Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

KIZUNGUMKUTI

  


MTUNZI : FADHY MTANGA


Dar es Salaam

 Jumatano, Aprili 9, 2003

"SAFI sana!  Hatimaye nimekutana nawe!"

"Nani?"

"Unauliza nani kwani we' unadhani naongea na nani?  Ama utasingizia umenisahau?"

Benito alionesha dhahiri kupandwa na ghadhabu kiasi cha kufikia hatua ya kumkunja Ali shati lake.  Ali akatazama pande zote, akaona watu karibia wote waliokuwapo eneo hilo wamegeuzia nyuso zao eneo walilokuwa wao.  Ali akajihisi kupata fedheha.  Akawaza namna bora ya kujinasua mikononi mwa Benito.  Ali alimkumbuka vema mtu huyo aliyekuwa amemkwida.  Lakini kamwe hakuwa amedhania ya kwamba, uhasama baina yao ungeweza kuwa umeendelea kudumu kwa kipindi chote hicho.  Ali akatambua bayana kuwa endapo hatokuwa makini basi siku hiyo ingeendelea kumshuhudia akiadhirika mbele ya watu wote hao waliokuwepo.

Akajikakamua na kuutoa kwa nguvu mkono wa Benito na kubwatuka.

"Mbwa wewe!  Hunitishi kwa lolote!  Tena, usinifuatilie.  Nitakuharibu!"

Wakati Benito bado akiendelea kushangaa, Ali akajivuta katikati ya kundi la watu kuelekea sehemu ya barabara. Akapanda daladala.  Benito alitoa msonyo mkubwa.  Akatoa leso.  Alijifuta kichwani kuyaondoa maji yaliyosababishwa na mvua ya rasharasha iliyokuwa ikinyesha kwa muda mrefu.

Benito alifikiri kidogo.  Akaingia haraka ndani ya daladala ile ile aliyoipanda Ali.  Alipoingia, alipitiliza hadi nyuma kulikokuwa na siti  ya wazi.  Aliketi.  Aliyaelekeza macho yake kwa Ali.  Kwa upande wake, Ali alijiuliza nini dhamira ya Benito kwake?

Hakuwa na jibu.

Kitu kimoja ambacho Ali alikuwa na hakika nacho ni kuwa Benito hapafahamu mahali anapoishi.  Miaka mingi imepita sasa.  Hata hivyo, Ali alielewa wazi ukubwa wa kisirani cha Benito juu yake.  Sasa jambo lililokuwa muhimu kwake ilikuwa ni kumpoteza.  Kwa ukubwa wa jiji la Dar es Salaam, Ali alijipa moyo kuwa ingemgharimu Benito muda mrefu hata kuweza kumpata tena.

Pembeni yake Ali, aliketi mwanamke mrembo.  Muda wote alitingwa na simu yake ya mkononi.  Ali hakuwa na muda naye.  Kichwani mwake, alimfikiria Benito.

Kila mmoja akaendelea na mambo yake hadi pale Ali alipomgeukia yule mwanamke.   Akamsemesha.

"Samahani aunt, hivi kituo kinachofuatia hapa kinaitwaje?"

Yule mwanamke alimtazama Ali kwa jicho la dharau.  Akaendelea na simu yake.  Nukta chache baadaye, akamjibu pasipo kumtazama.

"Sijui!"

Ali akachoka.  Akamsahau Benito aliyekuwa siti za nyuma.  Akamtazama mwanamke huyo aliyeketi kushoto kwake. Mwanamke huyo alikuwa mrembo hasa.  Macho makubwa mithili ya goroli.  Nywele fupi kichwani kwake.  Zilimeremeta kutokana na mafuta zilizopakwa.  Weusi wa nywele, uliung’arisha pia weusi wa ngozi yake.  Laini hata kwa kuitazama. Alivaa sketi ya kitambaa chepesi cheusi.  Ufupi wa sketi uliifanya sehemu ya mapaja yake kuonekana. Blauzi yake ya rangi ya waridi ilinogesha mwonekano wake.  Vifungo vya blauzi hiyo vilikuwa na kazi ya ziada kifuani pake.  Ali akayashusha macho yake chini na kuishuhudia miguu yenye supu nono. 

Macho yao yakagongana.  Ali akatabasamu.  Yule mwanamke akanuna zaidi. 

Nukta iliyofuatia, Ali aligutushwa na sauti aliyoifahamu.

"Tushafika mwisho wa gari.  Shuka sasa!"

"Nishuke niende wapi?"  Ali alijibu kwa jazba.

"Ulikokuwa unakwenda."  Benito alijibu kwa jeuri.

"Wewe unafahamu mi' nakwenda wapi?"

"Yah! Nafahamu na ndiyo maana nakuamuru ushuke chini."

"Kama sitaki kushuka?"

"Unasemaje?"

"Hivyo hivyo!"

Yule mwanamke akawatazama wote wawili.  Akainuka. Akaushika mkono wa kulia wa Benito.  Akuongea.

"Jamani kaka zangu mbona hivyo?"

Benito akamkazia jicho.  Akaongea, "Unasikia sister, hujui huyu bwege alichowahi kunifanyia maishani mwangu."

"Sawa, pamoja na hayo nyie nyote ni wanaume.  Kwanini msikae chini mkazungumza?"

"Nani? Mimi? Aah wapi!  Thubutu yake!  Mi' nakwambia hata siku moja sitosema kitu na mshenzi huyu!"

Ali hakuzungumza neno lolote.  Alijisikia fedheha na hasira. 

"Lakini kakaangu kwa nini usingetafuta njia nyingine ya kulitatua tatizo lenu kuliko ugomvi usio na msingi?" 

Kama moto wa kifuu, Benito akawaka.  "Nakuheshimu sana dadaangu! Haya mambo we'  hayakuhusu.  Siyo jukumu lako kufahamu endapo huu ugomvi ni wa msingi ama lah."

"It's ok!  Ngoja mi' niendelee tu na mambo yangu.  Kwa heri."

Mwanamke huyo aliitoa kwa heri hiyo kwa kebehi.  Alimkasirisha zaidi Benito.  Abiria wengine wote walikwishazikamata hamsini zao isipokuwa wao watatu.  Yule mwanamke alishuka.  Akawaacha wanaume wawili wakiendelea kuzozana.  

Alipofika chini wakati akilipa nauli aliongea na kondakta vitu fulani kwa sauti ya chini.  Kondakta huyo alizunguka hadi upande wa dereva.  Akaongea naye kwa sauti ndogo ambayo haikusikika kwa watu wengine.

Baada ya hapo, utingo huyo alirudi.  Akaingia garini akiwa amemshika mkono yule mwanamke.  Akawakuta Benito na Ali wakiendelea kujibizana kwa jazba. Utingo akawakata kauli.

"Samahani mabraza.  Nimepewa mashtaka mmemtukana huyu dada.”

Wote wawili, Ali na Benito wakapigwa na butwaa.  Ali akazungumza. "Hapana kaka.  Hatujamtukana hata kidogo.  Huu ni ugomvi baina yangu mimi na huyu bwana hapa."

Wakati Ali akitaka kusema zaidi, yule dada akaingilia kwa sauti ya juu.  "Mmenitukana nyie! Mi' nasema hivi, konda peleka gari hii polisi.  Mi' siwezi kudhalilishwa kiasi hiki hata kidogo!"

Utingo akaonesha kutishwa na kauli ya yule mwanamke.  Akasema, " Oyaa majita eeh, mi naona kama mnanizingua tu.  Kama vipi nyie shukeni ili mmalizane na huyu sister hapa, mi' nitambae zangu!"

Kauli hiyo ya utingo ilimfanya Benito aanze kushuka.  Utingo akasimama nyuma yake.  Kitendo hicho kikamzuia Ali kushuka.  Benito alipoiweka tu miguu yake chini, utingo akaubamiza mlango kwa nguvu. 

Akamwambia dereva, "Mwana, tambaa!"

Ile daladala ikaondolewa pale kwa kasi hata Ali akadondokea vitini.  Pale chini, Benito alibaki tu kushika kichwa kwa mikono yake.  Hakukiamini alichokiona. 

Ali aliketi kwenye moja ya viti alivyoangukia.  Naye, hakukiamini alichokiona.

Gari ikaendeshwa kwa mwendo wa kasi pasipo kusimama mahali popote hadi walipofika Tabata Mawenzi.  Yule mwanamke akaifungua pochi yake.  Akatoa noti ya shilingi elfu kumi.  Akampa kondakta.  Akamshika Ali mkono.  Akamwongoza kushuka chini.  Bado Ali hakuwa akielewa lolote juu ya kilichokuwa kikiendelea.  Aliendelea kuongozwa hadi mahali zinakopaki teksi.  Mwanamke yule akamwongoza Ali kuingia baa ya Mawenzi Garden, upande wao wa kushoto.

Walipoketi, yule mwanamke alimwita muhudumu.  Aliagiza bia ya Kilimanjaro.   Ali alikuwa angali amechanganyikiwa.  Hakuwa na hamu ya kunywa kitu chochote.  

Bia ilipoletwa, ndipo yule mwanamke alipoanzisha maongezi.  "It's ok Ali. Hebu jaribu kuachana na mambo ya yule fala.  Tafadhali rafiki yangu, we' ni mwanaume."

"Kwanza, sijui hata nikushukuruje sister angu.  Yule bwana angenishushia hadhi mbele ya kadamnasi."

Pamoja na kwamba Ali aliendelea kujaribu kuiamini hali halisi iliyokuwapo, bado alitawaliwa na fikra nyingi.  Alijaribu kukumbuka endapo kuna mahali ambapo pengine amewahi kukutana na mwanamke huyu, ambaye katika wakati usiokuwa umetarajiwa ameondokea kuwa mwokozi wake.

Yule mwanamke aliweza kuyasoma vema mawazo ya Ali.  Akamaizi Ali hakuwa na kumbukumbu yoyote juu yake.

"Ali, muda wote huu bado hujanikumbuka tu?"  Akamwuliza.

"Mh!  Kumbukumbu yaja halafu yanipotea."  Ali alimjibu.

"Mmh, kweli?  Basi kumbuka methali hii, 'akufaaye kwa dhiki.....?"

"Ndiye rafiki!"  Alipojibu hivyo, Ali alitabasamu.  Akagonga mkono wake wa kulia kwa dada huyo.

"Wow!  Rehema?"

"Ndiye mimi."

"Hapana!  Mbona umenenepa kiasi hiki rafiki yangu?"

"Ayaa!  Ulitaka nikonde watu wapate kusema nina ngwengwe?"

"Aisee! It's so nice to meet you!"

********************

ILITIMU saa nne hivi usiku. Ali alishuka kwenye basi la Hood akitokea Arusha.  Ilikuwa majira ya kiangazi cha mwaka 2001.  Baada ya kushuka pale Stendi Kuu, mjini Mbeya, Ali alijaribu kutazama pande zote angalau aweze kumwona mtu yeyote aliyekuwa akimfahamu.  Hakumwona mtu yeyote ambaye pengine angeweza kumfahamu.  Ali alilinyanyua begi lake dogo na kuuvaa mkanda wake kwenye bega lake la kushoto akaondoka eneo hilo.  

Ali hakuwa na pesa yoyote mfukoni mwake baada ya kuwa ameibiwa pesa zake zote akiwa safarini. Ilikuwa ni katika eneo la Mombo basi liliposimama kwa ajili ya chakula ndipo alipogundua kuwa ameibiwa.  Hakuwa na namna nyingine tena zaidi ya kulazimika kusafiri pasipo kula kitu safari nzima.  Na hata aliposhuka hakuweza kumudu kukodi teksi kufika nyumbani kwao.

Alitembea haraka kuifuata barabara ya Mbalizi hadi alipofika kwenye mnara wa ushirikiano wa Tanzania na Japan.  Akashika njia ya kulia hadi kuifikia barabara ya Jacaranda.  Hakuwa amefika Mbeya kwa zaidi ya nusu mwaka sasa, lakini hakuwa na hofu yoyote.

Alipoipita hosteli ya Moravian na kutaka kuingia barabara ndogo ya vumbi iliyokuwa upande wa kulia, akagutushwa na sauti za watu waliokuwa wakija upande wake.

"Wewe!  Simama hapo hapo!"  Sauti hiyo iliyoambatana na amri ilitosha kumfahamisha Ali kwamba kwa vyovyote vile, lazima watu hao wawe askari.  Hakuikaidi amri hiyo.  Akasimama.

"We' ni kibaka?"  Ndiyo iliyokuwa salamu ya askari hao.  Walikuwa tayari wamemfikia karibu kabisa.  Walikuwa sita kwa idadi yao, miongoni mwao wakiwepo askari wa kike wawili.  Wote kwa pamoja walimzunguka.  Askari mmoja wa kike akaushika mkono wa kulia wa Ali.  Akaunyanyua.  Akavinusa vidole vyake kimoja baada ya kingine.  Hali hiyo ilimkera Ali.  Hakujua akabiliane vipi na askari hao.  Hasira zilimpanda Ali.  Wakati askari hao wanaendelea kumsachi, Ali hakumudu kuidhibiti hasira yake.

"Mbona tunadhalilishana hivyo?  Semeni basi shida yenu."  Ali aliongea kwa hasira.

Kusikia kauli hiyo askari mmoja wa kiume akamchapa Ali kofi moja la nguvu juu ya shavu lake la kushoto.

"We' raia unasemaje?  Unajifanya kujua siyo?  Tumekukamata unazurura ovyo usiku halafu bado unachonga!"  Askari huyo aliwaka.  Matamshi yake yakiwa yameathiriwa na lafudhi ya Kijita. 

"Hapana wakubwa.  Mi' natoka safarini na tiketi ninayo, hii hapa."  Ali alisema akijaribu kuitoa na kuwaonesha askari hao tiketi hiyo.  Askari mmoja alimnyang’anya.  Akaichana.  Askari mwingine akamvisha pingu. Wakaanza kumwongoza kana kwamba wanakwenda kituoni.  

Njiani, Ali alijaribu kadri ya uwezo wake kuwashawishi ili waweze kumwachia.

Walipokuwa wanapita usawa wa duka la madawa la Bhojani, Lupa Way, askari wale wakasimama.  Ali alisimama pia.

"Haya jielezee fastafasta tukusaidiaje?"  Askari mmoja wa kiume alisema.

"Washikaji kama......" Ali akaanza kuomba ihsani kabla hajakatishwa na askari.

"Heee!  Rekebisha kauli yako, nani mshikaji wako hapa?"  Mmoja wa askari wa kiume akamjia juu.

"Nawaomba mniwie radhi kwa hilo."

"Enhee, endelea."

"Kama nilivyowaeleza, nimepoteza pesa yangu yote njiani.  Hapa nilipo sina kitu cha kusema niwatoe hata kidogo."  Ali alijieleza.  Hasira zilishamshuka siku nyingi.

"Unaona sasa!  Sisi tulidhani una cha maana cha kuzungumza, kumbe bado unapiga tu longolongo."  Aliongea yule askari mwenye lafudhi ya Kijita.

Ali akajitahidi kujitetea, "Hapana jamani.  Mi' mwenyewe naelewa mpo kazini, nisingependa kukusumbueni kabisa."

Askari mwingine wa kiume ambaye hakuwa amezungumza neno lolote tangu awali akamnyooshea Ali kidole chake cha shahada cha mkono wa kushoto.   Akazungumza kwa sauti yenye kukwaruza.

"We' mbona waongea maneno mingi hivyo?  Haina hela, twende kituoni."

Ali hakuwa na ujanja kabisa. Aliwaomba askari hao waongozane naye hadi nyumbani kwao akiwahakikishia kuwapa pesa waliyoihitaji.  Askari mwingine wa kike akatoa naye sauti yake.

"We' kijana, tangu lini umesikia kuwa rushwa inakopeshwa?  Ni simple tu, huna, sie tunakwenda kukuhifadhi sehemu salama zaidi ili ifikapo kesho, ndugu zako wakukute huko."

Wakiwa bado wanajibizana, askari mwingine wa kike, akawageukia wenzake.  Akawashauri wamwachie Ali huru kwa kuwa hakuonekana kuwa mhalifu hata kidogo.  Awali, askari wenzake hawakutaka kukubaliana naye.  Baada ya mjadala mfupi kidogo wote wakaafikiana kumfungua pingu.  Wamwache aendelee na safari yake.

"Lakini Rehema, mi' sometimes mambo yako ya kikanisa yananiboa sana."  Askari mmojawapo alimtolea kauli mwenzao aliyewashawishi kumwachia Ali huru.  Akamfungua pingu.

Alipokuwa amefunguliwa tayari, Ali akawashukuru askari wale.  Akaanza kuondoka.  Akawa hajaenda hatua nyingi, yule askari aliyemtetea ambaye kwa sasa Ali amekwishalifahamu jinale kuwa ni Rehema, akamfuata na kumsimamisha.

"Samahani braza, sijakufahamu hata jina lako."

"Naitwa Ali dadaangu."

"Nashukuru kukufahamu.  Pole sana, lakini usijali ni mambo madogo tu haya."

"Usijali dada Rehema.”  Ali alisema.  Tayari alilifahamu jina lake kutokana na maongezi ya wale askari wakati akifunguliwa pingu.  Ali akaendelea.  “Nakushukuru sana kwa msaada wako.  Sijui hata niseme nini kuonesha shukrani zangu za dhati."

"Yaache hayo Ali, akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki."

Aliposema hivyo, Rehema akageuka nyuma pasipo kuaga. Akaondoka akikimbia.  Wenzake walishakwenda hatua nyingi mbali.  Ali aliendelea kusimama.  Alimshangaa askari yule mrefu kidogo, mwembamba mwenye sauti ya kuvutia.  Pamoja na kuwa usiku, Ali hakushindwa kufahamu kuwa askari huyo ni mrembo.  Askari mrembo aliyemnasua. Aliendelea kuwatazama wale askari hadi walipopotelea gizani.

Naye akaendelea na safari zake.

SURA YA PILI

Dar es Salaam

Jumatano, Aprili 9, 2003

BENITO  aliishusha mikono yake chini akiwa haamini kilichotokea.  Aliiangalia ile daladala ilivyokuwa ikiondoka.  Akaichukua simu yake na kuandika namba za ile gari.  Alipandwa  hasira.  Akawa anaung’ata mdomo wake wa chini kwa meno yake ya juu.  Hakuwa na namna ya kumpata Ali.  Hata hivyo akajipa moyo.

Hakuona haja ya kuendelea kuumiza kichwa chake.  Akaanza kutembea taratibu kuifuata barabara hiyo inayokwenda Tabata Mawenzi.  Njia nzima alijaribu kumfikiria dada yule aliyemcheza shere wakati akizozana na Ali.  Benito akakosa jawabu la moja kwa moja endapo dada yule alikuwa safari moja na Ali, ama walikutana mumo humo. 

Kilichomshangaza zaidi ni kuwa muda wote akimkazia jicho Ali, hakuona dalili yoyote ya wawili wale kufahamiana.  Hata Ali alipomwongelesha yule dada kwa kumwuliza kituo kilichokuwa kikifuatia, Benito alilisikia vema jibu lililotolewa.  Jibu lile lilimfurahisha Benito na kumpa hakika Ali angebabaika katika kushuka hivyo kumwia rahisi kukumbana naye.

Mawazo mengi kichwani mwake yalimsukuma umbali mrefu.  Akajikuta amefika Tabata Mawenzi.  Njaa ilimwuma.  Akafikiria kwenda mahali kula chakula.  Akaongoza moja kwa moja hadi baa ya Mawenzi Garden akitaraji kula walau chipsi na mishikaki.

Alipokuwa anaikaribia ngazi ya kuingia pale ukumbini ambako sauti za muziki unaopigwa moja kwa moja zilikuwa zikisikika, kwa bahati mbaya akakanyaga maji yenye matope.  Mvua kubwa ilikuwa imenyesha na kuacha madimbwi chungu mbovu.  Benito alikitazama kiatu chake cha mguu wa kulia kilichokuwa kimechafuliwa na matope yale.  Alijisikia udhia mno.  Hamu yote ya kuingia mahali hapo ili kupata chakula ikamwondoka.  

Akageuza njia kwa soni hadi alipovuka barabara.  Akaenda kwenye kijiduka kilichoandikwa Muno Shop. Akanunua chupa ndogo ya maji ya kunywa pamoja na leso ya kitaulo.  Akaketi kwenye fomu nje ya kijiduka kile.  Akakisafisha kiatu chake.  Alijawa hasira.  Haikumgharimu muda mrefu hata akawa amemaliza.  Hakuwa na jambo tena la kumbakiza huko.  Akapanda daladala ya Ubungo ili aweze kufika nyumbani kwake maeneo ya Afrika Sana, barabara ya Shekilango.

Benito hakuwa ameoa.  Nyumbani kwake aliishi na mdogo wake wa kike, Mary.  Mary alikuwa amemaliza kidato cha nne.  Matokeo yake hayakuwa mazuri.  Hivyo alikuwa katika maandalizi ya kuirudia mitihani yake.

Benito aliwasili nyumbani akiwa mnyonge.  Ingawa alijaribu kadri ya uwezo wake kuficha hali yake, Mary aliweza kugundua haraka utofauti uliokuwepo.  Mary hakuwa akielewa jambo lililomsibu kaka yake.  Kabla hajafanikiwa kumdadisi, tayari Benito alishajifungia chumbani kwake.  Alilala hadi jioni alipotoka kwa ajili ya kutazama taarifa ya habari katika televisheni.  Kila mara Mary alitamani kumwuliza kaka yake kilichomsibu.  Kwa upole wake, ilimuwia vigumu kufanya hivyo.

Baada ya chakula cha jioni Benito aliingia tena chumbani kwake.  Akajitupa kitandani.  Kichwa chake kilizongwa na mawazo tele.  Aliwaza hili na lile ilimradi tu akijaribu kuyatafsiri matukio ya mchana wa siku hiyo.  Suala la Ali kumponyoka katika hali ambayo hakuwa ameitaraji lilimchanganya.  Likamkasirisha zaidi.  

Wakati mwingine, akawa anatazama kisa haswa.  Kuna wakati akajishauri kuwa ni utoto kufanya hivyo.  Lakini baada ya yote, akili yake bado ikamwambia kuwa ni lazima nadhiri yake itimie.

Pamoja na kwamba hakupafahamu mahali hasa alipokuwa akiishi Ali, Benito alikuwa na hakika ni maeneo ya Tabata.  Tabata ni kubwa, Tabata ipi hasa?  Hakuacha kujiuliza.  Aliazimia kuhakikisha anamsaka Ali hadi anampata. Hakufikiria kumshirikisha mtu yeyote.  Hakutaka kumwingiza ama rafiki yake ama mdogo wake, Mary.

Hakuwa mwenyeji wa jiji la Dar es Salaam.  Mwaka mmoja umekwishaondoka tangu ayaanze maisha ndani ya jiji akitokea kwao Songea.  Ugeni wake bado haukumfanya aone ugumu wa kazi ya kumtafuta Ali.  Mawazo hayo yalimfanya kukesha hadi usiku wa manane pasi hata lepe la usingizi.  Hata hivyo, alfajiri ilipobisha hodi, Benito alizama usingizini.   Hakushusha chandarua, wala kubadilii nguo, sembuse kujifunika shuka.

Siku mbili zilizofuata, Benito aliutumia muda wake kufanya kazi za ofisini alikoajiriwa.  Aliajiriwa kwenye kampuni ijishughulishayo na ujenzi wa minara ya simu, Ngoni Constructions Limited.  Kampuni hiyo ilishikilia zabuni nyingi za ujenzi wa minara hiyo.  Yeye alifanya kazi kama mwakilishi wa kampuni jukumu lake kubwa likiwa ni kutafuta, kukodi na kufanya mikataba ya maeneo mapya ambako minara ilikusudiwa kujengwa.

Benito alipokuwa amemaliza kidato cha sita alijiunga na kozi mbalimbali kwa njia ya mtandao.  Alifanikiwa kupata stashahada ya masoko yenye kutambulika kimataifa.  Alipata kazi katika kampuni ya Ngoni, ambayo inamilikiwa na mjomba wake.

Siku hizo mbili, Benito hakuwa amefanya kazi zake kwa ufanisi.  Kichwa chake kiliendelea kuwa kizito kupindukia.  Hivyo, ilipotimu siku ya tatu, Benito aliomba ruhusa ya siku nne.  Alidanganya anasafiri hadi Mbeya kumwona mdogo wake wa kiume anayesoma huko.  Hakunyimwa ruhusa kwa sababu ya mambo mawili.  Mosi, si mwombaji ovyo wa ruhusa kazini.  Pili, pengine kubwa zaidi, mtoto wa bosi.

Hakwenda Mbeya kama alivyoaga ofisini.  Joto kali la jiji la Dar es Salaam lilimwunguza akikata mitaa ya Tabata Mawenzi hadi Kimanga.  Hakuwa akifahamu Ali alijishughulisha na nini.  Alifahamu kuhusu Hafsa.  Kwamba, ni mwalimu wa shule ya sekondari maeneo ya Tabata.  Ugeni wake ukijumlisha na ukubwa wa eneo la Tabata pamoja na wingi wa shule za sekondari alitambua wazi ugumu wa jambo hilo.

Akiwa kwenye kituo cha daladala Tabata Kimanga alikutana na wanafunzi wengi.  Kwa kuwa ilikuwa ni majira ya saa nne asubuhi, Benito alielewa wanafunzi hao wapo kwenye mapumziko.  Hakusita, hakupoteza muda akaungana nao na kuanzisha soga.

“Washikaji mambo vipi?”

“Poa!”

“Bomba!”

“Freshi tu!”  Sauti zilisikika kutoka kwa wanafunzi hao.  Walionekana wachangamfu.  Ndivyo watoto wa mjini walivyo.  Wanajiamini daima.  Ndivyo alivyofikiri Benito.  Akakumbuka alivyokuwa yeye wakati akisoma shule.  Akawakumbuka rafiki zake aliokuwa nao wakati huo.  Akakitonesha kidonda moyoni mwake.  Ambacho, kimegoma kupona miaka yote hiyo.  Akatambua fika endapo ataziendekeza kumbukumbu hizo kwa wakati huo basi asingeweza kuzungumza tena na wanafunzi hao.

Akaachana na fikra hizo ili kuendeleza soga.  “Niambieni mabest shule niaje?”

Mwanafunzi mmoja wa kike aliyekuwa ameegemea kibanda cha kupumzikia abiria akajibu, “Shule.... shule poa tu kaka!  Si’ unajua ni lazima uikubali nd’o uienjoy!”

Benito akamtazama binti huyo aliyekuwa na rangi asilia nyeusi na macho makubwa.  Alipendeza ndani ya sare zake za shule.

“Shule mnayosoma inaitwaje?”  Benito akauliza.

Mwanafunzi mmoja wa kiume ambaye wakati Benito anawasili ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkubwa, akiyasherehesha maongezi yake kwa vichekesho na kuwaacha hoi kwa vicheko wasikilizaji, alikuwa na haraka ya kumjibu Benito.  “Kamene High School.”

“Ooh!  Ipo wapi sasa?”

“Siyo mbali bro.  Si unaona hiyo kona hapo inayoongoza mkono wa kulia....”  Mwanafunzi huyo sasa akawa anamwelekeza Benito kwa kunyoosha kidole chake cha shahada cha mkono wa kulia.  “Basi unaingia nayo kulia, mbele kidogo unapiga kona kushoto, geti lipo barabarani tu.  Yale majengo yote yanayoonekana nd’o skuli yenyewe.  Bonge la shule!”

“Kumbe hata siyo mbali”

“Yah!”

“Kuna sister mmoja nimesoma naye kitambo, ni mwalimu.  Sijui atakuwa hapa?”

“Mh!  Nani huyo?”

“Sina kumbukumbu nzuri ya jina lake, lakini ni somebody Hashim.”

“Si’ umesema sister, sasa inakuwaje aitwe Hashim?”

Kabla Benito hajajibu wala kufikiria ajibu nini, mwanafunzi mwingine wa kike akadakia.”Na wewe nawe!  Unakuwa kama hujui!  Si anaweza akatumia Hashim kama ubini.?”

Benito akatabasamu, ndipo akachangia, “Sawasawa mdogo wangu.  Hashim ni jina lake la pili.  La kwanza limenitoka kidogo.”

Mwanafunzi mwingine aliyekuwa akinywa maji ya chupa, aliushusha mkono wake kutoka mdomoni na kuitupa chupa iliyokuwa tupu.  Wakati wenzake wakiangaliana, akapata nafasi ya kulimeza funda la maji.  Akaongea,  “Siyo Hafsa huyo?  Nyie hamumjui mwalimu Hafsa kwani? Jina lake la pili ni Hashim.  Nd’o maana huwa anaandika HH?  Kwani bro huyo unayemzungumzia yukoje?”

Benito hakuweza kuyaamini masikio yake.  Ni kweli tangu wakiwa shule Hafsa alipenda kuandika jina lake kwa kifupi HH.  Akataka kujibu haraka kuelezea wajihi wa Hafsa lakini moyo wake ukasita.  Akaona hana haja ya kukurupuka.  Kwa mantiki hiyo, akadanganya.

“Dah!  Unajua ni muda mrefu sana  hata simkumbuki vema.”

“Aggrey!  Kwani ni nani unayemzungumzia wewe?”  Mwanafunzi mwingine akamtupia swali mwenzake.  Aggrey hakusita kujibu.

“Acha wewe!  Unataka kuniambia yule mwalimu wa history wa advanced humnyaki?  Yule anayeongea kwa mapozi.  Yule mwalimu mrembo sana.”

“Aah!  Kumbe yule tunamwita Miss Tanzania!”

“Sasa nd’o unasema humkamati?”

Benito akatulia tuli akiwashuhudia wanafunzi wale wanavyozinguana.  Hiyo ndiyo kazi iliyompeleka Tabata.  Mambo yanapojiweka kwenye mstari, ana haja gani ya kuwa na papara?  Benito akajipa jawabu kuwa Hafsa anafanya kazi pale.  Akatulia akiwaacha wanafunzi wakiendelea kumjadili mwalimu wao.

“Kama ni huyo nampata.”

“Sasa huyo nd’o anaitwa Hafsa Hashim.”

“Kwa hiyo bradha unataka kumwona tukupeleke?”

“Hapana jamani.  Nitamtembelea tu siku nyingine maadamu nimefahamu kuwa yupo.  Leo nimebanwa kidogo na ratiba.” Benito akajibu.

“Kwa hiyo tumwambiaje?”  Yule mwanafunzi mrembo mweusi akauliza.

“Hapana.  Wala msimwambie kitu chochote.  Siku nitakayokuja nataka iwe surprise kwake.  Nawashukuruni sana. Naomba nisiwapotezee muda zaidi.  Wacha niende.”  Benito akashukuru akiaga.

“Jamani bro, hata jina tu?”  Yule binti akasema.

“Ooh!  Very sorry!  Naitwa James.”

Akawadanganya jina lake akiwa na sababu yake ya msingi.  Akaondoka.  Wakati akiondoka aliwasikia wanafunzi wale wakijadiliana.  Alibahatika kusikia sentensi chache.

“Lakini mbona mwalimu Hafsa ameolewa?”

“Si ndiyo hapo!”

“Msiwe mafala nyie!  Kwani kuolewa kitu gani?”

Akavuka upande wa pili kwa minajili ya kupanda daladala madhali kazi yake imeleta mafanikio.  

Akawa ndani ya daladala.  Dereva na utingo wake waliporidhika, wakaondoa gari.  Ndani ya gari kukiwa na Benito aliyezama kwenye lindi la mawazo.  Akijaribu kukokotoa hesabu kadha wa kadha kwa kanuni alizozijua yeye mwenyewe. 

Lakini akawa na faraja sasa.

Amepata jibu.

Atajua la kufanya.

Atafanya tu.

Ndivyo alivyowaza.



“NAMI nafurahi sana kukutana nawe.”

“Dah!  Hata siamini!”

“Ndivyo hivyo Ali, kwa bahati mbaya tumekutana wakati mbaya.”

“Hapana Rehema, ni kama muujiza kukutana nawe leo.”

“Wakati wote mwujiza humaanishwa kuwatokea watu katika wakati na hali wasiyoitaraji.”

“Leo nimeamini hilo.  Sijui hata nikushukuruje!”

Ali alirejewa amani moyoni mwake.  Akamwita mhudumu na kuagiza bia ya Safari.  Ingawa tayari alimkumbuka Rehema na mahali walipowahi kuonana, bado shauku yake ilikuwa ni kufahamu ni namna gani Rehema aliweza kutokea ndani ya daladala ile na kumnusuru.  Kiu yake ilikuwa ni kufahamu mengi ambayo pengine hakuyafahamu.  Baada ya mhudumu kuileta bia yake, Ali akaendeleza maongezi. “Rehema nifahamishe basi.” 

“Inategemeana na wewe unataka kufahamu nini.”

“Kwa ufupi, napenda kufahamu ilikuwaje kuwaje hadi tukawa ndani ya daladala moja.”

“Aaah!  Unanipa raha Ali." Rehema akamtazama Ali kwa jicho tamu.  Ali akayakwepesha macho yake haraka.  Hata hivyo, bila shaka ujumbe ulikuwa umemfikia.  Rehema akanywa funda moja.  Akajipa muda wa kumeza funda hilo.

“Unajua nini Ali?  Ni kama bahati.  Nadhani Mungu wako anakupenda sana na akapanga iwe hivyo.  Mimi sikuwa na ratiba ya kufika Mnazi Mmoja kabisa.  Kuna rafiki yangu ambaye ni nesi pale ndiye aliyenipigia simu niende kumwona.  Amerudi kutoka likizo juzi.  Sikuwa nimeonana na shosti wangu huyo mwezi mzima akiwa Moshi kwa wakweze.  Baada ya kupiga naye stori nyingi nikawa naelekea pale kituoni ili nipande zangu daladala kurudi kwangu.  Tupo pamoja?”

“Yap!  Huniachi nyuma hata kidogo.”

“Unaona sasa?  Ni kama Mungu tu alipanga.  Wakati nakaribia pale kituoni nilikuona.  Basi nikawa nakuja usawa wako ili nikusabahi.  Ile nakaribia tu, ndiyo yule jamaa yako akakukwida.  Huwezi kuamini, nilijisikia vibaya kuliko ninavyoweza kueleza.  Niliumia mno.”  Rehema akaongea kwa hisia kali.  Ali alitulia tuli mithili ya maji ya mtungini.   Alifikiria mambo mawili matatu kichwani mwake.  Alishaisahau hata bia mezani pale.

“Unasikia Ali?”  Ali akatingisha kichwa kuashiria wapo sambamba.  Rehema akaendelea.  “Nikasogea hadi pale mlipokuwa.  Nikawa mmoja wa watu waliokuwa wanawatazama kwa karibu.  Uliporeact kwa kujiamini moyo wangu ukatulia kiasi.  Nikaendelea kuwa nyuma ya kila hatua uliyoichukua.  Nilipokuwa naketi tu ndani ya ile daladala pembeni yako, nikamwona yule mpuuzi naye akiingia.

“Nikajifanya nipo busy na simu ili tu wewe usipate nafasi ya kuanzisha stori nami katika kutafutasymphathy.  Nilitambua fika kwa hali ya kuchanganyikiwa uliyokuwa nayo, lazima ungetaka kujihami.  Na kama ungefanikiwa hilo pengine ungenikumbuka kwa urahisi.  Na ungenikumbuka, najua ungechachawa katika kutafuta upenyo.”

“Na nilipokuuliza kituo kinachofuatia, kwa nini ulinijibu kavukavu vile?”

“Subiri Ali.  Nitafika kote huko.  Nilipokujibu vile nilikuwa na sababu mbili.  Kwanza, kama nilivyosema awali, sikutaka upate muda wa kunikumbuka.  Pili, nilijua endapo ningekufahamisha jina la kituo kama ulivyohitaji, lazima ungekurupuka kutaka kushuka.  Nilifahamu yule jamaa alikuwemo ndani ya daladala kwa ajili yako.  Hivyo kama nisingekuwa makini, pengine siku moja ningejilaumu kwa kushindwa kukunusuru na zahama iliyokuwa mbele yako.”  Alipofika hapo, Rehema akashusha pumzi kidogo.  Akanywa bia yake kidogo jambo lililomkumbusha Ali.  Naye pia akanyanyua bia yake na kupiga pafu moja refu. 

“Rehema, nashindwa hata nisemeje!”

“Subiri kijana, acha upesi.  Bado sijamaliza somo.”

“Ok!  Lakini kabla hujaendelea tafadhali niruhusu nikuulize swali.”

“Yes.  Uliza.”

“Kwa hiyo hukutaka nishuke ukiwa na hakika ungenisevu kwa mtindo ule?”

“No Ali!  Haki ya Mungu sikuwa nafahamu ningefanyaje kukusevu.  Nilikuwa nikiumiza kichwa changu safari nzima.  Hadi daladala inafika mwisho wa safari sikuwa nimepata suluhisho.  Muda ule namsihi yule fala apunguze munkari ndipo alipocheza faulo mwenyewe.  Majibu yake yalinikasirisha zaidi.”

“Ndipo ikawaje?”  Shauku ya Ali ilikuwa kubwa.

“Anhaa!  Nilipokuwa namlipa nauli kondakta wazo likanijia kichwani.  Nikajaribu kuongea na konda akakubali.  Akaenda kwa dereva wake, wakakubaliana.”

“Ndiyo ukaamua kutudatisha kuwa tumekutukana?”

“Hujatulia wewe!  Wewe ulidhani mie ningefanyaje?  Hata hivyo huoni kuwa ni janja iliyosaidia?”

“Ni kweli Rehema.  Nikiwa mkweli mbele zake Mungu, nashindwa nitoe shukrani zangu kwa namna gani.”  Ali akawa anaingiza mkono wake kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake.  Akatoa waleti yake ndogo na kuanza kuchomoa noti kadhaa za fedha.  Hakuwa amefika mbali kabla hajashitukiwa na Rehema.

“Unafanya nini Ali?”

“Mh, nothing!”

“Be honest Ali.  Unafanya nini?”

“Tulia basi nimalize ndipo ujuwe nilikuwa nafanya nini.”

”Sikiliza rafiki yangu.  Naelewa unataka kufanya kitu gani.  Kama unakusudia kunirudishia pesa, utanikwaza.  Mimi ndiye nilyekuleta hapa.  Gharama zote ni jukumu langu.  Tumeelewana?”

“Ahsante sana Rehema.”

Wakapeana michapo mbalimbali wakiendelea na vinywaji taratibu.  Rehema alisema alihamia Dar es Salaam kikazi, katika kituo cha polisi Chang’ombe.  Ali naye akamfahamisha Rehema kuwa anajishughulisha na biashara.  Ali hakusahau kumweleza Rehema juu ya mke wake ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari ya Kamene iliyopo Tabata Kimanga.

Muda nao ukawatupa mkono.  Wakaagana kwa miadi ya kukutana wakati mwingine.  Wakapeana namba za simu.  Wakaelekezana mahali walipokuwa wakiishi.

Ali alipowasili nyumbani kwake, tayari mke wake alisharudi baada ya kazi.  Akili ya Ali haikutulia mara tu baada ya kuagana na Rehema.  Alifikiri juu ya Benito.   Hakuona umuhimu wa uhasama huo.  Hakuona mantiki yoyote.  Hata hivyo alipata wakati mgumu kujaribu kukisia ni hatua gani zaidi ambayo Benito angetembea.  Akajitahidi kutolizungumza jambo hilo kwa mkewe mapema.  Akamwacha amalize ratiba zake za shughuli za nyumbani.

Usiku wakiwa kitandani tayari kwa kulala ndipo Ali alipomsimulia mke wake habari yote kuhusiana na yaliyojiri siku hiyo.  Alisimulia kwa tuo, kwa sauti hafifu ambayo ilidhihirisha wazi hofu yake.  Simulizi hiyo ilamfanya mkewe kudondosha machozi mengi.  Ali akajivuta na kumkumbatia mke wake.  Akampiga busu kwenye paji la uso wake.

“Hafsa mpenzi, usilie mama.  Kwani nimefanya vibaya kukwambia?”

“Ha.... ha....... hapana.”

“Basi usilie mke wangu mpenzi.  Wewe uwapo nami jisikie amani.  Mimi nakupenda wewe nawe wanipenda mimi hofu yako ni ya nini?  Jikaze mpenzi.  Benito hana la kutufanya.  Amini hivyo kidani cha moyo wangu.”

Ali alimliza zaidi Hafsa.  Akaacha kumbembeleza.   Alimpapasa mwilini taratibu.  Ni mkewe.  Alimfahamu vizuri.  Muda mfupi baadaye Hafsa akawa anaogelea kwenye bahari ya mahaba.

Maisha yao yakaendelea kama kawaida.  Hafsa shuleni kwake.  Ali dukani kwake.  Kila mmoja akijitahidi kumfanya mwenzake asahau kabisa habari yoyote kuhusiana na Benito.  Hakuna aliyekuwa tayari kumwona kipenzi cha moyo wake akiumia zaidi.

Baada ya siku tatu, majira ya jioni, Ali aliingia nyumbani akitokea kwenye moja ya shughuli zake za biashara.  Alimkuta mkewe barazani akiwa ameegamia ukuta.  Ali alihisi kuna jambo lisilo la kawaida.  Alipomkaribia mkewe alimkumbatia kwa upendo kama ilivyo desturi yao.  Akampa busu zito mdomoni kiasi cha kumfanya ashushe pumzi zake kwa nguvu na kusahau masahibu yake.

“Nakupenda sana mume wangu.”

“Nakupenda pia Hafsa wangu.”

Wakaingia ndani wakiwa wameshikana viuno.  Mapenzi bwana!  Wapendanao kwa vituko huwawezi.  Ali na Hafsa walipoingia chumbani walikuwa bado wameshikana viuno.  Mara wajigonge kwenye viti wanapotembea.  Mara Hafsa amtekenye Ali kidogo ilimradi iwe burudani raha mustarehe!  Mule chumbani vituko viliongezeka maradufu.  Kurushiana midoli iliyokuwemo chumbani mwao.  Mara kurushiana nguo.  Huyu akachojoa sarawili yake na kumrushia mwenzake.  Huyu akaichojoa shimizi yake na kumrushia mwenzake.  Sasa wakawa wanakimbizana na kupigana chenga kama wapo mpirani vile.  Ikawa huku.  Ikawa kule.  Ikawa hapa.  Ikawa pale hata Ali akamzidi ujanja Hafsa na kumdaka.  Akamtupia kitandani.  Naye akafuatia.

“Ngoja nikupe mchapo sweetie.”  Hafsa alianza kuongea wakati akijivuta pembeni ya mwili wa Ali.

“Hafsa mwenzio nimechoka.  Twende kwanza bafuni tukaoge nd’o utanipa huo mchapo.”

“Haya twende basi tukaoge.”

“Nibebe basi.”

“Mwili huo!  Mi’ nimeshakubeba sana.  Saa hizi zamu yako kunibeba mimi.”

Wakaoga.

Wakawa mezani kwa chakula.

“Basi rafiki yangu, Benito leo kaja kunitafuta.”

“Wacha weh!”

“Nd’o hivyo honey.”

“Umeonana naye?”

“Wala.  Ameishia pale kituoni.  Akawakuta wanafunzi wakiwa break.  Akajifanya kuulizia ulizia kana kwamba kanisahau hata jina la kwanza.”

“Enhee!  Ikawaje?

“Wanafunzi wakamweleza ni kweli nipo.  Walipomwuliza wanifikishie ujumbe gani, unajua kawajibuje?”

“Enhee?”

“Eti wauchune ili siku atakayokuja iwe surprise.”

“Itakuwa surprise kweli.”

“Sasa unanitisha?”

“Usifike huko mpenzi.  Ni nani kakufikishia stori hiyo?”

“Kuna mtoto mmoja machepele ile mbaya anaitwa Lydia.  Mwenzangu, eti kawadanganya kuwa anaitwa James.”

“Usiogope laazizi wangu.  Siku akija, wala usikubali kutoka nje ya geti la shule.  Akitaka azungumze nawe mkiwa ndani.  Ukitoka nje anaweza hata kukudhuru kwa urahisi.  Si unamjua mtu mwenye alivyo mwehu utadhani akili zake kashikiwa na mtu mwingine.  Lakini pia jambo hilo lisisumbue sana akili yako.”

“Wewe unadhani ni rahisi akili yangu kutosumbuliwa?”

“Sidhani hivyo.  Bali kupotezea.”

Dar es Salaam

Jumatatu, Mei 5, 2003

NDIYO kwanza wanafunzi wa kidato cha sita walikuwa wametoka kwenye mtihani wao wa kwanza ambao ulikuwa General Studies.  Dakika kadhaa zilikwishayoyoma baada ya saa tano kamili ya asubuhi hiyo.  Hali ya hewa haikuwa mbaya.  Manyunyu kiasi yalisaidia kidogo kupunguza joto la jiji la Dar es Salaam.  Wanafunzi wengi waliotoka kwenye mitihani walisimama katika makundi madogo madogo wakijaribu kujadiliana hili na lile kuhusiana na mitihani yao hiyo.

Pembeni kidogo nje ya geti la kuingilia shuleni hapo ikapaki  gari ndogo iliyokuwa na rangi nyeupe iliyofubaa kidogo.  Dereva wa gari hiyo, Toyota Camry alitoka nje na kurekebisha kidogo mkanda wa suruali yake. Akamwita mwanafunzi mmojawapo kati ya wengi waliokuwa katika eneo hilo.  Alipotoa sauti kumwita mwanafunzi, wote walibaki kutazamana kwa sekunde chache hadi mmojawapo alipojitokeza na kuelekea kule ambako gari ilipaki na dereva wake kusimama nje yake akiwa ameliegamia.

“Mambo vipi best?.”  Mtu huyo aliyekuwa kavalia kinadhifu alianza kwa kumjulia hali mwanafunzi huyo.  Alivalia suruali maridadi ya rangi nyeusi.  Drafti za rangi nyeupe zilizojificha kwa mbali kiasi cha kumhitaji mtu kuwa karibu zaidi ili kuweza kuzibaini.  Mkanda wa suruali ulikuwa ni wa ngozi nyeusi ukiwa na chuma cha rangi ya fedha.  Shati lake jeupe liling’aa.  Nalo, likiwa na drafti za rangi nyeusi hafifu.  Lilisindikizwa vema na tai fupi nene ya rangi nyeusi ikiwa imelegezwa kiasi eneo la shingoni.  Unadhifu wa mtu huyo ulikolezwa sawia na jozi ya viatu vyeusi vya ngozi vilivyochongoka kwa mbele.

“Safi tu bro.  Shikamoo.”

“Ok. Fine!  Samahani kwa kukusumbua.”

“Usijali bro bila samahani.”

“Yah, eti kuna mwalimu hapa wa kike anaitwa Hafsa Hashim?”

“Ndiyo yupo.”

“Na sijui nitaweza kumpata vipi?”

“Dah!  Unajua nini bro?  Watu wapo katika paper sasa walimu kibao hawajatokea shuleni”

“Ok.  Samahani kwa usumbufu mdogo wangu.  Utajali kama utakwenda labda ofisini uweze kupata uhakika kama yupo ama lah?”

“Haina shida bro.  Dakika chache tu.”

“Ahsante sana.”

Sidhani kama mwanafunzi huyo aliisikia hiyo ahsante sana.  Alipokuwa amepotelea kwenye viunga vya miti ndani ya shule hiyo, Benito, aliendelea kuegamia gari lake.

“Halafu huyo mshikaji mbona nd’o mdogoake Teacher Hafsa!”  Mwanafunzi mmoja wa kiume ambaye alisimama karibu wakati Benito akizungumza na mwanafunzi wa awali.

Benito akashituka.  Akafanikiwa kuuficha mshituko wake.  Akauliza.  “Kweli?”

Mwanafunzi yule kama aliyelitaraji swali hilo, akajibu upesi.  “Kweli kabisa bro.”

Benito akamshukuru.  “Ahsante sana kaka.”

Yule mwanafunzi wala hakuijibu ahsante sana ya Benito.  Tayari alikwishaanza na hamsini zake.

 Benito akaingiza mkono mfukoni.  Akautoa ufunguo wa gari. Akawa anauchezea kwa kuuzungusha kwenye kidole cha shahada cha mkono wake wa kushoto.  Wakati zoezi hilo likiwa ndiyo linaanza kumnogea, yule mwanafunzi akarejea akitembea kwa kudunda.  Benito akamtazama kwa chati kama vile ana kitu anachojaribu kukijenga kichwani.

“Hayupo bro.”

“Ooh!  Bahati mbaya sana.  Sijui labda unapafahamu mahali anapoishi?”

“Hapana kaka.”

Mbona ametonywa kuwa mwanafunzi huyu ni mdogo wake Hafsa?  Benito alijiuliza.  Haikosi namna.  Aliwaza.

Kimya kifupi kikatawala.

“Mimi ninaitwa Benito, sijui mwenzangu waitwa nani?”  Benito alijitambulisha

“Mimi naitwa Maulid.”

“Upo kwenye mitihani siyo?”

“Hapana.  Mi’ bado nipo Form Five.”

“Sasa bwana mdogo ninahitaji unisaidie jambo moja.”

“Sawa hakuna tatizo.”

“Sijui una simu ya mkononi?”

Maulid akasita kidogo kujibu.  Akafikiri haraka kabla ya kujibu, “Hapana bro”

“Ok.  Sasa mimi nakupa namba yangu.  Ila ninachokuomba ni kwamba, siku mwalimu Hafsa atakapokuwa yupo hapa  tafadhali nenda kibanda cha simu hapo.”  Benito akaunyosha mkono wake ili kumwonesha Maulid kibanda cha simu kilichokuwa kikitazamana na lango la kuingilia shuleni hapo.  “Nenda hapo unipigie simu.”  

Maulid hakujibu kitu. Benito alipoona Maulid hajajibu neno lolote, akaendelea.  “Nahitaji sana msaada wako mdogo wangu Maulid.”

“Lakini bro, kwanini usiache ujumbe wako pale mapokezi?”

“No.  Unajua nini?  Namhitaji Hafsa na siyo mapokezi.  Pia naepuka mlolongo mrefu katika kuelezea shida yangu kwake.  Tupo pamoja?’

“Hapana.”

Benito akatabasamu kidogo.  Akaongea.  “Sikia mdogo wangu, nahitaji sana msaada wako.  Lakini pia ni jukumu lako kuamua kunisaidia ama lah.”

“Naweza kukusaidia.  Lakini siyo dhambi nikitoa mawazo yangu.  Unanipa mtihani mgumu sana bradha.”

“Kwanini?” 

“Style uliyomuulizia na pia maagizo unayonipa yananiacha na lundo la maswali kichwani.”

“Usiogope.  Niamini mdogo wangu.”

“Yah, naweza kukuamini.  Lakini bado napata wasiwasi.  Kwani wamtafutia nini?”

“Ahaa, Kumbe ndicho!  Usikonde kabisa.  Unajua unapokutana na mtu kwa mara ya kwanza, huwezi anza kumweeleza kila kitu unachokifahamu duniani.  Kadiri ya mazoea baina yenu yanavyokuwa, hata ufahamu juu ya kila mmoja wenu nao unakuwa.  Nataka kusema nini?  Jinsi tutakavyokuwa tukizoeana ndivyo utayafahamu mambo mengi.”

“Sure?’

“Hakika kweli.  Enhee, hujanijibu kama utanisaidia ama hapana.”

“Nitakusaidia.”  Maulid alitoa jibu ambalo hata hivyo hakuwa na hakika nalo.

“Kitu kingine, pamoja na kukuhitaji kunijulisha pindi mwalimu awapo hapa, pia ninakuomba uyafanye haya maongezi yetu kutojulikana kwa mtu yeyote zaidi yetu siye wawili.”

“Hilo, usitie shaka.”

Benito aliufungua mlango wa gari lake.  Akaingia.  Akatoa kadi yake ya mawasiliano.  Sambamba nayo, noti ya shilingi elfu tano.  Akampatia Maulid.

“Kuna namba yangu humo.  Pesa utaitumia kunipigia.”

“Poa.”

“Tunza ahadi.”

“Usijali bro.”

Benito akaliwasha gari lake.  Aliondoka kwa mwendo wa wastani.  Alipunga mkono wake wa kulia kumuaga Maulid.  Maulid alikimbia kiasi hadi kwenye kona ya ukuta wa shule ili apate kulishuhudia gari hilo likipotea kwenye njia inayoingia kituo cha daladala cha Tabata Kimanga.

Wakati Maulid akiwa ndiyo anaanza kuondoka kurudi tena mahali alipokuwa, simu yake ikaita kuashiria ujumbe umeingia.  Alipoufungua kuusoma, alikutana na ujumbe kutoka kwa mwalimu Hafsa ukimjulisha kuwa ameondoka kwenda nyumbani.  Ujumbe huo, pia ukamtaka Maulid amfuate huko pindi atokapo shuleni.

*****

HAFSA aliliona lile gari la Benito wakati linapaki pale.  Alijikuta tu kuvutiwa kuendelea kulitazama.  Alipotoka dereva wake, Hafsa alishituka kumwona Benito.  Japokuwa hakuwa amemwona kwa miaka mingi sasa, alikuwa na hakika ndiye kutokana na habari zake alizokuwa amekwisha zipata siku si nyingi.  Hafsa alijikuta anaishiwa nguvu ghafla, asijue la kufanya.  Yeye alidhani kuwa Benito angeingia ndani na kumuulizia kwenye utawala.  Akaanza kupanga namna ya kumkabili itakapotokea hivyo.  Hata hivyo, akawa katika wakati mgumu. 

Alipomwona Benito anamwita mwanafunzi walau hofu ikampungua kidogo.  Wanafunzi walipokuwa wakisita kwenda kwa Benito bado jicho lake lilikuwa kwao.  Maulid alipojitokeza, alizishusha pumzi zake kwa nguvu kumshukuru Mungu.  Alichokifanya ni kuendelea kubana kwenye kona aliyokuwepo.  Maulid alipopita, akamwita.

“Enhee, niambie dogo, yule jamaa alokuita amesemaje?”

Maulid akamsimulia mwalimu Hafsa maongezi yake na Benito.  Hafsa akamwambia Maulid akamjibu Benito kuwa yeye hayupo.  Akamwambia ana nia ovu juu yake.  Zaidi, watazungumza jioni. 

Hafsa na Maulid hawakuwa na undugu hata kidogo.  Lakini,  walifahamiana kwa muda mrefu kabla.  Walipata kuishi pamoja huko Iringa wakati baba yake Maulid akiwa meneja wa kampuni ya biashara ya mkoa (RTC) wakati huo.  Baada ya baba yake Maulid kufariki dunia miaka sita iliyopita, alienda kuishi na dada yake aitwaye Zuhura afanyaye kazi Shirika la Umeme (TANESCO), Makao Makuu Ubungo kama karani wa mahesabu.

Walizoweana. Vile vile, Hafsa alikuwa na ukaribu mkubwa na Zuhura, dada yake Maulid.  Kila mtu alijua ni ndugu wa damu.

Maulid alipohakikisha Benito ameondoka zake alikusudia kurudi pale alipokuwa amemwacha mwalimu Hafsa.  Alipoupata ujumbe wa simu kwamba amfuate nyumbani baada ya masomo, hakuwa na hamu ya kuendelea na ratiba ya shule.  Aliwaaga wanafunzi wenzake.

Hakutaka kupandia daladala papo hapo shuleni kwa kuwa huwa zinapita zikiwa tayari zimejaza abiria.  Akaamua kutembea hadi pale kituoni Tabata Kimanga.  Wakati anavuka barabara kuelekea upande wa pili zinakopaki daladala za Kisukuru, aliliona gari dogo linalofanana na lile alilokuwa amekuja nalo Benito.  Lakini hakulizingatia akijiaminisha kwamba Benito aliendelea na safari zake moja kwa moja.  Pia hakushughulisha nalo kwani hakuwa hata amezikariri namba za gari la Benito.

Aliongoza hadi kwenye daladala iliyokuwa imepaki hapo kituoni.  Hakuwa amezingatia walau kutazama nyuma.  Wakati akiwa anaketi kitini alistaajabu kumwona Benito akiwa amesimama mlangoni.

“Ooh Maulid!  Nikusumbue tena.”

Maulid alitaharuki, asijue hata azungumze nini. Kengele ya tahadhari ikaanza kugonga kichwani mwake.  Benito aliendelea kumtazama Maulid kwa jicho la kirafiki lenye chembe nyingi za huruma.  Alipoona Maulid anashindwa aongee nini, akapata nguvu ya kuzungumza.

“Aaaah!  Nakuomba ushuke garini tuzungumze kidogo.”

Tayari mapigo ya moyo ya Maulid yalikwishaanza kwenda kasi.  Maulid akatazama pande zote za pembeni kana kwamba anamtaraji mtu kumpa msaada.  Hofu ilitanda moyoni mwake, akahisi kwamba ameingizwa mtegoni mwa hawa watu wawili. Akapiga moyo wake konde.  Akateremka kutoka katika daladala hiyo. Akamfuata Benito hadi kwenye kiduka kidogo alikokuwa amelipaki gari lake.

“Vipi rafiki yangu, unarudi nyumbani?”  Ndivyo alivyoanza Benito baada ya Maulid kuketi.

“Ndiyo.”

“Kwani unaishi wapi?”

“Tabata Mawenzi.”

“Mbona unapanda daladala za huko Migombani?”

“Mmh!  Huko namfuata rafiki yangu mara moja then nd’o narudi nyumbani.”

“Je, ni muhimu kumfuata huyo rafiki yako leo?  Na pengine muda huu?”  Benito aliuliza akimtazama Maulid usoni.

Maulid akasita kidogo, hakufahamu kusudio la swali hilo.  Akafikiri kidogo, ndipo akajibu, “Yah, ni muhimu sana.  Tulipokuwa kwenye discussion mshikaji aliondoka na funguo yangu kwa bahati mbaya.  Nd’o naiendea.”

“Utajali kama badala ya kuhangaishana na daladala nikajitolea kukupeleka?”

Hapo tena Maulid akasita, lakini sasa akiwa ameweka tahadhari ya kutosha kichwani mwake, akaendelea kujibu.

“Hapana bro.  Nashukuru sana kwa ofa yako.  Nitafurahi kama nitakwenda mwenyewe.”

“Sawa.  Pia nami ningefurahi sana endapo ungeipokea ofa yangu.  Wewe ni mdogo wangu, lingekuwa jambo la heri kama ungeupa uzito msaada wangu.”

“Pamoja na hayo...”  Maulid akauinua uso wake na kumtazama Benito aliyekuwa amemkazia macho yeye muda wote.  Benito akayapeleka macho yake pembeni.  Tendo hilo likamjaza Maulid nguvu ya kuendelea.

“Ninakokwenda hawajawahi kuniona hata siku moja nimekwenda na gari, na wanafahamu fika kwetu hakuna gari.  Bro, huoni leo nitatafsiriwa vingine tofauti na vile nilivyo siku zote?”  Maulid alijitetea.

“Lakini ndugu yangu Maulid....”  Hapo Benito akawa anajaribu kuzungumza kwa sauti ya chini lakini yenye ushawishi.  “Huoni kuwa kutowahi kwako kwenda na gari bado hakuwezi kuwa kizuizi kwa wewe leo kwenda na gari?”

“Wananifahamu mimi siyo mtu wa hadhi hiyo.”

“Siyo suala la hadhi.”

“Bali?”

“Ni suala la wakati.  Hayo unayoyazungumza ni wakati uliopita.  Wakati uliopita hauwezi kutumika kama kigezo cha jambo fulani kwa wakati uliopo.”

“Sawa nimekuelewa bro.  Lakini at the end of the day, bado nitakwenda mwenyewe kwa daladala.  Hivyo ndivyo ninavyopenda kufanya.”

Benito akayainua macho yake na kumkazia Maulid ambaye hakujishughulisha kuyakwepesha macho yake.  Benito akawa anajaribu kupambana na hasira iliyoanza kuwa dhahiri usoni pake.

“Eti, Maulid...:”

“Naam!”

“Kuna kitu unajaribu kunificha?”

“Sina jambo la kukuficha bro.”

“Unadhani una akili nyingi sana, siyo?”

“Ah!  We vipi?”  Maulid akashindwa kutuliza akili yake.

Maulid ni kijana anayejiamini anapozungumza na mtu yeyote.  Mara chache, humtokea kuvamiwa na hofu.  Ni makini sana kupangilia hoja anapozungumza.  Shuleni amekuwa aking’ara daima katika midahalo mbalimbali ya masomo ya Historia na Lugha.  Ujasiri wake ulimfanya akubalike zaidi na wanafunzi wenzake na walimu wake.

Maulid alipoona Benito anataka kumburuza, naye akaghafirika.  Hata hivyo akawa amefanikiwa kuituliza akili yake haraka na kuzungumza kwa ujasiri. “Sikiliza bro.  We’ umekuja shuleni kwetu u mgeni.  Sikujui hunijui.  Si ndiyo?”

“Yah!”

“Umehitaji msaada kwangu.  Nami nikaondokea kukuamini japo sifahamu haswa dhamira yako kwa mwalimu Hafsa ni nini.  Lakini pia ukaniambia ni jukumu langu kuridhia kama nipo tayari kukusaidia ama lah.  Nakosea?”

“Hukosei.”

“Nikaridhia kukusaidia. Ukanipa maelekezo uliyoyaona ya muhimu.  Tukamalizana tukaagana...”

“Lakini bwa’mdogo...”

“No.  Subiri nimalizie”

“Ok.  Endelea”

“Enhee!  Kukutana kwetu hapa kumetokea kwa bahati mbaya.  Nilikuwa na uhuru wa kuukataa wito wako.  Nimekuheshimu.  Nimeitikia, nimekuja kukusikiliza.  Matokeo yake unakuwa mkali kwangu kwa mambo yasiyo na msingi.”

Benito akafahamu kuwa Maulid keshakasirika.  Ikamlazimu kuwa mpole, “Ok.  Nimekubali mdogo wangu.  Tafadhali niwie radhi.”

“Anyway, kwangu siyo tatizo.  Niruhusu niende, muda umekwenda sana.”

“Nashukuru sana kwa muda wako.  Leo ni Jumatatu, tafadhali nitafute Ijumaa jioni endapo utapata wasaa.  Tutayazungumza haya mambo kwa kirefu.”

“Sawa hakuna noma bro.”

“Thanks.”

Maulid akainuka kitini.  Akaelekea moja kwa moja kupanda daladala.  Akiwa garini aliweza kumwona Benito akiendesha gari lake taratibu kuondoka eneo hilo.  Mambo mengi yakawa yanamzonga Maulid kichwani mwake.  Akatamani kufahamu kilichomo ndani ya haya mambo.

Alipofika nyumbani kwa Hafsa, alimkuta kaketi barazani.  Hafsa alionekana kukosa raha. Nyumba aliyokuwa akiishi Hafsa ni kama hatua hamsini hivi baada ya kulipita kanisa la Kilutheri la hapo Kisukuru.  Nyumba hiyo ilikuwa na mandhari ya kupendeza.  Vichane vya maua vilizunguka pande zote. Urembo wa Mwalimu Hafsa na uzuri wa mandhari ya nyumba vilififishwa na hali ya unyonge aliyokuwa nayo.

Maulid alisimama kando kidogo ya Hafsa.  Hakuzungumza neno lolote.  Aliingiwa na huruma kumkuta Hafsa katika hali ile.  Akaanza kuhisi jambo lililo mbele ni kubwa kuliko alivyokuwa akilikadiria yeye.  Alizama kwenye lindi la mawazo hadi alipogutushwa na sauti ya mwalimu Hafsa.

“Ooh!  Maulid mdogo wangu, umekuja.  Karibu ndani.’’

“Hapa hapa panatosha.”

“Haya baba.  Kama nafsi yako i radhi.  Leo wapendelea nini?  juisi ama soda?”

“Chochote dadaangu.”

“Halafu kila siku nakukataza kusema chochote bwana!  Hakuna duka huwa wanauza chochote.  Haya ngoja nikupe soda.”

Hafsa aliingia ndani.  Si punde akatoka akiwa na chupa ya Pepsi kwenye sinia dogo lenye nakshi ya kupendeza.

“Karibu kakaangu.  Sijakuletea glasi najua unapenda kupiga tarumbeta.”

“Wala usikonde.  Kwa kiu niliyokuwa nayo, hapa umenipatia kabisa.”

“Enhee, dogo hebu niambie kilichojiri.”

Maulid akainywa soda yake funda kadhaa.  Akaiweka chupa chini.  Akaanza kumsimulia Hafsa yote yaliyotokea.  Alijitahidi kutobakiza chochote muhimu.  Hafsa akasikiliza kwa makini pasi kutia neno lolote hadi Maulid alipomaliza.  

Hafsa akashusha pumzi kwa nguvu. “Mmh, kazi ipo!”

“Kwani ni nini kisa sister?”

“Maulid, we acha tu!”

“Nakuomba uniambie sister.  Unajua nami nakosa sana amani ninapokuona katika hali hiyo.”

“Wala huna haja ya kukosa amani dogo.  We’ nenepa tu.  Hakuna lolote la kutisha babaangu.”

“Sister usinipe moyo kwa vitu vilivyo naked kabisa.”

“Tuliza moyo mdogo wangu.  Naomba uniache niweke vema akili yangu.  Itakapotulia nitakwambia, usiwe na haraka.”

Mara wakasikia hatua za mtu akitembea kuelekea mahali walipo wao.  Wote wawili wakashtuka na kutazamana pasipo kuongea neno lolote.  Na mtu huyo alipojitokeza mbele yao, wote wakaishiwa nguvu.




Dar es Salaam

Jumatatu, Mei 5, 2003

TAKRIBANI mwezi sasa ulikwishatimu tokea Ali akutane na Benito.  Ali akawa katika maandalizi kwa safari ya Hong Kong kufunga bidhaa.  Ilikuwa ni siku ya Jumatatu.  Yeye alitarajia kuondoka siku inayofuata.  Akawa anarudi nyumbani kwake.  Kwanza, akashangaa kuliona geti likiwa wazi.  Akapatwa na hofu.  Haikuwa kawaida kwa geti hilo kuwa wazi.  Akatembea kwa kunyata hadi alipokaribia nyumba.  Akasikia sauti za Hafsa na Maulid kutoka verandani.

“Wewe!  Siku nyingine utaua mtu na masikhara yako.”  Ilisikia sauti ya Hafsa.  Hafsa aliishiwa nguvu.  Mapigo ya moyo wake yalienda kasi zaidi.  Akashusha pumzi kwa nguvu.  Alipata mshituko fulani aliposikia hatua za mtu anayetembea kwa kunyata kuelekea mahali alipokuwa na Maulid.

“Pole sana honey.”

“Umenishtua sana Ali.”  Hafsa akawa anazungumza kwa sauti kali iliyojaa hasira na kuchanganyikiwa.  Maulid alitulia kuwashuhudia wanandoa hao.

“Nisamehe basi mke wangu.”

“Bwana eeh!  Yashaisha.”  Hafsa aliitoa kauli hiyo katika namna ambayo haikumpendeza kabisa Ali.  Alionesha dhahiri kukasirishwa na kitendo kile.  Ali naye akakasirishwa kwa kujibiwa kwa sauti ya ukali mbele ya Maulid.  Akajitahidi kutozionesha hasira zake na kumsalimu Maulid.

“Vipi mheshimiwa.  Mambo yako?”

“Aaah!  Safi tu shem.  Shikamoo.”

“Marahaba.  Vipi shule inakwendaje?”

“Safi tu shem.”

“Ok.  Mie nipo ndani.”  Ali akaitoa sentensi hiyo.  Akatembea kuelekea ulipo mlango.  

Hafsa alitambua Ali hakupendezwa kabisa na hali ile.  Ali si mtu wa kupenda malumbano bali ni mwepesi kukasirika.  Ingawa, penye watu, huhifadhi moyoni hasira zake.  

Alipoingia ndani, Ali alipitiliza hadi chumbani.   Akajitupa kitandani.  Alijaribu kumfikiria Hafsa.  Mara, Hafsa akaingia.  Akamwendea moja kwa moja na kumbusu shingoni.

“Nakuomba unisamehe mpenzi wangu.  Najua hujafurahishwa nilivyokujibu.”

“Sina neno.”

“Usiseme hivyo mume wangu utaniumiza.  Nimekukosea.  Tafadhali nisamehe.  Usipofanya hivyo utaniumiza sana.”  Hafsa aliomba radhi.  Sauti yake ilijaa sonona.

“Siku nyingine uwe unatumia akili.”  Ali alijibu.  Alionesha kuwa bado kakasirika.

Ali akamshika Hafsa shingoni kwa mkono wake wa kushoto na kumbusu taratibu juu ya mdomo.  Hafsa akawa anamwangalia Ali kwa macho malegevu mno.  Si punde wakawa nje wakiungana na Maulid ambaye alikuwa akiendelea kunywa soda yake.

Hafsa na Maulid wakautumia wasaa huo kumsimulia Ali habari ya ujio wa Benito shuleni kwao.  Ijapokuwa hakuonesha hofu yoyote, ukweli ni kwamba hali hiyo ilimgutusha Ali.  Alifahamu kuwa Benito anawatafuta, lakini bado hakudhani angeweza kuwa na dhamira kubwa hivyo.  Hata hivyo, Ali akajitahidi kumpa moyo mke wake ili kumfanya asizongwe na mawazo yatakayoendelea kumjengea hofu tele.

“Maulid usitie shaka.  Ni mambo madogo tu haya, yatakwisha muda si mrefu.”  Ali alizungumza wakimsindikiza Maulid kurudi kwao.

Wakati Hafsa anafunga geti, simu ya Ali ikaita.  Hafsa ndiye aliyekuwa ameishika simu hiyo.  Akaitazama kwa makini namba ya mpigaji.  Kwa kuwa namba ya mpigaji ilikuwa imefichwa, Hafsa hakubanduka kwa Ali.  Alikuwa na shauku tele ya kumfahamu mpigaji huyo na dhumuni lake.

“Helo!”

“Mambo vipi Ali?”

“Salama tu.”

“Mbona unajibu kwa hofu?”

“Hapana siyo hofu.  Kwani wewe ni nani mwenzangu?”

“Wewe!  Tuseme hujanitambua?  Mie ni Rehema.”

“Ahaa!  Tatizo hizi private number zenu zinatuchanganya.”  Hafsa aliposikia tu kuwa ni Rehema akasogeza sikio lake karibu kabisa na simu.  Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha anayapata mazungumzo yote.

“Vipi Rehema, mzima wewe?”

“Nipo gado best.  Nd’o nini kunisusa hivi?”

“Sijakususa hata kidogo.  Mambo fulani yalinitinga.”

“Sawa.  Nafahamu hilo.  Vipi Benito hajakutafuta tena?”  Aliposikia swali hilo, Ali alisita kidogo.  Akamtazama Hafsa.  Akaendelea. “Kidogo tu, wala usijali.”

“Sawa.  Nina ombi moja Ali.”

“Enhee, sema.”

“Alhamisi nitakuwa free.  Nakuomba tukutane siku hiyo mchana.”

“Ooh, sorry!  Kesho natarajia kusafiri Rehema.  Itanichukua almost two weeks.”

“Sawa.  Tutapanga siku nyingine.”

“Usijali.”

“Byee!”  Rehema akakata simu.

Hafsa alishabadilika. Ali akaimaizi hali hiyo lakini hakuwa na la kufanya.  Kama hajaona lolote vile, akamshika Hafsa kiunoni na kuanza kutembea taratibu kama ilivyokuwa desturi yao.  Hafsa hakuwa na furaha hata kidogo.  Akajilazimisha kutembea.  Walipofika chumbani Hafsa akaketi kwenye sofa.  Alikiinamisha chini kichwa chake. Ali akaendelea na kupanga panga vitu humo ndani akijifanya hana habari na linalomsibu Hafsa.

“Ali!”  Hafsa akaanzisha baada ya kuona Ali hana dalili za kumzingatia.

“Sema.”

“Hivi unanichukuliaje?”

“Kivipi?”

“Rehema ni nani yako?”

“Sikiliza Hafsa.  Unafahamu fika mie sipendi vitu vidogo vidogo kulazimishwa kuwa vikubwa.”

“Hivi ni vitu vidogo siyo?  Kama vidogo, jibu swali langu.”

“Anyway.  Inawezekana siyo vidogo.  Hebu nieleze nini tatizo lako?”

“Sikiliza Ali.  Nahitaji kufahamu ukweli.  Nini kipo kati yako na Rehema?  Tafadhali sihitaji unifiche kitu.”

“Wala sikutegemea kama ungefika mbali hivyo mpenzi wangu.  Kama umejisikia vibaya kwa simu aliyonipigia, pole sana mke wangu.  Wewe mwenyewe unafahamu Rehema ni nani.  Kumbuka siku ile yeye ndiye aliyenisaidia hata nikamkwepa Benito.”

“Ali, usiseme siku ile.  Sema siku zile.”

“Yah!  Ni kweli kanisaidia mara hizo mbili.”

“Tafadhali Ali.  Nakuomba unisikilize.  Na pia unielewe.  Kumbuka mimi ni mke wako.  Nahitaji sana kulindwa nawe kimwili na kihisia.  Hebu jaribu kufikiria mume wangu.  Nikiwa mkweli mbele ya Mungu, sipendi, sipendi, sipendi kabisa mawasiliano yako na Rehema.  Mawasiliano hayo yafe.  Unanielewa?”

“Nakuelewa vema.  Lakini sijajua ni kwa nini?”

“Nataka kuwa na amani moyoni.  Ni haki yangu kuwa na wivu juu yako.  Usinipe nafasi nianze kuwa na wasiwasi juu yako.  Hata kama wewe ndiye ungekuwa Hafsa ungelazimika kutafuta logic.”

“Kivipi?”

“Kumbuka wewe mwenyewe ndiye uliyenisimulia kuwa Rehema alishawahi kukusevu usiku ulipokutana na askari Mbeya.  Si ndiyo?”

“Ndiyo.”

“Pia akakusevu tena siku ile Benito alipokudhibiti mjini.  Japo uliniambia mlikutana by coincidence, nina mashaka nalo.  Bado kama haitoshi akakugharamia kila kitu siku hiyo utadhani wewe huna pesa.  Nikidhani yamekwisha, leo anakupigia simu kukuomba mkutane.  Inakuja kweli Ali?”

“Take it easy.”

“No Ali!  Kuna mambo ya kuyarahisisha.  Lakini siyo usalama wa ndoa.  Nakuhitaji uwe mkweli kwangu.  Niahidi kwamba utakaporudi hutomtafuta huyo Rehema.”

“Nakuahidi mke wangu.””

“Lakini ukumbuke kuwa wewe ndiye uliyenifundisha umuhimu wa kutovunja ahadi katika maisha.”

“Usijali.  Nitatunza ahadi.”

Hafsa akawa amerejewa na amani.   Akambusu mumewe shavuni.  Kwa asili, Hafsa ni mpole.  Lakini, mwenye wivu kupindukia juu ya mumewe.  Jambo lolote likitokea lenye kumhusisha Ali na jinsia nyingine lazima Hafsa atakasirika tu.  Ali amelifahamu hilo tangu kuanza kwa uhusiano wao.  Mara zote amekuwa akijitahidi kutomfanya mkewe akose raha. 

Siku hiyo ikaisha kama zilivyo siku zingine kwa wanandoa wapendanao.

Ali na Hafsa walikubaliana kuwa wakati Ali anakwenda safarini Hong Kong, Hafsa arudi Iringa akapumzike walau kwa muda mfupi ili kupunguza hizi rabsha ambazo pengine zingepunguza furaha katika ndoa yao.  Ukizingatia pia, Hafsa alikuwa mbioni kuanza likizo ya kumaliza muhula wa masomo shuleni kwake.

Asubuhi ya siku iliyofuata Hafsa akaenda shule kuomba ruhusa.  Alimwacha Ali nyumbani akifanya maandalizi ya safari kwani angeondoka mchana wa siku hiyo.  Hafsa akalazimika kumdanganya Mkuu wa Shule kuwa ana matatizo ya kifamilia yaliyotokea huko kwao Iringa yanayohitaji uwepo wake.  Mkuu wa Shule, mzee mmoja ambaye amefanikiwa kuufikisha umri uliokinakshi vema kichwa chake kwa mvi nyingi aliwachukulia walimu kama wanawe.  Kwa uzoefu wake kama mkuu wa shule mbalimbali za serikali tangu miaka ya mwanzo ya uhuru, Mzee Kyamani alifahamu vema nini maana ya matatizo ya kifamilia.  Aliyachukulia matatizo ya walimu na wanafunzi kwa uzito ulistahili.  Baada ya kuwa amestaafu utumishi wa umma, aliingia mkataba na mmiliki wa shule hiyo ili aweze kuendelea kuutumia vema ujuzi na uzoefu wake.  Hafsa alipewa ruhusa bila kikwazo.

Nyumbani, Ali aliendelea na maandalizi yake.  Wakati akimaliza kupanga nguo kwenye sanduku lake, simu yake ikaita.  Alipoiangalia, namba ya mpigaji ilikuwa imefichwa.  Lakini akaweza kukisia mpigaji.  Akaipokea.

“Mhuu!  Habari?”

“Safi tu.  Mambo?”  Sauti ya upande wa pili ilimtambulisha kuwa ni Rehema.

“Swadakta Rehema.”

“Unategemea kuondoka saa ngapi?”

“Saa sita kamili mchana.”

“Tunaweza kuonana kabla hujaondoka?”

“Hapana Rehema.  Itaniwia vigumu.  Kuna mambo kadhaa sijayakamilisha.”

“Japo dakika tano tu Ali.”

“Sidhani kama nitaweza.  Pilika za maandalizi zimenibana.”

“Ningependa sana kukuona Ali.”  Namna Rehema alivyokuwa akizungumza, walai nyoka angetoka pangoni.

“Usitie shaka Rehema.  Nitarudi, tutaonana.  Tutabonga hadi maneno yatuishe.” 

“Haya bwana maneno yako mie siyawezi.”

“Hakuna lolote katika maneno yangu.”

“Lolote lipo.  Unasema lolote?  Lipo sana.”

“Lipi tena?”

“Nakuzingua tu best.  Haya bwana, nikutakie safari njema.”

“Ahsante sana.  Nawe ubaki salama.”  

“Nani abaki salama?”  Ali akashituka kuisikia sauti hiyo.  Hafsa alisimama mlangoni.  

Ali hakuwa amemtegemea Hafsa.  Wala hakumsikia akiingia.  Akaishiwa pozi.  Hata hivyo, akajitahidi kumjibu.  “Kuna swahiba wangu tunafanya naye biashara.  Vipi shule umepewa ruhusa?”

“Nimepewa mpenzi.”  Hafsa akasema akitembea kuelekea kitandani.  Akaifuata simu ya Ali.  Akaibonyeza bonyeza bila kusema chochote. 

Ali akawa tuli akimtazama mkewe ilhali moyo wake ukienda  peapea.

Hafsa alipomalizana na simu akaenda jikoni kuandaa chakula.  Alishatambua Ali ametoka kuzungumza na Rehema.  Mara hii akaamua kubaki kimya ili asionekane mwenye kukurupukia mambo.  Lakini ndani ya moyo wake lilimchoma vilivyo.

Baada ya kumaliza kula, Ali akaondoka.  Hafsa alimpeleka hadi uwanja wa ndege.  Wakati akirudi, Hafsa alizongwa na simanzi tele akiufikiria upweke atakaokuwa nao hadi Ali atakaporudi.



MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog