa swali. “Hawa ndiyo vinara wa kuwatafuna mabinti hapa chuoni! Na si kama watu hawajui au hawaoni. Wanajua na wanaona!”

Rumi alibaki akimkodolea macho.

Wazo la kuwa Julius angeweza kuwa na msaada kwake lilimgonga akilini mara tu alipomwona pale mgahawani. Na ndilo lililomsukuma kumwuliza lile swali. Aliamua kuwa makini.

“Kwa hiyo, wewe uliona usikae kimya, ukajaribu kusema... ndio kikakukuta kilichokukuta?”

Julius alimkazia macho kwa muda. “Sikiliza Rumi. We’ bado mdogo. Usipoteze sehemu kubwa ya maisha yako kutaka kuamsha yaliyolala. Cha mno, utafelishwa tu na hiyo pepa  yako ikatupiliwa mbali. Nakwambia haya kutokana na uzoefu. Acha hii mambo kabisa, aisee!”

Rumi alidadisika. “Mbona unaongea kama vile hili ni jambo lisilopaswa kuongelewa kabisa, bro? Ni kipi kilichotokea kwako kwani? Hizi habari ninazozisikia humu chuoni kuhusu wewe, ni za kweli eeh?”

“Ukitumia kisa changu kama sehemu ya huo utafiti wako wa kimasomo siyo tu utafeli, bali pia hutagraduate kabisa hapa. Mi’ nakwambia!”

“Kama hutajali ningependa kukisikia. Halafu, miye niwe mwamuzi juu ya kuendelea au kutoendelea na hili ninalotaka kulifanya.”

Julius alimtazama kwa muda. “Najua kuna kitu hujaniweka wazi dogo. Niko smart enough kuliona hilo. Lakini nitalichukulia hili kama ni msaada kwa mwenzangu kwenye somo ambalo mimi nalimudu zaidi darasani kuliko yeye, sawa?” 

“Sawa, bro!”

Ndipo Rumi alipokisikia kisa cha Julius Kamili kutoka kwenye kinywa chake mwenyewe. 

Miaka miwili nyuma, alikuwa na mpenzi wake pale chuoni. Walipendana sana. Yeye aliyamudu sana masomo, na alimsaidia mpenzi wake kwenye baadhi ambayo alihitaji msaada. Kisha, akatokea mwalimu mmoja akaamua kuwa yeye alimpenda zaidi mpenzi wake kuliko Julius mwenyewe. Balaa likaanzia hapo. Mpenzi wake alimshirikisha kwenye hilo sakata. Akamthibitishia kuwa hatokubali ombi la mwalimu huyo, na Julius akamthibitishia mpenziwe kuwa atakuwa pamoja naye mpaka mwisho.

“Kilichofuatia, Mwanjaa akakamamatwa kwenye somo la yule mwalimu,” Julius alisema. 

Rumi alifumba macho kuisikitikia hali ile. “Loh! Ikawaje?”

“Maandiko yakawa wazi ubaoni. Atoe penzi au apigwe sup.”

“Doh, ikawaje tena?”

“Mwanjaa aligoma of course, na kwa kufuata maelekezo yangu, akaenda kushitaki kwa Dean.”

“Seriously?”

Julius akafyatua tena ile cheko-mguno yake, “Oh, yes! Chuo kilirindima hiki!  Mwalimu akaitwa na Dean. Hatujui kilichoongelewa, ila baadaye Mwanjaa akaitwa na kuambiwa kuwa kulikuwa kumetokea  makosa tu kwenye usahihishaji. Maksi zake zikatosha kuendelea na masomo bila kufanya sup.”

“Ah, aisee! Sasa vipi kuhusu ile kesi ya kuombwa ngono?”

“I asked the same question. Mwanjaa hakutaka kulikuza zaidi lile sakata. Suala la msingi lilikuwa ni maksi zake na sasa zilishatosha, si ndiyo? Ya nini kuyakuza?”

“Doh, aisee mlipambana! Sasa nini kikafuatia  tena?”

“We acha tu. Mtihani uliofuata? Darasa zima tulifeli somo lake.”

“Eeeh?”

“The whole God damn class, dogo,” Julius alisema kwa upole uliojaa ufahamu dhahiri wa kile alichokuwa anakiongea. 

Rumi aliguna tena kwa kuishangaa hali ile.

“Nd'o ujue, hawa jamaa ni nyoko dogo. Ina maana hapo darasa zima lilikuwa linakabiliwa na sup!”

“Sasa… mkakaa kimya tu?”

“Ah, kilichofuata ni full kuchanganyikiwa darasani. Taarifa zikaenea kuwa darasa lilikuwa linaadhibiwa kwa sababu ya Mwanjaa. Kamnyima  mwalimu tunda la Adamu na Hawa. Sasa, darasa zima litashikishwa adabu.”

“Siamini hiki ninachokisikia, Juli!”

“Sikia hii sasa,” Julius alisema. “Wakatumwa watu kwa Mwanjaa. Wakamwomba amkubalie mwalimu ombi lake ili maisha yasonge.”

“Amaa!” Rumi aling’aka. 

Julius akacheka.

“Pata picha nilivyong’aka mimi sasa! Nilipigana vikali dhidi ya hili. Mwanjaa alipigana vikali dhidi ya hili. Matokeo yake nd'o hayo, darasa zima tuka-sup.”

Rumi akatema tusi la nguoni kwa mshangao.

“Mbona hapo bado?” Juli akanogesha. “Taarifa zikaja sasa kutoka kwa mwalimu. Kuna watu wanajitia wajanja. Anakamata darasa zima kwenye sup. Tusubiri matokeo tuone nani mjanja sasa.” 

“Mmh! Hivi inawezekana kweli hiyo? Kwa nini msiende kwenye vyombo vya dola kama TAKUKURU?” Rumi alihoji.

“Kwa ushahidi upi dogo? We’ tulia nikupe hali halisi ili usije kufanya makosa kama yangu!” 

Alitulizwa. Akatulizana. 

“Mwanjaa akawa kwenye shinikizo kubwa sana kutoka kwa wanafunzi wenzetu, akubali ombi la mwalimu. Kutoka kwangu, asikubali, liwalo na liwe. Na kutoka kwenye mtima wake mwenyewe, alikuwa njiapanda. Maelewano yetu yakayumba sana. Nikaona isiwe taabu.”

“Ukafanyaje?”

“Nikamwibukia yule mwalimu kwenye baa ya chuo wakati akipata kinywaji na walimu wenzake. Nikampa makavu. Nikamchana kisawasawa kuwa anachofanya siyo sahihi. Alikuwa analazimisha ngono kwa mtego wa kufelisha wanafunzi. Unajua alisemaje? Alisema mimi ni kapuku tu na kwamba maisha yetu wote darasani yako mikononi mwake, kwa hiyo tuwe wapole tu."

Rumi alishika tama pasipo kutia neno. 

Julius akaendelea, “Nikataka kumtia vichwa palepale, ila baadhi ya wanafunzi wakawahi kunizuia. Wale walimu wenzake wakainglia kati. Wakaniambia niombe radhi haraka sana. Nikawachana na wao. Nikawaambia wote lao moja tu hapa chuoni.”

“Eh!”

Julius alitulia akiwa amemwaga tabasamu dhaifu .“Hapo ndipo nilipofukuzwa chuo, dogo. Kilichofuatia ni kuenea kwa hizo habari kuwa nimegombana na mwalimu kisa mwanamke. Not true! Nilikuwa napigania penzi langu.” 

"Daaah!"

Julius akafyatua cheko-mguno, “Penzi? Penzi CHUKIM?”

Akasonya.

Rumi akagwaya.

“Sasa kama ulifukuzwa, vipi leo uko hapa chuoni?”

“Ah, dogo, ni hadithi ndefu sana. Nilikata rufaa of course. Ilichukua mwaka kabla sijaruhusiwa tena kuja kumalizia digrii yangu. Ndiyo maana unaona niko nanyi hapa chuoni hivi sasa.”

Kimya kilitawala.

“Dah, sasa… ikawaje tena kuhusu hiyo sup yenu ya darasa zima?”

Julius akacheka kwa simanzi .“Sup yao sasa, siyo yetu. Mi’ sikuufanya tena ule mtihani. Nilishafukuzwa chuo.”

“Doh, pole sana, bro.”

“Sio ishu tena sasa. Ila kwa taarifa yako tu, darasa zima lilifaulu liliposapua, na Mwanjaa akiwemo. Unapata picha hapo?”

Rumi alichoka. Alibaki akimkodolea macho tu yule jamaa. Hakujua aseme nini. 

“I gotta go, man,” Julius alisema huku akiwa amekwishasimama. “Achana na hilo unalotaka kulifanya dogo.”  

Akaanza kuondoka na chombo chake cha chakula. 

Rumi alichanganyikiwa.

“Er, Juli!” alimwita tena. 

Julius alisimama, na kumgeukia taratibu.

What? Macho yake yalimwuliza.

“Huyo mwalimu aliyefanya udhalimu huo…aliishia wapi?” Rumi aliuliza.

Julius alimtazama kwa muda kidogo.

“Last time I checked? Kazi yake bado ilikuwa ileile, na jina lake bado lilikuwa lile lile…Dokta Tindo Masanga.” 

Akaondoka zake.

Rumi alibaki kinywa wazi.

****

Hubiri aliinua uso wake kutoka kwenye dondoo za kikao cha kila mwezi cha wakuu wa idara mbalimbali za TAKUKURU, ambacho mkuu wa idara yao huwa anahudhuria kwa niaba yao. Kitu kimoja kwenye dondoo za kikao kile kilimfanya ainue uso wake na kuitazama fremu ya picha iliyokuwa imetundikwa kwenye ukuta uliokuwa moja kwa moja mbele yake pale ofisini.

Badala ya fremu ile kuhifadhi picha au cheti fulani ndani yake, yenyewe ilihifadhi kipande cha makala ya gazeti ambayo kamwe hajataka kuisahau. Ndiyo kisa akaiwekea fremu kabisa pale ofisini kwake.

"RUSHWA YA NGONO YAWA KIAZI CHA MOTO KWA TAKUKURU". 

Ndicho kilikuwa kichwa cha habari ile.

Alimung'unya midomo na sura ikamkunjika pasi kujitambua, akiwa amekikazia macho kichwa cha habari ile iliyokuwa kwenye fremu pale ukutani.

Japo kutokea pale mezani kwake hakuweza kusoma maandishi madogo yaliyolala vyema chini ya kichwa cha habari ile, muktadha wake ulikuwa hai kichwani mwake.

Habari ile iliyotoka gazetini kiasi cha mwaka mmoja uliopita, iliibua tafrani kubwa ndani ya taasisi yao. Makala yalieleza kinagaubaga kwa jinsi gani TAKUKURU ilivyoshindwa kuzimudu kesi za rushwa ya ngono nchini, hususani kwenye sehemu za ajira, medani za kisiasa na vyuoni. 

Mwandishi alijituma vilivyo kwenye makala yale. Alitaja kesi kadhaa zilizowahi kufikishwa TAKUKURU na hatimaye zikashindwa kuwafikisha watuhumiwa panapostahili kwa kosa lile lile kutoka upande wa TAKUKURU, na hata waliofikishwa mahakamani, ushahidi kutojitosheleza kuwatia hatiani. 

Na mwaka mmoja baadaye, bado jinamizi la tafrani iliyowatafuna yeye na watendaji wenzake ndani ya taasisi bado lilikuwa linatawala hadidu za rejea za mikutano yao. Ndiyo maana, uongozi wa taasisi ukatoa hamasa kwa watendaji wake. Ukabuni tuzo maalumu kwa maafisa wa TAKUKURU. 

Ikapewa jina la “Tuzo ya Ngono.” 

Kila afisa wa TAKUKURU atakayefanikisha TAKUKURU kushinda kesi ya rushwa ya ngono alikuwa anapatiwa tuzo hiyo ikiwa ni cheti maalumu na zawadi ya fedha. 

Milioni tatu taslimu.

Na bado, hakuna aliyewahi kuinyakuwa tuzo hiyo.

Alijizungusha kwenye kiti chake na kuutazama ukuta uliokuwa nyuma yake. Huu ulikuwa umetapakaa fremu kadhaa mithili ya ile iliyokuwa kwenye ule ukuta wa mbele yake. Tofauti ni kwamba, fremu za kwenye ukuta huu, zilihifadhi  vyeti mbali mbali vya utendaji uliotukuka kazini, vyeti vya kuhitimu kozi mbali mbali za kitaasisi ndani na nje ya nchi, na picha kadhaa zikimwonesha akiwa ameshikana mikono na viongozi wakuu wa taasisi na wa nchi. 

Yeye alidhamiria kuinyakua tuzo hiyo, na alitaka aweke cheti chake pale ukutani.

Aliifikiria kesi mpya iliyopo mezani kwake kipindi kile. 

Kesi inayomhusu Dokta Tindo Masanga. 

Ni bahati ovu sana kwa kesi ile kuja mikononi mwake, maana hakuwa na nia ya kuongeza takwimu mpya kwenye namna taasisi yao inavyoshindwa kuzimudu kesi za rushwa ile ya ngono. Kesi ya utamu, kama jinsi ambavyo yeye na watendaji wenzake walivyozipachika jina la utani kesi za namna ile. 

Hakuna anayetema utamu baada ya kuuonja, na hivyo hakuna namna rushwa za ngono zitakwisha maana utamu wake hauchuji. Walaji huishia kuchekelea bila majuto, ilhali waliwaji huishia kuteketea kwa majuto. Ndiyo maana, hakuna anayediriki kuifikisha kesi ya namna kwenye taasisi yao, kwani mwishowe ni kudhalilika tu pasi mtuhumiwa kupatwa na adhabu yoyote. 

Hili lilimwuma sana.

Ndiyo maana, Rumi Dago alipomletea kesi ya Dokta Masanga kwa uhakika kabisa kuwa Eva alikuwa na msimamo thabiti wa kumfikisha mwalimu wake dhalimu mikononi mwa TAKUKURU, aliiona ni nafasi adimu sana ya kubadilisha ubao wa matokeo kwenye mechi ile kati ya taasisi yao na rushwa ya ngono.

Lakini sasa, inaonekana kuwa ubao hauelekei kubadilika.

Alisonya na kumpigia simu Bahati.

“Bahati, hebu njoo mara moja… kuna machache ya kujadili kuhusu huyu Eva Mazengo,” alisema simuni. Kisha, akajiegemeza kitini na kusubiri.




“NAAM,” Bahati alisema mara tu alipoingia ofisini kwa Hubiri.

“Aisee,” Hubiri alisema akimpa Bahati ishara  aketi. “Hili jambo linanikoroga sana kichwa changu.”

“Linavuruga sana akili.”

“Exactly.”

“Enhee?”

“Nataka tulijadili kwa kina hapa,” Hubiri alisema akiitazama ile fremu yenye kipande cha gazeti. “Sawa, hiki ni kiazi cha moto kwetu. Lakini, tumekwishafanikiwa kukabiliana na viazi vya moto vingapi?”

“Vingi tu,” Bahati alisema akimtazama Hubiri usoni. “Tena, tumeshakumbana na viazi vya moto kwelikweli, hiki hapa kikasome upya.”

“Speaking of that, akili yako inakwambiaje juu ya watu watatu?”

“Akina nani?”

“Eva, Rumi na Dokta Masanga.”

“Kuhusu Eva,” Bahati alisema na kutulia kuonesha kutafakari jambo. Akaendelea, “Aaah, Eva bado kuna jambo ananichanganya kidogo. Lakini, nikizitafakari tabia za wahanga wa vitu hivi kama rushwa za ngono, nahisi anaweza kuwa labda na woga fulani hivi…”

Hubiri akadakia, “Ama anaficha jambo hivi.”

“Kabisa.”

“Tukija kwa Rumi,” Bahati alisema. “Yule bwa’mdogo naye anaweza kuwa na kitu cha ziada.”

“Ukimaanisha?”

“Yule jamaa ni mwongeaji sana inavyoonesha. Najaribu kutafakari vipi kama alimshirikisha rafiki yake yeyote halafu huyo jamaa akauza faili kwa mwalimu?”

“Of which, I don’t buy the idea.”

“Hata mimi. Lakini, hatuwezi kuacha kuuchanganua huu uwezekano.” 

“Kuhusu mshukiwa mwenyewe?” Hubiri aliuliza.

“Yule jamaa is very smart,” Bahati alisema. “Huyu jamaa ana tuhuma nyingi za kulazimisha rushwa za ngono kutoka kwa wanafunzi wake wa kike. Si unakumbuka zile tuhuma kuwa mwaka jana, sijui mwaka juzi hapa aliwahi kufelisha darasa zima kwa sababu hiyo?”

“Zile zilikuwa stori lakini, si hazikuripotiwa kwetu?”

“Kutoripotiwa hakuondoi ukweli kuwa ilitokea. Achia mbali hiyo, unakumbuka lile sakata lilisosababisha ndoa kuvunjika baada ya jamaa kumla mwanafunzi wake aliyekuwa mke wa mtu? Yule jamaa alidaka hadi mawasiliano ya huyo jamaa na mkewe.”

“Nimekumbuka,” Hubiri alisema. “Umenikumbusha jambo la muhimu sana ambalo sasa tunaanza nalo.”

“Nidokeze.”

“Kitu cha muhimu kabisa, tunahitaji rekodi ya mawasiliano ya Dokta Masanga katika hizi wiki mbili tatu hivi. Tujue nani miongoni mwa marafiki wa Rumi na Eva waliwasiliana nao.”

“Nasi tunawajuaje hao marafiki?”

“Kuna options mbili,” Hubiri alisema. “Ya kwanza, ni kuwauliza moja kwa moja nani ni rafiki zao wa karibu. Halafu, watupe namba zao. La pili, ni kutazama rekodi zao wa mawasiliano kujua ni watu gani wanawasiliana nao mara kwa mara.”

“Zote mbili zimekaa vema. Hili linaanza mara moja.”

“Safi,” Hubiri alisema. “Lifanyie hili kazi haraka kisha tujadiliane hatua inayofuata.”

“Sawa,” Bahati alisema akiinuka. “Hili ni la muda mfupi tu.”

Bahati alipotoka, Hubiri alibaki katika mvurugo wa mawazo uleule aliokuwa nao kabla ya Bahati kuja ofisini kwake. Akakizungusha kiti chake kugeukia dirishani. Mandhari ya kuvutia ya jiji iliyapokea macho yake kwa bashasha. Mwonekano wa bahari ya Hindi kutokea ghorofani ulitia nakshi mwonekano wa majengo ya kila namna katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Alikiweka kidole chake cha shahada cha mkono wa kulia pembeni juu kidogo ya kidevu chake akitafakari. Tafakuri yake ikamrudisha hadi siku ile aliyokuwa na hakika wangemkamata Dokta Masanga akiwa chumbani hotelini Miami na mhanga Eva. Eva aliwaambia wamepanga miadi ya kukutana huko hotelini.

Mara, Dokta Masanga akampigia simu kuwa kuna jambo linamchelewesha hivyo amfuate ofisini. Wakafanya kila kitu kwa mpango mzuri. Wakaenda kumsubiri Eva kulekule chuoni kwao. Dakika kadhaa zikayoyoma kabla ya Eva kurejea.

Kwa nini Eva alirejea akiwa na mood tofauti kabisa? Hubiri alijiuliza. Swali hili lilimfanya akizingushe tena kiti chake. Alichukua shajara yake na kalamu. Akakizungusha kiti kurudi kulekule dirishani. Akakirejesha kidole chake cha shahada cha mkono wa kulia kichwani. Mkono wake wa kushoto ulishika kalamu yake nyeusi na kuanza kuchora kwenye ukurasa mtupu wa shajara yake.

Hivi Eva alitumia muda gani tangu aende hadi kurudi kutoka ofisini kwa mwalimu wake? Swali jingine likakikoroga kichwa chake. Akakisukuma kiti chake cha magurudumu umbali mfupi hadi mezani. Pasipo kugeuka, aliichukua rununu yake. Akakisukuma tena kurejea palepale panapompa uono mzuri dirishani. Akaitazama rununu yake.

Ziliyoyoma zaidi ya dakika ishirini. Aliwaza.

“Pumbavu zetu!” alisema kwa nguvu na kwa hasira kana kwamba anamtukana mtu. 

Aliinuka kutoka kitini. Alitembea akiongea peke yake maneno ambayo hata mwenyewe hakuyaelewa. Alikwenda kona moja baada ya nyingine. Ziliyoyoma dakika tatu hivi akiwa anazunguka tu ndani ya ofisini yake.

Alipoketi, aliifungua tarapakato mezani pake. Alikwenda moja kwa moja hadi kwenye mtandao wa You-Tube. Akatafuta simulizi za vitendo vya kingono baina ya walimu na wanafunzi wao. Alikutana na shuhuda nyingi za wanafunzi kutoka nchi mbalimbali wakisimulia namna walivyolazimika kuwapa walimu wao rushwa za ngono ili kufaulu mitihani.

Msichana mmoja ambaye uso wake ulizibwa alisimulia, “Mwalimu wangu alinilazimisha kwa muda mrefu nifanye naye mapenzi ndipo nifaulu somo lake. Nilikuwa nakataa. Kuna siku moja aliniita ofisini kwake. Nilipokwenda, alifunga mlango na kunilazimisha kwa nguvu. Sikuwa na namna yoyote ya kukataa. Niliishiwa ujasiri wote. Uso wa mwalimu ulinitisha na mishipa yake ilisimama. Ilinichukua dakika mbili tu kuupoteza utu wangu na mwalimu yule kupata alichokitaka. Niliondoka ofisini nikilia. Sikuwa na hamu na shule tena.”

Akafungua simulizi nyingine ambayo pia, msimuliaji alifichwa sura. “Nikiwa tu mwaka wa kwanza chuoni, nilikutana na mwalimu aliyenitaka kimapenzi. Siku moja nilikwenda ofisini kwake kwa ajili ya ushauri wa kitaaluma. Ofisi yake ilikuwa juu kabisa ghorofani. Ilitawaliwa na ukimya ulionitisha. Mwalimu alianza kunitongoza huku akinisogelea karibu. Mwanzoni, nilikuwa na ujasiri wa kumkatalia. Ujasiri wangu ulipungua kadri alivyokuwa akinisemesha huku akinishikashika mwilini mwangu. Ingawa nilijitahidi sana kukataa, nilijikuta nimelazwa kwenye kochi na kuvuliwa chupi yangu kwa nguvu. Ndiyo siku niliyopata UKIMWI na kuharibikiwa ndoto zangu zote.”

Hubiri alirudia kuitazama simulizi hii huku kitu kikimwumiza moyoni mwake. Alijikuta akimfikiria binti yake mwenye umri wa miaka mitano. Aliwaza, nini yatakuwa maisha yake atakapofikia umri wa kuwa chuoni? Ina maana naye atapambana na manyang’au kama haya? Alijiuliza. Roho ilimwuma.

“Dawa ya hawa washenzi ni kutokomezwa,” alisema kwa nguvu utadhani kuna mtu anayemtaraji kumsikia.

Akaitazama simulizi ya tatu. “Mwalimu wangu alinitaka kimapenzi. Baada ya kuzungushana sana tukakubaliana twende hotelini. Sikuwa na namna kwa kuwa zilibaki siku mbili kufanya mtihani na alinipa course work ikiwa pungufu ya alama mbili ili nifikie kiwango kinachotakiwa na chuo niweze kufanya mtihani. Nilimbembeleza sana mwalimu. Akaniambia, ‘quid pro quo’, ambayo ni falsafa ya kisheria kuwa ‘hakuna kiendacho bure’. Ujanja uliniisha siku hiyo. Nilikuwa njiapanda katika kuamua kama nisome somo hilo mwaka unaofuatia, ama nimpe anachokitaka. Nilipokwenda ofisini kwake kujaribu kumbembeleza, alibembelezeka ndiyo. Lakini, nilitoka ofisini kwake baada ya kuwa nimefanywa juu ya meza yake.”

Hubiri alijikuta akikasirika zaidi. Alitaka kufunga tarapakato yake afanye jambo jingine. Simulizi iliyoanza kucheza wakati akienda kwenye kona ya dirisha la You-Tube iliteka nadhari yake na kumfanya aitazame. “Mwalimu wangu alitaka rushwa ya ngono. Nikaamua kwenda kutoa taarifa kwa mshauri wa wanafunzi. Mshauri akaniambia jambo linafikishwa kwenye mamlaka za chuo kwa ajili ya ufumbuzi. Niliitwa kwenye kikao, nikatoa ushahidi wa mawasiliano yetu kwa WhatsApp. Nilikuwa na matumaini lile jambo limekwisha nami nimeshinda. Kilichokuja kutokea, ni kweli nilifaulu somo lake. Lakini, nilifeli masomo mengi na ku-disco. Baadaye sana, nikaja kufahamu, mwalimu yule aliamua kuwatumia walimu rafiki zake kuninyoosha. Sasa hivi, mimi nipo mtaani sina digrii. La kuumiza moyo, mwalimu yule bado anaendelea kuwafanya wasichana wengine wahanga wake.”

Hubiri aliifunga tarapakato yake. Akampigia simu Bahati.

“Naam,” Bahati alisema mara tu alipopokea simu.

“Hebu njoo mara moja.”

Simu ikakatwa.

Bahati alimkuta Hubiri akiwa wima dirishani akitazama nje.

“Bahati,” Hubiri aliita pasipo kugeuka.

“Naam.”

“Tumefanya jambo la kifala sana,” Hubiri alisema akigeuka.

“Jambo gani?”

“Dokta Masanga alimchapia Eva ofisini kwake,” Hubiri alisema kwa sauti iliyoshiba hakika.

“No, no, nooooo!” Bahati alisema akiketi mikono ikiwa kichwani mithili ya kibonzo cha WhatsApp. “Nani kakwambia?”

“Logic.”

“Kwa namna gani?”

“Nimejiuliza maswali mengi.”

“Maswali yepi?”

“Swali la kwanza, kwa nini Eva alikwenda kwa mwalimu akiwa very cooperative, lakini akatoka akiwa hostile?” Wakati Bahati akimwemwesa mdomo kutafuta jibu, Hubiri aliendelea, “Nimetazama Eva alikaa ofisini kwa mwalimu wake zaidi ya dakika ishirini. Unajua muda huo unatosha kufanya nini?”

“Kwamba muda huo ungetosha kumshawishi na hatimaye kutenda uhabithi wake?”

“Usiniulize mimi swali. Fikiria mwenyewe. Think like an investigator.” Kauli ya mwisho ya Hubiri kumtaka Bahati afikiri kama mpelelezi ilikuwa amri zaidi, kuliko ushauri.

“Fikiria kama taaluma yako inavyokutaka kufikiri. Kisha, nishirikishe uchambuzi wako. Umefikia wapi kwenye intel?”

“Nasubiria majibu kutoka kwa jamaa wa Mawasiliano. Printout ikiwa tayari wataniambia, ndipo nikaichukue.”

“Ukisharudi,” Hubiri alisema. “Nataka tukutane na Eva.”

“Tumlete hapa, ama tumfuate chuo?”

“Tutakutana naye kwenye mgahawa wowote mzuri karibu na chuo chao. Tunahitaji kuhoji wanafunzi kadhaa.”

“Bila shaka wa kike,” Bahati alisema.

“Hapana. Logic inataka na wa kiume pia.”

*****

Mwili wa Eva ulisisimka mkono wa Dokta Masanga ulipofika kwenye chuchu yake. Woga ulimpungua sana tofauti na siku mbili za mwanzo. Hata safari yenyewe ofisini kwa Dokta Masanga, ilikuwa kwa minajili ya kumwambia anahofia kupata mimba kwa kuwa alikuwa katika siku za hatari.

Ilikuwa saa nne ushei asubuhi. Mvua ilitandika hasa nje. Isivyo mazowea ya wakazi wa Dar, baridi ilipiga na kuwafanya wenye makoti na masweta wayavae. Wengine, waishie kujikunyata tu. Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa tahadhari kuwa kungekuwa na baridi kali kwa juma zima kutokana na mgandamizo mkubwa wa hewa ulioikumba bahari mashariki ya Afrika Kusini. Hivyo, hali ya hewa pwani yote ya mashariki mwa bara la Afrika ilishafuka hasa.

Na, wala halikuwa lengo la Eva kwenda ofisini kwa Dokta Masanga asubuhi hiyo. Ndiyo kwanza alikuwa ametoka kwenye kipindi cha asubuhi kilichomalizika saa nne kamili. Rumi alimtumia ujumbe wakutane mgahawani kwa ajili ya chai. Eva hakutaka kukutana na Rumi. Si kwamba hakumpenda. Alimpenda vilivyo. Hakutaka kukutana naye kwa sababu ya malumbano ambayo yameibuka baina yao hivi karibuni. Yalimsononesha. Zaidi, yalimkasirisha.

Mtu mwingine aliyemfanya asitake kwenda mgahawani muda huu ni Zena. Tangu walumbane mara ya mwisho, maelewano hayakurejea baina yao. Eva aliendelea kumtilia mashaka Zena, pengine aliuza faili kwa Dokta Masanga. 

Wakati wakitoka kwenye kipindi, Zena alimwambia waende kunywa chai. Akamjibu, atangulie kuna kitu anachukua kwa Rumi kisha angeungana naye. Zena akatangulia, akiwa na hakika Eva anamkwepa.

Aende wapi muda huo? Eva alijiuliza. Hawakuwa na kipindi kingine hadi saa sita mchana. Mvua ilimtamanisha arudi hosteli akajilaze kidogo. Wazo jingine lilimkatalia likimwonya usingizi ungemchukua kiasi cha kukosa kipindi cha mchana. Kipindi muhimu sana kwake, somo la Sociology of Social Change.

Akiwa katikati ya kuwaza, alimwona Dokta Masanga akiingia jengo la idara. Akili ikamwambia ni wazi anakwenda ofisini kwake. Ndiposa, akaamua kumfuata.

“Oooh, Eva,” Dokta Masanga alisema kwa bashasha alipomwona Eva akiingia ofisini kwake. 

“It’s so sweet to see you here. Have a sit, please,”

Dokta Masanga alisema huku akirejea mlangoni. Akautia kitasa.

Eva akashituka, “Mbona unalock mlango sasa?”

“Aaah, Eva,” Dokta Masanga alisema akitabasamu. “Wewe ni mtu special sana kwangu. Our conversations should not be interrupted na mpuuzi yeyote.”

“Lakini, usingefunga. Mimi sikai sana.”

“Hakuna aliyesema utakaa sana, Eva,” Dokta Masanga alisema huku akiegamia meza, mkabala kabisa na mahali alipoketi Eva.

Eva alimtazama Dokta Masanga akiwa na mawazo tele. Hivi, kwa nini lakini nilimruhusu mwalimu huyu kunifanya mara mbili zote? Kwa nini nilikubali kufanywa mjinga kiasi hicho? Kwa nini nimejiweka daraja moja na wasichana malaya? Maswali yalikigonga kichwa chake. Yakauchana moyo wake.

Kabla hajayapata majibu, ama tu, kujaribu kuyafikiria, kidole cha shahada cha Dokta Masanga kilitua kwenye paji lake. Dokta Masanga alikitembeza taratibu kushuka chini katikati ya macho, juu ya pua, juu ya mdomo hadi kidevuni. Akili ya Eva ilikufa ganzi kwa nukta kadhaa huku mapigo ya moyo wake yakienda peapea.

Alipofika usawa wa kidevu, Dokta Masanga alikiinua kidevu cha Eva kutaka kumbusu mdomoni. Eva aliukwepesha mdomo wake huku akiushika mkono wa Dokta Masanga kuuondoa. Mkono wa Dokta Masanga ulilitii katazo la Eva. Lakini, badala ya kwenda kwingineko, ulikwenda moja kwa moja shingoni kwa Eva.

Ubaridi wa mkono wa Dokta Masanga ulipokutana na joto la shingo ya Eva, joto lililohifadhiwa vema na kola ya shati lake, ulimsisimua badala ya kumkera. Zile nukta chache ambazo Eva alihitaji kuutafsiri ule msisimko, ama, kuufanyia maamuzi, zilimzubaisha.

Hivyo, hata hakuwa na kumbukumbu juu ya wakati gani mkono wa Dokta Masanga ulifika kwenye chuchu zake. Wakati akili yake ikijaribu kukaa sawa, ilivurugwa na mdomo wa Dokta Masanga uliokuwa tayari mdomoni mwake.

Haya mambo yalikwenda kwa kasi ambayo ilimzidi Eva nguvu na maarifa. Maarifa pekee aliyokuwa nayo, ni yale yaliyotokana na uzoefu wake akiwa na Rumi. Ambaye, kwa siku za hivi karibuni, hali ilikuwa si hali. Na, nguvu pekee alizobakiwa nazo, zilimtosha kusimama wakati Dokta Masanga akimwinua taratibu na kumpandisha sketi yake. 

"No, please!" Eva alisema. Si kwa kufoka, si kwa kubembeleza. Zaidi, kwa kumsukuma Dokta Masanga mbali naye. Huku pia, akipiga hatua pembeni ya pahala alipokuwa. 

“You’re so sweet, Eva,” Dokta Masanga alisema akimsogelea na kumwekea mkono kifuani kuzuga kutaka kumfunga vishikizo.

Eva aliiondoa mikono ya Dokta Masanga kwenye vishikizo vyake. “Nafunga mwenyewe.”

Dokta Masanga aliegamia meza yake akimtazama Eva. Mate yalimjaa mdomoni. Damu ilikimbia kwa kasi mwilini mwake. Mishipa ilimsimama. Hanjamu ilimjaa. Uanaume wake ulikuwa na njaa kali. Alijisikia ashiki kubwa kuliko mara mbili nyuma. Mwenyewe, hakufahamu ilichangiwa na nini hasa.

“Nakupenda sana, Eva,” alisema kwa hisia. Aliyamaanisha maneno yake. Pamoja na wanafunzi wengi aliokwishatembea nao, alijihisi tofauti kwa Eva. Eva mlimbwende hasa. Chombo chombole. Kaumbwa, kaumbwale akaumbika. 

“Kama unanipenda kweli, uache kunifanyia ofisini kwako,” Eva alisema akimtazama usoni Dokta Masanga. “Unanishushia thamani yangu kunifanyia hivyo.”

“Oooh, Eva. Sawa,” Dokta Masanga alisema. “Tutakwenda hotelini. Tena, tutakuwa na muda wa kutosha sana pamoja. Ama wewe unaonaje?”

“Sawa.”

“Lini utakuwa na nafasi?”

“Niambie wewe ratiba yako,” Eva alisema taratibu akimtazama Dokta Masanga. 

Dokta Masanga aliyatazama macho ya Eva yaliyokwiva. Macho matamu hata kwa kuyatazama. “Unaonaje tukienda mahali patulivu nje ya mji Ijumaa hivi halafu tukakaa pamoja hadi Jumapili?”

“Ni sawa.”

“Ijumaa hii jioni vipi?”

“Sawa utaniambia,” Eva alisema.

“Leo ni Jumatano. Kwa hiyo, keshokutwa.”

“Sawa.”

“Najua namna ya kukushukuru,” Dokta Masanga alimwambia Eva. “Wewe ni mtamu sana.”

Wasichana wangapi amewapa kauli hii? Eva alijiuliza. Hata hivyo, hakuwa na muda wa kutafakari jibu.

“Basi, mi naomba niende.”

“Mbona hata hujaniambia ulichokijia ofisini?” Dokta Masanga aliuliza.

“Aaah,” Eva alisita. “Hakina umuhimu.”

“Niambie tu.”

“Ntakwambia keshokutwa.”

"Please, Eva. Just tell me." 

"Nilikuja kukwambia," Eva alisema akimtazama Dokta Masanga. Hata mwenyewe, hakujua alikoutoa ujasiri wa leo. Nikimwambia leo nahisi nina mimba, haitokuwa sawa, aliwaza. Alipomwona Dokta Masanga akimakinika naye, akaendelea, "kama unataka wewe ufaidi mapenzi nami, na mimi pia nafaidi nawe, tusifanyie ofisini. Thamani yangu ni kubwa. Na, ahsante tumekwishaelewana." 

"Ooh, Eva…" Dokta Masanga hakujua aseme nini zaidi. 

Eva alielekea mlangoni.

“Nakupenda sana, Eva.” Sauti ya Dokta Masanga ilisikika nyuma yake wakati akiufungua mlango.

“Ahsa….” 

Sauti ilimkatisha, “Evaaa!”

Hakuhitaji kumtazama mtu aliyemwita kwa hasira ili kuitambua sauti. Wala, hakuhitaji kugeuka ili kumwona. Mtu huyo alisimama mbele yake. Kwenye kingo za ngazi zinazoitazama ofisi ya Dokta Masanga.

Rumi.

Miguu ilimwishia nguvu. Alitamani kuketi sakafuni. Rumi yupo pale tangu saa ngapi? Swali hili lilimpa nguvu miguu yake. Badala ya kutamani kuketi, alijikuta akimpita Rumi haraka. Akashuka ngazi huku akikimbia. Mara kadhaa, alinusurika kuteleza na kuanguka. Pengine, isingekuwa viatu vya kuchomeka vya soli fupi alivyovivaa, angeshapiga mweleka wa haja.

Alipofika chini ya jengo, alitoka mkuku kama mwizi anayekimbizwa na wananchi wenye hasira kali. Kila mmoja alimshangaa. Wapo waliodhani amewehuka. Wapo waliodhani kuna hatari huko atokeako. Nao, wakaanza kukimbia kuelekea nje ya geti la chuo.

Eva hakujua aende wapi muda huo. Kitu pekee alichokuwa na hakika nacho, hakutaka kukutana na Rumi. Nafsi yake ilijisikia hatia. Hatia iliyomwongezea maumivu kwa kutofahamu Rumi alisimama nje ya ofisi ya Dokta Masanga kwa muda gani Vipi kama amesikia kila kitu? Swali lilimkoroga.

Wakati amevuka kabisa barabara inayopita nje ya geti la CHUKIM, rununu yake ilianza kuita. Moyo ulimwenda mbio maradufu. Ukijumlisha na zile mbio, basi alihema juujuu. 

Aliitoa simu yake kwenye mkoba wake mikono ikimtetemeka. Namba ilikuwa ngeni. Hilo lilimwongeza hofu. Aliibonyeza pembeni ili kuondoa mlio. Akairudisha kwenye mkoba ikiendelea kuita kimyakimya.

Haikupita hata dakika, iliita tena. Hakuipokea.

Alikuja kuipokea ilipoita kwa mara ya tatu. “Haloo!”

“Habari yako, Eva?” Sauti nzito ya kiume ilisikika kutoka upande wa pili. Ilimzidishia hofu.

“Sa – la – ma,” alijibu kana kwamba anazihesabu silabi.

“Ninaitwa Hubiri kutoka TAKUKURU. Bila shaka unanikumbuka.”

“Ndiyo,” alijibu kwa hofu.

“Sasa,” Hubiri alisema. “Tupo hapa karibu na chuo. Opposite na geti lenu kwenye hiki kibarabara kinachokwenda round about kuna mgahawa. Mimi na Bahati tunahitaji kuzungumza nawe kwa kifupi sana.”

Eva alibabaika asijue la kujibu.

“Ni muhimu sana, Eva. Tunajua upo busy na masomo, lakini tafadhali sana tunaomba dakika zako chache.”

“Sa’izi?” Walau, aliuliza.

Hubiri akajibu, “Ndiyo, sasa hivi. Halafu, tunaomba Rumi wala mtu yeyote asijue unakutana nasi.”

Hilo la Rumi kutotakiwa kujua walau lilimpa amani. Akajibu, “Sawa. Nakuja.”

“Shukrani. Baada ya dakika ngapi?”

Eva aligeuka nyuma kuutazama mgahawa uliosemwa. Aliufahamu. Ulikuwa hatua chache kutoka mahali aliposimama. Akajibu, “Nipo close. Dakika moja.”

“Tunakusubiri.”

Simu ikakatwa.

Eva akaanza kutembea kuuelekea mgahawa huo.





Rumi Dago aliendelea kusimama pale kwenye kingo za ngazi zinazoitazama ofisi ya Dokta Masanga. Huku akitweta, aliutazama mlango uliofungwa na Eva sekunde chache zilizopita. Mikono yake ilitepeta mithili ya shati lililotota na kutundikwa. Miguu yake haikuweza kumfukuzia nyuma Eva, seuze kumwondosha yeye mwenyewe eneo lile.

Hakujua ajilaumu kwa kujileta pale au ajipongeze kwa aliyoyaona. Ni kama vile akili yake iliruka hadi nje ya kichwa, na kukiacha kitupu kama mtungi uliotoboka. 

Alipokutana na Zena kule mgahawani, wakati huo akiutafakari uamuzi wa Eva kukataa kustaftahi naye asubuhi hiyo, alijikuta tu akimwulizia mpenzi wake. Waama, hakujua kuwa jibu ambalo angepewa na Zena lingemkalifisha.

‘Mbona kaniambia kuna kitu anakuja kuchukua kwako!?’ Rumi alilikariri jibu la Zena.

Na jibu hilo ndilo lililomnyanyua Rumi kitini. Likamsomba mbiombio kuelekea lilipo jengo la Idara ya Sosholojia. Hisia zake zilitaka kumwaminisha kuwa Eva alimdanganya Zena kwa sababu zake binafsi. 

Sababu zipi? Kwa nini amdanganye anakuja kwangu?  Rumi alijiuliza wakati akipangua hatua ndefu zilizokaribia kugeuka kuwa mwendo wa mchakamchaka. 

Tangu alfajiri ya siku hiyo, yale maongezi yake na Julius Kamili yalijirudia  kichwani kama kipande cha filamu. Hata kipindi chake cha asubuhi,  aliingia darasani kutimiza wajibu tu. Hakuna alilolielewa.

Stori ya Julius haikutofautiana sana na yake. Kwa ghadhabu alizokusanya nafsini, aliona angekuwa bwege mtozeni kumwachia Dokta Masanga arudie tena kutamba kana kwamba alikuwa mwanaume pekee rijali kuliko wote pale CHUKIM. 

Ujasiri aliokuwa nao ulimbebesha nguvu na silaha za kufikirika. Ghadhabu ikamlisha yamini ya kuingia kwenye mapambano mithili ya askari mzalendo vitani. Afua ni mbili, kufa na kupona. 

Yale maswali yaliyomjia kichwani kupitia ile kozi yake ya ‘Maongezi Magumu’, yaliuchochea moto akilini. Alijiuliza mara idadi isiyokumbukika, katika sakata hili, Eva alikuwa nani? Adui, mhanga au mtu asiye na namna? 

Hivyo, uongo wa Eva kwa Zena ulimtia Rumi mshawasha wa kuanza kumfuatilia. Walau, apate jibu hata moja tu la kujua pa kuanzia. 

Alipotoka pale mgahawani, akilini alikuwa na mengi ya kutia na kutoa. Alijihakikishia kumkuta Eva jengoni mle. 

Aliwaza, akimkuta huko, atarusha mateke ya shingo kama salamu. Kisha, atarusha ngumi matata na kuitawanya ile pua ndefu nyembamba ya Dokta Masanga. Tena, angeufutilia mbali hata ule mwanya wake ambao kwake aliuona kama uchochoro tu. Hapana, alijikanya. Akajisahihisha, nikifika huko nitajibanza niwarekodi kwanza. 

Na sasa, hali halisi ilikuwa tofauti kabisa na yote aliyoyawaza na kuyapanga. Alikuwa pale akizikokota pumzi. Hata nguvu ya kusogea tu hakuwa nayo. Chambilecho wahenga, mkamia maji hayanywi.   

Akiwa bado amesimama palepale, mlango wa ofisi ya Dokta Masanga ulifunguliwa. Kumwona Dokta Masanga akitoka ofisini kwake, kulimghadhabisha zaidi.

Dokta Masanga alipomwona Rumi alitabasamu kwanza kabla ya kuugeukia mlango na kuufunga kwa ufunguo. Aliisikia barabara sauti iliyomwita Eva. Hakuitambua kama ni ya Rumi. Lakini, alijua kwa vyovyote vile, mwitaji alihamaki. Akaamua kutoka ofisini kwake, muda uleule aliotoka Eva.  

Hatua takribani nne zilitosha kumfikia Rumi pale alipojisimika. Walitazamana mboni kwa mboni kwa sekunde tano kukiwa na ukimya kati yao. Hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kusimama kwa ukaribu wa namna hii na kutazamana kwa kedi. 

“Eva hastahili unachomfanyia,” Rumi alitamka kuuvunja ukimya. Hasira ilijidhihirisha katika mdondoko wa silabi.

Dokta Masanga alijenga tabasamu fupi pana lililouficha mwanya wake. 

“Hastahili hata kidogo,” Rumi alizungumza tena kwa msisitizo. 

“Are you okay?” 

Macho ya Dokta Masanga yalihama toka usoni hadi unyanyoni. Kisha, akaitazama sakafu huku akianza tena kuumba tabasamu, wakati huo akiyarejesha macho usoni pa Rumi. 

Kwa Rumi, swali lile lilitafsirika kama dharau moja kubwa sana. Zaidi, Dokta Masanga alimtazama kama mtu anayepima thamani ya kiumbe kinachompotezea muda wake. 

Mishipa ya kichwa cha Rumi ilianza kusimama. Mkono wake wa kuume ulikunja ngumi iliyokakamaa na kuamsha misuli. Damu ilimchachawa. Taya zake ziliumana kwa nguvu, hali pua ikitanuka kuachia hewa iliyomjaa kifuani.

Alitafuta maneno makali ya kumpayukia huyo fidhuli aliyeanza kumkosesha usingizi. Akakosa.

“Rumi,” Dokta Masanga aliita kwa sauti ya chini mithili ya mzazi anayejiandaa kumtia moyo mwanaye. Alimtazama kwa macho ya huruma kana kwamba Rumi alimbembeleza amtendee jambo.

Kuitwa jina na adui yake kulimteteresha kidogo katikati ya ile ghadhabu. 

“Unawajua wanawake vizuri? Unawaelewa?”

“Kuwajua wanawake na ushenzi wako kunahusiana vipi?”

“Fanya kilichokuleta chuoni.”

“Usinitishe!” Uso wa Rumi ulijikunja kuonesha kinyaa. 

Dokta Masanga alitabasamu tena. Safari hii, aliuachia mwanya wake uonekane vyema. Aliipenda jeuri ya Rumi. Alizipenda vita za namna hii. Vita zilizomdhihirishia kuwa mwanamke anayemtafuna anaiwehusha barabara akili ya mwanaume mwingine. Kisaikolojia, ilimfanya ajisikie bora zaidi. Mwenye mamlaka zaidi. 

Ingawa alipata kumtamkia Eva kuwa angeweza kuendelea na Rumi huku akiwa naye. Ujeuri wa Rumi ulimfanya atamani kumpora kabisa mwanamke wake.  Maumivu yaliyoonekana usoni pa Rumi wakati ule yalikuwa burudani kabambe kwake. Aliitaka burudani zaidi ya ile. 

Taratibu, alijisogeza usawa wa sikio la Rumi na kunong’ona, “Back off Rumi. Stay in your lane, man!  Ni ushauri wa bure kutoka kwa mtu anayekujali.” 

Dokta Masanga aliligusa bega la kushoto la Rumi kwa mkono wa kulia. Akaliminya bega hilo kwa nguvu wakati akiliondoa tabasamu usoni na kumtazama Rumi kwa macho makali mno. 

Macho yaliyofikisha onyo kali kuliko hata maneno aliyomtamkia. 

Alipomwachia, alimpita na kuendelea na safari yake, njiani akipishana na mwalimu mwenzake aliyesalimiana naye kwa bashasha kubwa.

Rumi aliwayawaya. Maswali aliyotarajia kuyapatia hata jibu moja yalimpiga roba kabambe. Suala la Eva kumficha kitu lilijidhihirisha. Akaumia sana, kwa wivu na ghadhabu.

***

Eva alipiga hatua za taratibu, akiwa ameinamisha kichwa, mkoba wake aliubana kwapani. Hatua zake zilikuwa za mtu anayejilazimisha kusonga mbele. Aliongea mwenyewe kwa sauti ya kichwani na kujijibu. Mara kadhaa, alisonya na kutikisa kichwa kulia kushoto.

Ndani ya mwezi alikuwa ameyageuza maisha yake juu chini. Kila uchao kulikuwa na jipya lenye kumtesa na kumteteresha. Aliwaza cha kujitetea mbele ya Rumi. Akayatafakari yatakayojiri hiyo Ijumaa jioni. 

Alijiona akipelekwapelekwa kama ng’ombe. Kwa sababu tu alihofia Rumi kuzipokea salamu za Dokta Masanga. Alihofia Rumi kuumizwa. Labda, na mapenzi yao kuvunjika. Kubwa kuliko yote, alizihofia hesabu zake za kike kujibu. Alikuwa na hofu chungu nzima.

Akarejea kuutafakari wito wa afisa wa TAKUKURU. Wito aliouitikia haraka bila kujua anachokwenda kujibu endapo atahojiwa kuhusu mtuhumiwa wao. 

Mzigo wa mawazo ulimnyima kumakinika na yanayoendelea mbele yake. Mara kadhaa, alikaribia kupamiana na watu aliopishana nao wakati akichapua hatua kulifuata jengo lenye mgahawa.  Takribani mara mbili, aligeuka nyuma kama mtu anayehisi kufuatiliwa 

Alisonya tena wakati akiukaribia mlango wa mgahawa. Akainua kichwa na kujitazama kupitia mlango wa kioo wa mgahawani hapo. Mwili mzima ulimtia kinyaa. Alitamani hata kuchepukia msalani kwanza walau kuusukutua mdomo wake. Pengine, kuyanawa pia mashaka yaliyoshindwa kujificha usoni pake. Hata hivyo, muda haukumruhusu kufanya hivyo.

Kule ndani ya mgahawa, Hubiri na Bahati walimtazama Eva kwa udadisi wa hali ya juu. Walimtazama namna alivyosimama akijitazama kwenye kioo cha mlango kwa sekunde kadhaa, kabla ya kuinua mguu kupanda ngazi mbili tatu mbele yake. Alipousukuma mlango na kuingia ndani, Hubiri alinyoosha mkono kidogo kumjulisha sehemu alipo.

Eva aliwafuata huku akijaribu kutabasamu. Majaribio ya tabasamu lake yalisomeka vizuri mbele ya maafisa waliokuwa mbele yake. Kila hatua na tendo alilofanya lilisomwa kwa umakini mkubwa. 

“Tuwie radhi sana kama tumekuvurugia ratiba zako,” Hubiri alimpokea huku akivikutanisha viganja vyake pamoja na kuvipishanisha.

“Wala, nilikuwa na mambo mengine tu,” Eva alijibu. Alivuta kiti na kuketi.

“Mambo,” Bahati alimsabahi.

“Safi tu.”

Mhudumu aliyekuwa akisafisha meza ya pembeni yao, alikuja na kusimama wima akimtazama Eva.

“Mi sihitaji chochote,” Eva alijieleza.

“Hata maji?” Hubiri alidakia. Eva akajilazimisha tena kutabasamu. 

“Basi niletee maji madogo ya baridi,” Eva alijibu baada ya kuzitazama bilauri mbili za juisi za wenyeji wake zilizokuwa zimekwishakufikia nusu. Pengine, hakuvutiwa na rangi ya juisi hiyo ya stafeli.

Hubiri alilala kiubavu na kuchomoa pochi yake. Alifanya malipo. Mhudumu alipoondoka, Hubiri aliitenga mikono yake mezani na kuilaza, vidole vikikamatana. Alikuwa makini mno kumsoma Eva kila sekunde wakati akizungumza naye. 

Macho ya Eva hayakudumu usoni pa Hubiri hata kwa sekunde tano. Alitazama chini. Huko nako hakudumu. Aliinua uso na mboni zake zikazunguka bila mpangilio, huku kope zake zikifunga na kufunguka kwa kasi kuashiria kukosa utulivu kichwani. 

Hubiri alimsaili hili na lile, na Eva akajitahidi kujibu kwa uchangamfu wa kukopa. Wakati maongezi yakiendelea.

Aliuma mdomo wake, akaikuna sehemu ya nyuma ya shingo kisha akaupigapiga utosi mara kadhaa. Taratibu, alipeleka dole gumba mdomoni na kutafuna kucha kwa bidii. Halafu, akajishika shingo mithili ya mtu anayetaka kujikaba ilhali akiteremsha pumzi ndefu iliyokiinua na kukishuka kifua chake. 

Hubiri alitabasamu. Hizi zilikuwa dalili za mtu mwenye hatia au wasiwasi uliopitiliza.

‘Wasiwasi wa nini mbele ya afisa mwenye nia ya kumsaidia?’ Hubiri aliwaza. 

Mhudumu aliporejea na chano chenye chupa ya maji na bilauri, wakanyamaza kidogo kumpisha awahudumie. 

“Kwa hiyo, ameacha kabisa kukutumia ujumbe kwa sasa?” Bahati alimwongezea swali kuendeleza maongezi yao baada ya mhudumu kuondoka.

“Labda ana sababu zake.”

‘Hajajibu hili swali straight’ Hubiri alimakinika kwenye jibu la Eva.

“Lakini, nilisema akianza nitawasiliana nanyi. Kwani kuna kitu kimetokea?” Eva aliuliza.

“No! hapana, hapana. Huwa tuna kawaida ya kufuatilia kesi zetu ambazo bado ziko hai, ili kujua wahanga wana changamoto zipi,” Hubiri alimjibu akitabasamu.

“Mnafanya vizuri, basi mi niko poa kwa sasa. Likitokea tatizo nitawajulisha mara moja.”

Kwa namna macho ya Eva alivyomweweseka na kasi ya kudatisha vidole vyake kuongezeka, walijua, ahadi aliyoitoa ilikuwa ya funika kombe mwanaharamu apite. 

“Tumekubaliana Rumi hapaswi kujua juu ya wito huu,” Hubiri aliikazia kauli yake.

Eva akatikisa kichwa juu chini, “ni sawa, ni sawa kabisa.” Aliuma mdomo tena.

‘Oh, kuna kitu anaficha. Ameshaliwa huyu. Dah!’ Hubiri alianza kupata alichotaka kupata. Moyoni aliangusha tusi la nguoni. 

Wakaagana. Eva akiwaacha pale. 

“Nadhani kuna kitu anaficha huyu,” Bahati alisema, wakati macho yakimalizia kumtazama Eva aliyekuwa amekwishafika mlangoni.

“Si suala la kudhani, huyu hana mpango na hii kesi tena.”

“Kwa hiyo inawezekana kweli hatamwambia Rumi kwamba tumeongea naye?”

“Akimwambia Rumi ukweli nidai mshahara wangu wote ujao hata na mafao ukipenda,” Hubiri alijibu, akiinua bilauri ya kinywaji chake na kupiga funda moja refu. Bahati alicheka.

Hubiri akagongagonga meza kwa kidole cha shahada akisisitiza baadhi ya maneno yake, “mwenye nia na kesi hii, lazima angehoji na kushangaa kwa nini mpenzi wake afichwe?  Unaona kilichotokea kwa Eva? Hamna kitu hapa. Yule mshenzi ameshamvuruga juu chini.” 

“Sasa?” Bahati alimtegea sikio bosi wake. 

“Inabidi tujue kwanza nini kinaendelea. Nimeshapata uhakika Eva hawezi kutupa ushirikiano kwa hiari yake. Hapa kuna mambo mawili. Ametishwa akatishika au ameingia line. Kama ametishwa yule mshenzi anajiongezea kesi, na kama Eva ameingia line hiyo inaitwa kujiandaa na vita ya janja kumvaa janjaure. Hachomoki mtu.  Twen’zetu.” 

Hubiri aliinuka. Bahati akafuatia. Wote wawili waliitazama chupa ya maji iliyoletwa kwa ajili ya Eva. Aliondoka pasipo kuigusa hata kidogo.  Wakajikuta wanatazamana na kutabasamu. Bahati akiikwanyua ile chupa na kuondoka nayo.  

***

Alipotoka mgahawani, Eva alikwenda moja kwa moja hosteli. Alihitaji kuufanyia usafi mwili wake. Alihitaji hata wasaa wa kulia peke yake. Muda wote kichwani, wakati alipokuwa bafuni, alikuwa akiyapangilia maongezi yake na Rumi. Alitafuta njia na sababu zote za kujitetea ili kuusawazisha mtafaruko uliotokea.

Hakujua Rumi alikuwa wapi na mwenye hali gani. Mpaka dakika ile, Rumi hakuwa amemtafuta. Si kwa kumtumia ujumbe, wala kumpigia. Roho ilimwuma vilivyo. Kheri angemshutumu na kumhoji kuliko hivi alivyomkalia kimya. 

Hata hivyo, alijipa moyo ukimya huo ulimaanisha hakuwa amevaana na Dokta Masanga. Vinginevyo, mmoja kati yao angeshamwendea hewani. Uhakika pekee aliokuwa nao ni hasira ya Rumi juu yake. 

Alipotoka bafuni, alinyata kwenda chumbani kwake. Baridi iliyokuwa inapuliza ilipenya mpaka kwenye mifupa. Alipoingia chumbani. Ukimya ulimlaki. Wenzake walikwishaelekea kwenye ratiba zao. 

Eva, alijifuta maji mwilini kwa khanga ileile aliyoivaa. Kisha, akalifuata kabati lake na kutoka huko akiwa na chupa ya lotion. Aliimimina mkononi, na taratibu, mawazo yakamchota tena. 

Ilimpasa kuharakia kumsaka Rumi. Aliamini alitakiwa kumtafuta na kumtuliza kabla hajalipuka. Kabla hajamtafuta Dokta Masanga na kumpayukia. 

‘Dokta Masanga’ jina hili likapita tena kwenye akili yake.

Alitulia kama zoba. Mikono yake yenye lotion ikipokezana kuitelezesha viganjani pasipo kuipaka. Akili yake ilisafiri maili nyingi. 

‘Nafunga mwenyewe’ aliyakumbuka maneno aliyoyatamka wakati akimkatalia Dokta Masanga kumsaidia kufunga vishikizo vya blauzi yake. Eva alimtazama Dokta kwa kuibia, pale alipokubali kuachana na vishikizo hivyo na kuiegemea meza. Namna Dokta Masanga alivyokuwa akimtazama, ilimpa nguvu ya kujikuta akileta ombi la kutofanyiwa ule ubaradhuli ofisini pale.

Dokta Masanga alimtazama kwa upendo na mahaba. Vile ambavyo mwanamke yeyote angependa kutazamwa na mwanaume anayedai kumhusudu. Kwa dakika alizomtazama Dokta Masanga usoni bila mzozano kati yao, alikiri, sura si roho.  

Ombi alilolitoa kwa sauti ya deko, mwanaume aliyemdekea alilipokea. Alideka kwa majaribio. Lipo alilotaka kujaribu kulipata. Wakati Dokta Masanga akishughulika naye, kuna wazo la hatari lilimjia akilini. Wazo hilo ndilo lililomsukuma kumdekea mtekaji wake. 

Hakujua kama yu sahihi au la. Hakujua kama lingemrudi na kumtafuna au la. Alichojiaminisha, kuchomoka toka mikononi mwa Dokta Masanga kulihitaji akili yake kuliko ujeuri. Hii ilimaanisha, kumtumikia kafiri. 

Taswira ya Dokta Masanga ikimtazama na kumtamkia maneno matamu ya kimahaba ilimjia tena kichwani. Kisha akamuwaza Rumi. Alimpenda sana. Angefanya chochote asiingizwe kwenye balaa hili.

 Eva alitabasamu. Hakujua tabasamu lile lilikuja kwa huzuni ya msongamano wa mambo au kwa kumfikiria Rumi au pengine Dokta Masanga. 

 Akaikumbuka lotion iliyokaribia kukaukia mikononi. Alijipaka kwa pupa. Akavalia nguo nyingine. Suruali ya jeans iliyomkamata kisawasawa na fulana iliyomkaa sawia. Juu ya fulana yake alivalia poncho iliyomkinga na hali ya ubaridi uliowatembelea tangu asubuhi ya siku hiyo.

 Hakuelekea darasani kama mipango yake ilivyokuwa kabla ya mambo kuvurugika. Huu ulikuwa mguu wa kumsaka Rumi.  

 Alitamani kumpigia simu kumjulisha juu ya ujio wake. Lakini, kwa kile kilichotokea kule ofisini kwa Dokta Masanga, mawasiliano ya simu yasingefaa kitu. Na kama si hofu ya Rumi kumvaa Dokta Masanga, pengine baada ya kuoga, angejitupa kitandani na kujikunyata hapo. 

***

Rumi aliishi nje ya chuo. Alipanga chumba Kigamboni, mtaa wa Ferry. Ingawa, mara kwa mara alipatikana hosteli moja katikati ya jiji, almaarufu kama Big Brother House, alikoishi  rafiki yake, Shija. 

Hosteli hiyo ilikuwa ni mali ya mtu binafsi. Lilikuwa jengo la ghorofa tatu, lililokuwa mtaa wa pili tu toka yalipo  majengo ya CHUKIM.  Ilikuwa hosteli ya kisasa ambayo kila chumba kilikuwa na mwanafunzi mmoja au wawili. Hali iliyopelekea mara nyingi itawaliwe na hali ya utulivu.

Eva alijua pa kuanzia kumpata. Kama angemkosa huko Big Brother House kwa Shija, basi angepanda pantoni kuelekea Kigamboni. 

Alimkuta hosteli, kwa rafiki yake. 

“Sijui kama nataka kukusikiliza Eva, naomba uniache mwenyewe kwanza,” Rumi aliunguruma mara tu alipomwona Eva akiingia pale chumbani na kuufunga mlango.

“Mpenzi wangu, si’vyo unavyofikiria jamani.” 

“Usiniite mpenzi wako. Unajua hata ninachokifikiria? Nilipokutumia ujumbe tuonane cafeteria ile asubuhi ulinijibuje?”

“Rumi nilikuwa na sababu za kutokuja.”

“Ooh! Ulikuwa na sababu za kutokuja kuonana nami ila ukawa na sababu za kwenda kuonana na Dokta Masanga bila kuniambia, wacha we!” Rumi alikejeli kwa hasira.

“Basi angalau nisikilize baba, najua una hasira, naelewa…yaani…I mean…hata mimi nimekuwa nikiumizwa na hii hali.”

“Eva, hebu toka nje!” Rumi alimkunjia sura.

“Hunitendei haki Rumi, umekuwa ukinihoji sana kama vile huniamini au nilifanya kusudi Dokta kutokamatwa. Ndiyo maana niliamua kuanza kukusanya ushahidi mwenyewe kimyakimya.”

Rumi akacheka cheko fupi la dharau.

“Hivi unajua unachokiongea?  Wewe uliyekuwa hutaki kesi ifike mbali, ukusanye ushahidi mwenyewe? Eva, nimekukuta unatoka ofisini kwa Dokta Masanga, na uliponiona ukakimbia. Kwa nini ulikimbia?”

Eva, alishusha pumzi. Itakuwa hakuyasikia maongezi yetu, Angekuwa ameyasikiaa angeshaniwakia juu ya hilo. Aliwaza. Akapata nguvu ya kuendelea kujitetea. 

“Nilikuwa nimetoka kujibizana naye. Akili yangu haikuwa sawa. Unajua ni namna gani natamani kumalizana na jambo hili. Nilikuwa nataka nipate ushahidi ambao utarejesha amani kati yetu.”

“Okay, so far, umefika wapi na huo ushahidi unaoutafuta mwenyewe?” Sauti ya Rumi alijaa dharau.

Eva hakujibu. Alitulia akimtazama Rumi pasipo kupepesa macho. Aliyaacha machozi yaliyofukuta kwenye mboni, yajae kwa kasi na kuteremka mashavuni. Alifumba macho na kuruhusu yatiririke yatakavyo. Mkusanyiko kwa mambo mengi yaliyomvuruga ulichochea mtiririko na kumpa nguvu ya kulia. 

Alitamani kumweleza hofu zote alizonazo, ikiwemo hofu ya yeye Rumi kutumika kumtisha. Lakini, kuyaelezea hayo kungeyamulika mpaka yale aliyotaka yabaki gizani.

Alipoyafumbua macho, alipiga hatua kumsogelea Rumi. Hakujishughulisha kuyafuta machozi yaliyotapakaa mashavuni pake. 

Rumi akatikisa kichwa kulia kushoto. Hakuyaamini machozi ya mpenzi wake.

“Kama utaamua kuachana na mimi sababu tu umenikuta nikitoka ofisini kwa Dokta Masanga, sawa. Sasa hivi hata nikijieleza huwezi kuniamini. Nitapambana mwenyewe, sijashindwa,” Eva aliyafuta machozi kwa vidole vyake. 

Rumi alijikuta njiapanda. Alitaka kumwamini Eva, lakini kuna mengi mno yalimwonya kutomwamini. Wakati huohuo, maneno ya Eva yalimwumiza. Kumwachia Eva apambane peke yake kulimaanisha kusalimu amri mbele ya Dokta Masanga. Alilikumbuka onyo alilopewa. Lilimtia hasira zaidi. 

Naye Rumi alitamani kumweleza dharau na vitisho alivyopewa. Akajikuta anashindwa kufanya hivyo. Nafsi ilimsuta, hata yeye sasa alikuwa anamficha kitu mpenzi wake.

Wakati akilitafakari jibu la Eva, mikono ya Eva ilikuwa inatalii maungoni mwake. Alitaka kuizuia ila nguvu ya kufanya hivyo ilimvuka mwilini na kusimama kando. Akajikuta anajikabidhi mikononi mwa Eva. Kesi za wapendanao, zipeleke uwanja wa fundi seremala. Huko ndiko iliko mahakama yao.

Kulikuwa na hali ya kukamiana, pengine kutokana na hali ya kutokuelewana iliyodumu kwa muda kati yao. Rumi alipoutawala mchezo uwanjani, simu ya Eva ilianza kuita. Wakaipuuza. Wakaipuuza mara tatu na ya nne. Mlio wa kuingia kwa ujumbe ukasikika. 

Eva akamtazama Rumi kwa jicho tepwetepwe; jicho la kuomba kumtoa kifuani pake. 

“Babe, ngoja nione kwanza  ni nani,” Eva alitamka akitaka kuinuka.

“Evaaa! Tulia basi.”

“Inaweza kuwa dharura mpenzi, subiri kwanza.” Eva alizungumza akijiinua kumbusu Rumi pajini.

Akainuka. Akalikusanya shuka na kulitundika mwilini kihasara. Hatua mbili tu zilimfikisha mbele ya meza iliyokuwa na simu. 

Akaufungua ujumbe ulioingia, tayari tumbo likimcheza kwa kuliona jina la mpigaji simu. 

'Najua upo naye, najisikia wivu sana. Usimpe kama unavyonipa mimi.'

Eva alipigwa na butwaa. Dokta Masanga alijuaje kuwa yuko na Rumi? Butwaa lake halikujificha. Hawakuwa na mazoea ya kutumiana meseji baada ya kukutana. Imekuwaje? Hakuzungumza na yeyote juu ya ujio wake eneo lile. Amejuaje?

“Eva, nipe hiyo simu,” Rumi aliamrisha akiinuka toka kitandani.

“Hamna kitu mpenzi, ni ni Zena ana… ana… ame…”

Rumi akampandishia sauti zaidi, “nimekwambia leta hiyo simu hapa!”

Alifikiria kuufuta haraka ujumbe ulioingia. Lakini, simu yake ilianza kuita tena. Mpigaji akiwa yule yule, Dokta Masanga. Rumi aliposimama wima mbele yake na kunyoosha mkono kuiomba simu. Eva alitamani kuitia simu mdomoni na kuimeza.

Akautazama mlango, kana kwamba ungemwamulia cha kufanya.

Mlangoni, nje ya chumba walichokuwemo, alisimama mwanaume mrefu aliyevalia maridadi. Sikio lake moja lilikuwa limetegwa mlangoni. Mkononi akiwa na simu iliyoonesha ilikuwa imetoka kutumika au ilikuwa ikitumika. Mwangaza juu ya kioo cha simu ulidhihirisha hilo. Machache aliyoyanasa kutoka ndani yalimfanya atabasamu.  



Kule ndani, Eva akajitutumua na kumgeukia tena Rumi. Alimwona akivaa bukta yake haraka haraka, uso umemkunjamana.

“Ina maana tumefikishana hapa kweli, Rumi?”

Badala ya kumjibu, Rumi alimkazia macho ya kushurutisha.

“Tumefikia kukaguana hadi kwenye simu? Tangu lin—” Eva alizidi kumlalamikia huku akili ikimtembea.

“Hebu niondolee hizo sob story zako mimi hapa! Leta simu hiyo!” Rumi alimkoromea huku akipiga hatua kumfuata, majigambo ya Dokta Masanga yakiwa hai akilini mwake.

Eva alihamanika. Hakuwahi kumwona Rumi katika hali kama ile hapo kabla. Alianza kurudi nyuma taratibu, ujumbe wa simu kutoka kwa Dokta Masanga ukijizonga tena na tena akilini mwake. 

Aah, Rumi hatakiwi kabisa kuiona hii meseji!

“Rumi! Umm, umekuwaje lakini?” aliuliza huku akiiweka mgongoni kwake ile simu, akirudi nyuma.

Swali hili lilimjaza hasira Rumi.

“Eva! Nipe hiyo ss—”

Wakagutushwa na sauti kutokea nje ya mlango wao. Wakageukia kule ilipotokea ile sauti, kisha wakageukiana, Rumi akisajili mwonekano mpya huku akimtazama Eva kwa jicho la kushutumu.

Seriously?

Hakutaka kuamini, lakini alijua njia ya kulithibitisha hilo ni moja tu. Akaruka kwa hatua moja kubwa kwenda mlangoni akiwa na kibukta tu.

“Uuuwwii!” Eva aliachia kilio cha woga, huku akijiinamia na kujikinga kichwa kwa mikono yake, akidhani anarukiwa yeye. 

*

“Vipi... Nikusadie?” Shija, mmiliki wa chumba walichokuwamo akina Rumi muda ule, alimsaili yule mtu mrefu aliyekuwa asimama mlangoni—nje ya chumba.

Tabasamu likamyeyuka mtu huyo aliyevalia kitanashati.  Ile sauti iliyotokea nyuma yake ilimfanya ageuke kwa gutuko la kufumaniwa. Wakati akigeuka viatu vyake vikajisugua sakafuni na kutoa sauti isiyofichika, huku kiwiko chake kikijigonga kwa nguvu pale mlangoni na kuwashitua waliokuwa upande wa siri wa mlango ule.

Kabla hajatanabahi,  Shija, alishitukia kofi kali la uso. Akabweka kibweko cha mbwa koko. Papo hapo akashindiliwa dochi la korodani. Akadondokea magoti sakafuni huku akiachia yowe jingine kubwa la maumivu.

Mlango wa chumba chake ulifunguliwa kwa pupa, baada ya kupotea kwa sekunde kadhaa za kukorokochwa ufunguo kwa papara kitasani.

Rumi aliruka nje akiwa amejiandaa kumshindilia mangumi mazito mtu aliyeamini ni Dokta Masanga. Aliamini alimfuata hadi pale chumbani kwa rafiki yake alipokuwa akijivinjari na Eva.

Akapigwa butwaa kumwona rafiki yake akigaragara kama joka lililokatwa kichwa pale sakafuni. Wakati huohuo, alisikia vishindo vya hatua za mtu akimbiaye vikishuka ngazi na kutokomea kutoka eneo lile.

“Shija!” alimwita rafiki yake aliyelala miguuni kwake pale kizingini. “Whats up? Mbona hiv—”

“Anakk, anakimbia! Huko!” rafiki yake alimwambia kwa kugumia huku akioneshea kule kwenye ngazi ambako vishindo vya mkimbiaji vilizidi kufifia. 

Rumi alikurupuka. Akazifuata kasi zile ngazi. Hakuona mtu, ila vishindo alivisikia. Akarukia kituo kilichofuata kwenye zile ngazi na kujaribu kuchungulia kule chini vilipokuwa vinapotelea vile vishindo. Akaona sehemu ya mgongo tu wa mkimbiaji huku mkono wake ukiwa unarambaza ukingo wa zile ngazi, ghorofa ya kwanza ya jengo lile la ghorofa tatu. Alijua kutokea pale kwenye ghorofa ya pili alipokuwa asingeweza kumwahi.

Akamkumbuka Eva, aliyemwacha kule chumbani.

Oh, Shit!

Akapiga ubapa wa ngumi kwenye ukingo wa ngazi huku akiachia sauti ya kukereka na hasira. Akageuza na kurudi mbio kule chumbani. Alimkuta Shija amekaa kiwetewete nje ya chumba chake huku amefumbata korodani. Mchirizi wa machozi ulikuwa umegandia mashavuni kwake. Mlango wa chumba chake ulikuwa nusu wazi.

“Ah, mshikaji unazidisha makeke mpaka watu wanakuja kupiga chabo bwana!” Shija alimshutumu kwa uchungu.

“Nisubiri hapo!” Rumi alimwambia huku akimwoneshea kidole. Akapitiliza mpaka ndani.

Kitanda kilikuwa kimetandikwa, na Eva alikuwa akivaa nguo zake haraka haraka.

“Unakwenda wapi?” Alimkoromea.

Eva hakumjibu. Alijishughulisha kuweka nywele zake sawa. Wala hakutaka kujisumbua kuiremba upya sura yake. Rumi akamtazama kwa viulizo. Eva alikuwa anatiririkwa machozi huku akivuta kamasi nyepesi, kimya kimya.

“Nakuuliza swali wewe!” alimfokea kwa sauti ya kunong’ona akijua Shija alikuwa nje ya mlango.

“Narudi chuoni, Rumi. Unataka nilale hapa?”

“Nilikuuliza ule ujumbe ulioingia kwenye simu yako ulitoka wapi… kwa nani?” Rumi aliuliza tena.

“Simu hiyo hapo,” alijibiwa. 

Rumi akasonya huku akiitazama ile simu iliyokuwa kitandani.

“Kwa hiyo sasa unaweza kunipa simu, baada ya kuwa umeshaufuta huo ujumbe?” alimkoromea.

Alijua kuwa ule muda aliokurupuka na kutoka nje akidhani ni Dokta Masanga ndiye aliwafuata pale, ulimtosha sana Eva kuufuta ujumbe wowote ambao uliingia na ambao hakutaka yeye auone.

Eva alivaa viatu vyake, akanyakua mkoba wake. Akaichukua simu yake kutoka pale kitandani.

“Rumi, naomba niondoke. Najua tunahitaji kuliongea zaidi hili suala, lakini ni wazi kuwa leo sio siku yenyewe.”

“Ni yeye ndiye aliyekutumia huo ujumbe ulioufuta, si ndiyo?” Rumi alimwuliza, akihisi miguu kumwisha nguvu na mvuke wa moto sana ukipanda na kushuka ndani ya tumbo lake.

Eva alimtazama kwa hisia, kisha akashindwa kuendelea kukutanisha macho yake na yale ya yule ampendaye. Akajipangusa machozi huku akiinamisha uso.

“Sijui kwa nini unashikilia hili suala Rumi… ila naomba tuliongelee wakati mwingine. Naamini tutalishinda na kulivuka hili.”

“Umeshanasa kwake, siyo?” Ni kama kwamba Rumi hakuwa amemsikia. “Umeshasalimu amri kwake, si ndiyo?”

“Rumi…”

“Na lengo ni nini sasa… ndio ili ufaulu mitihani au nd’o umesha-fall in slave love?” Rumi alizidi kumshindilia shutuma. 

“Oh, Rumi!” Eva aliangua kilio cha kwikwi huku akikimbilia nje ya chumba kile.

Rumi alilipiga godoro ngumi ya hasira, godoro lililotoka kuwakirimu muda mfupi tu uliopita. Moyo wake ulimwuma na alijiona amesalitika visivyo.

Shija aliingia akiwa amejikunja kutokea kiunoni, na kujibwaga kitandani.

“Lah! Yule mshenzi nusura anitoe kizazi wallah!” alilalama.

Rumi akawa makini. "Ilikuwaje?” alimwuliza. 

Shija akamweleza kilichotokea . Hakuwa anapiga chabo huyo.

“Kwa hiyo, unadhani alikuwa anapiga chabo?” alimwuliza tena.

“Sasa kumbe itakuwa nini kingine? We’ umo ndani unapiga jalamba kwenye uwanja wa seremala, jamaa kapita nje kasikia mashamshamu kama yote humo ndani… asitake kupiga chabo?” Shija alimkoromea.

“Haya hapa anapiga chabo kupitia wapi wakati we’ unasema umemkuta mlangoni? Hata mi’ nimesikia kishindo kutokea mlangoni!” alimhoji.

“Ah, bwana eenh, mi sijui. Ila hali ndiyo hiyo. Na kwa kutaka asijulikane akanizaba kofi la uso na akanikalisha kwa teke la chumbani kwa baba (akamtukania mama yake). Dah!” Shija alisikitika.

Rumi akauma meno na kutikisa kichwa. Akawaza, huyu ni mshirika wa Dokta Masanga tu huyu. Ina maana huyu bwege ana mikakati mizito namna hii?

“Kwa hiyo kumbe yule mtu hujawahi kumwona kabla?”

“Siyo tu kabla, hata baada! Yaani alinigeukia na kofi la uso hata sura yake sikuweza kuiona!”

Duh!

Rumi alijisikia vibaya sana. Baada ya kukabiliana na Dokta Masanga uso kwa uso, alijua moja kwa moja kuwa yule mshambuliaji alikuwa ni kibaraka wake. 

“Pole sana, Shija.” Alimhurumia rafiki yake.

“Ah, sio ishu. Haya maumivu yatapoa tu.”

Kimya kifupi kikapita.

“Ni nini kinaendelea kati yenu, Rumi?”

Rumi alimtazama rafiki yake. Akatikisa kichwa kwa masikitiko. Uchungu na wivu vilimfanya asitamani kumjibu lolote. Lakini alijua hilo lisingekuwa sawa.

“Ah, tumetibuana tu... kaniboa sana kwa kweli.”

Shija akaguna.

“Kwa namna alivyoondoka hapa, naona ni wewe ndiye uliyemboa. Ila si neno. Mambo ya mademu mi’ nayajua,” Shija alimwambia.

Rumi hakuwa na la kujibu. Alibaki akiwa amejiinamia huku akimung’unya papi za mdomo.

Nimemkabidhi mwenyewe Eva kwa yule boya, shenz taipp! Alihisi mfukuto moyoni, na mkwamo kooni.

“I gotta go, Shija... pole sana kwa yaliyokukuta.” Hatimaye aliamua kuaga.

“Poa mwana. Mi’ najilaza kidogo,” Rafikiye alimjibu huku akijinyoosha pale kitandani.

*

Dokta Masanga aliingia kwenye baa iliyokuwa  eneo la chuo na kuchagua meza iliyokuwa kwenye kona, akatulia. Muda si mrefu mhudumu alifika, akaagiza kinywaji alichopendelea.

Eva alikuwa akilini mwake. 

Namna yule mtoto anavyojisalimisha kwake kila mara anapombana wakiwa ofisini kwake, ilimfanya ajisikie rijali aliyepata uamsho upya. Eva alikuwa akimpokea tofauti na wasichana lukuki aliowahi kuwanasa na kuwatumia kwa mtego wake wa maksi za mtihani. Hakumfanya ajione kunyanyapaliwa wakati wa tendo.

Ina maana na yeye hatimaye amenipenda? Tabasamu la kibwege likauvuruga uso wake.

Alipiga funda la kinywaji chake, akakirudisha mezani kwa uangalifu mkubwa kana kwamba alihofia kuivunja bilauri iliyohifadhi kinywaji kile. Kumfikiria Eva kulimfanya hivyo.

Akamfikiria Rumi. 

Akauma meno kidogo, akaguna. Ni muda mrefu hajatokea kijana wa kumkabili kama alivyofanya Rumi siku ile alipomwona Eva akitoka ofisini kwake. Hili lilimtia hamu ya kujua kila hatua ya Rumi, ili aweze kumzidi kete kwenye kila anachokipanga dhidi yake.

Kama alivyomzidi kete kwenye lile jaribio lake la kwanza.

Alijua kuwa asipochukua hatua madhubuti yule kijana angeweza kumletea shida. Ndiyo maana ni lazima amvunje nguvu na moyo wa kuendelea kumfuatilia. Akajiambia kuwa hakukuwa na njia bora ya kulitimiza hilo zaidi ya kumwaminisha kuwa hata mpenzi wake sasa hakuwa upande wake.

Na hili alishahakikisha kuwa limetokea.

Akatabasamu. Hivi hawa vijana wanasahau kuwa mimi ni mwalimu wa Sosholojia, eeh?

Simu yake ikaita. 

Alipotazama jina la mpigaji akajua kuwa mtu aliyekuwa akimsubiri pale baa alikuwa amefika. Akapokea. Akamwelekeza mahala alipoketi. Dakika tatu baadaye, kijana mrefu aliyevalia maridadi aliketi kwenye kiti kilichokuwa upande wa pili wa ile meza aliyokuwapo.

“Nipe habari tamu,” Dokta Masanga alimwambia bila hata ya salamu.

“Mmh, bosi, sio tamu kama nilivyotaka iwe, ila inalika tu.”

Dokta Masanga akaguna. “Kulikoni?”

Kijana akamweleza kilichotokea kule hosteli. 

“Una hakika hajakuona sura?” alimwuliza.

“Asilimia mia moja. Lile palanja nililomkata lilihakikisha hilo.”

“Simwongelei huyo mpambe aliyejipendekeza… namwongelea Rumi!”

“Ah, yule bwege hajaambulia kitu. Hajaniona.”

Dokta Masanga alitabasamu.

Kutokea kwenye kaunta iliyokuwa nyuma yake, mteja aliyekuwa akinywa bia taratibu huku akichezea simu yake kwa namna ya kupitisha muda tu, aliitanua picha iliyokuwa kwenye kioo cha simu janja yake kwa vidole, na sura ya mshirika wa Dokta Masanga ikajaa kwenye kioo cha simu yake. 

Akaendelea kuitazama ile sura huku simu ikiendelea kurekodi kwa mfumo wa video, kile kilichokuwa kikiendelea baina ya yule kijana na Dokta Masanga, pale baa. Hakuweza kurekodi sauti za maongezi yao, lakini hilo silo alilolitaka. 

Alizitaka sura zao zikiwa pamoja. 

Aliporidhika, alihifadhi kile alichorekodi kwenye simu yake.

Aliendelea kubaki pale baa kwa muda zaidi baada ya yule kijana mfua uji kuondoka na kumwacha dokta Masanga akiendelea kupata kinywaji peke yake. 

Hatimaye, Bahati aliweka pesa iliyotosha kulipia bia yake pale kaunta, akaondoka.

*

Eva alijilazimisha kuinuka kutoka kitandani. 

Mwili wake ulikuwa ni kama uliochacha kwa kulala kitandani siku nzima bila kujishughulisha. Hakuwahi kutarajia maishani mwake, kuishi maisha ya mtindo huo. Ilimfanya ajione mchafu na msaliti sana kwa siku nzima iliyofuatia siku ile mbaya kabisa maishani mwake. Kumbukumbu zilimrudisha nyuma hadi siku aliyolala na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza alipotoka kucheza muziki. Alizidi kujiona takataka.

Kimsingi, alijiona malaya. Na hili lilimwuma sana.

 Usiku wa siku ile aliyoondoka kwa kilio cha kwikwi pale chumbani kwa Shija, ulikuwa ni usiku mzito sana kwake. Alilolifuata kwa Rumi hakulipata. Yaani alilipata, kisha likamponyoka mikononi mwake kwenye dakika ya mwisho kabisa. 

Kwa sababu ya ujumbe wa Dokta Masanga. 

Ujumbe uliokuja kumpotezea kabisa nafasi ya kuwa kwenye maridhiano na Rumi, jambo ambalo alikuwa ameshalimudu.

Siku ile alipoachana na Rumi hakurudi hosteli. Alienda kukodi chumba hotelini. Hakutaka kuonana na yeyote miongoni mwa rafiki zake kule chuoni. Akajifungia humo chumbani na kupitia hatua zote za mtu anayetaka kulala, ipokuwa kulala kwenyewe.  

Siku nzima iliyofuatia, hakutoka nje ya chumba chake pale hotelini. Hakupokea simu wala kujibu ujumbe kutoka kwa mtu yeyote. Ila, alipata vipindi vya hapa na pale vya kuutafakari mustakbali wake.

Na asubuhi ile ilikuwa ni siku ya tatu tangu yamkute ya kumkuta kule chumbani kwa Shija, swahiba wa Rumi.

Aliguna na kuanza kupiga mswaki, akili yake bado ikiwa imezongwa na mawazo lukuki. Mawazo yaliyoranda kutoka kwa Rumi, kwenda kwa Dokta Masanga, na kwenda kwa Zena…na kurudi tena kwa Rumi…kisha, kwa Dokta Masanga mwenye tabasamu la mamba. Tamu, lakini lenye sumu tele nyuma yake.

Sasa, alimchukia maradufu mwalimu wake. 

Alimfikiria tena Rumi, na jinsi alivyombadilikia kwa namna ambayo hajawahi kuona hapo kabla. Alijaribu kujiweka kwenye nafasi ya Rumi ili angalau amwelewe. 

Akashindwa. 

Aliingizwa kwenye mtego asioukusudia hata kidogo, na aliyemtumbukiza kwenye mtego huo amemwacha peke yake. Sasa alikuwa amenasa na hakuwa na namna ya kujinasua. Hakujua iwapo amchukie Rumi au amlaumu. 

Alichojua, ameumizwa hisia zake, na amechezewa staha yake. 

Kimsingi, aliingizwa kwenye chumba chenye kiza kizito cha ubakwaji, unyanyaswaji na utumwa wa ngono.

Alisimama mbele ya kioo na kujitazama. Hakujipenda hata kidogo. 

Kukaa peke yake mle hotelini kwa zile siku mbili kulimpatia muda muhimu sana wa kuitumia akili yake tangu aachane na Rumi siku ile ya tukio. Jambo moja alilojua ni kwamba, sasa alikuwa peke yake. Kama Rumi ataamua kuja kuungana naye, basi itambidi akubaliane na namna yake ya kukikabili hiki kiza alichomtumbukiza.

Ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yake. 

Amekuwa akipokea jumbe za mfululizo mara tu baada ya kutoka pale kwa Rumi. Na amekuwa akiendelea kupokea jumbe hizo kwa siku nzima iliyofuatia, akiwa pale hotelini. Kinyume na matarajio yake, hakuna hata ujumbe moja uliotoka kwa Rumi. Meseji zote zilikuwa zikitoka kwa Dokta Masanga na kwa Zena.

Yaani ni kama waliopangiana zamu za kumtumia hizo meseji.

Jumbe za Zena zilikuwa za kumtaka wakutane wamalize ‘sintofahamu’ iliyotokeza kati yao, wakati zile za Dokta Masanga zilikuwa ni za kutaka kumjulia hali yake na kumwomba afike mahala alipo ili waonane. 

Hakuzijbu.

Na sasa aliifugua meseji nyingine tena kutoka kwa Dokta Masanga, iliyoingia asubuhi ile.

U-hali gani Eva, all okay? Why hukuwa ukijibu meseji zangu tangu juzi? Leo ndio Ijumaa. Ahadi yetu ipo palepale. 

 Sehemu ya mwisho ya ujumbe wake haikuwa swali wala ombi. Ilikuwa ni amri kali iliyomrukia usoni kutoka kwenye yale maandishi yaliyokuwa kwenye kioo cha simu yake. 

Donge likamsakama kooni.

Rumi alishamsukumia kwenye kizingiti cha chumba chenye kiza bila hata kipande cha mshumaa. Na sasa Dokta Masanga, alimvutia ndani ya kile chumba chenye kiza kwa nyuzi laini za wino mwekundu wa kalamu yake ya kusaishia mitihani. 

Alijua alibakiwa na namna mbili tu za kufanya. 

Arudi kwa Rumi na atoke nje ya chumba kile huku akifeli, au amfuate Dokta Masanga na azidi kujitoma kizani huku akivuna ufaulu utakaomtesa maisha yake yote yaliyobakia. 

Hakukuwa na uchaguzi wa kubaki kizingitini hapo. 

Ni aidha ndani, au nje.

Akakumbuka nukuu aliyowahi kuisoma kwenye kitabu cha mwandishi mmoja maarufu wa riwaya nchini. 'Njia pekee ya kukiingia chumba chenye kiza, ni kuufungua zaidi mlango wa kuingilia.' 

Akaamua kuijibu ile meseji.

I can’t wait. Niambie unanifuata saa ngapi tuelekee.

Muda si muda jibu la Dokta Masanga likatinga simuni.

Smart girl!

Eva akajiuma mdomo na kufinya macho. Silo jibu alilolitamani. Akili ikaanza kumzunguka. Kabla hajajiuliza afanye nini, ujumbe mwingine ukaingia, naye akautazama kwa pupa. 

Alitumiwa pesa kwenye simu yake. Laki moja. Kutoka kwa Dokta Masanga.

“Eish, hii mpya!” aliropoka bila kujielewa. 

Ujumbe mwingine ukaingia.

Hiyo hela chukua Uber sasa hivi uje Kibaha Super Trooper Executive Motel. Room 202. Utanikuta.

Eva akatabasamu. 

Hii ndiyo aina ya maelekezo aliyokuwa akiitarajia tangu awali. 

Alijua alikuwa ana vipindi siku ile. Lakini pia, alijua kuwa alishakosa vipindi tangu siku iliyopita, na kwamba akili yake haikuwa na uwezo wa kuelewa lolote darasani wakati ule.

Aliingia bafuni na kuanza kujiandaa.

*

Asubuhi ile, simu ya Rumi nayo iliita. 

Alipoona kuwa ni Hubiri ndiye anayempigia alikunja uso kwa hasira. Hakutaka kuongea naye. Amwambie nini, wakati kila kitu kimeshasambaratika sasa? Hata hatima yake na Eva sasa hakuwa akiijua.

Simu ikakatika, kisha hapohapo ikaita tena.

Akaipokea.

“Rumi mambo vipi?” Hubiri alimsalimu.

“Ah, poa tu. Ila sina taarifa yoyote ya kukupa kaka. Bado—”

“Huenda mimi nikawa nina taarifa za kukupa?” Hubiri alimkatisha. 

Rumi akamakinika .“Kuhusu Eva?” alimwuliza kwa kiherehere. 

Upande wa pili wa simu, Hubiri akamtupia jicho Bahati aliyekuwa akiufuatilia mjadala ule kutokea kwenye spika ya simu ya Hubiri. Hubiri akamtupia tabasamu lililomwambia ‘Si nilikwambia?’

“Kuhusu Eva sisi ndiyo tunataraji kusikia kutoka kwako...”

“Na si n’shasema kuwa sina taarifa zozote mpya hapa?” Rumi akamjia juu.

Hubiri na Bahati wakatazamana tena, wote wakiusajili fahamuni mwao ukali usio na sababu kutoka kwa Rumi.

“Basi itabidi uje ofisini Rumi. Tunapaswa kuongea kuhusu Dokta Masanga,” Hubiri alisema.

Rumi akasita. Alitaka kuwaambia kuwa hakuona umuhimu wa kuendelea na lile jambo, lakini akajua kuwa hapo ndiyo kabisa atapaswa kwenda kujieleza zaidi.

Akashusha pumzi ndefu za kusalimu amri.

“Sawa kaka... lini?”

“Leo hii Rumi. Angalia ratiba zako tu halafu unijuze.”

Rumi alikuwa ana ratiba ya vipindi vitatu mfuatano asubuhi ile.

“Okay leo sina ratiba. Niambie muda gani.”

“Good. Unaweza kuja sasa hivi?”

“Poa,” Rumi alijibu, na kukata simu.

*

Dokta Masanga alimfungulia mlango wa kile chumba namba 202 akiwa na simu iliyoonesha kuwa ilikuwa imetoka kutumika muda mfupi tu uliopita.

Alikuwa anaongea na nani? Eva alijiuliza. Hakuwa amempigia simu tangu amtumie ujumbe kumjuza kuwa ndiyo alikuwa amepanda gari na ameanza safari.

Dokta Masanga alimvutia ndani ya chumba kile, kisha akachungulia huku na huko kwenye korido nje ya chumba kile, kabla ya kuufunga na kuukomea ule mlango kwa ndani.

Ana mashaka na nini?

Kilikuwa ni chumba cha kifahari sana. 

Dokta Masanga aliyekuwa amevaa joho maalumu lenye nembo za ile hoteli bila nguo yoyote zaidi chini yake, alimtazama Eva kwa uchu. Alikuwa ana uhakika kuwa Eva alikuwa ameingia peke yake pale hotelini. Simu aliyopigiwa na yule kijana wake mfua uji aliyekuwa nje ya ile hoteli muda ule, ilimthibitishia hilo. 

Alimvuta Eva na kumkumbatia.

“Oh, Eva! Thanks for coming, sweetheart. Nakupenda sana we mtoto ujue…?” Alimwambia kwa chombezo huku mikono yake ikimtambaa mwilini taratibu, hali akimtazama moja kwa moja machoni.

Mmh! Ananisachi? “Oh, dokta, subiri basi kwanza jamani…”

“Niite Tindo, Eva. Achana na hii habari ya dokta dokta sasa…”

“Ah siwezi bwana…” Eva alisema kwa deko.

“Nakuhakikishia baada ya leo utaweza tu, Eva.”

“Mh! Haya…”

Dokta Masanga akamwachia. Akamwambia azime simu yake. Eva akatii pasi hiyana. Akaitumbukiza tena ndani ya mkoba wake baada ya kuizima, kisha akauweka ule mkoba juu ya meza mle chumbani. 

Dokta Masanga akamtia tena mikononi. Akampapasa mwili wake kwa pupa huku akimpelekea mdomo wake kwa ajili ya busu la kinywa. 

Eva akaukwepesha mdomo wake.

“Naomba nivue nguo kwanza basi dokta…” alimwambia huku akijichomoa mikononi mwake. 

Dokta Masanga hakubisha. Alirudi nyuma na kuiegemeza sehemu ya nyuma ya mapaja yake kwenye ile meza iliyokuwa mle chumbani, akimtazama kwa uroho ulio wazi.

Huku moyo ukimpiga, Eva alivua koti la jinsi alilokuwa amelivaa juu ya fulana nyepesi. Akalipachika lile koti kwenye mfumbati wa kitanda cha kifahari kilichokuwa mle ndani. Kisha, akaivua ile fulana ya kijivu aliyokuwa ameivaa chini ya lile koti na kubaki matiti wazi. 

Hakuwa amevaaa siridia chini ya ile fulana.

Kwa pembe ya jicho lake, alimwona Dokta Masanga akitumbua jicho na akitanua miguu aliyokuwa ameibana pamoja pale mezani alipokuwa amejiegemeza huku akitweta kisirisiri. 

Eva akamfuata hadi pale mezani alipokuwa amejiegemeza. Akamgeuzia mgongo.

“Naomba unisaidie kufungua kifungo cha hii sketi,” alimwambia kwa deko ya mtoto wa shule ya chekechea.

“With pleasure!” Dokta Masanga alimjibu kwa sauti yenye kukwaruza.

Eva akamgeukia kwa sura ya kujali, na macho yaliyomtumbuka kichochezi.

“Vipi dokta, kuna tatizo?” aliuliza.

Dokta Masanga akamwemwesa. “Kwani, kwa nini?” alimwuliza kwa sauti iliyokwaruza zaidi, pumzi zikimtoka kwa kudukua dukua.

Eva akamgandishia jicho kubwa aliloliweka nusu mlingoti, kisha akamgeuzia tena mgongo kama alivyokuwa awali.

“Sijui sauti yako imekuwaje leo?” alisema kwa sauti ya mtoto anayeweweseka ndotoni.

Dokta Masanga akaanza kumfungua kile kifungo kwa pupa, sasa pumzi zake zikimtoka kwa nguvu na papara kiasi vimbinja vyembamba vilisikika kila alipohema, na Eva akalihisi joto la pumzi zake nyuma ya shingo yake.

Kifungo kikaachia.

Eva akaanza kuishusha taratibu ile sketi iliyoukamata vilivyo mwili wake hali bado akiwa amemgeuzia mgongo yule mwalimu wake wa darasani. 

Aliivutia chini kwa upande wake wa kushoto huku wakati huohuo akiliinua hip lake la kulia. Kisha, akaishusha upande wake kulia huku akiliinua hip lake la upande wa kushoto.

Dokta Masanga alibaki akiitumbulia macho hali ile huku sehemu ya maumbile yake ikimtutumka, na mishipa ya kichwa ikimsimama.

“Ai, jamani... hii sketi nayo…” Eva alilalamika kwa deko huku akiendelea kubinua kiuno chake kulia na kushoto kwa zamu wakati akiishusha ile sketi taratibu sana, na wakati huo huo akichutama nusu mlingoti ili aitoe ile sketi.

“Oh shit, come on, Eva! I can’t take this anymore!” Dokta Masanga aliropoka huku akiivutia chini kwa mkupuo mmoja ile sketi, Eva akaachia kiyowe kilichompoteza mapigo ya moyo Dokta Masanga.

Eva akabaki bila nguo zaidi ya kijiuzi tu kilichopotelea kwenye makalio yake. Dokta Masanga akaganda. Siku zote amekuwa akimwingilia kimwili wakiwa na nguo zao, bila ya utulivu mwafaka. Kama jogoo na mtetea. Kumwona Eva akiwa bila nguo namna ile, kulimlegeza na kumsisimua kwa wakati mmoja. 

Wivu wa hali ya juu ukamchipuka dhidi ya Rumi.

Eva hakugeuka wala hakujisogeza. Alibaki akiwa amesimama hali amemgeuzia mgongo huku ile sketi yake ikiwa imejirundika chini ya miguu yake.

Dokta Masanga alivuta pumzi moja kubwa na kumshika mabega kutokea nyuma, na ndipo Eva alipogeuka. Dokta Masanga akafungua mikono ili amkumbatie, lakini Eva akamwekea mkono kifuani, akamzuia.

“Tulia dokta…leo mimi ndio nitakuwa in charge, kama hutajali,” alimwambia kwa sauti ya deko iliyoizidi ile aliyomtolea kule ofisini kwake ile mara ya mwisho walipokutana.

Mdomo ukamwanguka Dokta Masanga. Macho yakafumba na kufumbuka haraka haraka. Akameza funda kubwa la mate.

“Oh really?” Hatimaye aliuliza huku tabasamu la faraja likimchanua.

“Yes, dokta…really,” Eva alimjibu huku akimvua lile joho na kuliacha likianguka sakafuni. 

Mtu mzima alibaki kama alivyozaliwa mbele ya binti aliyeweza kuwa mwanaye.

“Can you come this way, please?” Eva alisema kwa sauti ya kimasihara, huku akimwongoza hadi pale kitandani na kumlaza. Dokta Masanga akawa mtiifu kuliko mbwa anayeufuata mdomo wa chatu. Sasa, akiwa amelamlaza chali pale kitandani, Eva akaanza kutembezea vidole vyake kutoka chini ya kitovu chake na kuvipandisha taratibu kuelekea tumboni, kifuani na kuvituliza kwenye chuchu ya kulia ya yule mzee.

“Nataka uniahidi jambo moja tu dokta…” alimnong’oneza kimahaba huku akiwa amemlegezea jicho.

Doka Masanga akaafiki kwa kichwa huku akimtazama kwa macho malegevu, pumzi zikimshinda kasi.

“Utaniacha niuchezee mwili wako bila kuniingilia?” Aliulizwa huku akizungushiwa ncha ya kidole kwenye chuchu.

“Aaah! Ndiyo Eva, ndiyo!”

“Good boy!” Eva alisema na kufyatua cheko fupi sana iliyotekenya mshipa fulani kwenye hafamu za dokta Masanga.

Kidole cha Eva kikafika sikioni. Kikarambaza miinuko na mitumbukio ya sikio lile. Dokta akakosa utulivu kitandani.

“Utanijibu maswali yangu kwa ukweli na upendo?” Eva aliuliza, huku mkono wake mwingine ukitembeza kijitaulo kidogo kilichokuwa pale kitandani, kutokea katikati ya miguu yake na kukipandisha sehemu ya juu ya mwili wake.

“Massww-alih, ganh… gani?” Dokta akahoji, kidole sikioni na mtambao wa kitaulo mwilini vilimkosesha umakini.

“Shhh, dokta, I am in charge, remember?”

Dokta akacheka kibwege.

“Yes Eva, lakini…”

“Shhh!”

Dokta akabaki anamtumbulia jicho legevu. Eva akamfunika uso kwa kile kitaulo. Mkono wa dokta ukainuka kutaka kukitoa.

“I am in charge Tindo, remember?” Eva alimnong’oneza huku akiuzuia ule mkono. 

“Oh! Napenda ukiniita Tindo, Eva!” Dokta Masanga akabwabwaja.

Eva alimfyatulia tena kile kicheko chake cha kutekenya mshipa, na Dokta akagumia mithili ya mtu anayekamuliwa chunusi. Eva akainama na kumramba chuchu kwa ncha ya ulimi na Dokta Masanga akatoa muungurumo tekenyevu.

“Tulia hapo hapo Tindo… don’t move!” Eva akamnong’oneza. 

Akainuka kutoka pale kitandani na kwenda kusimama nyuma ya mfumbati wa kile kitanda huku akiwa makini kuona iwapo dokta Masanga atatoa kile kitaulo.

Akaingiza mkono kwenye mfuko wa kifuani wa lile koti lake alilokuwa amelipachika kwenye mkono wa mfumbati wa kile kitanda kwa lengo maalumu.

Akabonyeza kwa usiri mkubwa kijirekoda chake chenye nguvu, ambacho huwa anakitumia darasani kuwarekodi walimu ili kujipunguzia kazi ya kuandika kila wanachoongea.

“Eva…”

“Shhh, I said!” alimjibu kwa sauti yake mtekenyo.

“Ah, I want you Eva… I want you now!” Dokta Masanga alinung’unika, na kiungo cha mwili wake kilidhihirisha hilo.

Eva akarudi na kusimama ubavuni mwa kitanda. Bila kuongea lolote, akamtoa taratibu kile kitaulo pale usoni. 

Dokta Masanga akamgeukia. Mdomo ukammwagika. 

Sasa Eva alikuwa amesimama akiwa mtupu kabisa, kile kichupi chake chembamba hakikuwepo tena mwilini mwake.

“Oh! We mtoto mtamu balaa…hebu do come to me, please!” Dokta Masanga alimwambia huku akimnyooshea mkono.

Eva akaketi kando yake pale kitandani.

“Dokta Masanga, si unajua mimi nafanya hivi kwa kuwa umenishinikiza tu na si vinginevyo?” aliuliza kwa sauti laini, ya manung’uniko.

“Eva, si tulishalimaliza hilo? Mimi nina unachokitaka, na wewe unacho ninachokitaka… hapa tunapeana tu kile ambacho kila mtu anahitaji kutoka kwa mwenzake. Isitoshe, mi’ nakupenda!”

“Yaani kweli unaita kunifelisha makusudi na kushinikiza tendo la ndoa ili nipate maksi zangu halali ninazozistahili… unakuita huku ni kupenda?” Eva alizidi kuuliza huku akimtazama kwa jicho legevu na akimtembezea ncha ya kidole kifuani.

Dokta Masanga alichanganyikiwa. What is this sasa?

Alijihisi ni kama anayerambishwa sukari iliyochanganywa na chumvi.

Akakunja uso. 

“Uliahidi kunijibu maswali yangu yote kwa ukweli na upendo… unakumbuka?” Eva alimkumbusha.

“Why, why now?”

Eva akainama na kuingiza ulimi kwenye kishimo cha kitovu chake, na matumbo ya Dokta Masanga yakalitafuta koo lake lilipo.

“Dokta Masanga, nimekuwa nikijisalimisha kwako zaidi ya mara tatu mpaka sasa…ofisini kwako. Na leo niko hapa na wewe…kwa siku tatu mfululizo, kama ulivyotaka. Basi angalau na wewe uniridhishe kwa kunihakikishia hili…” Eva alimwambia kwa deko.

“Nini, nikuhakikishie nini, Eva?” Dokta Masanga aliuliza huku akili ikimtembea.

“Kuwa unanipenda kweli!” Eva alimwambia huku akimregezea jicho. “Na kama ni hivyo, kwa nini ulitumia njia ya kunifelisha makusudi na kushinikiza tendo la ndoa ilhali ungeweza tu kuendelea kunitongoza?”

Dokta Masanga akapiga kimya. Akamtazama kwa macho yaliyotatizika.

Taratibu, akaukamata mkono wake na kuubinya.

“Eva, unafanya nini wewe?” Alimkoromea, huku akimtazama kwa macho makali. 

----




Rumi aliketi kwenye kochi eneo la mapokezi, ndani ya ofisi ya TAKUKURU. Kwa muda mfupi aliowasili ofisini hapo, na kujitwalia gazeti alilolikuta mezani, alipumzisha kichwa chake kwa kuzama kwenye gazeti, walau kwa muda, maumivu ya hisia aliyosababishiwa na Eva. Alivalia fulana nyeusi yenye ufito mweupe shingoni na mikononi, pamoja na suruali ya rangi ya hudhurungi.

“Rumi,” Bahati aliyewasili ofisini, alimsemesha. “Mambo vipi?”

“Oh, mkuu,” Rumi alijibu baada ya kuinua kichwa kumtazama. “Poa. Vipi hali?”

Rumi alisimama. Wakapeana mikono.

“Safi bosi, karibu aisee,” Bahati alijibu.

“Ah, lakini mimi ndo napaswa kukukaribisha wewe…umeingia na kunikuta.”

Wote wakacheka.

“Na kweli. Umekuwa mwenyeji kwa muda,” Bahati alisema.

Rumi akarudi kuketi kochini.

“Wala usikae tena,” Bahati alimwambia Rumi. “Twende tu ofisini. Hubiri amekwishafika.”

Rumi alisimama na kumfuata. Walikatiza korido za jengo lile, huku kumbukumbu zikimrejesha  alipofikisha shauri lake kwa mara ya kwanza. Alianza kuhisi huenda hakufanya maamuzi sahihi kwa kushirikisha vyombo vya sheria.  

Bahati aligonga mlango na kuusukuma. Wakaingia.

Hubiri alizunguka kwenye kiti hali ya kuwa simu yake ikiwa sikioni. Alipowaona wakiingia, alitoa ishara kwa mkono kuwakaribisha waketi kwenye viti viwili vyeusi vilivyotazamana mbele ya meza yake.

Baada ya sekunde kadhaa, Hubiri aliondoa simu sikioni. Akaiweka mezani na kuwatazama. “Aisee karibuni.”

“Shukrani mkuu,” Bahati alijibu.

“Ahsante kaka,” Rumi alijibu.

“Sasa, bila kupoteza muda,” Hubiri alisema. “Tumekuita ili kupeana mrejesho wa mawili matatu kuhusu issue yetu. Tangu siku ile mpango ulipovurugika mmekuwa kimya sana…je, kuna taarifa zozote ambazo sisi tunapaswa kuzijua?”

Baada ya ukimya kutamalaki kwa muda mfupi, Rumi alifunua kinywa, “Hapana. Sijapata habari yoyote.”

“Hujapata habari yoyote kwa Eva?” Hubiri alisaili. “Au kwa Dokta Masanga?”

Aliyakumbuka maneno ya Juli, moyo ukamlipuka. Kwa mara ya kwanza alisikia sauti kichwani ikimcheka: Ukajiona wewe nd’o wajua kupenda. Kupenda utapenda wewe bwana? Hiko ni kimbelembele tu.

Mtu anaponyanyua kinywa chake kuongea unaweza kuujua udhaifu wake, ujuzi wake na uwezo wake wa kufikiri. Namna anavyotumia lugha, mpangilio wa matamshi yake na matumizi ya misamiati. Hubiri na Bahati walijitahidi kumjua Rumi, kupitia hayo.

“Samahani mkuu, hii kesi naona itanimalizia muda, nami nahitaji kuconcetrate na masomo.”

Hubiri na Bahati wakatupiana macho ya chini kwa chini.

“Hilo si jibu mdogo’angu,” Hubiri aliseama.

“Sina majibu, na sidhani kama ninaweza kuyapata, ndo maana nikaomba kuachana na jambo hili,” Rumi aliongeza.

“Kanuni na taratibu zetu hazipo hivyo. Lazima tuhakikishe tunamtia nguvuni mtuhumiwa, na kama ikishindikana, ni lazima kuwe na sababu za kushindikana. Hatuwezi kufuta shauri kwa sababu tu mmejisikia kuachana nalo.”

“Okay, mnaweza kuendelea na Eva, cause yeye ndiye mhusika mkuu, anayo hiari ya kuamua kuhusu hatma ya maisha yake. Mimi kama nitahitaji kusaidia lolote nitafanya hivyo.” 

Hisia ni kama mche unaohitaji maji, mbolea na hewa ili kumea. Kukosekana kimojawapo hupelekea mmea kutokustawi vyema na hata kufa kabisa. Kwa namna hisia za Rumi kwa Eva zilivyoonesha kila dalili ya kutochanua tena, ilikuwa dhahiri kwa Hubiri kwamba, vile virutubisho vya hisia za kimapenzi, baina ya Rumi na Eva, vilitoweka. Hilo, lilimpa shauku ya kudadisi zaidi.

“Una maana gani kusema kinachoendelea kwenye maisha ya Eva? Ninyi ni wapenzi. Au kuna kitu kisicho cha kawaida?” Hubiri aliuliza.

“Aah, hakuna kitu. Mimi nachotaka ni kubaki huru na ratiba zangu za masomo. Na kama kuna taarifa mpya nadhani itabaki kuwa wajibu wake kukutafuteni.”

Bahati alimtazama Rumi. Akatabasamu. Akayahamishia macho yake kwa Hubiri. Kisha, akaachia mwayo kama mtu aliyeelemewa na uchovu wa safari. Alikwishaona dalili ya kukwama kwa mchakato wa kesi hiyo.

Hubiri hakukata tamaa. Aliendelea kudodosa. “Kuna kitu chochote ambacho Eva alichokwambia labda-”

“Hapana.” Rumi alibebetua papi za mdomo wake kama aliyechoshwa na maswali.

Hubiri alisimama na kuzunguka ndani ya ofisi akichezea kalamu mkononi. Alifanya vile kana kwamba anajaribu kuyachakata majibu ya Rumi kabla ya kufanya maamuzi. Alirudi mezani na kuketi juu ya meza, mguu mmoja ukiwa sakafuni, mwingine ukiwa unaning’inia. Akasema, “Sikia Rumi. Serikali yetu iko makini kufuatilia kesi za unyanyasaji wa kijinsia. Hivyo, jambo likishafika ofisini kwetu linakuwa chini ya uangalizi wa macho mengi. Nikisema leo niifunge kienyeji tu, mtaingia matatani, hususani wewe ambaye ndiye ulisimama kama msaidizi wake. Wewe ni mdogo wetu, mimi na kaka yako ni marafiki, sitaki yakufike makubwa ukiwa chini ya uangalizi wangu mimi. So, ni jukumu lako sasa, kuzungumza nami kama kaka yako ili nijue kama kuna shida nikusaidie, au nikuache ukabiliane na taratibu za kiofisi.”

Rumi alishusha pumzi kwa nguvu. Dhamira ya kugoma kusema chochote ilianza kukabiliana na wasiwasi wa kuamsha vita asiyoimudu. Akawa katikati ya wimbi la mgogoro ndani ya nafsi yake mwenyewe. 

“Rumi,” Bahati alisema, “Kama alivyokwambia Hubiri, kesi hizi za rushwa ya ngono mashuleni, ni mwiba ulioota mizizi. Mwiba huu kwenye kuung’oa husababisha maumivu. Lakini, Serikali haitojali maumivu hayo atayapata nani. Jihadhari usionje ladha ya maumivu hayo.”

“Kimsingi, hii kesi inategemea sana ushirikiano wa Eva kwetu,” Rumi alifunua mdomo na kuanza kuongea. “Nimeamua kukaa pembeni baada ya kuona hakuna dalili za Eva kuonesha ushirikiano kwetu. Ninahisi Eva ameamua kukubaliana na takwa la Dokta Masanga.”

Hubiri alizunguka nyuma ya meza yake, akavuta kiti na kuketi.

“Kwa nini unadhani Eva hana dalili ya kuonesha ushirikano tena?” Bahati alirusha swali.

“Eva amebadilika tu. Hataki hata kulizungumzia suala hili tena kwangu. Mbaya zaidi, nahisi ameanza kwenda ofisini kwa Dokta Masanga peke yake. Kuna kitu wameshaafikiana. Nahofia hata usalama wangu kwa sasa.”

“Kuwa na amani kuhusu usalama wako,” Hubiri alidakia. “Tupo hapa kukusaidia. Popote utakapohisi usalama wako uko matatani hapo ndipo sisi tutakapoanzia kukulinda. Cha msingi, tushirikiane. Tusifichane. Sawa?”

Rumi alitikisa kichwa kuafiki.

Hubiri alimgeukia Bahati na kumfanyia ishara.

Bahati aliitoa simu yake kwenye mfuko wa suruali. Akafungua faili la picha kisha akaiweka simu mezani, mbele ya Rumi.

Papo hapo, Hubiri akamwuliza, “Unamjua huyo?”

Rumi aliivuta vizuri simu na kuitazama picha ile kwa utulivu. Haraka akamtambua Dokta Masanga. Akamtaja.

“Na huyo mwingine aliyeketi naye mezani?” Hubiri aliuliza.

Rumi alirudi kuitazama tena picha ile. Akatikisa kichwa. “Huyu simfahamu.”

“Hebu mwangalie tena vizuri,” Hubiri aliongezea. “Hujawahi kumwona hata mara moja?”

“Simjui kwa kweli,” Rumi alisisitiza. “Lakini kuna kitu nahisi, sijui kama nitakuwa sawa.”

“Umehisi nini?” Hubiri alihoji.

“Juzi, kuna mtu alitufuata sehemu,” alijibu. “Akataka kutuvamia chumbani, tulipomshitukia, alimjeruhi mwenzangu na kukimbia. Sikuwahi kumwona lakini niliona sehemu ya mgongo na mkono tu. Alivaa shati kama hili.”

Hubiri na Bahati walitupiana macho tena.

Rumi aliikuza picha ile ili kumtazama vizuri mtu yule. “Yes. Ndo hilihili, shati la mikono mirefu la drafti, la rangi nyeusi na njano.”

“Huyo mtu aliwafuata wapi? Na mlikuwa na nani?” Hubiri alisaili.

Rumi aliwasimulia mkasa mzima uliotokea kule kwa rafiki yake, baada ya kuvamiwa na mtu asiyejulikana, na baadaye kutoweka.

*****

Dokta Masanga alijiinua na kuketi kitandani. Macho yake makali yalimtazama Eva kwa sekunde kadhaa bila kukapua. “Unataka kufanya nini?”

Eva hakutarajia mabadiliko yale ya ghafla. Akakosa cha kujibu.

Dokta Masanga alisimama. Alikwishahisi dalili ya hatari. Maswali ya Eva yalimwonesha kila dalili kuwa kuna sababu ya kuulizwa vile. Alihisi labda Eva alikuwa akimrekodi. Akakumbuka,alivyokumbatiana na Eva wakati alipowasili, alimpapasa kwa lengo la kuangalia kama amebeba kinasa sauti, lakini hakukiona. 

Sasa ananiuliza maswali ya nini, Dokta Masanga alijiuliza. 

“Mbona sikuelewi Dokta?”

“Hebu simama!”

Eva alipoinuka kitandani, Dokta Masanga akapekua kitanda chote. Hakuona kitu. Akainuka kumtazama Eva, aliyekuwa amebaki mtupu.  Hakuwa na sehemu ya kumpekua zaidi. Akachukua simu na kubofya namba, kisha akaiweka sikioni.

Baada ya simu kupokelewa, akasema, “Vipi dogo!”

Kikapita kimya. Dokta Masanga akasema, “Una uhakika hakuna dalili ya utata?”

Eva aliganda akimtazama Dokta Masanga. Hakujua alikuwa anaongea na nani.

“Sawa. Nitakupigia tena,” Dokta Masanga alijbu simuni. Akakata simu.

“Simu yako ipo wapi?” alimgeukia Eva na kumwuliza.

“Simu yangu ya nini?”

“Eva, don’t play games with me. Simu yako iko wapi?”

“Jamani Dokta, simu si uliambia niizime, nikaiweka kwenye mkoba.”

Dokta Masanga akatembea kuelekea mezani ulipo mkoba. Akaufungua.

Eva alihisi akitetemeka kama mtoto aliyeshikwa na homa kali. Uzalendo ukamshinda, akamfuata Dokta hadi mezani.

Simu ilikuwa juu ya meza ikiwa imefunikwa na nguo za ndani. Dokta Masanga alipoishika, alikuta ikiwa imezimwa vilevile.

“Inamaana huniamni kiasi hicho, mpenzi?” Eva aliuliza huku akiomba Mungu asipekuliwe zaidi.

Dokta Masanga aliukazia macho mkoba wa Eva. Akaupekua kwa kumwaga vitu juu ya meza; lipstick, body spray, diary, pen na vikokoro vilisambaa huku na kule. 

“Kuna jambo unanificha, Eva.” Pamoja na kuwa mwalimu wa Sosholojia, Dokta Masanga alijibidiisha kufahamu maarifa ya Saikolojia. Yakampa uwezo wa kuzisoma tabia za binadamu kwa kuzungumza naye au hata kumtazama tu kwa muda mrefu. Alijaribu kuuliza huku akitafuta upenyo utakaompeleka kwenye jibu.

Eva hakujibu haraka.  

“Kwani shida nini Dokta?”

“Ulikuwa unafanya nini nilipofumba macho?”

Eva alihisi mshituko wa mkubwa moyoni. Akashindwa kuyazuia mapigo yake ya moyo. “Hakuna kibaya nilichofanya Dokta. Ina maana huniamini? Kwa yote niliyokubali kufanya nawe bado huniamini?”

“Sijasema sikuamini. Nimeuliza ulikuwa unafanya ni –”

“No, Dokta,” Eva alidakia. “Huniamini. Nd’o maana nilipoingia tu ukataka nizime simu. Si kama sikukuelewa, nilikuelewa sana, nilijikaza tu. Lakini sasa, unavuka mipaka. Yaani ndani ya hoteli uliyochukua mwenyewe, umenitaka nizime na simu, lakini bado huniamini?”

Dokta Masanga alishusha pumzi kwa aibu. Alijihisi kukosa busara na utulivu. Akasema, “Sasa kwa nini uliniuliza maswali ambayo tayari tulishamalizana?”

“Nilitaka tu kujua upendo wako kwangu,” Eva alijibu huku akilazimisha machozi machoni mwake. “Leo nilitaka kukubali kuwa na mahusiano ya uhakika nawe yatakuaje hali ya kuwa lengo lako halikuwa mapenzi? Lengo lako lilikuwa ni kunipata tu ili kunipatia alama kwenye mtihani…hilo ndilo linaloniumiza kwa sasa.”

“Eva kila mahusiano yana historia yake,” Dokta Masanga alidakia. “Tunaweza kuwa na mahusiano mazuri japo njia niliyotumia kukupata isiwe sahihi sana…”

Eva aliuendea mkoba wake. Akaufungua zipu ya ndani, akatoa karatasi ya rangi ya njano na kurudi nayo karibu na Dokta Masanga. Akamkabidhi. Ni karatasi yake ya mtihani.

“Kama ni kweli unamaanisha unachosema, naomba unibadilishie alama,” Eva alisema akipapasa kifua cha Dokta Masanga.

“Lakini Eva, hapa hatukuja kubadilisha alama. Haya ni mambo tunayoweza kuyafanya siku nyingine kwa utulivu,” Dokta Masanga alijitetea huku bado akiwa na wasiwasi machoni.

“Hilo si tatizo Dokta, kumbuka hata mimi siku ya kwanza sikuja ofisini mwako kufanya mapenzi, lakini ukafanikiwa kufanya ulichotaka. Nami leo ni zamu yangu,” Eva alisema huku akitabasamu. “Tafadhali, nisaidie kama unanipenda kweli. Kumbuka, haya ni maisha yangu. Kumbuka tena, sikuzistahili hizi alama. Nilifanya vyema.”

“Nitabadilisha kwenye system ya chuo, Eva,” Dokta Masanga alisisitiza.

“Kwani ulisahihisha kwenye system ya chuo, Dokta? Nibadilishie kwanza hapa, then huko kwenye system utabadili kwa muda wako.” 

“Sina kalamu nyekundu.”

Eva akaurudia mkoba wake na kuchomoa kalamu nyekundu kule kwenye zipu ya ndani. Akamkabidhi.

Dokta Masanga aliipokea kalamu. Akambadilishia alama na kumpatia ufaulu wa juu.

“Ahsante, Dokta,” Eva alisema huku ametabasamu.

“Nilishakukataza kuniita Dokta.”

Eva alimtazama Dokta Masanga kwa macho malegevu. Akapokea karatasi yake na kwenda kuiweka kwenye mkoba wake. Alipomrudia Dokta Masanga akamkuta amekwisharudi kitandani. Akamfuata.

Wakakumbatiana.

“Umefurahi sasa!” Dokta Masanga alisema. “Nilishakwambia, mtihani ni wangu mimi, nina hiyari ya kufanya nitakavyo.”

“Ni sawa. Lakini alama hizi zilikuwa stahiki yangu. Ulinifelisha tu makusudi, uongo?”

Kauli ya Eva ilimshtua tena Dokta Masanga. Aliitoa mikono ya Eva shingoni mwake. Akasema, “Hebu simama.”

Dokta Masanga alisimama katikati ya chumba akiangaza macho yake kama kinyonga aliyehisi hatari. Macho yake yalitua kwenye koti lililotundikwa. Alikazia macho koti la Eva. Kuna kitu kilimsukuma moyoni aende kuchungulia kwenye mifuko ya lile koti.

Eva alishusha pumzi nzito. Akamwomba Mungu kimyakimya. Akasema kwa upole, “Siamini ninachoshuhudia hapa. Nimejitoa kwa ajili yako sikutaka mimi mahusiano nawe lakini umeona haitoshi unanidhalilisha.” 

“Tulia,” Dokta Masanga alijibu kwa sauti yake nzito.  Akazidi kusogelea koti iliyotundikwa kwenye mfumbati wa kitanda.

Eva akaachia shuka lililokuwa limestiri maungo yake kwa hofu. Miguu yake ilitetemeka alihisi dalili zote za kutaka kuanguka na kupoteza fahamu. Feni iliyopepea chumbani hakuisikia, alihisi tumbo la kuhara na haja ndogo kumshika kwa pamoja. Akarudi kinyume nyume na kujipweteka kitandani. Vitone vya mikojo vikatuama kwenye shuka jeupe.

Macho ya Dokta Masanga yalitua kwenye koti la Eva. Mfukuo ambao Eva aliweka kinasa sauti, kwa kusudi la kumrekodi.

Dokta Masanga akaunyoosha mkono wake kwenye koti. 

“Nina mimba,” Eva alisema kwa sauti ya kitetemeshi.

“Unasema?” Dokta Masanga aliushusha mkono uliokuwa ukielekea kwenye koti lenye kinasa sauti na kumtazama Eva.

“Hujanisikia? Au unataka kupata uhakika kwa nilichokisema?” Alisema Eva kwa kiburi kilichochanganyika na uoga.

“Unahisi au una uhakika?” Dokta Masanga alijibu kwa njia ya swali. Tabasamu pana likaujaza uso wake mithili ya mwana aliyeona ziwa la mamaye.

Likazidi kumchafua Eva. 

Laiti Dokta Masanga angefanikiwa kuona kinasa sauti, hakujua hatma yake ingekuwa ni nini. Akanyanyuka na kuliendea friji ndogo iliyokuwa kwenye kona ya chumba karibu na runinga. Dokta Masanga alimuwahi Eva na kusimama mbele yake.

“Nipishe nichukue maji.”

Ilikuwa ni amri ambayo Dokta Masanga alikaidi. Akayatoa maji chupa ndogo, na kuyafungua. Eva aliyapokea.

Taarifa za ujauzito zilimwongeza furaha Dokta Masanga maradufu, akasahau muda mfupi uliopita alijipa cheo cha ukachero. 

“Ooh Eva wangu, hizi ni habari njema sana,” Dokta Masanga alijaribu kuweka mkono wake wa kulia kwenye tumbo la Eva, Eva akautoa kwa ghadhabu.

Walikuwa mithili ya watu waliokuwa wakiaguliwa kwenye mizimu. Tupu zao zilitazamana na kushangaana kwa kilichokuwa kikiendelea. Maungo ya Dokta Masanga yalilegea mithili ya tango lililotepeta. 

Eva alifanikiwa kuhamisha fikra za Dokta Masanga. Ni kweli, hakuziona siku zake lakini hakujiaminisha asilimia mia moja kwamba ilikuwa ni ujauzito, alijipa matumaini huenda ni mabadiliko ya homoni yaliyosababisha kuchelewa kuziona. 

“Baba huna haya wewe! Umeona kunifanya mtumwa wa mapenzi haitoshi umeamua kunipekua. Unataka kunipekua hadi wapi?” Akapiga hatua na kuiweka chupa ya maji juu ya meza.

“Hapana, Eva. Sio hivyo, mpenzi wang—” Dokta Masanga alimsihi.

“Si hivyo ni nini hiko sasa? 

“Hapana, Eva. Sio hivyo. Mi’ nakupenda mpenzi wangu. Nipo tayari kufanya chochote kulinda penzi letu,” Dokta Masanga alimsihi.

“Mtu unayempenda ungemfukunyua kiasi hiko?” Eva alichukua sketi yake akaipitisha maungoni. “Huniamini, na hakuna penzi lililowahi kudumu bila imani ya wawili.”

“Eva, ningekuwa sikupendi au sikujali basi nisingethubutu kuonana nawe, si rahisi lakini nakuthamini.” Dokta Masanga alijitetea. “Nakupenda. Tayari tunataraji mtoto, utaondokaje namna hiyo? Tunahitaji kuyatatua haya, kukimbia sio solution.”

Eva alibinua midomo yake huku akivaa nguo zake. Alichukua koti lake taratibu ili kutoangusha kinasa sauti na kulitia mwilini. Akili yake ilimchakata kwamba alitakiwa kuondoka pale haraka sana. Akautumia udhaifu wa Dokta Masanga kuondoka. Kwa Dokta Masanga ilikuwa ni Eva kaondoka kwa hasira za maudhi aliyoyasabisha, lakini kwa Eva ilikuwa ni kukimbia kukamatwa na Dokta Masanga baada ya kunusurika. 

“Kwa heri.”

Dokta Masanga alipagawa. Magoti yake yalikuwa chini alipobembeleza penzi la Eva. Mikono yake ilijaribu kumsihi Eva asiondoke lakini hakufanikiwa. Kwa Dokta Masanga ilikuwa ni mithili ya kisu kilichopita kwenye sehemu ya nyama ya moyo wake. 

Muda mwingine inabidi kufikiri kwa hisia na siyo intellectually. Vitu kama hivi ni hisia tu zinahitajika ona sasa nimeidhulumu nafsi kipuuzi, Dokta Masanga aliwaza baada ya Eva kubamiza mlango na kutokomea.

*****

Eva alikuwa sawa na bomu ambalo linalotaka kulipuka muda wowote, lakini ilikosekana sehemu ya kulipukia. Alipotoka nje tu, akachukua bodaboda ambayo ilimshusha kituo cha daladala na kuita Uber  iliyomrudisha chuoni. 

Alihisi njaa ikiutafuna utumbo wake. Laiti zisingetokea purukushani basi angekula hukohuko hotelini. Aliachama mdomo kwa mwayo uliomtoka pasina kuuziba mdomo wake na mkono. Alikuwa chumba cha hosteli akimsubiri Zena.

Alikaa juu ya meza, alishika simu yake akiwa kwenye mtandao wa Instagram akiperuzi kurasa za udaku. Alimsubiri Zena aliyekuwa atoke bafuni. Alisoma udaku huku akili yake ikirejea tukio lilimtokea saa chache zilizopita.

Zena alitoka bafuni akiwa na upande mmoja wa kanga. Alishtuka kumwona, Eva lakini akajitahidi kukausha.

Eva akaachia tabasamu hafifu.

“Ooh Eva, karibu shoga yangu.”

“Asante, mami.”

“Tunaweza kuongea?” Eva alihoji akitamzama Zena alivyojipinda akijifuta maji.

“Sasa hivi?”

“Ndiyo.”

“Basi ngoja nivae mara moja, tutoke nje. Wezangu watarudi si muda.”

“Nimelipenda hilo, dela. Rangi nyekundu hukupendeza vilivyo,” Eva alisema wakikaa kwenye moja ya mawe makubwa nje ya hosteli.

Zena alitabasamu. Fikra zilimjia kulikuwa kuna jambo. Uwepo wake pale haukuwa bure. Alilisoma hilo kwenye sura ya shoga yake.

“Kuna jambo nataka kukwambia, Zena.” 

“Vipi shoga, kuna biashara gani?”

Nafsi ilimsuta Eva kwa maneno ya mara ya mwisho aliyomtolea, Zena. Alimshutumu kwa kusema maneno ya kumtonya Dokta Masanga ambayo mpaka sasa yalishamgharimu vya kutosha. Fedheha ilijidhihirisha usoni mwake. Kwa kipindi chote cha usuhuba wao hawakuwahi kufanyiana inda.

‘Samahani kwa kukukwaza, rafiki yangu. Sikuwa sahihi.”

“Mh—” Zena akanyanyua mabega yake na kugongesha mikono yake. “Nimekusamehe muda, kipenzi.”

Zena hakuonesha hali ya ghaidhi, alimwonea huruma rafiki yake ambaye uso wake haukuwa sawa.

“Asante sana unaj—”

“Shiii—” Zena alitoa sauti ya kumzuia rafikiye kuendelea kuongea. “Limepita hilo, vipi kuna jipya?”

Eva alimpa kumbato rafikiye kwa sekunde kadhaa.

“Jipya lipo, mama’angu.” Eva alisema na kusimama mbele ya Zena.

Eva alihisi kupitiliza kiwango cha ufasiki. Kwa alichotaka kuzungumza ilikuwa ni ghilibu ya kiwango cha juu. Mpaka hapo, Dokta Masanga alishamchachafya vya kutosha. Alipoteza dira zaidi ya bendera iliyofuata upepo. Nafsi yake ilidhoofu kwa ulaghai wa Dokta Masanga na matendo aliyoyafanya. Aliyaona maisha yake yakienda halijojo kwa maamuzi aliyoyafanya nyuma tena kwa siku moja tu.

Eva alifungua kinywa.

“Nimetafakari kile ulichokizungumza. Nitamkubalia Dokta Masanga.”

“Kwa nini? Mbona ghafla hivyo?”

“Sababu ni moja kubwa, sina nguvu ya kushindana na mnoa visu. Na nyama siwezi kuila bila kuikata.”

“Una hakika?” Zena alimvuta mkono na kumketisha. Walitazamana.

“Ndiyo. Lakini sijui nitaanzaje,” Eva alijibu akibebetua papi ya mdomo wake wa chini.

“Ngoja nikupe mpango.” Zena alinong’ona na kujivuta karibu zaidi na Eva. 

“Mtafute kwenye simu, namba yake si unayo?” 

Eva alimkodolea macho.

“Mwambie umekubali. Na chochote atakachosema, kubali mama! Kwani ukimpa mara moja kuna ubaya gani?”

Eva alitoa mguno ambao Zena hakulewa ulikuwa ni mguno wa kwamba amemuelewa au la! 

“Maisha yako hayo Eva, shauri yako! Wewe umetembea na Rumi mara ngapi? Dokta Masanga hataondoka nacho rafiki yangu, mara moja haidhuru.” 

Eva akazidi kumkodolea macho.

“Ukienda huko sasa ucheze lakini sio mpaka—upewe kadi nyekundu. Muoneshe tu mandingo ya hapa na pale asuuzike nafsi yake.” 

Kwa maelezo hayo, Eva akatamani Zena aingie uwanjani kucheza na si yeye. Lakini, kocha anachezaje? Na kama ni ligi, ilishaisha. Labda, iwe mchezo wa mtoano tu.

------------------------


Zena alimtazama Eva kwa muda. Eva akakwepesha macho yake kwa fadhaa. Hilo lilimtatiza Zena, hakujua ni kwa nini Eva amejawa na junaa usoni, ilhali mazungumzo yao yalikuwa ni ya kawaida kabisa kwa marafiki wa kike.

“Kinachonihofisha kwa sasa ni Rumi,” Eva alisema huku akirejesha macho yake kwa Zena. “Amekwishaanza kunishtukia. Tunalumbana mara kwa mara.”

Amekushitukia jambo gani na ilhali hata huyo Dokta bado hujamkubalia? Zena alitamani kurusha swali hilo, badala yake akasema, “Ukitaka kumeza nazi kwanza ujihakikishie njia yako ya haja kubwa.”

“Khaa!” Eva alibutwaika. “Una maana gani?”

“Lazima ujiandae kukabiliana na matokeo ya jambo unalodhamiria kutaka kufanya. Ukianza kuwa na mambo mawili mawili kichwani utafeli. Jipange. Wewe ndiye utakayeamua kuziba nyufa au kuachia mianya itakayompa majibu Rumi.”

Eva alinyamaza kwa muda akijitafakari. Maneno ya Zena yalimchoma moyoni. Kwa namna Rumi alivyombadilikia baada ya kuanza kumshuku nyendo zake, ni dhahiri amekwishachelewa kuziba hizo nyufa, na sasa ana kazi ya kujenga ukuta.

“Kama Rumi ataamua kunichunguza kimyakimya, hapo ndipo nahofia kukamatwa kama kuku, unajua Rumi ana tab–” Eva alisema.

“Ukimpa nafasi ya kuchunguza kimyakimya maana yake umeshindwa kumdhibiti? Kuwa mjanja, tuliza ulimi wako kila unapozungumza naye. Maneno ni kama funguo, ukiyapanga vema yanaweza kufungua mlango wa mahaba moyoni mwake, lakini ukiyatapanya vibaya yanaweza kufungua bahari ya ghadhabu kichwani mwake.”

Kwa namna walivyokuwa wametopea kwenye mazungumzo, hawakuweza kumgundua yule kijana mrefu, mweusi, na mwembamba, aliyefika na kuketi kwenye vimbweta vilivyokuwa kushotoni mwao, akijaribu kufuatilia mazungumzo yao. Kwa namna alivyochomekea shati lake jeupe kwenye suruali nyeusi kiasi cha kuufanya mwonekano wake ushabihiane na ule wa madereva teksi wa miaka ya sabini, isingelikuwa rahisi kumtofautisha na wale wanafunzi waliotumwa na kijiji.

“Zena, unajua Dokta ni mtu mshaufu na mwenye silka ya kujitutumua, anaweza kuanza kumwoneshea Rumi. Hapo hata nikituliza ulimi maneno yangu hayatafaa kitu…sitaki kabisa kumpoteza Rumi!”

Zena alitabasamu. Akatulia kwanza wakati kundi la wanafunzi wa kike lilipopita karibu yao. Alipohakikisha hakuna wa kumsikia zaidi ya Eva, akasema, “Rumi ni kama mwezi na Dokta ni kama jua; huyu akija mchana, yule anaingia usiku. Hawapaswi kukutana asilani abadani.”

Eva hakujibu. Aliganda mithili ya sanamu. Ni kama aliyekuwa akiyatafakari maneno ya rafikiye. Haikuchukua muda akajipapasa kifuani upande wa kushoto, kwa juu ya koti lake kama aliyekumbuka jambo. Akaingiza mkono ndani ya koti, akatoa ile recorder yake na kuiweka kwenye pochi. Kitendo cha kuishika recorder ile, kikamwondolea hamu ya kuendelea kubaki eneo lile.

"Kwa hiyo, unashauri niwasiliane naye lini?” Eva alimsaili Zena.

Yule kijana mrefu, aliyekuwa akiwafuatilia, alisimama taratibu bila kuchokoza umakini wa akina Eva. Akaenda kuketi kwenye kimbweta kingine cha pembeni kidogo. Akatoa simu mfukoni, akabofya namba na kuibandika sikioni.

“Niambie, Senga!” Sauti ya Dokta Masanga ilisikika upande wa pili wa simu.

“Naam. Nimemfuatilia mpaka chuoni hapa…aliingia Block A kisha akatoka na yule rafiki yake… now wameketi nje wanaz–” kijana mrefu, aliyetajwa kwa jina la Senga, alijibu.

“Rafiki yake gani? Zena au?” Dokta Masanga alimkatisha kwa swali.

“Yes, huyohuyo! Naona wamezama kwenye mazungumzo mazito, lakini nashindwa kuwasikia kutokana na umbali.”

“Hakuna mtu mwingine yeyote aliyekutana naye njiani?”

“Hakuna,” Senga alimjibu Dokta Masamga huku akiendelea kuwatazama akina Eva kichinichini. “Alipotoka tu pale hotelini alichukua bajaji, ndipo nami nikamwunganishia kwa nyuma na bodaboda hadi chuoni.”

Kimya kifupi kikapita. Dokta Masanga alisikika kwenye simu akivuta pumzi na kuzitoa kwa nguvu. “Na je, hujaona wakipeana au kuoneshana chochote hapo?”

“Mmh, no,” Senga alisema huku akijaribu kuvuta kumbukumbu. “Yes! Kuna muda nimemwona Eva akitoa kitu kwenye kijikoti chake na kukiweka kwenye pochi.”

“Kitu gani?” Dokta Masanga alisaili kwa haraka. “Au ni simu yake?”

“Lakini simu yake anayo mkononi muda mrefu tu.”

Kilipita kimya cha sekunde kadhaa, kisha Dokta Masanga akasema, “Huo mkoba inabidi tuupate, Senga.”

“Siyo rahisi, Dokta. Tutaupataje?”

“Ngoja. Usiondoke hilo eneo,” Dokta Masanga alisema na kukata simu.

Senga alirudisha simu mfukoni. Akainuka na kurejea kuketi kwenye kile kimbweta alichokuwa ameketi awali – si mbali sana na mahali walipokuwapo akina Eva.

Zena alikuwa akiendeleza somo kwa Eva. “Usiwe na papara. We anza kumtumia meseji za kujibebisha tu, lazima atalipuka, kisha hap–”

Kabla Zena hajaifikisha mwisho hoja, simu yake iliita. Akaingiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake na kuitoa. Alipotazama jina la mpigaji kwenye kioo cha simu, alihisi misuli ya tumbo ikikakamaa. Akaganda kwa sekunde akiitumbulia macho simu yake, kisha akainua uso kumtazama Eva.

“Vipi?” Eva alimsaili.

Hakujibu.

Akarudisha macho simuni.

Jina la Dokta Masanga lilitanda kwenye kioo cha simu.

“Una madeni shosti?” Eva alirusha swali lingine.

“Aheri ingelikuwa madeni,” Zena alijibu huku akikata simu na kuirejesha mfukoni. “Tuendelee shosti.”

Kabla Eva hajaongeza neno, simu ya Zena iliita tena.

“Aah,” Zena alimaka huku akimtazama Eva. “Ni shemeji yako huyo.”

“Kuna usalama lakini?”

“Kuna issue anataka nikamwangalizie,” Zena alisema na kusimama. “Dakika moja please.”

Zena aliondoka eneo lile huku simu yake ikiendelea kuita mfukoni.

Alipoifikia korido ya kwenda chumbani kwao, akatoa simu mfukoni na kupokea.

“Zena, kwa nini unakata simu yangu?” Dokta Masanga alilalamika.

“Aah, samahani Dokta, kuna ujumbe nilikuwa namalizia kuandika hapa ndo maana nikakata.”

“Si kwamba umekata kwa sababu uko Eva?” Dokta alirusha swali la mtego. “Uongo si tabia yako Zena!”

Zena alipigwa butwaa. Akahamanika vilivyo. Alishangaa kusikia Dokta ameijua sababu ya kumkatia simu. Aibu ya kujaribu kumdanganya ikamtandika moyoni. 

“Samahani, Dokta. Ni kweli nilikuwa naye, nikakata ili kwanza nisogee pembeni.”

“Eva amekuja kukwambia nini?”

Swali la mtego.

Zena alipiga kimya kwa sekunde. Alitaka kwanza kuunganisha ulimi wake na ubongo kabla hajafunua kinywa.

“Aah ni story za kawaida tu, Dokta.”

“Unajua madhara ya kusema uongo, Zena? Hivi hata hujiulizi nimejuaje kuwa umekata simu kwa sababu uko na Eva?”

Zena hakujibu.

Dokta Masanga akaendelea kumtega, “Wakati unazungumza na Eva, uliona ametoa nini kwenye koti na kuweka kwenye pochi?”

“Ni recorder yake tu,” Zena alijibu haraka. “Huwa anaitumia kurekodia wakati wa lecture.”

Ikawa ni zamu ya Dokta Masanga kupiga kimya. Bila shaka, jibu hilo lilimtandika moyoni. Haikuchukua muda, akaendelea kuongea kwa utulivu ingawaje sauti yake iliacha taashira ya wasiwasi. “Kwa hiyo, hukugundua namna alivyoitoa kwenye koti, akaihakiki kama iko on kisha akaiweka mkobani ili iwe karibu yako?” 

“Mmh! Sijakuelewa, Dokta!”

“Utanielewaje na ilhali unanificha alichokuwa akikwambia?”

Zena alihisi kuchanganyikiwa. Maneno ya Dokta Masanga yalimdhihirishia hali ya hatari ambayo hakujua sababu yake. Ni kama aliyetegewa kitendawili ambacho ilimbidi kusema ukweli japo kidogo ili asaidiwe kuteguliwa.

“Okay, Eva alikuwa tu ananiambia kuhusu wewe, pamoja na boyfriend wake Rumi. Mimi nilikuwa namshauri akukubalie wewe tu,” Zena alisema.

“Sasa mwenziyo alikuwa anakurekodi hapo…na kwa taarifa yako, hapo alipo ametoka kwangu. Amejaribu kunirekodi lakini hakupata la maana, ndipo amekufuata ili nawe ajaribu kukurekodi. Hatimaye amekunasa. Kama amenasa vizuri sauti yako ukisikika kumshawishi jambo lolote, akizifikisha kwenye vyombo vya usalama ili kunishughulikia mimi, watakunasa wewe. Upo hapo?”

Zena hakuamini anachosikia. Alihisi kuishiwa nguvu. Alihisi kubanwa mkojo. 

Kuhusu mpango wa Eva kushirikiana na vyombo vya usalama, Zena aliyaamini maneno ya Dokta Masanga, kwa sababu kabla urafiki wao haujaingia dosari, Eva mwenyewe alipata kumdokeza. Na kuhusu Eva kumrekodi Zena, taratibu taswira ya Eva akijipapasa kifuani wakati walipokuwa wanazungumza, pamoja na kitendo cha kuitoa recorder yake kisha kuiweka kwenye mkoba, vilimjia Zena kichwani bila chenga.

“Mungu wangu!” Zena alimaka bila kujizuia.

“Tulia!” Sauti ya Dokta Masanga ilirindima. “Maadamu tumeshamjua, tutamdhibiti tu. Cha msingi, usipaniki! Tulia na ufuate maelekezo yangu.”

Dokta Masanga ni mtu mwenye tajriba ya hadaa na mkwasi wa maneno ya hadaa. Alihakikisha anatumia talanta yake vizuri kumcheza shere Zena. Na alifanikiwa. Hatimaye Zena alilegea mithili ya mraibu wa tambuu.

“Kwanza,” Dokta Masanga aliendelea. “Hakikisha hagundui kuwa umemshitukia. Mchangamkie vizuri tu huku ukifanya kila hila uichomoe hiyo recorder…na ukishaipata usifanye lolote mpaka kwanza umewasiliana nami–”

“Recorder tayari amekwishaiweka kwenye pochi. Nitaichomoaje na pochi anayo kwapani?”

“Tuliza akili Zena,” Dokta Masanga alimsihi. “Hakikisha unamganda kila anakokwenda. Atafanya mistake tu. Huo mkoba hajaubandika kwa gundi kwapani.”

Zena alinyamaza akijaribu kutafakari namna ya kufanya. Akasema, “Sawa, Dokta.”

Simu ikakatwa.

Zena akarudi kwa Eva.

“Sasa miye nakukimbia shosti,” Eva alimwambia Zena baada ya kurudi na kuketi. “Tutaonana baadaye.”

Eva alihisi kukabiliwa na hali ya hasira na wasiwasi. “Mmh mbona haraka hivyo!”

“Nataka nikajimwagie maji then nitoke kidogo. Kuna mtu ninahitaji kwenda kumwona,” alijibu huku akisimama.

Oh, Mungu wangu! Nitaipataje hii recorder? Zena aliwaza. Hakutaka kufanya ghilba wa papara ya kuipata recorder.

“Okay,” Zena alisema huku akisimama. “Basi twende tukapigepige umbea, utakapoondoka nitarudi zangu.”

***

Hubiri aliifumbata mikono yake kifuani huku akijizungusha kwenye kiti chake, baada ya Rumi kuhitimisha simulizi yake ya namna alivyofuatwa na mtu asiyejulikana kule nyumbani kwa rafikiye.

“Ima fa ima tunahitaji kumjua huyu mtu,” Hubiri alisema huku akitazama ile picha kwenye simu ya Bahati. “Baada ya hapo, Dokta Masanga hatokuwa na muda mrefu tutamtia mikononi..”

“Dokta Masanga ni mjanja sana. Anakula huku ameficha meno, mtafanyaje kumkatama?” Rumi aliuliza huku akiachia tabasamu la uchungu.

Hubiri aliganda akimtazama Rumi bila kutingishika. Kisha akamwuliza, “Ulishawahi kuona nyoka anavyofanya mapenzi?”

“Nyoka?” Rumi alimwuliza Hubiri huku akigeuka kumtazama Bahati kana kwamba anahitaji washirikiane kustaajabu pamoja. Ghadhabu na mshangao vilitamalaki usoni mwake.

“Yes, Nyoka. Umeshawahi kuwaona wakif–”

“Mimi siyo nyoka na wala sina udugu nao, nitayajuaje mambo yao!”

“Good boy!” Hubiri alitabasamu. “Kama huwezi kujua namna nyoka wafanyavyo mapenzi kwa sababu wewe si nyoka na wala huna udugu nao, vivyo hivyo ni ngumu kujua namna wapelelezi wanavyoweza kumpeleleza na kumdaka Dokta Masanga ilhali wewe si mpelelezi. Namna upelelezi unavyofanyika hushabihiana kwa karibu sana na namna nyoka wafanyavyo mapenzi. Hivyo, ukifanikiwa kujua namna nyoka wanavy–”

Kabla Hubiri hajahitimisha majibu yake ya kifalsafa, simu yake iliita. Akaitoa mfukoni na kuitazama. Kuliona jina la mpigaji kulimfanya apoteze staamala ya nafsi. Alihangaika pale kitini kama aliyemeza nyuki. Alijaribu kuwatazama Bahati na Rumi ili kuona kama wamemshitukia.

Alipoona hakuna dalili ya kushitukiwa, akapokea simu, “Haloo!”

Kimya cha sekunde kadhaa kilipita kabla ya Hubiri kujibu, “Ndiyo. Nipo.”

Bahati alimtazama Hubiri na asielewe anazungumza na nani.

“Yeah! Unaweza!” Hubiri alijibu na simu kukatwa.

Baada ya kuirejesha simu mfukoni, Hubiri alimtazama Rumi na kusema, “Anyway, Rumi, unaweza kurudi chuoni now. Ujio wako umekuwa wa faida sana. Nakuhakikishia, kwa kuanza na huyu jamaa’ake na Dokta Masanga, zoezi hili tutalifikisha mwisho. Lakini kama nilivyokusisitiza, hakikisha unatoa ushirikiano wako kwetu cause haitakugharimu chochote.”

Ni kama Rumi alikuwa akiisubiri kwa hamu ruhusa ya kuondoka mle ofisini. Kabla Hubiri hajatamatisha maelezo yake, alikwishasimama na kusema, “Nimekuelewa kaka. Ahsante sana.”

Hubiri alimtazama Rumi akitembea kuelekea mlangoni. Alipohakikisha ametoka na kuufunga mlango, akamgeukia Bahati. “Eva amenipigia simu!”

“Kunani tena?”

“Sauti yake iko chini sana halafu ni kama vile eneo aliloko kuna mwangwi.”

“Amesemaje?”

“Ameuliza kama nipo ofisini. Nilipomwambia ndiyo nipo, akasema ana jambo la muhimu, anakuja.”

Bahati alibetua mdomo na kupandisha mabega juu.

“Sawa. Tumsubiri.”

“Haya…umemsikia Rumi. Nini maoni yako?” Hubiri alibadili mada.

Bahati alishusha pumzi nzito. Akajinyoosha maungo yake kama mtu aliyetoka kulala. “Kwa maelezo yake, kuna uwezekano mkubwa Eva amekwishatusaliti.”

“Sidhani kama ametusaliti, bali yawezekana ni yeye ndiye amesalitika kwa Dokta Masanga.”

“Unamaanisha nini?”

“Hisia zinaniambia tulifanya makosa siku ile tuliporuhusu Eva amfuate Dokta Masanga ofisini mwake. Bila shaka, kila kitu kilimalizwa that day,” Hubiri alisema huku akijikuna nywele kwa kidole cha shahada. “Unajua mwanzo, Eva alikuwa na dhamira ya dhati kabisa, lakini tangu alipotoka ofisini kwa Dokta Masanga alibadilika moja kwa moja.”

“Bosi, unajua sometimes rushwa ya ngono ni suala la ugavi na utashi, kwamba, mmoja anayo bidhaa inayohitajika sokoni ilhali mwingine ana uhitaji wa bidhaa hiyo, ni vigumu kuwakamata kwa sababu kunakuwa na kitu kama ‘mkataba haramu’ baina ya mtenzi na mtendwa. So, kwa kesi hii, endapo Eva amejikabidhisha mwenyewe mikononi mwa yule bazazi, na anajaribu kumfichia udhalimu wake, bila shaka wamekwisharidhiana.”

Hubiri alifanya tabasamu la fadhaa usoni mwake. Alionesha kumsikitikia Bahati kwa kile alichokitamka. “Hivi umekwishawahi kusoma kitu kinachoitwa Rape myth?”

“No.”

“Okay!” Hubiri alijitengeneza mkao kwenye kiti. “Rape myth ni dhana kwamba, kuna mazingira hutokea mtu akaridhia au kufurahia kutendewa ukatili wa kijinsia. Dhana hiyo huja pale ambapo huonekana mhanga wa tukio alinyamazia ukatili huo!”

“Swadakta,” Bahati alidakika. “Huwa tunasema The absence of no is yes. Unamkuta mwingine hiyo no anavyoitolea puani mpaka unahisi labda amesema yes!”

Hubiri alicheka na kusema, “Haina maana hiyo. “Ngoja nikupe somo. Utafiti mkubwa uliofanywa kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia ulionesha kwamba, asilimia 70 ya wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia, walikiri wazi kwamba, wakati walipokuwa wakitendewa vitendo ya ubakaji walikumbwa na hali ya kushindwa kujiokoa japo kwa kupiga kelele tu au hata kwa kugoma kushikwa. Kitaalamu hali hiyo huitwa involutary inability to move during assault. Nd'o maana nahisi kwa uzoefu wa Dokta Masanga, yumkini alimbananisha Eva siku ileile na kutimiza uhabithi wake. Na kama ilivyo kwa wahanga wengine duniani, pengine Eva naye alikumbwa na hali hiyo ya kushindwa kukabiliana.”

“Duh. Hii kali bosi,” Bahati alisema.

“Tatizo husomi, Bahati. Mbona hii ni study maarufu sana duniani! Kamwe usije ukamlaumu mwanamke aliyetendewa ukatili wa kijinsia kwa kushindwa kukataa wakati alipokuwa akitendewa udhalimu huo…kwa wakati huo, tendo hilo haliwi kwenye milki ya maamuzi yake, bali ni taathira ya kibaiolojia. Hali hii huwatokea hata wanyama…ukiingia YouTube utaona, inaitwa Tonic immobility.”

“Yeah. Kwa wanyama nilishaona kitu kama hicho. Unakuta mnyama anaganda na kushindwa hata kunyanyua mguu wakati wa hatari!” Hatimaye, Bahati alisadikisha kauli ya Hubiri.

“Now we’re talking!”

“Lakini, hiyo ni wakati wa tukio,” Bahati aliendelea kujenga hoja. “Kwa nini sasa, baada ya tukio, kama ni kweli lilitokea, bado Eva anajaribu kukwepesha ukweli?”

“Shida ni kwamba, wahanga wengi hawana elimu hii. Hivyo, baada ya kutendewa ukatili huo na kushindwa kwao kujinasua, baada ya tukio hubaki wakijilaani na kujilaumu wenyewe huku wakijihisi wachafu wa roho na mwili. Na hapo ndipo wengi wao hupatwa na msongo unaosababisha ugonjwa uitwao PTSD, yaani, Post-traumatic Stress Disorder. Laiti siku ile ungemwona Eva aliporudi kwenye gari akiwa amepagawa kabisa; mara afoke, mara asonye, mara alie, ungekubaliana nami kuwa alikumbwa na PTSD!”

“Kwanza, alisema anakuja saa ngapi?” Bahati aliuliza.

“Alisema tu anakuja sasa hivi,” Hubiri alijibu huku akitazama saa ya ukutani. “Kama akichelewa tutampigia kujua kinachoendelea.”

“Nadhani kuna haja ya kuhakikisha elimu kama hizi zinatolewa vyuoni ili kuwanusuru wahanga wa kadhia hizi,” Bahati alisema baada ya kuonesha kuafikiana na hoja ya Hubiri.

“Yes. Nimekwishaandika mpango wa namna Serikali inavyoweza kuwasaidia wanafunzi kujilinda dhidi ya manyang’au kama akina Dokta Masanga. Lakini kwanza, tunapaswa tunyakue TUZO YA NGONO ili tuache alama ya namna tulivyofanikisha kukamata walau manyangumi kadhaa wa rushwa za ngono, ili kujijengea uhalali wa kusikilizwa na kuaminika.”

“Nakubaliana nawe, lakini shida ni kwamba, baadhi ya hayo manyangumi nayo yamo humohumo serikalini au mengine yana ndugu zao humo. Hivyo, mpango mzuri kama huo wako unaweza kuvujishwa na kunajisiwa kabla hata haujatekelezwa.”

“Suala si kudhibiti usiri wa huo mpango mkakati, bali ni kuwa na mfumo madhubuti dhidi ya janga hili. Ukishakuwa na mfumo thabiti, hata kama hao mahayawani wataujua, ni rahisi kwao kuogopa kuliko kuujaribu. Ngoja nikupe mfano, nchini Marekani mwanafunzi mpya anapojiunga na chuo, hutakiwa kujaza fomu maalumu kisha hupatiwa secure number atakayopiga pindi akumbanapo na ukatili wa kijinsia. Namba hiyo inaficha jina lake wakati anapotoa taarifa, na pia taarifa yoyote atakayotoa inapitia kwenye system zaidi ya moja; kuanzia serikalini mpaka kwenye mamlaka za chuo. At least, hata mwanafunzi anajihisi salama ku-report ukatili.”

“Speaking of ujasiri wa–”

Kabla Bahati hajamaliza alichokusudia, Hubiri akamkatisha, “Hebu cheki hapo mapokezi. Nimeona kama kuna mtu amepita nje na akielekea hapo.”

Bahati alitoka na kwenda mapokezi. Punde akarejea akifuatana na Eva.

“Oh Eva, karibu,” Hubiri alimlaki huku akimwonesha mahali pa kuketi.

“Ahsante kaka,” Eva alijibu na kuketi katika kiti kilichoachwa wazi na Rumi.

Bahati alikwenda kuketi kwenye kochi pembeni.

“Najua kuna habari njema…” Hubiri alifungua mjadala huku mikono yake akiitenga mezani.

“Nusu kwa nusu. Kuna njema na mbaya,” Eva alijibu na kujinamia miguuni.

Japo alikuwa amebeba taarifa nzito moyoni, lakini alisalitika mdomoni. Alijishitukia mwenyewe kwa yale aliyokusudia kuyasema. Hisia za namna ambavyo angetafsirika ziliubabua moyo wake.

“Kivipi?”

Eva hakujibu wala hakuinua uso.

“Eva,” Hubiri aliita.

“Abee,” Eva alijibu na kuinua kichwa. Machozi yalikwishamtapakaa usoni.

Hubiri alikunja ndita usoni kiudadisi.

“Nini kimetokea?” alimwuliza huku akimkabidhi karatasi za shisha kutoka kwenye kikasha maalumu kilichokuwa pale mezani kwake, kwa ajili ya kujifutia machozi.

“Ni stori ndefu, kaka. Kwanza naomba mnisamehe sana. Najua nitawakwaza lakini sikuwa na ujanja,” Eva alimjibu baada ya kujifuta machozi kwa zile karatasi laini.

“Kuwa huru, Eva. Madhali umeamua kutushirikisha, funguka tu kila kitu. Nasi tutakuwa pamoja nawe.” 

Eva akafunguka mkasa mzima baina yake na Dokta Masanga, ulioanzia mle ofisini siku ile miadi ilipoharibika.

Hubiri aliganda mithili ya barafu kwenye jokofu. Hakutaka kuonesha mshituko wala mshangao mbele ya uso wa Eva. Alichoweza kufanya ni kumtupia jicho Bahati aliyekuwa ameketi sofani, ili kuona kama amesikia simulizi hiyo, ambayo yeye alikwishaanza kuibashiri tangu mapema.

“Well. Hakuna kilichoharibika, Eva. Hayo mambo huwakumba wengi. Wewe si wa kwanza. So, baada ya tukio lile nini kiliendelea baina yenu?”

Eva alinyamaza kwa muda, akauma mdomo wake kwa ghadhabu, akafuta tena machozi yaliyokuwa yakiendelea kutengeneza michirizi mashavuni. Kisha, akaendelea kusimulia namna Dokta Masanga alivyoanza kumfanya mtumwa wa ngono kila alipoingia ofisini mwake.

“Alichofanikiwa Dokta Masanga ni kuzidi kujilimbikizia idadi ya makosa ya kwenda kuyajibu mbele ya sheria,” Hubiri alisema kwa sauti ya chini yenye kuliwaza na kutia matumaini. “Kuna meseji zozote ulizohifadhi kama ushahidi?”

“Ndiyo. Lakini ni meseji za kawaida tu za kimapenzi. Zile za kunishurutisha zilipotelea kwenye simu niliyokuwa nikitumia mwanzo. Na hiyo nd'o sababu iliyofanya nichelewe kuja kuripoti chochote ili kwanza nikusanye ushahidi mwingine.”

“Bado si neno. Mara ya mwisho kukutana naye ilikuwa lini?”

“Leo,” Eva alijibu na kutulia kidogo. Walau sasa alijizuia kulia. Akaendelea, “Aliniita hotelini. Nikaenda. Na bila ya yeye kugundua nikafanikiwa kumrekodi sauti, akikiri kuwa alinifelisha makusudi ili kunipata kingono. Pia nilifanikiwa kumrubuni anibadilishie alama kwenye paper yang–”

“Are you serious?” Hubiri alimkatisha kwa wahka. “Umemrekodi kwa simu?”

Bahati naye uzalendo ulimshinda. Akainuka na kusogea mezani.

“Nilitumia recorder yangu. Hii hapa,” Eva alisema na kufungua mkoba wake.

Macho ya Hubiri pamoja na yale ya Bahati yaliganda kwa pamoja kwenye mkoba wa Eva.

Eva alitumia takribani dakika moja kuchakua mkobani. Taratibu macho yalianza kumbadilika rangi huku mishipa ya kichwa ikimtutumka. Akasimama na kumwaga mezani kila kilichokuwamo mkobani.

“Oh my God!” Eva alimaka.

“Vipi tena?” Bahati alihoji kwa kihoro.

Eva hakujibu. Aliendelea kuchakua mkobani. Baada ya muda, aliachana na mkoba. Akasimama na kusema, “Recorder haimo.”

Hubiri aliondoa mikono yake mezani na kujitwisha kichwani, huku akijiegemeza kitini.

***

Zena alisimama nje ya hosteli, mkononi akiwa ameshika recorder. Baada ya kufanikiwa kuichomoa kwenye mkoba bila Eva kugundua, aliondoka nayo kwa kasi ya ajabu, akidhamiria kwenda kusikiliza hicho kilichorekodiwa. Lakini kutokana na wingi wa wanafunzi wenziye chumbani, alishindwa. Ndipo akatoka chumbani akitafakari afuate njia gani.

Akiwa bado amesimama, simu yake iliita. Mpigaji alikuwa ni Dokta Masanga. Tangu alipomjulisha kuwa amekwishaipata recorder, haikupita japo dakika moja bila ya kupokea simu yake, akimhimiza aifikishe kwake. Kwa kuwa hakudhamiria kumpelekea kabla hajaisikiliza, akaamua kuzima simu.

______________




MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog