Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

MGENI WANGU WA USIKU

   


MTUNZI: ABYAS MZIGUA



Ilikua asubuhi tulivu na mujarrab kabisa, iliyoshabihiana na 'tatata' za manyunyu ya mvua iliyokua inaishia kunyesha, huku kajiupepo kakiwa kanapuliza kwa mbaaliii! na kufanya wakazi wa Dar es salaam kufurahia shughuli zao walizokua wanazifanya kwa wakati huo vilivyo.


Ni katikati ya jiji hili,eneo maarufu sana la kariakoo, shamra shamra za machinga kunadi biashara zao zikiwa ndiyo zinaanza anza. Nazo honi za magari zikigombea abiria wanaotoka ndani ya kituo cha mabasi yaendayo kasi (a'lmaarufu Mwendokasi) zikipamba moto.


Ilikua ndani ya kituo cha Gerezani, kama wengi wanavyokifahamu. Macho yangu yalikua 'bize' kutafuta daladala inayoelekea eneo la Temeke. Punde tu wakati naendelea kuangaza, nikaliona gari lenye mstari wenye rangi ya kijani tupu, likiwa halina hata abiria ndani yake. Moja kwa moja nikaelekea lilipo na nikapanda tayari kwa safari yangu.


Kama kawaida , huwa napendelea sana kuvaa fulana, hasa zile wabongo walizozibatiza jina la 'form six'. Chini nikiwa nimevalia suruali ya kadeti yenye rangi ya kaki na raba nyekundu zilizoendana na rangi ya fulana. Ukiniona nilivyokua nimependeza, lazima utarudisha tu uso wako mara ya pilI uniangalie tena.


Siti ya mwisho kabisa ndiyo niliyoichagua, niliweka begi langu la rangi nyeusi pembeni kisha nikakaa. Kwakua abiria walikua wanaingia ndani ya daladala ile kidogo kidogo, ikawa imechukua kama dakika tano au saba bado tuko palepale kituoni.


Mikononi nikiwa nimeshikilia kitabu cha RICH DAD POOR DAD kilichoandikwa na muandishi mashuhuri ROBERT KIYOSAKI, kilinifanya kutoona kabisa kama muda ulikua unazidi kuyoyoma na bado hatujaondoka pale kituoni. Kwakweli mimi ni mpenzi mkubwa sana wa vitabu vya aina hii.


"Twende mwanangu, naona 'chenga' tu hapa!!". Niliisikia sauti ya konda akimwambia dereva wake waondoe gari na wajaribu labda watapata abiria mbele ya safari, maana muda wote tuliokua mule kituoni walipakia abiria watatu ndani ya daladala lile.


Dereva bila ajizi akaanza kusogeza 'chombot kabla halijafika mbali hata nje ya kituo hatujatoka

...


" Oy!! Oy!! Oy!! Unaniachaje mwanaaa??", Teja aliyekua anapiga debe akadandia na kudai pesa kama malipo ya kazi aliyofanya.


"Hebu acha 'shazi' mtu wangu, huoni gari nyeupe kabisa hii?", Konda alimjibu kwa kumkoromea huku kama anamsukuma kumtoa kwenye gari.


" Aaan'h au sio? Haina nomaa!!! Si unanifanyia umafia?! Haina noma mwana!!". Yule teja alishuka chini na kuanza kufoka kwa kulalama huku nyuma, gari ikiwa inaondoka.


Nilitabasamu kwa kioja kile kifupi nilichokishudia kisha nikasikitika kidogo, kwa sababu inauma sana barobaro kama yule anashindwa kufanya kazi ya maana na kujiingizia kipato. Badala yake anashinda vituoni kupiga makelele ili apate pesa ya 'ganja' tu!!. Baada ya hapo nikarudisha macho yangu katika kitabu nilichokua nakisoma.


"Tilili!! Tililiii!! Tililiii!!", ilikua ni sauti ya simu yangu iliyokua mfukoni ikataarifu kuna ujumbe ulikua umeingia.


" Oy uko wapi mzee baba?". Hiyo ilikua ni meseji ya mshkaji wangu Ben ambayo ilisomeka hivyo, baada ya kuitoa simu mfukoni na kuisoma.


"Nipo hapa.......". Sijamaliza kujibu ujumbe ule, mara gari ilifunga breki kali na kunipeleka mbele kwa nguvu mpaka simu ikanidondoka mkononi.


" Aaakhh!!", Nilikerekwa kidogo kisha nikaikota maana hata hivyo ilikua ni 'kisimu cha tochi' tu. Kwahiyo haikupata madhara makubwa.


Sasa ile nanyanyuka tu juu hivi baada kuinama kuiokota simu iliyokua imedondoka, kumbe breki yote ile alikua ni abiria aliyetaka kuchukuliwa. Abiria huyu alinifanya nisahau kabisaa kama kuna meseji sijamalizia kuijibu kwenye simu yangu.


Alikua ni msichana mrembo, tena mrembo hasa!!!. Rangi yake nyeupe ya ngozi iliyong'aa, shepu ya dondola na gauni lilimshika vilivyo mwilini ndiyo ilifanya nibaki mdomo wazi. Mwili wote ulikua unanisisimuka na picha ya kuwa na msichana yule kimapenzi haraka ilishajichora akilini mwangu. Kiukweli nilitokea kuvutiwa nae ghafla tu yani.


Macho yaliendelea kuduwazwa na msichana yule aliyegoma kukaa kabisa kwa kudai anashuka kituo cha mbele tu hapo, kitendo kilichofanya niendelee kufaidi 'ushubwada' maridhawa aliokua nao mtoto yule.


"Niache darajani hapo!!", Aliomba ashushwe kituo kilichokua kinafuatia.


"Mmmnh hapana!! Ngoja nijaribu bahati yangu!", Nilijisemea kisha nikarudisha simu mfukoni na begi nikaweka mgongoni.


" Konda na mimi niache darajani hapo!!!". Ingawa nilikua naelekea safari nyingine, nikaomba nishushwe kituo kile kile ambacho msichana yule anataka ashuke.


Si muda mrefu gari ilishafika kituoni, msichana yule alishalipa nauli, alivyoshuka tu akaanza kuchanganya mwendo. Nikawa nataka kumuwahi na mimi baada ya kushuka, konda akanidaka shati...


"Oya nauli yangu mwanangu!!!"


Hahahah!! Yani mpaka nilisahau kulipa nauli unaambiwa, macho huku yakiendelea kuangalia anapoelekea yule msichana ili asije akanipotea, Nikamtolea jero mfukoni nikampa, tena sikutaka hata kusubiri chenchi maana ilibidi anirudishie mia. Huyoo nikaanza kuchangamsha hatua ili nimuwahi yule msichana mrembo, aliyefanya niione asubuhi yangu kama ni asubuhi ya ngekewa!!.


Naye konda hakutaka kushughulika kunirudishia wala nini ile chenchi, akaendelea na shughuli zake. Nilijitahidi kutembea mpaka nikakaribia nyuma ya msichana yule, jambo la kwanza lilonijia kichwani ni kumuita.


"Dada samahani!!!", Nilimuita.


Lakini hakunisikia sijui au alifanya makusudi tu ya kutoitika, na badala yake alizidi kuongeza mwendo,utafikiri ni mtu aliyekua amechelewa mahali anakoelekea.


Nikamuita tena huku safari hii nikiongeza sauti yangu, " Dada samahani!!". Na hapo ndipo akanigeuzia sura yake!!



Baada ya kumuita mara ya pili ndipo akageuka, ghafla ubongo ukacheza na kutoa tafsiri ya kama naiona sura ambayo si mara ya kwanza taswira yake kutua mbonini mwangu. Wakati huo nae alinitazama na kuniangushia tabasamu zito, jambo lililozidi kunitilia shaka moyoni na kuhisi ni mtu ninayefahaminia nae...


"Samahani sana,Nahisi kama nimekufananisha hivi?". Hiyo ndiyo ikawa gia yangu ya kwanza ili nijue naanzia wapi kumteka mtoto yule


" Hahahah!!, ujue na mimi nahisi kama nakufananisha hivi?!!!".Yule msichana alinijibu huku akionesha kama anataka kurudisha kumbukumbu ya kitu fulani. Nilikua nahisi kama ndoto, kwakua nilimuita msichana yule kwa kutegemea majibu ya shombo lakini hali ikawa tofauti kabisa na nilivyotegemea.


"Nishakumbukaa, wewe ni Fadhili!!". Nilishtuka sana mrembo mkali kiasi kile kulifahamu jina langu, nilikua nahisi namfananisha tu kumbe tuliwahi fahamiana hapo kitambo kidogo. Sikukumbuka niliwahi kuona wapi sura yenye mfanano ule ambayo inanifahamu mpaka jina langu, hadi pale aliponitajia jina lake.....


" Ina maana umemsahau Nsagali jamani"

Baada tu ya kuniambia hivyo, ndipo jibu la haraka la kumtambua msichana yule ni nani likanijia, Alikua ni msichana tuliyesoma nae na kumaliza pamoja darasa la saba,na mpaka hapo tunaonana ilishapita takribani miaka kumi tayari. Alikua amebadilika mno, hapo nikazidi kuamini ile kauli ya kuwa "wasichana wanakua kwa kasi sana".


Kila nikikumbuka jinsi msichana yule alivyokua enzi tunasoma, nilijikuta nam'bishia yule demu kuwa si Nsagali...


"Mmmnh!!. Hahah sitaki kuamini kuwa wewe ni Nsagali, Unataka kuniambia ndiyo umerefuka kiasi hiko?".


Ilikua ngumu kuamini kama msichana aliye mbele yangu ndiye huyu anayenitajia. Nsagali niliyekua namkumbuka mimi ni yule aliyekua msichana mdogo zaidi darasani kwetu, Lafudhi yake ya kinyaturu ndiyo ilifanya watu wengi wamtambue, tulipenda sana kumuiga vile alivyokua anaongea.


" Daaah! Wewe si ndiyo ulikua mchezaji wetu bora jamani??!, Ulikua unajiita nani vilee (Akakuna kichwa chake na kujikumbusha kitu kwa muda), eenhee!! Ulikua unajiita PHADHELIC SANTACRUZ!!"


"Hahahh Daah!!! kweli una kumbukumbu!!".


Baada ya kunitajia jina nililokua napenda sana kujiita, hapo ndipo nikathibitisha kuwa ananifahamu kweli.


" Vipi inaonekana kuna sehemu unawahi hivi?", Nilimuuliza

"Yeah!!",Alinijibu huku macho yake ya mapozi yakizidi kunichanganya kichwa changu na tamaa ya kumpata ikizidi kunipanda.

"Basi nitajie namba yako kisha badae nitakucheki".


Bila ajizi msichana yule alinipa simu yake kisha nikaandika namba yangu halafu tukaagana na kila mtu kuchukua njia yake.


" Mmnh!! huu upande niliolalia leo inabidi kila siku ndiyo uwe upande wangu. Sio kwa bahati hizi za asubuhi asubuhi!!". Nilijisemea huku nikiwa kituoni kusubiri daladala ili niendelee na safari yangu nilikokua naelekea.


***

"Yani nakutumia meseji haujibu, mpaka nikashindwa nimueleze vipi mama wa watu. Na kasema baadae atarudi kuja kuchukua kitanda chake, laa si hivyo kasema pesa yake aikute mikononi!!".Muda mchache tu baada ya kufika Ben akaanza kunishushia lawama za uzembe nilioufanya katika ishu za kazi.


Kwa majina naitwa Fadhili Mbwana, ni mhitimu wa kidato cha sita miaka miwilii tu iliopita. Ni kijana ninayeamini mno katika masuala ya kujiajiri, hivyo nilivyomaliza tu kidato cha sita nikaamua kufanya kazi ili nijue changamoto za Maisha zikoje.Lakini Maisha ya nyumbani kwetu niwe mkweli tu, yalikua safi mno!!.


Keko au keko fanicha kama wengi wanavyopafahamu ndipo nafanya kazi zangu za useremala, ukiacha kipaji kikubwa cha mpira ambacho nilikua nacho ila nikajikuta kinakufa kabisa kutokana na msukumo Mkubwa kutoka kwa wazazi wasiotaka kusikia kabisa kuwa nacheza kabumbu.


" Hahahah yule mama naye anaoneka mtata kinoma!!", Nilijibu kisha nikaweka begi langu pembeni na kutoa nguo za kazi, huku pamba zangu nikizivua tayari kwa kushughulika na misumeno.


.......


Saa 3 usiku, nikiwa nyumbani kwetu, maeneo ya Ubungo kibangu, Nikatoa simu yangu ya smartphone ambayo huwa sipendelei kabisa kuishika mchana na badala yake mida ya usiku ndiyo huwa inakua mkononi mwangu...


"Mambo vipi Phadhelic?", Kuiwasha tu ikaingia meseji WhatsApp ya msichana ambaye nimetokea kuzoeana nae mno TAMARA CHARLES, Na chanzo cha kuzoeana nae ni zile posts zangu za vichekesho nilizokua naziachia katika mtandao wa Facebook hadi tukapeana namba kabisa.


Nikaifungua kumjibu, lakini kabla sijamaliza meseji nyingine tena ikaingia ila safari hii ilikua imeingia messenger au inbox ya Facebook , alikua ni msichana anayejiita PENDO DE JONES. Usishangae mpenzi msomaji , yani Mimi kwa wasichana kama nimerogwa.


Sasa wakati nataka kufungua text ya Pendo, Mara kale kasimu changu kadogo kakawa kanaita, namba ilikua ngeni....


" Hellow Fadhili, Nsagali hapa!!", Alikua ni Nsagali, yule msichana niliyekutana nae asubuhi na kumpa namba yangu.


"Ooh kumbe wewe, vipi za tangu mida ile?", Nilimjibu kwa furaha sana, maana kwa uzuri aliokua nao msichana yule sikuwa na hakika kama angenitafuta.


"Salama tu, Niko nje hapa kwenu njoo unifungulie!!".


" Uko nje ya nyumba yetu?!!!!!!!", Moyo wangu uliwaka kwa mshtuko.





"Aaanh acha masihara bwana, wewe kwetu umepajuaje?". Nilihisi moja kwa moja kuwa alikua ananifanyia mzaha tu, maana sikuwa na kumbukumbu ya Nsagali kufika nyumbani kwetu, pamoja na kusoma nae mkondo mmoja mpaka kumaliza darasa la saba mazoea baina yangu na yeye yalikua ni hafifu mno kwa kipindi hiko.


" Hahahah!! Nakutania bwana, mimi niko zangu home tu hapa.",Alinijibu


"Mmnh, umenishtua ujue"


"Hahahah!! Kumbe na wewe muoga hivyo?"


"Hahah uoga muhimu bwana!!"


Basi bwana, Story za hapa na pale ziliendelea huku tukikumbushana baadhi ya wanafunzi tuliowahi kusoma nao, kwenye vituko tulicheka na kwenye simanzi tulihuzunika wote kwa pamoja.


Nilizama katika dimbwi la mazungumzo na simu ile ya Nsagali, kuja kuangalia tayari ni saa nne kasorobo, wakina Pendo wote nilisahau kama tulikua tunachat kwa siku ile, sauti ya kukosha ya mrembo yule nilikua naihisi ikipenya kutoka katika tundu za masikio moja kwa moja hadi moyoni mwangu, daah! Mapenzi haya jamani. Kiufupi mtoto alinogewa kinyama yani na story zangu. Maana mimi mwenyewe pia ni mtu wa mikasa sana, ukikaa na mimi huwa cha kuzungumza baina yetu hakikosekani kabisa, tukilimaliza hili nalianzisha jingine. Sasa baada ya muda kidogo, nakumbuka kuna kitu cha kuchekesha sana nilimwambia...


"Hahahahah!! Unajua Fadhili una vituko sana wewe, inaonekana wifi yangu anafaidi sana!!",Hapo ndipo Nsagali alijikanyaga, alinipa nafasi a'dhimu sana ya kujitengenezea kigoda ndani ya chumba kimojawapo cha mtima wake. Kitu alichokifanya ni sawa na kumualika askari mkereketwa wa kikundi cha Al-qaeda katika sherehe inayofanyika ndani ya ikulu ya Marekani tena bila kumkagua, lazima ajiongeze tu (kama wasemavyo vijana wa kisasa). Na hivyo ndivyo nilivyofanya...


" Noo, mimi sina msichana hivi sasa. Sijawahi kuona msichana aliyenivutia, ila leo asubuhi nimekutana na msichana aliyepiga bomu zito lilofanya moyo yangu ulipuke punde tu aliponigeukia ila sasa, sina hakika kama tayari ana mtu wake msichana huyu. Hivi una boy friend Nsagali??". Hahahah!!!Hapa nilipiga kitu moja inaitwa "Kaunta ataki", wale watu wa mpira wanaijua hii. Nilijianzisha mwenyewe fasta fasta nikapiga chenga mafowadi wa timu pinzani, pale kati viungo nikawavuruga navyotaka, nikatia matobo na kuvisha vidali beki mmoja mmoja halafu nikakokota mbele kabumbu, nikabaki mimi na kipa tu, nikawa namsikilizia ili nijue napiga upande gani.....


"Mimi sina mtu kwa sasa, wanaume nyie hamuaminiki siku hizi. Ila siamini kama hauna mtu!!", Nikaona hapo kipa kashakubali mwenyewe kupisha golini bila hata ya kumpiga chenga, macho yangu yakawa mimi na nyavu, maamuzi yalibaki kwangu aidha niukokote mpira ule mpaka nyavuni au nipige shuti tu....


"Sasa kama mimi nimeweza kuamini kuwa hauna mtu, iweje wewe usiamini?. Nahisi unipe muda tu na nina hakika utathibitisha upendo wangu kwako", Niliongea maneno bembelezi na laini sana yaliyofanya mtoto ashindwe kabisa kuongea na kuendelea kusikiliza, hapo ndipo nikamuita jina lake....


" Nsagali!!!"


"Abeee!!", Aliitika kwa sauti fulani hivi iliyoambata na pumzi nyembamba ambayo imeshushwa katika tundu zake za pua kwa kasi sana.


"Nimetokea kukupenda Nsagali, Nakupenda sana!!!". Sikutaka kuchelewesha, wala sikutaka kujali ile kauli inayoogopwa sana na wavulana wengi kutoka kwa wasichana ya: "mbona mapema mno?", nafahamu fika ule msemo wa wakulu unaosema " Ukichelea sana utakuta mwana si wako". Mapema tu, nililifungua fundo lililokuwepo ndani yangu..


"Mmnh, ujue nini Fadhili naomba nipe muda. Simaanishi kama sikupendi, ila naomba nipe muda kidogo!!". Jibu lake hili ilikua kama ni mtu akwambie "Hebu chukua hii pesa halafu usitumie mpaka nikwambie!!", Yani tayari mtoto alishaingia line. Kama angekua hanitaki angenichomolea pale pale.


Mazungumzo hayakuchukua muda mrefu sana baada ya hapo na tukatakiana usiku mwema. Hata hamu ya kuingia facebook kusoma story katika page nayoipenda sana ya " Simulizi za kipekee" ilikata, uchovu mzito sana niliokua nao ulinifanya nile kidogo sana na kuwahi kulala ili asubuhi nidamke mapema katika kibarua changu cha kila siku...


****


Kesho yake ofisini simu ilikua haikatiki kupokelewa, kila saa Nsagali alinipigia kunijulia hali, kiufupi mrembo huyu alishaingia tayari kwenye anga zangu. Kama ni kuku alianza kuelekea kibla mwenyewe.Muda mwingine nililazimika kuizima na baadae kumdanganya kuwa simu ilizima chaji ili kazi ziendelee.


Siku zilivyokua zinazidi kusonga mmea wa penzi ulizidi kuweka mzizi mipana na mirefu ndani yetu, Tulijikuta tunabadilishana majina kutoka majina yetu halisi mpaka kuitana kina love, dear, baby, honey na mengineyo mengi ya kimahaba.


Siwezi kusema eti ndiyo aliniteka mpaka wale mademu wengine wa mwanzo, wakina Tamara na Pendo nikawapotezea laa hasha!!!. Yani nilikua kama kiraka uwanjani, namba zote nilizimudu. Kila mmoja nilimpa nafasi yake na akahisi kama vile yuko peke yake.


Ingawa kwa kusema ukweli, Nsagali alinikamata kuliko wote, Mazoea yalizidi mpaka kudiriki kuja ofisini kunipitia na kuondoka naye, alitamani muda wote awe nami msichana wa watu masikini. Hakujua alikua anapoteza muda wake kwa mtu fedhuli na m'badhilifu wa penzi kama mimi.


****

Siku moja katika mazungumzo na mshikaji wangu Ben tukiwa pale kazini, jamaa aliamua kunivunjia ukimya kwa jambo moja...


"Oy mwana, unajua naonaga kuna katoto kanakuja hapa halafu mnaondoka wote, hatuambiani rafiki yangu?!!"


"Hahah!! Hamna bwana, kawaida tu!!".


" Aagh hamna nini kaka, vipi lakini umeshapita tayari?". Jamaa Aliniuliza kumaanisha kuwa kama tayari nimeshawahi kufanya nae mapenzi.


"Mmmmh hapana ndugu yangu!!"


"Ohoo!!! Utanifanya nikushushe cheo sasa, unajua demu atakudharau yule nwisho wa siku afuate vibrazameni aruke navyo. Atakuona boya yule, wewe Shauri yako!!!"


"Hahaha!", Nilicheka na kujifanya kama nimepotezea kauli ya Ben, ila kauli ile ilibaki kichwani mwangu ikiranda randa ikiwa haielewi kwa kukaa. Jambo lililonifanya nishawishike na kuanza juhudi za kumshawishi Nsagali nifanye naye mapenzi. Niliona kweli anaweza akaja kuniona bwege mwisho wa siku.


Kila nilipokua namshawishi Nsagali tufanye alikua anakataa, nilifanya mbinu za kila aina ila alikua ananinyima uhondo!!!. Aliahidi na kunambia kuwa zawadi ile ni kwa ajili ya mumewe tu, akimaanisha mwanaume atakayekuja kumuoa.


Ndipo siku moja nilijaribu mbinu ya kumpatia dawa ya kumlewesha ili nimuingilie kwa lazima. Ndiyo!, nilidhamiria kum'baka. Kiukweli nilikua kila nikimtazama tunapokutana na msichana yule mate ya uchu wa ngono yalikua yananijaa katika shimo la mdomo wangu.


Nilichonga na Ben freshi kabisa, nilimtaka ajifanye kama ametukaribisha vile nyumbani kwake. Kisha yeye atatupisha na kutoka, atatuacha mimi na Nsagali mule kwake tukiwa na vinywaji, vinywaji ambavyo ndani ya kinywaji cha Nsagali kuna dawa ya usingizi..


Sikuwa naogopa wala kujali kitakachonikumba baada kuzinduka nikishamfanyia kitendo kile, maana kisheria nitahukumiwa ni mbakaji. Lakini kilichokua bongoni mwangu ni kukamilisha tu hitajio langu..


Sasa baada ya kunywa kidogo tu kinywaji kile, nilianza kushangaa Nsagali kutoa mapovu mdomoni. Alitoa mapovu mengi mdomoni na kudondoka chini huku akipapatika kama samaki aliyetolewa majini na kuwekwa nchi kavu, sikutambua kuwa dawa tuliyomuwekea kama ilikua imezidi kiwango ama ni nini?!, nikawa sitambui cha kufanya. Haraka nikatoa simu na kutafuta namba ya Ben ili aje na tujue tunasaidianaje, lakini kabla simu haijapokelewa Nsagali aliacha kupapatika na kupoa kama mtu aliyezimia.


Dakika tano nyingi Ben alisharudi, aliwahi kumcheck Nsagali kama atakua amezimia au kafariki, mimi wenge likiwa limenipanda sielewi nikae au nisimame...


"Daaaah!! Tumeua ndugu yangu!"


"Acha masihara bwana kaka!!",Nilihisi ananitania kuniambia kauli ya kuua, katika maisha yangu sikuwahi kufanya unyama mkubwa kiasi huo tena kuua!!. Ila sikuwa na budi kuamini kilichotekea, jasho lilinitolea katika kila tundu la kinyweleo lililopo katika ngozi yangu.


Tulikaa muda mrefu kutafakari cha kufanya, tuliogopa kabisa kesi ya aina ile kuifikisha katika chombo chochote cha dola na kuhisi ndiyo itakua mwisho wa maisha yetu ya uraiani na kuingia katika maisha ya kuvalishana 'yunifomu' ama sare za rangi ya machungwa.


Hatukuamua kingine tofauti na kwenda kuifukia maiti ile maporini, bila kuchelewesha tulifanya kazi hiyo kwa kuita tax ambayo tuliilipa pesa mara nne zaidi ya aliyohitaji ili tu akubali na tukaelekea pori lililokua mbali sana na mji kwenda kumfukia Nsagali.


***

Nikiwa nyumbani mida ya saa tano na nusu usiku, mawazo yakiwa yamenijaa. Hamu yote ya kushika simu siku hiyo sikuwa nayo, huku kitu usingizi kikiwa hakipo kabisa machoni mwangu, nikiwa naendelea kukumbuka zile nyakati za furaha nilizokua pamoja na Nsagali..


Mara simu ikawa inaita, kuicheck ilikua imeandika jina Nsagali, Kheee!! Nilishtuka sana na kuogopa kuipokea ila nikahisi ni Ben, labda tuliisahau simu ya Nsagali kule nyumbani kwake, kwahiyo ndiyo kaamua kunipigia kwa kutumia simu ile, nikajishauri niipokee!!


Ile kuipokea tu, sauti na maneno niliyokua nimeyasikia nilitamani niitupe ile simu ivunjike kabisa...


"Hellow Fadhili, mpenzi wako hapa Nsagali. sasa mbona umeniacha kule mbali jamani?. Mimi nimekufuata ili umalize ulichokua unataka unifanyie. Niko nje hapa naomba unifungulie!!!!





Kisha simu ile ikakata..


Niliingiwa ganzi mwili mzima, nikawa sielewi cha kujibu katika simu ile. Akili ya kufanya chochote kwa wakati ule haikuwepo kichwani mwangu, nilikua najihisi kama niko ulimwengu fulani hivi wa peke yangu. Hadi pale nilipoanza kusikia mlango wa chumbani kwangu ukiwa unagongwa...


"Ngo ngo ngo!!!" (uligongwa mara moja tu, kisha kimya kikatawala).


Kwa kweli hapo meno yangu ndipo yalianza kusuguana kwa woga, vijichirizi vyembamba vya jasho vikianza kuteremka usoni mwangu. Nikajitia ujasiri ili niulizie ni nani aliyekua anagonga, maana simu niliyotoka kuipokea muda mchache ilinitisha mno...


"Nani??", Niliuliza kwa sauti iliyokua inatetemeka sana kwa wasiwasi niliokua nao.


Ila hakuna jibu lolote nililolisikia kutoka mlangoni zaidi ya ukimya uliokuwepo kabla hata ya mlango kugongwa, nikaona hapa sasa mambo yanaanza kuwa mabaya, ile mikasa ya kutisha ninayoisikia isikia watu wakiisimulia, yaweza ikawa ndiyo inaanza kunikumba na mimi. Haraka niliinuka kutoka kitandani nilipokua nimejilanza na kuelekea mlangoni, nilijiweka tayari kwa lolote nitakalokumbana nalo, kisha nikaufungua mlango...


Nilistaajabika mno kwa kile nilichokiona, nilikuta gauni la Nsagali likiwa chini ya mlango wangu, gauni ambalo siku hiyo tuliyotoka kumzika ndiyo alikua amelivaa, lilikua limetota damu mno ambapo kwa haraka sikuelewa ilikua ni ya kiumbe gani.


Ile nguo niliiruka kama kinyesi vile, mkuku mkuku mpaka sebuleni, kisha nikakunja kuelekea chumbani kwa wazazi wangu ambao kwa wakati huo walikua wamelala tayari. Ingawa sipendagi kuwasumbua wakiwa wamepumzika, hasa kwa nyakati hizo lakini kwa siku hiyo inibidi..


" Ngo!! Ngoo!! Ngoo! Babaaa!! Babaa!!", Nilogonga kwa nguvu huku miguu ikiwa haitulii kwa woga, unaweza ukasema ni yule mtu aliyebanwa na haja ndogo sasa anashinikiza apishwe msalani.


"Vipi? kuna nini Fadhili?!", Baba alifungua mlango huku kakunja uso kutokana na kukurupushwa kutoka katika usingizi mzito uliokua tayari umemchukua.


" Baba kuna.. Kunaa...", Nilijikuta nashindwa kuelezea yale maajabu yaliyonikuta na kuishia kupata kigugumizi.


"Hebu usipige kelelee.. Kuna nini??!", Baba aliongea kwa sauti ya chini chini na kunituliza huku akielekeza uso wake upande ilipo sebule, yeye alihisi ni kitu cha hatari hasa majambazi.


Baada ya kuona nashindwa kuongea sawa sawa ikabidi anichukue tuingie ndani kwake ili nimuelezee vizuri...


" Hebu nieleze Fadhili kuna nini?", Baada kuingia ndani na kuuloki mlango, alinituliza huku akinishawishi nimueleze kipi kimejiri. Macho yake yaliyokua yameiva kwa rangi nyekundu na kuyatumbua kwa woga yalionesha ni kiasi gani alihitaji kufahamu kilichotokea.


Muda wote huo purukushani zile zilivyokua zinaendelea, mama yeye alikua wala hana hata habari, alikua katika usingizi mzito mno...


"Nime...nimeota baba!!", Nilikua sina cha kumueleza baba zaidi ya kumdanganya, woga wa kumwambia ukweli uliuziba ukingo wa matamshi yangu..


Huku taswira ya wasiwasi taratibu ikianza kufutika usoni mwake, na hali ya kawaida ikianza kumrejea, baba alishusha pumzi kisha akaniambia..


" Hahah! Acha woga mwanangu, ndoto ni jambo la kawaida sana. Kwani umeota ndoto ya kutisha sana?"


"Ndiyo mzee, inanitisha sana". Nilimjibu huku mapigo ya moyo wangu yakiwa hayajaacha kwenda kasi, pamoja na baba kufanya jitihada za kunituliza. Ile hali ilikua inatisha sana kwa kweli.


Baba alitazama pembeni, kisha akatoa saa yake kuu kuu iliyokua kwenye meza na kuiangalia.....


" Ni saa sita kasoro sasa, hiyo ni mojawapo mwa zile ndoto za kiakili tu, hazinaga ukweli ndani yake. Wewe nenda kalale tu!!"


Kauli yake hii nilihisi kama ananimwagia makaa ya moto usoni, kule ndani ambapo vioja vimenikumba ndipo yeye anahitaji nirejee nikalale.Hataa!! Niligoma kwenda mwenyewe na ikabidi nimuombe mzee kitu kimoja...


"Mzee mimi naomba nilale hata hapa chini, kule ndani pamenitisha sana!" Nilimuomba, wajihi wangu ukiwa umetota khofu. Hali iliyomfanya baba kushindwa kunikatalia na kuniruhusu nilale.


***


Ni saa 12 na dakika zake ndipo nilizinduka kutoka katika usingizi uliotanguliwa na fadhaiko zito jana yake. Wakati huo nashtuka, bado baba na mama walikua wapo katika sayari ya ndoto.


Sikutaka kuwabughudhi, nilijiinua nikatoka nje. Bado moyo wangu ukiwa una woga, taratibu nilijongea kukaribia mlango wa chumba changu. Nikatazama chini kama ile nguo niliyoiona jana ipo, lakini haikuwepo.


Nikashusha pumzi, huku mkono wangu wa kulia ukiwa umeshika kitasa cha mlango wa chumba changu, nikawa najipa shauri la kuufungua ama kutoufungua. Mwishowe nikajipa ukauzu, pole pole nilizungusha kitasa huku nikichungulia kwa jicho moja moja ndani, nilikua naogopa kwa kuhisi kama naweza nikakuta kitu cha ajabu mithili ya yaliyonikuta jana yake.


Hakukuwa na kitu chochote ambacho macho yangu yalikutana nacho zaidi ya hali ya ushwari chumbani mule, kila kitu kilikua kipo sawa bin sawia, ishara yoyote haikuwepo kuonesha kama kuna kitu kibaya mule ndani. Kidogo nikaanza kujipa matumaini akilini....


"Aagh! Saa nyingine yalikua ni mauzauza tu ya woga!!". Hali ile ya usalama, ilisababisha nione kuwa hakuna chochote zaidi ilikua ni kujitisha kwangu tu.


Kama ilivyo ada yangu, nilijiandaa haraka haraka nikaanza safari ya kuelekea kwenye kibarua changu. Simu toka jana yake nilikua nmeizima na sikuwasha hata kusema niweze kuwasiliana na Ben kujua hali yake ikoje.


Mawazo mazito yakiwa yanaongoza kikao ndani ya ubongo wangu, mwili wangu ulikua uko safarini lakini akili ilikua inawaza tu kuhusu Nsagali.


Nikiwa niko njiani, kabla sijafika barabara kuu ili nikachukue daladala. Ghafla ikatokea Noah nyeusi na kupaki mbele yangu. Nilisimama kidogo, nikanyanyua macho kuitazama kisha nikaendelea kutembea bila kushughulika nayo kwa lolote,nilihisi ni mtu tu na mambo yake, kabla sijafika mbali...


" Piii!! Piii!!" Ile Noah ikanipigia honi mara mbili, ikabidi nigeuke kuitazama. Mara mkono ishara ya kunipungia, mkono ulitokezwa kwenye kioo cha dereva ambacho muda huo kilikua kimeteremshwa.


Bila ajizi ya aina yoyote nilirudi kuelekea kwenye ile Noah, sura ya mwanamke aliyekua anaendesha ilikua si ngeni kabisa machoni mwangu. Mama Abyas ndiyo jina nililomfahamu kwalo, huwa namuona sana anapokuja kumsalimia mama nyumbani, yeye na mama yangu wameshibana sana utafikiri mtu na dada yake, kumbe ni mtu na shosti yake tu.


"Vipi hujambo Fadhili?" Alinijulia hali na tabasamu zito akilishusha juu yangu.


"Salama tu, shikamoo mama!!", Nilimjibu kisha nikamuamkia huku na mimi nikitabasamu. Maana nilianza kuona kijiishara cha kupata mtelezo (lifti).


" Marhabaa!, vipi si unaelekea Ubungo?", Aliniuliza.


"Ndiyo mama, naelekea Ubungo".


" Basi panda twende nikusogeze kidogo hapo!!" Nilishkuru MUNGU kweli, kwakua tayari nilikua nimeshachelewa kibaruani.


Kabla hatujafika mbali, tulikuta mwanaume na mwanamke njiani wakiomba msaada, waliashiria kuwa walihitaji usafiri, kwa sababu yule mwanamke alikua ni mjamzito na anaonesha tayari uchungu wa kujifungua ulianza kumkamata. Kilichonishangaza yule mama hakusimamisha gari...


"Lakini mbonaa....mnh!!!" Kabla sijamaliza kumhoji kwa kitendo alichofanya, nilijishtukia nakabwa na kuzuiwa kuzungumza kutoka kwa mtu aliye kwenye siti ya nyuma. Sikutambua chochote kilichoendelea baada ya kudungwa sindano na mama yule, nahisi ilikua ni sindano ya usingizi mpaka nakuja kushtuka niko ndani ya chumba chenye kiza kizito mnoo...


"Usiogope Fadhili uko mahali salama tu, tunachotaka kutoka kwako ni utueleze yule msichana umempeleka wapi!!!" Ilitokea sauti ya kiume mule mule kizani, nikiwa siioni suraye aliyekuwa anazungumza.


"Msichana gani?" Kwa sauti ya uchoovu sana nilimuuliza, mikono yangu ikiwa imefungwa nyuma ya kiti nilichokua nimekalishwa.


"Nsagali!!", Alinijibu. Nilihisi kama sijamsikia vizuri nikamuuliza tena..


" Unasema nani?"


" Fala nini, ina maana huna masikio au? Nimekwambia N..saa..gaaa..liiii!! Nsagali!!", Alinijibu kwa kufoka.


"Mungu wangu weeeh nimeshakamatwa na polisi!!".. Akili ilishanituma tayari polisi ndiyo wamenikamata ila bado kuna maswali yasiyo na majibu yakawa yanajijenga kichwani mwangu...


" Ina maana Mama Abyas ni polisi? Mbona nilikua sijui?! Na kama ni polisi, polisi gani wanakamata kwa kumlewesha mtu na kumkaba? Au ndiyo wale usalama wa taifa nini?", Nilihisi kama niko katika sinema fulani hivi ya kihindi ambayo inaanza mpaka inaisha steringi hajulikani ni nani.


Kabla hata sijafika mbali na yale mawazo niliyokua nayo, nilipigwa bonge moja la bao mgongoni, bila hata mpigaji mwenyewe kumuona. Kisha ile sauti ikaendelea kuuliza..

"Nsagali yuko wapi?"


"Mi!..mi!..mimi sijui yuko wapi!" Nilijibu kwa kubabaika na mnung'uniko nikitamani niangushe machozi, yule jamaa alizidi kung'ang'ania nimueleze wapi alipo Nsagali, alinipiga ngumi za tumbo, alinibana sanaaa!!! Ila sikutaka katakata kusema ukweli kuwa nilimuua Nsagali na tayari kafukukiwa.


"Oy JIBABA!!! Mida hii, achana nae mjinga huyu. Twende kwanza huko, kisha tukirudi atatueleza vizuri laa si hivyo. Tutamtoboa tundu hilo!!", Niliisikia sauti nyingine ikitokea pembeni ikimwambia mwenzake aliyekua ananipa kibano waondoke na badala yake watarudi baadae kuendelea kunihoji, na kama sitoeleza watanifanya kitu kibaya.


Nilihisi wakati wa ahueni kwangu baada ya wao kutoka, lakini vile vile nikawa naona kifo ndiyo kinaninyemelea zaidi wakirudi huko waliokoenda. Kabla hazijapita dakika nyingi, nilishanga kuona mtu ananivua kitambaa usoni mwangu, hapo ndipo nilipogundua kuwa halikua ni giza ndani ya chumba kile bali macho yangu ndiyo yalikua yamefungwa.


Mwanga mkali wa chumba kile ulitua machoni mwangu na kunifanya niyafumbe kwa dakika chache kisha nikafumbua, sikuamini kwa yule niliyekua namshuhudia mbele yangu, yule yule tuliyetoka kumfukia usiku wa jana yake, alikua mbele yangu.


Nilianza kuona nakuwa mwendawazimu sasa, maana taharuki nazozipitia nashindwa kuzielewa kabisa, nilitamani kuinuka kukimbia lakini kila nikitaka kujaribu nashindwa, mikono yangu na miguu yangu yote ilikua imefungwa juu ya kiti nilichokua nimekalishwa...


"Sssshhhh!!"Nsagali alininyamazisha na kuniwekea kidole chake cha shahada mdomoni mwangu, kuashiria nisizungumze lolote.


" Ndiyo umeniua, lakini kwa bahati mbaya mimi si kiumbe wa kufa. Unaweza ukawa unanihisi unanifahamu ila mimi nakufahamu mara mbili ya ufahamu wako juu yangu, Ni historia ndefu sana Fadhili. Nachotaka kusikia kwako hapa ni ahadi, ndipo nami nitakusaidia kutoka eneo hili. Bila ya hivyo, wakirudi lazima watakuua tu!!" Yule Nsagali aliongea kwa sauti ya chini chini sana akiangilia huku na kule, ndani ya lile godauni kubwa nililokua nimefungiwa.


"Niko tayari kwa lolote tu!, ili mradi nisife. Lakini ni msaada gani huo unautaka kutoka kwangu?", Nilimjibu huku nadadisi kipi alichokua anakihitaji.


" Sitokwambia, mpaka uniahidi kwamba utanisaidia jambo langu!! Kama hutaki nikuache tu hapa hapa!!", Alijibu huku akionesha msisitizo kwa anachozungumza.


"Hapana! Hapana!! Usiniache tafadhali!! nitaku... Nitakusaidia, niko tayari!!", Nilijiingiza katika makubaliano na kuweka ahadi nisiyoijua.


"Funga macho!?", Yule Nsagali aliniambia nizibe macho, haraka nikafanya kama alivyohitaji.


Kufumba na kufumbua, nilijikuta katikati ya msitu, giza la usiku likiwa limetawala na milio ya ndege ikichachama katika msitu ule, hakuna nilichokua nakiona kingine . Ilikua ni peke yetu yani, mimi na yule msichana, Nsagali. Nikiwa niko vile vile kwenye kiti changu huku nimefungwa mikono,yule msichana akaanza kuzungumza..


" Pamoja na ukatili ulionifanyia lakini nimekusaidia, hahah! Inashangaza sana Fadhili. Najua una maswali mengi mno kichwani mwako kuhusu mimi. Mimi ni nani? Inakuaje sijafa wakati ulinifukia kabisa? Yule mama Abyas anahusikaje? Mbona ulitekwa kisa mimi? Na mengine mengi. Ngoja nikupe historia fupi kidogo!!",Nsagali alizungumza na kusogea karibu yangu kisha akaendelea tena kuongea...


"Mimi si binadamu na wala si jini, ila ni kiumbe niliyetengenezwa Fadhili".


"Kiumbe uliyetengenezwa?! Kivipi yani?" Nilishangaa sana na kumuuliza.


"Hahahah (alicheka), Ngoja nikuambie kitu. Mnamo mwaka 1962, kuna wafungwa watatu walifanikiwa kutoroka katika jela ngumu sana, inayoitwa ALCATRAZ!!!. Alikua ni bwana mmoja anayeitwa Frank Morris na mapacha wawili John Anglin pamoja na wenzake Clarence Anglin. Kutokana na jela hii kuwa imezungukwa na bahari ilisadikika watu hawa walifariki kwa kuzama baharini au kuuliwa na samaki wakubwa kama vile papa, ikapelekea FBI kufunga jalada la kesi zao...(Nsagali aliendea kunielezea, nilikua ni mwenye kushangaa tu, maana naona kama ni mapicha picha fulani hivi aniambiayo)


...Kumbe walikua wanajidanganya, hawa watu watatu walikua hai kabisa. Miaka mingi baadae, kama mwaka 2013 hivi, kuna barua ya ajabu iliokotwa karibu na chombo cha habari. Barua hii ilikua inatoka kwa yule pacha mmojawapo, yani JOHN ANGLIN, akitoa taarifa kuwa yeye yuko hai na ana miaka 83, alisema Frank tayari amekufa 2008 huku pacha mwenzake Clarence akiiaga dunia mwaka 2011".


" Sasa mimi nahusikaje kwenye hayo mambo jamani?!!, Au kosa langu ni vile kutaka kukubaka na ikashindikana hadi nikakufukia?, Naombeni mnihurumie jamani, ni tamaa tu za kibinadamu na najutia sana kwa tukio nililofanya!!" Nilizungumza huku uso ukiwa umetekwa na woga, sauti iliyonitoka ilikua inaashiria ni mtu anayetaka kulia.


"Hahah! Kosa si hilo Fadhili, Mimi nilikua nakuwinda mda mrefu sana ila wewe hujui tu. Usiku wa leo kuna UGENI utaupata. John Anglin alituchukua tukiwa katika kituo cha mama Abyas,kituo cha kulea watoto yatima,tulikua kama watatu hivi kwenda kufanya majaribio ya kutengeneza viumbe ambao WANATAKIWA KUITEKETEZA DUNIA!!!, John anahisi ndugu yake amefariki kutokana na chuki binafsi kutoka katika serikali ya Marekani, hivyo anataka alipe kisasoli. Mama Abyas akiwa kama mshirika wetu mkuu hapa Afrika, alitakiwa akuchunge mpaka usiku wa leo. Muda mchache kuanzia hivi sasa wenzangu kama watatu hivi wanakuja kukumaliza. Usiku wa leo ndiyo usiku pekee ambao shujaa wa ulimwengu wetu unaweza ukafa!!"


"Shujaa wa ulimwengu?! Mbona sikuelewi wewe??" Nilikua simulewi kabisa alichokua ananiambia muda ule.


"Utanielewa tu Fadhili, usijali" Nsagali alinijibu akiwa na ujasiri mno na kuonesha matumaini fulani kwangu. Nilishindwa kuelewa kwanini, mpaka pale aliponipa maelezo haya...


"John baada ya kuangalia katika teknolojia yake, amegundua kuwa wewe ndiyo mtu pekee utakayekuja kuzuia mpango wake. Kwahiyo ametutuma sisi ili tuje tukuangamize. Naweza kusema nimewasaliti wenzangu katika hilo, kwakua nimejikuta nakupenda sana Fadhili!!, pamoja na ukatili ulionifanyia, naelewa ni tamaa tu ila kwa muda niliokua na wewe nimetokea kukupenda. Nitasaidiana na wewe kuikomboa dunia ila tu niahidi kwamba utaishi na mimi milele!!!"


Wakati Nsagali akiwa anaongea maneno yale, mwili wangu mzima uliingiwa na ganzi ya ghafla, maswali mengi yakianza kuja kichwani...


"Nitampandaje mtu ambaye tayari kashaniambia kuwa yeye si binadamu wa ukweli?"


"Na hii dunia nitaisaidiaje mimi Fadhili wa watu??, sijui hata teke linarushwaje???".


Kabla sijapata jibu lolote kichwani, nikasikia kishindo na mwanga mkali sana pale mbele yetu tulipokuwepo, mimi na Nsagali.


'Puuuuuuuuuh!!!!!"



INAENDELEA:


"Nini tena hii?" Niling'atuka kwa woga huku nikijilazimisha kunyanyuka hali ya kuwa mikono yangu na miguu yote ilikua imefungwa kwenye kiti nilichokua nimekalia. Nsagali yeye wakati huo hakuwa na wasiwasi kabisa, pamoja na kishindo kilichoambata na mwanga mkali uliopiga mbele yetu. Hali ile ilinifanya nianze kumtilia mashaka mshichana huyu.


"Hebu punguza woga Fadhili.." Nsagali alizungumza, akaweka kituo kidogo kwa kutabasamu kisha akaendelea kuongea..


"Hii ni ishara nzuri!!"


"Ishara nzuri??!!", Nilishtuka kwa kujiuliza kimoyomoyo, macho yangu yaliyojaa khofu hayakubanduka usoni mwake, sikumuelewa anamaanisha kitu gani kusema ishara nzuri, yani anasema ishara nzuri wakati kishindo kikali kimetua karibu yetu?!, laiti ingekua ni kutuangukia tayari umarehemu ungekuwa viganjani mwetu. Kila nilipokua namtazama msichana yule, nilikua namuona kama alikua anajizungusha tu ila lengo lake ni KUNIUA!!. Ni kama mwalimu darasani afundishe moja jumlisha moja jumlisha moja nyingine sawa na tatu (1+1+1= 3) wakati angeweza kusema mbili jumlisha moja ni tatu(2+1=3) na ingejitosheleza.


Yeye mwenyewe tayari pia alishajishtukia kuwa ninamhisi vibaya, akawa anajitahidi kadri awezavyo kunipa muonekano utakaoniridhisha na kufuta matone ya woga yaliyotapakaa katika kuta za moyo wangu.


" Hii ni ishara kutoka angani my dear, eneo hili linaitwa THE LIBRARY OF DESTINY (MAKTABA YA HATIMA), katika maktaba hiyo kuna vitabu vingi, kikiwemo kimoja kinachoitwa BOOK OF HEROES ( KITABU CHA MASHUJAA). Katika kitabu hiki kuna mashujaa wengi mno walioorodhoreshwa kwa majina. Sasa kila mwaka tarehe tano mwezi wa tano, siku kama ya leo, muda kama huu, yani saa tano na katika tano usiku huwa kitabu hiki kinafungua ukurasa mpya. Ukurasa ukifunuka tu, ndipo ishara kama hii inateremka duniani, kwa spidi sana karibu na eneo lile ambapo shujaa huyo atakuwa anapatikana kwa wakati huo. Lakiniii…" Nsagali alizungumza kwa tabasamu kubwa, sura yake ikionesha mfano wa mtu kupata uhakika juu ya kitu kizuri alichokuwa anakitegemea ila kabla hajamaliza kilimjia kitu kichwani, ile furaha yote taswirani kwake ikaanza kufutika.


"Lakini nini?" Nilimuuliza,huku nami nilishasmbukizwa ile shaka ya ghafla iliyomuingia.


"Nina wasiwasi John Anglin, atatumia teknolojia yake kufuatilia huu mwanga ulipoangukia na mwishowe atagundua wapi ulipo, hapa inabidi tuondoke tu!!"


"Tutaondokaje wakati umenifunga mikono?", Nilimuuliza ili tu nipate nafasi ya kufunguliwa pale kwenye kiti cha kimateka nilichokua nimekalishwa.


" Kwani tulikujaje?" Na yeye akanijibu kwa swali lililofanya nikose cha kujibu na kuwa kama mtu fulani hivi niliyeshushuliwa nikashushuka. Hapo hapo nikageuza sura yangu na kuweka huruma, kwakua mtoto alikua tayari kanizimikia hakuwa na la kufanya zaidi ya kunifungua.


"Tunaelekea wapi sasa? Maana inaonekana tuko porini sana hapa!!" Baada ya kufunguliwa na kusisima nilimuuliza huku nikiwa najinyoosha nyoosha viungo.Hakunijibu chochote zaidi ya kukaa kimya, aligeuka pembeni kulikokua kuna miti iliyojikusanya kwa pamoja, taratibu alisogelea miti ile mpaka karibu nayo, kisha akaichanisha achanisha miti ile mithili ya kuku apekuwapo makolombwezo jalalani, punde! akatoka na kajimkoba kidogo cheusi mkononi mwake , alinigeukia na kuniangalia usoni, macho yangu yaliyojaa machale yakimtazama kila alichokua anakifanya, nikijiweka sawa kwa lolote litakalonikumba. Huku akitasamu alinikabidhi kajimkoba kale mikononi mwangu…


"Wanini huu?" Nilimuuliza.


" leo tisa kamili usiku, ule ugeni niliokuelezea ndiyo utakua unafika. Mtu pekee ni wewe wa KUWAZUIA!!"


"Bado hujanijibu Nsagali, kwahiyo hili begi ni lala nini mimi?"


"Usiwe na haraka sana Fadhili, ndani ya hilo begi kuna taarifa nimekujazia, naomba uzisome taarifa hizo. Nakutakia safari njema mpenzi!!!"


"Safari nje…", kabla ya kumuuliza ama kumjibu lolote, 'vuuuuuh!!!'… upepo ulio mkali sana ulinisomba na kunipeperusha. Sikujua kilichoendelea baada ya hapo.


Muda mchache najukuta pembezoni mwa barabara, mkononi nikiwa bado nimeushikilia mkoba ule. Hali ya uchovu ikiwa imeuchota mwili wangu, nilijiinua taratibu na kusimama, macho yangu yakiangaza kulia na kushoto. Magari machache ndiyo yaliyokua yanakatiza katika barabara safi iliyo mbele yangu.


" Huu ni mkoa gani?" Nilijiuliza, huku uso wangu ukiwa uko juu juu kushangaa mataa yaliyokua yanaangaza katika kila pande ya barabara ile, niliendelea kutazama mpaka nikakutana na majengo yenye mfano na yale magofu ya kisultani kule Zanzibar…


"Au niko Zenji nini?" Nilijiuliza tena, lakini kabla sijapata jibu hata mojawapo kati ya maswali hayo mawili, niliona mimea ambayo naifahamu kabisa. Ingawa sijawahi kuiona kiuhalisia kabisa ila nilishaionaga sana katika runinga na mtandaoni, ilikua ni MITENDE, mitende iliyooteshwa vizuri pande zote mbili za barabara na kufanya mazingira yale yavutie machoni mwangu. Nikakumbuka ile kauli ya mwisho kabisa Nsagali kuniambia…


"Usiwe na haraka sana Fadhili, ndani ya hilo begi kuna taarifa nimekujazia, naomba uzisome taarifa hizo. Nakutakia safari njema mpenzi!!!"


Haraka nikafungua kijibegi kile chenye mfanano na 'briefcase'. KARIBU NCHINI ERITREA FADHILI, baada ya kufungua tu nilikutana na faili ambalo juu liliandikwa maneno hayo!!.Nilishtuka kwa kweli..


"Ina maana nipo Eritrea??!, hapana hakiwezekani kitu kama hicho!!" Nilipinga huku macho yangu yakiendelea kusoma kile kilichoandikwa ndani ya faili lile.


"JAHWEED LITIKA (The father with no wife)"Baada ya kupitisha macho kwa chini, nilikutana jina hilo, JAHWEED LITIKA (Baba asiye na mke), hili jina halikunishtusha hata kidogo, ila hii a.k.a yake ambayo iliwekwa kwenye mabano ndiyo taratibu ikaanza kunipa hamu ya kuendelea kusoma faili lile, kwanini aitwe Baba asiye na mke?, kwanini jina lake lipo ndani ya faili hili? na ndani ya faili hili kuna taarifa gani?. Taratibu nilijisogeza pembezoni mwa ile ile barabara, nikaweka makalio chini huku mwanga wa kutosha uliokuwepo eneo lile ukinipa wasaa mzuri wa kulisoma faili lile ili ning'amue majibu ya maswali hayo yaliyotia nanga bongoni mwangu. Faili lilisoma hivi..


" JAHWEED LITIKA ni raia wa Misri, ambaye ni mjukuu wa tajiri mmoja mkubwa sana aliyewahi kuishi Misri kwa wakati huo. Miaka mitano iliyopita alihamishia makazi yake nchini Eritrea, Huyu jamaa udhaifu wake mkubwa ni wanawake (Hahah! baada ya kufika eneo hili, fundo la mate likajisukuma kooni, na kujishtukia huenda faili hili linanizungumzia mimi nini?. Kisha nikaendelea kusoma), Anaitwa 'Baba asiye na mke' kwa sababu kila siku usiku huwa lazima apate mwanamke mpya wa kulala naye. kiufupi harudii mwanamke!!. Wanawake wengi aliowahi kuwa nao wamepata ujauzito lakini amekua ni mwenye kukana watoto wake, mtu huyu hajawahi kuwa na mke wa ndoa katika historia ya maisha yake yote. Na huyo ni JAHWEED LITIKA!!"


"Agh! sasa hayo si maisha yake, mimi inanihusu nini sasa?!!" Nilijiuliza, kwakua baada ya kusoma sijaona la kunihusu walau mojawapo katika yale. Lakini kumbe nilikua sijamalizia kusoma faili lile vizuri bwana….


"Huyu JAHWEED LITIKA ndiyo ana nguvu zako kichwani mwake, unatakiwa umuue kisha umchome sindano kichwani, sindano hiyo ipo kwenye begi humo (Nikaangalia kwenye kile kijibegi kweli nilikuta kuna sindano, kisha niliendelea kulisoma faili...). Ukishamchoma tu basi, nguvu zako zitaanza rasmi kufanya kazi kuanzia leo.."


"…Na naomba ukumbuke Fadhili, muda umebaki mchache sana! Tafadhali jitahidi um'malize mtu huyo haraka kadiri uwezavyo. Taarifa za jinsi ya kumpata zipo karatasi ya mwisho kabisa iliyomo ndani ya faili hili"


Kuna kitabu kimoja niliwahi kukisoma, kinaelezea MTU HURU ALIYEAMUA KUWA MTUMWA ILI KUPATA UHURU, hivyo ndivyo nilikua kwa wakati huu. Nililazimika kuingia katika majukumu mazito, japokuwa nilikua niko katika maisha yangu safi tu lakini nalazimika kuingia katika maisha magumu, maisha ya mauza uza, maisha ya tabu nzito kiasi hiki ili nipate maisha safi tena. Mmnh! Kweli dunia duara, unapoanzia ndipo unaishia.


Niligeuza lile file kwa nyuma kisha nikatoa hiyo karatasi ambayo nimeelekezwa, taratibu nikaifungua ilikua inasema hivi…


"Barabara ya tatu nyuma yako utakuta magari matatu ya kifahari, yakiwa yamepakiwa(yameegeshwa) kwa kuongozana,humo kuna danguro la siri. Jitahidi umuue JAHWEED kabla hajatoka humo ndani!!!".


Sikutaka kupoteza dakika, niliinuka nikarudisha faili ndani ya kijimkoba na kukifunga, kisha nikaanza kuzunguka nyuma kama nilivyoolekezwa tayari kwa kulisaka jengo lile ili nimuangamize huyu bwanamkubwa JAHWEED na nichukue nguvu zangu!!


Kabla sijafika hata huko ambako nilikua naelekea, nikapishana na mwanamke aliyekua amevaa nguo fupi sana. Kitu ambacho nilipasua kichwa changu kwa mshtuko. Ninavyoifahamu Eritrea ni nchi yenye kufuata taratibu na mahadhi ya kiarabu, iweje mtu huyu avae vibaya kiasi hiki.


Kwa bahati nzuri mimi ni mtaalamu wa lugha mno, Kiitaliano ambacho ndiyo lugha watu wengi wa nchi hii wanakitumia ndicho nilianza kumuingia nacho mlimbwende huyu…


" Ciao, come stai?"

(Hello, habari yako?), Nilianza na salamu.


"Sto bene, cosa posso aiutarti? Hai bisogno del mino servizio?"

(Niko poa tu, vipi nikusaidie nini? Unataka huduma yangu?). Aliongea huku akibenulia benulia kajiumbo chake cha kishombe shombe, ingawa tamaa yangu ilishaanza kufanya yake ila niliamua kujituliza kidogo.Maana hawa madada poa si viumbe wa kuwakurupukia hata kidogo.


"Porta Inglese?"

(Unafahamu kiingereza?), Mtoto aliniuliza, baada ya kuona napata shida kidogo katika kuzungumza na kujibu.


"Yeah! sure, do you know it?"

(Yeah! hakika, wewe unakijua?), Nilimuuliza huku matumaini ya kufanikiwa lengo langu kwa msichana huyu nikiwa naona yanazidi kupamba moto.


Baada ya kuona kiingereza anakifahamu vizuri, nilimuomba msichana huyu akanipambe!! Ndiyo, yani akanirembe niwe mwanamke wa nguvu mpaka JAHWEED (Baba asiye na mke) apagawe, na ikiwezekana akiniona tu! atangaze ndoa kwa mara ya kwanza. Unaweza ukasema huo ni UMAMA, lakini sikuwa na namna nyingine kwa kweli zaidi ya kufanya hivyo.


Bila ajizi yule mrembo alikubali kufanya nilochoomba si unajua tena wasichana kama wanajeshi, huwa muda wote hawachi silaha zao, utakuta bonge moja la pochi, humo ndani kajaza vitu utafikiri anaenda kufungua saluni.


Tulitafuta chocho akanipara nikaparuka mtoto wa kiume, kisha nikampa baadhi ya fedha ambazo nilikua nimewekewa mule mule ndani ya kile kijimkoba.Na kwa bahati nzuri zaidi kule katika kale kajidanguro anapafahamu vyema kabisa, nikamlipa pesa nyingine ili anisindikize. Nikiwa nimejafungwa kajigoro cha kuumua kishepu huku nyuma kama sio mimi yani, taratibu unaambiwa safari ilianza...


Kufika tu, kumbe pale nje bwana kuna mijibaunsa. Inakagua mtu yoyote kabla ya kuingia ndani.


"Mmmnh!! sasa ntafanyaje pale?", Nilijiuliza bila kupata jibu.


" I can fight with them, do you have money?"

(Ninaweza kupigana nao, je una pesa?), Yule msichana alizungumza, nikageuka nimcheki kwanza vizuri, maana ile minjemba si ya kitoto ati, na yeye asinigeuzie uso wake sasa?. Daah! sikutaka kuamini kwa sura niliyoiona tena kwa mara nyingine, Kumbe msichana yule muda wote huo alikua ni Nsagali bwana!!




"Ni wewe?", Nilishtuka kwa ghadhabu.


Hakunijibu kitu, aliendelea kunitazama kwa dakika kadhaa. Kisha akanitolea tabasamu hafifu. Sikucheka! Niliendelea kumuonesha uso wangu ule ule uliojawa hasira.


Sikujali kitu. Sikujali kuwa muda huo nimesharembwa tayari na kuonekana mzuri tu, sitishi; sikujali hilo. Nilichozingatia kwa wakati ule, Ni kudhihirisha hasira yangu kwa Nsagali.


" Kwanini unanifanyia hivi Nsagali?. Nsagali inatosha! Inatosha nimesema! Tatizo liko wapi? Kufa au? Basi na mimi niue, Ni bora nife kuliko.."


"Hivi unajua unapoteza muda?", kabla ya kumaliza kuzungumza, Nsagali hakuonesha kujali maneno niliyokuwa nayatoa, badala yake akanikatisha na kunikumbusha kuwa; tunazidi kuchelewa.


Pamoja na kutonielekezea uso, wakati ananitolea maneno hayo, hata baada ya kumuangalia--yeye hakunitazama; nilielewa kuwa alimaanisha katika kile anachokizungumza. Sikuhitaji mambo yawe mengi.


" Okay, twende! Ila nitahitaji msaada wako.", Nilimwambia


"Msaada wangu kwako lazima, ndiyo maana niko hapa." Alinijibu, wakati huu lile tabasamu jepesi, linalosukumwa na upendo likiwa limerudi wajihini mwake.


Niliitoa ile sindano, ninayotakiwa kwenda kumchoma JAWHEED LITIKA kichwani. Taratibu nikafunua gauni nililovaa, nikaichomeka mapajani. Sikuogopa kukaguliwa tena, uhakika wa msaada nimeshapata.


"Ongoza! Mimi nitakufuata nyuma.", Nsagali aliniambia, bado uso wake ulikuwa tabasamuni. Tabasamu lililonipa matumaini, kuwa hatanisaliti mtegoni, minjemba ikaniSUKUMA NDANI.


Kwa hatua za kike, narudia tena; kwa hatua za kike, nilitembea kuelekea langoni, kuingia danguroni. Hofu iliukumbata moyo kadiri nilipowakaribia walinzi wale. Niligeuka kila Wakati, kuhakikisha uwepo wa Nsagali.


Walilishwa dawa za usingizi, walirogwa au walifanywa kitu gani?, sikuelewa. Nilichokiona mbele yangu ni walinzi wale -- wote kwa pamoja, kulegea, wakadondoka chini. Nikageuka haraka kumtizama Nsagali, laahaula! Hakuwepo.


Kwani nilihitaji msaada gani? Walinzi si washadondoka? Nisubiri nini tena?, nikaingia ndani tu.


Taa za humu ndani, zilikuwa hafifu mno kwa mwanga, rangi zake nyekundu kama udongo wa Tanga, kuashiria vinavyoendelea ni visanga.


Pande zote za kutani, kulibandikwa picha na kuchorwa makatuni, yako uchi; hayana suruali wala gauni, Ilimradi tu ufirauni.


Sikutaka kushangaa mno, nikachangamsha mwendo, japo si kwa kiasi kikubwa sana. Ukizingatia humu ndani, bado ningali nina kamba mguuni.


Kilichofanya nisiweze potea, hakukuwa na njia nyingi, ilikuwa ni ya moja kwa moja. Nilizidi kuongoza! Kumbukumbu ya kitu fulani, ikaanza kuingia ubongoni, ikajirudia akilini…


"…Unatakiwa umchome sindani hii kichwani".


Nilianza kutafakari, namna gani sindano ile nitamchoma. Kabla sijapata jibu, wala wazo mahbibu! Nilianza kuona kilichonishtusha, kikanisukuma kusogea mahali pale. Kulikuwa na wanawake wengi mno, wengi!. Kila mmoja akionekana na habari zake, lakini wote walikuwa wanasubiri kuingia mlango mmoja.


Kila aliyekuwa anatoka baada ya kuingia, alitembea kwa kuchechemea. Kuna nini hapa? Nilijipiga swali huku nikijua kabisa sikuwa na jibu. Ikabidi nijaribu kuuliza, nilimsogelea msichana mmoja wapo.


Kwa sauti yangu ya kirijali, haikuwa kazi rahisi kumuongelesha.Pia haikuwa ngumu, kwa shida niliyokuwa nayo wakati ule.Nilianzisha mazungumzo…


"Come stai?, Cosa sta succedendo qui?.",

(Habari yako?, kunaendelea nini hapa?.), nilimuuluza kwa lugha ya kiitaliano. Nikidhani itakuwa rahisi mno kunielewa.


Alinigeuka, kwa mshangao uliosindikizwa na shaka. Akanitazama, kuanzia juu mpaka chini, akashusha pumzi ndefu, kisha aligeuka na kuendelea na yake, yaliyomhusu. Sikuelewa kitu!, nilimeza funda gumu la mate, nikageuza macho yangu kuangaza angaza mionekano ya wanadada walioko eneo lile.


Wasiwasi fulani ulianza niingia, japo haukuwa ni wa uhakika; nilianza kuhisi, yawezekana hawa ni wanawake wanaojiuza. Ila inakuaje ni wengi hivi? Tena wote wanaelekea ndani ya chumba kimoja?, Haya maswali yalizi kulisuta wazo langu. Likakosa nguvu, likanywea.


Kabla sijayatoa macho yangu, yaliokuwa yanawatazama wasichana wale, niliona sura ninayoifahamu, nikarudisha mboni zangu sawia. Naam!, alikuwa ni Nsagali. Kafuata nini huku huyu? Wakati najisaili, naye aliniangaza, akanifinyia jicho moja. Ndipo nikaelewa cha kufanya, kuwa yanipasa kuwepo eneo hili.


Nilitafuta pa kukaa, makalio nikaweka chini kusubiria. Zikapita dakika kadhaa, foleni ilizidi kusogea. Zaidi ya yote, bado nilikuwa nina shauku kubwa ya kutambua-- Humo ndani kuna nini? Mpaka watu wanaingia, dakika tano wanatoka wanachechemea!.


Mkusanyiko ule ulizidi kupunguwa, kadiri ya "ingia toka" zilivyopamba moto. Hatimaye tulijikuta tumebaki wawili tu, mie na Nsagali.


Nsagali aliinuka, akanitazama na kunionesha ishara ya 'tuingie sote'. Nikainuaka, moyo wangu ukibadilisha midundo ya kila aina, wakati huu ukipiga biti la singeli. Nilihisi ungepasua kifua, woga ulinikomba wallahi.


Sikuamini kile nilichokuwa nakiona machoni, ila kile nilichokuwa nakiwaza mwanzoni. Ulikuwa ni zaidi ya ufuska. Ni jamaa mmoja, akiwa mtupu wa unyama, kabananisha binti mmoja ukutani, anapeleka vishindo kwa kasi si utani, ile ya chui mbugani, kama si pikipiki barabarani, Aisee! wengine tunavamia tu hii fani.


Kwa hiyo, jamaa ndiyo amechechemesha wasichana wote hao?, nilijiuliza.


Baada ya kuhisi uwepo wa mtu ndani, tofauti na wao wawili, refa akapuliza kipyenga, jamaa alisimamisha mchezo, Akawa anageuka kutizama huku nilipo Mimi….


Mtima ukiwa katika "spidi" ya mteremkoni, nilitetemeka nywele mpaka nyayoni, nikimtafuta Nsagali simuoni, ardhi ipasuke nilitamani, nipotee kabisa Duniani, kitu ambacho hata hakiwezekani.


Alivyogeuka, nilimtazama chini ya kiuno chake. Daah! Sijui utaniamini mpenzi msomaji? Halikuwa ni "dushelele" la kawaida, hata kidogo!. Na hapo ndipo nikapata majibu ya maswali yote, ndipo pia niling'amua aliye mbele yangu ni nani?


Na zaidi, nilielewa ile maana ya kuambiwa NIMCHOME SINDANO KICHWANI, Nasisitiza tena; Kichwani!.


MWISHO





0 comments:

Post a Comment

Blog