Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

SUPASTAA

  

MTUNZI: NYEMO CHILONGANI 



Jina lake lake aliitwa Phillip Zachariah ila alijulikana zaidi kama Phiza. Huyu alikuwa mwanamuziki mkubwa aliyekuwa akitamba nchini Tanzania. Umaarufu wake ulimpatia fedha nyingi, akatembea na wanawake wengi huku akibadilisha magari kadri alivyotaka.

Kipindi cha nyuma, hakuwa tajiri kama watu walivyokuwa wakidhani, na yeye alikuwa masikini mkubwa ambaye alipigana kila siku mpaka kuwa na fedha kama alizokuwa nazo sasa.

Katika maisha yake, kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa wakila kupitia yeye, walikuwa wakibadilisha nguo na magari kupitia yeye. Phiza hakuwa mchoyo, kila alipofuatwa na mtu mwenye shida, alimsaidia pasipo kuangalia alikuwa nani.

Watanzania wengi wakatamani kuyajua maisha yake, wengi wakapiga simu katika Kituo cha Televisheni cha Global ili mtangazaji mahiri, Sofia Michael afanye mahojiano na mwanamuziki huyo na Watanzania wenye kiu ya kutaka kufahamu alipotoka mwanamuziki huyo wapate kufahamu.

Kumpata Phiza halikuwa jambo jepesi hata kidogo, kila siku alikuwa akipigiwa simu, jibu lake lilikuwa moja kwamba hakuwa jijini Dar es Salaam. Kama ulikuwa haujamzoea, ungeweza kusema kwamba alikuwa akiringa lakini kile alichokuwa akikizungumza ndicho kilikuwa ukweli wenyewe.

Hakuwa mtu wa kutulia, leo alikwenda Shinyanga, kesho alikwenda Kigoma na mtondogoo alikwenda Kilimanjaro, maisha ya kuzunguka huku na kule ndiyo yalikuwa maisha aliyokuwa akiishi.

Baada ya miezi minne kupita, mtangazaji Sofia akafanikiwa kumpata Phiza, aliamua kwenda kumpokea mwenyewe uwanja wa ndege alipokuwa akitoka Marekani, huko, akamuomba sana aonane naye kesho katika jumba kubwa la kituo cha Televisheni cha Global, Phiza akakubali.

Siku iliyofuata, gari lenye thamani ya shilingi milioni 200 lilikuwa likipaki katika eneo la jengo hilo na kisha mwanamuziki mwenye sura nzuri kuteremka na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo hilo.

Baadhi ya watu waliokuwa mahali hapo, wakaanza kumpiga picha kwa simu yao huku wengine wakiomba kupiga naye picha, bila kinyongo na bila maringo, akakubali kupiga nao picha.

SOFIA: Umependeza sana

PHIZA: Asante, hata wewe umependeza pia. Niambie, what’s next.

SOFIA: Twende ndani.

Wakaanza kuondoka nje ya jengo hilo na kuingia ndani. Ilikuwa studio nzuri lakini kwa Phiza ambaye alikuwa ametembelea studio nyingi Afrika Kusini, Malawi na nchi nyingine, ile ilionekana kuwa ya kawaida.

SOFIA: Ninataka kuanza kipindi, upo tayari?

PHIZA: Kama kawa. Vipi kuhusu mapoda?

SOFIA: Usijali, kuna dada atakufanyia yote hayo.

Wala haukupita muda mwingi, dada mmoja, mrembo mwenye asili ya kiarabu akamfuata na kuanza kumfanyia ‘make up’ kabla ya kuanza kipindi, alipomaliza, akaruhusiwa na kukaa sehemu husika, kamera zilikuwa mbele ila hazikuwa zimewashwa.

SOFIA: Upo tayari?

PHIZA: Yaap yaap....kwa hiyo nizungumzie nini sasa?

SOFIA: Historia ya maisha yako, ila utakuwa ukijibu maswali yangu.

PHIZA: Hakuna noma.

SOFIA: Twende hewani.

Hapohapo kamera zikawashwa. Watanzania wengi walikuwa mbele ya televisheni zao, kila mmoja alikuwa na shauku ya kutaka kufahamu historia ya maisha ya Phiza, kule alipotoka mpaka kuingia katika ulimwengu wa kuogelea fedha.

Maisha yake yalikuwa siri lakini siku hiyo, mbele ya kamera, alikuwa tayari kuzungumzia kila kitu kilichotokea katika maisha yake, likiwepo suala la kuupata umaarufu kupitia muziki wake.

SOFIA: Karibuni sana watazamaji wetu wa Kipindi cha Keeping Up With Sofia ambacho kinaletwa na Kituo chako Bora cha Global. Leo, kama ilivyo kawaida yetu tunakuletea msanii anayetamba sana kwa sasa nchini Tanzania, huyu si mwingine bali ni Phillip Zachariah au kwa jina jingine la a.k.a hujulikana kama Phiza.

PHIZA: (Anatoa tabasamu pana)

SOFIA: Karibu sana Phiza.

PHIZA: Asante sana.

SOPHIA: Kwanza ningependa ujitambulishe kwa watazamaji kabla haujaanza kusimulia kile kilichotokea katika maisha yako.

Phiza akaanza kujitambulisha kwa ujumla, japokuwa watu wengi walikuwa wakimfahamu lakini kwake haikuwa tatizo, alipomaliza, akamgeukia Sofia.

SOFIA: Asante. Sasa uwanja wako.

PHIZA: Koh koh koh (alianza kwa kukohoa) Ukiniangalia kwa sasa hivi na kisha mtu akatokea na kukwambia kwamba nilikuwa masikini kama asilimia kubwa ya Watanzania walivyo, nahisi utakataa. Kitakachokufanya kukataa ni kwa sababu unaiona gari yangu aina ya Range SV ya milioni 200, unaziona nyumba zangu za kifahari, unaiona ndege yangu na kusikia kiasi cha fedha nilichokuwa nacho benki.

Sofia, nilikuwa masikini kama wengine, sikuzaliwa na fedha na hata wazazi wangu hawakuwa na fedha. Nilimsikia mara kwa mara mama akiniambia kwamba siku ambayo alinizaa hospitalini, hawakuwa na fedha, gharama zote ambazo walitakiwa kulipia hospitalini, zililipwa na majirani zangu, mzee Mkude, bi Amina na mzee mmoja ambaye kwa sasa ni marehemu, mzee Issa Madevu.

SOFIA: Kwa hiyo ulizaliwa katika familia masikini sana?

PHIZA: Naweza kusema hivyo. Mara baada ya kuzaliwa, mama alikaa hospitalini kwa siku mbili na ndipo akaruhusiwa kutoka na kurudi nyumbani. Kipindi hicho walikuwa wakiishi Tandale na nilizaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

Of course kulikuwa na daladala, lakini hawakuwa hata na senti tano, huku mama akiwa mgonjwa-mgonjwa, wakaanza kutembea kwa miguu kurudi nyumbani huku baba akiwa amenibeba (ananyamaza, anafumba macho na kuyafumbua tena, machozi yanaanza kujikusanya machoni mwake, anaendelea...)

Mama alizidi kuniambia kwamba nyumbani hakukuwa na kitu, siku hiyo ambayo walirudi nyumbani, hakukuwa na chakula, walikaa tu ndani huku nikilia mno, nilionekana kuwa msumbufu lakini ndiyo tayari nishakuwa mtoto wao, wangefanya nini sasa? Wakaamua kunionyeshea mapenzi ya dhati.

Baada ya kukaa kwa takribani masaa mawili, majirani wale waliokuwa wamejichangisha fedha kulipia gharama wakafika nyumbani hapo na kuwapa hongera wazazi wangu na kisha kuwaachia kiasi cha fedha kwa ajili ya matumizi.

SOFIA: Ikawaje?

PHIZA: Siku hizo zilikuwa ni za mateso makubwa, nilikuwa msumbufu sana kwa kulia, mama alikuwa akininyonyesha japokuwa kuna siku alikuwa zilikuwa zikipita bila kula kitu chochote kile.

Baada ya miezi sita, baba akaanzisha biashara ya kuuza samaki. Alikuwa akiwatoa samaki kule Feri na kuwaleta Tandale ambapo alikuwa akiwauza. Kidogo akaanza kupata fedha za kubadilishia chakula.

SOFIA: Kwa hiyo kipindi hicho mlikuwa kwenye nyumba ya kupanga?

PHIZA: Ndiyo. Familia yetu ilikuwa masikini sana. Unajua unaweza kusema masikini halafu mtu mwingine akachukulia poa, ninaposema masikini, elewa kwamba ni masikini kupitiliza.

Kabiashara hako kakaendelea. Ndiyo iliyokuwa ikiingiza fedha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Kuna watoto wa majirani walikuwa wakivalishwa pempas lakini amini usiamini, sikuwa kuvalishwa vazi hilo, kitu pekee nilichokuwa nikivalishwa ni kanga na nailoni, nilipokuwa najisaidia, mama aliitoa kanga ile ambayo ilikuwa kama tambala na kisha kuifua, ilipokauka, akanivalisha tena, hayo ndiyo yalikuwa maisha yetu.

SOFIA: Biashara ya baba yako iliendeleaje?

PHIZA: (Haongei kitu kwanza, ananyamaza kwa muda na kumwangalia Sofia, anayafumba tena macho yake na kuyafumbua, machozi yanaanza kumbubujika) Baba alifilisika. Sijui ilikuwaje. Mama aliniambia kwamba alifilisika kwa kuwa fedha zilitumika zaidi kwangu kuliko kuziendesha biashara tuliyokuwa nayo.

SOFIA: Ikawaje baada ya hapo?

PHIZA: Baba akaanza kukaa nyumbani. Alichokifanya ni kujifundisha ujenzi. Alikuwa na rafiki yake mmoja, jina lake silikumbuki na ndiye alikuwa mtu pekee ambaye alimsaidia baba katika kumtafutia kazi ya ujenzi sehemu mbalimbali.

Bado maisha yalikuwa ni ya shida mno, umasikini ulitutafuna sana. Leo unaponiona naendesha gari la kifahari, wazazi wangu wanakula maisha, acha tu wale. Maisha tuliyopitia ni ya dhiki mno, ninawapenda sana wazazi wangu na ndiyo maana my Ex Bertha aliponitukania wazazi wangu miezi kadhaa iliyopita nikataka kumpiga risasi. Walinihangaikia mpaka kufika hapa, leo sitaki waguswe wala kudharauliwa.

SOFIA: Ikawaje baada ya hapo?

PHIZA: Baba aliendelea na kazi ya ujenzi kwa miaka kadhaa. Baada ya miaka saba, nikaanza darasa la kwanza, hiyo ilikuwa mwaka 1994.

SOFIA: Kwa hiyo hukusoma chekechea?

PHIZA: Sikusoma kwa sababu bado gharama ilikuwa kubwa, walichoona kufaa ni kunipeleka darasa la kwanza. Kiukweli sikuwahi kushika nafasi za juu, naweza kusema kwamba sikuwa na akili darasani. Kila mtihani nilitoka wa mwisho, kidogo nilipoingia darasa la nne, nikafanikiwa kufaulu mtihani wa taifa na kuingia darasa la tano.

SOFIA: Maisha ya nyumbani yalikuwaje wakati huo?

PHIZA: Umasikini haukumalizika, bado uliendelea kututafuta. Sikuwahi kupewa fedha ya matumizi kwenda nayo shuleni, katika maisha yangu ya shule sikuwahi kupanda daladala, ile shilingi mia mbili ambayo nilitakiwa kupewa, mama alikuwa akininunulia vitafunio kila niliporudi nyumbani na kunywa chai.

SOFIA: Ilikuwaje huko shuleni?

PHIZA; Nilipata marafiki wengi sana, rafiki mmojawapo alikuwa huyu Stellah Kimario.

SOFIA: Huyu Stellah Miss Tanzania?

PHIZA: Ndiyo huyohuyo.

SOFIA: Kwanza nilisikia kwamba ulikuwa ukitoka naye kimapenzi, ni kweli?

PHIZA: (anamwangalia Sofia na kuanza kutoa kicheko cha chini) Wakati mwingine ni fununu tu, unaweza kuziamini fununu au kuachana nazo. Ila nilimchukulia Stellah kama rafiki yangu mkubwa,

SOFIA: Tuendelee, ilikuwaje?

PHIZA: Kati ya wanafunzi ambao wazazi wao walikuwa na uwezo, basi naweza kusema kwamba Stellah alikuwa wa kwanza. Nilimuogopa sana kwa kuwa alitoka familia bora, cha kushangaza, huyu Stellah akaja kuwa karibu na mimi mno. Kumbuka hapo tupo darasa la tano. Kila alichokuwa akinunua, alinipatia na mimi. Sikuwahi kupewa hela ya matumizi lakini huwezi amini, Stellah alinifanya kushiba shuleni.

Wakati huyo masikini mimi nilikuwa na sare moja tu ya shule, bukta imechanika matakoni na kuweka kiraka huku shati likiwa limechanika maeneo ya makwapani, sikujali japokuwa nilijisikia sana aibu.

SOFIA: Stellah hakuiona hali hiyo?

PHIZA: Aliiona lakini angefanya nini? Alitamani kunisaidia lakini nahisi ilikuwa ngumu kufanya hivyo. Ninajivunia Stellah, alikuwa akipenda kuwa mwanamitindo toka zamani. Mara kibao alipokuwa akibaki darasani peke yake, alikuwa akiniita na kuniambia nimwangalie jinsi alivyokuwa akitembea kwa maringo huku mkono wake mmoja ukiwa kiunoni. Alipendeza sana na nilivutiwa naye mno, ila kumwambia kwamba nampenda, lilikuwa suala gumu sana.

SOFIA: Kwa hiyo hukuwahi kumwambia ukweli?

PHIZA: Hahaha! Mbona unakuwa na presha Sofia? Subiri.

SOFIA: Sawa, nakuwa mpole, tiririka mwanaume.

PHIZA: Daah! Stellah!




PHIZA: Huu uzuri alionao Stellah, ulikuwa hivyohivyo toka kipindi cha nyuma. Unajua Sofia umasikini ni mbaya sana, unapokuwa nayo, automatic moyo wako unakosa kujiamini, unapowaona wanawake wazuri, moyo wako unakwambia kwamba huyo si msichana anayetakiwa kuwa nawe kwa kuwa huna kitu, ndivyo ilivyotokea kwangu na Stellah.

Nilijua fika kwamba Stellah alikuwa akinipenda, lakini ningefanya nini masikini mimi, nikaamua kubaki kimya tu. Kila siku Stellah alikuwa akiniita na kunitaka nimwangalie katika kipindi alichokuwa akifanya mazoezi ya kuwa mwanamitindo.

SOFIA: Ilichukua muda gani mpaka kumwambia ukweli?

PHIZA: Kipindi kirefu, tulizoeana sana na tulipofika darasa la saba, hapo ndipo nilipoamua kumwambia ukweli. Siku hiyo nilijiandaa vilivyo, nilifua nguo zangu vilivyo, nilikuwa nimenyoa na kesho yake safari ya shuleni ilianza.

Stellah aliutesa sana moyo wangu. Najua kwa sasa ananisikiliza kwa kuwa nilimpigia simu na kumuuliza kama ingekuwa sahihi mimi kulizungumzia suala hilo kwenye televisheni na alinikubalia. Stellah, wewe ni msichana wa tofauti sana kwangu, nilikupenda sana na siwezi kujizuia, bado moyo wangu unakupenda mno.

SOFIA: Ikawaje baada ya kujiandaa sana kwa kunyuka pamba zilizopigwa pasi?

PHIZA: Hahaha! Acha tu. Nilipofika shule, hakuwa amefika hivyo nikamsubiria huku moyo wangu ukiwa na presha kubwa. Siku hiyo, mara kwa mara nilikuwa nikijitazama kama nilikuwa nimependeza au la.

Japokuwa nilikuwa masikini sana lakini kwa siku hiyo nilikuwa tofauti sana. Baada ya dakika kadhaa, Stellah akafika shuleni hapo. Sikufichi, siku hiyo alionekana kuwa tofauti kabisa na siku nyingine, alikuwa mrembo hasa, aliponiona tu, akaanza kunisogelea huku akiachia tabasamu pana.

Akanisalimia, muda wote mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakidunda sana kana kwamba moyo ulitaka kuchomoka.

SOFIA: Hahaha! Hukumkumbatia?

PHEZA: Weeee! Ningeanzaje? Mwili ulikuwa ukinitetemeka mno. Kuna kipindi aligundua hilo na kila alipotaka kuuliza, nilikuwa nikimpa maongezi mengi mfululizo ili mradi tu asiongee kitu chochote kile.

Baada ya mapumziko, nikaomba kuonana naye in private, akanikubaliana na hivyo kukaa naye sehemu moja.

SOFIA: Ulimwambia?

PHIZA: Nilimwambia.

SOFIA: Akasemaje?

PHIZA: Alishtuka sana, akaniangalia mara mbilimbili, akajifanya kutokuamini kile nilichomwambia. Yaani ishara zangu zote nilizokuwa zimemuonyeshea, leo hii alikuwa akijifanya kushangaa.

SOFIA: Akasemaje? Yes au No?

PHIZA: Daaa! Huwezi kuamini, Stellah alikasirika sana. Kuanzia siku hiyo, akakata mawasiliano nami tena alinitishia kwamba angekwenda kumwambia mwalimu wetu wa darasa. Kiukweli nilinyong’onyea sana.

Kuanzia siku hiyo, nikajiona kuwa kama panya na Stellah kuwa paka. Kila nilipomuona, nilijificha na nilipokuwa nikimuona akiongea na marafiki zake, hata kama walikuwa wakipiga stori nyingine nilihisi kama wananizungumzia mimi.

SOFIA: Hahaha! Ikawaje sasa mtu mzima? Manake sikupatii picha kipindi hicho, ukawa mdogo kama priton vile.

PHIZA: We acha tu, yaani tena bora ya priton, nilijiona mdogo kama mchanga wa baharini.

SOFIA: Kwa hiyo huo ndiyo ukawa mwisho?

PHIZA: Kitu kilichokuwa kikinishangaza ni kimoja tu. Stellah alikuwa amenikasirikia sana lakini alikuwa akiongoza kwa kuniangalia darasani. Unajua kwa sisi vijana wa zamani hasa miaka ya 90 ukiona msichana anakuangalia sana, unahisi kwamba anakupenda, tofauti na mwaka huu wa 2016.

Nakumbuka siku ya mwisho kabla ya kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba, Sofia akaniandikia Wimbo wa Nitamwambia ulioimbwa na The Ruler, nadhani unamkumbuka.

SOFIA: Yeah!

PHIZA: Alijua kwamba niliupenda sana wimbo huo na ndiyo maana mashairi yote alikuwa ameniandikia huku akisisitiza kwamba alikuwa akinipenda ila hali ya kunikataa ilikuwa imetokea tu.

Sikufichi Sofia, nilifurahi mno, nilishindwa kujizuia, usiku wa siku hiyo nikaondoka nyumbani kuelekea kwao Tabata kwa miguu. Nilipofika huko, nikaenda kwenye kibanda cha simu na kuomba kupiga simu, nikampigia na kutoka nje.

SOFIA: Hahaha! Kweli ulipenda. Kutoka Tandale mpaka Tabata kwa miguu tena usiku?

PHIZA: Ndiyo hivyo. Nilipofika nikaonana naye na kupiga naye stori. Kwa mara ya kwanza siku hiyo ndiyo nikabadilishana mate na msichana, japokuwa kipindi cha nyuma niliwaona watu wanaofanya hivyo kwamba ni wachafu, lakini kwangu nilijisikia poa kabisa.

SOFIA: Na hali ya nyumbani ilikuwaje kipindi hicho?

PHIZA: Unafikiri basi kulikuwa na mabadiliko, hakuna, bado maisha yalikuwa yaleyale tu. Baada ya hapo tukafanya mitihani, Stellah akafaulu na mimi kufeli. Yeye akajiunga na Jangwani Sekondari, ile shule ya Wasichana na mimi kuingia maisha ya mitaani.

Hapo ndipo nilipoanza kufikiria kwamba nilitakiwa kufanya kitu kingine cha ziada. Hapo nilikuwa na miaka kumi na tano. Nikaanza ishu ya kuuza ice cream nyumbani kwa mzee mmoja ambaye ni marehemu, huyo mzee Madevu aliyewasaidia wazazi wangu fedha za hospitalini.

Nilifanya biashara ile kwa kipindi cha mwaka mzima, biashara ilikuwa ngumu sana. Kuna wakati mwingine nilikuwa nikikutana na majanga kama kupigwa na kunyang’anywa deli la ice cream, wakati mwingine matusi kutoka kwa wanafunzi kwamba sikutakiwa kufanya biashara ile.

Nilipofikisha miaka kumi na sita, mwaka 1999 , nikaanza kujichanganya na makundi ya mitaani. Hayakuwa makundi makundi mazuri. Nakumbuka kipindi hicho kwa Tandale, kulikuwa na camp moja tu ambayo ilikuwa nzuri na ambayo vijana wake hawakuwa wahuni, hii iliitwa Mafyoso Camp, ila hizo nyingine ikiwepo ile ambayo nilijiunga nayo iitwayo Mazaga, ilikuwa ni ya kihuni sana.

Unavyoniona hapa, nimekwishawahi kuvuta sigara, bangi, nilishawahi kubwia unga na uchafu mwingine mwingi tu, hata kubaka nilikwishawahi kubaka ila namshukuru Mungu sikuathirika.

SOFIA: Pole sana. Ikawaje baadae? Haukumtafuta Stellah?

PHIZA: Kwanza nashukuru Mungu katika kipindi hicho sikuonana na Stellah kwani angenishangaa sana kwani nilikuwa mhuni mkubwa tu.

Mwaka 2003 ambapo The Ruler anatoa Wimbo wa Nitakutafuta Tu, ndipo nikakumbuka kwamba kulikuwa na mtu ambaye nilitakiwa kumtafuta, huyu alikuwa Stellah. Sikujua ningempata wapi kwani hata nilipojaribu kwenda kwao, mlinzi wa getini hakutaka kuniruhusu kuingia kwani aliniona mhuni sana, akanifukuza.

SOFIA: Pole sana, ikawaje baada ya hapo.

PHIZA: Nakumbuka baada ya kufukuzwa na mlinzi, nikaondoka zangu huku nikiwa nimejiinamia. Nilipofika pale Mwananchi, nikamuona msichana ambaye hakuwa mgeni machoni mwangu, alikuwa amesimama nje ya gari fulani hivi akiwa na mwanaume, nilipomwangalia vizuri, nikagundua kwamba alikuwa Stellah, alipendeza mno.

Huku nikiwa na kipensi changu, kaoshi kwa juu na huku nikitembea kwa kudunda, nikamsogelea Stellah, aliponiona, hakunijua, nilikuwa tofauti sana, sura yangu ilikuwa imekwishaharibiwa mno.

Nilipomfikia, nikamuita. Akashtuka, akaniangalia kwa makini huku akivuta kumbukumbu kwamba alikwishawahi kuniona sehemu lakini bahati mbaya hakukumbuka. Nilipoendelea kumsogelea, yule jamaa aliyekuwa naye ambaye alionekana kuwa smart sana akanizuia, hakutaka niendelee kumsogelea.

Nilijaribu kumuita tena Stellah lakini hakuonekana kujali kwa kuwa hakunitambua.

SOFIA: Kwa hiyo hata hukujitambulisha?

PHIZAL Huo ndiyo ujinga nilioufanya. Niling’ang’ania kumuita lakini sikujitambulisha, akaingia ndani ya gari na kuondoka zao.

SOFIA: Ulijisikiaje moyoni?

PHIZA: Kuna maumivu ambayo unaweza kuyaelezea lakini kuna mengi ambayo kamwe huwezi kuyaelezea. Ni afadhali angekuja mtu mmoja na kunichanachana na wembe ningesikia nafuu lakini si vile ambavyo Stellah alikuwa amenifanyia. Niliumia mno.

Hebu jifikirie, kwa ajili ya mapenzi, nilitoka Tandale mpaka Tabata tena kwa mguu, n imefika kule, nikafukuzwa na mlinzi, niliporudi, nakutana na mtu niliyemfauata halafu haonekani kunijali, ungejisikiaje? Hivyo ndivyo nilivyojisikia.

SOFIA: Ikawaje hapo baadae?

PHIZA: Nilirudi nyumbani huku nikiwa na majonzi, nilichokuwa nimekigundua ni kwamba vilevi ndivyo vilivyokuwa vimeniharibu, hivyo nilitakiwa kuachana navyo. Kitu cha kwanza nilichokifanya ni kuachana na camp mbaya na kuhamia Mafyoso Camp. Haikuwa kazi rahisi, kwa kuwa hawakuwa wahuni, nilipowasogelea, walinitenga sana ila baadae wakanizoea na kuanza kuwa nao, nikaachana na madawa na hivyo kuwa kijana mzuri.

Mwaka mmoja baadae, nikagundua kwamba nilikuwa na kipaji cha kuimba hivyo nilitakiwa kuwa msanii kama wengine. Nilichoshauriwa ni kumtafuta The Ruler. Kiukweli nilipafahamu alipokuwa akiishi zamani kabla hajawa staa, hivyo nilitakiwa kumfuata.

Hiyo ilikuwa mwaka 2004, nikafanikiwa kwenda alipokuwa akiishi, ilikuwa maeneo ya Sinza Mori, nilipofika kule, sikuweza kumpata. Mwaka mzima nikawa namtafuta yeye lakini bado sikufanikiwa kumpata kwa ajili ya kumshirikisha wimbo wangu.

SOFIA: Vipi kuhusu Stellah?

PHIZA: Kiukweli sikupata mawasiliano naye tena, niliamua kuwa kivyanguvyangu tu. Nilihangaika sana kutunga nyimbo nzuri lakini sikupata fedha za kurekodia, hivyo niliendelea kusota mtaani huku nikiishi maisha ya kugongea, leo nakula hapa, kesho nakula kule.

Ilipofika mwaka 2006, huwezi amini, nilikakutana na Stellah kwa mara nyingine tena, mara hii ilikuwa ni katika duka moja hivi kule Sinza, lilikuwa duka la kukodisha mashela ya harusi. Nilikwenda hapo kwa kuwa mmiliki aliniambia kwamba niende ili anisaidie japo kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kurekodi nyimbo zangu.

SOFIA: Ulipomuona Stellah ilikuwaje? Alikuwa peke yake?

PHIZA: Kwanza nilifurahi sana, aliponiangalia usoni, akaonekana kunikumbuka. Sikuwa mhuni kama kipindi kile, nilikuwa mtanashati japokuwa sikuwa nimevaa nguo za gharama. Hakuwa peke yake, alikuwa na yule jamaa niliyemkuta naye siku ile, yule mchizi smart.

SOFIA: Nini kilitokea?

PHIZA: Hahahaha! Otea!

SOFIA: Alikukumbatia kwa furaha?

PHIZA: Hapana.

SOFIA: Sasa kilitokea nini?

PHIZA: Ngumi. Ugomvi ambao hakukuwa na mtu aliyeweza kuuzima.





PHIZA: Kwanza yule jamaa alikuwa akiniangalia kwa macho ya chuki, alionekana kunikumbuka kwamba mimi ndiye nilikuwa yule msela wa kipindi kile nilichomfuata Stellah nje ya gari huku nikiwa muhuni, nilimuita lakini aliamua kuondoka.

Kwa jinsi jamaa alivyokuwa akinicheki, ilionekana wazi kwamba ni lazima ningepokea kichapo mahali hapo. Alipoona Stellah amenifuata na kunikumbatia, alisaga meno yake kwa hasira. Hakuendelea kuwa kwenye hali hiyo, alishindwa kabisa kuvumilia, akanifuata na kuanza kunipiga mikwara.

SOFIA: Ikawaje hapo kwa mtoto wa Tandale kupigwa mikwara.

PHIZA: Unajua nilibadilika. Kipindi cha nyuma nilikuwa mhuni sana lakini katika kipindi hicho nilibadilika. Nilijua fika kwamba endapo ningeanzisha mtiti wangu jamaa angeshindwa kabisa kuuzima na sidhani kama kungekuwa na mtu ambaye angeuzima, nikajifanya kutulia tu.

Jamaa alinisukumasukuma huku na kule na hata kunikunja shati langu. Akaichomoa tai yangu na hata ule usmart wa kuchomekea ukatoka. Jamaa wa duka lile alikuwa pembeni, kwanza yeye mwenyewe alishangaa ni kwa sababu gani mshikaji alikuwa akinifanyia vile, eti kisa demu jamaa alikuwa akinizingua kihivyo.

Jamaa alipoona nimekuwa mpole huku Stellah akimuomba anikaushie, mshikaji akazidi kujiona yeye tembo, akaendelea kunikunjakunja kiasi kwamba kikafika kipindi nikaanza kummaindi.

SOFIA: Ikawaje?

PHIZA: Nikaona kama ningeendelea kujifanya mnyonge mshikaji angenipanda kichwani, na mimi nikaanza kumletea timbwili. Ilikuwa ni kizaazaa mtu wangu. Jamaa alikuwa akinikunjakunja tu lakini mi sikufanya hivyo, kitu cha kwanza nikampiga apakati.

SOFIA: Apakati ndiyo nini?

PHIZA: Hiyo ni aina ya ngumi unayopigwa ubavuni. Nilipompiga apakati ya kulia na kumalizia ya kushoto, mshikaji akakaa chini na kuanza kuugulia maumivu.

Wanawake waliokuwa mahali hapo ambao walikuja kununua mashela walikuwa wakishadadia kwamba nilichokifanya kilikuwa sahihi kabisa kwani jamaa ndiye alikuwa chanzo.

Unajua mapenzi mapenzi tu. Huwezi amini Stellah alikuwa upande wangu. Aliishia kububujikwa na machozi huku akinikumbatia. Kuna kitu nilianza kukiamini, unajua unaweza kuwa na mtu ambaye unahisi kwamba unampenda lakini ukweli wa moyo wako ni kwamba mapenzi ya dhati yapo kwa mtu mwingine kabisa.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Stellah, ni sawa alikuwa na msela lakini kwangu alionekana kuwa tofauti sana, alionekana kunipenda mno mpaka nikashangaa.

SOFIA: Ikawaje baada ya mshikaji kuugulia maumivu.

PHIZA: Unafikiri msela alirudia, ngumi nzito nilizompa zikamfumbua macho kwamba sikuwa mtu wa mchezo hata mara moja, hata aliposimama, hakutaka kubaki hapo, akatoka zake, akaingia ndani ya gari na kusepa.

SOFIA: Kwa hiyo hakuondoka na Stellah?

PHIZA: Hakuondoka naye, alimuacha, nikawa sina jinsi, nikajichukulia mtoto kiulainiiii, kama nanawa vile.

SOFIA: Hahaha! Na vipi siku hiyo, jamaa mwenye duka alikusaidia?

PHIZA: Hakuna. Nilikwishakinukisha hapo na kumfukuzia mteja wake, unafikiri angenisikiliza tena! Alinimaindi kinoma, akanitimua, nikaondoka na Stellah wangu.

SOFIA: Mlikwenda wapi?

PHIZA: Stellah alinichukua na kuelekea kwenye mghahawa fulani hivi upo hapo Afrika-Sana, tukakaa na kuanza kula. Aliniuliza maswali mengi mno, nilimsimulia mpaka kipindi kile nilichomfuata huku nikiwa msela, alishangaa sana, hakuamini kama nilikuwa mimi.

Ndiyo hivyo, tuliendelea kupiga stori na aliniuliza nilifuata nini kwenye duka lile, nikamwambia kwamba nilihitaji fedha na jamaa alikuwa ameahidi kunisaidia ila baada ya ugomvi, msela akanitosa.

Alichokifanya, akanitaka tuondoke mahali hapo. Tukaelekea mpaka pale Kijiweni, akateremka kutoka kwenye bajaji na kuelekea katika mashine ya ATM, akatoa kiasi cha shilingi milioni moja, akanikabidhi.

SOFIA: Mmmh! Ulijisikiaje?

PHIZA: Siwezi kuielezea furaha niliyoisikia kipindi hicho. Nakiri kwamba Stellah amenifanikisha kufikia mahali hapa, kwani kiasi kile cha fedha nilichokipata nikakitumia katika kurekodi wimbo wangu wa kwanza unaoitwa Malaika, nafikiri unaukumbuka.

SOFIA: Naukumbuka sana. Si ndiyo uliokutoa!

PHIZA: Yeah!

SOFIA: Ulijisikiaje kuingia studio kwa mara ya kwanza?

PHIZA: Acha aiseee....nilijisikia furaha isiyo kawaida. Nakumbuka siku hiyo nilikwenda na Stellah mpaka studio, ilikuwa ni furaha kubwa, kila nilipokuwa nikiiangalia studio ile nilijisemea kwamba huo ndiyo utakuwa mwanzo wa ndoto zangu za kuwa mwanamuziki mkubwa hapo baadae.

Hata nilipoanza kuimba, nilijisikia kufarijika. Katika kila mistari niliyoiimba ndani ya chumba kile, nilikuwa nikimwangalia Stellah tu, bado alikuwa msichana mrembo sana ambaye sidhani kama niliwahi kukutana naye kabla.

Nilitumia zaidi ya masaa kumi studio, baadae nikaondoka, ilikuwa kama saa kumi na mbili jioni hivi. Kuna kipindi nilikuwa nikimwangalia Stellah, sikufichi, kama mtu unampenda, anapokuwa na kitu moyoni ambacho hakimpi furaha, utagundua tu. Ndivyo ilivyokuwa kwa Stellah.

SOFIA: Ulimuuliza?

PHIZA: Ndiyo. Nilitaka kujua tatizo nini.

SOFIA: Akasemaje?

PHIZA: Alikuwa na kitu ambacho hakutaka kuniambia. Alitakiwa kusafiri kuelekea nchini Marekani, alikuwa amebakisha siku tatu tu za kuishi nchini Tanzania. Unajua ngoja nikwambie kitu Sofia. Nilihitaji kuwa karibu na Stellah kwa kipindi kirefu sana, nilikuwa nimekwishamzoea. Tulipomaliza darasa la saba, nilikuwa nimempoteza hivyo sikutaka kumpoteza tena, nilitaka niendelee kuwa naye siku zote za maisha yangu.

Ila ikawa haina jinsi, siku ilipofika, akasepa zake na kuelekea Marekani kusoma, aliniambia kwamba angechukua miaka minne ya masomo.

SOFIA: Maisha yalikuwaje bila Stellah?

PHIZA: Yalikuwa ni magumu, muziki bila msichana ilikuwa ni mateso. Japokuwa niliishia darasa la saba lakini nakumbuka kuna mstari kwenye wimbo fulani wa Timberland aliomshirikisha Drake uitwao Say Something ambapo kuna mstari Drake alisema ‘What's a star when its most important fan is missing?’ yaani akimaanisha kuna umuhimu gani wa kuwa staa na wakati shabiki muhimu amekosekana?

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu, yaani hata Stellah alipoondoka na kuelekea Marekani, nilikuwa mnyonge, wakati mwingine nilikuwa nikibaki chumbani na kuanza kujiuliza kwa nini aliondoka katika kipindi muhimu kama hicho.

SOFIA: Kuna changamoto gani ulizipata?

PHIZA: Hapo ndipo kulipokuwa na kazi Sofia. Nilikuwa nimetoa Wimbo wa Malaika lakini kuwafanya watu wausikilize ilikuwa shughuli sana. Katika redio nyingi nilipokuwa nikiwapelekea wimbo wangu kwa ajili ya kuupiga walinitaka nilipie kiasi fulani cha fedha, hakika kwangu ilikuwa ngumu sana kwa kuwa sikuwa na fedha.

Nilipata tabu sana mpaka kufikia kipindi nilipokuwa nikiona kuna kijisherehe uswahilini Tandale, nilikuwa nikienda na kuwaomba niimbe, tena bure kabisa, walikuwa wakinikubalia ila mwisho waliamua kunipoza elfu kumi.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu. Wimbo wangu ulikubalika sana lakini haukuwa ukisikika redioni hivyo hakukuwa na raia wengi waliokuwa wakiusikia.

SOFIA: Ila ndiyo wimbo ambao ulikutoa na kupigwa sana redioni kuliko nyimbo za wasanii wote, ilikuwajekuwaje hapa?

PHIZA: Elimu ni kitu bora sana. Unajua hata ukiwa tajiri bila kuwa na elimu, kuna vitu unakosa. Kuna siku nilikuwa nimechili tu kwenye Camp yetu ya watoto wastaarabu ya Mafyoso Camp, kuna msela alikuja, alikuwa na demu wake fulani hivi, demu fulani mkali sana...hahaha! Ila hajamshinda Stellah.

Alipokuwa akipita, akaniona, akanifuata na kuanza kunipa darasa la ujasiriamali. Sikuwa nikimfahamu na sidhani kama alikuwa akinifahamu lakini aling’ang’ania sana kunipa darasa hilo. Kiukweli nilimuona msela akinizingua sana, alipomaliza somo lake huku nikiwa sijaingiza kitu chochote kile zaidi ya kuona akinipigia kelele, akaniuliza kama nilikuwa na biashara, nikamwambia sina.

Jamaa akasikitika weee, mwisho wa siku akasema nilikuwa na kipi cha kufanya, nikamwambia muziki ila wimbo wangu wangu haukuwa ukipigwa redioni. Msela akanipa idea fulani ambayo sikuwa nimeifikiria kabisa, akanitaka niuchukue wimbo wangu na kuwapelekea watu wa bodaboda na bajaji wawe wanaupiga kila siku.

SOFIA: Duuh! Kumbe umepitia mbali,

PHIZA: Wee acha tu. Nikaanza kuusambaza wimbo huo, ilikuwa kazi lakini namshukuru Mungu kwani masela waliupokea na kuanza kuupiga. Niliusambaza sehemu mbalimbali ikiwepo Tandale, Mwananyamala, Kijitonyama, Manzese na sehemu zote, huko kote wana wakawa wanaupiga.

Huwezi amini Sofia, baada ya mwezi mmoja tu wimbo wangu kupigwa na waendesha bodaboda na bajaji, nilipigiwa simu kutoka kituo fulani cha redio kwa ajili ya interview, nikaenda na hapo ndipo nilipoanza kuupata usupastaa.

Baada ya hiyo interview na wimbo kupigwa, nikaanza kupata matamasha, nikapiga sana matamasha ila dau langu lilikuwa ni shilingi laki moja, ikizidi sana laki mbili. Nilipiga sana na kufanikiwa kung’aa.

Sikuamini siku moja nasikiliza redio fulani, nikashtuka kusikia wimbo wangu umeshika namba moja, nilibaki nikibubujikwa na machozi ya furaha chumbani. Nilirukaruka sana.

SOFIA: Huo ndiyo ukawa mwanzo wa mafanikio bila shaka. Na vipi kuhusu chuchuziii, hawakuanza kusumbua?

PHIZA: Hahaha! Aiseee! Chuchuziii tena! Utawaeleza nini hapo. Demu wa kwanza kabisa kuwa naye toka nilipoanza kuukwaa ustaa alikuwa huyu My X, Bertha ambaye juzijuzi tu nilimkosakosa kumpiga na risasi kwa kuwa aliwazingua wazazi wangu.

SOFIA: Ulikutana naye wapi?

PHIZA: Hahaha! Daaah! Bertha...Bertha...Bertha...nilikutana naye kwa mara ya kwanza pale Maisha Klabu.

SOFIA: Ikawaje.

PHIZA: Daah! Ni stori ndefu sana. Yaani kwa matukio yote ambayo Bertha amenifanyia mimi na wazazi wangu, acha tu afanye vile, alistahili. Mapenzi niliyompa, nahisi hakuwahi kuyapata kwa mtu yeyote yule, hata huyo jamaa aliyekuwa naye sijui kama aliwahi kumpa mapenzi kama niliyompa.

SOFIA: Yapi hayo?

PHIZA: (Ananyamaza na kuanza kucheka)



PHIZA: Unajua hapo kabla sikuwa mtu wa kwenda klabu, si kwamba sikuwa nikipenda, hapana, nilipenda sana lakini sikuwa na fedha, hivyo kwenda ilikuwa ngumu sana. Kulikuwa na washikaji zangu ambao kila wikiendi walikuwa wakienda huko na walitamani sana na mimi niende kwa kuwa kulikuwa na mademu wengi wakali lakini sikuweza kufanya hivyo, kwanza kuwa na demu yeyote mpenda klabu ilikuwa ni lazima uwe na fedha.

Mara baada ya kupata vijisenti kadhaa, nikaona basi lisingekuwa jambo baya sana kama ningekwenda japo mara moja kwenda kusafisha macho, niwaone hao mademu ninaosikia kwamba walikuwa wakali, yaani nilitaka nione upande mwingine wa pili, matukio ambayo hutokea kipindi ambacho nimelala.

Ilipofika saa tano, tukaelekea huko. Nakumbuka nilikuwa na washikaji kama wanne hivi akiwepo Jafari Sharifu, Rajabu Sharifu na mshikaji fulani aliyekuwa akiitwa Monero. Kile kilichokuwa kikisemwa ndicho nilichokutana nacho, niliwaona wasichana warembo wakiwa nusu utupu, mapaja hayooo, makalio usiseme, sura za kitoto, vifuani mambo yalikuwa yamebustiwa, ilikuwa ni mzuka ile mbaya, na kila niliyemuona, nilitamani kuondoka naye, yaani nilitaka niwe na mademu wote humo klabu.

SOFIA: Hahaha! Uliwachukua?

PHIZA: Subiri nikupe mkasa. Hii siku sijui kama nitaisahau. Kabla hata hatujaingia ndani, kuna manzi fulani nilimuona amekaa pembeni kabisa, kwa kumwangalia tu, alikuwa demu mkali tu, nikaanza kupiga hatua kumfuata, nilipomfikia, nikamsalimia, japokuwa alikuwa amekiinamisha kichwa chake chini, akakiinua na kunitazama.

Msichana huyu alikuwa pini kweli, pale alipokuwa amekaa, mapaja yake yalikuwa yakionekana vizuri tu, alipokuwa akiniangalia, na mimi nilikuwa nikimwangalia, ila alipoyahamisha macho yake kutoka usoni mwangu, macho yangu yalikuwa yakitua katika mapaja yake.

SOFIA: Huyo ndiye alikuwa Bertha mwenyewe nini?

PHIZA: Ndiye yeye. Nikaanza kupiga naye stori na kumuomba tuingie ndani, hakuwa na neno, tukazama zetu ndani ambapo tulicheza sana muziki. Sijui kama Dj alikuwa ameambiwa au la, baadae nikasikia akitangaza kwamba Phiza alikuwa ndani ya nyumba.

Kipindi hicho sikuwa nimetoa video na wala sikuanza kuuza nyago magazetini, sasa watu waliposikia Phiza yupo mjengoni, masela wakataka kuniona. Nikamwambia Bertha anisubirie ili niende kujitambulisha, nahisi yeye mwenyewe hakuamini kama yule aliyekuwa akicheza naye alikuwa ndiyo Phiza mwenyewe, alionekana kupagawa.

SOFIA: Mpaka hapo, nina uhakika ulichukua mzigo kiulainiiii!

PHIZA: Unauliza mapanga kwa Panya Road. Mtoto nikang’oa siku hiyo na uhusiano mpya kuanzia klabuni hapo.

SOFIA: Sasa ilikuwaje mpaka ukaja kummwaga?

PHIZA: Unajua unapokuwa supastaa kunakuwa na mademu wengi wanaokufagilia, kila msichana anataka kulala na wewe tu. Bertha alipata tabu sana, kila siku alikuwa akinilalamikia, leo alikuwa akiona Salama anapiga simu, kesho Amina, kesho kutwa Susan, yaani ndiyo ilikuwa hivyo.

SOFIA: Kwa hiyo kote huko ulikuwa unadokoadokoa?

PHIZA: Naweza kusema ndiyo. Unajua nilizaliwa katika familia masikini sana huku nikiamini kwamba kutembea na mademu wakali ilitakiwa uwe na fedha kwanza, sasa mimi nikawakosa kwa kuwa sikuwa na fedha. Nilipoanza kuunyaka usupastaa, kwa nini nisiwatafute sasa? Ndiyo hivyo, nikaanza kulala na wanawake mbalimbali na Bertha alikuwa wa kuzugia tu.

SOFIA: Wakati huo ulikuwa ukiwasiliana na Stellah?

PHIZA: Toka aondoke, sikuwa nikiwasiliana naye kabisa kwani hata namba yake sikuwa nayo.

SOFIA: Hali iliendelea vipi?

PHIZA: Niliendelea kusikika zaidi, nilipotoa wimbo wa pili ule wa Mama Afrika, hapo ndipo watu wakapagawa zaidi, nikaalikwa kwenye matamasha zaidi kitu kilichonifanya kuingiza fedha kwani hapo ndipo kwa mara ya kwanza nikaanza kupiga shoo mpaka milioni moja.

Sikuwasahau wazazi wangu, nilichokifanya, nikawapangia nyumba nzima maeneo ya Kijitonyama. Unajua mimi ndiye nilikuwa mtoto pekee hivyo nilitakiwa kuwafanyia kila kitu. Nyumba ilikuwa kubwa na kadri walivyokuwa wakinishukuru na ndivyo baraka zilivyozidi kumiminika.

Baada ya miezi sita, nikajikuta nikianza kuandikwa sana magazetini kitu kilichonipaisha sana. Japokuwa nilikuwa nikijitahidi sana kuishi pasipo skendo lakini hiyo ilishindikana kabisa, nikajikuta nazivaa skendo nyingi mpaka nikachanganyikiwa. Kama unakumbuka mwaka ule ndiyo kulikuwa na ishu ile iliyonichanganya ya Lilian.

SOFIA: Daah! Swali muhimu sana umenikumbusha, hivi ilikuwaje wewe na Lilian, alidai ulimbaka, ni kweli?

PHIZA: Daaah! Kwanza jua kwamba hakukuwa na kitu kilichoniuma kama kusingiziwa maneno hayo. Mimi ni staa, mademu wananishobokea, nachukua mademu wa kila kona kuanzia ushuani mpaka uswahili, sasa ilikuwaje nimbake Lilian? Kweli ingewezekana?

Ishu yenyewe ilikuwa hivi; kuna siku moja wakati nimechill chumbani kwangu katika moja ya nyumba niliyopanga maeneo ya Sinza Makaburini, nikapokea simu kutoka kwa Lilian, sikuwa nikimfahamu ila alitaka kuonana na mimi.

Ilikuwa ngumu kumkubalia kwani niliamini kama ningemkubalia yeye, kwenye maisha yangu ya ustaa ningewakubalia wangapi? Nikakataa. Lilian hakuishia siku hiyo, aliendelea kunisumbua kila siku. Nikaona kwa sababu anataka kuonana nami basi halikuwa tatizo, nikamwambia kwamba ningeonana naye pale Chagga Bites.

SOFIA: Ikawaje? Alikuja?

PHIZA: Yeah! Alikuja, tena mapema kabisa kabla yangu. Nilipofika maeneo hayo, sikutaka kuteremka garini kwa kuhofia macho ya watu, si unajua waandishi walikuwa wamewekwa kila kona kunicheki, na ukiachana na waandishi hata raia wa kawaida nao walikuwa wakinitafuta kwa ajili ya kuuza habari yangu.

Nikamtuma mtu aende akamuite, kweli akaja na kuondoka naye.

SOFIA: Mlikuwa mnaelekea wapi?

PHIZA: Nilimwambia kwamba lingekuwa jambo jema kama ningekwenda naye katika Hoteli ya Atriums kwa ajili ya chakula lakini akanikatalia, yaani hakutaka nikae naye katika sehemu ilipokuwa na mkusanyiko wa watu, alitaka tukae sehemu ambayo tungekuwa wawili tu, nikajua kwamba alikuwa akimaanisha chumbani. Basi nikamchukua mpaka pande za home, mjengoni kwangu. Nikatulia naye sebuleni.

SOFIA: Haha! Lete utamu baba.

PHIZA: Nikakaa naye sebuleni, hakuwa muongeaji, kila nilipomwambia kwamba aniambie alichotaka kuniambia, alikuwa akijichekeachekea tu. Nikaona siyo tatizo, nikaondoka na kuelekea zangu chumbani. Nikiwa navua nguo zangu, ghafla akaingia chumbani kwangu, kifua kilikuwa wazi, alikuwa na nguo ya ndani tu, akaja na kunikumbatia kwa nyuma.

SOFIA: Duuh! Ikawaje sasa?

PHIZA: Alinishangaza sana, alichokuwa akijua ni kwamba ningeweza kuweweseka lakini hakukuwa na kitu. Unajua hata sisi wanaume si kila wakati huwa tunakuwa kwenye hali ya matamanio ya kufanya ngono, kuna wakati mwingine huwa hatupo kwenye mihemko.

Nilimchukulia kawaida, nikataka aniachie lakini hakutaka kufanya hivyo. Nikaona kwamba hilo lingekuwa tatizo, kwa nini niongee kiupole na wakati sikutaka kuwa naye chumbani, nikaanza kumfokea, ilimuuma sana, akaondoka zake, kesho, nashangaa naambiwa kwamba kuna kesi ya kubaka ambayo ilinihusu na mshtaki alikuwa Lilian.

SOFIA: Duuh! Kumbe ndivyo ilivyokuwa? Sasa mbona hukutaka kuliweka wazi raia tujue?

PHIZA: Unajua mimi si muongeaji, wakati mwingine niliona kwamba Lilian alikuwa akitafuta umaarufu, kama ningeamua kumtangaza sana ningempa kiki, kitu ambacho sikuwa nikihitaji kabisa.

SOFIA: Kesi ilikwendaje?

PHIZA: Kwanza yule msichana mpumbavu sana. Unajua nadhani alikuwa hajui vizuri kesi za kubaka zinavyokuwa. Hakuwa na uthibitisho, yaani hakuwa akielewa chochote kwamba msichana anapobakwa hatakiwi kuoga kwa ajili ya ushahidi na wakati mwingine mpaka anachunguzwa kuona kama kaingiliwa, yeye, hakuwa akilifahamu hilo. Kwa hiyo mwisho wa siku nikashinda kesi.

SOFIA: Huo ndiyo ulikuwa mwisho wako na wanawake?

PHIZA: Unapokuwa mtu wa wanawake wewe ni wa wanawake tu. Nilikwishasema kwamba baada ya ishu ya Lilian sitotaka kumchukua msichana yeyote lakini baada ya wiki, kama kawa kama dawa, tabia yangu ikarudi tena.

SOFIA: Hebu tuendelee na Bertha kwanza, nahisi kuna mambo matamu kuhusu yeye.

PHIZA: Hahaha! Kwa Bertha, daah! Unajua yule msichana alikuwa akijua sana kupenda. Kipindi cha nyuma nilimchukulia kama kicheche au mlupo fulani hivi lakini demu alikuwa makini sana. Alikuwa akinipenda mno na hakutaka nimuache, njia nyepesi ambayo aliifanya ni kunipagawisha kitandani.

Alikuwa makeke sana mpaka nikaona kweli kazi nilikuwa nayo. Ila si unajua wali ukipikwa vizuri kila siku kuna siku utauzoea na utahitaji mapishi mapya, ndivyo ilivyokuwa kwa Bertha. Alijitahidi sana kunipagawisha lakini kwangu, baadae nikasahau na kuanza kuwashughulikia wengine.

Bertha alikuwa mvumilivu sana ila mwisho wa siku alipoona ameshindwa, eti akaamua kulipa kisasi, akaanza kudate na washikaji zangu kisiri. Nikabaki nacheka tu.

SOFIA: Haukuumia ulipojua?

PHIZA: Wala sikuumia, ndiyo kwanza nikawapa big up washikaji. Nikaanza kufocus vizuri katika maisha yangu. Kwa kipindi fulani nikaachana na mambo ya mademu na kuendelea kufanya michongo yangu.

Nilikuwa kwenye maisha ya umasikini hivyo nilitakiwa kuhakikisha kwamba fedha nilizokuwa nazo hazimaliziki zaidi ya kuongezeka tu, nilichokifanya ni kufungua biashara. Biashara ya kwanza ambayo niliifanya ilikuwa ni kuagiza nguo kutoka China na kufungua duka maeneo ya Sinza Kijiweni na kuweka jina langu kubwa ambalo lilinitangaza.

Biashara ilikuwa na faida, baada ya kuendelea kupiga shoo, nikanunua bodaboda kumi, zote hizo nilitaka ziniingize fedha za kula tu nyumbani. Nilikuwa na kiu ya fedha, unajua mpaka leo hii, japokuwa nina fedha nyingi lakini bado nahitaji fedha nyingine za watu wote zije kwangu.

Baada ya hapo, nikanunua bajaji, daladala na kuendelea na mchakato mzima wa kuendelea kuingiza fedha nyingi. Nilipoona kwamba bado nilitakiwa kuchuma fedha zaidi, nikaanzisha baa ambayo kwa kiasi kikubwa ilinipa fedha kwani kwa siku ilikuwa ikichukua wateja zaidi ya mia tano, tena ilipokuwa ikifika wikiendi, nami nilikuwa mhudumu kitu kilichowakusanya watu zaidi.

SOFIA: Mpaka katika kipindi hicho haukununua nyumba?

PHIZA: Nyumba zilikuwa gharama sana, nyumba moja ilikuwa ni shilingi milioni 400, ningepata wapi fedha hizo, hizihizi biashara ndogondogo ndizo niliamini zingenipa hizo milioni mia nne.

Mwaka 2009, nikaanza kufanya matangazo mbalimbali ya kibiashara, yalikuwa na fedha, matangazo niliyofanya yalikuwa yakiniingiza zaidi ya shilingi milioni mia moja. Kwa mwaka nilifanikiwa kufanya matangazo manne, niliingiza milioni 400, fedha za nyumba zikapatikana.

SOFIA: Hongera sana. Kwa hiyo ulinunua nyumba?

PHIZA: Hapana. Nisingeweza kununua nyumba kiasi chote hicho, nilitaka fedha zangu ziwe kwenye mzunguko. Nikafungua biashara nyingine. Kwa kweli nilikuwa na biashara nyingi sana, zaidi ya ishirini na zikanifanya kuingiza milioni ishirini kwa mwezi. Nilianza kufanikiwa sana, baadae, nikaja kugundua kwamba sikutakiwa kuwa mfanyabishara bali nilitakiwa kuwa biashara.

Kama magazeti yanauza kupitia mimi, kama watu wa makampuni wanauza kupitia mimi, hivi kweli na mimi siwezi kuuza kupitia mimi? Nikaona inawezekana. Nilichokifanya ni kutengeneza fulana zangu ambazo nilizipa jina la Face My Book huku zikiwa na picha zangu na kampuni nikaisajili, nilitengeneza sana fulana na kuziweka mitaani, zilinunulika mno, nadhani kwa wajanja wote walikwishawahi kuzivaa.

Biashara ya fulana iliniingizia zaidi ya milioni mia tatu, baadae nikahamia kwenye kofia, nilikuwa kama Bakhresa. Kila nilipokuwa nikikaa kitandani, badala ya kufikiria nilitakiwa nionane wapi na Magreth kesho, nikawa nafikiria kesho nianzishe biashara gani kutengeneza fedha.

SOFIA: Kwa hiyo umasikini ukaukimbia?

PHIZA: Ndiyo hivyo, sikukumbuka tena shida nilizokuwa nimezipata, kila kitu kilichokuwa kimetokea nyuma, kikabaki na kuwa historia. Kiukweli sikuweza kuwasahau wale watu waliowasaidia wazazi wangu wakati mama alipokwenda kujifungua, nilichokifanya ni kuwasaidia fedha nyingi tu na kuzirekebisha nyumba zao na kuzifanya kuwa za kisasa zaidi huku nikiwasisitizia kwamba fedha nilizowapa ilikuwa ni lazima wafungue biashara.

Kwa mzee Madevu ambaye alikuwa amekwishafariki, matunda ya wema wake nikawapa watoto wake na mkewe, hakika nilifarijika sana lakini niliumia kidogo kwa kuwa nilitaka mzee huyo ayaone mafanikio hayo.

SOFIA: Tuendelee na Bertha.

PHIZA: Unajua katika kipindi ambacho nilikuwa na Bertha nilimthamini sana, nilimpa kila kitu alichokuwa akitaka na hata gari nilimnunulia. Kuna wakati mwingine najiuliza, hivi msichana alikuwa akihitaji kitu gani ili atulie lakini nikakosa jibu.

Nilikuwa kicheche lakini sikutaka Bertha awe hivyo, nilitaka kumfanya kuwa mama bora wa baadae. Sasa kwa mambo ambayo alikuwa ameyafanya yalinikera sana.

SOFIA: Baada ya Bertha, ulimsubiria Stellah?

PHIZA: Stellah nilimsubiria sana. Mwaka mmoja baadae nikaona simu yangu ikiita kwa namba ngeni, tena haikuwa ya nchini Tanzania. Kwanza nilishtuka kwani kwa kipindi hicho sikuwahi kufanya shoo nje ya Tanzania, nilipopokea simu, niliisikia sauti ya msichana mrembo, iliyosikika vizuri masikioni mwangu, alikuwa Stellah.

Nilishtuka kwa furaha, sikuamini kwamba hatimae Stellah alikuwa amenipigia simu. Nilifurahi sana na kuanza kuongea naye. Kwanza akanipongeza kwa hatua niliyokuwa nimepgia kimaisha, sikutaka kuishia hapo nilimwambia wazi kwamba kitu nilichokuwa nikikifikiria ni kumuoa tu.

Alicheka kwa furaha na kuniambia kwamba sikusahau tu, nikasema siwezi kusahau kwa sababu nilihisi kwamba yeye ndiye alikuwa msichana pekee ambaye nilipangiwa kuishi naye.

Aliniambia kwamba alibakiza miaka mitatu mpaka arudi nchini Tanzania na hivyo tungekaa chini na kuongea, sikutaka kukubali, nikasema kwamba ninamfuata nchini Marekani kwa ajili ya kuongea naye.

Unajua unapokuwa na fedha, kila sehemu duniani ni kama unakwenda Kariakoo kununua nguo. Baada ya mwezi mmoja, nikakamilisha kila kitu na hivyo kwenda nchini Marekani.

Hebu fikiria, KUTOKA TANDALE MPAKA NEW YORK, hakika ilikuwa ndoto nzuri ambayo sikuwahi kuiota hata siku moja. Ndege ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa John F Kennedy, nikateremka na nilipofika nje, nikakutana na msichana ambaye kila siku nimekuwa nikimuota, alikuwa Stellah.

SOFIA: Mmmh! Ilikuwaje?

PHIZA: Wewe acha tu. Uzuri wake ulikuwa umeongezeka, aliponiona, akanikimbilia na kunikumbatia. Katika hali ya kushangaza, tukaanza kubadilishana mate hapohapo uwanjani.

SOFIA: Duuh! Mlitisha sana. Nini kiliendelea?

PHIZA: Tukaondoka na kuelekea hotelini. Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimepanda ndege na kwa mara ya kwanza nilikuwa nimefika nchini Marekani. Mazingira yalikuwa mazuri sana, tulipofika hotelini, kazi ikaanza, yaani kwa mara ya kwanza toka niwe na Stellah.

Baada ya kukaa kwa wiki nzima huku tukipanga mikakati ya kuishi pamoja nikarudi nchini Tanzania. Kiukweli nilikuwa na fedha sana, baada ya miezi miwili, sikuamini nilipokwenda kwenye akaunti yangu na kukuta nina zaidi ya bilioni mbili...sikuamini, nikakaa chini kwenye kijumba cha ATM na kuanza kububujikwa na machozi ya furaha, SIKUAMINI kama masikini mimi, leo hii nilikuwa bilionea.

SOFIA: Ikawaje sasa?

PHIZA: Hapo ndipo nilipojenga nyumba yangu kubwa kule Mbezi Beach na kisha kununua zaidi ya nyumba tano, hizo nikapangisha. Unajua katika maisha yangu nilitaka kuwekeza sehemu mbalimbali, hasa nilitaka kuwekeza kwenye ardhi.

Ninapohadithia historia ya maisha yangu naomba watu waelewe kitu kimoja, sipo hapa kwa ajili ya kujisifia na kuwatangazia watu mali nilizonazo bali ninahitaji watu wajifunze kwamba maisha ni safari ndefu, unapotafuta mafanikio kuna mengi yanaweza kutokea, kuna watu ambao kazi yao kubwa itakuwa ni kukucheka tu na kukudharau lakini hautakiwi kurudi nyuma.

Mwingine anaweza kusema kwamba hawezi kufanikiwa kwa kuwa ni mlevi, mimi mbona nilikuwa mlevi? Mwingine atasema hawezi kufanikiwa kwa kuwa hajasoma, mbona mimi niliishia darasa la saba na tena nilifeli vibaya?

Unapoanza kutafuta mafanikio, usifikirie kwamba hautoweza kwa kuwa haujasoma au wewe ni mlevi kupingukia, unaweza kufanikiwa kama mimi. Pamoja na hayo, pia mtu unatakiwa kujipanga. Nilipoanza kuachana na starehe ndipo nilipofanikiwa zaidi. Niligundua kwamba mademu kazi yao kubwa ni kukurudisha nyuma na si kukufanya upige hatua ya kwenda mbele, hivyo niliachana nao na kweli nikafanikiwa zaidi.

SOFIA: Hapo umesomeka sana. Ila ningependa kukuuliza kitu. Utaniruhusu?

PHIZA: Nitakuruhusu.

SOFIA: Una mtoto?

PHIZA: Hapana.

PHIZA: Ila unakumbuka kuna msichana aitwaye Leah alisema kwamba mtoto aliyezaliwa alikuwa wako, ulipofuatwa na waandishi wa habari, mdomo ulijaa kigugumizi. Hebu tuambie leo kuhusu Leah na yule mtoto. Ni wa kwako au la! Na kama siyo, kwa nini hukutaka kuweka wazi na kwa nini hata ulipofuatwa na waandishi wa habari mdomo ulikuwa na kigugumizi.

PHIZA: (Anatoa tabasamu pana, anaonekana kukumbuka kitu, tabasamu linapotea, anakiinamisha kichwa chake chini, anapokiinua, anashusha pumzi ndefu)

Leah na yule mtoto wake anayeitwa Phillip Jr, yaani akimaanisha Phillip mdogo badala ya mimi mkubwa. Daah! Hii ni stori ndefu na yenye kusisimua sana, sikutaka nielezee kabisa, ila ngoja niseme ili kila kitu kiwe wazi.

SOFIA: Sawa.....tunakusikiliza.

PHIZA; Koh koh koh....ooopppsss....!!!!




PHIZA: Leah alikuwa miongoni mwa wanawake wazuri ambao nilibahatika kuwa nao. Alikuwa ni msukuma aliyeumbika kwa kila kitu, kwa nyuma, alikuwa amejazia huku kifua chake kikimvutia kila aliyemuona.

Nakumbuka siku moja nilikuwa Mwanza, na ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kuonana na huyu Leah, nikatokea kuvutiwa naye kwa sababu umbo lake kwa nyuma lilinipa shida sana. Aliponiona, Leah akatokea kuvutiwa na mimi, sijui kama mimi ni handsome au alivutiwa na ustaa wangu, ila akanipenda na siku hiyo nikaomba kuonana naye faragha, akanikubalia.

Kwa hiyo ikawa hivyo, nikaanzisha mahusiano na Leah, nilipoona kwamba kwa Mwanza ilikuwa mbali sana, nikamuhamishia Dar ili niweze kuwa karibu na tunda langu. Sikutaka awe nyumbani kwangu, nikampangishia nyumba nzima maeneo ya Kijitonyama.

SOFIA: Kwa nini hukutaka kukaa naye nyumbani?

PHIZA: Mimi ni mzee wa majanga, kama ningekubali kukaa naye nyumbani basi kuna siku ningetoa boko tu. Sikuwa mtu wa kutulia lakini kwa Leah, kiasi fulani nilitaka kutulia kabisa kwani kwa muonekano wa nje, alikuwa msichana ambaye nilikuwa nikimuhitaji ukiachana na Stellah.

Wakati mapenzi yamepamba motomoto, kuna siku nikaanza kusikia tetesi.

SOFIA: Tetesi gani?

PHIZA: Kuna msanii mmoja naye alikuwa akimega kisela kwa Leah. Kwanza nilikasirika mno, kumegewa mtu wako na wakati una kila kitu, hizo ni dharau, kingine mtu aliyekuwa akimmega alikuwa wa kawaida sana, japokuwa alikuwa staa lakini hakuwa na fedha kama nilizokuwa nazo, hivyo nilimmaindi na kuamua kuachana naye.

SOFIA: Hukukaa naye kulizungumzia hilo?

PHIZA: Kukaa ilikuwa ngumu, nilikuwa bize sana huku nikiwa mtu mwenye hasira, baada ya kuambiwa hivyo sikutaka kuchukua uamuzi wa haraka nikaanza kuchunguza na mwisho wa siku nikawafuma pamoja kule Msasani Beach. Niliongea kiutaratibu na huo ndiyo ukawa mwisho wa kila kitu.

Baadae kabisa nikasikia akisema kwamba alikuwa na mimba yangu na alijifungua salama, mara ya kwanza nilihofia lakini baada ya kuyakumbuka majanga yangu, nikasema sawa, kama vipi tukapime. Kweli tulikwenda kupima na kugundulika kwamba hakuwa mtoto wangu.

Sikutaka kulizungumzia hilo kwa kuwa niliamini ningemchafua, sikutaka achafuke kama nilivyochafuka, nilitaka aendelee na maisha yake bila kujisikia aibu mitaani. Sikuhusika naye, na hata baada ya kodi kuisha, sikutaka kumlipia. Pia, hata gari langu sikutaka nilichukue, nikamuachia aendelee kuwa nalo, nadhani atakuwa ameliuza. Hayo ndiyo yaliyotokea kwangu na Leah.

SOFIA: NA vipi kuhusu Bertha, hakuendelea kukusumbua?

PHIZA: Hahaha! Nilimwambia kwamba nilikuwa tofauti sana na wanaume aliokuwa nao kabla, nilimpenda na kumthamini mno, nilipomuacha, alijitahidi sana kutaka kujirudi lakini sikuwa tayari kwa hilo, niliamua kwamba ninataka kuwa peke yangu tu.

Baadae ndiyo likaja suala la kuwatukana sana wazazi wangu mpaka kutaka kumlipua kwa risasi, alinikasirisha sana. Alipokuwa akiwatukana wazazi wangu, nilikumbuka kipindi kile walipokuwa wakipata shida kisa mimi, nilikumbuka kipindi kile walipokuwa wakifanya kila liwezekanalo kisa mimi, halafu leo mtu aje kuwatukana kizembezembe, nilikasirika sana.

Baada ya kupita kipindi fulani, nikakaa chini na kujitafakari sana kwamba kama kutembea na wanawake, nilitembea wa aina zote, wanawake wote wazuri unaowafahamu wewe, nishatembea nao. Nimetembea na waswahili, wazungu, wahindi, waarabu na wengine wengi, nikajiuliza, nilipata nini? Kuna faida niliipata? Jibu likaja kwamba hakukuwa na nilichokipata, hivyo nikaamua kutulia na kufanya muziki.

Nilijitanua zaidi na kupiga mpunga wa maana, biashara zangu zikakua na nilifanya sana shoo za nje. Kuna kipindi nilitaka kuwanunulia wazazi wangu magari ya kifahari, wakasema hawataki magari bali walitaka fedha hizo za magari niwajengee nyumba nyingine kwa kuwa ingekuwa ni faida kwangu pia, nikawajengea.

Kuna wamama wengi ambao wanapenda kununuliwa magari na watoto wao, lakini wangu, waliona magari si kitu chenye faida, leo zima na kesho bovu na mwisho wa siku linatelekezwa gereji, lakini kwa nyumba, ilikuwa ni hazina tosha, hivyo nilifanya hivyo na wao kuwapa gari la chini sana la milioni nane.

SOFIA: Kwa hiyo wewe na Stellah inakuwajekuwaje?

PHIZA: Kiukweli ninataka kumuoa, nikisema kwamba ninataka awe mpenzi wangu tu, nitakuwa najidanganya. Nimepanga kumuoa na kuishi naye na ndiyo maana mambo ya kuwavua wanawake sketi nimeachana nayo.

SOFIA: Una ujumbe gani kwa Watanzania?

PHIZA: Wajitume, mafanikio hayaji kiwepesiwepesi kama wengi wanavyofikiria, mafanikio huwa yanapatikana kwa watu wanaopambana tu. Ili uyafikie mafanikio, yakupasa kujituma sana. Tatizo letu ni moja sana, wengi tunatamani kuwa na mafanikio lakini hatutaki kufanya vile vitu ambavyo vinaweza kutupa mafanikio.

Mbali na hivyo, starehe zimekuwa nyingi sana. Kwenye historia ya maisha yangu, utagundua kwamba kila nilipofanya starehe, sikupiga hatua kubwa ila nilipoacha, fedha zilikaa na nilipiga hatua kubwa.

Kama unafanya starehe na kununua gari ya milioni tano, amini kwamba usingekuwa mtu wa starehe ungenunua hata gari la milioni kumi na tano. Tubadilike tu na tumuamini Mungu. La mwisho labda ninapenda kuwakaribisha katika harusi yangu nitakayofunga na Stellah mwezi ujao katika Kanisa la Praise And Worship pale Mwenge.

SOFIA: Ninashukuru kwa muda wako.

PHIZA: Nashukuru pia.

Kipindi kinakwisha.


MWISHO






0 comments:

Post a Comment

Blog