Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

FUMBO

   


MTUNZI : MAUNDU MWINGIZI


PUA za Leila ziliipokea harufu ya manukato iliyopozwa na kiyoyozi, mara baada ya kufungua mlango na kuingia ofisini. Chini, sakafu ilifichwa na zulia la sufi. Juu, taa zenye rangi anuwai zililizunguka dari mithili ya nyota zipendezavyo anga. Nusu ya kila dirisha ilifunikwa kwa mapazia ya rangi ya samli ilhali nusu ya pili ikikingwa na vioo. Mvuto wa ofisi na umaridadi wa samani zake, vilipambanua haiba na tajriba ya bosi anayeimiliki. Alitembea taratibu, akiyapita makochi yaliyopangwa kwa kuizunguka meza ya vioo katikati ya ofisi.

Mama Mbegu alikuwa ameketi nyuma ya meza ya duara, akiendelea kuperuzi kompyuta yake. Hata Leila alipomsabahi, bado hakujikalifisha kunyanyua uso wake, aliishia kuitika salamu hali macho yameganda kwenye kioo cha kompyuta. Leila akiwa amesimama asijue la kufanya, ndipo aliinua uso, akivua miwani na kuitenga mezani, na kwa mkono wake wa kushoto akamwashiria aketi. Kisha, akajitengeneza wigi lake, lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na kahawia, lililofunika kichwa pamoja na masikio, na kushuka hadi usawa wa mabega. Alipomaliza, akavitenga viwiko vya mikono juu ya meza kiasi cha kufanya bangili na pete za dhahabu kumeremeta. 

Leila alivuta kiti kimoja, kati ya viwili vilivyopangwa mbele ya meza. Hata baada kuketi, bado alijihisi kama bado amesimama. Mapigo ya moyo yalimgomea kutulia. Kitendo cha kuitwa ofisini na mama Mbegu, ilikuwa ni sawa na mwanafunzi kuitwa na mwalimu wa nidhamu ofisini – ambapo kwa kawaida huwa haiingi yeyote bali kuna walakini.

“Enhe, una matatizo gani na Seba?” mama Mbegu alimrushia swali. Japo sauti yake ilikuwa tulivu na isiyo papara, walakini ilijaa shari.

“Hakuna tatizo, bosi,” Leila alijibu kwa indhari, huku akiminya macho yake kiudadisi.

Mama Mbegu alipandisha nyusi juu huku macho yake makubwa yaliyokolea wanja wa chini, akiyazungusha tamthili ya mtoto mwenye degedege.

“Unajua, muda niliopanga kuzungumza nawe ni dakika tano tu,” alisisitiza huku akiinua mkono kutazama saa, “na mpaka sasa umekwishatumia dakika mbili. Sasa, usipokuwa makini, nazo zitakwisha kabla sijajua cha kukusaidia. Umenipata?”

“Ndio bosi.”

“We ndiye msaidizi wa Seba, na mlipaswa mwende pamoja Kanada, kikazi. Nimeambiwa uligoma kusafiri naye, na bado unasema hakuna tatizo!”

Kimya kifupi kilitanda wakati wakitazamana. Leila aliinamisha macho chini, akihisi baridi ya hofu ikimzizima maungoni. Hakuwa amepanga kumwambia mtu yeyote kuhusu chochote baina yake na Sebastian. Lakini kwa kuhofia kisirani cha mama Mbegu, alifunua kinywa, “Seba amenikasirikia, bosi.”

Mama Mbegu aliachia ucheko hafifu, japo sauti iliyotoka haikuwa ya cheko halisi, bali ni kama madebe mabovu yaliyonyeshewa mvua.

“Kwa hiyo unasubiri nikuulize hadi sababu ya ugomvi wenu?”

“Hapana, bosi,” Leila alijibu haraka na kuendelea, “Seba alianzisha tabia mbaya. Kila mara alipoingia ofisini, alianza kunishikashika bila ridhaa yangu. Nikamwambia sipendi hiyo tabia. Akaacha. Ghafla, siku hiyo nilikuwa nimeinama kabatini nachuk–”

“Eh! Eh! Makubwa haya,” mama Mbegu alidakia huku tabasamu la ugwadu likijijenga usoni mwake. “Kwa hiyo mwenzetu kushikwa tu mpaka uandikiwe barua ya maombi?” 

Kama ipo walau chembe ya aibu machoni mwa mama Mbegu, ingelihitajika darubini kuweza kuiona. Leila alipoinua uso kumtazama kwa tahayari, alikutana na uso mkavu usio na soni.  Akaishia kuvuta pumzi nyingi na kuzitoa taratibu.

“Lakini bosi, nilikwishamweleza na akanielewa. Mimi ni mke wa mtu. Mume wangu akijua itak–”

“Atajuaje? Utaenda kumwambia? Au amekufunga Bluetooth mwilini?”

Leila hakujibu. Akainamisha kichwa chini.

Mama Mbegu aliinuka kitini. Akasimama na kujitengeneza kivazi chake; blauzi ya rangi ya hudhurungi iliyodariziwa kwa riboni za kahawia, na kubandikwa vishikizo vyeusi vilivyofunikwa kwa papi pana juu yake, viliupendezesha mwonekano wake. Sketi ya rangi ya damu ya mzee, iliyoishia juu ya magoti iliruhusu miguu yake minene kuonekana vizuri, kadri alivyopiga hatua kuelekea kwenye korido ndefu iendayo maliwatoni. Alipoifikia meza ndefu ya mninga iliyobanwa ukutani kando kando mwa korido, alisimama na kushika chupa ya chai. Akajimiminia kahawa kwenye kikombe kidogo. Akarudi nayo mezani.

“Seba anarudi leo usiku, na kwa taarifa nilizonazo, tayari anayo barua yako mkononi,” alisema huku akiweka kikombe cha kahawa mezani. “Hakuhitaji tena kazini.”

Leila alihisi misuli ya tumbo ikikakamaa. Ngurumo mithili ya radi zilirindima tumboni mwake. Taratibu, jasho likaanza kutengeneza chemchemi makwapani.

“Bosi nakuomba nisai–”

Mama Mbegu alimnyooshea kiganja kumzuia asiendelee kuzungumza. Akaketi na kusema, “Unaelewa namna nifanyavyo kazi na Seba. Hatuingiliani kwenye maamuzi. Nilipokutafutia nafasi ya kazi, nilimsisitiza mama Mainda akwambie kuwa, jukumu la kuipigania na kuilinda nafasi yako si langu tena. Nadhani alifanya hivyo. So, sitokuwa na mahali pengine pa kukupachika endapo Seba ameamua kukutimua.”

Leila alimeza funda la mate na kufanya koromeo lake kucheza saka-mke-wangu. Ndani ya muda mfupi, tayari uso ulimshuka mithili ya mbuzi anayesubiri kuchinjwa.

Tangu mzee Dominic Mbegu, mmiliki wa kampuni ya Crops Investment Limited, alipougua kiharusi na kushindwa kutimiza majukumu yake, mama Mbegu kwa kushirikiana na Sebastian Mbegu, mdogo wake mzee Mbegu, walisimamia na kuendesha kampuni. Mafanikio ya kampuni chini ya usimamizi wao, yalichagizwa na namna walivyolindana na kwa kila mmoja kuchunga mipaka waliyowekeana.

Mama Mbegu akaendelea, “Leila, bahati ikibisha hodi mlangoni, unainuka kwenda kuifungulia – usisubiri hadi na mlango ijifungulie.”

Leila aliinamisha kichwa huku mikono ameifumbata mapajani wakati mama Mbegu akizungumza. Alipoinua kichwa kutaka kusema neno, tayari alikuwa amechelewa.

“Endapo nami ningejifanya malaika kama wewe, leo nisingelikuwa bosi hapa. Nilianza kazi hii kama secretary wa mzee Mbegu, nikiwa nimekwishaolewa – kama wewe tu. Lakini ndani ya miezi yangu hiyo,”– alitandaza vidole vitatu vya mkono wa kushoto– “mitatu tu. Nikaanza kulipwa mshahara mkubwa kumzidi hata meneja. Unadhani humo ofisini nilikuwa namkenulia meno tu?”

Leila alifumba macho kwa fadhaa na izara. Kila silaha ya maneno aliyopanga kuitumia ilizidiwa nguvu na ulimi wa mama Mbegu.

“Mumeo yuko wapi?” mama Mbegu alivunja ukimya.

“Amekwenda Arusha.”

“Good.” Alinyanyua kikombe cha kahawa na kupiga funda moja, kisha akakirejesha mezani. “Seba anaingia leo. Saa moja usiku. Aliniomba nipeleke mtu akamsafishie nyumba. Sasa, huu ndo muda wa kucheza karata yako ya mwisho. Hakikisha ukitoka kazini unakwenda kufanya hiyo kazi. Akifika akukute kwake. Hapo sasa juhudi zako ndo zitaamua, ama akupe barua ya kukufukuza kazi au ya kukuongeza mshahara.”

Leila alifunua kinywa kusema, maneno yakakwama kwenye kuta za koromeo lake. Akabaki anahangaika mithili ya nzi aliyenasa kwenye utandu wa buibui.

***

Basi la Kilimanjaro Express liliwasili Kituo cha Mabasi jijini Arusha, na kupokelewa kwa shangwe na mbinja toka kwa wapiga debe. Mara baada ya kuegesha mahali pake, tayari likazungukwa na wajasiriamali – kila mmoja akinadi biashara yake kwa sauti kubwa, ili kukabiliana na sauti za muziki zilizohanikiza eneo lote la stendi.

Ikunji Almasi ni miongoni mwa abiria walioteremka mwishoni kabisa ili kukwepa rabsha za wasafiri waliokuwa wakiharakia kushuka, pamoja na bughudha za wajasiriamali  waliokuwa nje ya basi. Bado hilo halikufaa kitu. Aliposhusha tu mguu mlangoni, alilakiwa na kundi la madereva bodaboda pamoja teksi; baadhi wakiwa juu ya pikipiki zao, wengine wakiwa wima – wote wakiwania abiria.

“Salaam aleykum, kaka,” kijana mmoja, aliyekuwa amesimama mbele kabisa ya mlango wa basi, alimlaki Ikunji kwa bashasha. “Habari za Dar?”

Kwa mazingira yale ya stendi, ilikuwa muhali kwa mtu asiyefahamiana naye kumlaki moja kwa moja kwa salamu ile. Hilo likachota nadhari ya Ikunji, akidhani pengine wanafahamiana.

“Waaleykum salaam,” alijibu akimtazama usoni kijana mrefu, mweusi, mwenye nyusi hafifu zilizoyazunguka macho yake makubwa. Kidevuni alifuga mzuzu mrefu. Alivalia suruali ya bluu na kubadhi za kahawia. Shati lake jeusi la mikono mirefu alilikunja nusu yake.

“Utahitaji teksi kaka?” kijana aliuliza kwa taadhima, akinyoosha mikono ili kupokea mkoba wa Ikunji.

Swali hilo ndilo lilimtanabahishia Ikunji kuwa, kijana yule alikuwa dereva teksi au shanta. Hakufanya haraka kumjibu wala kumpatia mkoba wake. Akaendelea kutembea taratibu kuelekea kwenye geti la kutokea.

“Nahitaji hoteli nzuri, lakini isiwe mbali sana,” Ikunji alisema baada ya kupiga hatua chache, akiinua mkono kutazama saa. “Nimeambiwa maeneo ya Sanawari kuna hoteli nzuri, na si ghali sana.”

Ikunji hakuwa mwenyeji wa Arusha. Hii ilikuwa mara yake ya pili kufika jijini humo. Mara ya kwanza ilikuwa ni takribani miaka mitano nyuma.

“Wala usijali bosi. Hapo Soweto tu kuna hoteli nzuri zaidi, na za bei poa. Nitakupeleka.”

Waliendelea kutembea hali Ikunji ameudhibiti mkoba wake ubavuni. Waliifikia teksi nje ya geti. Wakaingia na kuondoka. Kiasi cha dakika kumi, waliwasili nje ya uzio wa hoteli nzuri. White Rose Hotel. Ikunji alilipa nauli, akateremka na kuelekea ndani.

Nyuma ya meza ya mapokezi, aliketi msichana mweupe, mnene. Alivalia fulana nyeupe yenye ukosi mwekundu, aliyoshabihisha na kapelo nyeupe yenye chepeo nyekundu. Macho yake meupe yenye kiini cheusi, yalionekana vizuri nyuma ya miwani myeupe iliyoshikiliwa vema kwa mwamba wa pua yake pana.

“Nahitaji chumba,” Ikunji alisema baada ya kumsalimu.

Mhudumu alimsogezea Kitabu cha Wageni. Akamwekea na kalamu juu ya kitabu. Ikunji akajaza taarifa zake. Alipomaliza akarejesha kitabu pamoja na kiasi cha pesa alichotajiwa.

“Ghorofa ya pili,” mhudumu alisema huku akimkabidhi funguo, “chumba namba 225.”

Hapakuwa na lifti. Kwa hivi, ilimlazimu kupanda vidato vya ngazi kwa miguu. Mandhari ya hoteli pamoja na utulivu wake vilimfurahisha. Alihitaji sehemu tulivu kama ile. Hadi anafika ghorofa ya pili, ni mwanamume mmoja tu aliyepishana naye koridoni akikokota mabegi yake.

Alifungua mlango na kuingia. Alipowasha taa macho yake yalilakiwa na kitanda cha futi tano kwa sita, kilichowekwa upande wa kulia, kikiwa kimetandikwa shuka nyeupe pamoja na mito iliyovishwa foronya za rangi hiyo. Upande wa kushoto, kabati refu na pana lilipangana na jokofu dogo jeupe. Dari na marumaru vilishabihiana kwa rangi ya maziwa. Alikwenda kuketi kitandani huku akiuzungusha mkoba miguuni. Alipoufungua na kujiridhisha usalama wa vilivyomo, akaufunga na kuuweka juu ya meza ndogo, pembezoni mwa kitanda, kisha akjilaza chali.

Haikuchukua muda, alisimama na kujinyoosha viungo. Alitia mkono kwenye mfuko wa suruali na kutoa chaja ya simu. Akaisogelea swichi ya ukutani na kuibandika, kisha akaipachika simu. Ilikwishatimu saa mbili na robo usiku.

Aliingia msalani ambako macho yake yalipokelewa na kioo kirefu, kilichowambwa ukutani juu kidogo ya karo ya maji. Ndevu nyeusi zilimtapakaa mashavuni huku macho yakimlegea kwa usingizi na uchovu wa safari. Shati la mistari ya kahawia na njano pamoja na jinzi ya bluu, havikuonesha taathira ya safari, kwa sababu basi alilopanda, pamoja na ubora wa barabara, havikuruhusu vumbi kupenya ndani yake. Baridi kali iliyokuwa ikizizima kila kona ya jiji la Arusha, ilisababisha mpango wake wa kuoga uyeyuke tamthili ya mvua ya kiangazi juu ardhi kame. Akaishia kujimwagia maji kichwani na kurejea chumbani.

Njaa ilianza kumshambulia tumboni. Akachomoa simu kwenye chaji kabla haijajaza moto lau kidogo. Akachukua mkoba wake na kutoka nje kwenda kutafuta chakula.

Kwakuwa hakuwa akienda mbali, hakuona haja ya kukabidhi funguo. Alimpita mhudumu angali ameketi nyuma ya kaunta. Alitoka hadi nje kidogo tu ya hoteli, ulipo mgahawa wa chakula. Nyuma ya meza kubwa mgahawani, aliketi kwa kujilaza bwana mmoja mfupi, maji ya kunde na mnene kupindukia.

“Habari mzee?” Ikunji alimsalimu.

Bwana yule hakujitaabisha kufunua kinywa. Alitingisha kichwa kama ishara ya kuitika salamu.

Ikunji akaendelea, “Nifanyie chipsi kavu, ndizi mbili na mishikaki mitatu.”

Bwana yule alibaki vile vile amejilaza kizembe hali ya kuwa macho ameyafumba. Kifua chake kipana kilipanda juu na kushuka chini kadri alivyopumua. Baada ya sekunde kadhaa ndipo  alichezesha mboni zake, kisha akafumbua jicho moja kivivu huku tumbo lake kubwa akilikuna kizezeta.

“Utakula hivyo hivyo kavu kama nyoka?”

Ikunji alihisi ghadhabu pamoja na cheko kwa mkupuo. Alitaka kununa, na papo hapo alitamani kucheka. Kila alichofanya mhudumu yule kilijaa mzaha na upuuzi. Ule msemo wa ‘mteja ni mfalme’ ulionekana mgumu kwa bwana yule kuliko msamiati wa ‘kuchina’.

“Okay, niwekee na juisi ya embe.”

Bwana yule alijiinua kidogo, akajitengeneza kitini, na kujinyoosha kwa nguvu hadi kishikizo cha shati kikaachia na kumwacha tumbo wazi. Hakujali hilo.

“Sasa, unaonaje kama ukilipa kabisa ili tukufanyie chap kwa haraka!”

“Ni bei gani?” Ikunji alimwuliza.

“Ukinipa elfu tano utakuwa umejitendea haki,” alijibu huku akiachama mdomo mithili ya mamba anayewinda wadudu.

“Ukifungua akaunti mtandaoni utapata followers wengi sana,” Ikunji alisema, huku akifungua wallet kutoa pesa.

“Kwa nini?”

“Yeah, mtandaoni watu hupendelea zaidi upuuzi.”

“Kwa hivyo unaona nafanya upuuzi hapa, siyo?” aliuliza kwa hamaki.

“Sijasema unachofanya hapa, bali unachoweza kunufaika nacho mtandaoni,” Ikunji alijibu na kumkabidhi pesa huku ametabasamu. “Kama hutojali niajiri nikufungulie akaunti mtandaoni.”

Bila kuongeza neno, aliikwapua pesa toka kwa Ikunji, akifuatisha na msonyo mrefu kama kasuku.

Kwa uvivu aliouonesha bwana yule, pamoja na kisirani chake, Ikunji aliiona dalili ya kusubiri chakula kwa zaidi ya nusu saa. Kwa hivyo, aliona aheri arudi chumbani kuchajisha simu yake, ndipo ashuke tena mgahawani kufuata chakula. Akaondoka.

Alipokifikia chumba na kutaka kupachika funguo kitasani, alishangaa kuona mlango uko wazi. Akakunja sura kiudadisi. Aliposhika kitasa na kusukuma mlango, papo hapo mlango ukadhibitiwa kwa ndani. Ikawa kama mashindano; wa ndani anauzuia – wa nje anausukuma. Alipouachia, ukajibamiza kwa nguvu. Alirudi nyuma hatua kadhaa akiwa bado hajaelewa kinachoendelea. Mwanzo alidhani amekosea chumba. Akainua macho kuangalia namba ya chumba juu ya mlango. Ni chumba namba 225.

Akiwa bado amesimama, macho yalipiga chini ya mlango. Mchirizi wa damu ukitokea chumbani, ulitiririka taratibu sakafuni. Alikunja ndita kiasi cha macho yake kusinyaa. Alihisi damu ikimsisimka kwa woga. Hakuwa tena na ujasiri wala sababu ya kuendelea kusimama. Alirudi hatua moja nyuma na kutimua mbio bila kugeuka.

Alipofika mapokezi aliangaza huku na kule, hakumwona mhudumu. Mtu mmoja tu alikuwa ameketi kwenye viti vya wageni akisoma gazeti. Kwa mtazamo wa Ikunji mtu yule alionekana kama ni mgeni anayemsubiri mhudumu, au ni mtu aliyekaa hapo mahsusi kumshikia nafasi mhudumu aliyetoka kwa dharura.

“Eti, mhudumu yuko wapi?” Ikunji alimsaili mtu huyo baada ya kumsogelea.

Mtu yule aliweka gazeti pembeni, akamtazama, kisha akarudisha macho gazetini kana kwamba hakusikia alichoulizwa.

“Samahani kaka, namuulizia mhudumu,” Ikunji alirudia.

“Ndo salamu hiyo?” alijibu bila kuondoa gazeti usoni.

“Aah!” Ikunji alirusha mikono hewani.

Aligeuza na kutoka nje. Hakuona busara kuendelea kubaki maeneo yale. Alivuka upande wa pili wa barabara na kwenda kusimama mkabala na hoteli. Alihakikisha mkoba haumponyoki kwa namna yoyote. Maswali mia–hamsini–kidogo yalimpitikia kichwani.

Kwanza alifikiri pengine ni mpangaji wa chumba jirani ndiye aliingia chumbani mwake kimakosa, na kwamba alipofika yeye na kufungua mlango kwa nguvu, ndipo ulimbamiza kichwani na kumtoa damu iliyokuwa ikichuruzika. Lakini kumbukumbu zake zote zilimwambia kuwa aliufunga mlango alipotoka.

Sasa ni nani aliyeingia? Alipata wapi funguo? Na dhamira yake ni ipi juu yangu? alijiuliza.

Kadri alivyojilazimisha kutafuta majibu, ndivyo maswali mengi yalichipuka kichwani mwake mithili ya uyoga kichuguuni. Hisia zake ziliposhindwa kumshawishi chochote, akaona ni busara kuondoka eneo lile. Lakini si kabla ya kumpigia simu mkewe kumjuza kilichomsibu. Na kisha Sudi Chotara, mmiliki wa mzigo aliotoka nao Dar es Salaam.

***

Sebastian Mbegu aliwasili nyumbani kwake majira ya saa mbili usiku, akitokea nchini Kanada. Mlango wa kuingilia ndani ulikuwa wazi. Hakushangaa kwa sababu alikwishapewa taarifa na mlinzi getini juu ya uwepo wa mgeni ndani. Aliingia sebuleni akiangaza huku na kule. Alikutanisha macho sako kwa bako na Leila aliyekuwa anapanga vyombo kabatini.

 “Oh, Leila!” Sebastian alisimama na kuweka begi sakafuni.

 Leila aliyekuwa amevalia shimizi nyepesi ya rangi ya samli, iliyoishia juu ya magoti, ikiacha wazi sehemu kubwa kuanzia mabegani hadi makwapani, aliachia tabasamu hafifu. Akaachana na vyombo kabatini na kumwelekea Sebastian. Kila hatua alizopiga, miguu ilipishana mithili ya Twiga. Mikono yake iliyotengeneza mbonyeo kwenye maungio ya viwiko, ilipepea taratibu mithili ya kishada kiendacho arijojo.

“Karibu, bosi,” Leila alimlaki kwa insafu, huku akiinama kuchukua begi.

Sebastian aliwahi kumshika mikono kabla hajakamata begi. Akamnyanyua huku akimtazama machoni. “Asante Leila. Unapendeza mno ukiwa katika kivazi cha nyumbani.”

“Asante,” Leila alisema na kukwepesha macho pembeni. “Pole kwa uchovu.”

“Aah, shukrani. Nilipokuona tu, uchovu wote ukayeyuka.”

Leila akatabasamu asiwe na la kuongezea.

“Nawe pole kwa usumbufu,” Sebastian alisema angali amemshika mikono. “Kusafisha jumba lote hili si kazi ndogo.”

“Usijali. Wanawake tumeshazoea shughuli hizi.”

Kimya kilitanda kila mmoja akipandisha na kushusha pumzi. Sebastian aliendelea kumchezea Leila viganja vya mikono yake kwa namna iliyoibua ghamu.

“Nilikumiss, Leila,” Sebastian alivunja ukimya.

“Mimi pia.”

Kama aliyekuwa akisubiri jibu hilo, Sebastian alimwinamia na kumbusu kwenye paji la uso. Kisha, akamzungushia mkono wa kushoto kiunoni ilhali wa kulia akiupeleka kichwani kumchezea nywele nywele.

Leila alihisi vipepeo vikimnyevua mwilini. Bila ajizi, naye akainua mkono wa kulia na kumwekea begani, hali ule wa kushoto akimwekea kifuani. Alihisi chemchemi ya asali ikimtiririka ndani ya uti wa mgongo wakati Sebastian alipopenyeza mikono ndani ya shimizi yake na kuipachua loki ya sidiria. Aliinua macho kumtazama wakati sidiria ikadondokea katikati ya miguu yao. Kasi ya upumuaji ilimwelemea. Akaachama mdomo.

Sebastian alitumia fursa hiyo kumpokea. Papi za midomo yao ziligandana kwa sekunde kadhaa, kabla Sebastian hajambeba Leila na kwenda kumbwaga taratibu kwenye makochi.

“Seba,” Leila alinong’ona, macho yakiwa nusu mduara kama mbalamwezi. “Please, naomba iwe siri.”

Kabla Sebastian hajajibu chochote, simu ya Leila iliyokuwa mezani iliita. Wakaganda kwa pamoja wakiisikilizia.

“Oh my God,” Leila alisema kwa mshituko, akimsukuma Sebastian pembeni. “Ikunji huyo anapiga simu.” 

“Umejuaje kama ni yeye?”

“Mwito huo nimemsetia yeye.”

Akiwa amebakiwa na nguo ya ndani tu, Leila alisimama na kujongea mezani. Akaikwapua simu yake mezani huku akitweta. Aliendelea kuitazama ikiita hadi alipojiridhisha kuwa pumzi zake zimekwishatulia.

“Hallow!” 

Kimya.

Akaita tena, “Hallow mume.”

Hakuna majibu. Akatoa simu sikioni na kuitazama. Bado ilikuwa hewani.

Alipoirejesha tena sikioni, pumzi nzito upande wa pili wa simu ilisikika ikipanda na kushuka. Alipotaka kuongea tena, ndipo akamsikia: “Leila, uko wapi?”

Dhambi huandamwa na hofu ya kukamatwa. Kuulizwa yuko wapi, kumlimfanya ahisi kugundulika. Taratibu mapigo ya moyo yakaanza kushika kasi kama garimoshi.

Sasa ajibu nini? Hayupo nyumbani. Hayupo kazini. Yuko kwa Sebastian.

“Ahm… niko… niko nyumbani. Kuna nini kwani?”

“Una–” Simu ilikatika kabla Ikunji hajamalizia alichokusudia kusema.

“My God,” Leila alisema, huku akiiondoa simu sikioni na kuitazama.

“Kuna nini mpenzi?” Sebastian alijiinua sofani na kumfuata Leila mezani.

“Iku ameniuliza niko wapi? Halafu sauti yake haiko sawa kabisa,” alimjibu huku macho yangali yameganda simuni. “Kuna kitu ametaka kusema lakini simu imekata.”

“Sasa wahi kumpigia kabla hajapiga tena. Jiamini. Akirudia tena swali hilo, mwambie uko maeneo ya nyumbani, jifanye hata uko dukani.”

“Je, kama kuna mtu aliniona nikiingia humu kwako ndo akampigia?”

Swali hilo lilimvuruga kichwa Sebastian. Akaanza kunusa harufu ya hatari. Sebastian na Ikunji walipata kuwa marafiki; Ikunji akiwa ni msimamizi kwenye kampuni ya Sebastian inayohusika na michezo ya bahati nasibu. Ilikuwa ni wiki baada ya mzee Dominic Mbegu, kaka yake na Sebastian, kuugua ghafla kiharusi kiasi cha kushindwa kufanya kazi, na kumteua Sebastian, kwa kushirikiana na mke wa mzee Mbegu, kusimamia makampuni yake, ndipo siku hiyo Sebastian alimjia Ikunji na habari iliyozaa uhasama baina yao.

“Niambie kaka,” Ikunji alimlaki Sebastian. “Ofisi mpya inakwendaje?”

“Nashukuru Mungu nimeingia na mguu wa bahati,” Sebastian alijibu huku akiketi. “Nimefika tu nimekutana na mwajiriwa mpya huyo; kifaa cha nguvu. Haraka nimemwamishia ofisini kwangu kama msaidizi wangu.”

Kengele ya hatari iligonga kichwani mwa Ikunji. Ni kipindi kama cha mwezi mmoja nyuma, Leila alikuwa ameajiriwa katika kampuni hiyo ya mzee Mbegu. Wakati huo walikuwa kwenye uchumba. Hofu yake ikawa, isijekuwa Sebastian anamaanisha Leila.

“Anaitwa nani?” Ikunji alimsaili.

Alipotajiwa jina la Leila, Ikunji alihisi kisu cha moto kikimchana katikati ya moyo wake. Baada ya Sebastian kumwaga sifa za Leila, ndipo Ikunji akamweleza kuwa Leila ni mchumba wake.

“Umeshaanza, kila mwanamke ni mchumba wako. Kwa huyu bora tugombane. Mwenye kisu kikali ndiye atakula nyama.”

Siku hiyo, baada ya kutoka kazini, Ikunji alikutana na Leila na kumsaili kila nukta kuhusu Sebastian. Leila alikiri kuhamishiwa ofisini kwa Sebastian, na alikiri kuwa Sebastian alianza kuonesha dalili za kuvutiwa naye. Kadri siku zilivyokwenda mbele, Sebastian alianza kudhihirisha ghadhabu zake kwa Ikunji. Kazi ikatawaliwa na nongwa na visasi. Majukumu yasiyotekelezeka yakaongezeka. Mifarakano ya mara kwa mara ikashamiri. Hatimaye ikamlazimu Ikunji kuacha kazi.

Ili kumkata ngebe Sebastian, mwezi mmoja baada ya kuacha kazi, Ikunji alifunga ndoa na Leila. Dhamira ya Ikunji ikawa ni kumwachisha kazi Leila pindi atakapopata ajira sehemu nyingine. Haikuwa hivyo, alipuyanga takribani mwaka mzima bila kupata kazi. Kila senti aliyohifadhi ilipukutika kama nywele kwenye kichwa cha mtoto mwenye vibarango. Akaanza kuishi kwa kutegemea mshahara wa mkewe.

Uhasama huo baina ya Ikunji na Sebastian, Leila aliufahamu vilivyo. Kwa hivi alijua bayana kuwa, endapo Ikunji amegundua kuwa ameingia nyumbani kwa Sebastian, hakuna ushawishi utakaopenya masikioni mwake ili kuuhadaa ubongo wake.

Bila kufanya zohali, Leila aliufanyia kazi ushauri wa Sebastian. Akabofya namba za Ikunji na kubandika simu sikioni.

Namba unayopiga kwa sasa haipatikani, tafadhali jaribu tena baadaye.

“Nahisi kuna kitu hakiko sawa, Seba,” Leila alisema. “Hapatikani. Acha tu niende.”

Sebastian alianza kuhisi mchoko wa safari ukimwingia ghafla. Moto wa mapenzi ulikwishawaka kichwani mwake. Kuachwa ghafla namna ile kulimsononesha.

“Leila, natamani kukuzuia usiende.”

“Usijali, Seba. Next time.”

Leila alimalizia kuvaa nguo zake. Akaita usafiri wa Uber na kuondoka.

****

Ikunji alisonya kwa ghadhabu baada ya simu yake kuishiwa chaji na kujizima. Hakuwahi kumwambia chochote Leila. Kibaya zaidi, hata Sudi Chotara hakumpigia simu tangu alivyowasili jijini Arusha.

 Sudi Chotara ni mfanyabiashara wa madini, ambaye licha ya ukwasi mkubwa anaomiliki, hakuendekeza anasa wala ghururi za dunia. Alijitenga mbali na ayuni katika nyendo zake kiasi kwamba, akafanikiwa kudhibiti mawimbi ya umaarufu wake.

Urafiki wa Sudi na Ikunji hauna muda mrefu tangu walipofahamiana. Ni Sudi ndiye aliyeanza kuvutiwa na Ikunji, takribani miezi mitatu nyuma, alipofika Dar es Salaam kwa mfanyabiashara mwenziye wa dhahabu, ambapo Ikunji ni mfanyakazi.

“Vipi biashara?” Sudi alianza kumsaili Ikunji, aliyekuwa ameketi dukani.

“Aah kidogo kidogo kadri ya hali…kuna nyakati za maji kupwa na maji kujaa.”

Hivyo ndivyo mahusiano yao yalivyoanza kumea. Baada ya Sudi kugundua umakini wa Ikunji, alizidi kuimarisha mizizi ya ukaribu wao.

“Nafikiri tunahitaji kuzungumza kidogo kuhusu maisha,” Sudi alipata kumwambia Ikunji siku moja alipofika hapo dukani.

Baada ya muda wa kazi, walikutana maeneo ya Posta, kwenye mgahawa wa New Grano Coffee. Ikunji ndiye alikuwa wa kwanza kuwasili, robo saa kabla ya muda wa miadi. Kwa mshangao, alimkuta Sudi Chotara tayari ameketi mgahawani. Sudi akamlaki Ikunji kwa taadhima kubwa.

Baada ya kuketi na kusabahiana, Sudi alianzisha mazungumzo, “Kwanza, kama hutojali, ningependa kujua una muda gani tangu uajiriwe pale dukani, na una mkataba wa muda gani?”

Si swali lililompendezesha Ikunji. Akapiga kimya kwa sekunde chache akitafakari. Lakini kwakuwa alikwishaanza kuelewa dhamira ya Sudi, akajibu, “Sina mkataba. Bado sijaajiriwa rasmi.”

“Vema. Sasa, kuna kazi nataka tufanye pamoja. Nitakulipa vizuri.”

Ikunji alipandisha nyusi zake juu kama ishara ya kumtaka Sudi afafanue zaidi kuhusu kazi hiyo pamoja na malipo yake.

“Kwa ufupi, mimi na bosi wako tunafanya kazi kwa muda mrefu sasa. Lakini mwaka jana, alitaka kununua kizimba cha dhahabu Geita. Nikamkopesha pesa nyingi. Mpaka leo malipo yamekuwa tabu. Tukaafikiana kuwa, ataniachia soko hapo dukani ili nikilangua dhahabu kwa bei ya chini na kwenda kuuza kwa bei ya juu, nitajilipa kiasi cha gharama zangu. Nalo limeshindikana. Ananipa wateja watatu kati ya kumi mnaowapata.”

“Aah. Pole sana. Niliwahi kusikia hizo story hapo dukani nilipoanza kazi, lakini sikujua kama ziko kwa ukubwa huo.”

“Ndo hivyo. Sasa, kwakuwa wewe ndiye unayepokea wateja. Nataka tufanye kazi mimi na wewe bila kumshirikisha bosi wako.”

Kazi  yenyewe ilikuwa ni Ikunji kudhibiti wafanyabiashara wa dhahabu, wanaofika dukani kuuza dhahabu zao na kupatana nao bei kabla hawajaingia ndani kuuza, kisha azilangue kwa niaba ya Sudi Chotara. Sudi aliahidi kuwa anamtumia pesa kwa ajili ya kufanikisha biashara ile. Kiasi alichopanga kumlipa, ni mara dufu ya alipwavyo hapo dukani. Ingelikuwa muhali kwa Ikunji kukataa ofa ile.

Biashara hiyo mpya ya siri, ilikuwa ni yenye tija kwa Ikunji. Akaifanya kwa ustadi na uangalifu mkubwa. Ikafika safari ya mwisho ambapo mzigo aliolangua ulikuwa mkubwa. Sudi akamtaka asafiri nao hadi Arusha, ili pamoja na mambo mengine, wapate wasaa wa kufanya makubaliano makubwa zaidi kibiashara. Ikunji akamfikia bosi wake. Akaomba ruhusa kwa kisingizio kuwa anaumwa. Aliporuhusiwa, akafanya safari ya siri kwenda Arusha.

 Akiwa bado amesimama mkabala na hoteli, Ikunji aliendelea kutafakari ikiwa ni salama kwake kurudi hotelini au kuondoka. Hatimaye alikata shauri. Aheri ya nusu shari kuliko shari kamili. Alimfuata dereva bodaboda aliyekuwa ameketi juu ya pikipiki yake.

“Wapi nitapata hoteli nzuri? Isiwe mbali sana na hapa.”

 Dereva bodaboda alimtazama Ikunji usoni kwa muda, akamwambia. “Kaka, naitamani kweli hela yako, lakini kama ni hoteli tu ingia hapo patakufaa.” Alimwonesha hoteli ile ile aliyoikimbia.

 “Sihitaji mitaa hii.” Ikunji aliitazama hoteli aliyotoka, bado hakukuwa na dalili zozote za utata.

“Basi sawa,” dereva alijibu huku akivaa vizuri koti lake pamoja na kofia. “Twende Sanawari kuna hoteli nzuri pia.”

 Ikunji alipanda pikipiki bila kuongeza neno. Wakaondoka. Mwendo wa dakika tano, waliwasili na kuegesha nje ya Nyati Inn Hotel. Akateremka na kulipa nauli aliyotajiwa, kisha akatembea kuelekea ndani. Pale Mapokezi, alilakiwa na mhudumu wa kiume. Safari hii, hakujaza majina halisi kwenye kitabu cha wageni, akihofia usalama wake. Baada ya kulipa akapatiwa ufunguo na maelekezo. Ghorofa ya tatu. Chumba namba 397. Kama ilivyo hoteli ya mwanzo, hii pia haikuwa na lifti. Hivyo alipanda juu kwa miguu.

Koridoni, ghorofa ya tatu, alikutana na mama mmoja mnene, mfupi, maji ya kunde, akitokea mwishoni mwa korido ile. Aliambaa upande wa kushoto ili kurahisisha upishanaji. Katika hali asiyoitegemea, mama yule naye alihama upande aliokuwa na kumfuata usawa wake. Walipokaribiana akasimama.

“Mambo,” mama yule alimsalimu huku ametabasamu.

Meno yake ya mbele yalikuwa ya rangi ya dhahabu. Alivalia fulana nyeupe yenye kola ya kijani, na bukta pana nyeusi iliyoshuka hadi chini ya magoti. Chini ya makwapa, juu ya fulana, aliongezea kujitanda kwa upande wa khanga. Miguuni alivaa raba nyeusi zenye ufito mweupe.

“Safi, shikamoo,” Ikunji alimwamkia. 

“Karibu mdogo’angu.” Aliikwepa shikamoo. “Utahitaji chakula nikuletee?”

“Oh hapana, dada. Asante.”

“Hapa hotelini hawauzi chakula.” Aliweka chini mifagio pamoja na ndoo iliyokuwa na chupa za sabuni pamoja na vitambaa vya kusafishia vioo. “Kama ukitaka nitakufuatia kule mtaa wa pili. Wanatengeneza chakula safi kabisa; kuna biriani kuku, makange ya mbuzi, mandi ya kondoo, pia wanauza sek–”

“Sawa dada, nikihitaji kula nitakuagiza.”

“Poa mdogo’angu. Na kama umechoka sana, naweza kukuletea mtu wa kukufanyia masaji. Nina wasichana wazuri hapa. Wazuri mno. Ikiwa utapenda alale chumbani mwako, nitakuchagulia dogodogo.”

“Ondoa shaka. Nitakucheki,” Ikunji alimkatiza. Akamshika mkono na kumkabidhi noti. Walau akaweza kupata upenyo na kumpita.

Hadi Ikunji anaufikia mlango wa chumba, mama yule alibaki palepale akiendelea kushukuru kwa takrima aliyokirimiwa.

Ikunji aliingia chumbani akiwa amechoka akili kuliko mwili. Akaenda moja kwa moja kujibwaga kitandani. Chumba hakikutofautiana sana na kile alichokikimbia, kwa ajili hiyo, tukio zima likaanza kurindima kichwani mwake. Dhana ilimganda kichwani kwamba, ni wahalifu tu ndiyo waliofungua chumba chake ili wakwapue mkoba. Alihisi kuna watu wameshajua kuwa amebeba dhahabu. Changamoto ni kwamba hakujua wamejuaje, kwani zaidi ya mkewe, pamoja na mzee Kizamba, mume wa shangazi yake, hakuwahi kumwambia mtu mwingine yeyote kuhusu safari yake ya kupeleka dhahabu Arusha.

 Aliingia msalani akiwa na mkoba wa dhahabu kwapani. Safari hii alijilazimisha kuoga ili kuupumzisha mwili. Alipotoka akafungua runinga ili kupunguza mawazo. Kila idhaa aliyofungua haikumpa afua. Akaamua kuacha muziki ukiendelea kujiburudisha wenyewe. Alitamani kushika simu ili kuperuzi, lakini haikuwa na chaji. Na isivyo bahati, hakuwahi kuchukua chaja yake hotelini alikokimbia. Akabaki amejilaza chali kitandani akiendelea kuwaza hili na kuwazua lile. Usingizi usivyo na hiyana ukamchota.

 Aliota amebebwa kwenye gari ya wagonjwa, akiwahishwa hospitalini baada ya kupigwa risasi na majambazi waliomvamia, ili kumwibia mkoba wa dhahabu. Aliyeongoza genge la majambazi waliomshambulia alikuwa ni Sudi Chotara. Na dereva wa gari la wagonjwa, aliyekuwa akihangaika kuokoa maisha yake ni Sebastian Mbegu. Alistaajabu mno. Iweje Sudi Chotara, ambaye ndiye tajiri yake mpya, amtumie majambazi kukwapua dhahabu zake mwenyewe? Halafu kwa vipi Sebastian Mbegu, ambaye ni adui yake mkubwa, awe ndiye dereva wa gari ya wagonjwa anayepambana kuokoa maisha yake?

 Akiwa amelazwa kwenye machela, Ikunji alihisi maumivu makali ya kichwa, yaliyokuwa yakichagizwa na kelele za ving’ora vya gari hiyo ya wagonjwa.

“Zima hivyo ving’ora tafadhali,” Ikunji alimpigia kelele Sebastian.

 “Bila ving’ora hatutopata nafasi ya kupenya kwenye foleni. Tunafanya hivi kwa ajili yako. Vumilia maumivu ya muda mfupi kwa ajili ya faraja ya muda mrefu,” Sebastian alijibu, akiendelea kukamatia usukani.

Sauti za ving’ora ziliendelea kupenya masikioni mwake. Kichwa kilizidi kumuuma mara dufu. Uzalendo ukamshinda. Akapiga kite kwa ghadhabu na kujiinua kwa nguvu kwenye machela. Nguvu aliyotumia kujiinua kwenye machela, ndiyo ilimnyanyua ghafla kitandani na kushituka toka usingizini.

Aliketi kitendani. Alijinyoosha mwili huku akitweta. Akaupapasa mkoba wake mchagoni. Kabla hajaitafakari ndoto aliyoota, aliduwaa macho yake yalipopiga kwenye saa ya ukutani. Ilikwishatimu saa kumi na mbili asubuhi. Siku ya pili jijini Arusha.

 Ina maana nimepitiliza hadi asubuhi? alijiuliza kwa mshangao.

 Akiwa ameketi kitandani ndipo alipogundua kuwa, sauti za ving’ora zilizomtaabisha usingizini, zilikuwa zikitoka runingani, ingawaje si kwenye gari ya wagonjwa kama alivyoota, bali kwenye magari ya polisi yaliyotanda nje ya jengo kubwa huku umati wa watu ukitapakaa mbele ya tepe za njano zilizofungwa na polisi, kuzunguka eneo lote la jengo hilo.

Ikunji alipikicha macho mara mbili, akihisi kulitambua jengo lililozungukwa na polisi runingani. Alipothibitisha hisia zake aliketi sawia, macho runingani, mikono mapajani. Ilikuwa ni White Rose Hotel. Hoteli ile ile alikokimbia usiku uliopita.

 Baada ya hekaheka za maofisa wa polisi, walioonekana kupita huku na kule, kuchunguza hiki na kile, pamoja na kuzungumza hili na lile kupitia redio zao za upepo, hatimaye alionekana Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, ACP Livinus Kamugisha, akithibitisha kutokea kwa tukio:

“…tulifika hapa mara baada ya kupigiwa simu na uongozi wa hoteli, ndipo tukakuta mwanaume mmoja ameuawa ndani ya chumba namba 225 kilichopo ghorofa ya pili.”

 “Mungu wangu!” Ikunji alijitwisha mikono kichwani huku akisimama toka kitandani.

 Chumba kilichotajwa ndicho alichokuwa amepanga na baadaye kukuta damu ikitiririka mlangoni. Kitendo cha mtu kukutwa ameuawa humo, kitamfanya kuwa mtuhumiwa namba moja. Ikunji alitulia kusikia sehemu ya mwisho ya maelezo ya Kamanda wa Polisi, yaliyourarua moyo wake mara elfu zaidi.

“…maiti imekwishatambuliwa. Ni mfanyabiashara wa madini, aliyefahamika kwa jina la Sudi Chotara.”

“No!” Ikunji alipayuka huku akisimama na kujipigapiga kichwani. “Sudi? Haiwezekani.”

Baada ya ACP Kamugisha kumaliza kuthibitisha tukio hilo, mtangazaji aliihitimisha taarifa ile, na vipindi vingine vikaendelea. Ikunji alijipigapiga kichwani akidhani yungali ndotoni.

Inawezekanaje? alijiuliza.

Bado hakuamini kila alichokiona na kukisikia. Kwamba mtu aliyemfuata jijini Arusha ndiye ameuawa, tena ndani ya chumba alichopanga yeye.

Ina maana ile damu iliyokuwa ikitiririka toka mle chumbani ilikuwa ni ya Sudi? aliendelea kuwaza.

Tukio zima likaanza kujirudia kichwani mwake.

***** NI NANI aliyemuua Sudi Chotara? Na iweje maiti yake ikutwe chumbani mwa Ikunji? Itakuwaje hatma ya Ikunji? Na vipi kuhusu Leila na Seba?

Tutaendelea na hadithi hii hapo kesho, ifikapo saa kumi na mbili jioni. Cha msingi hakikisha, unaLike, comment, na kuShare ili iwafikie wasomaji wengi zaidi.




Ndani ya chumba cha upelelezi, Kituo Kikuu cha Polisi, Sajini James Kinabo aliketi kwenye dawati lake. Alivalia koti la rangi damu ya mzee, kwa ndani fulana ya kijivu ikionekana. Kofia ya mzula ilifunika sehemu kubwa ya kichwa chake hadi usawa wa masikio. Nyusi zake pana zilitengeneza nusu mduara juu ya macho yake, huku ndevu zikiwa zimechongwa mduara kuzunguka mdomo wake.

Mezani palikuwa na kikombe cha chai, faili moja lenye karatasi chache katikati. Simu janja yenye kioo kipana iliendelea kucheza video ya wimbo wa BongoFlavor kwa sauti ya chini. Mbele ya meza, aliketi kwenye benchi, bwana Alphonse Mmari, meneja wa hoteli yalikotokea mauaji. Kinabo alivua glavu na kuziweka mezani, kisha akapikicha viganja vya mikono kwa sekunde kadhaa. Baridi ilikuwa imeshitadi vilivyo jijini Arusha.

 “Bwana Mmari, unakumbuka muda ambao mauaji yalitokea?” Kinabo alisaili.

 “Ha–pa–na siwezijua ni muda gani. Sikuwepo huko chumbani kipindi tukio linatokea. Nachokumbuka nilikuwa ofisini majira ya saa mbili, Glady aliponipigia simu kunipa taarifa ya damu inayotoka chumbani kwa mteja, ndipo tukaenda na kukuta maiti.”

 “Ulitumia kifaa gani kumpima ili kujua kuwa amefariki?”

“Sikumpima.”

 “Lakini umesema mlikuta maiti!”

 “Kwa mwonekano tu tulijua amekufa.”

 “Mwonekano upi?”

 Mmari alivuta pumzi nzito na kuziachia taratibu. Akasema kwa sauti iliyopungua kasi, “Alikuwa hapumui tena, na alishaanza kubadilika rangi na kuwa kama wa zambarau. Hata macho yake yalikuwa kama yameanza kudidimia kwa ndani.”

 Sajini Kinabo aliinama kuandika kwenye faili lake. Alipoinua uso akamtazama Mmari na kupandisha nyusi juu kumwashiria aendelee kuzungumza.

 “Tulipofika eneo la tukio, tulikuta mlango uko wazi. Lakini kabla hatujaingia, tuliwagongea wapangaji wa vyumba jirani, tukaingia nao pamoja. Tulikuta mwili umelala sakafuni, damu ikiwa imetapakaa sehemu ya nyuma ya kichwa chake.”

 Kinabo alinyanyua kikombe cha chai, akapiga funda moja, kisha akakirudisha mezani kabla ya kuuliza, “Hoteli yenu ina kamera ngapi?”

 “Haina kamera.”

 “Oh, mlijipanga vizuri sana,” Kinabo alisema, akigongagonga kalamu mezani. “Maiti haikukutwa na pesa wala kipande cha dhahabu. Si jambo rahisi Sudi kutembea mifuko mitupu. Je, unadhani ni nani aliyemchomoa mali na pesa zake?”

 “Mnh! Hapana. Siwezi kujua hilo.”

 “Unadhani ni nani aliyemuua Sudi?”

 “Mpaka sasa sina ninayemhisi.”

 “Kama huna unayemhisi na ilhali ameuawa hotelini kwako, then wewe ndiye mtuhumiwa wa nambari moja. Na umefanya hivyo pamoja na wenziyo kujipatia mali za bure.”

 Mmari aliduwaa kwa sekunde kadhaa. Mishipa ya kichwa ilimtutumka huku mashavu yakimtetemka. Akasema, “Hata angelikuwa na pesa nyingi kiasi gani, nisingekuwa mjinga kumwua ndani ya hoteli yangu.”

 “Sasa utachagua mwenyewe, kueleza ukweli hivi sasa au mpaka tukakukamue kwanza biringanya,” Kinabo alisema na kusimama. Akaizunguka meza kwa mbele na kuketi juu yake, mguu mmoja chini, mwingine ukining’inia juu. “Kwenye maelezo yenu mmesema Kitabu cha Wageni hakionekani. Ni nani aliyekichukua?”

 “Bado sijafahamu, afande. Lakini leo nikirudi nitakwenda kutaf–”

  “Huwezirudi leo. Wala kesho. Wala keshokutwa.”

 Pamoja na baridi kutanda kila kona ya jiji la Arusha, Mmari alihisi jasho likitota makwapani. Alizifahamu hekaheka za polisi.

 “Koplo Kisesa,” Kinabo alimwita askari aliyekuwa ameketi nyuma ya meza nyingine, pembezoni mwa chumba. “Niletee yule msichana. Huyu bwana akanisubiri selo. Nitaongea naye tena kesho akishabanikwa kidogo jikoni.”

Kisesa alimchukua Mmari na kutoka naye. Kinabo akarudi kuketi nyuma ya meza yake. Haikuchukua muda, Kisesa alirejea ofisini na msichana mnene, mweupe, aliyevaa dera la manjano, kichwani akijitanda kilemba cheusi.

“Glady, wewe ndiye ulikuwa zamu wakati tukio limetokea?” Kinabo alimrushia swali kabla hajaketi.

 “Ndio afande,” Gladness alijibu angali amesimama. Sauti yake ilitetema kwa hofu.

Kinabo alimwashiria kwa mkono aketi. Akatii.

 “Hebu niambie, Sudi Chotara alipofika kuchukua chumba, alikuwa peke yake au alikuja na yule jamaa’ke?”

 “Hapana. Sikumhudumia Sudi. Na wala sijawah–”

 “Kumbe ni nani uliyempa hicho chumba namba 225?”

 “Ni mteja mwingine aliyechukua chumba hicho.”

 “Anaitwa nani?” Kinabo aliuliza, akichukua kalamu na kufunua faili kwa ajili ya kuandika.

 “Simkumbuki jina.”

 Kinabo aliinua uso kumtazama Gladness akiwa amefura. Akaweka kalamu pembeni na kufunika faili.

“Unajaribu kunitania? Mauaji yametokea kazini kwako, kwenye chumba ulichopangisha wewe, Kitabu cha Wageni kikiwa mezani kwako, ulishindwaje hata kupekuapekua tu ili kuhakiki taarifa za mteja baada ya tukio kabla hujakiondoa?”

 Pumzi zilianza kumzidia Gladness. Macho yalimtoka pima. Mishipa ya kichwa ilikuwa ikimdunda mithili ya koromeo la kinyonga. “Hmh…hapana afande… mi si–jaki–ficha.”

 “Hakuna aliyesema umekificha. Nimesema ulikiondoa. Mmari amesema pia we ndiye unajua kilipo.”

 “Haki ya Mungu sikukiondoa.”

“Kwa maana hiyo Mmari anakusingizia? So, ni yeye ndo alikiondoa?”

 “Mi sikumwona aliyekichukua.”

 Kinabo alifumbata mikono kifuani huku macho yangali kwa Gladness. Baada ya ukimya wa muda mfupi, akamtupia swali lingine, “Ulijuaje kuwa damu inavuja chumba namba 225?”

 “Mi nilikuwa kaunta wakati mama Linda alipokuja mbio kuniamb–”

 “Mama Linda ndo nani?”

 “Ni mfanya usafi pale hotelini.”

Gladness akapiga kimya. Sajini Kinabo akatikisa kichwa kumwashiria aendelee. Akaendelea, “Akaniambia alikuwa anadeki koridoni ndipo akaona damu ikitoka humo chumbani.”

 “Ulipokwenda kumpa taarifa Mmari ofisini mwake, ulimkuta anafanya nini?”

 Gladness alipiga kimya. Alionekana kuchanganywa na swali lile. Kinabo akamtazama kwa macho makali kuashiria hitaji la majibu ya haraka.

“Nilimkuta amekaa mezani anachezea simu.”

 Mmari alisema kuwa alipigiwa simu na Gladness kujulishwa kuhusu damu inayotokea chumbani. Gladness anasema alimfuata Mmari ofisini kumjulisha juu ya kadhia hiyo. Alimpigia simu au alimfuata ofisini? Siku zote, hakuna kweli mbili zinazokinzana. Lazima kuna mmoja amedanganya – ni nani? Na kwa maslahi gani? Kinabo alijiuliza. Akafunua faili na kuandika.

Alipoinua kichwa, Gladness akaendelea kuzungumza, “Mi nilirudi kaunta, wakati Mmari na mama Linda wakipanda ghorofani.”

 “Kwa nini uliamua kumfuata ofisini badala ya kumpigia simu?”

 “Nilihofia angechelewa kupokea, nikaona nimfuate haraka.”

 Kinabo alipachika mguu mmoja juu ya mwingine, mikono akiipakata mapajani, huku akitikisa kichwa taratibu. “Yaani kutoka kaunta hadi ofisini kwa Mmari – ghorofani – ni rahisi zaidi kuliko kumpigia simu?”

 Gladness hakujibu.

Kinabo akaendelea, “Muda huo ulikuwa umeshajua kuwa kuna mtu amekufa chumbani?”

 Gladness alitikisa kichwa kukataa.

 “Kwa hiyo unataka kuniambia kilichokufanya ukahamaki hadi ukamfuata Mmari ofisini, badala ya kumpigia simu, ni damu tu? Yaani damu tu?”

 “Si kwa sababu ya damu tu. Mara nyingi kukiwa na dharura huwa namfuata ofisini moja kwa moja.”

 “Ulijuaje kuwa kitabu cha wageni hakipo mezani?”

 “Niliporudi kaunta, kabla akina Mmari hawajarudi, aliingia mgeni kutaka chumba. Nilipoangalia Kitabu cha Wageni hakikuwepo mezani. Wakati nakitafuta ndipo akina Mmari walishuka wakisema kuna maiti chumbani.”

 “Ukimwona unaweza kumkumbuka?” Kinabo aliuliza huku akitazama saa yake ya mkononi, “I mean huyo mteja aliyepanga chumba namba 225.”

 Gladness alifinya macho kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu, kisha akabetua mdomo na kutikisa kichwa. “Sina hakika. Ni kama dakika 15 tu zilipita tangu achuke chumba ndipo likatokea tukio hilo. Sikuwahi kumkariri vizuri.”

 Kinabo aliuma papi ya chini ya mdomo wake. Akasimama na kuanza kutembea akikizunguka chumba kama mfalme anayehakiki mipaka ya himaya yake. Akaenda kusimama nyuma ya Gladness.

 “Sikia Glady,” alisema huku mkono mmoja akimwekea begani. “Inabidi unisaidie ili nikusaidie. Maiti imekutwa chumba namba 225. Kitabu cha Wageni kimepotea. Hakuna anayemjua mtu aliyechukua chumba hicho. Ni wewe pekee ndiye ulimwona wakati akiingia. Ukisema humkumbuki itabidi wewe ndiye uwe mtuhumiwa namba moja.”

 Gladness alihisi tumbo likimcheza. Akainamia mapaja huku uso akiufambata viganjani. Kinabo akarudi mezani na kuketi.

“Humkumbuki jina, hukumkariri sura, na wala hujui kitabu kilipo. Tukisema ni wewe ndiye uliyemuua utakatalia wapi? Sasa nisaidie jambo la mwisho, ni nani unayemhisi kuhusika na mauaji yale?”

 Gladness aliinua uso ukiwa umetota machozi. Akasema, “Ni tukio la ghafla. Sijamhisi mtu yeyote.”

***

Ikunji alikwapua mkoba wake. Akauvaa vizuri begani na kutoka nje. Akiwa anamaliza kufunga mlango, sauti ya mtu nyuma yake ilipenya masikioni. “Hey!”

 Aligeuka kwa taharuki. Tayari alikwishaanza kuishi kwa mashaka. Alikutanisha macho na yule mama aliyekutana naye koridoni usiku. Wakasabahiana.

 “Mbona jana hukunicheki tena? Ina maana ulilala bila kula?”

 Kutajiwa chakula tu ndipo akahisi utumbo ukimcheza kwa njaa. Tangu alipowasili jijini Arusha, kuanzia White Rose mpaka hapo Nyati Inn, hakupata nafasi ya kutia kitu mdomoni.

“Oh, nilipotoka sikukuona,” alimdanganya.

 “Ungeniulizia tu. Naitwa Nyakanga.”

 “Okay, hakijaharibika kitu. Basi naomba ukaniletee supu ya ng’ombe, chapati mbili,” alisema huku akitoa pesa kumpatia Nyakanga, “na chaja ya simu. Ni smartphone ya namna hii.”

 Nyakanga alipokea pesa na kuondoka.

Ikunji alifungua mlango na kurudi chumbani. Kiasi cha dakika kumi, Nyakanga alirejea na vyote alivyoagizwa. Ikunji alimshukuru na kumpatia ujira wake. Cha kwanza, alichomeka simu kwenye chaji kisha akaanza kula. Alipomaliza kula, akawasha simu kabla hata haijajaa. Alianza kumpigia mzee Kizamba. Licha ya utofauti mkubwa wa umri baina yao, ilitokea tu wakashikana urafiki kwa kiwango kikubwa. Wakawa kama chanda na pete, au ulimi na mate, au uta na upote.

Mzee Kizamba alipokea simu kwa wahka. “Niambie kilichotokea?”

Ikunji alipigwa butaa. Swali la mzee Kizamba lilimstaajabisha na kumhofisha. Ni dhahiri mzee Kizamba amekwishajua kinachoendelea.

“Kivipi?”

“Nimeona kwenye vyombo vya habari,” mzee Kizamba alisema kwa sauti ya chini, “kuwa Sudi Chotara ameuawa. Nikakupigia hukupatikana. Mlikuwa mmeshaonana?”

Ikunji alishusha pumzi. Akamsimulia mkasa wote bila kuruka nukta wala koma. Ni simulizi ya ajabu isiyokubali kupenya kwenye masikio ya mtu yeyote makini. Isingelikuwa usuhuba mkubwa baina yao, basi mzee Kizamba angeomba kushushwa kwenye treni hiyo ya kufikirika.

“Pana jambo hapo. Yumkini ni mpango uliosukwa dhidi yako. Lakini, cha kujiuliza, hao waliosuka huo mpango walijuaje kama ungelifikia hoteli hiyo?”

“Hapo nami ndo nalewa bila kunywa. Kila nikifikiri sipati jibu.” Alinyama kupisha mate yamlainishe koo. “Kosa kubwa nililofanya, niliandika majina yangu halisi kwenye kitabu cha wageni. Hapo ndipo watakaponipata kirahisi mno.”

“Hilo si kosa hata kidogo,” mzee Kizamba alimsahihisha. “Hukupanga kutenda uhalifu, hivyo, hukuwa na sababu ya kuandika majina ya bandia. Kosa naloliona, ni kitendo cha kukimbia na kuhama kabisa hoteli usiku usiku. Hii inafanya uonekana unahusika.”

“Sikuwa na namna nyingine. Kwa wakati huo, akili yangu ilidhani ni wahalifu walionifuata kwa ajili ya kuiba dhahabu. Nisingeweza kurudi hotelini katika mazingira tatanishi kama yale. Unajua upokumbwa na mshtuko mkubwa kama ule, ukakusababishia mtanziko wa fikra, akili huruka kwa muda. Na zikija kurudi hukuta umekwishafanya maamuzi ya ovyo.”

“Tuachane na hayo. Nani mwingine uliyemwambia kuwa ungelifikia hoteli hiyo?”

“Hata mimi mwenyewe sikujua kuwa nitafikia pale. Dereva teksi niliyemkodi stendi, ndiye aliyenipeleka pale.”

“Huyo ndo wa kuanza naye.”

“Kwa nini?”

“Pafukapo moshi kuwaka moto si ajabu. Naona moshi unafuka chini ya pua za huyo dereva. Hoteli aliyokuchagulia ndiko umekumbana na nakama. Sidhani kama ilitokea kwa bahati mbaya. Ukifanikiwa kumpata unaweza kubaini kadha wa kadhalika. Ukimwona unaweza kumkumbuka?”

“Nusu kwa nusu.”

“Tumia nusu ya kumbukumbu kumtambua. Rudi maeneo ya hapo stendi anakopaki teksi kabla sura yake haijakutoka. Ukimwona usimsemeshe. Ulizia jina lake kwa mtu mwingine. Na ukiweza kupajua mahala anapoishi utakuwa umeua ndege wawili kwa jiwe moja.”

“Sawa.”

“Aidha, kwa sasa usiharakishe kurudi Dar. Bila shaka kutakuwa na msako mkali hivi sasa. Ukisafiri haraka haraka, na ikiwa kuna mtu hata mmoja aliyekukariri, unaweza kukamatwa. Jichimbie sehemu walau hadi keshokutwa. Na uhakikishe unabadili nguo kila itakapokulazimu kutoka.”

“Sawa uncle. Nitakupigia baadaye,” Ikunji alijibu na kukata simu.

***

Miale ya mwanga wa alfajiri ilipenya dirishani na kumkuta Leila kitandani. Siku hiyo hakula wala kulala. Usingizi haukupanda kichwani wala chakula hakikumshuka rohoni. Hofu na mashaka vilimzizima moyoni. Kadri alivyojaribu kumpigia simu Ikunji, hakupatikana. Kutokujua madhila yaliyomsibu mumewe, kulimzidishi maumivu ya moyo. Alibaki kitanda kwa muda mrefu akiwaza na kuwazua.

 Baadaye alishusha miguu sakafuni hali ya kuwa ameketi kitandani. Alipiga mwayo huku akijipikicha macho kwa kutumia sehemu ya nyuma ya viganja vyake. Aliposimama kujinyoosha, ndipo simu yake ikaita. Haraka akainyanyua kumtazama mpigaji. Jina la Ikunji lilimulika kwenye kioo cha simu.

 “Hallow,” alipokea haraka huku akirudi kuketi kitandani. “Umepatwa na nini mume wangu?”

 “Niko salama. Usiwe na wasiwasi. Jana kuna vibaka walikuwa wananiwinda wanikwapue mkoba. Nilifanikiwa kuwatoka.”

 Sauti ya Ikunji ilijaa wasiwasi na haraka. Leila akaling’amua hilo. “Lakini mbona kama bado una wasiwasi?”

“Niko poa mbona. Labda ni uchovu tu.”

“Umeshamalizana na huyo uliyemfuata?”

“Nani? Sudi? Nitamcheki leo.”

“Kwa hiyo unarudi lini?”

“Kama si kesho, basi keshokutwa. Jumatatu.”

“Uwe makini mume wangu. I love you!”

“I love you too baby.”

Leila alishusha pumzi kama aliyetua mzigo mzito. Akajibwaga kitandani. Faraja ya kujua mumewe yu mzima, ilimrejeshea utulivu wa akili. Akainuka akiwa na nguvu mpya. Akatoka sebuleni na kuanza usafi wa nyumba.

***

Mara baada ya kumaliza kuongea na Leila, Ikunji aliigia bafuni kuoga. Alipotoka akavaa nguo zake haraka. Akachomoa chupa ya mafuta kwenye mkoba na kujipaka. Hakukumbuka hata kuchana nywele. Akautundika mkoba wake begani na kutoka hadi mapokezi. Alimkuta mhudumu yule yule aliyempokea usiku.

“Bado nipo kaka,” Ikunji alisema, akimkabidhi mhudumu ufunguo wa chumba. “Nafika madukani mara moja.”

Alikusudia kwenda kununua nguo za kubadili ili kuepuka uwezekano wa kutambulika kirahisi mtaani. Hakuwa mwenyeji hapo mjini, hivyo kila alikokwenda alitumia usafiri na msaada kutoka wa madereva waliombeba.

Kiasi cha takribani dakika tano tangu alipokabidhi funguo kaunta na kuondoka, aliwasili bwana mmoja mfupi, mweusi, mwenye mwili wa wastani. Uso wake mpana haukuonesha dalili ya ndevu kidevuni wala sharafa mashavuni, bali chini ya pua zilijisokota sharubu mithili ya duduwasha. Alivaa shati la mikono mirefu, la rangi ya kaki, alilochomekea kwenye suruali nyeusi. Aliingia kwa kunyenyemea akihofia kumkwaza mfanyausafi aliyekuwa akiendelea kudeki sakafuni. Kwa bahati, viatu vyake vyeusi vilivyokolea kiwi, havikuachia taathira ya uchafu kila alipokanyaga na kunyanyua unyayo sakafuni.

“Karibu tajiri,” mhudumu alimlaki.

“Asante,” alijibu, akichomoa kitambulisho mfukoni na kumwonesha. “Naitwa Lameck Kisigino, afisa wa jeshi la polisi toka Kituo Kikuu.”

“Oh, karibu afande,” mhudumu alijibu baada ya kukitazama kitambulisho. “Naitwa Simon.”

“Umepokea mgeni aitwaye Ikunji Almasi?” Meno yake ya manjano kama mahindi ya Yanga, yalipandiana kinywani mithili ya gome la tangawizi.

Simon alifinya macho kutafakari. Akavuta kitabu cha wageni na kuanza kuperuzi taratibu. “Hapana afande, sijapokea mtu huyo.”

Punde aliingia mtu mwingine. Mrefu, mwembamba, mweupe. Akaenda kusimama jirani na afande Kisigino. Alivalia jinzi ya bluu na sweta jeusi. Kola ya shati jeupe alilovalia kwa ndani ilichomoza kwa juu ya sweta. Kichwani alivaa kapelo ya kijani. Simon aligeuka kumtazama.

“Niko naye,” Kisigino alisema, huku akatoa picha ndogo mfukoni na kumwonesha Simon. “Unamtambua huyu?”

Simon aliitazama picha ile kwa muda. Akainua uso kumtazama Kisigino bila kusema neno. Akarudisha tena macho yake pichani kwa sekunde chache na kusema, “Ndio nimemtambua.”

“Mbona ulisema hujapokea mtu huyu?”

“Hapa amejiandikisha kwa jina la–” Simon alifunua tena kitabu cha wageni. “Kaisi A. Kaisi. Nilimpa chumba namba 397.”

“Yupo?”

“Mmepishana naye si punde tu. Ila, amesema anarudi muda si mrefu.”

Yule aliyeingia akifuatana na afande Kisigino, alisema kwa lafudhi yenye kithembe. “Tumsubiri nje.”

“Akifika mwache aende chumbani, kisha utushitue,” Kisigino alimwambia Simon huku akimkabidhi karatasi yenye namba zake za simu. “Usiseme naye kitu kingine chochote.”

Simon alipokea karatasi yenye namba za simu. Kisigino na mwenziye wakatoka nje wakimwacha Simon akiwatazama kwa nyuma. Simon alitamani kudadisi mengi zaidi lakini alihofia kujiingiza kwenye balaa lisilomhusu.

Kiasi cha dakika kumi na tano baadaye, Ikunji alirejea hotelini. Mkononi alishika mfuko mweusi ukiwa na nguo za kubadili. Japo mapokezi palikuwa na mteja mwingine anahudumiwa, ila Simon alipomwona tu, haraka alitungua ufunguo na kumkabidhi.

Simon alimtazama Ikunji kichinichini akiiendea kona ya kuelekea zinapoanzia ngazi. Alipohakikisha amekwishakunja kona na kupanda ngazi, haraka akabofya namba za afande Kisigino kumtaarifu.

***

Simu ya Leila iliita chumbani wakati akiendelea na usafi wa nyumba. Akaenda chumbani kuiangalia. Hakumjua mpigaji. Namba mpya.

Akapokea, “Nani mwenzangu?”

Sauti nzito ilikohoa upande wa pili wa simu. “Sorry. Seba hapa.”

Leila alishusha pumzi, macho akiyafumba.

“Oh, Seba. Mambo?”

“Si mabaya,” Sebastian alijibu, akitoa mwayo kwa sauti, “Jana hukunipa mrejesho tena. Ilikuwaje?”

“Aah anasema kuna vibaka walitaka kumvamia, ndo alitaka tu kunipa habari. Nadhani atarudi kesho au keshokutwa.”

“Anha! Sawa,” Sebastian alijibu. “Kwa hiyo?”

Kwa hiyo nini? Leila alitamani kujibu kishujaa, lakini kumbukumbu ya tahadhari aliyopewa na mama Mbegu, kuwa tayari Sebastian anayo barua yake mkononi ilimfany ajioinye mwenye. Badala yake akaitika kana kwamba hakumsikia vizuri, “Abee!”

“Unakuja saa ngapi?”

Alikwishaelewa maana ya swali lile. Bado analo deni kwa Sebastian. Anatakiwa kulilipa.

“Ah–hm au nitakuja kesho tu, Seba.”

“Lakini umesema Ikunji anaweza kurudi kesho.”

Leila alitafuta hoja nyingine ya kujinasua kwa haraka bila kumkwaza, hakuipata. Alibaki ameshikilia simu huku akijikuna kichwa kwa mkono wa kushoto. “Ahm, okay s–a–wa.”

“Usichelewe basi,” Sebastian alijibu na kukata simu.

Leila alibaki ameduwaa na simu yake mkononi. Taratibu alianza kuikubali hali ile. Hofu ya kuchepuka na Sebastian ilianza kutoweka taratibu kama giza la alfajiri.

Alipomaliza usafi wa nyumba na mwili. Aliketi mezani kustaftahi. Aliifikiria safari ya Upanga kwa Sebastian. Hakuwa na pesa ya kutosha kupanda teksi, hivyo kila alipofikiria adha za usafiri wa daladala hamu ilimwisha.

***

Afande Kisigino na mwenziye walifika mapokezi kabla Simon hajashusha mkonga wa simu mezani. Simon alimalizia kumhudumia mteja aliyekuwa amesimama mbele yake ili awahi kuwapeleka chumbani kwa Ikunji.

Waswahili husema, sisimizi hajioni kivuli. Ikunji aliendelea kukwea vidato vya ngazi taratibu mithili ya chatu aliyevimbiwa. Hakujua kuwa kuna mtego amewekewa. Alipokata kona ya kwanza, ghorofa ya pili, ghafla alikamatwa mkono na kuvutwa kwa nguvu kuelekea chumba cha kwanza kwenye kona. Alitaka kupambana lakini alipomwona mtu aliyemvuta mkono, hakutoa upinzani. Alimfuata nyuma kama mbwa aliyeona chatu.

Aliingizwa chumba cha kwanza, mkono wa kushoto. Mlango ukafungwa. Akabaki amesimama, akiwajihiana uso kwa macho na mtu aliyemvuta. Ni Nyakanga. Hakuwahi kuwa na ukaribu mkubwa na Nyakanga, kwa heri wala kwa shari, kiasi cha kufanyiana mchezo ule. Hakufanya haraka kuuliza lolote, aliendelea kutweta, akisubiri ajuzwe sababu ya kuchukuliwa hangehange namna ile na kuingizwa mle chumbani.

“Unatafutwa wewe,” Nyakanga alisema. “Ulipoondoka tu, walifika polisi wawili kukuulizia. Na umewapita nje hapo nje wanakusubiri urudi.”

“Mungu wangu! Nimekwisha,” Ikunji alisema akijishika kichwa. “Nani amewaambia niko hapa?”

“Unaniuliza mimi?” Nyakanga alisema kwa kedi. “Inawezekana wametonywa na mtu, au kama wana namba yako ya simu wanaweza kujua ulipo bila kutonywa na mtu.”

Haraka Ikunji aliitoa simu yake mfukoni ili kuizima. Hakuwa na ubishi kwamba ni simu yake ndiyo imemkamatisha. Kabla hajaizima, ujumbe uliingia kwenye simu yake. Akaufungua.

Mkeo ameshindwa kudhibiti nguo yake ya ndani.

Fuatilia, juzi Ijumaa, kuanzia saa moja usiku, alikuwa wapi?

Ndimi rafiki ninayekujali.

Kabla hajajua cha kujibu, Nyakanga akamkaripia, “Zima hiyo simu, acha ujinga.”

Ikunji akabonyeza kwa nguvu kitufe cha kuzimia simu. Si punde baada ya simu kuzima, kwa mbali zikaanza kusikika nyayo za watu zikipanda ngazi. Nyakanga akamnyamazisha kwa kumfanyia ishara ya kidole mdomoni, kisha akachungulia nje ya chumba kupitia tundu la funguo na kuwaona afande Kisigino na mwenziye, pamoja na Simon, wakipanda ngazi. Akarudi nyuma na kumpisha Ikunji achungulie. Simon alikuwa amekwishakatiza, akabahatika kumwona afande Kisigino, akifuatiwa na mwenziye, wakiziendea ngazi zinazokwenda ghorofa ya tatu.

“Umewaona?” Nyakanga alinong’ona.

Ikunji aliafiki kwa kichwa.

Baada ya sauti za nyayo kutoweka, Nyakanga alifungua mlango taratibu. Akachungulia nje kuhakiki usalama, kisha akamgeukia Ikunji. “Haya potea fasta. Ukikamatwa simo.”

“Asante sana,” Ikunji alijibu huku akimtazama Nyakanga machoni. “Sitakusahau, dada.”

Ikunji alitoka chumbani kwa kasi ya mshale. Akateleza kwenye ngazi mfano wa kambale kwenye tope. Aliipita meza ya mapokezi bila kugeuka nyuma kama aliyeshurutishwa na mganga.

Nyakanga alifuata kwa nyuma taratibu, akateremka hadi mapokezi. Alikwenda hadi kwenye sofa tatu za kupumzika wageni, zilizopangwa kwa kuizunguka meza ndogo ya mbao. Akainama mezani na kuanza kupanga vizuri magazeti kana kwamba alikuwepo hapo muda wote. Mara akasikia sauti ya nyayo zikiteremka kwa kasi toka ghorofani.

“Dada,” Simon aliita.

Nyakanga aliacha magazeti. Akageuka na kuitika, “Abee.”

Pembeni ya Simon, alisimama Kisigino pamoja na mwenziye wakiangaza huku na kule.

“Kuna mtu yeyote umemwona akiteremka sasa hivi?” Simon aliuliza.

Nyakanga alifinya macho yake kana anayevuta kumbukumbu. Akasema, “Nadhani ni yule kijana aliyevaa shati la mistarimistari.”

Simon alimgeukia Kisigino, akisema, “Ndiye huyo. Au aliwaoneni nje wakati alipoingia?”

Kisigino alipuuza swali la Simon. Akamgeukia Nyakanga na kumsaili, “Ametokea juu tulikokuwa sisi?”

“Hmh! Sikumtilia manani sana. Nimemwona akiwa ameshafika hapo kaunta akielekea nje.”

“Haiwezekani,” mwenziye Kisigino alijibu, akimgeukia Simon. “Hukumwambia kitu chochote alipofika?”

“Kwanza kanikuta nahudumia mteja mwingine mezani. Nisingeweza kuongea naye chochote zaidi ya kumkabidhi funguo.”

“Sasa tumepishana naye vipi na njia ndo hiyo hiyo?” Kisigino alisaili kwa ghadhabu na jazba.

***

Leila aliwasili nyumbani kwa Sebastian majira ya saa sita mchana. Kama zilivyo kaya nyingi maeneo ya Upanga, kutawaliwa na ukimya na utulivu, vivyo hivyo nyumbani kwa Sebastian. Mlinzi alimruhusu kuingia baada ya kujitambulisha. Aliingia sebuleni na kwenda kuketi sofani; mguu mmoja juu ya mwingine, macho yakituama runingani.

Muda si muda, Sebastian alichomoza koridoni akiwa amejifunga taulo kiunoni. Walipokutanisha macho, wakatabasamu kwa pamoja.

 “Mbona umechelewa baby?” Sebastian aliuliza, akimfuata sofani.

 “Mnh!” Leila aliinua mkono wake kutazama saa. “Mbona ni kama saa moja tu na ushee tangu tuongee.”

 “Aah basi labda nimekuwaza sana,” Sebastian alijibu na kuketi sofani, “ndo maana saa naiona kama mwaka.”

 Mwanzo wa ngoma ni lele. Sebastian alinyanyua mkono wa kulia na kuuzungusha begani kwa Leila. Akamvuta karibu yake na kumbusu chini ya taya. Mwili wake ulikuwa ukinyemanyema maji na kunukia harufu nzuri ya sabuni. Leila alimgeukia Sebastian na kumwekea mkono pajani, huku akimtazama machoni. Kama sumaku, midomo yao ikavutana; na kama mwezi upatwavyo na jua, macho yao yakajifumba.

 “Twende chumbani, baby!” Sebastian alisema.

 Badala ya kujibu, Leila alilaza kichwa chake begani kwa Sebastian. Hakuwa na pingamizi tena. Alikwishasalimu amri. Alichohitaji tu kubembelezwa zaidi. Waswahili husema, asiyejua kurai si mlezi wa mapenzi.

Akiwa anasubiri kubembelezwa zaidi, ndipo macho yake yakapiga runingani. Marudio ya matukio ya juma zima yaliendelea kurushwa katika idhaa ya taifa. Macho yalimtoka pima kufuatia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kuonekana akielezea tukio la mauaji ya mfanyabiashara, Sudi Chotara. Alitambua kuwa safari ya Ikunji jijini Arusha ilikuwa kukutana na Sudi.

 Sudi ameuawa? Leila aliwaza, kwanini Ikunji amenificha taarifa hii?

 “Inuka basi baby,” Sebastian alisema kwa sauti ya chini, huku akisimama.

Macho ya Leila bado yaliganda kwenye runinga. Sebastian akamshika mkono na kumnyanyua sofani.

 “No,” Leila alisema baada ya kusimama, “Seba naitarudi baadaye.”

 Kwanza Sebastian hakuamini anachosikia. Aliganda akimkodolea macho Leila kama aliyekwamwa na mwiba wa samaki kooni. Uso wa Leila ulishasawajika ghafla.

“Shida nini?”

 “Ahm, Seba samahani,” alijibu huku akitafuta uongo wa kujazia. “Nilisahau kitu muhimu. Shangazi yake Ikunji, alisema atakuja nyumbani kwangu kwenye saa sita kuna mzigo ananiletea. Ndo nimekumbuka hivi sasa. Akinikosa anaweza kumpigia Ikunji. Acha nikimalizane naye kisha nitarejea.”

 Leila alisimama wima, akajishika matiti kwa mikono miwili, juu ya sidiria, na kuyapindisha juu. Akajitengeneza wigi vizuri na kuukwapua mkoba wake.

Sebastian alibaki amesimama mbele ya sofa, akimwangalia Leila kwa mshangao. Hakuwa na lugha nyingine ya kumshawishi asiondoke baada ya majibu yake kumaanisha kivitendo.

***OOPS! Kwa mara ya pili, Seba amelala doro. Tukiachana na upuuzi wa Seba, hivi kama wewe ndo Ikunji ungemlipa nini Nyakanga kwa wema ule? Tukiachana na Nyakanga, unadhani Ikunji anawindwa kiharamia au anapelelezwa kihalali? Pamoja na yote hayo, tusisahau kujiuliza, iweje maiti ya Sudi Chotara ikutwe chumbani kwa Ikunji na ilhali pamesemwa kuwa hakuonekana kuingia hotelini humo?



Ikunji alilala chali kitandani, mikono akiizungusha kisogoni. Alifanikiwa kupata chumba katika hoteli ya D&G baada ya kuwachomoka polisi. Jambo moja lilimdhihirikia bayana, kwamba imekwishajulikana kuwa yeye ndiye aliyepanga chumba ilimokutwa maiti ya Sudi Chotara. Makosa makubwa aliyoyakiri moyoni, ni kuandika taarifa zake halisi kwenye kitabu cha wageni hotelini, pamoja na kuendelea kutumia simu yake baada ya tukio lile.

Kuendelea kukimbia na kujificha kungemfanya atafisirike kuwa ni muuaji. Hivyo, alifikiria kujisalimisha polisi. Aliamini akielezea vizuri mkasa mzima angeweza kujinasua na kadhia ile. Lakini kila alipoyafikiria mapokezi ambayo angelipewa na polisi, kama mtuhumiwa wa mauaji, hamu yote ilimwisha. Alijitengezea taswira ya kitu cha kwanza ambacho polisi wangekifanya mara baada ya kumpata. Alijua isingelikuwa mahojiano ya mdomo, bali wangeanza na mchakato wa kumlainisha viungo kwa virungu na nyaya za umeme. Alijua ni lazima angelazimishwa kuutapika ukweli ambao hautambui. Aidha, alijua fika, kukosa kutapika walau chembe ya ukweli ambao polisi walitaraji kuusikia kutoka kwake, pasipo kujali endapo anao ama la, kungefanya viungo vyake vilemazwe badala ya kulainishwa. Hilo hakuwa tayari limfike.

Kwa kuwa alikwishafahamu, kwa namna yoyote ile, yeye ndiye mtuhumiwa namba moja, hivyo, ili kujinasua ilimbidi ahakikishe anakusanya kwanza walau dondoo chache kuhusu tukio hilo la mauaji, kabla ya kujikabidhi mikononi mwa pilisi.

Ni nani aliyemuua Sudi? Amemuua kwa maslahi gani? Kwa nini amuulie chumbani kwangu? Mtungo wa maswali ulizidi kujirefusha kichwani mwake.

Alisimama akijipigapiga kichwani. Alijaribu kila mbinu kuchangamsha kichwa ili kuchakata maswali yote. Mawazo yaliutafuna vilivyo ubongo wake, kiasi cha kupoteza mustawa wa utendaji kazi. Hakuna hata jibu moja lililompeleka kwenye ukweli. Kwa mara ya kwanza alihisi huenda kichwani mwake amebeba makamasi badala ya ubongo.

Je, inawezekana ilitokea tu kama sadfa? Kwamba wauaji hawakujua kuwa chumba walichokwenda kumwua Sudi Chotara, kilikuwa kimechukuliwa na mgeni wake? Kama sivyo, basi walipanga kuniangushia jumba bovu. Lakini je, walijuaje kuwa nitafikia chumba hicho? Ikunji alijiuliza.

Ikunji ni mpenzi mkubwa wa muziki, hususani wenye mdundo mzito kama hiphop. Lakini muziki aliopambana nao safari hii, mdundo wake ulitishia kumchana kifua.

Alitamani kumpigia simu mzee Kizamba kumjulisha kilichojiri baada ya kufanikiwa kuwakimbia polisi, lakini alihofia kutumia simu yake kwa kujua kwamba polisi wangejua mahala alipo kupitia simu hiyo. Hofu ya kuwasha simu, ikamkumbusha ujumbe aliotumiwa na namba mpya kmhusu mkewe. Aliielewa vema falsafa ile, kwamba mkewe ameshindwa kudhibiti nguo yake ya ndani. Maumivu ya kusalitiwa yaliubabua moyo wake mara dufu.

Je, nianze kumpigia Leila au nimtafute kwanza aliyenitumia huo ujumbe? alijiuliza.

Ukiwasha tu simu umejikamatisha! Indhari ilimpitikia kichwani mwake.

***

Sajini Kinabo alitembea taratibu kulielekea geti la hoteli ya White Rose, huku akiyasawiri mazingira yote kwa umakini mkubwa. Shughuli mbalimbali ziliendelea nje ya hoteli ingawaje hapakuwa na mtu aliyeonekana kutoka wala kuingia hotelini. Lakini mlango wa hoteli ulikuwa wazi. Kinabo akaingia.

 “Hakuna huduma kaka,” msichana aliyekuwa ameketi kwenye kochi alisema.

 Kinabo alipiga kite, akisema kwa mshangao, “Hivi duniani bado kuna wahudumu wa aina yako?”

 Haraka msichana yule alishusha miguu sakafuni na kujitengeneza, akionesha kuhofishwa na kauli ile ambayo haukuelewa maana yake.

“Kwa nini?”

 “Si wa karibu wala salamu.” Kinabo alijibu.

 “Oh, nisamehe bure kaka yangu. Kichwa changu hakipo sawa kabisa leo.”

 “Haya pole,” Kinabo alisema huku akiketi sofani, karibu na msichana yule. “Mi naitwa James. Nawe wanakuitaje?”

 “Naitwa Maisara.”

 “Oh, jina zuri sana japo mwenye jina ni mzuri zaidi ya jina lake.”

 Maisara akashindwa kulizuia tabasamu lake.

Kinabo naye akatabasamu. “Sema hata ahsante basi, mrembo.”

 “Haya asante.”

Kinabo aliyasanifu mazingira kwa haraka, lakini hakubaini kitu. Licha ya rabsha iliyotokea hotelini hapo, bado mazingira yalionekana nadhifu muda wote. Hapakuwa na dalili ya mtu mwingine mle ndani zaidi ya msichana huyo.

 “HiI ndo hoteli yangu kila nifikapo Arusha, lakini sijawahi kukuona hata mara moja. Ni mfanyakazi mpya?”

“Hapana. Nina muda mrefu tu mbona.”

“Anha, basi yumkini tunapishana,” alijibu kwa bashasha kana kwamba wameshafunga urafiki, “Haya Mmari yuko wapi?”

 “Mnafahamiana?”

“Ndo maana nikamuulizia.”

“Hayupo. Amechukuliwa na polisi tangu jana usiku.”

“Na polisi? Kunani tena?”

“Jana palitokea tukio la mauaji hapa.”

 “My God! Wateja walifumaniana, au?”

 Maisara alifunguka mkasa wote kama ambavyo naye alisimuliwa baada ya kuingia zamu hotelini asubuhi hiyo.

 “Sasa kama aliyeuawa hakuonekana kuingia hotelini, iweje maiti yake ikutwe ndani?” Kinabo alichagua kudadisi eneo hilo, baada ya Maisara kuhitimisha simulizi.

 “Ya kuacha tu mwenzangu,” alijibu huku akizungusha macho na kubetua mdomo. “Mmari akiamua kuingiza mtu utajua? Hao wanawake zake tu analala nao humu na hakuna anayejua wanakopitia.”

 “Mmari naye aache ukware sasa, umri unasonga,” Kinabo alisema huku akicheka kwa sauti. “Sasa kama huwa hawapitishii mlango huu, huwa anawaingiza kwa ungo?”

 Maisara akacheka akijibu, “Ndo maana nikakwambia ya kuacha tu.”

 “Aisee poleni sana,” Kinabo alisema na kusimama. “Basi acha nikatafute chumba sehemu nyingine.”

“Haya. Karibu tena siku nyingine.”

Kinabo alitoa pochi katika mfuko wa nyuma, akafungua na kutoa noti mbili za shilingi elfu kumi kumi. Akampatia Maisara. “Haya utakunywa soda basi.”

Soda ya elfu ishirini? Maisara alijiuliza huku akishangaa. Lakini hakuzikataa.

“Ubarikiwe sana.”

“Kama hautojali, jioni nitarudi kukutembelea. Au hata kesho panapo majaaliwa,” Kinabo alisema huku akirejesha pochi mfukoni.

 “Karibu,” Maisara alijibu huku akizitia mfukoni pesa zake. “Japo sijui kama utatukuta. Mwenye hoteli anaingia leo jioni toka Dar, huenda tukafunga kwa muda.”

 “Oops! Kwa hiyo sitakuona tena?”

 Maisara akatabasamu akisema, “Jamani simu si zipo.”

 Ndicho nilichokuwa nasubiri, Kinabo aliwaza. Akatoa simu huku akimuuliza, “Unatumia mtandao gani?”

 Akautaja. Kisha akataja na namba yake ya simu.

Kinabo alitoka hotelini huku akimalizia kuhifadhi namba simuni. Moja kwa moja akaenda kusimama upande wa pili wa barabara, mkabala na hoteli hiyo akiangaza huku na kule kutafuta usafiri.

“Unahitaji bodaboda, bosi?” Sauti ya kijana aliyetokea pembezoni mwa kichochoro ilimzindua Kinabo.

“Ndio, lakini sioni bodaboda hata moja hapa.”

“Njoo huku bosi. Bodaboda haziwezi kupaki hapo leo.”

Kinabo alimfuata hadi mbele kidogo. Kijana aliichomoa pikipiki yake uchochoroni na kuiwasha.

“Mbona unaificha mbali huku? Au hauna vibali mzee?” Kinabo alifanya kutania baada ya kupanda.

“Si bora ingekuwa vibali tu,” kijana alijibu, akivaa kofia. “Tunaelekea wapi bosi?”

“Sanawari Petrol Station, karibu na Kituo cha Polisi.”

Dereva akakitia moto chombo, safari ikanza.

“Kuna mtu ameuawa mle hotelini – White Rose. Sasa kama ujuavyo tena kamatakamata ya polisi, ndo maana tunafanya kazi kiujanja ujanja.”

“Nilisikia kuna mtu ameuawa ila sikujua kama ni hoteli hiyo. Ilikuwaje?”

“Aah hata najua basi! Mi nilikuwa nimepaki kijiweni kama kawaida, akatokea abiria mmoja anataka kupelekwa sehemu yenye hoteli nzuri, nikampeleka Sanawari.”

Kwa nini umpeleke mbali ilhali hapo karibu kuna hoteli? Kinabo alitamani kumtupia swali hilo, badala yake akasema. “Duh bodaboda mnawaza pesa tu! Yaani hapo jirani kuna hoteli lakini ukaona umpeleke mbali ili upate pesa.”

“Hapana. Mi siko hivyo. Nilimwonesha White Rose Hotel, akakataa, ndo nikampeleka Nyati Inn, Sanawari. Niliporudi sasa ndo nikakuta umati umefurika.”

Kwanini akatae hoteli iliyo karibu? Kinabo aliishia kugunia tumboni. Ilikuwa ni kama bahati ya mtende kuota jangwani au mbuzi kufia kwa muuza supu.

“Aisee, binaadamu tumekuwa kama wanyama,” Kinabo alijaribu kubadili mada. “Basi ukute alifumaniwa na mke wa mtu.”

“Sudi mtu muungwana, hawezi kufanya uchafu huo.”

“Hakuna muungwana kwenye mapenzi. Kila mtu ana udhaifu wake.”

“Na hata kama angeamua kufanya hivyo, kwa utajiri alionao, asingeweza kupeleka mwanamke kwenye hoteli ya hadhi ya chini kama ile.”

Mazungumzo yao yalishamiri hadi walipofika mwisho wa safari. Kinabo alimtaka asimame pembeni mwa Kituo cha Polisi. Akatii. Alipoegesha tu, Kitabo aliteremka na kwenda kusimama mbele.

“Hivi nikihitaji baadaye uniijie tena utaweza?”

“Ndo kazi yangu bosi.”

“Poa.” Kinabo alitoa pesa mfukono na kulipa nauli yake. “Basi nipe namba yako ya simu. Nikiwa tayari nitakupigia.”

Dereva bodaboda alipokea nauli huku akitaja namba zake za simu. “Jina andika Isaka.”

Baada ya Isaka kuondoka. Sajini Kinabo aliita bodaboda nyingine impeleke Nyati Inn Hotel. Alikwishamtilia shaka huyo kijana aliyegoma kuchukua chumba White Rose, na kutaka apelekwe Nyati Inn.

***

Ikunji alisimama mbele ya meza ya mapokezi akiwa amekwishabadili mavazi. Alivalia suruali ya kadeti na sweta la kijivu juu ya fulana nyeusi. Kichwani alivaa kapelo nyeusi yenye nembo  nyeupe. Akakabidhi funguo kaunta na kutoka.

Alidhamiria kujaribu kufanya uchunguzi wa kifo cha Sudi. Kwa kuwa alitaka kucheza gizani, ilimpasa aanze kwanza kujifunza kufumba macho. Katika nukta ndogondogo zilizokuwapo mbele yake, aliamua kuanzia kulekule Nyati Inn Hotel. Ingawaje uwezekano wa kukamatwa ulikuwa mkubwa mno, lakini ili kushinda vita inayomkabili ilimbidi kuhatarisha usalama wake. Akachukua bodaboda nje ya hoteli na kuondoka. Kiasi cha dakika kumi, alikwishawasili maeneo ya Nyati Inn Hotel.

Badala ya kwenda kuingia hotelini, alikwenda kwenye duka kubwa la rejareja mkabala na hoteli. Akanunua sigara na kuiwasha papo hapo. Alipamaliza, akasogea pembezoni mwa duka na kusimama. Macho yalitazama mlango wa kuingilia hotelini wakati akipuliza angani moshi mweupe. Kuyaona tena mazingira ya hoteli ile, kukamrejeshea tena kumbukumbu za namna alivyonusurika kunaswa na polisi. Macho yakiwa bado yameganda hotelini, aliiona teksi nyeupe ikiwasili na kwenda kuegesha mbele ya hoteli. Kwa dakika tano, hakuna aliyeshuka.

Ni mapolisi? alijiuliza. Chambilecho wahenga, mguu ulioumwa na nyoka ugusapo jani hushituka. Alikwishanusurika kukamatwa na polisi, hivyo, kitu chochote chenye walakini kilimfanya azidishe umakini. Alitamani kuondoka kabla hajatimiza kilichompeleka. Kabla hajakata shauri kuondoka, akamwona Nyakanga akitoka hotelini na kuifuata teksi iliposimama.

Kinabo aliwasili eneo hilo wakati macho ya Ikunji yakiendelea kumakinika na Nyakanga. Kama ilivyokuwa kwa Ikunji, Kinabo naye hakufanya papara kwenda kuingia hotelini. Alisimama nje akiyasawiri mazingira. Kisha naye akelekea dukani, alikokuwa amesimama Ikunji. Ndilo eneo pekee palipokuwa na urahisi wa kusimama pasi na kuvutia nadhari za watu.

Ikunji alichomoa sigara mdomoni. Akautawanya moshi angani. Bado macho yake yaliganda kwenye teksi. Hakuweza kumwona mtu aliyekuwa akiongea na Nyakanga kwa sababu aliketi upande wa pili. Alipojaribu kumkazia macho dereva, akahisi kumtambua.

Nilimwona wapi? aliwaza. Kumbukumbu zilimgomea, lakini sura ilimjia.

Baada ya sekunde kadhaa za kuvuta kumbukumbu, hatimaye akamkumbuka. Alihisi vinyweleo vikitutumka juu ya ngozi yake. Kabla hajajua cha kufanya alihisi kuguswa begani. Machale yakamcheza. Alipogeuka, akakutanisha macho na Kinabo. Aliganda akimtazama bila kusema neno.

Kinabo alikuwa ametoa pakiti ya sigara kwenye mfuko wa shati. Akachomoa sigara moja na kuipachika mdomoni, kisha akapiga kidole gumba na cha kati, akiashiria kuomba sigara ya Ikunji ili awashie yake. Ikunji alitii mara moja.

“Mambo vipi?” Kinabo alimsalimu huku akipokea sigara.

“Poa poa.”

Baada ya kuwasha, alimrejeshea sigara na kumuuliza, “Ni mwenyeji mitaa hii?”

Ikunji alipokea sigara na kujibu, “Hapana.”

Wakati anamrejeshea sigara yake, Kinabo aligundua mikono ya Ikunji inatetemeka. Akamkazia macho usoni. Ikunji akakwepesha na kugeuka upande wa pili. 

Teksi iliyosimama nje ya hoteli ilianza kuondoka taratibu. Akaonekana Nyakanga akirejea hotelini. Ikunji hakufanya ajizi. Haraka akaondoka dukani. Kinabo aliendelea kumtazama akielekea barabarani. Alishindwa kuelewa endapo alikuwa akitetemeka kwa hofu ya uhalifu au ni maradhi. Kinabo hakumtambua Ikunji, kwamba ndiye sababu ya yeye kuwapo pale. 

 Ikunji alisimamisha bodaboda iliyokuwa akipita barabarani na kupanda. “Tunaifuata teksi ile.”

“Inakwenda wapi?” dereva aliuliza huku akiingiza gia na kuondoa pikipiki.

“Popote inapokwenda.”

Njia nzima, Ikunji alihakikisha teksi haiwapotei machoni. Kauli ya mzee Kizamba kuwa, ni muhimu kumpata dereva aliyembeba siku alipowasili Arusha, ilirindima kichwani mwake. Alipanga kitokeo cha hapo White Rose, ndipo aelekee stendi kumsaka dereva huyo, lakini kwa bahati akamwona ndani ya teksi hiyo iliyomfuata Nyakanga hotelini.

Takribani dakika ishirini, teksi ilisimama nje ya nyumba moja ya matofari ya kuchoma. Maeneo ya Daraja Mbili. Ikunji na bodaboda wake, nao walisimama hatua kadhaa nyuma, mbali kidogo na teksi hiyo. Ikunji alichomoa kalamu na karatasi kwenye mkoba akanakili namba ya teksi kwenye sahani ya njano; tofauti na kanuni ya teksi kuwa na sahani nyeupe za namba. 

Haikuchukua muda, abiria aliyekuwa ameketi pembezoni mwa dereva, aliyekuwa akiongea na Nyakanga kule hotelini, alisuasua kuteremka toka kwenye teksi kwa sababu ya unene. Alipoteremka, akabaki amesimama huku ameegemea mlango wa teksi. Alionekana kuzungumza mambo kadhaa kwa msisitizo, akiirusha mikono yake huku na kule. Pamoja na kwamba masikio ya Ikunji yasingaliweza kunasa chochote kwa umbali ule, walakini macho yake yalivuta vizuri taswira ya mtu yule. Alihisi kuwahi kumwona mahali. Alipotuliza zaidi macho akamtambua. Ni yule bonge aliyekuwa akimjibu kwa dharau na kedi, nje ya hoteli ya White Rose, kwenye mgahawa wa chakula.

Kengele ya hatari ilianza tena kurindima kichwani mwake.

Kitendo cha kumwona dereva wa teksi, aliyembeba stendi siku alipowasili na kumpeleka kwenye hoteli iliyomletea, akiwa ameambatana na mhudumu wa mgahawa wa hoteli ile ile, kulimzidishia tashwishi ya kudadisi mualaka baina yao. Alitamani kuwachunguza zaidi, lakini alielemewa na wasiwasi kiasi cha kupoteza mhimili wa kujiamini. Mgogoro mkubwa baina ya dhamira na hisia uliibuka moyoni mwake. Hakujua kipi sahihi kati ya kurudi nyuma na kuondoka au kusonga mbele na kuchunguza mengi zaidi. Alihofia kuufungua mlango asiojua namna ya kuufunga.

***

Baada ya kumaliza kuvuta sigara, Kinabo alivuka barabara na kwenda kuingia hotelini. Simon, aliyekuwa ameketi akitazama runinga alimlaki kama ilivyo desturi kwa wateja wengine.

Baada ya kusabahiana, Kinabo alimwonesha kitambulisho chake, akisema, “Naitwa Kinabo. Sajenti James Kinabo. Natokea Kituo Kikuu cha Polisi. Nahitaji kuangalia orodha ya wageni waliochukua vyumba juzi usiku hotelini kwako.”

 Kumbukumbu za Simon zilirudi kwa afande Kisigino. Tayari alikwishamaizi kuwa uwepo wa Kinabo hotelini hapo, ni mwendelezo wa upelelezi wa tukio lile lile. Alivuta kitabu cha wageni kabla ya kuhoji zaidi. Akafunua ukurasa wa siku husika na kumkabidhi Kinabo.

Kati ya wateja watano waliochukua vyumba usiku, Kinabo alivutiwa na mmojawapo. “Naweza kumwona huyu Kaisi?”

“Hayupo,” Simon alijibu, akilaza mikono yake mezani. “Lakini pia haitwi Kaisi.”

Sajini Kinabo alifunika daftari na kumtazama Simon usoni. “Unamaanisha nini?”

Simon alianza kusimulia mkasa ulioibuka baada ya afande Kisigino kufika hotelini hapo, kumtafuta mtu ambaye ilikuja kugundulika kuwa ameghushi jina. Kinabo alipigwa butwaa, akijiuliza endapo mtu huyo anaweza kuwa ndiye mhusika wa mauaji ya Sudi.

“Unalikumbuka jina halisi la huyo kijana – ulilotajiwa na afande Kisigino?”

 Kabla Simon hajajibu, Nyakanga alifika kaunta akijitupia mtandio kichwani. Akasimama pembezoni mwa Kinabo. “Nafika sokoni mara moja.”

 “Sawa dada,” Simon alijibu, kisha akarudisha macho kwa Kinabo na kujibu, “Hapana. Sikulikariri.”

 “Unaweza kunielezea mwonekano wake?”

 “Ni mrefu, mweupe kiasi, nyusi zake ni nyeusi sana, na ndevu nyingi mashavuni. Pia, ana kitu kama kidoti cheusi karibu ya pua.”

 Kinabo alihisi damu ikimsisimka. Sifa zote alizotajiwa zilimranda mtu aliyekuwa amesimama naye mbele ya duka, mkabala na hoteli hiyo, muda mfupi kabla hajaingia hotelini humo. Alikumbuka alivyomkaribia na kumgusa begani. Walivyotazamana. Na namna alivyoondoka ghafla. Suala la kwanini kijana yule alikuwa akitetemeka mikono, lilipata jibu kichwani mwake.

***

Ikunji alirudi tena na bodaboda maeneo yale yale, mbele ya duka la rejareja, mkabala na Nyati Inn Hotel. Safari hii hakutaka kusimama dukani, aliamua kwenda kuingia moja kwa moja hotelini. Hakujua kuwa mtu aliyemwazima sigara, ambaye ni ofisa wa jeshi la polisi, alikuwamo ndani ya hoteli akipeleleza kesi inayomhusu yeye. Alivuka barabara kwa uangalifu, moja kwa moja akielekea hotelini.

Kiu yake kubwa hapo mwanzo, ilikuwa ni kukutana na Nyakanga ili kumdodosa hali ilivyokuwa baada ya kufanikiwa kuwachomoka polisi. Sasa, kitendo cha kumwona Nyakanga akiongea na yule bonge, mhudumu wa mgahawa wa White Rose Hotel, tena akiwa amebebwa na dereva teksi aliyepanga kumtafuta, kilimzidishia shauku na sababu ya kuonana naye.

Kama mbwa aliyenusa mtara wa windo, alipoinua macho alimwona Nyakanga akitoka hotelini kwa madaha, akijitupia huku na kule mithili ya Nguruwe aliyekanyaga kaa la moto. Akiwa amekwishafika katikati ya barabara, Ikunji alipunguza mwendo asijuwe endapo amuwahi papo hapo nje ya hoteli, au asubiri kuona uelekeo wake kisha amfuate kabla hajafika mbali. Hakufanya papara ya kumwita wala haraka ya kumfikia. Alimwacha afike mbali kidogo ndipo akaanza kumfuata kwa nyuma.

Alipomkaribia akamwita, “Dada!”

Nyakanga aligeuka na kukutanisha macho na Ikunji. Alimkumbuka mara moja. Akabutwaika kumwona tena maeneo yale.

“Wewe! Umefata nini tena?”

“Nimekufuata wewe, dada,” Ikunji alijibu, akiangaza huku na kule. “Nimekuja kukushukuru.”

Nyakanga alimshika mkono na kumvutia pembeni ya barabara. Wakaenda kusimama kwenye uchochoro wa nyumba iliyokuwa karibu na kona ya barabara.

“Haya vipi mwenzangu?”

“Dada nakushukuru sana. Una moyo wa ajabu mno,” Ikunji alisema, akimtazama Nyakanga kwa jicho la huruma. “Nilijiapiza ni lazima nirudi kukushukuru. Nimefika muda mrefu hotelini kwenu, tangu wakati ule ulipotoka kuongea na mtu kwenye teksi, nikashindwa kukusemesha.”

“Aah muda ule nilitoka kuongea na Mufuruki, shemeji yako yule ila tumegombana, basi kila mara anajipitisha kuomba msamaha.” Nyakanga alianza kufungulia maneno kama ilivyo desturi yake. “Lakini usimwone bonge vile – bahili kama nini.”

“Sikumwona. Nilikuwa nimesimama upande ule wa dukani,” Ikunji alijibu, akionesha kwa mkono mwelekeo wa alikokuwa amesimama. “Nilimwona tu yule dereva teksi mwenye mzuzu.”

“Aah, ni Kibwana,” Nyakanga alijibu na kucheka, “Siyo dereva teksi yule.”

“Kumbe nani?”

Nyakanga alipigika kimya kama anayetafuta cha kujibu. “Aah wajanja wa mjini tu. Hebu kwanza niambie, una kesi gani?”

“Hata ni kesi basi, dada,” Ikunji alijibu, akiuzungusha mkoba wake kifuani. Akafungua zipu ya kati kumwonesha kilichomo.

Macho yalimtoka Nyakanga baada ya kukutana na dhahabu kwenye mkoba.

“Kumbe unafanya biashara ya madini? Uko vizuri mdogo wangu. Kwa hiyo wanakutaka nini? Kukudhulumu au? Mapolisi wa siku hizi njaa tupu – basi mwanzo nilidhani ni hii kamatakamata ya sakata la Sudi Chotara.”

“Hivi kwani hiyo issue ya Sudi nayo inaendeleaje?”

“Nasikia waliomuua, walitaka kumwangushia jumba bovu kijana aliyekodi chumba pale hotelini, lakini akawahi kukimbia.”

“Ina maana aliyekodi chumba siye muuaji?”

“Aah, mtu hawezi kuchukua chumba, akaandika majina yake halisi, kisha akaua humo humo chumbani na kukimbia,” Nyakanga alijibu.

“Huo kweli utata. Lakini kama ni kweli ameua, Polisi hawatamwacha kirahisi. Watamwandama kila kona hadi watampata.”

“Polisi hawawezi kumpata. Nasikia waliocheza hiyo dili waliwahi kuficha Kitabu cha Wageni kabla polisi hawajafika.”

“Kwa nini wakifiche sasa?” Ikunji alitupa tena ndoano.

“Nadhani wanahofia endapo polisi wangekipata hicho kitabu, wangemsaka hadi kumpata. Na endapo akihojiwa, ukweli utabainika kuwa si yeye aliyeua. Hapo wanajua itapelekea msako mkali dhidi ya wauaji halisi. Na kama hao wahusika wakiwahi kumpata mapema huyo kijana, watauua kupoteza ushahidi. Baadaye utashangaa kusikia ni wafuasi wa Sudi ndio wamelipa kisasi.”

Ikunji alihisi maini yakimtetemeka tumboni. Akasema, “Mmh! Kama muvi vile. Lakini dada, stori za mitaani si za kuamini sana. Si ajabu huyo huyo aliyepanga chumba, baada ya kumuua Sudi alitoka chumbani na kukibeba kitabu cha wageni na kutoweka nacho.”

“Kama alikuwa na mpango wa kumuua, kwanini sasa aliandika majina yake halisi halafu baadaye ajitaabishe tena kukiiba kitabu?”

Ikunji alitafakari hoja hiyo na kuibirua tena, “Yumkini hakupanga kuua, pengine ilitokea tu baada ya kuona pesa tamaa ikamjaa. Au pengine walitaka kudhulumiana mali ndipo kijana akamwahi tajiri.”

  “Kama hivyo ndivyo, alipotoka chumbani baada ya kuua, na kwenda kaunta kubeba kitabu cha wageni, muda huo mhudumu wa mapokezi alikuwa anacheza mahepe?” Nyakanga alibetua mdomo upande kwa dhihaka. “Sasa kwa taarifa yako, watu wanajua mpaka kilipo hicho kitabu.”

Ikunji alihisi mwili umekufa ganzi. Akageuka huku na kule kuhakiki usalama. “Kwani dada hatuwezipata sehemu nzuri ya chakula, tupige stori?”

“Mmh, kwa leo sidhani. Hapa nimetoroka tu kidogo kazini, nakwenda sokoni fasta kuhemea chakula cha usiku. Leo nitaenda kulala kwa shemeji yako.”

“Sasa itakuwaje? Nilitaka baada ya stori mbili tatu nikupe na asante yako.”

Kusikia kwenda kupewa asante yake, Nyakanga akabadili maamuzi. “Mmh…inawezekana, lakini sijui kama Simon atakubali nitoke mapema. Ila nitaongea naye. Tunaweza kukutana pale King Garden? Wana vyakula pale si vya nchi hii; kuku wa kienyeji, sekela, mturo kwa ndizi, makange na k–”

“Okay,” Ikunji alimkatisha, “saa ngapi?”

“Saa moja kamili jioni,” alijibu na kutoa simu yake mfukoni. “Nipe namba yako nikifika nikupigie.”

“Namba si ndo ile wanaifuatilia. Niliitoa kwenye simu, na sijasili nyingine. Vitambulisho vyangu viko Dar.”

“Sasa itakuaje?”

“We huna kitambulisho unisajilie kwa muda tu?”

“Mmh, inaweza kuniletea matatizo endapo itatumika kufanya uhalifu.”

“Ndo maana nimesema kwa muda tu. Nitakaporejea Dar nitakukabidhi namba yako. Au unaweza hata kuirenew.”

Baada ya ushawishi wa Ikunji, Nyakanga hakuona sababu ya kupoteza miadi na mtu anayehitaji kwenda kumpa bahshishi, kisa namba ya simu tu.

***

Kinabo aliondoka kaunta na kwenda kusimama nje ya mlango wa hoteli. Akatupa macho upande wa pili wa barabara, kule dukani alikokutana na Ikunji. Hapakuonekana na mtu yeyote aliyesimama. Akawa anatazama eneo walilokuwa wamesimama, akakumbuka namna Ikunji alivyokuwa amemakinika na teksi iliyokuwa imeegesha mbele ya hoteli. Ikawa kama anamwona tena namna alivyowahi kupanda bodaboda baada ya ile teksi kuondoka. Japo hakuwa amemjua jina, lakini alikiri kuwa ndiye mtuhumiwa anayemsaka. Akarudi kaunta.

 “Je, afande Kisigino alikwambia ni kwa nini anataka kumkamata?”

 “Hakuniambia,” Simon alijibu.

“Na huyu dada mnene aliyetoka hapa ni nani?

 “Nyakanga?” Simon aliuliza, kabla hajajibiwa akaendelea, “ni mhudumu wetu wa usafi.”

 “Kuna muda alitoka nje kuongea na bwana mmoja kwenye teksi, ni nani yule?”

 “Aah yule bonge? Anaitwa Mufuruki.”

“Anatokea wapi?”

“Ana mgahawa wa chakula pale White Rose, Soweto.”

 Taa nyekundu ilianza kumulika kichwani mwa Kinabo. White Rose ndiko yalikotokea mauaji ya Sudi Chotara. Kitendo cha kumwona mmiliki wa mgahawa uliopo eneo la tukio, akiwasiliana kwa karibu na mhudumu wa usafi katika hoteli ambayo yawezekana ndiko mtuhumiwa alilala, kilimsisimua akili na kumchachafya ubongo. Taharuki ilimjaa kiasi kwamba alihisi chafya inataka kumtokea masikioni.

 “Ni nani yake?” Kinabo aliuliza.

 “Ni bwana’ake. Ila nasikia wametengana, sina hakika sana.”

 “Kipindi afande Kisigino alipowasili, huyo dada alikuwa wapi?”

 Simon alifumba macho na kuinua kichwa juu akitafakari. Alipofumbua akasema, “Nakumbuka kama alikuwa akideki hapo mbele.”

 “Na wakati huyo kijana aliporudi hotelini, Nyakanga alikuwa wapi?”

 “Sikumbuki vizuri. Ila baada ya kuwa tumemkosa chumbani, tuliporudi hapa tulimkuta akipanga magazeti hapo mezani.”

 Kinabo alishusha pumzi. Akabaki akimtazama Simon ilhali mawazo yake yakisafiri kumfuata Nyakanga.

 “Amesema anakwenda wapi?”

 “Nani – Nyakanga? Nadhani sokoni.”

 Kinabo alitoka bila kuaga. Akafuata njia aliyoelekea Nyakanga.

*****ENHEE MAMBO YANANOGA SASA. Kinabo amemshamhisi Nyakanga kumnusuru Ikunji. Je, atafanikiwa kumpata? Na atampata akiwa peke yake au atamfuma akiwa na Ikunji? Ni yepi mahusiano ya Mufuruki (tumbotumbo) na dereva teksi aliyembeba Ikunji? Kuna siri gani hapa katikati?




Jumatatu asubuhi, kama ilivyo desturi, Leila aliingia ofisini mapema. Kwa kuwa hakuwasiliana chochote na Sebastian tangu alipoondoka ghafla nyumbani kwake, alidhamiria kumkwepa kwa kuwahi mapema kuingia ofisini na kumwandalia kila kitu mezani kabla hajawasili. Akiwa anakaribia kuufikia mlango wa ofisi, alisikia akiitwa. Alipogeuka, akakutanisha macho na Daud Mzawa, akitokea ofisini mwake.

 “Mambo vipi, Daud,” Leila alimsalimu baada ya kumsogelea.

 “Poa kabisa,” alijibu huku akisimama kwa kujiegemza mlangoni. “Mmh, Leila umependeza.”

 Leila alitabasamu. “Ahsante.”

 Daud Mzawa ni kijana mpole, mtanashati na mwenye mvuto. Mwonekano wake wa nje unashabihiana na ubora wake wa ndani. Kama alivyo mng’avu mwilini, ndivyo alivyo mweupe rohoni; kama alivyo jamali wa sura, ndivyo alivyo mkarimu wa moyo. Haikuwahi kutokea kwa yeyote, akakutana naye kisha akaondoka akiwa ameharibikiwa siku. Isipokuwa siku hii kwa Leila haikumwacha salama.

 “Okay, kuna barua yako hapo kwa secretary wa mama Mbegu. Leo Seba amefika mapema sana, akaacha barua yako na kuondoka.”

 Tabasamu la Leila liliyeyuka ghafla. Akabaki amemkodolea macho Mzawa. “Okay, shukrani.”

 Daud aligeuza na kuelekea nje, wakati Leila akielekea kwenye dawati la katibu muhtasi wa mama Mbegu. Alikabidhiwa barua yake. Akapokea na kwenda nayo moja kwa moja maliwatoni.

Kabla hajamaliza kuisoma, alihisi macho yakipoteza nuru. Giza likatanda mbele yake na mwili ukaanza kuishiwa nguvu. Dalili zote za kupoteza fahamu zilianza kumshambulia. Akawahi kuegemea ukutani. Haikufaa kitu. Alianza kuteleza taratibu na ukuta hadi chini. Akajikujikuta ameketi sakafuni hali mikono ameitenga magotini.

 Kama alivyotegemea, ilikuwa ni barua ya kusimamishwa kazi, kwa kukaidi safari aliyopaswa kwenda pamoja na Sebastian. Barua haikuwa na maelezo mengi zaidi ya kutakiwa kukaa nyumbani hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.

 Alijaribu kujikaza. Hakutaka kulia. Lakini macho yalimsaliti. Yakaanza kububujisha machozi. Uso ukamtota chapa. Uzalendo ukamshinda. Akaanza kulia kwa sauti. Alikwishatambua kuwa, alichomkwaza Sebastian hadi kufikia maamuzi yale ni kitendo cha kuondoka ghafla nyumbani kwake. Na sasa ni dhahiri ameamua kumkomesha.

Kusimamishwa kazi kusingelikuwa tatizo kubwa kwake, endapo Ikunji angelikuwa na uwezo wa kumudu gharama za maisha. Walakini, ujira wa Ikunji kwenye kibarua chake kipya alichopata bado ulikuwa mdogo sana. Hivyo, kuondolewa kazini katika kipindi ambacho, majukumu ya msingi ndani ya familia yalitegemea mshahara wake, lilikuwa ni pigo mujarabu kwake. Mbaya zaidi, hakuwa na akiba ya pesa kumwezesha kujipanga japo kwa mwezi mmoja mbele, kipindi awapo nyumbani.

Aliinuka na kwenda kwenye karo. Akanawa uso wake. Alipomaliza akaweka barua yake mkobani. Akatoka msalani na kuondoka ofisini. Akiwa amesimama usawa wa maegesho ya magari, mbele ya jengo la ofisi yao akitafakari njia ya kufuata, gari ndogo aina ya Toyota Mark X lilisogea taratibu hadi usawa wake. Akiwa anarudi nyuma kuikwepa, vioo vya gari vikashushwa.

“Leila!” Alikuwa ni Daud Mzawa. “Ingia nikusogeze mbele.”

 Leila alifungua mlango na kuingia. Akafunga mkanda bila kumtazama Daud. Kila alivyojaribu kudhibiti maumivu moyoni ndivyo yalivyodhihirika usoni. Alihisi dunia nzima ikimtazama na kumdhihaki. Alihisi machozi yakitaka kuumbuka machoni mwake. Akajidhibiti. Hakutaka kuonesha udhaifu. Alihakikisha anaficha maumivu yake. Bado hakuwa amefanya maamuzi ya mahali pa kuelekea kati ya nyumbani kwake, au Sinza kwa shangazi yake Ikunji.

 “Leila uko sawa kweli?” Daud alimwuliza, akimtazama usoni.

 Ni kama aliyekuwa anasubiri kuulizwa ili machozi yatumbuke. Chemchemi ikatengeneza mifereji mashavuni. Akaufumbata uso wake kwenye viganja vya mikono na kuangua kilio kwa uchungu.

 “Oh Leila, usilie sasa,” Daud alimbembeleza huku akimgusa begani. “What’s wrong?”

 Si kwamba Daud hakujua masaibu yaliyomfika Leila, la hasha. Alijua fika. Na hata sababu iliyomtoa nje ya ofisi mara baada ya kumwelekeza Leila kwenda kuchuka barua yake, ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kuja kumsaidia kumpeleka nyumbani kwake, ili kumwepusha na ajali kwa sababu ya msongo wa mawazo.

 “Seba amenisimamisha kazi,” Leila alisema huku akijifuta machozi.

“Oops! Kisa nini?”

 “Nilikataa kwenda naye Kanada,” Leila alisema. Akamsimulia mkasa mzima, japo hakugusia kabisa matukio mawili ya kwenda nyumbani kwa Sebastian na kuondoka ghafla.

 “Basi usilie, Leila. Na wala usjilaumu kwa maamuzi yako. Ulichofanya ni sahihi kabisa. Katu usiuze utu wako kwa ajili ya kutetea ugali. Kama ni kazi utapata kwingine.”

 “Nina hali ngumu Daudi – ngumu mno. Nguzo pekee niliyokuwa nimeegemea ni hii kazi,” Leila alijibu na kuanza kulia tena.

 Mzawa aliendelea kumbembeleza akimfuta machozi.

“Kwani Ikunji yuko wapi?”

 Ikunji na Mzawa wanafahamiana. Walikutana kwa mara ya kwanza kwenye mafunzo ya JKT kama wahitimu wa kidato cha sita. Baada ya matokeo kutoka, Mzawa alikwenda kuendelea na Chuo Kikuu. Ikunji hakupata matokeo mazuri, hivyo alibaki chuoni, na baadaye akarudi mtaani. Walikuja kukutana tena miaka mitano baadaye, Ikunji akiwa ameajiriwa na kampuni ya bahati nasibu, inayomilikiwa na Sebastian Mbegu, ilhali Mzawa akiwa amejiriwa kama afisa utawala, kwenye kampuni ya mzee Dominic Mbegu. Japo hawakuwa tena na ukaribu mkubwa, lakini Ikunji na Mzawa walijitanabahisha kama marafiki kila walipokutana.

 “Ikunji hana kazi; kuna sehemu wamemchukua kama kibarua tu, anafanya kazi nyingi kwa ujira kiduchu. Karibu miezi sita sasa, yuko kwenye kipindi cha uangalizi kabla ya kuajiriwa. Na hivi sasa hayupo, amekwenda mikoani huko kuhangaika.”

“Ndivyo maisha yalivyo,” Daud alisema, huku akilitia moto gari na kuliingiza barabarani. “Cha msingi kwa sasa, tuliza jazba uzungumze na Ikunji kwa utulivu.”

Leila aliguna na kutikisa kichwa. Akaendele, “Vema apatikane sasa. Hata mawasiliano yamekuwa magumu. Inaweza kupita hata siku mbili hatujaongea. Naiishi kwa kujihudumia mwenyewe.”

Leila aliona aheri kusingizia vile, kuliko kubainisha safari ya Ikunji na kinachofanya asimpate kwenye simu.

“Kuishi bila kazi ni changamoto sana, hususani kwa mtu mwenye familia kama yeye, wala simlaumu sana, naelewa hali ilivyo.”

Safari iliendelea huku wakiendelea kubadilishana mawazo na kupeana matumaini, hadi walipofika mtaa anaoishi Leila.

“Pale aliposimama yule mama,” Leila alisema, akimwona Daud nyumbani kwake.

Mama aliyekuwa amesimama mbele ya nyumba, aliendelea kutamba huku na kule, na simu yake sikioni, “…hebu nisikilize mjumbe, kuimba kupokezana usiongee sana utadhani simu umepiga wewe. Sasa niambie, kama sipewi haki yangu ulitaka nikashitaki wapi? Ujue mi sishindwi kujichukulia sheria mkononi!”

 Leila alibaki ameganda ndani ya gari. Alitamani kumwambia Daud akamshushie mbele, ili asubiri mpaka mama yule atakapoondoka ndipo arudi kuingia ndani. Kila kilichosemwa na mama yule kilimhusu yeye.

 Daud alifungua pochi yake, akatoa shilingi elfu hamsini, akamkabidhi Leila. “Zitakusaidia japo kwa siku mbili tatu.”

 “Oh my God!” Leila aliganda akimtazama Daud. Alitamani kuzikataa kwa aibu lakini hakuwa na jeuri hiyo. “Asante sana, Daud. Sina cha kukulipa lakini Mungu mwenyewe anajua.”

 “Usijali, Leila. You’re my friend. Ni wajibu wangu kusaidia unapokuwa na shida.”

 Leila alishuka garini taratibu. Akafunga mlango kwa taadhima. Taratibu akajongea alikosimama yule mama. Alipomkaribia, mama yule aligeuka. Walipokutanisha macho, uso ukambadilika kwa ghadhabu.

“Mjumbe tulia nitakupigia baadaye, mtu mwenyewe huyu hapa nimeshambamba.”

Alitoa simu sikioni na kuikata.

 “Shikamoo, mama Karume.”

 “Shikamoo itanifaa nini ikiwa hata maji mnayotumia chooni hamtaki kulipia,” mama Karume alijibu kwa sauti ya juu, kana kwamba anaongea na mtu aliye nyumba ya tatu.

 “Si kama hatutaki mama–”

 “Kumbe ni nini? Mwafanya kusudi siyo?” Akafungua mtandio kichwani na kujifunga kiunoni. “Kodi hamlipi, maji mwatumia bure. Isingelikuwa kukufungieni luku yenu, saa hizi tungelikuwa twashikana mashati na umeme.”

 “Mama tulikwama kidogo, lakini mume wangu akirudi tu tutakulipa,” Leila alijibu kwa sauti ya chini ili kuepusha nadhari ya majirani.

 “Hivi wanifanya miye punguani enh?” Aligonga viganja vya mikono yake. Akarudi hatua chache na kuketi kibarazani. “Hii ni mara ya tatu sasa, kila nikija wasema mumeo katoka. Hivyo yeye huwa atoka tu, haingii siyo?”

 “Mama,” Leila alisema huku akifumba macho na kulaza kichwa upande, “mume wangu hayupo–amesafiri, ndo maana mara zote ulizokuj–”

 “Niondolee mahubiri yako miye,” Alimkatiza. Akabetua mdomo huku akimpandisha juu na kumshusha chini kwa macho. “Kama mmefulia aheri mrudi vijijini kulima. Ya nini kutafuta sifa ya kuishi mjini na uwezo hakuna?”

Leila alibaki kimya, ameduwaa kwa fadhaa. Kila neno alilotaka kulitumia kujitetea, hakupata nafasi. Mdomo wa mama Karume ulikuwa zaidi ya cherehani.

“Au mwenzetu mume kakukimbia?” mama Karume alisema na kuachi cheko ya haja. “Kama umetelekezwa sema tukuoneshe madanga.”

 “Mama tuheshimiane tafadhali!” Leila alijibu alighadhabika. “Tena ushike adabu yako. Unitafutie danga, huo ukahaba ulinifundisha wewe?”

 “Anhaa, kumbe ni fundi wa maneno, eeh?” mama Karume alisimama na kuweka mikono kiunoni. “Basi n’takufunza adabu. Namwendea fundi bomba–anakata maji leo hiihii. Wakati huo, kumbuka kodi yenu imekwisha tangu mwezi wa jana. Ujiandae kuokota vifurushi vyenu barabarani.”

 Mama Karume aliachia msonyo mrefu kama kasuku. Kisha akaondoka eneo lile. Leila aliyekuwa ameganda kama sanamu, alifungua mlango na kuingia ndani baada ya mama Karume kutoweka. Akajibwaga kochini na kuanza kulia.

***

¬¬¬¬Njia nzima, sajini Kinabo alitembea akiangaza huku na kule, akijaribu bahati yake ya kukutana na Nyakanga. Simulizi aliyopewa na Simon, namna mtuhumiwa alivyowaponyoka, iligoma kukita kichwani mwake kwamba, ilitokea kama mazingaombwe tu, bali hurufu ya uhusika wa Nyakanga katika mchezo ule ilinusika katika ubongo wake.

 Baada ya jitihada za kumpata Nyakanga kugonga mwamba, alikata shauri, akabadili uelekeo na kwenda moja kwa moja White Rose Hotel. Japo umbali haukuwa mkubwa sana, lakini aliamua kukodi teksi.

Kiasi cha dakika saba tu, alikwishafika hotelini. Alipoteremka, hakuelekea ndani ya hoteli. Moja kwa moja alikwenda kusimama pembeni mwa mgahawa wa chakula. Ndani ya mgahawa, alionekana mteja mmoja tu akihudumiwa. Kabla mhudumu hajamfikia kumhudumia, alimwona Mufuruki akiwasili na kwenda moja kwa moja nyuma ya meza ya mapokezi.

Kinabo alijiinua na kumfuata. Alimkuta amekwishaketi na kujilaza kivivu.

 “Habari yako bwana,” Kinabo alimsalimu.

 Mufuruki alifumbua macho kwa tabu, kisha akayafumba na kujibu, “marahaba.”

 Kinabo aliuma mdomo wake upande kwa ghadhabu. Alijua jibu lile amepewa kama dhihaka, kwamba kwa umri wake, alipaswa kumwamkia. Kikapita kimya cha sekunde kadhaa Kinabo akiwa anatafuta neno la kusawazisha. Hakulipata.

Mufuruki alipoona kimya, akafumbua macho yake taratibu. Hapo akakutana na kitambulisho cha kazi cha Kinabo, kikiwa mbele ya macho yake.

“Naitwa sajenti Kinabo, natokea Kituo Kikuu cha Polisi. Ninakuhitaji Kituoni muda huu.”

 “Mimi?” Mufuruki aliuliza kwa hamaki, akiyafumbua vizuri macho yake pasi na kuyafumba tena kama awali. “Nimefanya nini kibaya?”

 Haikuwa dhamira ya Kinabo kumpeleka kituoni. Ilimbidi kutumia njia hiyo kumtikisa ili kumvua joho la kiburi. “Utakwenda kujua kituoni.”

 “Kwani hatuwezi kuongea hapa, afande?” alisema, akijiweka vizuri kitini.

 Kinabo alichomoa sigara mfukoni, akaipachika mdomoni na kuiwasha. Akajibu, “Endapo tutazungumzia hapa, sikuoni kabisa ukitoa ushirikiano kwa adabu.”

 “Hapana, afande,” alijibu huku akivikutanisha viganja vya mikono kwa taadhima na utii. “Siwezi kubishana na serikali. Tunaweza kwenda kuketi pembeni tukaongea.”

 Kinabo aliutawanya moshi wa sigara angani. Kisha akasema, “Sihitaji kuongea sana. Naomba tu uniambie Kitabu cha Wageni kiko kwa nani?”

 Macho yalimtoka Mufuruki. Akaduwaa akimkodolea Kinabo, akiwa hajui cha kujibu.

 Kinabo akaongeza, “Bada ya kunijibu unanishangaa. Ndo maana nilitaka tukaongelee kituoni. Hapa utanisumbua.”

 “Si hivyo bwana afande. Nami nasikia tu kuwa Kitabu cha Wageni kimepotea. Lakini nakuapia sijui lolote kuhusu kitabu hicho. Hata humo ndani huwa siingii mara kwa mara.”

“Leo ulifuata nini kule Nyati Inn hotel?”

“Leo?” aliuliza huku akimtazama Kinabo usoni, kisha akajibu haraka, “Nilimpitishia shemeji yako pesa ya matumizi. Nilikuwa nakwenda nyumbani mara moja.”

“Unajua kama tumetoka hapo Nyati Inn sasa hivi, na ametueleza vitu vingine?”

“Amewaambiaje?” Mufuruki aliuliza kwa wahka.

“Alichotuambia ndicho kimenileta kwako unieleze. Kitabu kiko wapi?”

“Kwa kweli sijui chochote, afande.”

Kinabo akabadili mada, “Ni mara ngapi umewahi kumwona Sudi Chotara akiingia humu hotelini?”

 “Sijawahi kumwona, afande.”

 “Ni nani aliyekupa taarifa, kwa mara ya kwanza, kuwa ameuawa?”

 “Nakumbuka tu kulikuwa na makelele humo hotelini huku baadhi ya wapangaji wakitoka nje,” alijibu huku akifanya kuvuta kumbukumbu, “nikasikia watu wakisema kuna mtu ameuawa…sikuingia kumwangalia, na hata sikujua kuwa ni yeye aliyeuawa hadi polisi walipofika na kumtambua.”

 “Inawezekanaje usikie taarifa za mtu kuuawa ndani, halafu ubaki tu nje umerelax?” Kinabo alisaili kwa mshangao.

Mufuruki alipiga kimya akitafuta jibu.

Kinabo alitabasamu huku akitingisha kichwa. Akasema, “Nitakurudia baadaye.”

 Mara baada ya Kinabo kuondoka, Mufuruki aliinuka kwa kasi na kuelekea msalani. Kwa takribani dakika kumi na tano  alizotumia msalani, ngurumo mithili ya mabomu ziliwastaajabisha waliokuwa vyumba jirani na alichoingia yeye. Alipomaliza, akatoka moja kwa moja hadi nje ya mgahawa. Akachukua bodaboda na kuondoka.

 Alifika Nyati Inn Hotel baada ya mwendo wa takribani dakika kumi. Alimalizana malipo na dereva wa bodaboda kuondoka, akabaki amesimama akiangaza kila kona kwa uangalifu. Alipojihakikishia hakuna anayemfuatilia, akaingia hotelini.

 “Karibu, bro,” Simon alimlaki.

 “Nyakanga yuko wapi?” Mufuruki aliuliza huku akitweta.

 “Kuna usalama?”

 “Yeah, nina shida naye tu kidogo.”

 “Ametoka muda si mrefu. Alisema ana udhuru, kuna mahali anakwenda, hivyo leo hatorudi.”

 Anakwenda kuonana na nani? Mbona nilipoonana naye mwanzo hakuniambia kama ana miadi na mtu yeyote? Mufuruki aliganda kwa muda akijiuliza.

 “Labda umpigie simu,” Simon alisema na kumzindua fikrani.

 “Nitampigia,” alijibu huku akigeuza na kutoka. Kabla hajafika mbali, akamgeukia Simon na kumuuliza, “Kuna mtu alifika hapa leo kumtafuta?”

 Simon alifunua kinywa kujibu, ghafla akasita. Akaishia kujilamba mdomo na kumeza mate.

 Sauti nzito nyuma ya Mufuruki, ikasikika ikijibu, “Ndo nimefika hivyo.”

 Mufuruki aligeuka nyuma. Ana kwa ana, akakutanisha macho na Kinabo. Alihisi kuishiwa nguvu. Hofu ilimzizima mwilini. Akaganda kama aliyeopolewa kwenye jokofu. Hakujua acheke au alie, atabasamu au anune, asimame au akae. Kinabo alitembea taratibu akimpita, na kuelekea kaunta alikosimama Simon.

 Kinabo alipofika na kusimama kaunta, aligeuka na kumtazama Mufuruki akiondoka taratibu bila kuaga wala kugeuka nyuma. Hakutaka kumzuia haraka. Alipohakikisha ametoka nje, akamrushia swali Simon. “Ameongea naye chochote?”

 “Kuongea na nani? Na Nyakanga?” Simon aliuliza. Kinabo alipoafiki kwa kichwa, akaendelea. “Hajamkuta. Nyakanga aliomba udhuru. Alisema kuna sehemu anakwenda anahitajika haraka.”

 “Anahitajika wapi?”

 “Hakusema.”

 “Kwa hiyo Mufuruki alifuata nini?”

 “Alikuja kumtafuta Nyakanga. Hakujua kama ameondoka.”

 Kinabo alitoka nje haraka kumuwahi Mufuruki. Hakumwona. Akaangaza mashariki na magharibi, hakumwona. Akarudi ndani.

 “Nyakanga anaishi wapi?”

 Simon akamwelekeza.



Ndani ya saluni ya mama Mainda, wateja waliendelea kuhudumiwa huku wengine wakifika na kuketi sofani kwa ajili ya kupiga soga.

“Hivi, ni msanii gani huyo aliyevujisha picha za utupu?” mama Mainda uliuliza, huku akiendelea kujipoadoa kwenye kioo kipana cha ukutani.

 “Maimuna huyo,” msichana aliyeketi kwenye mashine ya kukaushia nywele alijibu, “lakini hakuzivujisha yeye. Ni yule boyfriend wake ndo ameamua kumharibia.”

 “Hakuna cha boyfriend hapo,” msichana mwingine aliyekuwa anaseti nywele alidakia. “Ni yeye mwenyewe ndiye amejirekodi na kuzisambaza.”

 “Si rahisi kihivyo Diana,” mama Mainda alijibu. “Yaani ajidhalilishe namna ile kisa nini? Amechanganyikiwa au?”

 “Hizo ndo kiki sasa ukisikia. Hazipatikani kirahisi,” Diana alijibu huku akishikilia kitambaa kilichopachikwa masikioni kuzuia joto kali la mashine. “Na utaona haitochukua hata muda mrefu ataachia filamu mpya.”

 Gari aina ya Toyota Prado ilifika na kuegesha nje ya saluni, wakati wakiendelea na mazungumzo. Mama aliangalia nje kupitia kioo cha saluni, huku akijiweka sawa kumpokea mteja.

 “Kama Maimuna mwenyewe amevujisha, kwa nini akawa anamwambia huyo jamaa kuwa akizivujisha tu anajiua?” msicha wa mwanzo aliendelea kumtetea Maimuna.

 “Kumruhusu mpenzi wako akupige picha za utupu halafu umkataze asizisambaze, ni sawa na kujaribu kuzuia jani la mti lililoangukia mtoni; hapo jani haliwi na maamuzi tena, litapelekwa kokote maji yakatapoamua kuelekea,” mama Mainda alisema na kuangua kicheko.

 “Mapenzi jamani,” msaidizi wa mama Mainda, alidakia. “Ukishapenda utafanya lolote. Hayo ya kuhofia kuvujishwa huja baadaye kabisa.”

 “Unadhani wao hawalitambui hilo?” Diana alihoji akimtazama mama Mainda. “Ule ni mchezo tu. Wanacheza na akili zetu ili kukuza umaarufu. Hata ukiiangalia ile video, Maimuna alikuwa anaangalia kabisa kamera – alijua kuwa anarekodiwa.”

“Sasa kama sanaa ndo ngumu hivyo, aheri watafute kazi nyingine za kufanya. Waje hata humu masaluni tugawane umasikini,” mama Mainda alijibu kwa kedi.

 “Kazi zenyewe ziko wapi?” Diana alicheka kwa sauti. “Mama Mainda, shukuru Mungu mwenzetu una kwako. Hudaiwi kodi ya mlango wa biashara wala ya chumba cha kulala.”

 Mama Mainda aliachia tabasamu kama la mamba. Hakuna raha aipendayo kama kusifiwa kuhusu nyumba na biashara anazomiliki. Kabla hajajibu, kupitia kioo kikubwa kilichowambwa ukutani, alikutanisha macho na mama Mbegu aliyefunua pazia na kuingia.

 “Oh, somo huyo,” mama Mainda alimlaki. “Karibu.”

“Nimeshakaribia,” mama Mbegu alijibu, akiwa amesimama katikati ya mlango, akijipepea usoni kwa kipande cha gazeti. “Wasichana hamjambo?”

 Wasichana waliokuwa wakipiga soga wakamsalimu.

 “Bahati, we endelea basi,” mama Mainda alimwambia msaidizi wake wa kazi, kisha akaweka mkebe wa vipodozi mezani na kumgeukia mama Mbegu. “Twenzetu ndani basi.”

Walitoka saluni na kufuatana hadi mlango wa kuingilia nyumba kubwa. Wakaingia na kuambaa koridoni. Milango ya vyumba vya wapangaji ilijipanga kulia na kushoto kwa kutazamana.

Mama Mainda na mama Mbegu walikutana yapata miaka kumi tisa nyuma, katika vikundi vya mikopo ya akina mama. Tangu hapo wakashikana urafiki. Wakashibana mno, kiasi cha kushirikishana na kusaidiana mambo mbalimbali.

 “Yaani Dar utadhani tuna laana jamani,” mama Mbegu alisema wakati wakitembea koridoni. “Si kwa joto hili aisee.”

 Mama Mainda akacheka na kusema, “Unaweza kuwa unatembea huku unasikia harufu ya mishikaki, kumbe ni wewe mwenye ndo unaungua.”

 Mama Mbegu alicheka. Wakaufikia mlango wa barazani. Mama Mainda alifunua pazia na kuingia akifuatiwa na mama Mbegu.

 “Bwana Temu hajambo?” mama Mbegu alisaili.

 Mama Mainda alimgeukia na kumfinyia jicho, huku akiweka kidole mdomoni kumwashiria afumbe mdomo. Mumewe, mzee Kizamba, alikuwemo barazani amejilaza sofani.

Mzee Kizamba alipomwona mama Mbegu akiingia ndani, alijiinua na kuketi. “Oh, karibu shemeji.”

 “Ahsante shemeji. Tumekuvamia ghafla,” mama Mbegu alijibu.

 “Hakuna taabu shemeji,” mzee Kizamba alijibu huku akipunguza sauti ya runinga. “Habari za nyumbani?”

 “Mungu ni mwema, shemeji. Hatujambo.”

 “Utakunywa nini?” mama Mainda alimuuliza mama Mbegu. Kabla hajajibiwa akamgeukia mzee Kizamba. “Baba Mainda tupishe kidogo, tuna mazungumzo.”

 “Naomba maji tu,” mama Mbegu alijibu.

 Mzee Kizamba alisimama. Akatoka nje na kuwaacha peke yao ndani.

 Baada ya mzee Kizamba kutoka, mama Mbegu aliuliza kwa sauti ya chini, “Hivi hakunisikia kweli?”

 “Hata akisikia atafanya nini?” mama Mainda alisema na kucheka. “Mbona amekwishamjua. Alikuta meseji kwenye simu yangu.”

 “We!” Mama Mbegu aliganda kwa mshangao. “Na hajakufanya chochote?”

“Anifanye nini sasa? Alijaribu kujitutumua, nikamwambia isiwe taabu anipe talaka yangu, kila mmoja ashike hamsini zake. Alikuwa mdogo kama punje ya mtama. Kabaki tu kutishia kuwa siku akinikuta naye atanipasua.”

Mzee Kizamba ni miongoni mwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme, waliopitiwa na mchakato wa kuondolewa makazini kwa sababu ya vyeti feki. Tangu hapo, amekuwa akiishi kwa kuungaunga na kutegemea biashara za mama Mainda.

Waliendelea kupeana michapo ya maisha pamoja na raha na karaha za michepuko yao, hadi mama Mbegu alibadili mada. “Leo hata sikai mwenzangu. Nimepitia tu hiyo pesa.”

 Mama Mainda aliinuka na kwenda chumbani. Akarudi na kijibegi mkononi. Akakifungua na kutoa pesa pamoja na daftari. Wakahesabiana na kukabidhiana. Zoezi hilo hufanyika kwa siri pasi na mtu mwingine kugundua.

 Nyumba anayoishi mama Mainda na mzee Kizamba, ni mali ya mama Mbegu. Kwa hofu ya kuonekana anafuja mali za mumewe, mzee Dominic Mbegu, ndipo alimweka mama Mainda kwenye nyumba kama kivuli, ili asimamie kila kitu kwa niaba yake. Akamwachia vyumba viwili na sebule, pamoja na mlango mmoja wa biashara kwa ajili ya saluni bure. Milango mingine ikapangishwa. Kila baada ya miezi mitatu akawa anafika kuchukua kodi yake.

 Wakiwa wanamalizia makabidhiano, Leila aliwasili akiwa amechoka mwili na akili. Alifungua mlango wa mbele na kuingia ndani. Akiwa koridoni, mbele ya mlango wa sebuleni kwa mama Mainda, macho yake yaligongana na mzee Kizamba, aliyekuwa amesimama uani akichanganya chakula cha kuku. Mzee Kizamba alimpungia mkono akimwita kule alipo.

 Kupitia pazia nyepesi mlangoni, mama Mbegu alimwona Leila akipita na kuelekea uani. Akamgeukia mama Mainda na kusema, “Halafu kuna mchapo nilisahau kukupa.”

 “Haukaukiwi na michapo kila uchao,” mama Mainda alijibu. “Enhee kuhu nini tena?”

 “Kuhusu mtoto wako, Leila.”

 “Kafanyaje tena?”

 “Hivi si nilikwambia kuwa, sasa hivi tuko na Seba pale ofisini?” mama Mbegu aliuliza, akitafuta pa kuanzia. Mama Mainda alipoafiki kwa kichwa, akaendelea, “Sasa, bahati imemdondokea Leila.”

 Mama Mainda akacheka. Hakujali kama Leila ni mkwewe, bali alichokiona ni fursa. “Yale yale ya mama Mbegu na mzee Dominic Mbegu. Sasa hivi tutasikia naye ana mjengo Tabata.”

 “Si mpaka angekuwa na akili hizo sasa. Hivi tunavyoongea, Seba amemsimamisha kazi.”

 “Imekuaje kwani?”

 Mama Mbegu akamsimulia mkasa mzima.

 “Huyu mtoto ni mpumbavu kumbe?” mama Mainda alisema. “Anajua kabisa hali ya Ikunji kwa sasa. Hana senti tano kipande. Badala aokoe jahazi, yeye anajifanya malaika. Mwache aonje joto ya jiwe, mwenye atasalimu amri.”

 “Nimemwona ameingia, amepitiliza uani.” mama Mbegu alijibu huku akichungulia koridoni. “Labda amekuja kumshitakia mzee Kizamba.”

 Mama Mainda akabetua mdomo, “Atakuwa amepeleka msiba matangani. Kizamba mwenye amesalimu amri kwa Temu, atamsaidia nini yeye?”

***

Leila alimfikia mzee Kizamba uani na kumjulia hali. Bila kurefusha muda, alimsimulia kuhusu taarifa za kifo cha Sudi Chotara na namna anavyohofia usalama wa Ikunji. Hakujua kama mzee Kizamba amekwishapata taarifa.

 “Ni kweli hapatikani kwenye simu, walakini hilo lisikuumize kichwa. Iku ni mzima, bukheri wa afya. Amenipigia simu kunijuza kila kitu.”

 “Nini kimetokea?” Leila alimkodolea mzee Kizamba.

 “Kwanza shangazi yenu hatakiwi kujua lolote kwa sasa,” mzee Kizamba alisema, huku akijipinda kuchungulia koridoni.

 Leila alitingisha kichwa kuafiki.

Mzee Kizamba alimsimulia mkasa ulivyo kwa kadri alivyosimuliwa na Ikunji. Lakini baadhi ya maeneo yenye ukakasi hakuyabaisha haraka.

Leila alijitwisha mikono kichwani. Akaomboleza, “Mungu wangu! Tumekwisha.”

“Wewe ukianza kuonesha udhaifu ndo utaharibu kila kitu. Kuwa mtulivu ili umfariji, na Mungu atasaidia. Alisema atakupigia simu leo. Jitahidi uongee naye kwa utulivu badala ya kumzidishia sonona.

Leila alinyamaza kwa muda, kisha akasema, “Sawa.”

“Umemwona bosi wako sebuleni?” mzee Kizamba alisema huku akichungulia usawa wa mlango wa kuingilia barazani.

 “Sio bosi wangu tena.”

 “Amaa!” mzee Kizamba alibaki kinywa wazi. “Imekuwaje?”

 “Wamenisimamisha kazi.”

 “Yeye na nani?”

 “Na Seba.”

 “Kisa?”

 Kabla Leila hajajibu, pazia ya mlangoni ilifunuliwa, mama Mbegu akachomoza, akifuatiwa na mama Mainda. Kwa pamoja wakakunja kona kuelekea uani aliko mzee Kizamba.

 “Shemeji,” mama Mbegu aliita baada kutokeza uani, akifuatiwa na mama Mbegu. “Mi nawakimbia hivyo.”

 “Mbona leo juu juu sana?” mzee Kizamba.

 “Nilipita tu mara moja, kuna kikao na kampuni mchana huu, hivyo inabidi nikapambane na foleni.”

 “Shikamoo,” Leila aliamkia.

 Mama Mainda hakuitika.

 Mama Mbegu akaitika, “Marahaba.”

 “Basi sawa. Nikutakie kikao chema.”

 “Nashukuru sana.”

 Mama Mainda na mama Mbegu wakarudi koridoni na kuondoka.

***

Ikunji alirudi hotelini, baada ya kuachana na Nyakanga. Alihitaji muda japo kidogo kupumzisha mwili na akili. Kwa bahati, alipojilaza tu usingizi ukamchota. Alikuja kushituka majira ya saa kumi alasiri. Kiu ya kwenda kukutana na Nyakanga ilimjaa rohoni. Alikwishaamini Nyakanga ndiye mtu pekee atakayemsaidia kufumbua fumbo hilo. Aliandaa msururu wa maswali ya hadaa na mitego atakayoyatumia pindi watakapokutana.

Kwakuwa muda wa miadi ulikuwa bado haujatimu, akatoa simu na kumpigia mzee Kizamba.

 “Hallow, nani?” sauti ya mzee Kizamba ilirindima simuni.

 “Ikunji hapa,” alijibu kwa utulivu. “Shikamoo.”

 “Oh Iku, marahaba. Mzima? Mbona namba mpya?”

 “Aah ni hadithi ndefu,” alisema huku akipiga mwayo. “Lakini kwanza, nimefanikiwa kumpata yule dereva wa teksi aliyenipokea. Na kwa bahati alikuwa kwenye teksi ileile.”

 “Alhamdulillah! Enhe ulimpataje? Na anazo dalili zozote?”

 Ili kupata mtiririko mzuri, wa namna alivyompata dereva, Ikunji alianza kumsimulia kuanzia alivyonusurika, kwa msaada wa Nyakanga, kukamatwa na polisi hotelini, na kufikia hapo ndipo akabainisha jibu la kwa nini alizima simu yake. Alieleza namna alivyomwona yule dereva mara baada ya kurejea hotelini kumfuata Nyakanga.

 Kujibu swali la endapo dereva yule ana dalili za kuhusika, Ikunji akasema, “Hisia zinaniambia anahusika kwa namna moja au nyingine. Kwa bahati, nili–” kabla hajamalizia alichokusudia kusema, alivuta mkoba wake na kuufungua zipu ya pembeni, akatoa ile karatasi aliyoandika namba, kisha akamalizia kusema, “–nilifanikiwa kuchukua na namba ya gari.”

 “Safi. Umecheza kama Samatta hapo.”

 “Sasa, hatimaye nilifanikiwa pia kuonana na Nyakanga, yule mama aliyeniokoa kule hotelini,” Ikunji aliendelea kusimulia mkasa mzima, akitanabahisha na maelezo ya Nyakanga kuwa, hao wauaji wamedhamiria kumwua ili kutengeneza hisia kuwa ni kisasi kilichofanywa na wafuasi wa Sudi Chotara.

 “Wanaweza hata wasikuue, bali wakakuvizia na kukubambikia hicho Kitabu cha Wageni, alimradi tu ukikamatwa na polisi itaonekana ni kweli ulitoroka nacho baada ya kuua.”

 Ikunji alipomaliza kuelezea mengi kumhusu Nyakanga, mzee Kizamba akasema, “Ni dhahiri huyo mama anajua mengi. Nahisi anajuana na mmoja kati ya wahalifu. N’na imani anajua hata mahali kilipo hicho kitabu. Kama sivyo, basi huenda anamjua mtu aliyenacho.”

 “Na kwa vyovyote vile, yeyote aliye nacho hicho kitabu, atakuwa anahusika naa mauaji,” Ikunji aliongeza.

 “Na kama hivyo ndivyo, basi huyo mama ni mtu wa karibu na muuaji. Hivyo, unapokwenda kuonana naye zidisha umakini. Huwezijua baada ya kuonana nawe amekwenda kuzungumza na nani mwingine.”

 Ikunji alipiga kimya. Mawimbi ya hofu yalianza kurindima katika kingo za moyo wake. Taratibu akaanza kumtazama Nyakanga kwa jicho la indhari na walakini.

 “Nimekuelewa, uncle. Acha sasa nikaoge nijiandae kwenda.”

 “Mkoba wako utamwachia nani?”

 “Nimwachie nani tena?” Ikunji alijibu kwa mshangao. “Nitakwenda nao popote.”

 “Umesema huyo mama anaonekana ni mtu wa tamaa sana. Na amekwishajua kuwa unatembea na dhahabu kwenye mkoba. Huoni kwamba, kwa tamaa yake anaweza kukusukia mpango ukavamiwa na kuporwa?”

Ikunji alishusha pumzi. Alihisi kupigwa shoti mwilini. Hakuwa amelifikiria hilo. Akasema, “Lakini kuuacha hotelini ni risk sana.”

“Ndiyo. Ni hatari kuuacha hotelini. Lakini pia ni hatari kutembea nao barabarani. Sasa utachagua hatari yenye nafuu.”

“Sawa. Nitajua cha kufanya–”

“Na umekwipanga hatua itakayofuata baada ya kujua mahala kilipo hicho kitabu?”

“Ikiwa ni sehemu ninayoimudu, nitavamia na kukichukua. Lakini kama ni sehem–”

“Usithubutu kufanya hivyo,” mzee Kizamba alimkatisha. Kisha akaendelea. “Ukikamatwa nacho, kila mtu ataamini kuwa ni wewe ndiye uliyekichukua hotelini baada ya mauaji. Usitafute makuu. Ukijua tu mahali kilipo, haraka jisalimishe mwenyewe polisi, na uwaambie mtu unayemshuku. Wao watakapomvamia huyo mtu na kumkuta nacho, simulizi yako itaanza kuaminika.”

“Nimekuelewa.”

“La mwisho, Leila alikuja hapa,” mzee Kizamba aliendelea. “Amekwishajua kuwa Sudi ameuawa. Na amepagawa mno. Analaumu kwa nini ulimficha mlipowasiliana. Amekutafuta sana simuni haupatikani.”

Kutajiwa jina la mkewe kukamvuruga kichwa. Akaukumbuka ujumbe aliotumiwa kumhusu. Moto wa wivu ukaanza upya kumbabua moyo. Ghadhabu zikamjaa.

“Aah achana naye.”

“Usiseme hivyo. Yule ni mkeo. Anayo haki ya kupata taarifa muhimu hata kama si zote. Kumkalia kimya kunaweza kumsababisha aropoke kwa mashoga zake kuhusu safari yako ya Arusha. Hapo kila kitu kitaharibika.”

Ikunji hakufanya papara kumweleza lolote mzee Kizamba, juu ya ujumbe aliotumiwa kuhusu Leila. Alipanga kupeleleza mwenyewe pindi arejeapo Dar es Salaam.

“Sawa. Nitampigia nikishamalizana na Nyakanga.”

***

Sajini Kinabo aliwasili kituoni, akitokea hotelini. Aghalabu kesi nyingi kituoni hapo huripotiwa asubuhi, na mahojiano mbalimbali hufanyika mchana. Kwa sababu hiyo, haikumwia ugumu kupata utulivu wa kutosha, kuzungumza na watuhumiwa wake kwa muda huo. Kwa sababu ya haraka aliyokuwa nayo, hakufanya zohali. Alianza na Gladness. Alimtoa mahabusu na kwenda naye ofisini kwake.

Wekundu wa macho ya Gladness ulishabihiana na sehemu ya ya juu ya mashavu yake. Bila shaka alilia mchana kutwa na usiku kuchwa.

“Hivi unavyoniona, tumetoka gereji kumkarabati Mmari. Kwa bahati, yote uliyojaribu kunificha, mwenziyo amefunguka ukweli wote.”

“Ndiyo bosi,” Gladness alijibu, akitetemeka mashavu.

“Mi siyo bosi wako,” Kinabo alisema huku akifunua faili mezani. “Niambie, kwanini baadhi ya wateja huwa unawapitisha mlango wa faragha badala ya ule wa kawaida?”

“Siyo mimi, afande.”

“Kwa hiyo Mmari anakusingizia?”

“Ni yeye mwenyewe ndiye huwapitisha huko nyuma.”

“Inawezekanaje akawapitisha kinyemela bila kukuarifu Mapokezi? Anajuaje kama chumba husika hakina mtu?”

“Huwa anaulizia kwanza vyumba vilivyo wazi, kisha ndiyo anaelekeza chumba fulani tusikiuze.”

“Ni wateja wangapi walioingizwa kwa njia hiyo siku ya tukio?”

Gladness alinyamaza. Akainamisha kichwa chini huku akiupakata uso viganjani mwake. Kinabo alipiga meza kwa nguvu, kwa kutumia viganja vyake, huku akisimama kama chui aliyeona swala.

“Wangapi?”

Gladness aliachia ukelele wa woga, baada ya kuhisi Kinabo anataka kumrukia kwa ghadhabu. Akawahi kusema, “Mmoja afande – mmoja tu.”

“Ndiye huyo kijana aliyechukua chumba namba 225?”

“Hapana afande, huyo nilimhudumia mimi.”

“Huyo wa Mmari alipewa chumba namba ngapi?

“Sikumbuki vizuri, lakini nadhani ilikuwa namba 223.”

“Yukoje huyo mteja?”

“Sikumwona wakati anaingia, afande. Niliambiwa tu na Mmari kuwa chumba namba 223 kina mtu ili nisikiuze.”

Kinabo alirudi kuketi. Akafunua faili na kuandika mawili–matatu. Alipomaliza, akamrushia swali lingine kwa sauti isiyo na papara, “Naomba unitajie mwonekano wa kijana aliyechukua chumba namba 225.”

“Ni mrefu, mweupe–mweupe, na ana ndevu nyingi mashavuni.”

Kwenye mahojiano ya mwanzo, Gladness alidai kumsahau kijana huyo. Lakini sasa amemkumbuka. Kinabo aliandika kwenye faili lake.

“Kingine?”

“Ana lips nyeusi hivi–nadhani ni kama anavuta sigara.”

Kinabo aliweka kalamu mezani, akainuka na kumrudisha Gladness mahabusu. Kisha, akamtoa Mmari na kurejea naye ofisini.

“Nimekuita ili kukuuliza baadhi ya vitu,” Kinabo alisema baada ya Mmari kuketi kwenye benchi, mbele ya dawati lake. “Majibu yako ndo yatakayoamua utoke kwa dhamana au uingizwe kwenye ngwe ya pili ili kutapishwa ukweli ulioumeza.”

 Mmari alishusha pumzi nzito kama nguruwe anayefukua mihogo. Hali yake ilikwishaanza kudhoofu kwa uchovu na mashaka.

 Kinabo akaendelea, “Marehemu Sudi Chotara alifuata nini hotelini kwako siku ya tukio?”

 “Niamini, afande,” Mmari alijibu huku akikumbata viganja vya mikono yake kwa taadhima, “sikumwona kabisa Sudi akiingia hotelini.”

 “Ulipataje taarifa kuwa kuna mtu ameuawa chumbani?” Ikunji alirudi swali alilokwisha kumuuliza mara ya kwanza.

“Niliambiwa kuna damu inavuja toka chumbani.”

 “Taarifa hiyo uliitoa kwa nani? Na alikupaje taarifa hiyo?”

 Mmari akarudia maelezo yale yale aliyoyatoa awali. Kinabo akafungua faili na kuandika. Kisha akatumia dakika kadhaa kuperuzi baadhi ya maswali aliyoyandaa kabla hajanyanyua tena uso wake.

 “Najua unapoingiza michepuko yako hotelini, huwa hautumii mlango wa mbele kwa kuhofia kuonekana. Hilo halinihusu. Nachotaka uniambie ni wateja wenye hadhi gani ambao pia hutumia mlango wa faragha kuingia?” Kinabo aliyapanga maswali moja baada ya lingine. “Na nikukumbushe tu kuwa, punde tumetoka kumminya mbavu Gladness. Amefunguka kila kitu. Ole wako upishane naye maelezo.”

Kusikia Gladness amefunguka kila kitu, Mmari hakuwa na ujanja tena. Aliinua uso akiwa amelainika. Akasema kwa sauti ya chini, “Ni wateja wasiotaka kuonekana ndiyo hutumia mlango ule.”

“Ni mara ngapi Sudi Chotara ametumia mlango huo wa faragha?”

Mmari alijikuna kichwa na kidevu mfululizo kama anayepiga kinanda. Alihisi kuwashwa mwili mzima kama aliyepuliziwa upupu.

“Sudi hakuwahi kuingi hotelini kwan–”

“Kwa hiyo Gladness ni mwendawazimu mpaka amtaje?”

“Sijawahi kumwingiza Sudi hata mara moja. Labda kama ni yeye ndiye alimwingiza bila kuniambia. Niamini afande.”

“Nitakuamini endapo utaweza kulamba pua yako kwa ulimi wako mwenyewe. Utaweza?” Kinabo alisema huku akiinama kuandika kwenye faili. “Naomba unitajie jina la mteja uliyempa chumba namba 223 siku ya tukio.”

Mmari aliganda kama sanamu, mpaka Kinabo alipoinua uso kumtazama ndipo akasema, “Anaitwa Ali.”

“Ali nani?”

“Simjui jina lake la pili.”

“Yukoje?”

“Ni kijana tu. Mrefu. Mwembamba. Anapenda kufuga mzuzu.”

“Mwekundu au wa njano?”

“Ni mweusi.”

Kinabo aliendelea kuandika. Alipomaliza akainua tena uso kumtazama Mmari. “Ilikuwaje akataka kutumia mlango wa faragha?”

“Alisema kuna jamaa huwa anafanya nao biashara ila hawapendi kuonekana. Alisema atakuwa anakuja kuwachukulia vyumba mara kwa mara wanapowasili Arusha.”

“Ameshakuja mara ngapi kuwachukulia vyumba hao wafanya biashara?”

“Hii ilikuwa mara pili.”

“Unawajua hao wafanyabiashara?”

“Hapana. Mara zote hizo, alikuwa anakuja peke yake kwanza, nikishamfungulia mlango, anaingia ndani kuwasubiri wenziye. Hivyo, huwa sifungi mlango. Wenziye wanapofika ni yeye ndiye huenda kuwachukua na kuwaingiza ndani. Mimi huwa nakuwa ofisini.”

***

Ikunji aliwasili Golden King saa moja kasorobo, magharibi. Alidhamiria kuwahi kabla ya Nyakanga, ili apate wasaa wa kutosha kuyasawiri mazingira, na namna ya kukabiliana na hatari yoyote endapo ingetokea. Golden King ni ni mgahawa mashuhuri wa chakula, ambapo kwa wakati wa jioni, viti na meza hutolewa na kupangwa vizuri nje ya mgahawa katika eneo lenye kivuli na hewa mwanana. Watu walienea kila kona wakipiga soga na kupata maakuli mezani. Harufu ya kuku wa kuchoma, nyama ya mbuzi, samaki, na aina nyingine za maakuli zilipisha kwa kadri ya mvumo wa upepo.

 Wahudumu walikuwa juujuu wakipishana huku na kule, kukabiliana na wingi wa wateja. Zilikakatika takribani dakika kumi na tano pasi na japo mmoja wao kumfikia Ikunji mezani pake. Giza la magharibi likiwa limeanza kumeza nuru, ndipo Ikunji alipomwona Nyakanga akiwa amekwishaketi kwa mbali kidogo toka eneo aliloketi yeye. Hakumwona wakati akiwasili, hivyo hakutambua amefika muda gani.

Alijaribu kutuliza macho ili kuona endapo kuna mtu yeyote jirani na Nyakanga, ambaye angelimtilia mashaka, walakini halikumdhirikia baya lolote machoni.

 Nyakanga alionekana akiinuka mezani pake, akiacha chupa ya maji na mfuko wa kitambaa. Akatembea taratibu kuelekea msalani. Humo njiani alisalimiana na watu kadhaa waliomsemesha kwa jina lake, kuonesha namna alivyofahamika. Kama kawaida yake, alivaa bukta pana nyeusi iliyoshuka hadi chini ya magoti, pamoja na fulana ya kaki iliyofunikwa kwa juu na mtandio wa bluu. Miguuni alivaa raba nyepesi za rangi ya maziwa.

 Ikunji aliamua kutangulia mezani alipokuwa ameketi Nyakanga, ili atakaporejea amkute pale. Hakuwa amebeba chochote. Alisimama na kuelekea mezani kwa Nyakanga. Alivalia kadeti ya bluu, na juu ya fulana ya kijivu alivalia koti jeusi. Kichwani, alivaa kapelo ya mabaka mabaka. Miguuni, alibaki na araba zilezile alizotoka nazo Dar es Salaam.

 Alifika mezani na kuvuta kiti karibu na kile alichokuwa amekalia Nyakanga kabla hajainuka. Akaketi. Macho yake yalipiga kule kwenye njia ya kwenda msalani, alikoelekea Nyakanga, lakini hakumwona tena. Alikwishakunja kona mwishoni mwa jengo. Akavua kapelo na kuiweka mezani. Macho yake yalipiga kwenye mfuko aliouacha Nyakanga mezani, ukiwa wazi sehemu ya mbele. Ndani ya mfuko kulikuwa na pochi ndogo nyeusi na kitambaa laini cha jasho, vikiwa juu ya kitabu kipana cha rangi ya chungwa. Sehemu juu ya kitabu kile, yalisomeka maandishi yalikamata hisia za Ikunji na kumtengenezea mshituko mkubwa moyoni.

 “Habari bosi,” muhudumu alimsalimu Ikunji. “Hiyo meza ina mtu, unaweza kuketi hapo mbele kama hutojali.”

 “Si alikuwa ameketi Nyakanga hapa?” Ikunji aliuliza. Mhudumu alipotingisha kichwa kuafiki, akaendelea, “Ndo alikuwa akinisubiri mimi.”

 “Oh, samahani,” mhudumu alijibu kwa taadhima. “Naweza kukuletea chakula?”

 “Ngoja arudi basi tutaagiza kwa pamoja.”

 Mhudumu alipoondoka, Ikunji akarusha macho kwenye mfuko kusoma maandishi juu ya kitabu. Haikuwa rahisi kusoma maandishi yote kwa sababu ya vitu vidogo vidogo vilivyokuwa juu ya kitabu. Sehemu ya mwisho ya maandishi, kwenye mstari wa juu, yalisomeka “Cha Wageni”. Na mstari wa chini, sehemu ya maandishi ilisomeka “ose Hotel”. Moyo ukafanya sarakasi kifuani mwake. Akainua macho kule alikoelekea Nyakanga, bado hakumwona.

Kuna sauti ikawa inamwambia akichomoe kwenye mfuko. Hofu ikawa kwa mhudumu aliyetoka kuzungumza naye. Alihofia endapo angemwona akipekua mfuko, na ukizingatia amekwishaonesha mashaka juu yake. Aliinua macho kumuangaza mhudumu. Hakumwona. Taratibu, akapeleka mkono kwenye pochi, akavuta kitabu kwa uangalivu mkubwa. Kabla hajamaliza kikitoa, tayari maandishi yalisomeka vizuri.

Kitabu cha Wageni

White Rose Hotel

S. L. P 10101

Arusha.

Ikunji alipigwa butaa. Mishipa ya fahamu ilimtutumka kichwani. Alihisi mapigo ya moyo yakimdundia mgongoni. Wazo pekee lilipota ithibati kichwani mwake ni kukichukua na kutoweka nacho. Lakini alijihadhari kuwa, endapo atatoweka nacho hatopata fursa ya kujua mengi, toka kwa Nyakanga. Na kama akitoweka nacho, nani atakayemwamini kuwa alikikuta kwa Nyakanga? Hilo lilizidi kumvuruga. Alikilazimisha kichwa chake kufanya kazi kwa kasi ya umeme bila mafanikio.

 Akiwa anajaribu kupambana na mgogoro ulioibuka kichwani mwake, akahisi kama mchakacho nyuma yake. Alitulia kisikilizia. Nusu ya Kitabu cha Wageni ilikuwa mkononi mwake ilhali nusu iliyobaki ikiwa bado imo kwenye mfuko. Taratibu akageuza kichwa upande wa kushoto. Kupitia kona ya jicho, akaona mtu amesimama kwa nyuma yake. Akarudisha uso wake mbele, na kugeuza kichwa upande wa kulia, napo akathibitisha kuna mtu amesimama nyuma yake. Kilichofanya ajue ni mtu mmoja tu aliyesimama nyuma yake, ni namna alivyovaa. Alichoona kulia, ndicho alichokiona kushoto; raba ya rangi ya maziwa, na bukta pana nyeusi.

 Ni yeye.

 Hakujua alifika muda gani nyuma yake. Lakini alikuwa na hakika kuwa ni yeye.

 Hakujua afanye nini? Amalizie kukitoa kitabu au akirejeshe? Kila alichotaka kufanya alisita. Alibaki akihangaika kwenye kiti kama aliyemeza nyuki. Aliamua kukiacha kitabu na kugeuka nyuma. Akakutanisha macho na Nyakanga.

 “Oh dada,” alijisemesha. “Nilifika ukiwa unaelekea kule…nadhani msalani…nashangaa tena unatokea kwa nyuma kama msukule.”

 Nyakanga hakujibu. Aliganda akimtazama usoni. Hacheki, hanuni.

Papo hapo yule mhudumu aliyataka kumzuia Ikunji asiketi pale mezani alifika haraka. Akamwuliza Nyakanga. “Kuna usalama?”

Ikunji alihisi kutepeta. Alimtazama mhudumu hali uso ukiwa umemsawajika ghafla. Hatma yake ilibaki mikononi mwa Nyakanga. Japo macho yalikuwa wazi lakini alihisi hayaoni. Na ingawaje masikio yake hayakuwa yamezibwa lakini alihisi yamepoteza usikivu. Kila kiungo alihisi kimepoteza uwezo wa kufanya kazi. Kitu pekee alichokuwa na hakika nacho ni kifua chake kushindwa kuhimili mapigo ya moyo.



Kinabo aliingia maeneo ya Tengeru majira ya saa kumi na mbili jioni. Na kama alivyoelekezwa na Simon, aliwauliza watu wawili watatu, nyumba anayoishi Nyakanga mpaka akaipata.

 Ni nyumba ya matofali ya kuchoma, iliyozungushiwa uzio wa michongoma. Mlango wa kuingilia, ulioko baina ya madirisha mawili ulikuwa wazi. Kinabo akabisha hodi lakini hakujibiwa. Akasukuma mlango na kuingia. Ukimya ulitanda nyumba nzima. Hapakuonekana dalili ya mtu. Vyumba vinne vilivyojipanga kulia na kushoto, viliitenganishwa na sebule ndefu inayokwenda hadi uani. Juu, hapakuwa na dali, kiasi cha kufanya utandu wa buibui kutengeneza mfano wa nyavunyavu angani. Chini, hapakuwekwa sakafu, kiasi cha kulazimu kila atokaye kuoga aingie na viatu.

 Kinabo alibisha hodi kwa mara ya pili akiwa tayari sebuleni, akitembea kuelekea mlango wa uani. Sauti ya mwanamke ilimkaribisha. Hakujua inatokea chumba gani. Alipogeuka nyuma, akawajihiana na mwanamke aliyekuwa amesimama kwenye mlango wa chumba chake; nusu ya kiwiliwili kikiwa nje kama anayechungulia, huku nusu iliyobaki ikiwa kwa ndani imekingwa na pazia mlangoni. Ni mwanamke wa hirimu ya Nyakanga japo alionekana kuwa mfupi zaidi.

 “Habari yako,” Kinabo alimsalimu.

 “Njema. Karibu.”

 “Ahsante,” Kinabo alisema huku akimsogelea. “Samahani kukuharibia usingizi.”

 “Ahh usijali, kaka. Hata sikuwa nimelala.”

 “Sawa. Mi naitwa Jimmie. Ninamuulizia Nyakanga.”

 “Mmh sidhani kama yupo,” alijibu huku akichungulia mlango wa chumba cha pili. “Naona ameshatoka.”

 “Ametoka zamani sana?”

 “Imekuwa muda kidogo. Alipofika tu aliingia kuoga, kisha hakukaa sana.”

 “Hakusema anakwenda wapi?”

 “Atuage tena siye makapuku?” alisema huku akibetua mdomo. “Nilimsikia tu analumbana na mtu kwenye simu kuhusu hela…mara aseme hakubali mpaka sijui apewe laki tano, mara aseme vile…kama alikuwa ananikoga, shauri yake.”

 “Kaishaingizwa chaka huyo,” Kinabo alisema na kucheka kwa kebehi. “Nyakanga apate wapi dili ya laki tano?”

 “Mwenzangu we! Acha na sisi tutafute kazi za kufua mashuka ya gesti labda tutapata hizo dili.”

 “Basi sawa, dada yangu,” Kinabo alisema huku akitoa pochi mfukoni. Akachomoa noti na kumkabidhi yule dada. “Nawe utanunua hata dagaa basi.”

 “Asante sana. Ubarikiwe,” alijibu huku akipokea pesa. “Kama wote waliokuja leo kumuulizia wangekuwa na moyo kama wako, ningenunua hata dera jipya.”

 Ikunji alicheka. Akamuuliza, “Ametembelewa na watu wengi sana leo eenh?”

 “We mtu wa tatu leo.”

“Basi nitakuja tena kwenye saa mbili usiku.”

 “Mmh! Sidhani kama atakuwa amerudi, maana nilimsikia akimwambia huyo aliyekuwa anaongea naye kwenye simu, kuwa kwenye saa moja jioni atakuwa pale King Garden.”

 “Oh, King Garden eeh! Asante. Nitajaribu kumcheki pale.”

 Kinabo aliaga na kutoka nje.

Ilikwishatimu saa kumi na mbili na nusu. Safari ya King Garden ikaanza.

***

Nyakanga alimgeukia mhudumu akiwa ametabasamu. Akasema, “Hakuna tatizo. Tuko pamoja.”

“Sawa. Samahani kwa usumbufu,” mhudumu alimjibu Nyakanga ilhali macho yameganda kwa Ikunji. “Nilidhani kuna shida.”

“Kuwa na amani tu,” Nyakanga alisisitiza.

Mhudumu alipowapa mgongo, Nyakanga alisogea na kukitoa Kitabu cha Wageni kwenye mfuko. Akaondoka nacho bila kuongeza neno. Akaelekea kule kule kwenye kona ya kwenda msalani, alikoelekea mwanzo.

Ikunji alibaki ameduwaa asijue cha kufanya. Japo kitabu amekiona, lakini hakuwa na ujanja wa kufanya lolote. Hakujua amfuate au amsubiri. Alijilazimisha kutafakari na kufanya maamuzi ya haraka. Kichwa kiligoma. Kwa mara ya nyingine, alihisi kama kichwani mwake mna kitu basi ni majivu ya takataka, na si ubongo.

Alibaki kitini ameganda akisubiri hatma yake. Alisubiri kwa takribani dakika kumi bila kumwona Nyakanga akirejea.

Amekwenda kunichomea? aliwaza akiyakumbuka maneno aliyonasihiwa na mzee Kizamba.

Kwenye kona aliyoelekea Nyakanga, pilika za watu ziliongezeka maradufu. Walionekana wakienda kuchungulia na kurudi mezani mwao. Ikunji hakuelewa kinachoendelea. Haikuchukua muda, taharuki ikaongezeka. Idadi ya watu walioonekana kuvutiwa na kinachoendelea huko konani. Baadhi walikwenda huko na kuchukua muda bila kuonekana wakirudi.

“Kuna nini kule?” mteja mmoja aliyekuwa jirani na meza aliyoketi Ikunji, alimsaili bwana mmoja aliyetokea kule konani.

“Aah hata sikusogea karibu. Kuna mtu sijui anaumwa kifafa, naona kama amepoteza fahamu hivi.”

Baada ya Ikunji kuona wahudumu nao wakielekea huko kwenye kona, naye alisimama. Akavaa kapelo yake kichwani, na kuelekea eneo la tukio akiwa amesahau hata kuondoka na vitu vya Nyakanga.

Nyuma ya jengo la mgahawa, karibu na jengo la milango minne ya vyoo; viwili vya wanawake, viwili vya wanaume, ndipo ulipoanzia umati wa watu. Watu walikuwa wamesimama kwa mduara wakijaribu kumchungulia aliyekuwa amelala katikati yao.

“Pigeni simu polisi haraka,” kijana mmoja alisema huku akichomoka katikati ya watu.

Ikunji alipenya hadi katikati ya kadamnasi. Alichoshuhudia, kwanza alihisi yu ndotoni. Macho yake yalishuhudia picha mbaya kabisa. Mwili wa Nyakanga, ukiwa umetapakaa damu na mchanga, ulilala chali. Chini ya kidevu, palionekana kuchimbwa vilivyo na kitu cha moto. Ikunji alishindwa kujizuia, akajichomoa katikati ya kundi watu na kwenda kusimama nyuma yao akiwa amejitwisha mikono kichwani.

“Uwiii…siamini…huyo mama anafanya kazi pale Nyati Hotel,” mwanamke mmoja, aliyeshuhudia mwili wa Nyakanga, alisema huku akiwa amehamanika.

Mhudumu aliyewafuata mezani akina Nyakanga, akitaka kujua kama kuna tatizo, naye alijichomoa katikati ya kundi lililozunguka mwili wa Nyakanga. Akasimama mbele kidogo akiwa amempa mgongo Ikunji. Akasema, “Ni mimi ndiye nilimpokea huyu mama, akaniagiza maji. Wakati namfungulia maji, akapokea simu kama nusu dakika tu, kisha akaikata. Nilipoondoka, akainuka akifuata uelekeo huu. Baada ya muda kuna jamaa alifika na kuketi mezani kwake, lakini inaonekana hawakuwa na maelewano mazuri.”

Ikunji alibaki ameganda nyuma ya mhudumu anayezungumza. Alikwishanusa harufu ya hatari. Akaanza kutafuta upenyo wa kutoweka.

“Huyo jamaa unamkumbuka ukimwona?” mtu mmoja wa makamo, mnene – mrefu, aliyeonekana kama kiongozi wa mgahawa ule, alimsaili yule mhudumu.

Ikunji aliganda vile vile, akipiga mahesabu ya kutoweka eneo lile. Akaishindilia vizuri kapelo yake kichwani, huku akihakikisha hakutani uso kwa uso na mhudumu yule.

“Ni mweupe, ndevu zake zimeenea mashavuni. Na kichwani pia ana nywele nyingi kiasi,” mhudumu alijibu, akiwa anageuka huku na kule. “Na niliongea naye kabisa, nikamuuliza kama kuna tatizo. Lakini huyu mama akasem…”

“Basi atakuwepo maeneo haya haya. Hawachezagi mbali wakishajua wameua,” mtu mwingine, aliyesimama nyuma ya Ikunji alipaza sauti.

“Hilo nalo neno,” yule mhudumu alijibu huku akigeuka nyuma kumtazama aliyetoa rai ile. Hapo ndipo akakutanisha macho na Ikunji.

Idadi ya watu ilikwishaongezeka maradufu. Wateja pamoja na majirani wa eneo lile walifurika kutazama tukio la mauaji.

“Hapa kwanza watu wazuiliwe kujaa, ili waliopo watambuliwe,” Ikunji alisema huku akigeuka nyuma. Alijaribu kuuhadaa umma, hususani mhudumu aliyekutanisha naye macho, kana kwamba naye anaunga mkono hoja iliyotolewa nyuma yake.

“Tukaanzie kule mezani,” yule mtu wa makamo alisema, huku akimpiga begani mhudumu ili waondoke.

Ikunji aliporudisha uso wake mbele baada ya kauli hiyo mpya, mhudumu alikuwa amekwishageukia mbele. Yule mhudumu akiwa kama anayetafuta usahihi wa taarifa zinazojichakata kichwani mwake, aligeuka tena nyuma kumtazama Ikunji. Haraka, Ikunji aligeukia pembeni akiendelea kujadiliana huku na kule kuhusu tukio hilo.

Yule mtu wa makamo, alimvuta mkono mhudumu aliyekuwa anataka kumtazama Ikunji usoni. Wakaondoka na kuelekea mezani alipokuwa ameketi Nyakanga. Kitendo bila kuchelwa, Ikunji alipenya katikakati ya makundi mawili matatu ya watu, ili atokee nyuma ya vyoo na kutokomea kusikojulikana. Japo hakuwa mwenyeji kiasi cha kutosha kuielewa njia hiyo ya nyuma, lakini aliona ni aula kupita huko kuliko kurudia njia ya mbele, ambako anayetafutwa ni yeye.

Akiwa hatua kadhaa mbele, macho yake yalipiga moja kwa moja chini, pembezoni mwa watu, na kukiona Kitabu cha Wageni alichokuwa nacho Nyakanga. Hakuamini kama ni chenyewe. Akasimama na kutuliza macho ili kuthibitisha.

Ndicho chenyewe.

Kimefikaje, hakujua. Lakini ndicho.

Imekuwaje kikaenea vumbi, hakujua. Lakini ni chenyewe.

Kitabu cha Wageni. White Rose Hotel.

Alisimama akitafakari endapo akichukue au aendelee na safari. Watu waliendelea kumiminika eneo lile.

*****************

*****************

Ikunji aliwasili maeneo ya D&G Hotel kwa usafiri wa pikipiki, akiwa amekishika kwa kukikunja, Kitabu cha Wageni mkononi. Alishukia mbali kidogo na hoteli. Hakutaka dereva wa bodaboda ajue anakoelekea. Tayari alikwishaanza kuishi kwa machale.

 Baada ya bodaboda kuondoka, Ikunji alitoa simu kumpigia mzee Kizamba ili kumpasha habari. Simu iliita muda mrefu bila kupokelewa. Akairudisha mfukoni na kuanza kutembea kuelekea hotelini.

 Akiwa tayari amekaribia kufika, aliwaona watu wawili wakitokea hotelini; mmoja mrefu, mwingine mfupi. Giza lilikwishaanza kuingia, hivyo hakuweza kuwatambua kwa haraka. Alipunguza mwendo ili kuchungua nyendo zao. Kengele ya hatari ilimgongea kichwani baada ya kugundua jambo moja lisilo la kawaida. Alimwona mmoja kati ya watu wale wawili, akiwa amebeba mkoba wa rangi ya udongo. Akautambua. Ni mkoba wake.

 Kuutambua mkoba wake, kukamwongezea umakini juu ya watu wale. Haikumchukua muda mrefu zaidi, akawakumbuka. Alipata kuwaona kupitia tundu la funguo, kwenye mlango wa chumba, alikohifadhiwa na Nyakanga.

 “Mungu wangu,” alijisemea, na kuanza kurudi nyuma kwa indhari bila kuamsha nadhari zao.

 Akiwa amemakinika kufuatilia wanachojadiliana, ingawaje kwa umbali aliokuwepo asingeliweza kuwasikia, simu yake ikaita. Akaitoa na kuitazama. Ni mzee Kizamba.

 “Uncle,” alipokea simu kwa maombolezo. “Nimekwisha! Nyakanga ameuawa.”

 “Nyakanga?”

 “Yule mama, niliyekwambia naenda kuonana naye.”

 “Oh! Imekuwaje?”

 Ikunji alimsimulia kuanzia alipofika pale Golden King na kuonana na Nyakanga, mpaka alipokuja kushuhudia maiti yake.

 “Una hakika hakuna aliyekuona naye hapo mezani?”

 Ikunji alimsimulia kisa cha yule mhudumu aliyempokea, na namna alivyoonesha walakini baada ya Nyakanga kumfumania akichakua mfuko wake, na dalili alizoonesha walipokutanisha macho baada ya Nyakanga kuuawa.

 “Huo tayari ni utata,” mzee Kizamba alisema kwa sauti ya chini. “Kwa hiyo huyo Nyakanga alikitoa wapi hicho Kitabu, na alikuwa anakipeleka wapi?”

 “Maiti haizungumzi, uncle,” Ikunji alijibu, huku akiendelea kuwatazama afande Kisigino na mwenziye, wakiingia kwenye teksi iliyokuwa imeegesha nje ya hoteli.

 “Nilikwambia lakini, pua yangu ni ndefu inawezanusa hatari iliyo mbali,” mzee Kizamba alijigamba, “huyo mama nilimtilia shaka tangu mwanzo, ndo maana nikakushauri usitembee na mkoba.”

 “Na ushauri huo hadi sasa umeshanigharimu pakubwa vile vile.”

 “Kivipi?”

Ikunji aliendelea kuitazama teksi iliyowabeba akina Kisigino ikitoweka. Kwa namna fulani alihisi teksi hiyo ndiyo ile ile iliyombeba siku aliyowasili jijini Arusha. Hakuweza kusoma namba kwa sababu ya giza kuyafunika macho yake.

“Niliuacha mkoba hotelini, na hivi ninavyoongea tayari uko mikononi mwa polisi.”

“We!”

Ikunji alimweleza namna alivyofika hapo hotelini na kuwaona akina afande Kisigino wakitoka na mkoba wake.

“Sasa hiyo imekwishakuwa dhahama kubwa. Ondoka haraka hapo. Ikiwezekana na hicho kitabu kitupe. Usitembee na kidhibiti.”

Ikunji alikata simu na kuiweka mfukoni. Kinyume na ushauri wa mzee Kizamba, aliamua kuvuka barabara na kuelekea hotelini. Alitembea kwa tahadhari na umakini mkubwa hadi ndani.

Mapokezi hapakuwa na watu zaidi ya mhudumu aliyekuwa ameketi nyuma ya kaunta. Mhudumu alisimama baada ya kumwona Ikunji. Akatungua ufunguo wa chumba chake na kumkabidhi.

“Ahsante,” Ikunji alisema huku akiipokea funguo na kuondoka.

Ikunji hakuonesha wasiwasi wala mashaka. Alitembea taratibu kuelekea kwenye ngazi. Alipopanda ngazi ya kwanza tu, mhudumu akanyanyua simu na kubofya namba alizoachiwa. Akawapigia.

Baada ya kumaliza kupanda ngazi za mwanzo, ule utulivu aliouonesha ukayeyuka. Ngazi zilizofuata alipanda kwa mwendo wa mbwa mwizi. Alikuwa na hakika lazima afande Kisigino ameacha maelekezo ya kupigiwa simu kama alivyofanya Nyati Inn Hotel.

Alifungua mlango wa chumba chake na kuingia. Cha kwanza alitazama ukutani alipoacha mkoba wake. Haukuwepo. Akajihakikishia kuwa ndiyo ule aliouona mikononi mwa polisi. Hakufanya ajizi, moja kwa moja akaenda kitandani na kutandua shuka. Akaligeuza godoro chini–juu.

Kabla hajatoka kwenda kwa Nyakanga, alilichana godoro katikati kwa kisu, kisha akatoa dhahabu zote kwenye mkoba na kuzificha humo. Hivyo, hakuwa na wasiwasi na mkoba waliochukua. Hofu yake ilikuwa ni endapo walipekua mpaka kwenye godoro na kuzikuta.

Alipopenyeza mkono katikati ya godoro huku mishipa ya kichwa ikiwa imemsimama, aliganda kwa sekunde kadhaa macho yakiwa yamemtoka. Akashusha pumzi nzito na kusimama. Akaweka mikono kiuononi, akiangaza huku na kule kutafuta mfuko. Akauona mfuko mweusi aliopewa dukani ili kubebea nguo, alizokwenda kununua kwa ajili ya kubadilisha. Ulikuwa kwenye kijipipa cha taka. Akauchukua na kuufuta vumbi. Akarudi nao kitandani. Akaingiza tena mkono kwenye godoro na kuzitoa dhahabu zote taratibu. Akaziweka kwenye mfuko, kisha akatoka.

Alikutanisha macho na mhudumu, mara baada ya kushuka ngazi ya mwisho. Mhudumu alionekana kujawa na taharuki.

“Umeshawapigia simu?” Ikunji alisema huku akimsogelea mhudumu kaunta. “Sasa wapigie tena, waambie nimekwishaongea na bosi wao. Warudishe haraka mkoba wangu. Nawasubiri hapo nje.”

Mhudumu alipoteza mhimili wa kujiamini. Macho yalimtoka mithili ya mtoto aliyekamatwa akilamba sukari. Hakuelewa Ikunji amejuaje kuwa ni polisi ndiyo wamechukua mkoba wake, na waliacha maagizo ya kupigiwa simu.

“Na kama kuna chochote kitakuwa kimepotea, nitaanza na wewe uliyeruhusu wahuni kuingia chumbani mwangu.”

“Lakini bosi hilo si kosa langu,” mhudumu alijitetea huku akimtazama Ikunji kwa huruma, “nisingeweza kuwazuia polisi kufanya kazi yao.”

“Walikuwa na search warranty? Waliambatana na mjumbe wa serikali za mitaa? Una dakika moja ya kuhakikisha wanarudi na kila kilichomo kwenye mkoba.”

Ikunji alihakikisha anamtetemesha mhudumu vilivyo hata asipate wazo la kuomba msaada kwa watu ili kumzuia asitoke mpaka polisi watakapofika. Alimjengea mazingira kuwa amekwishajua kuwa anatafutwa, lakini haogopi, na anawasubiri kwa hamu hao wanaomtafuta. Alijua tayari mhudumu amekwishampigia simu afande Kisigino, hivyo, kwa muda aliotumia chumbani pamoja na hapo kaunta, hakupaswa kuzidisha japo dakika moja mbele. Akatoka nje akitembea kwa ujasiri ilhali moyoni akiungua kwa hofu na woga.

*****MDUNDO WA MUZIKI UMEBADILIKA GHAFLA, INGAWAJE MNENGUAJI ANABAKI YULEYULE, BWANA IKUNJI. NAAM, NDIYE ALIYEONEKANA NA NYAKANGA MUDA MFUPI KABLA HAJAUAWA. ANAYO KESI YA KUJIBU.

Je, ni nani aliyemuua Nyakanga? Na Je, hicho kitabu amekiacha makusudi au alikidondosha?

WAKIMKOSA IKUNJI KWA SUDI CHOTARA, WATAMNASA KWA NYAKANGA. HACHOMOKI.

Ungekuwa wewe ungefanyaje? Ungeendelea na uchunguzi wa kifo cha Sudi Chotara au ungeanza rasmi uchunguzi wa kifo cha Nyakanga? Wakati huo usijisahaulishe yanayoendelea baina ya Leila na Seba.




Ikunji alihakikisha anamtetemesha mhudumu vilivyo hata asipate wazo la kuomba msaada kwa watu ili kumzuia asitoke mpaka polisi watakapofika. Alimjengea mazingira kuwa amekwishajua kuwa anatafutwa, lakini haogopi, na anawasubiri kwa hamu hao wanaomtafuta. Alijua tayari mhudumu amekwishampigia simu afande Kisigino, hivyo, kwa muda aliotumia chumbani pamoja na hapo kaunta, hakupaswa kuzidisha japo dakika moja mbele. Akatoka nje akitembea kwa ujasiri ilhali moyoni akiungua kwa hofu na woga.

Afande Kisigino na mwenziye walirejea hotelini dakika tatu baada ya Ikunji kutoweka. Simulizi waliyoikuta kwa mhudumu iliwaacha midomo wazi.

***

Kiasi cha saa tatu asubuhi, kama ilivyo ada, Kinabo aliwasili Kituo cha Polisi. Siku hiyo aliamka akiwa amejawa na hamu na ghamu ya kulifumbua fumbo lililofumbwa kiustadi juu ya kadhia ya mauaji ya Sudi Chotara. Baada ya uchunguzi wake wa kina kubaini mambo kadha wa kadhalika, sasa alijiandaa kuanza kuunganisha nukta. Shauku yake ilianza kuingiwa na walakini, baada ya kukuta gari ya OC-CID Dotto Hamduni, ikiwa imeegeshwa nje ya kituo. Alikuwa na miadi naye asubuhi hiyo, na alipotazama saa yake, aligundua kuwa yuko nyuma ya muda kwa takribani saa nzima.

 Kinabo alipita kaunta kwa kasi ya mshale. Alipoingia ofisini, koplo Kisesa alimlaki kwa salamu iliyoambatana na saluti. “Jambo afande.”

 Kinabo alipokea salamu kwa ukakamavu. Kisha akauliza, “Mzee Hamduni hajaniulizia?”

 “Hata dakika haijaisha ametoka kuniagiza nikupigie kujua uliko.”

 Kinabo alikwenda kufungua kabati. Akatoa mafaili kadhaa, akayatawanya mezani. Akachukua mawili na kutoka nayo bila kuongeza neno. Alipoufikia mlango akagonga na kuingia. Alimkuta mzee Hamduni ameketi mezani.

Unadhifu pamoja na mazoezi ya mara kwa mara, vilimfanya mzee Hamduni aonekane kijana kuliko uhalisia. Shati la mikono mirefu la rangi ya bluu bahari, liliukamata vema mwili wake. Pete ya fedha katika kidole cha katika pamoja na saa ya Omax vilipendezesha mikono yake.

Dalili kwamba hakuwa na chembe ya furaha usoni, hazikumshitua Kinabo. Kilichomshitua ni kumkuta akiwa pamoja na afande Kisigino, aliyekuwa ameketi mbele ya meza. Tangu alipogundua kuna mkono wa afande Kisigino katika kesi anayoichunguza, alianza kumtazama kwa jicho la wasiwasi. Aliwasabahi na kuketi.

 Afande Kisigino alivaa shati kubwa jeupe, la mikono mirefu, na kulichomekea kwenye suruali nyeusi, kiasi cha kufanya litune kwa kujaa upepo kila alipopulizwa na feni, na kutengeneza taswira ya njiwa manga wa kwenye mashamba ya mpunga. Mustachi wake mpana ulijitengeneza mfano wa kiota cha ndege chini ya pua yake. Alitulia kwenye kiti kana kwamba hajamwona mtu aliyeingia.

 “Naomba kujua ulipofikia na uchunguzi wako wa,” afande Hamduni alisema huku akiperuzi shajara yake, “kesi ya Sudi Chotara.”

 “Ndiyo, afande,” Kinabo aliitika huku akimkabidhi mafaili mezani kwake.

 Afande Hamduni aliyapokea na kuyaweka juu ya makabrasha mengine yaliyokuwa yamezagaa mezani kwake. Macho yake madogo yaliyozungukwa na nyusi zenye mvi, na kukingingwa na miwani ya duara, yalibaki yamemganda kwa Kinabo.

 “Ni nani aliyemuua Sudi?”

 “Tuendelea na upelelezi, afande,” Kinabo alijibu.

 “Sababu yoyote ya mauaji?”

 “Ndo tunaendelea na ukusanyaji wa ushahidi, afande.”

 “Sasa umenipa hii takataka ya nini hapa?” alisema huku akiyatupia macho mafaili mezani kwake. “Three days huna ulichofanya. Kwa hiyo mpaka sasa umegundua nini?”

 “Nimebaini mambo machache, afande. Kwanza, inaonekana meneja wa hoteli ana maslahi na tukio hili. Anajaribu kuficha ukweli mwingi. Kwa mfano, Sudi Chotara alifariki muda mrefu tofauti na maelezo yake.”

 “Kivipi?”

 “Anadai kwamba, alipofika chumbani mara baada ya kuitwa na mhudumu wake aliyeona damu ikitokea humo, alimkuta tayari amekufa. Anasema alijua amekufa baada ya kuona hapumui, macho yakiwa yamedidimia ndani, na ngozi ikiwa imechujuka na kuwa ya zambarau. Hizo ni sifa za mtu aliyekufa kwa zaidi ya saa moja. Kama ni kweli angekuwa amefika chumbani, wakati ule ule damu ikiwa inatiririka, kwa maana ya muda aliotoka kuuawa, basi asingemkuta amebadilika kwa haraka namna ile.”

 “Kwa hiyo kama alikufa zaidi ya saa moja moja nyuma, inaondoa ukweli kuwa amekufa?”

 “Inaondoa uhusika wa kijana anayetajwa kupanga chumba hicho. Kwa sababu kwa muda huo, alikuwa bado hajafika hotelini. Na kama kijana huyo hahusiki, basi kuna uwezekano kuna kitu kinafichwa ili kumlinda mwuaji.”

 “Kwenye maelezo yako unamtaja zaidi meneja, vipi kuhusu mhudumu aliyempa chumba huyo kijana?”

 “Mhudumu anasema, baada ya kuletewa taarifa kuwa kuna damu inavuja chumbani, alimfuata meneja ofisini kwake kumjulisha. Lakini meneja anadai mhudumu hakumfuata ofisini, bali alimpigia simu kumjulisha jambo hilo. Mbali ya mkanganyiko huo, pia nilibaini kuwa meneja hufanya mchezo wa kuingiza baadhi ya wateja hotelini, kwa kutumia mlango wa faragha. Na siku ya tukio kuna mteja aliingia kwa njia hiyo. Yumkini ni Sudi Chotara au muuaji wake. Yote haya meneja pamoja na huyo mhudumu walinificha mpaka nilipoyapata kwingine ndipo wakakiri.”

 “Umeweza kupata japo mwonekano wa huyo kijana aliyepanga hicho chumba?”

 Kana kwamba alijiandaa kwa swali hilo, Kinabo alimgeukia Kisigino na kumuuliza, “Ile picha yake unayo hapo?”

 Afande Kisigino alipigwa na mshituko. Hakutegemea swali hilo. Kila jibu alilotaka kulitoa, alihisi likikinzana na swali.

 Afande Hamduni alipiga meza kwa ghadhabu. Akakaripia, “Nijibu mimi, sajenti. Picha uikose wewe mpelelezi, then awe nayo mtu mwingine?”

 “Samahani afande,” Kinabo alijibu, akirudisha uso wake mbele. “Kisigino amekwishafika maeneo kadhaa kumtafuta huyo kijana, akiwa na picha yake.”

 Afande Hamduni alihangaika kumeza mate kama aliyekabwa na mkate. Alionesha dalili ya hofu kuliko ghadhabu. Akasimama na kwenda kusimama dirishani akitazama nje kwa dakika nzima. Ukimya uliotanda ni zaidi ya ule wa makaburini wakati wa usiku.

 “Kazi imekushinda, sajenti,” afande Hamdani alisema, akirudisha macho yake kwa Kinabo.

Kinabo alibaki kimya.

Afande Hamduni akaendelea, “Ulitakiwa kuchukua likizo yako lini?”

 “Tangu mwezi uliopita, afande.”

 “Vema. Kesho utaanza likizo yako. Kuanzia hivi sasa mpelelezi wa kesi hii atakuwa Sajenti Kisigino,” afande Hamduni alisema na kurudi kuketi.

 “Afande, naomba muda kidogo – japo wiki moja – nimalizie uchunguzi. Nina imani utafurahia matokeo. Mahali nilipofikia ni kuanza tu kuunganisha matukio niliyokwisha kuyachunguza.”

  “Ungestahili kuondolewa kwenye kesi hii kwa kutokuwa na weledi wa kutosha. Nimekusaidia tu kukuondoa kwa likizo,” afande Hamduni alisema huku akigongagonga meza kwa kalamu. “Bila shaka huo uchunguzi uliokwishafanya, umeujumuisha kwenye hii report yako, right?” 

 “Ndiyo, afande.”

 “Then, Sajenti Kisigino ataanzia ulipoishia. Nakutakia likizo njema.”

*****

Leila aliamka mapema sana siku hiyo, lakini hakutoka kitandani. Si tu kwa sababu hakuwa na mahali pa kwenda, bali pia uchovu na mawazo vilimdhoofisha mwili. Kila mara alishika simu kuangalia endapo Ikunji amemjibu meseji zake, lakini alichokutana nacho, kilimrudisha kitandani kufuta machozi kwa shuka. Kila alipofikiria kadhia ya mauaji ya Sudi Chotara na kitendo cha Ikunji kutokupatikana alijihisi kuchanganyikiwa.

 Akiwa katikati ya mtanziko wa fikra, hatimaye simu yake iliita. Kwa wahka na mshawasha, alijiinua kitandani. Aliikwapua simu na kuitazama. Namba mpya. Akapokea.

 “Hellow!”

 “Unaendeleaje sweetheart?” Sauti ya Vicky Mshana.

 “Oh, niko poa mummy,” alijibu huku akishusha pumzi taratibu. “Mbona namba mpya?”

 “Simu yangu imeishiwa chaji. Hii ni namba ya bodaboda wangu. Uko home?”

 “Ndiyo.”

 “Haya naja.”

 Vicky na Leila kwa mara ya kwanza walikutana kwenye kampuni ya Crops Investment Limited, Vicky akiwa na mwaka mmoja kazini ilhali Leila akiwa na siku moja. Japo hawakufanana majukumu yao ya kikazi, lakini walishikana urafiki. Siku Leila alipopewa barua ya kusimamishwa kazi, Vicky hakuwepo ofisini. Hivyo, hakujua lolote hadi Leila alipompigia kumjulisha.

 Kiasi cha dakika ishirini na tano tangu wamalize kuzungumza kwenye simu, Vicky akawasili. Leila alikuwa sebuleni akimalizia kunywa chai na vipande vya mihogo. Vicky anazo sifa zote za kushiriki mashindano ya ulimbwende na akashinda; mwembamba asiyechusha, ngozi ya ung’avu yenye isiyohitaji vipodozi aghali zaidi ya poda na wanja wa kuchonga; uchaguzi wa mavazi yake haukumtofautisha na wanamitindo wa Uajemi; alivalia gauni fupi la kitenge, lililoanzia juu ya magoti na kumwacha wazi sehemu kubwa ya mikono yake. Miguuni alivaa viatu virefu vya mikanda, vyenye rangi ya damu ya mzee; mkoba wake ulioshabihiana rangi na viatu, aliuning’iniza kwenye kiwiko cha mkono wa kushoto.

 Leila aliketi sakafuni huku akiegemea sofa kwa mgongo. Vicky alijitupia sofani, akipachika mguu mmoja juu ya mwingine. Baada ya kusabahiana na kupeana michapo ya hapa na pale, Leila alianza kusimulia mkasa uliopelekea Sebastian kumsimamisha kazi.

 “Nisikilize Leila,” Vicky alisema kwa sauti kavu iliyojaa ushawishi. “Nilichogundua, Seba anakupenda. Ila anachojaribu ni kukutikisa tu ili akupate kirahisi. Acha mapepe. Usipozichanga vizuri karata zako atakusumbua.”

 “Ah. Sina haja tena ya kujikombakomba. Nachotaka wanilipe tu mshahara wangu wa mwezi huu niliofanya kazi, tuachane.”

 “Hapo utaharibu kila kitu. Ukianza mambo ya kudai sijui–haki yako, watajua sasa umeingia vitani. Watakushughulikia kama hawana akili nzuri. Si unawajua lakini?”

 “Sasa nifanye nini? Hali yangu ni mbaya mno. Nahitaji pesa inisaidie japo kujipanga kwa mwezi huu tu. Kama nilivyokwambia, Ikunji hayupo na hapatikani hata kwenye simu.”

 “Sasa hata ukipewa hiyo salary ndo itatosha chakula, nauli, bills, na kila kitu? Ikunji asiporudi kwa wakati utaishije? We jaribu tena kumtafuta Seba.”

 “Niongee naye nini?”

 “Sema naye kiutu-uzima. Hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Mweleze kuwa hukumkimbia makusudi…akiona umejishusha kwake na umwa–”

“No,” Leila alidakia. “Nimeshaghairi. Kutembea na Seba kisa kazi ni kujidhalilisha. Acha abaki na pesa zake nami nibaki na mwili wangu.”

“Kwani alikwambia anataka mwili wako abaki nao kwake? Utakwenda nao na kurudi nao,” Vicky alitania. Wakacheka. “Kama umeamua hivyo, it’s okay, lakini bado sikushauri kwenda kudai pesa za mshahara kwa sasa. Jaribu kumtafuta kiupole, usidai mshahara, bali fanya kumlilia hali kirafiki tu. Jifanye unamuomba akukopeshe japo pesa kidogo…pamoja na yote hayo, Seba ana huruma sana. Atakukopesha na hatokuja kukudai tena.”

Ni kweli Seba ana huruma, Leila aliwaza, hawezi akashindwa kunikopesha pesa, lakini ni yeye ndiye aliyenisimamisha kazi bila kunipa mshahara ili nisalimu amri. Hivyo, ili akubali kunikopesha ni lazima ahitaji penzi kama dhamana ya mkopo.

 “Ah, ndo yaleyale tu,” Leila alijibu baada ya kujifikiria. “Nitakuwa nimeruka majivu na kukanyaga moto.”

 “Hivi shoga’angu, we ni mtakatifu kiasi cha kukataa kuchepuka? Kumbuka, Seba angekufaa sana katika kipindi hiki cha matatizo ye–”

 Kabla Vicky hajamalizia sentensi yake, mlango wa mbele uligongwa. Wakapiga kimya wakiutazama mlango kwa pamoja. 

 “Mungu wangu,” Leila alinong’ona huku hofu iliyomjaa moyoni ikidhihiri machoni. “Mama mwenye nyumba.”

 “Atafanya nini?” Vicky alijibu huku macho yamemtoka. “Leo tutaumana naye meno hapa.”

Mlango ukagongwa tena.

“We! Huyo mama ni mtata dunia nzima.”

 “Tulia. Akijaribu nikuoneshe sinema ya bure,” Vicky alijibu na kuinuka. Akajongea hadi mlangoni na kuufungua.

 Aliingia msichana mnene, mweusi. Si mrefu sana, wala si mfupi. Macho yake manene ya duara, aliyahifadhi nyuma ya miwani myeupe. Alivaa suruali ya rangi ya bluu, pamoja na blauzi nyeupe yenye picha ya minazi kifuani.

Leila alishusha pumzi nzito alipomwona akiingia. Akalaza kichwa chake kwenye sofa kama aliyetua mzigo mzito.

 Vicky naye alifanya mshangao baada ya kumwona. Akasema huku ametabasamu, “Kumbe ni wewe mtu mnene.”

 Wakacheka kwa pamoja.

 “Karibu Mwantumu,” Leila alimkaribisha. “Tulijua ni mama mwenye nyumba. Ananifanya niishi kama digidigi.”

 “Kwani alirudi tena tangu mlivyoachana jana?” Mwantumu aliuliza.

 Leila na Mwantumu wanatokea wilayani Muheza, jijini Tanga. Wakiwa Tanga, hawakuwahi kuwa na ukaribu hadi walipokutana chuoni, jijini Dar es Salaam. Hapo ndipo waliposhikana urafiki. Baada ya kumaliza masomo, Mwantumu alipata kazi bandarini na Leila akapata kazi Crops Investment Limited. Urafiki wa Leila na Mwantumu ukamjumuisha na Vicky.

 “Hajarudi mpaka leo.”

 “Kuna kitu kinaendelea. Kwa jinsi mlivyotoleana maneno, lazima angeshakurudia hapa kwa tambo zote.”

 “Keti basi, mbona wima?” Vicky alimwambia Mwantumu.

 “Jifunze kushusha sauti mtoto wa kike,” Mwantumu alimwambia Vicky. “Yaani niko nje kabisa huko nakusikia na hiyo sauti yako ya zege unavyomshawishi mwenziyo kuchepuka.”

 “My God,” Vicky alimaka. “Kumbe tulikuwa tunasikika hadi nje.”

 “Vuta picha angekuwa ndo Ikunji amefika hapo mlangoni na kukusikia,” Mwantumu aliendelea kumshushua. “Enhe kisa cha kushawishiana michepuko?”

 Leila akaachia ucheko hafifu.

 “Ah, bwana eeh, nani asiyechepuka duniani hapa?” Vicky alihoji.

 “Nyie danganyaneni tu,” Mwantumu alisema akiwatembezea macho. “Mmeshaandaa mbeleko ya kumbebea Ikunji pindi atakapojua?”

 “Atajuaje?” Vicky alidakia. “Kama hadi sasa hajulikani alipo na wala simu haipatikani. Je, kama ndo amekimbia familia hivyo? Leila awe amekosa mwana na maji ya moto!”

 “Kumbuka Ikunji alikubali kuacha kazi kwa ajili ya Seba huyohuyo,” Mwantumu alisema, akimtazama Leila. “Leo akisikia kumbe unatoka naye, unajua ataumia kwa kiwango gani?”

 “Kwa hiyo, hapo issue siyo kuchepuka, bali ni kuhakikisha hagundui kuwa amechepuka,” Vicky alisema, “Waswahili wanasema, usichokijua hakitokuumiza.”

 Mwantumu alimgeukia Leila. Akasema, “Seba hana mapenzi na wewe hata kidogo. Anachotaka ni kumkomoa tu Ikunji. Yuko radhi hata kumdhuru ili tu kukupata wewe. Hata umpe nini, atakutafuna kisha akuteme kama Big G.”

 “Na hilo ndo tatizo la wanaume wengi. Kama amedhamiria kumkomoa mumeo, basi hata umwambie mfanye siri, yeye atafanya kila hali ilimradi taarifa zimfikie ndipo lengo lake litimie,” Leila aliyasadiki maneno ya Mwantumu.

 “Kwani hata zikimfikia si unakataa tu? Au utabaki na alama?” Vicky alisema na kuangua ucheko. “Mwili ni mali yako. Una hiyari ya kuutumia utakavyo kwa maslahi yako.”

 “Mwanaume mkware, utampa chochote lakini atakavyokutema utadhani hakuona lolote,” Mwantumu alisisitiza. “Waswahili husema, mwenye haiba ya paka halei panya. Seba ni paka tu.”

 “Tena paka shume,” Vicky alisisitiza.

 Wote wakaangua cheko.

 “Yaani umeshamgeuka mara hii?” Leila alimwambia Vicky kwa mshangao.

 “Kumbe nifanye nini sasa?”

 “Jamani me hata sikai,” Vicky alisema na kusimama. “Nilitaka tu kukuona. Now, ndo nakwenda job. Tumecheleweshewa salary mwezi huu. Lakini leo tukilipwa nitakutumia kidogo shosti kikusukume.”

 Wakaagana. Mwantumu akaondoka.

***

Asubuhi ilimkuta Ikunji katikati ya mashuka ya Kisumu Lodge, iliyopo Usa River, Makao Makuu ya Wilaya ya Arumeru. Alipata chumba hapo Kisumu, majira ya saa sita usiku, akitokea Arusha mjini. Kilichomkimbiza Arusha usiku wa jana yake, ni hatari ya kukamatwa endapo ungefanyika msako kwenye nyumba za kulala wageni. Lakini pia changamoto za usafiri nyakati za usiku, ndizo zilimfanya ashuke Arumeru kwa minajili ya kupumzika kabla ya kuanza safari siku hiyo iliyofuata.

Kufikia saa tano asubuhi, baada ya kujiswafi mwili na kupata staftahi, alikuwa tayari kutoka kwa ajili ya kuendelea na safari ya jijini Dar es Salaam. Lakini, kabla hajaondoka aliamua kuweka sawia baadhi ya vitu alivyodhani vingelimfaa katika uchunguzi wake.

Alitoa karatasi aliyoandika namba za teksi iliyombeba siku ya tukio. Akaiweka mezani. Akawasha kamera ya simu na kuipiga picha. Alifanya hivyo, akiamini njia hiyo ni salama zaidi kutunza namba kuliko kuendelea kubeba karatasi inayoweza kuchanika au kupotea muda wowote. Alipomaliza, akazima simu na kuchomoa kadi yenye namba aliyosajiliwa na Nyakanga, na kupachika kadi yenye namba yake. Hofu yake ikawa ni endapo namba hiyo bado inafuatiliwa mtandaoni, ingeweza kuonesha mahali alipo. Lakini kwa kuwa alikuwa njia moja kuondoka eneo hilo, na ilikuwa ni lazima afanye vile kwa muda ule, akaona haidhuru hata kama wanaomfuatilia watajua kuwa yuko pale. Alipowasha simu, haraka alifungua sehemu ya meseji, na kuutafuta ujumbe aliotumiwa kuhusu mkewe. Akanakili pembeni namba ya simu iliyomtumia ujumbe ule. Kisha, aliingia kuangalia baadhi ya jumbe zilizokuwa zikiendelea kuingia kwa wingi muda huo.

Ujumbe uliomvutia zaidi, ni wa fedha. Alitumiwa na namba mpya, ambayo hakuitambua. Kilichofanya ajue kuwa fedha hizo ni mshahara wake, ni kima alichotumiwa. Kima hicho ndicho alipwacho kwa mwezi. Kutumiwa pesa katika nyakati alizozihitaji zaidi kama zile, kulimfariji na kumwongezea nguvu. Hakufanya haraka kubadili kadi ya simu, kwani ilimlazimu kwanza akatoe fedha hizo ndipo abadili kadi ya simu. Akakusanya kila kilicho chake, tayari kuianza safari.

Akiwa amekwishafika mlangoni ili kuondoka, akakumbuka jambo muhimu. Hakuwa amechukua Kitabu cha Wageni cha White Rose Hotel. Akarudi hadi kitandani. Akabinua godoro na kukichukua. Alikificha huko ili kupunguza hatari ya kukamatwa nacho endapo angevamiwa ghafla chumbani. Akiwa amekishika mkononi, mshawasha wa kukiperuzi ukamjia. Akakifunua angali amesimama. Joto lilianza kumpanda na macho yakimtoka mara baada ya kuufikia ukurasa wa mwisho. Hakuona jina lake. Alirudia kutazama na kusoma taarifa zote kwa umakini. Ukurasa wa mwisho kuandikwa kwenye kitabu ulijaa taarifa za watu wengine. Alipotazama tarehe kuandikwa sehemu ya juu ya ukurasa huo, akabaini kuwa ukurasa huo ulijazwa siku moja nyuma, kabla hajafika Arusha na kuchukua chumba hapo hotelini.

Alipotuliza macho kwenye pachipachi za ukurasa, akagundua ukurasa uliokuwa unafuata umechanwa na kuondolewa kwenye kitabu. Na ndiyo ukurasa ule ule aliojazaa taarifa zake.

Kwa vyovyote vile, aliyemuua Nyakanga ndiye aliyeondoka na ukurasa ule ili kuendelea kuficha ushahidi, Ikunji aliwaza.

Akiwa anaendelea kuyatafutia majibu maswali yaliyoshonana kichwani mwake, mlango wa chumbani ukagongwa. Akaugeukia na kuukodolea kana kwamba anasubiri umjulishe aliyegonga ni nani.

Mungu wangu! Nani tena? alijiuliza.

Kama aliyenusa hatari ya ghafla, aliingiza haraka mkono mfukoni, akachomoa simu yake na kuikodolea macho. Hakuwahi kuchomoa kadi ya simu yenye namba yake.

“Ah! Nimekwisha,” alijisemea.

Kabla hajajua cha kufanya, mlango uligongwa tena. Awamu hii kwa nguvu zaidi.


MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog