Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

KIAPO

  


MTUNZI : LAURA PETTIE


Kibarazani, nje ya jengo la ofisi yetu ya ghorofa moja.

Nilikuwa nimesimama hapo nje mithili ya nguzo. Nafsi yangu ikiigomea miguu kuutosa mwili juani. Ingawa lilikuwa jua la alasiri tu, ila kwa jiji la Dar es Salaam bado makali ya jua hilo yalitosha kuutotesha uso wa mtu.

Kwa vile sikuwa na haraka yoyote, niliendelea kujisimika hapo barazani, huku nikiitafuta nguvu ya kuchapua miguu hadi kituo cha daladala.

Ndiyo kwanza nilikuwa nimepata ajira yangu ya kwanza. Na miezi kama sita hivi ikawa imekwishapita. Kile kiwewe cha kushika laki mbili tatu zangu mwenyewe kikawa kimeshapungua. Tayari, maisha yalishaanza kusimama dede, fimbo mkononi. Nilianza kuona mshahara haunitoshi tena. Yalikotokea hayo majukumu ya kunimalizia hela hata sijui.

Kiuhusiano, nilikuwa niponipo tu. Sikuwa na mtu. Ulikwishakatika mwaka mmoja tangu niachane na mpenzi wangu. Mwanaume niliyempenda juu, chini, kulia na kushoto. Kisa cha kuachana naye; alinuna ghafla tu kama kawaida yake.

Alikuwa akininunia hivi kila mara. Ungelikesha ukimpigia simu na kumtumia meseji kama opereta, naye huko aliko, angelikaa kimya mfano wa mashine mbovu.  Safari hii aliponinyamazia, nami nikampotezea. Nilijiambia nafsini, nenda mwana kwenda ufike unakokwenda.

Nilishayachoka mapenzi ya undugu wa nazi kukutana pakachani. Mpaka lini hata wapi tungefikishana kwa penzi la aina hii? Sijui.

Niliuuguza moyo wangu kwa mwezi moja hivi na pengine zaidi. Taratibu nilianza kumsahau. Hatimaye, nikamsahau kweli. Kumpenda nilimpenda sana, ila ilikuwa lazima maisha yaendelee. Nikaona nikae tu mwenyewe, nitengeneze maisha yangu.

Niwe mkweli, sikukaa tu kama kipande cha ugali wa jana. La!

Wanaume wengi walikuja na abracadabra zao. Aliyeeleweka kidogo nilimfanya rafiki tu. Tukaalikana kupata bia mbili tatu, tukaagana. Mwingine, angeniambia nakupenda Mima. Nami ningemjibu nakupenda zaidi huku nikimng'ong'a. Zilipokuja habari za kutifua kitalu, nilikimbia mbio za kuruka viunzi. Nilijifunza kujitunza. Nilijitunza hasa!

Baada ya maumivu makali ya  kujeruhiwa moyo, niliapa, kamwe nisingekuja kupenda tena kwa dhati maishani. Niliapa kwa machozi na majonzi. Kamwe!

Huyu aliyenitenda, hakuwa mwanaume wangu wa kwanza mapenzini. Walakini, nakiri alikuwa mwanaume wa kwanza kuukata mtama moyo wangu. Sikutaka kumkosa. Nami nilijua dhahiri shahiri, pasipo kuufunga moyo kitanzi ningelihiari mauti au mwili kubaki gofu.

Mwaka ukayoyoma kimzahamzaha.

Alasiri hiyo baada ya kazi, nikiwa nimesimama hapo kibarazani, ofisini. Rafiki yangu kipenzi, Tutu Mzigoz, alinitumia ujumbe wa maneno. Ujumbe wa kunijulisha kuwa yuko sehemu matata kwenye viti virefu. Akipiga mluzi wa Yohana Mtembezi. Hivyo, nifanye nifanyavyo, nimfuate.

Niliangalia salio langu mkobani. Kulikuwa na shilingi 6,500/- tu. Nilipopiga hesabu za Uber niliiona hatari ya kushushiwa kituo cha polisi. Nikawaza kuchukua usafiri wa bajaji.

Abwe! kwa umaskini jeuri niliokuwa nao sikutaka kujitweza na tukutuku mitaa ya uzunguni. Kwangu, nisingeweza kunyata nayo huko. Kwa kelele zake ningeonekanaje? Nikamjibu Tutu, nimechalala hata moja sina.

Kabla hata sijairudisha simu mkobani, akanijibu.

‘We njoo nauli utaikuta hukuhuku.’

Nilianza kuwaza tena, nipande daladala mpaka wapi. Halafu nikanyage mwendo gani mpaka huko kiotani. Yarabi! Nitafika na uso wa posta, miguu ya Goba.

‘Mmh, mmh hapana!’ Nafsi ilikataa huku ikikiri kweli umaskini matusi.

Unakula upatacho si upendacho.

Hapo, nilikuwa nikiusubiri kwa hamu mshahara wangu wa mwezi huo ilhali ukiwa umekwishachanjiwa majukumu. Sawa, sikuwa na umasikini wa sina sinani ila na utajiri wa kufuru pia sikuwa nao.

Nilimtumia Tutu meseji ya kumjulisha hali halisi. Punde si punde, akanitumia hela kwenye simu. Nikapata nauli ya teksi na ziada. Nikaondoka zangu tutituti huyo!

Ilinichukua takribani dakika 40 kufika eneo la tukio.

Tutu alikuwa juujuu akinisubiri. Aliponiona, alinipungia mkono kunijulisha uwepo wake. Nikadondosha mwondoko maridadi kabisa. Naapa, si mwondoko huu ninaonyatuka nao huku mtaani.

Ulikuwa mwondoko maridhawa wa kuwafanya hata wadudu ardhini wamsifu Karima kwa uumbaji wake. Nilikuwa naujua ulimbwende wangu. Mungu aliniumba nikaumbika. Shingo mbili tatu za pale mgahawani zilinisindikiza. Nami mikogo ikanivaa almanusura kuipita hata meza aliyoketi Tutu.

Nikafika!

Tulisalimiana kwa kukumbatiana. Matashtiti ya kike yakitibwirika.

Mezani pake, kulikuwa na vijana wengine wanne. Nadhifu hasa! Yaani hupati shida kujua wametoka kwenye viyoyozi. Wamelegeza tai zao nusu kifua. Sharafa zimechongwa kiustadi. Udevu ulionawiri, ukakakatwa kwa umakini mkubwa.

Miili yao ilikuwa imesimama; imeenda hewani kinyamwezi ikakita ardhini kikakamavu. Kwa mwenye kitambi basi ni kile cha kufutia simu. Hicho, kamwe hukikuti huku kwenye yale matangazo ya kupunguza tumbo. Mungu fundi!

Waliinua vichwa vyao kunitazama.

“Huyu ni Mima, pacha wangu kabisaaa!’ alinitambulisha kwa bashasha tele.

Nami nikaikusanya midomo yangu mbele kama samaki. Ulimi ukiyagusa meno ya mbele bila kutokeza nje. Nikawapa mikono kwa awamu. Wakitambulishwa pia kwangu kwa kila niliyempa mkono.

Kati yao, kuna mmoja alikuwa ameketi mwishomwisho kwa mtindo wa kukalia mgongo.

Kiti chake kilikaa mbali kidogo na meza. Alikuwa kakunja nne ya kifahari, glasi ya mluzi mkononi. Yeye hata mkono hakuupokea sembuse kunitabasamia alipoinua uso kunitazama. Aliinyoosha tu glasi yake juu kidogo kimaringo, kuijibu salamu yangu.

Na ndiye aliyekuwa wa mwisho kutambulishwa kwangu.

“Na huyu ni Teri Balokwa, mshikaji wangu kinoma.”  Hayo maneno yalipotamkwa na Tutu, ndipo naye akaiinua glasi yake hewani.

Akauacha mkono wangu wa salamu ukining’inia mithili ya nyama buchani.

Macho yake tulivu yalinitazama kwa sekunde tatu, kisha yakarejea kwenye simu yake pana iliyolazwa pajani. Ni kama vile sikuwa na maana yoyote kwake, fakaifa kuwa na mvuto wa kuipata salamu yake. Kwa mwanamke niliyezoea kukoga makumi ya wanaume, nafsi iliinama.

Nikaketi, nuru ikiwa imepooza usoni.

Moyo ulivyo na hila. Hila ya kwenda kushoto akili inapokwenda kulia. Huyo aliyenifanyia dharau za Lodi Lofa ndiye aliyenifanya niwe namkodolea macho ya kuibia kila sekunde. Alikuwa kijana jamali. Alivutia. Alivutia kwa namna alivyonena na kutenda.

Hakuwa mtu wa maneno mengi. Alipokifunua kinywa chake kuzungumza, hadhira yote ilimpa umakini. Sauti yake mantashau ilipenya masikioni na kukita akilini kama mwangwi.

Ungetamani kuinyamazisha halaiki, sauti yake ipate kukita vizuri, pengine pasipo hata kuelewa azungumzacho. Ungeyataka mateso yake bila chuki.

Mluzi uliponikolea kidogo, nilichangamka. Nilianza kumtazama pasi kuibia.

Nyakati kadha wa kadha, macho yetu yalipogongana nilitabasamu. Mwenzangu aliendelea kuliweka akiba tabasamu lake. Sikuwahi kujisikia hivi siku ya kwanza ya kuonana na mwanaume nisiyemjua katu. Akili yangu yenye kilevi ilitia na kutoa bila majibu.

Si niliapa mimi! Si nilikwishaapa sitaneng’eneka tena?

Sasa ni nini hiki kilikuwa kinanipata?

Ikawa, akiita mhudumu nami natamani kumsaidia kuita. Akiuliza swali miye kicheko hiki hapa. Pombe hizi, ptuu!

Kuna wakati aliinuka, nadhani alikuwa anakwenda msalani. Alipita karibu yangu kabisa. Nikaisikia vizuri ile harufu ya manukato yake. Hesabu za kichwani zikatosha kuniambia haukuwa unyunyu wa bei chee. Naapa, alijua kukisumbua kichwa changu barabara.

Niliitafuta simu, huku glasi ya kilevi ikienda mdomoni kulainisha koo.

‘Huyu Teru ana mje?’ nikamtumia meseji Tutu.

Nilidhamiria kumuuliza, ‘Huyu Teri ana mke’. Ila lile wenge la pombe, ongeza mwanga wa simu, nilikuwa naona batani za simu zimebebana. Nikaandika tu ujumbe ufike pasipo kujali kama nimeuandika sawasawa.

Tutu aliijibu meseji yangu kwa emoji ya kicheko hadi machozi, huku yeye mwenyewe akicheka kwa sauti hadi kuniegemea. Kwa wakati ule sikujua achekacho ila alicheka mpaka wale marafiki zake wengine nao wakaanza kucheka.

Katikati ya kile kicheko, Teri alirejea. Hakukaa. Alimwinamia rafiki yake mmoja na kumnong’oneza kitu.

“Tutu mnaelekea wapi? Teri anasepa hivyo?” yule kaka aliyenong’onezwa na Teri alizungumza kwa sauti ya juu kidogo.

Muziki uliokuwa umetamalaki, ulifanya masikilizano yawe ya kupaziana sauti.

“Mi nipo bado,’ Tutu alijibu akikata viuno vya kumsusia nyakanga.

Alivikatia hapo kwenye sofa tulilokuwa tumekalia huku akifuatisha midundo ya muziki wa bolingo uliokuwa hewani. Pombe ilishampanda kichwani. Kuna muda, Tutu aliishika tena simu yake, akaanza upya kucheka tena kwa sauti.

“Tutu umeshalewa mama inuka basi twende.”

Sauti ya Teri,  sauti ileile nzito ya rijali jamali, iliyobeba mamlaka, ilipita kwenye fahamu zangu kama pepo za Harmattan. Kidogo zinipeperushie ufahamu wangu wote Nikausihi na kuunasihi moyo wangu utulie mjini kuna vya watu. Nao ukanifanyia inda tu.

Nikajikuta nimeinuka kana kwamba mimi ndiye Tutu. Teri alinitazama mithili ya nguzo ya umeme iliyokosa matangazo, kisha akanyoosha shingo kumtazama Tutu aliyekuwa bado ameketi akicheza muziki.

Nilijaribu kumwelekeza ninakoishi, ila wala hakunisikiliza. Ndiyo kwanza alinyoosha shingo kumchungulia tena Tutu kule sofani. Nami nikazuga kumtazama Tutu pia.

Nilianza kujishtukia kuwa pengine nimezidisha kisebengo. Maana mtu niliyekuwa nalonga naye alinitazama, kisha akaachana nami kana kwamba nilikuwa naongea na mtu mwingine nyuma yake. Alionekana wazi kuiweka akili yake yote kwa Tutu.

Sikutakiwa kumlaumu kwa yale majitwezo aliyokuwa nayo. Alimfahamu Tutu zaidi kuliko mimi, hivyo kunipa nadhari yake lilikuwa jambo muhali.

Baada ya maongezi na Tutu, dakika 5 baadaye tulikuwa garini. Mimi na Teri.

Kilichotokea, Tutu hakutaka kuondoka muda ule. Zaidi, miye na Teri tulikuwa njia moja.

Alitakiwa kuniacha njiani, kituoni. Nami ningejua namna ya kufika nyumbani.

Garini, tulikuwa kimya. Kiyoyozi mwanana kikiizungusha hewa iliyonukia vilivyo.

Redioni, nyimbo za mahaba zilipokezana. Sauti ya mwanamuziki wa mkongwe Brandy Norwood ilipoanza kulalamika kupitia kibao chake cha Have you ever, Teri alinyoosha mkono kupunguza sauti ya redio. Sikujua kwanini.

Wakati huo, matairi yalisererekea kushoto upande ambao mita kadhaa mbele palikuwa na kituo ninachoshukia.

Nilitamani kumwomba namba yake ya simu. Nikaona aibu.

Atanionaje. Na hivi alivyo na pozi. Akinijibu vibaya je? Nilijisahili.

Nilitamani japo kumsemesha tu ili nipate kuisikia tena ile sauti yake. Nikaona soni.

Sikuongea njia nzima, halafu ghafla  tu nianze kuongea kama cherehani. Ningeacha wasifu gani? Nikanyuti kimya.

Brandy aliendelea kulalamika redioni, na maneno yake yakaninyong’onyesha zaidi.

Nilikuwa naangukia mapenzini. Oh, moyo wangu.

Sikujua nishike wapi nisizame zaidi.

Au nimwambie ninavyojisikia juu yake? Akinitolea nje je?

Au nimkaribishe chakula cha mchana kesho? Ila watu wa hivi shurti mahoteli ya kifahari, nami kwa hela gani niliyonayo kwa sasa?

Nilijiuliza maswali mara idadi nisiyoikumbuka.

Tukakikaribia kituo cha kushukia, moyoni nikipaparika.

Teri, geuka hata unitazame tu basi!



Dua yangu haikujibiwa. Macho ya Teri yalikuwa mbele. 

Nilikilaza kichwa changu upande wa kushoto, macho yakitazama dirishani. Wakati huo tulishakikaribia kabisa kituo. Utimamu wa akili yangu ukaanza kurejea. Lile wenge la mapenzi ya ghafla likaanza kunivuka. Nilianza kutafakari mwenyewe kichwani; hivi nikishuka pale kituoni nitafikaje nyumbani kwangu? 

Ulikuwa usiku wa saa saba kasoro vichapo kadhaa. Umbali wa kutoka kituoni hadi kwangu haukuwa mkubwa sana. Hata hivyo, kwa muda huo, mitaa ya huku kwetu huwa imeshakuwa na ukimya wa kusisimua. Kwa mtu mwoga, kivuli chako mwenyewe kingeweza kukupigisha yowe kuwa unanyatiwa na mtu.

Nilivyokuwa zuzu na nusu, sikuyawaza yote haya tangu natia mguu kwenye hili gari. Nilikuwa nimetuna tu humo ndani kama jagi la maua. Nikimuwewesekea mwanaume. Mwanaume ambaye uwepo wangu haukumchezesha hata mshipa wa fahamu. 

Umajinuni mtupu!

Niliendelea kuwaza, sijui nianze kumtafuta bodaboda wangu Shomari Kipande au nimwite yule mtu wa bajaji, ‘nani sijui.. nani huyu … aargh!’ 

Nilighadhibika kulisahau jina la mtu wa bajaji. Nikasonya kwa sauti. Nisikumbuke niko kwenye mkoko wa watu vo! Baada ya msonyo kunitoka tu ndiyo nami nikagutuka toka mawazoni. 

“Oh! Samahani sana…” nilitamka nikigeuka kumtazama Teri huku nikiwa nimekishika kifua changu kana kwamba kilitaka kuchomoka na ule msonyo. 

Kwani alijibu? Wapi! 

Alinitazama na kuachia tabasamu fulani la kutanua papi za midomo pasi kuonyesha meno. Kisha, alilikata lile tabasamu kwa kuzizamisha papi za midomo yake kwa ndani, wakati huo akisereresha gari kuingia kituoni kabisa. 

Akasimama.

Nilichungulia nje kijanja. Kituo kilikuwa kimya. Hakukuwa hata na paka wa kumtupia jiwe. Nilishusha pumzi ndefu nikiukumbatia vyema mkoba wangu tayari kushuka. Dakika hizo, sikumuwaza tena Teri. Hofu ya kubaki mwenyewe kituoni na kule kutokujua nitafikaje nyumbani, ndiyo viliutafuna ubongo wangu.

“Asante sana… usiku mwema,” nilimshukuru. 

Naye alitikisa kichwa chake juu chini kuiitikia shukrani yangu.

Kabla sijashuka. Simu yake iliita. Aliitoa mfukoni, nami nikawa namtazama anavyoipokea na kuzima redio garini. 

Aliiweka simu hewani, mbele yake, na kuruhusu sauti kubwa. 

Nilikuwa nangoja amalize maongezi yake, japo nami nimpe mkono wa kwa heri.  Licha ya yeye kutonichangamkia, mwenzie moyo ulikuwa taabani. Moyo wangu uliozoea kibatari ulikuwa umekutana na kandili. Tafrani!

“Halo Teri, bado upo na Mima?” niliisikia sawa sawia sauti ya Tutu.

“Yeah!” alijibu. 

Alinitazama kwanza kwa jicho pembe, kabla ya kurejesha macho yake simuni.

“Please! Naomba umfikishe kwake. Please Teri mida hii si mizuri ujue… au hata msubiri basi apate usafiri wa kumfikisha kwake. I know this is too much to ask… ila nakuomba at least usimwache mwenyewe hapo kituoni. Nakuomba Teri jamani!” Tutu alikuwa anaongea harakaharaka kwa sauti ya kurai. 

Teri alishusha mzigo wa pumzi. Pumzi iliyoinuka na kushuka na mabega yake. 

Hakujibu chochote.

“Haloo… Teri!... Teri!” Tutu aliita simuni.

Teri aliileta simu karibu na mdomo wake na kujibu, “Sawa!”

Alikata simu na kuitupia pale kwenye kirungu cha kupangulia gia. Hakukuwa na haja ya kunieleza chochote. Sote tulikuwa tumeyasikia vyema maneno ya Tutu. Aliushika usukani tayari kuliondoa gari eneo lile. 

“Tunaeleka wapi?” aliniuliza pasipo kunitazama. 

Alikuwa anatazama upande wa barabara akijiandaa kulirejesha gari barabarani. 

Manyunyu ya mvua nayo yalianza kama mzaha.

Nami nikaanza kumwelekeza njia. Huenda, nilitaraji huu ungekuwa mwanzo wa maongezi marefu kati yetu, walakini haikuwa hivyo. Muda mwingi Teri alikuwa kimya zaidi. Kumzoea bwana huyu ilikuwa kama kujitwika kiroba cha misumari ya moto pasipo kutukutia.

Dakika 10 hivi, tukawa tumefika mbele ya nyumba ninayoishi. 

Yale manyunyu ya ta! ta! ta! yakawa yameshakuwa mvua ya kuleta maafa. 

Nilimpa mkono wa kuagana, naye akaupokea. Niliteremka mbiombio, mkoba wangu kichwani kulinda nywele zangu. Sijui hata kama nilizilinda kweli. Kwanza nadhani mbio nilizopiga zilimchekesha yeyote aliyeniona wakati huo. Nilikuwa nayumba kama kuti!

Kufika mlangoni, nikaukumbatia mkoba kifuani wakati nikiupekua kutafuta funguo. Nikazipata. Shughuli ikawa kuuchomeka ufunguo mlangoni. Wenge lilikuwa linanifanya nichomeke ufunguo wa mlango wa mbao kwenye ule mlango wa chuma. Nikahangahanga kwelikweli. 

Upepo nao ulikuwa unaelekea pale niliposimama, changanya na ile mvua. Nilionekana kama mwizi hapo mlangoni.

Katikati ya kukurukakara zangu, nikahisi kukingwa kwa nyuma. Nikaacha purukushani za mlango na kutulia kidogo. Kifua kikipanda na kushuka. Ile harufu ya manukato iliyotoka nyuma yangu kuja puani, ilinifanya nimeze funda la mate kwa taabu kidogo. Alikuwa Teri. 

“Hebu leta hizo funguo,” alitamka kwa sauti ya kunong’ona. 

Ile pumzi yake ya mdomo iligota sikioni. Vinyweleo vikanisimama. Shetani alivyo hana maana kabisa, akanikwapulia akili na kuniachia kichwa kitupu mithili ya mtungi uliotoboka.

Niligeuka nikiwa nimelowa chapachapa. Mkoba wangu na funguo kifuani. Badala ya kumpatia funguo alizoomba, nilimtazama usoni. Tukatazamana kwa sekunde kadhaa. Kope zetu zikifumba na kufumbuka kichovu. Hakuyakwepa macho yangu, nami sikuyakwepa yake. 

Ile mvua sasa ilikuwa inampiga yeye, mgongoni. 

Nadhani kuna lugha iliyosahaulika kule mnara wa Babeli iliibukia hapa. Macho yetu yaliiongea hiyo lugha katikati ya ile mvua. Huko alikombilia na akili yangu, shetani aliyekuwa ananema, akapiga msamba wa ushindi. 

Nilimsogelea zaidi. Urefu wake uliiadhibu shingo yangu, lakini sikujali. Sikujali hata kidogo. Wakati nikiviinua visigino vyangu kuukaribia mdomo wake, macho yangu malegevu yalifumba taratibu.

Mkono wake wa kuume ulipita mbavuni na kugota mgongoni. Alinipokea, akanimiliki. Kwa pupa isiyoumiza, huba jingi na utaalamu wa kutosha. Tuliyumba huku, tukayumba kule. Tusiijali ile mvua pale mlangoni. 

Aliniachia, akirudia kunitazama usoni. 

“Mima…” aliita kwa sauti ya kubembeleza. 

“Abee!” nikaitika hali tukiendelea kutazamana.

Sikumbuki ilikuwaje baada ya hapo mpaka kujikuta uwanja wa fundi seremala. 

Kwa mdundiko uliochezwa, nilijiapiza nafsini pale ngomani. Ningemfanya Teri kuwa manju wangu wa maisha. Treni ilikuwa imefika Kigoma mwisho wa reli. Ngariba alikuwa anajua kukitumia kisu chake. Mkwezi alikuwa amedondosha nazi za mwaka mzima kwa ufundi wa hali ya juu.

Kandoni mwa kitanda changu. Kulikuwa na kijistuli kilichobeba taa ya urembo. Kando ya taa hiyo, kulikuwa fremu yenye picha. Picha ambayo nakiri haikustahili kuwa hapo.

Ilikuwa picha ya mimi na yule mwanaume niliyekwishaachana naye. 

Ilikuwa picha ya enzi hizo tukiwa tunaimiliki dunia ya mahaba. Siku zote ilikuwa hapo. Si kwamba nilikuwa namkumbuka, la hasha! Ilikuwa ni picha yangu ya kwanza mimi kwenda kuipigia studio. Na vile nilivyopendeza, ndiyo sababu hasa ya mimi kuendelea kuiweka pale.

Katikati ya mchakato, ghafla Teri alijiinua kwa kasi ya ajabu mno. Macho yake yakiwa kwenye ile picha pembeni ya taa. Kwa namna alivyoshtuka na kuruka, hata mimi niligutuka. 

Nililikusanya shuka haraka na kulivutia kifuani. Macho ya Teri bado yalikuwa yameganda kule kwenye taa.

Huku midomo yake ikimwemweseka. Teri aliyarudisha macho yake usoni pangu. 

Safari hii akiwa na sura mpya kabisa.

“Huyu... huyu si... si ni Boazi?” aliniuliza kwa sauti yenye kitetemeshi. 

Mboni zake zikicheza kulia kushoto. Kidole chake cha shahada kikiisonta ile picha na uso ukinitazama mimi.

Niligeuka na kuitazama ile picha, kisha nikamjibu kwa wasiwasi, nikitikisa kichwa juu chini. Sikuelewa ni namna gani alilifahamu jina la huyu mpenzi  wangu wa zamani na kwa nini alishtuka namna ile.

Teri alihema kwa  kishindo. Alijiinua toka kitandani. Pasipo kunisemsha kitu aliingia bafuni. Bafu lililokuwa mumo humo chumbani. Nami niliinuka kumfuata nikiwa naburuzana na mashuka yangu mwilini. Alijifungia huko. 

Nikamuita kwa sauti nikiugongagonga mlango, huku nikihoji juu ya mabadiliko yale.

“Teri!…Teri kuna nini?” nilihoji kwa unyonge nikiwa  pale mlangoni. 

Hakunijibu.

Alipotoka alivaa harakaharaka nguo zake, vilevile zikiwa zimetota. 

Nilimfuata nyuma wakati akikivuka kizingiti cha mlango wa chumbani kuelekea sebuleni. 

Mvua nayo ilikuwa ingali ikinyesha japo si kwa kasi ile ya mwanzo. Miale ya radi ilipasua anga na kupenya vyema ndani. Mwanaume aliyeniwewesesha alikuwa ananiponyoka mithili ya maji kiganjani.

“Hunitendei haki Teri, what is happening?” nilibabaika.

Roho ilikuwa inaniuma.

Alienda mbele, akarudi nyuma. Akaweka mikono kichwani. Mikono iliyoparaza kichwa toka utosini hadi shingoni, ikagota hapo. 

“Shiiit!!” Alilaani kwa ghadhabu akirusha ngumi hewani.

Alienda mpaka mlangoni kisha  akarejea kwangu kwa kasi, huku akihemea mdomo.

“Mima...” alinitazama kwa macho yake mazuri. 

Macho ambayo sasa yalijaa kiwewe zaidi. Akaendelea, “Fanya kama vile hatujawahi kuonana… sawa? hatujawahi kufanya chochote… sawa Mima? Iwe hunifahamu nami sikufahamu, naomba iwe hivyo.”

Kwa mara ya kwanza tangu tufahamiane, alizungumza nami kwa sentensi ndefu. 

Kilichoniuma, zilikuwa sentensi ndefu zilizoukwangua moyo wangu na kuniadhibu. Ni heri basi asingeongea kitu. Ni heri angeondoka pasi kusema neno. Sikujibu, ningejibu nini. Ghafla tu kuna donge la jazba lilinikaba kooni. Machozi yakanilenga.

“Unasemaje?” nilimkunjia ndita usoni

“I’m sorry!” alitamka kwa upole akitaka kunigusa, nikaipangua mikono yake.

“Baada ya hiki kilichotokea hapa ndani, unaniambiaje!?” nilijitutumua kumsaili tena, koo likididimia ndani kwa hasira na uchungu.

“Mima huwezi kunielewa.”Alitaka kunigusa tena, nikampa ishara ya kutonikaribia. 

 “Naomba kwa sasa iwe hakuna kilichotokea. Sahau kuhusu hilo… nakuomba hii  ibaki kuwa siri kati yetu. Tuyazike humu ndani. Nisamehe kwa hili Mima… I’m so sorry,” alinivunja nguvu zaidi. Akageuka kuufuata mlango. 

Nilimtazama namna alivyoufungua na kutokea nje. Nilitembea kwa kuburuza miguu na kusimama mlangoni. Nilimwangalia vile alivyotembea kwa kasi mvuani kulifuata gari lake. Kweli, aliingia garini  na kutokomea. Nilikuwa natamani iwe ndoto. Nilikuwa natamani kumwita, naye ageuke akicheka na kusema ule ulikuwa utani. 

Haikuwa hivyo. Teri hakugeuka, alitoka akatokomea.

Nilisimama pale kizingitini kama punguani. Machozi yakianza kunitoka. 

Kila kope zangu zipofunga na kufunguka michirizi ya machozi ilifanya njia mashavuni. Baada ya mwaka mzima wa kujilinda na kujitunza. Nikiruka viunzi vya aina zote. Nilikuwa nimeishia mikononi mwa mtu katili kirahisi hivi, kijinga namna hii. 

Nilihisi hasira mno.

Boazi ni nani kwa Teri mpaka anibadilikie hivi. 

Mungu wangu ni nini hiki tena? Kuna majuto makali sana yalipita nafsini. Nilitamani kuurudisha wakati nyuma na kubadili kila kitu. Hata gari la Teri nisingepanda, labda nisingemtazama kabisa.

Nilirudi ndani, mwili ukitetemeka. Nikaitafuta simu yangu mkobani. 

Nilikuta ikiwa na missed calls kibao za Tutu. Sikuzijali. Nilikuwa naisaka namba ya Boazi kama bado ipo simuni. Niliisaka huku machozi yakinitiririka bila kuyafuta. Pombe yote ilinitoka kichwani.

Kwa mara ya kwanza baada ya mwaka kupita, nilitamani kumpigia simu ex wangu Boazi. Nilitamani kumuuliza juu ya jina Teri Balokwa. Niliamini ingenipa ahueni.

Teri alikuwa nani? Alikuwa ni nani hasa!?



Niliendelea kuisakanya namba ya Boazi kwenye listi ya majina.

Pruuu! kwenda juu. Pruuu! kushuka chini.

Niliisakanya mara idadi isiyokumbukika. Hata akili yenyewe ilishindwa kujua cha kufanya. Hivi huyu mjusi nilimsevuje jamani? Nilijiuliza, vidole vikiendelea kuyapandisha majina na kuyashusha.  Sikumwona Boazi wala chochote cha kumfanania. Msonyo wa nusu kilo uliniponyoka wakati nikiidondosha simu mapajani.

Mikono ikikutana utosini.

Machozi yalikata kama pombe ilivyokata kichwani, ila maumivu nafsini yalinigomea. Nilikuwa naumia sana kiasi cha kuhisi uzito kifuani. Au nimpigie Tutu usiku huu nimweleze kisanga kilichonikuta?

Kwamba, baada ya kukitunza kitalu changu mwaka mzima, kirahisi tu, shetani alinikwapulia akili nikajikuta nimesaula kwa Teri Balokwa. Saa chache tu baada ya kuonana naye.

Halafu? Niseme nikabwagwa chapuchapu kama kiroba cha taka. Niseme hivyo? Si nitaonekana nina mdondo wa kichwa.  Wanasema hakuna kovu la masimango lakini johari za mja ni mbili; akili na soni.

Nilijitazama vile nilivyokuwa nimejitundika mashuka mwilini kama myahudi wa kale. Nilijihurumia mwenyewe. Nimepatikana Mima mimi. Yaani kimenikuta kile Kigawo Kikubwa cha Shirika a.k.a KKS. Nimegawanywa sijabaki hata na akili moja kichwani.

Usiku ule sikulala. Nilijiegesha tu kitandani.

Akili ilipotulia ndiyo mambo ya msingi yakaanza kutiririka kichwani. Hivi ningeipata namba ya Boazi na kumpigia ni nini kingetokea? Teri si alisisitiza nikae kimya? Hivi nikikaa kimya nitapungukiwa nini? Kuhusu kinga je? Sikutumia vo! Kuna magonjwa ya zinaa, kuna mimba.

Toba! Toba! Yarabi! Vipi kama ndiyo tayari?

Niliwaza mpaka nikatamani kupiga nduru.

Niliinuka kwenda msalani, ambako hata kushuta tu sikuweza. Nikarudi kitandani pale.

Eneo lilelile nililokuwa nikinyanyua miguu nusu ya kuitundika dirishani kwa raha niliyokuwa nakopeshwa. Eneo lilelile nililopiga miondoko ya nzawise nusu ya kutegua nyonga. Saa hizo nilikuwa nalitazama eneo hilohilo kama kichaka cha michongoma. Kisichositiri wala kuhifadhi.

Chambilecho wenye kauli zao, kikupacho utamu na uchungu kitakupa.

Hauchi Hauchi kukakucha. Nilidamka japo ilikuwa Jumamosi. Siku ambayo ilikuwa ya mapumziko kwangu. Bado nilikuwa njia panda na hali ya kiwewe nafsini haikuniisha. Namba ya Boazi sikuwa nayo lakini nilikuwa najua wapi pa kumpata. Nilijua anakofanyia kazi Boazi. Teri je? Zaidi ya kulijua jina lake la pili hakuna kingine. Lahaula Walakuata!

Mzigo wa hofu, maumivu ya nafsi na hasira vilicheza ukuti na moyo wangu. Nikalia tena. Nikaomboleza sana. Peke yangu, kimya kimya. Sala za toba na rehema zikinitoka. Nilishinda siku nzima nikiwa mnyonge sana.

Tutu aliponitafuta kucheki kama nilikuwa sawa. Nilimdanganya, ingawa alihisi kitu kupitia sauti yangu dhaifu.

Jumapili asubuhi niliamkia hospitali. Nilienda kucheki afya. Kila kitu kilikuwa sawa. Nilipata afueni kidogo. Nilipotoka hospitali, nilipita kwa Tutu. Tutu ni rafiki yangu. Lakini pia, tunafanya kazi jengo moja ijapokuwa kampuni tofauti.

“Huonekani kuwa sawa Mima, nini shida?” Tutu alinihoji.

Sikumjibu.

“Hatutatui matatizo kwa kuyaficha, ndiyo maana tuna marafiki,” aliendelea kunisihi nizungumze.

Suala la Boazi kutajwa na Teri bado lilikuwa linautesa moyo wangu kimyakimya. Zaidi, moyo ulikuwa umekwama kwa Teri, sikujua ni kwa mapenzi au hasira. Waliowahi kuipitia hii hali wanajua. Vinginevyo, isipokuwasha basi hujailamba.

Sikumweleza Tutu chochote. Sikujua nianzie wapi.

Ila, pamoja na yote hayo bado nilikuwa nahitaji maelezo kutoka kwa Teri mwenyewe. Walau, nipate kujua nini kilimfanya anifanyie vile. Alikuwa ameniumiza sana kibinadamu.

Kuna mfadhaiko ulikuwa unanitafuna vibaya mno. Siku hadi siku, nilikosa furaha. Nilianza kukonda. Uso wangu ulipoteza nuru. Teri alikuwa ananitesa kuliko hata Boazi niliyedumu naye miaka. Nafsi ilikuwa inataka kuongea na mtu, lakini nani sasa? Tutu? Angenionaje? Angenihukumu vipi?

Nikafa na tai shingoni.

Mwezi mmoja na wiki mbili hivi vikapita tangu tukio lile litokee. Nikiwa naamini kuwa sasa naelekea kuyazoea maumivu mapya. Ilitokea tu. Nikadondoka ofisini. Wakanibeba juujuu hadi hospitali. Ikiwa tayari nilishaishiwa nguvu kama siku mbili nyuma hapo ofisini.

Majibu niliyotoka nayo huko hospitali yalinifanya nimfuate Tutu kwake baada ya kumkosa ofisini kwake.

“Mpigie Teri simu, mwambie anitafute sasa hivi,” nilimweleza nikiwa wimawima. Mara tu baada ya kuingia ndani mwake.

‘Kuna nini Mima?’ Tutu alinisaili kwa wasiwasi.

Sikumjibu, niliifuata simu yake iliyokuwa kwenye sofa, nikaileta na kumpatia mkononi.

“Mpigie tafadhali!” nikatamka machozi yakinilenga.

“Unaweza kuniambia nini kinaendelea?”

“MPIGIE SIMU TERI… HIVI HUNIELEWI?” nilimpayukia nikihema kwa nguvu.

“Mimaaa!!!” alinishangaa maradufu.

Nilimpora simu yake. Nikaanza kutafuta jina Teri kwenye listi ya majina. Nikalipata.

Nikampa simu.

Aliipiga ile namba huku akiendelea kunitazama kwa mashaka. Simu ilipopokelewa. aliongeza sauti nami nipate kumsikia Teri.

“Haloo…” Tutu aliita huku akinitazama mimi.

“Yes T!” Teri alijibu, akimwita Tutu apendavyo kumwita.

“Mima ana shida nawe anase…” hakumalizia.

“Mima? Mima yupi?” sauti yake ilijaa mshtuko.

“Mima, rafiki yangu.”

“Oh, T… habari za huyo Mima kwa sasa hapana… Hapana Tutu, niko busy sana now.”

“Teri siki…”

Alitukatia simu.

Tukampigia tena, hakupokea. Nikakopi namba yake, nikampigia kwa simu yangu, hakupokea. Alipopigiwa mara ya nne, akazima simu. Nikadata. Nikadata kwelikweli!

Tutu akawa anahaha kuniuliza kilichotokea. Bado alikuwa gizani.

Aliponibana sana, nikabwatuka.

“Nina mimba!”

“Mimba?! Ya nani?” alihamanika

“Ukimpata Teri hewani… mwambie nimeenda kuonana na Boazi.” Sikujibu swali lake.

Akaduwaa. Mdomo ukiachama taratibu ilhali macho nayo yakitanuka polepole. Pengine ombi langu lilimpa jibu. Nilimwacha hapo akiwa amenitolea macho pima. Nikatoka nje mbiombio. Nilimsikia alivyokuwa akiniita kwa wahka, ila sikugeuka.

Teksi niliyokuja nayo bado ilikuwa inanisubiri nje kama nilivyoomba inisubiri.

Niliingia garini machozi yakiwa yameshaanza kutiririka. Nikapambana yasimwagike, nikashindwa. Nikalia kwa kwikwi. Dereva wa teksi aligeuka kunishangaa na kule nje Mima akija kwa kasi.

“Tuondoke…” nikatoa kauli moja kwa kujikaza na teksi ikaondoka.

Niligeuka nyuma kumtazama Tutu aliyekuwa anaikimbilia teksi huku akiniita kwa nguvu zote.

Haikusaidia kubadili mawazo yangu. Jeuri ya Teri ulikwishanitibulia nyongo.

Nakwenda kweli kwa Boazi, kumweleza nini? Nikawa najiuliza.

Hasira na uchungu vilikuwa vinanitafuna mpaka kwenye mifupa. Tulipoingia barabara ya lami, nilimwambia dereva anipeleke Kijitonyama. Ilipo ofisi ya Boazi. Sikufikiria mara mbili na wala sikuwa na mood ya kufikiria kitu mara mbili.

Nilishavurugwa! Nikaitamani akhera ilhali ya duniani sijamalizana nayo.

Simu yangu ilipoanza kuita. Niliitumbukiza mkobani nikaachana nayo, mpaka ilipoacha kuita.

Nilimkuta Boazi.

Baada ya mwaka mzima kupita, nilikuwa nimesimama mbele yake nikiwa namna hii. Vululuvululu!

“Mima! “ aliniita kwa mshangao mkubwa wakati akikimbilia kuufunga mlango wa ofisi yake. Niliingia hata pasipo sekretari wake kuniruhusu.

“Nahitaji kuzungumza na wewe kitu muhimu sana, una nafasi?” nilimuuliza mara tu aliporejea mbele yangu baada ya kuufunga mlango.

Sura ya Boazi ilibadilika polepole. Toka kwenye mshangao wa kutanua uso mpaka kwenye mshangao wa kukunja ndita.

Kabla hata ya kunijibu chochote simu yangu ilianza tena kuita kwa fujo. Niliitoa mkobani nikaileta usoni.

Ooh! Alikuwa Teri Balokwa! Nilitabasamu kifedhuli kwanza. Nilikuwa na hasira mno. Iliita sana ndipo nikaipokea.

“Mima si tulishaongea kuhusu hili…” alinidaka haraka.

“Nani mwenzangu?” nilimuuliza kwa kedi, nikijua wazi Tutu alishamfikishia ujumbe.

“Mima acha hizo basi, njoo tuongee kwanza. Sikujua kuhusu mimba… wait… muweke Boazi nje ya hili… njoo tuongee kwanza mama… nakuomba… nakusihi sana sana Mima wangu pleeease!… Mima naku...” japo aliongea kwa kubembeleza vilivyo sikumwacha amalizie nikakata simu.

Alipiga tena, nikakata. Akapiga tena, nikakata. Nikazima simu.

“Ni nani huyo?” Boazi aliniuliza akinisogelea.

Makumi ya majibu yalikimbizana kichwani.

Niseme au nisiseme!




Sikumjibu. 

Akili yangu iliingia kwenye mabishano ya sema usiseme. Niliirudisha simu mkobani huku nikishusha pumzi yenye ratili za kutosha. Mpaka hapo shetani naye alishanigusa bega la kushoto na kuninong’oneza, ‘Jeuri mwenziye kiburi Mima, hebu bananga mambo bwana umkomeshe yule baradhuli!’

Nilimeza tena funda la mate, safari hii kwa taabu kidogo kana kwamba nilikuwa naimeza shilingi hamsini. 

Boazi aliacha kunitazama vile nilivyokuwa nimesimama mbele yake kama gogo la buchani. Akanionyesha sofa la wageni niketi, huku yeye akielekea mezani pake. 

Nilimsindikiza kwa macho, alivyoifuata simu ya mezani kwa minajili ya kuagiza kipooza koo. Sikumshangaa yeye kuinua simu na kuagiza kinywaji kilekile nikipendacho, bila hata kuniuliza. Baada ya mwaka mmoja wa ukimya kati yetu, bado alikuwa anakumbuka barabara ni nini hasa nilikuwa nikinywa kila mara nilipokuwa katika hali kama ile isiyoeleweka mbele yake.

Alinifanya nimkumbuka yule afriti aliyekuwa simuni akimuuliza Tutu, ‘Mima yupi?’

Boazi alikuwa anajua kujali akiamua kujali. Ugomvi wetu ulikuwa unaletwa na kule kununa kwake, au sijui niseme kupotea. Angeweza kunikalia kimya miezi miwili hata mitatu. Kimya ti! Kama kivuli. Ningelia, ningejiombesha msamaha usio na kosa. Ningeneng’eng’eka mimi nusu ya kufa. 

Halafu ghafla tu, angerejea na zawadi kabambe na maneno kemkem. Ningesamehe yote na huba kuchipuka upya. Ningepewa mahaba niparure tani yangu. Kisha boom! Angetoweka tena. 

Kwa kuwa tulikuwa na uhusiano wa kimyakimya, sikujua pa kumshtakia. Nilipomfuata kwake mara nyingi sikumkuta pia. Basi, tukawa wapenzi wa kukaliana kimya na kurudiana. Mpaka nilipojuhudika kufanya maamuzi magumu.

Nilijiongeza tu, lazima kutakuwa na mtu wa tatu kwenye penzi letu. Nilimzika kwa block kila kona na matanga juu nikamwekea.

Nilikuja kumu-unblock baada ya miezi mingi sana kupita. Tena baada ya kupata kazi na kuhama kimyakimya pale kwa dada yangu nilipokuwa naishi. Maisha yakasonga.

Boazi alipomaliza kuagiza vinywaji, alinifuata akanishika mkono na kuniketisha sofani. Tulitazamana usoni wakati nikimwemwesa midomo yangu tayari kuyachimba matatizo. Oh! Boazi jamani. Nilinung'unikia moyoni.

“Boazi…” niliita kisha nikasita kwanza. 

Moyo ulikuwa unanienda mbio hasa. Nilijiinamia na kufumba macho huku nikiiuma midomo yangu kwa ndani. Nilitaka kuomba dua, nikashindwa. Mishipa ya koo ilinisimama wakati nikilitafuta neno sahihi la kuanza nalo.

Nadhani aliiona ile hali yangu ya kubabaika. Nilikigusa kiganja changu na kukishikilia kwa nguvu. Mkono wake mwingine ulikishika kidevu changu na kukiinua kichwa. 

Niliinua kichwa na kumtazama usoni. Akatabasamu. 

“Nakuelewa Mima. Mimi pia sijawahi kukusahau. Nilipogundua umeniblock niliumia mno. Niliumia sana. Kwa mara ya kwanza maishani nilijua nimekupoteza moja kwa moja.” 

Alikuwa anaongea taratibu. Kwa mahaba ya wazi kabisa. Lakini hili si jambo lililonileta hapa. 

“Boazi…!” nilimwita tena katika namna ya kumkatisha. Kwa vyovyote vile, Boazi alikuwa amechanganya ujio wangu pale na uhusiano kati yetu. Sikuwa pale kwa ajili yake.

Nilipomwita, alikiweka polepole kidole chake cha shahada katikati ya midomo yangu. Alikitelezesha kidole kile kimahaba na kuiparaza midomo yangu taratibu kuninyamazisha. Akaendelea.

“Mima, niliiombea nafasi hii. Mungu akurudishe kwangu. Ulete furaha maishani mwangu. Nilijua nikikufuata hutanipokea, hutaniamini kwa kuwa nimeshakuumiza mara nyingi... sikuwahi kuombea mwanamke anirudie ila kwako nimefanya Mima… niliapa ukirudi kwa namna yoyote sitafanya ujinga wowote tena... nashukuru umekuja wakati sahihi… I still love you and i still need you… chochote unachotaka kuniambia, niambie ukijua bado nakupenda sana, pengine na zaidi. Nitafanya chochote kwa ajili yako. Niruhusu nikupende kwa dhati sasa, niruhusu Mima.”

Alitulia akinitazama. Uso wake mtulivu ulijaa mahaba na huruma. Nilizikokota pumzi ndefu. Hii risala  yake tamu kuja kwangu, ilikuja wakati mbaya sana. Mungu wangu! Hiki ni nini sasa. Niliwaza kichwani, mawazo yenyewe yakikosa mpangilio unaoeleweka. 

Niliikumbuka hasira yangu kwa Teri. Nikarudi kwenye mstari. 

“Boazi, sijaja kuzungumzia kuhusu sisi. Nisamehe kwa hilo, nisamehe sana. Ila kuna kitu nataka kukuuliza.”  Nilinyoosha maelezo.

Hakujibu kitu, alinitazama tu kisha akainamisha kichwa chini. Sijui jibu langu lilimkata maini kiasi gani. Koromeo lake lilipanda na kushuka, likadidimia kuonyesha ni namna gani aliyameza maelezo yangu kwa shida. 

“Uliza!” alitamka uso wake ukiwa bado umetazama chini. 

“Unamfahamu… unamjua… I mean… una... una… Teri Balokwa ni nani?’ nilinyoosha swali langu baada ya kigugumizi cha ghafla kunitembelea. 

Kule kutazama kwake chini ndiyo kulinijaza nguvu zaidi ya kuuliza hili swali.

Taratibu, Boazi alikiinua kichwa chake na kutazama mbele. Aliyafinya macho yake kidogo kwa mkazo kisha akageuza shingo kunitazama. Ni kama vile alinisikia ila hakunielewa, na kama alinielewa basi hakuamini alichosikia . 

“Hebu rudia ulichouliza,” utulivu wake ulinitisha.

“Te..te…ri Balokwa ni nani?” 

“Teri Balokwa ni nani!!?” sauti yake ilitetemeka wakati akilirudia swali langu kwa mtindo wa kushangaa.

Macho yake yalitanuka. Wakati akinitazama hivyo, mlango uligongwa kidogo na kufunguliwa. Alikuwa sekretari wako akiwa na chano chenye vinywaji. Boazi alimtazama yule sekretari wake huku akiwa amemtolea macho!

Alimtazama vile alivyoweka chano kule mezani na kutukaribisha. Alimtazama anavyoishia na kuufunga mlango na macho yake yakaganda mlangoni. Kifua chake kilipanda na kushuka dhahiri.

Nina uhakika, yale yote aliyokuwa akiyatazama hayakuwa akilini mwake. Si ajabu hakumwona hata huyo sekretari machoni pake. Ghafla, kama mtu aliyezinduka kidogo, Boazi aliinuka na kusimama mbele yangu. Nililaza kichwa nyuma ili kumtazama usoni. 

“Kwa nini unaniuliza habari za Teri?” aliniuliza kwa upole kabisa. Upole ambao nilijua wazi ulikuwa upole wa mamba.

“Nina shida naye…” nilimjibu nikiinuka pia.

“Ipi!?” alifumbata mikono kifuani

Nikakwama. Majibu yaliyonijia kichwani yaligongana vibaya mno. 

“Amekufunua tayari?… na wewe umeangukia mikononi mwake?!” maswali haya yalitoka kwa upole tu ila yalinifikia kama kejeli fulani. Alibebetua mdomo wake kwa kinyaa wakati akisubiri jibu langu.

Sikujibu, nilijiinamia. Alikuwa amekisia sawasawa. Ajabu!

Nilimsikia akicheka. Akacheka kwa sauti ndogo iliyopanda sekunde hata sekunde. Kicheko chake kilinitisha. Kwa sababu alicheka kama mtu aliyewehuka. Alicheka uso wake ukiwa na ghadhabu. 

“Nijibu Mima! Umefanya nini? Umefanya niniiii? Nijibu… umelala na Teri?” aliacha kucheka na kunipayukia kwa hasira, macho yake yakimwemweseka vibaya mno.

“Boazi sikiliza kwanza basi, nami nilipayuka kwa kiwewe nikitaraji walau angetulia. 

Ndiyo niliharibu kabisa!

Mwenyewe nilikuwa najiandaa kukanusha. 

“Boazi kitu gani… nisikilize nini? Nini Mimaaa?” aliunguruma akikishika kichwa chake kwa mikono miwili akiwa amenitolea macho kiasi cha kunitetemesha. Ni kama vile alijishika vile ili kujizuia asinitie mikononi. Ama pengine alitamani kuking'oa kichwa na kukitupilia mbali. Sijui! 

Alihemea  mdomo kwa sauti, tena kwa nguvu. Niliogopa, niliogopa sana.

Alitoka pale nilipokuwa nimesimama na kuifuata meza yake. Akaibamiza kwa pigo moja kali akiwa anaendelea  kuhema kwa fujo. Sikuwahi kumwona Boazi akiwa katika hali hii. Shetani aliyenisukuma niyabanange alishasepa, nikabaki kumuita Mungu anisaidie!

“Teriiiii!... That bastard!... Damn youuu! Aaargh” kauli yake ilienda sambamba na mngurumo wa hasira, kisha mparazo wa mkono wake juu ya meza. Mparazo uliosomba baadhi ya vitu mezani likiwemo lile chano la vinywaji na kulisereresha kuelekea chini, umbali mfupi tu toka niliposimama. 

“Uwiiii!” niliruka hatua moja nyuma na kuliparamia kochi nikiachia ukelele wa hofu na mshtuko. 

Mikono yangu ikiziba masikio, kukabiliana na sauti ya mpasuko wa vitu sakafuni.

Nadhani, mdondoko wa chano, kuvunjika kwa bilauri na chupa za vinywaji pamoja na ule ukelele wangu, viliwashtua watu kule nje ya ofisi, akiwemo yule sekretari wake. 

Haraka aliufungua mlango na kusimama kizingitini

Wakati huo, tulishuhudia Boazi akielekea nyuma ya meza na kuvuta saraka ya chini. Akaikwanyua bastola iliyokuwa sarakani humo na kuishika mkononi. Mkono uliokuwa unatetemeka waziwazi.

Amba! Yule sekretari  kule mlangoni aliiona milango ya kuzimu kabla yangu. Alitoweka katika namna ambayo sikuelewa ni kukimbia au kupaa. 

“Mungu wangu… Mungu wangu!” niliachia kibwagizo.

Nikaliparamia kochi na kujitutumua kudumbukia kule nyuma ya kochi. Japo sikutoshea, ila angalau niliweza kuhifadhi nusu ya mwili kikiwemo kichwa.  

Kifo huwa kinakupa tiketi moja tu, ya kwenda! Ukienda umeenda. 

Niliposikia ukimya kidogo nilichomoa kichwa toka kule nyuma ya kochi. Haraka, nikiwa na wenge fulani, nikatazama huku na kule nikimtafuta Boazi. 

Hakuwepo! 

Nilikimbilia dirishani, nikivivuka kwa kurukaruka vile vitu vilivyolala shaghalabaghala sakafuni. Nilimwona Boazi akielekea eneo la maegesho. Nikaunyakua mkoba wangu nami miguu ikichanganya hatua za kukimbizia jogoo la shamba.

Nilifika nje ya ofisi. Gari la Boazi lilikuwa linaanza kutoka eneo la maegesho. Nikajua kumzuia pale nisingeweza. Nilikimbilia getini. Nikatoka nje ambako kulikuwa na kituo cha teksi mchanganyiko na bajaji. Nikaikimbilia bajaji moja na kujitoma.

“Tunaifuata hii gari kaka. Usiipoteze tafadhali. Gari hiyo… hiyo inayokata kona,”  katikati ya pumzi ndefu zilizokosa mlingano wa kuingia na kutoka,  nilitamka mkono  mmoja ukiwa kifuani, huku mwingine ukilinyooshea gari la Boazi lililokuwa linatoka getini na kukata kona kuingia barabara kuu. Tukaanza kulifukuzia nyuma. 

Anakwenda wapi huyu sasa? nilijiuliza mara kumi kidogo.

Papo hapo, nikaikumbuka simu yangu. Nilimkumbuka Tutu. Wakati namzimia simu Teri niliona meseji toka kwa Tutu ila sikuzisoma, sikuhangaika nazo. Saa hizo, dakika hiyo, ndiyo nilizikumbuka. Huku mikono ikitetemeka nikaitoa simu mkobani. 

Macho yangu yalikuwa yanatazama mbele na kurudi simuni kwa kasi ya ajabu. Kuna nyakati ilibidi kuachana na vyote ili kujishikilia vizuri kwa kuwa bajaji ilikwenda kama upepo, isijali mashimo wala makorongo. 

Msisitizo wangu wa kutolipoteza gari la Boazi, ulimkolea dereva. 

Simu ikawaka. Zile dakika za kusubiri mtandao ukae sawa, zilikuwa kama kusubiri miaka 10 ipite. Meseji za Tutu za whatsapp zikawa za kwanza kuingia. Nikaifungua moja.

‘Mima usiende huko kwanza. Usiongee chochote.’ Nikaisoma moyoni nikijisemea, amekwishachelewa!

Nikaifungua nyingine.

‘Teri anakupigia msikilize please. Nakusihi sana msikilize kwanza.’

Ikaja nyingine

‘Watu watauana Mima, ndiyo maana nakwambia usiongee chochote’

‘Mima nakupigia hupatikani jamani. Mima niko chini ya miguu yako’

Sikuendelea kusoma. Meseji hazikuwa na maana tena.

Niliifungua meseji moja ya Teri kati ya nyingi alizotuma.

‘Chochote kitakachotokea Mima usimpoteze mtoto wetu’ 

Niliisoma hii meseji ya Teri mara tatu, pengine zaidi. Kwa nini aliiandika kama mtu aliye mapenzini na mimi? Si leo hii alimwambia Tutu kuwa hataki kusikia habari zangu. Imekuaje? Hivi ni nini kinaendelea? Aaarh! Niliwayawaya. 

“Sista cheki huku…ona jamaa anaingia hapo…” dereva wa bajaji alinishtua nami nikagutuka na kuchungulia kule nilikoonyeshwa. 

Nilitunduwaa!

Nguvu zikaniishia.

Tulikuwa tumesimama nje ya jengo analoishi mtu ninayemfahamu kabisa. Jengo nililotoka saa chache zilizopita nikielekea kwa Boazi. Tulikuwa nje ya nyumba anayoishi rafiki yangu Tutu Mzigoz!

Nikiwa nimecharangwa vibaya na lile butwaa.

Nilishuhudia Boazi akiteremka na ile bastola akiifutika ndani ya koti ubavuni. Niliweka tena mkono kifuani. Oh Mungu wangu! Mungu wangu!

Kabla sijaamua cha kufanya, nikaliona gari ninalolifahamu fika. Gari nililopanda usiku ule wa majanga likifika eneo lile. 

Gari la Teri Balokwa!

Nilimwona Teri akishuka pia garini. Kwa mwendo wa mchakamchaka uliopeperusha koti lake nyuma alikimbilia kulekule alikoelekea Boazi.

Nilimtazama dereva wa bajaji nikiwa nimechoka mwili na roho.  Hivi nimefanya nini hiki mimi Mima! 

Sasa itakuwaje? 




Wahka ulinifanya nami nihemee mdomo. 

Simu niliyokuwa nayo mkononi iliniponyoka na kudondoka chini. Mikono ilikuwa inatetemeka, ama niseme mwili mzima ulikuwa unatetema. Akili ilikuwa imekimbilia kusikojulikana na kuniachia kichwa kama nyumba iliyoezuliwa paa. 

Kiranga hiki, kiranga komo!

Dereva wa bajaji aliniokotea simu na kunikabidhi mkononi. Alikuwa ananisaili maswali ambayo yalipita huku yakatokea kule. Akilini iliyorejea nusu iliwaza mamoja kwa makumi. Nigeuze na hii bajaji nikimbie nitokomee zangu, ama nishuke hapa nikazijue mbivu zipi, mbovu zipi!

Baada ya kusita kidogo, nilifanya maamuzi. Nilipeleka mkono kwenye mkoba na kuchomoa noti ya elfu 10 iliyokuwa kwenye kimfuko cha ndani ya mkoba. Nikampatia yule dereva. Sikusubiri chenji. Nikaachana naye. 

Mwendo niliotoka nao pale nje kuelekea ndani siwezi kuupatia jina sahihi. Kuna wakati nahisi sikuikanyaga ardhi.

Nyumba anayoishi Tutu ni moja kati ya nyumba tatu zilizo katika kiwanja kimoja na uzio mmoja wa michongoma. Nyumba yake ipo katikati. Mara nyingi geti la nyumba hii ambalo ni la nondo ndefundefu zinazoonyesha mpaka ndani, nyakati za asubuhi na mchana huwa linaegeshwa tu. 

Hivyo, huwa ni  rahisi mtu yeyote kuingia. Hata hivyo nyumba mbili za pembeni huwa hazina watu mpaka usiku. 

Nje ya nyumba, kuna eneo kubwa kidogo kabla ya kuifikia barabara. Hapo ndipo magari ya wanaume hawa wawili yalipoegeshwa hobelahobela.

Mlango wa mbele wa nyumba ya Tutu ulikuwa wazi. Kadiri nilivyopiga hatua kuukaribia, ndivyo masikio yangu yalivyopokea kelele zilizotoka ndani. Niliharakisha zaidi. Nilipokivuka kizingiti cha mlango, ghafla nilifunga breki za visigino. Hali ya sebule ilikaribia kunitoa nduki. 

Nilirudi nyuma na kuzishikilia kingo la mlango kwa mikono yote miwili kana kwamba nilikuwa nikizuia zisinibane katikati. 

Boazi alikuwa amesimama kulia na Teri alikuwa kushoto. Walitazamana kila mmoja kwa namna yake. Tutu alikuwa katikati yao, akiwa ameichanua mikono yake huku na huku kama mtu anayejiandaa kuwazuia kukaribiana tena. 

Tutu alikuwa anahema kiasi cha kuonyesha mpando na mshuko wa kifua chake.

Teri alikuwa anavuja damu kwenye tundu moja la pua na pembeni ya mdomo. Naye alikuwa anahema kwelikweli na kuyumba kidogo. Boazi alikuwa amefura, mkononi ngumi ilikuwa imekunjwa kiasi cha mishipa ya kiganja kusimama. Huo mkono wenye ngumi ukitetema.

Meza ndogo ya kioo ambayo hukaa katikati ya sebule, ilikuwa imebinukia upande ilhali vitu kadhaa vikiwa sakafuni ovyoovyo. Vilivyonusurika na kupasuka vyote vililala pale chini. Nilitembeza macho huku na kule, safari hii mkono wa kushoto ukiwa mdomoni. Nilijizuia kutopiga yowe. 

Wamepigana hawa, uwiii! kulikuwa na ngumi za chapuchapu hapa. Hivi wanajua ana bastola? Hivi akiitoa akafanya pah! pah! pah! si tutakufa wote hapa? 

Nilikuwa nawaza haya yote nikimalizia kutembeza macho mikononi mwa Boazi. Wao sasa walikuwa wananitazama mimi kama marehemu aliyefufuka. 

Kimya kifupi kilitanda.

Nilipiga hatua kuwakaribia. Kuna maneno walirushiana upya, wakakaribia kushikana tena mashati. Niligeuka nyuma kuangalia mahali mlango ulipo. Hizi vita kwangu hazikuwa za kugombelezea. Kwa mwoga huenda kicheko kwa shujaa huenda kilio. Mimi sikuwa nautaka huo ushujaa. 

Tutu aliyepambana kuwaachanisha, alipayuka kwa nguvu.

“Guuuys!! Let’s settle this once and for all,” alimaanisha wasuluhishane kwa mara mwisho.

Alimgeukia Teri, “naomba umchukue Mima, umtoe hapa kwanza.”

“Ampeleke wapi? Kibali cha kumtoa hapa anakitoa wapi?” Bozi aliuliza kwa ukali. 

Kisha, akaninyooshea kidole huku akimtazama Teri. 

Akatamka kwa kujiamini, “Mima ni mwanamke wangu atatoka hapa kwa amri yangu.” Akamalizia kwa kujisonta kifuani kwa dole gumba. 

Nikamtolea macho ndi! na yakamkodolea hasa! Kidogo mdomo uropoke, ‘Tangu lini mimi ni mwanamke wako?’ Kichwa kikaukumbusha mdomo ‘Usituponze kuna bastola ujue!!’

Nikatulia, sikusema neno lolote. Sikukubali wala kukanusha.

Teri akabeua, huku akifuta damu puani.

“Amri yako!? Umeshindwa kuzipa amri hasira zako unataka kumpa amri nani?” aliwaka.

“Teriiii!” Tutu aliita kwa hamaniko, akiwazuia tena kukaribiana.

“Nimechoka! Nimechoka Tutu… safari hii sitaomba msamaha wa mtu… I won’t back off, Mima is mine! Mima ni wangu mimi.”  Teri alijibu kwa kujiamini kabisa.

Nikayatoa macho tena mara mbili ya mwanzo. Nilihisi macho yenyewe yalikaribia kudondoka chini. Ilibaki kidogo nipayuke kuwauliza, “Kwani wanamgombea Mima yupi hasa!” 

Kiuhalisia, Boazi hakuwa mpenzi wangu tena. Teri hakuwa mpenzi wangu pia. Walikuwa wanatoa wapi mamlaka ya kuvimbiana juu yangu, huku kila mmoja akiwa ameshaniumiza vya kutosha. 

Boazi alitaka kupiga hatua. Tutu akamuwahi, “Boazi tulia kwanza basi!” 

Ni kama vile ile kauli yake ilipita juu kwa juu. Boazi aliachia tusi la nguoni wakati mkono wake wa kulia ukiingia ndani ya koti, ubavuni. Papo hapo mkono wa kushoto ukimsukuma Tutu pembeni ili kumtoa katikati yake na Teri.

Ule mkono ulioingia kotini ulichomoka na bastola. 

Mimi na Tutu tukapiga yowe la kwanza, “Mamaaa!”

Vuu! Jamaa aliachia mngurumo hali kiwiliwili chake cha juu kikirudi nyuma. Mguu wa kulia uliinuka juu nyuzi 90, na kuachia pigo moja matata la Front Kick. Pigo lile lilimfikia Teri tumboni kisawasawa. Likampepesusha.

Lilikuwa pigo la haraka mno.  Pamoja na kujitahidi kutolamba sakafu, lakini lile teke la ghafla lilimjia vibaya. Teri alienda chini mzima mzima huku mikono ikitapatapa kutafuta pa kukamatia hewani. 

Alitua kwa kishindo, mikono ikilikamata tumbo kwa maumivu aliyoyapata. Aligagaa sakafuni akigugumia. Kisha, akakutana na mdomo wa bastola mara tu alipoinua uso kutazama juu. 

“Sasa unaweza kurudia tena ulichoongea,” Boazi alitamka kwa sauti iliyojaa amri, bastola ikiwa imemuelekea Teri pajini ilhali akitabasamu.

Tutu aliyeruka kando kwa hofu na kula mweleka chini. Aliduwaa pale chini akihema. Kuna ukimya mdogo ulipita. Kisha mimi na Tutu tukajikuta tunamwita Boazi kwa pamoja. 

Hakuitika wala kugeuka. Tutu aliinuka na kuanza kumsihi aishushe ile bastola. Nami nikahoji ni nini kilikuwa kinaendelea? Boazi akataka kuikoki bastola yake tayari kumlipua Teri. 

Kwa hali aliyokuwa nayo, lolote lingeweza kutokea. Mishipa  ya kichwa ilishamsimama. Jasho jembamba lilidhihirisha mchemko wa hasira ndani yake. Angeweza kutumaliza wote mle ndani. 

“Boazi jamaniiii!!” yowe la pili la kusihi na kunasihi likatutoka kwa pamoja. 

Nilikuwa natetemeka kuliko mwanzo. Maishani mwangu sikuwahi kuiona bastola kwa ukaribu hivi, sembuse kuona mtu akiwa ameelekezewa. 

Teri aliyekuwa amekumbatiwa na hofu pale chini, alitaka kusema neno. Lakini, mdomo wa bastola ulipomkaribia zaidi, naye jasho lilimtiririka.

“Nilitakiwa kufanya hivi kitambo na unajua hilo.” Boazi alimsemesha Teri. 

“Boazi please!” Tutu alimsihi.

“Shut up!...” alimkemea Tutu, “Shut uuup!” alikemea tena akipaza sauti. Alikuwa akimtazama Tutu kwa macho makali. Tutu aliinua mikono juu kama mateka. 

“Nakuchukia! Nakuchukia kiasi kwamba natamani kuua. Nilikwishapa nitakuua. Pengine ni leo nitafanya hivyo, nakuchukia mno.” Boazi alituteteresha.

“Boazi, mama yako ataumia sana,” Tutu alijaribu tena.

“Unadhani najali hilo! Baada ya yote unadhani najali kitu?” 

Kwa sauti ya mkwaruzo Boazi alihoji. 

N dipo sasa, nikaujua mkasa nyuma ya hekaheka yote hii.

Sikia!

Alipata kuwepo mwanamke mrembo sana aliyeitwa Clara Metsu. Clara alikuwa mchumba wa Boazi. Mchumba kabisa wa kutambulishana kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki. Walikuwa na mapenzi yao motomoto. Boazi akionekana kumpenda zaidi Clara.  

Wiki chache kabla ya ndoa yao, Boazi alianza kulalamika kuwa Clara amebadilika na ameamua kuisogeza mbele tarehe ya harusi yao pasipo maelezo ya kutosha. Kipindi hiki kilikuwa kigumu mno mno mno kwa Boazi. 

Maana alikuwa anampenda Clara hakuna mfano. 

Akiwa haelewi kinachoendelea, Boazi alienda kumsimulia mtu aliyeamini ni kama rafiki mkubwa wa Clara, aliyekuwa kama ndugu kwake pia. Mtu huyu alikuwa Teri Balokwa. 

Teri na Boazi ni watu waliozaliwa sehemu moja na kufuruka pamoja balehe hata ujana. Walisoma shule moja na kuhitimu chuo kikuu pamoja katika chuo kimoja. Teri na Boazi walikuwa zaidi ya marafiki. 

Walikuwa kama ndugu wa kuchanjia damu.  

Teri alimpa moyo.  Alimpa matumaini makubwa rafiki yake. Kuna wakati Clara aliitwa kwenye vikao vyao na Teri kuzungumza nao. 

Bila kujua kuwa Clara alikuwa amesogeza mbele tarehe ya harusi kwa sababu ya Teri. 

Clara alikuwa kwenye mapenzi ya siri na Teri kwa muda mrefu. Huku mbele za watu wakiuaminisha ulimwengu wao ni kaka na dada. Clara alikuwa anampenda Teri kuliko Boazi.

Siri yao ilikuja kufichuliwa na Sabra, mpenzi wa Teri.  Ambaye alimfuma Teri akimbembeleza Clara asisitishe ndoa  kwa sababu ya mimba aliyoipata. Mimba ambayo Clara alikuwa na uhakika ilikuwa ni mimba ya Teri. Hivyo, alikuwa akimtaka Teri aachane na Sabra na yeye Clara aachane na Boazi ili waambatane pamoja. 

Teri alikataa. 

Fumanizi hilo likazua vita kubwa kuliko ile ya Kosovo.

Ilikuwa aibu na robo tatu yake. 

Boazi alichanganyikiwa. Na namna alivyokuwa akimpenda Clara, alikuwa tayari hata kumsamehe na taratibu zingine kuendelea. Alikuwa tayari kumpokea mtoto wa Teri kama wake. Lakini, Clara hakuwa tayari kuolewa na Boazi. 

Teri pia hakuwa tayari kumuoa bibie, kwa kuwa Boazi aliapa Clara akiolewa na Teri, ni bora mmoja wao afe wamkose wote. 

Teri na familia yake waliomba radhi sana kwa Boazi na familia ya Boazi. Upendo na ukaribu baina ya familia hizi mbili ulikufa na kuacha jitimai kubwa. Ikiwemo hasara ya ushirikiano wa kibiashara kufa. 

Teri aliapa asingemwoa Clara. Na kweli alivunja uhusiano wake na Clara. Ijapokuwa, haikusaidia kufuta izara iliyotokea. 

Kwa fedheha na msongo alioupata, Clara almanusura ajiue. Aliokolewa yeye. akapoteza mtoto tumboni. Clara alihama nchi. Akatokomea. Tukio la kunusurika kufa na kupoteza mtoto liliharibu mno maisha ya Clara huko alikoelekea. Taarifa zilirudi, Clara amefariki.  

Uadui wa Teri na Boazi ulizidi kupamba moto kuanzia hapo.

Baada ya misukosuko mingi, angalau Boazi alikaa sawa. Maisha yakawa kama vile yanaendelea. Akajikuta anaufungua moyo wake kwa msichana mpya. Alivutiwa na namna msichana huyo alivyokuwa mcheshi na mkarimu. 

Msichana aliyekutana naye kwenye kiunga cha starehe. Msichana ambaye urafiki wao ulimsaidia mno kutoka kwenye sonona. Alirudi kuwa Boazi mwenye utulivu. 

Wakati akihangaika kumnasa bibie kisawasawa, akagundua kitu kilichomuumiza sana. Teri naye alikuwa anamsarandia mwanamke huyohuyo aitwaye Tutu Mzigoz!!

Teri na Tutu walikutana kwenye mkutano wa kazi. 

Kabla maafa hayajatokea tena, Tutu aliwaweka chini pamoja akawapa ukweli, hakuwa na mpango wa kutoka na yeyote kati yao. Lakini viapo vya jazba vilitoka. Wakati Teri akiomba radhi kuwa hakujua kama Boazi anampenda Tutu, Boazi yeye alitoa onyo kwa Teri kukaa mbali na mwanamke yeyote ambaye yeye Teri atagundua yu karibu na Boazi. Walikubaliana hivyo!

Waliapishana hivyo.

Tutu akawa rafiki katikati yao maadui.

Lakini, ilikuwa dhahiri Tutu alikuwa anampenda Teri. 

Nikaja mimi Mima!

Nikaingia maishani mwa Boazi, nakiri nilimpenda kuliko alivyokuwa ananipenda. Kumbe wakati mimi nasahaulika ni Tutu ndiye aliyekuwa anapewa mahaba niue. Kila alipokwazwa au Tutu aliposafiri alikuwa anarudisha majeshi kwangu. 

Hakunitendea haki.

Nilikuja kufahamiana na Tutu nilipoanza kazi kwenye jengo analofanyia kazi pia. Sikuwahi kumweleza kuhusu Boazi, na hakuwahi kujua chochote. Pengine angeiona picha ya Boazi angenipa hii stori mapema. Yumkini, ndiyo maana alicheka sana usiku ule nilipomuuliza kama Teri ana mke. Alikuwa anajua Teri anampenda yeye.

Hakika, dunia rangirangile.

Wakati Boazi alipotoka ofisini kwake kule akiwa na jazba pomoni alipokea simu kutoka kwa Tutu. Baada ya Boazi kusema anamfuata Teri. Ilibidi Tutu amdanganye Boazi kuwa Teri alikuwa pale kwake. Papo hapo alikuwa amemdanganya Teri pia kuwa mimi nilikuwa nimerejea pale kwake. Ndiyo sababu ya wote wawili kufika pale mbiombio.

Tutu alidhani angeweza kuwaweka sawa nyumbani kwake, kuliko wangekutana sehemu nyingine wakiwa wao wenyewe. Hakujua kama alikosea au alipatia.

Sasa nami nilianza kupata majibu, kwa nini Teri aliposikia nina mimba, alibadilika. Alikumbuka alichokifanya kwa Clara Metsu. Alikumbuka kilichomtokea Clara wao. Nilipata majibu, kwa nini Teri alidata usiku ule alipoiona picha yangu na Boazi. Nilipata majibu, kwa nini Teri na Tutu walinisihi vilivyo nisiseme kitu chochote kwanza kwa Boazi.

Sikuyajua haya yote!

Boazi alikuwa anatiririkwa na machozi, jasho likimtoka zaidi. Mishipa ya jazba ikiwa imemsimama mpaka usoni wakati akieleza kila kitu.

“Nilistahili haya Mima? Nastahili kufanyiwa hivi na huyu mshenzi kwa mara nyingine tena?” aliniuliza akigeuka kunitazama.

Mimi niliitazama ile bastola kwanza, nikajikuta tu natikisa kichwa kulia kushoto. Mikono yangu ikisaidia kukataa kuwa hakustahili.

Ingawa nafsi ilitamani kumwambia, safari hii Teri hakuwa na makosa yoyote. Ni mimi ndiye niliyemwingiza majaribuni. Ulikuwa ni usiku mmoja wa bahati mbaya kwetu sote. 

Mdomo usingeweza kutamka hayo mbele ya ile silaha.

Pale chini Teri alikuwa kimya, pengine sala zote zilishamtoka. Hata yeye aliumia kutanabahishiwa makosa aliyoyafanya. Kumzunguka mtu unayemchekea kila siku inahitajika roho ngumu kwelikweli. Na maafa yaliyokuja kutokea baadaye yalikuwa yameacha makovu makubwa mno na majuto yasiyoelezeka.

Tutu aliendelea kujaribu kumsihi Boazi atulie, akimweleza hata yeye Tutu hakujua mimi ni mpenzi wa zamani wa Boazi. Alimsihi na yeye machozi yakimtoka. 

“Hata nikiishia jela, sitakuwa na cha kupoteza huyu baradhuli akiwa futi sita chini.” Boazi alimtazama Tutu kisha akanitazama mimi. 

Ukimya ukapita kati yetu. Mwisho, Tutu akamfunulia ukweli Boazi, kuwa hapo nilipo nilikuwa na mimba ya Teri Balokwa. 

Nami nilijikuta natokwa na machozi. Sikuelewa ni huruma, hasira au kitu gani. 

Boazi aliinamisha kichwa chini. Alifumba macho. Mabega yake yakazcheza kwa kwikwi. Taya zake zilisigana na kututumka. Mishipa ya mkono wenye bastola ilimsimama. Akaukaza mkono huo kwa nguvu zake zote kisha taratibu akaiachia, akaidondosha ile bastola chini.

 Alifumbua macho na kugeuka kunitazama. Machozi yalikuwa yanaendelea kumtiririka. Kuna kitu alitaka kukitamka lakini kilikwamia kooni pake na kulichezesha koromeo juu chini. 

Asteaste, alipiga hatua kuelekea nje. Alinipita kama kinyago. 

Nilimhurumia, nilitamani kumfuata. Nilitamani kumsemesha. Maumivu yake yalionekana wazi. Ooh! Boazi wangu jamani. Nikalia, nikalia kwa kugugumia huku nikitetemeka kwa uchungu.

Tutu alimfuata nje.

Tulibaki mimi na Teri.

Tulitazamana tu. Mimi nikilia yeye akilengwa machozi.

Aliinuka toka pale chini  kwa taabu na kuchechemea akiwa ameshikilia tumbo kwa mkono wake wa kulia. Alikuja moja kwa moja kunikumbatia. Nililia mikononi mwake kama mfiwa. Naye akanibana zaidi kifuani pake. Nilipopunguza kasi ya kulia, alinitoa kifuani na kuuinua uso wangu uliokuwa umelowa machozi.

Macho yake mazuri yalikuwa yamejaa machozi. Niliukumbuka usiku ule wa mvua kali. Tulitazamana namna hii. Lakini, katika hali ya mahaba. Leo tulikuwa tunatazamana tukitokwa machozi ya uchungu. 

“Nitakulinda… sawa!... Nitakupenda Mima… hata kama itagharimu uhai wangu.”

Alinitamkia kwa hisia kali. Nikafumba macho nikiruhusu machozi yafanye tena njia mashavuni. Nikalihisi busu lake la pajini. Akanikumbatia tena kwa nguvu zote. 

Ajabu! Nilikuwa nataka kwenda kumkumbatia Boazi. Baada ya kuusikia mkasa mzima, nilijihisi kama mtu niliyemuumiza mno Boazi. Nilijitoa mikononi mwa Teri na kuelekea nje. 

Niliwakuta Boazi na Tutu wakiwa wamekumbatiana wakilia. Nikainamisha kichwa chini. Kuna sehemu ya moyo iliumia. Nilihisi nilipaswa kuwa pale mikononi mwa Boazi na si Tutu.

Niligeuka nyuma. Nilimwona Teri mlangoni. Akaninyooshea mikono kama ishara ya kunipokea. Nikarejea mikononi mwake. Alininong’oneza.

“Mima, usije ukajaribu kurudia makosa. Usije ukajaribu kurudi kwa Boazi. Nakuomba!” 

“Siwezi, siwezi Teri, nakuapia hilo,” nilimjibu nikimkumbatia zaidi.

Unajua nini…

Mimi na Tutu sasa ni marafiki ambao wapenzi wetu hawapatani hata chembe. Tutu yuko na Boazi na mimi niko na Teri. Naweza kukiri Teri ananipenda sana, nina amani kuwa mikononi mwake. Tuna mipango mingi ya pamoja. Amezama penzini nami kisawasawa.

Boazi amekuwa akinitazama kwa namna inayoshawishi majanga. 

Nami mara kadhaa nimekuwa nikitamani kumtumia ujumbe wa kumjulia hali. Naye hali kadhalika amekuwa akinipigia simu pasipo kuongea lolote. 

Wakati mwingine wivu hunichoma kumwona Tutu mikononi mwa Boazi. Nahisi, hilo hutokea kwa Tutu pia. Zipo nyakati Tutu hutazamana Teri katika namna inayoacha maswali. Ni vipi kama na wao wamewahi kuwa wapenzi sirini? Sijui. Kuna wakati nahofia sana yasije kujirudia yale yaliyotokea enzi za Clara Metsu. 

Cheche za moto huchoma msitu. Nachelea, hizi cheche mioyoni mwetu zisipozima zitakuja kutuunguza sisi sote.

88888

Alfajiri, Simu yangu iliita nikiwa kitandani. Nilipapasa chini ya mto na kuitoa. 

Alikuwa Boazi. 

“Usipoongea ni bora usipige tena simu Boazi,” niliuvunja ukimya simuni.

“Nakupenda Mima!” Boazi alimudu kutamka.

Nilifumba macho nikiruhusu msisimko unitambalie mwilini.

“Nina kiapo kwa Teri, nami sitakivunja,” 

“Mbele ya nguvu ya mapenzi, wakati wowote kiapo hugeuka kuwa batili!” alinijibu na kukata simu.

Niliiteremsha simu toka sikioni. Nikaitazama picha ya Teri na mimi kwenye ile taa ya urembo. 

Kama hivi ndivyo mapenzi yalivyo, basi dunia na ijue, kuna muda viapo huvunjwa kwa nguvu ya mapenzi. Mapenzi yanayokuletea usiyoyatarajia hata baada ya kiapo cha damu, unatetereka. 

Ni nani alipambana na nguvu ya mapenzi akashinda? 

Ni nani KIAPO kimewahi kumzuia kupenda?

“Hivi nami kiapo changu kikiyumba ni nini kitatokea?” nilijiuliza nikivuta shuka hadi utosini. 

Sikutaka kuwaza hilo kwa wakati huo. 


MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog