Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

SARAFU YA GAVANA

  

MTUNZI: WILBARD MAKENE


[Takadam]

Boniphace alikunja mkono na kisha kuuelekeza upande wa

kushoto wa kichwa. Spika ya simu alilengesha vizuri sikioni. Alimeza

mate kulainisha koromeo lake, kisha akasema, “Ameshafika ila amekuta

mlango wa mbele umetiwa kufuli. Amegonga kengele bila mafanikio.”

Kabla hajajibiwa simuni, Boniphace alichungulia nje ili kuhakikisha

hakuna anayemsikia wala kumwona. Alipojiridhisha, akarudisha uso ndani.

Makwapa yake yalilowa jasho kwa hofu, moyo ulimwenda mbio, miguu

iliyokuwa imeachia breki za gari ilikuwa ikitetemeka kama mcheza kiduku.

Kiyoyozi cha gari hakikufua dafu kuzituliza tezi za jasho kutoa taka.

Boniphace alijitahidi kuficha kilichoendelea ndani ya akili yake, lakini mwili

ulimsaliti; kila kiungo cha mwili, kuanzia utosini hadi kidole cha mwisho

cha mguuni, vilidhihirisha wazi kile kilichokuwa kikiendelea kichwani

mwake.

“Sina hakika na usalama eneo hili,” Boniphace alindelea kuongea

huku akimwangalia bosi wake, Gavana wa Benki Kuu ya Weusi Kusini.

Boniphace alikuwa amemaliza kumshusha kwenye gari Gavana

aliyekuwa ametoka kazini.

Kiutaratibu na kulingana na mafunzo aliyopewa, Boniphace

alitakiwa kuhakikisha bosi wake anaingia ndani akiwa salama kabla ya yeye

kuondoa gari. Aliendelea kumtazama Gavana akitembea hadi alipoufikia

mlango. Gavana aligonga kengele mara kadhaa bila kufunguliwa.

Boniphace, akiwa yu-ndani ya gari na simu sikioni, aliendelea

kuzungumza, “Mimi mwenyewe sina hakika na usalama wangu mahali

hapa.”

Mtu aliyekuwa akizungumza naye simuni akajibu, “Acha woga,

endelea kufanya kazi. Kila kitu kitakuwa sawia. Maelekezo mengine

nitakupa baadaye.”

Simu ikakatwa.

Boniphace alitoa mkono sikioni, na kuuelekeza mfuko wake wa

mbele. Aliiachia simu itulie iserereke kuelekea ukingo wa mfuko.

Baada ya Boniphace kuuondoa mkono wenye simu sikioni, na

kuiweka simu kwenye mfuko wa suruali yake, alirudisha macho kule

mlangoni alikosimama Gavana. Bado mlango ulikuwa haujafunguliwa.

Hali hiyo ilimtatiza Boniphace, hakujua kama ni hali ya kawaida tu hivyo

anaweza kuondoka. Ni hali tatanishi hivyo anapaswa kwenda kutoa msaada.

Laiti angelijua, asingeliendelea kupoteza muda kwenye gari.

....

[Baada ya TAKADAMU hiyo...sasa tuanze SURA YA KWANZA]

Boniphace ni kijana wa makamo, mcheshi na asiyependa makuu.

Alikulia katika familia duni kijijini Iyovu, mkoani Iringa. Alipata elimu ya

msingi, na kuhitimu elimu ya sekondari kwa kupata daraja la tatu. Alimaliza elimu ya sekondari miaka ya tisini. Ni katika kipindi

hicho, Serikali ilikuwa na shule chache. Ufaulu daraja la kwanza na la pili ndiyo uliopewa kipaumbele. Hilo lilisababisha ashindwe kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita. Hata hivyo, aliweza kujiunga na shule za maarifa ya jamii. Alichukua fani ya udereva. Alipohitimu aliajiriwa serikalini. Akiwa kazini, alijiendeleza katika

fani hiyo ya udereva. Akapata daraja la umahiri na kuajiriwa na Benki Kuu. Tofauti na vijana wenziye wengi hapo kazini, walioendekeza anasa,

Boniphace alikuwa na nidhamu ya pesa. Kiasi kidogo alichopata kwa

mshahara, alikitumia kwa mahitaji ya msingi, pamoja na kuwatunza wazazi wake. Mara zote alizowatumia pesa wazazi wake, alitumia muda huo pia

kuwajulia hali. Wazazi walimpenda sana na kumwombea dua kila uchao.

Mbali na kuwasaidia wazazi wake, pia alikuwa akiwasomesha wadogo zake. Majukumu mazito ya kifamilia yalimfanya kuwa makini

na mwenye nidhamu kwenye maisha. Hakutaka kabisa kuwa sababu ya

kuwaangamiza wazazi na nduguze. Lakini kuna mzigo wa siri, alioubeba

kwa muda mrefu, akihofia kuutoa kwa kuchelea kuangamia yeye na familia

yake, ulimsumbua sana kichwa kiasi cha kuanza kukata tamaa.

Alifanikisha kuificha siri hiyo kama mwanaume kubeba ujauzito. Tofauti ni kwamba, ujauzito unaonekana kwa wote lakini siri haionekani kwa macho, na mara nyingi, ujazito huleta neema ufikiapo tamati, walakini siri huleta madhara

kwa mtunzaji endapo itatoka nje.

Mara chache, Boniphace alipojaribu kuwashirikisha watu wake wa karibu, aliishia kupigiwa simu zikitoa onyo kwake kuacha mara moja tabia hiyo. Ujanja wake wa mjini pamoja na mwili wake uliojengeka kimazoezi havikumfanya athubutu kukabiliana na genge hilo lililomsakama. Nguvu

zake binafsi dhidi ya genge hilo ilikuwa ni sawa na tone la maji katika bahari.

*****

*****

Annakova Boris alikuwa amejilaza kizembe kwenye kochi wakati

simu ya mezani ilipoita. Alijiinua na kwenda kupokea. 

Hallo,” alisema baada ya kuinua mkonga na kuubandika sikioni.

“Naweza kuzungumza na Anna?” Sauti kavu ilijibu upande wa pili

wa simu.

“Ndiye anayeongea hivi sasa,” Anna alisema kwa utulivu. “Nani

mwenzangu?”

“Good,” sauti ile upande wa pili ilisikika tena. “Napiga simu toka

Ikulu ya Kremlim!”

Kimya kikatanda.

Kupokea simu kutoka Ikulu ya Kremlim lilikuwa jambo zito sana.

Anna alijua wazi kuna tatizo sehemu. 

Kabla hajajua ajibu nini, sauti ile ikaendelea, “Unahitajika Kremlim haraka iwezekavyo, Okay? Sihitaji

kurudia mara mbili kwamba ni haraka!”

Simu ikakatwa.

Anna alirudisha mkonga wa simu mahala pake. Akarudi kochini na

kujibwaga. Haikuchukua hata dakika moja, akasimama tena na kuelekea

bafuni kwa ajili ya kujisafi mwili, tayari kuanza safari ya Kremlim.

Annakova Boris, almaarufu kama “Mwanamke wa Chuma” ni mwanamke shupavu asiyemithilika. Alipigana Vita Vikuu vya Pili vya

dunia, baadaye alikwenda kutumikia jeshi kama shushushu. Aliaminika na

viongozi wengi kwa namna alivyokuwa tayari muda wote kutekeleza amri kutoka kwa wakuu. Katika mapambano ya Vita Vikuu vya Pili ya dunia. Alipoteza figo moja ili kuokoa maisha ya askari mwenzake aliyejeruhiwa vibaya na figo zake zote kuharibika. Serikali ya Urusi ilimpeleka nchini Cuba kusomea masomo ya Kemia, na hatimaye kuhitimu shahada ya

uzamivu. Huko alijifunza masuala muhimu ya uchanganyaji kemikali kwa matumizi mbalimbali ya kiusalama. Baadaye alirudi Urusi kuendelea na kazi zake za ushushushu jeshini.

Akiwa bafuni anaendelea kujisafi mwili, Anna alisikia sauti toka

sebuleni. Mlango wa sebuleni uligongwa. Alitupa dodoki chini na kufungua maji yatiririke kwenye mwili wake kuondoa povu. Kisha alijifunga taulo

haraka na kukimbilia sebuleni.

Alipofika sebuleni, alisikia tena mlango ukigongwa.

“Nakuja,” alijibu huku akikimbia chumbani kujisitiri mwili na

kujiweka tayari.

Kwa haraka alivalia fulana nyeupe na jinzi ya bluu. Kisha, alianza

kupiga hatua kuelekea sebuleni. Alipoufikia mlango, kabla hajafungua wala

kumfahamu mtu aliyekuwa mlangoni, akasema, “Samahani kwa kukuweka

mlangoni muda mrefu!”

Hakujibiwa.

Hilo lilimshitua kidogo. Hivyo, kabla hajafungua mlango, alihoji,

“Nani mwenzangu?”

Kimya!

“Hallo!” aliita tena.

Kimya tena.

Mlango ulikuwa na tundu lililowezesha kuchungulia nje. Alisogeza

kichwa chake. Kisha, kupitia tundu hilo, alichungulia nje.

Mlio mkubwa ulisikika mlangoni. Vipande vya mbao vilivyokuwa

vimezunguka sehemu ya tundu la kuangalizia nje vilisambaa na kuacha

tundu kubwa. Kwa bahati, Anna alikwishagundua hila za mvamizi wake, na akawahi kuruka pembeni. Kisha, kwa umakini mkubwa, aliamka na

kusogea kuelekea ulipokuwa mlango huku akiwa na bastola mkononi.

Alipoufika mlango na kuangalia nje kupitia tundu kubwa

lililotengenezwa, aliliona gari aina na Mercedes Benz lililokuwa sehemu ya maegesho–upande wa pili wa barabara, likirudi nyuma na kuondoka kwa kasi.

Ni akina nani hawa na kwa nini wadhamirie kunidhuru? Anna

aliwaza, huku akijaribu kulihusianisha tukio hilo na ile simu toka Kremlim

aliyotoka kupokea muda mfupi nyuma.

*****

*****

Baxter aliinuka toka kitini. Akajongea kuelekea meza iliyokuwa

pembeni. Meza ilikuwa ndogo, tofauti na iliyotumika kufanya

mazungumzo. Alipofika, akafungua chupa ya chai na kisha kuiinamisha.

Maji moto yalitiririka katika kikombe kidogo kilichokuwa chini ya chupa. Kilipojaa, akarudisha chupa wima na kuifunga. Akaweka kijiko kimoja cha

kahawa na kingine cha sukari, akakoroga na kisha akabeba kikombe kidogo mkono wa kulia na kijiko mkono wa kushoto. Alipofika alipokuwa amekaa

rafikiye wa siku nyingi, Alister, alisimama. Akashusha kikombe cha chai mezani, mbele ya Alister, huku akisema, “Karibu sana.”

Baxter alijongea sehemu yake ya kuketi na kisha kuketi huku akimwangalia Alister. “Benki ya Ulaya imepata ombi kutoka kwa Rais Bonge wa Jamhuri

ya Weusi Kusini,” Baxter alinza mazungumzo.

“Mhhh..” Alister aliitikia.

“Anahitaji mkopo wa dola za Marekani bilioni moja ili kuongeza nguvu kwenye vita.”

“Sijasikia kama ana vita!” Alister alibisha.

“Si vita yake; ni ile anayowasaidia nchi ya Matoke, Kaskazini-

Magharibi mwa nchi yake,” Baxter aliongeza, “Endapo akishinda, Bongo atakuwa

amejiongezea ushawishi katika kanda ya maziwa makuu na hata nchi za

Kusini mwa Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ujumla.”

Baxter aliendelea, “Kuna uasi umezuka nchini Matoke, na hivyo

Bonge anajitahidi kadri iwezekanavyo kushirikiana na Rais wa Matoke, kuzima uasi. Lakini ajenda kubwa ya Bonge ni kuleta amani eneo la maziwa makuu, kwa namna hiyo atakuwa ameongeza ushawishi wake.”

“Unadhani mkopo utalipika?” Alister aliuliza. “Na kama utalipika, tunatumia mbinu gani kuwaeleza bodi ya wakurugenzi kwamba, mkopo kwa Rais Bonge utalipika?” Alister alisisitiza.

“Hilo niachie mimi,” Baxter alijigamba.

*** Kabla hatujayajua ya Boniphace na Gavana wake, yakaibuka ya Annakova na wavamizi wasiojulikana. Na sasa, akina Baxter wamekuja na "mchongo" wa Rais Bingo kutaka kutoa "mpunga" kwa jamaa yake wa nchi ya Matoke. Stori zote hizi zinatakiwa kukutana ili kutupa jibu la maana ya SARAFU YA GAVANA. Uko tayari? 



Gavana Bongo aliposhuka kwenye gari, alielekea mlangoni ili

aingie ndani. Alisimama na kulegeza tai shingoni. Alinyoosha mkono wake wa kulia, akitanguliza kidole gumba. Kidole kilikutana na kitufe cha kengele mlangoni.

Gavana Bongo aliendelea kupiga kengele kwa muda mlangoni

kwake bila kujibiwa.

Gavana alikuwa amepiga marufuku upigaji wa

honi nyumbani kwake, laa sivyo Boniphace aliwaza kupiga honi ya

gari. Wasiwasi ulianza kumtafuna.

“Wamekwenda wapi hawa?” Gavana Bongo alijisaili mwenyewe.

“wamelala!”

Maswali yake hayakumpa majibu ya kwa nini hajafunguliwa

mlango muda wote huo.

Boniphace alisogeza gari mbele kidogo, karibu na mlangoni alikosimama Gavana. Simu bado ilikuwa sikioni.

Gavana aligeuka kumtazama Boniphace. Akasema, “Boni,

nahisi kuna kitu hakipo sawa. Haijawahi kutokea hata mara moja watu wote nyumbani kwangu wakatoka bila kunijulisha. Hata mlinzi

naye haonekani.”

Boniphace alimwangalia Gavana Bongo huku paji lake la uso likiwa limekunja mistari midogomidogo.

Gavana aliposogea karibu zaidi, alisikia Boniphace akiongea simuni.

Boniphace alimtazama Gavana bila kumjibu. Bado alishughulishwa na mtu aliyekuwa akiongea naye kwenye simu. 

Gavana alimsikia Boniphace akilalama: “…unaniingiza katika hatari

pia…”

Mwendokasi wa upumuaji wa Gavana uliongezeka;

Makwapa yalipokea jasho jembamba na kufanya shati lake lionekane kama limemwagikiwa matone ya mvua. Gavana hakuwa na hakika; hakuwa na hakika na mawasiliano aliyokuwa akifanya Boniphace. Hakuwa na hakika kama mawasiliano hayo yalikuwa salama na yenye heri. Pamoja na kuyasikia maneno ya Boniphace, lakini hakutaka

kudadisi zaidi. Aliheshimu mawasiliano yake kwa sababu ni jambo binafsi.

Gavana alipolifikia gari, Boniphace alikuwa tayari ameshakata simu. Alijaribu kuonesha tabasamu, lakini zaidi ya mwanya katikati

ya meno yake ya njano, hakuna chembe ya furaha iliyoonekana.

Mikono ya Gavana iligusa sehemu ya mlango wa gari na

kuvifanya vidole vyake vinene, vilivyoakisi unene wake kuonekana

vyema. Kitambi kiligusa sehemu ya mlango wa gari katika jitihada za

kumsogelea karibu zaidi Boniphace.

Boniphace alifungua mlango wa gari ili ashuke kumsikiliza Gavana. Lakini kabla hajashusha mguu chini, walisikia mngurumo wa gari likiwajia usawa wao. Wote wakageuka kwa pamoja.

*****

*****

Annakova alishuka kwenye gari mara baada ya kuwasili katika

viwanja vya Kremlin. Idara ya mapokezi ilimlaki kwa taadhima.

Taratibu za kawaida za kiusalama zikazingatiwa kabla ya kumpeleka

alikohitajika.

Urusi ilikuwa chini ya Rais Baranova. Rais wa kwanza mwanamke

kutawala nchi hiyo ya Kisoshalisti. Ilikuwa ni fahari kwa Annakova

kufanya kazi chini ya mwanamama huyu.

“Karibu, Anna,” Rais Baranova, aliyekuwa ameketi nyuma ya

meza pana, alimlaki Annakova mara baada ya kufunguliwa mlango

na kuingia.

“Ahsante Mhe. Rais,” Annakova alijibu huku akijongea karibu

na meza ya Rais.

Kwa kutumia mkono wake wa kulia, Rais Branova alimwashiria Annakova aketi kwenye kiti mbele ya meza.

Alipoinua mikono yake kumuonyesha sehemu ya kukaa, wembamba wa mikono ya Rais Baranova ulionekana dhahiri shahiri. Alikuwa ni mwanamke mwembamba mwenye nyama kiasi,

kitu kilichofanya ukubwa wa macho yake meusi kujidhihiri katika wajihi wake.

Baada ya Annakova kuketi. Walisabahiana, na kufuatiwa na

porojo za hapa na pale, kabla Rais Baranova hajafunua mdomo

kusema: “Nimesikia mengi kukuhusu, Anna.”

“Ndiyo mkuu!”

“Napokea taarifa zako karibu kila siku,” Rais Baranova aliendelea,

“Hata jaribio la kutaka kukushambulia asubuhi hii pia nimelisikia.”

Annakova alitikisa kichwa huku akimwangalia Rais Baranova.

Alielewa fika kuwa, kwa nafasi yake ya urais, taarifa nyeti kama ya

tukio lake zinafika kwenye meza yake kila baada ya masaa au dakika kadhaa.

“Ni kweli mkuu,” Annakova alisadiki maneno ya Rais.

Baranova lilikuwa jina lake la ukoo. Jina la kwanza aliitwa

Svetlana—Svetlana Baranova. Rais Baranova ndilo lililowakaa Warusi

wengi kichwani kwa sababu kuu mbili. Kwanza, kasumba ya mfumo dume ilikuwa bado ikirindima miongoni mwa Warusi wengi. Kwa

hiyo walipenda kumtambua Rais kwa jina lake la ukoo, iliwafanya

wajivunie ukoo wa Baranova wenye historia ya wanasiasa wengi. Pili,

Baranova lilikuwa rahisi kimatamshi. Baranova lilikolea.

“Vyema, wanafanya haya yote kwa sababu wanakuogopa.

Wewe ni mwamba, Annakova. Umeendelea kuwadhirishia kuwa bado

wameshindwa kukudhuru.”

Annakova hakujibu, ila sentensi za Rais Baranova zilimtafakarisha

kwa uchache.

Alijikuta akiuliza, “Mhe. Rais ni akina nani hao?”

Annakova alikuwa na uhakika, Rais ana taarifa muhimu za makundi mbalimbali ya kihalifu na kigaidi. Kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu, taarifa za namna hii ni muhimu ili kumuwezesha kufanya

maamuzi sahihi.

Rais Baranova alimwangalia Annakova kwa sekunde kadhaa,

kisha akafafanua, “Unachopaswa kufahamu kwa sasa ni kwamba,

kuna watu wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa

utawala wangu unashindwa.”

“Kivipi?”

“Wanajua kuwa kuna kazi nataka kukupa unisaidie,” akasita

kidogo, kisha akaendelea “si mimi, kuna kazi nahitaji uisaidie nchi

yako. Ni kazi itakayotuletea heshima kubwa kama Warusi. Itatufanya

tutembee kifua mbele. Lakini kuna watu wanataka kuzuia hili

lisitokee.”

Aliinuka alipoketi, kisha alipiga hatua chache kutoka alipokuwa

na kusogea karibu zaidi na alipoketi Annakova. Aliketi kiti alichokaa

Annakova, na kisha kumnongoneza sikioni, “

“Sina hakika kama wahuni hawa walikudukua kwenye simu au

la…” Rais alikatisha sentensi ili kuangalia mapokeo ya Annakova,

kisha akaendelea, “Au wamepata taarifa toka ndani ya ofisi yangu.”

Anna alitulia. Aliruhusu alichokisikia kichakatwe ndani ya ubongo wake.

“Sina muda mrefu wa kuongea nawe,” Rais aliongea huku

akinyoosha mkono kumkabidhi Annakova kabrasha alilokuwa nalo

mkononi, “Humu kuna kila kitu utakachohitaji, maelezo na taarifa

zote unazohitaji. Utatoa mrejesho kwangu tu. Maofisa wachache

waaminifu wa kufanya nao kazi wameorodheshwa.”

Annakova alipokea kabrasha.

Kabla Annakova hajasema lolote, Rais alimwambia, “Tafadhali

ondoka, muda wako umeisha!”

*****

*****

Kamati ya mikopo ilikuwa ikiendelea na mkutano.

“Hawa si ni wajamaa? Mnawapaje hela wajamaa?” Mjumbe wa

kwanza wa bodi, alionesha wasiwasi wake huku akifunua mikono

yake.

Wajumbe wa Benki ya Ulaya walikuwa wamegawanyika

kiitikadi. Hii ilitokana na ukweli kuwa baadhi ya nchi ndani ya umoja

huo zilikuwa na itikadi iliyofuata misingi sawa na ya kijamaa- serikali

zao ndizo zilimiliki njia kuu za uchumi za nchi husika. Nchi nyingine

ndani ya umoja, zilikuwa zikifata mfumo wa kipebari, ambapo njia

kuu za uzalishaji zilikuwa mikononi mwa sekta binafsi. Bodi ilikuwa

na mchanganyiko wa watu wenye historia na itikadi tofauti. Kila mmoja aliamini katika itikadi aliyokulia. Historia zao ziliwaweka

katika majaribu.

“Kwa sababu gani? Kwani wajamaa hawatengenezi faida?

Viwanda vyao havizalishi? Uchumi wao haukui?” Mjumbe wa pili

alidakia.

“Kwa sababu tu njia zao za uzalishaji zinamilikiwa na serikali,

haina maana ya kuwa serikali zao ni mbumbumbu na haziwezi tengeneza uchumi bora,” mjumbe wa pili alikazia.

“Kweli, takwimu zinaonyesha kuwa wanaweza fanya vyema tu kama walivyo mabepari. Tofauti ni kuwa, mabepari uchumi unakuwa mikononi mwa wachache; maskini wakitamalaki. Hawa wenzetu wajamaa, wana tabia ya kubeba kada ya chini kabisa ya kipato ili

kwenda nayo sambamba,” aliongeza mjumbe wa tatu.

“Na kwa namna hii wanaepuka matabaka makubwa ya

kijamii; wanaziba tofauti za vipato kati ya wananchi wao; na kwa

kiasi kikubwa inawasaidia kudhibiti usalama wa nchi zao. Wote tunafahamu, uzalishaji wa makundi makubwa ya maskini na matajiri kumepelekea mapinduzi kwenye nchi nyingi.”

“Kwa hiyo hoja kwamba hawawezi kulipa mkopo kwa sababu

ya ujamaa wao ni hoja mfu,” aliongeza mjumbe wa pili.

Mjumbe wa kwanza alionekana akiumauma meno bila kusema

neno . Alijitahidi kujidhibiti, ilimradi asiwakere wajumbe wenzake. Kisha kwa sauti ya chini, yenye sikitiko akasema, “Jamani

kumbukeni, hawa Weusi Kusini si ndiyo juzi tu wamefutiwa madeni

hawa? mmekwishasahau mara hii?”

“Wana rasilimali au hawana?” Mjumbe wa pili aliuliza.

“Wanazo,” Mjumbe wa tatu alidakia.

“Sasa kwa nini tunabishana?” Mjumbe wa pili aliuliza.

Majibizano yaliendelea kwa muda.

Baxter alikuwa pembeni kama mjumbe. Alisikisikiliza kwa

makini, hoja baada ya hoja. Alijipanga!

*****

*****

Masikio mapana ya Gavana yalikaa mkao wa kusikiliza zaidi, mithili ya ungo wa televisheni unavyotegwa kupata

mawimbi . Macho yake makubwa yakatoka pima. Pua yake yenye matundu makubwa, ilitoa hewa nje kwa nguvu.

Alinyoosha kiganja kumwashiria Boniphace asiongee huku akimwambia kwa sauti ya tahadhari, “Hebu sikiliza kwa makini.” 

Alifanya kusikilia sauti iliyotambuliwa na kumbukumbu ya ubongo

wake. Haikuwa sauti mpya kwake. Hata hivyo hakuitambua mara moja, kumbukumbu zilikuwa

zikimijia na kupotea. Alimuangalia Boniphace usoni na kisha

alimwambia, “Unasikia hiyo sauti.”

“Ipi?”

“Hiyo inayotokea nyuma ya nyumba….”

“Sijasikia,” Boniphace alijibu huku akitikisa kichwa.

“Hebu nijongee…”

Gavana alindoka kuelekea nyuma ya nyumba. Alitembea kwa tahadhari kubwa. Mwili wake mpana ulionekana

kupinda kiasi. Ulitengeneza umbo kama la mwanariadha anayejiandaa kuanza mashindano kipenga kitakapopulizwa.

*****

*****

Asubuhi na mapema Annakova aliondoka nyumbani. Alikwenda

mpaka eneo aliloelekezwa baada ya kusoma kilichokuwemo kwenye kabrasha.

Kabrasha alilokabidhiwa lilikuwa na taarifa zote muhimu. Lilikuwa na picha ya mtu anayekwenda kukutana naye na misheni zote muhimu.

*****

*****

Annakova alipofika kituo cha basi, alikaa na kusubiri kwa muda.

Mara alimuona mtu wa makamo akija kwa mbali akiwa mbele yake. Alionekana kuwa mzee wa takribani miaka hamsini. Kichwani

alivaa kofia nyeusi ya mviringo iliyofunika sehemu kubwa ya kichwa chake ili kujikinga na baridi. Mwilini alikuwa na koti refu la baridi

lililofika usawa wa viatu vyake vya ngozi. Suruali yake ya kitambaa

ilifichwa na koti refu. Alipozidi kusogea Annakova alibaini makunyazi machache katika sura yake. Kilichoufanya sura yake itishe kiasi,

yalikuwa makovu mawili ya visu. Moja likionekana juu ya paji la uso

na jingine likionekana kwenye kidevu.

Annakova aliamka toka kitini na kisha kumfuata. Alikuwa na uhakika ndiye picha yake iliyokuwa kwenye kabrasha. Bila

kusemezana maneno mzee aligeuza njia na kuanza kurudi alikotoka.

Sasa walikuwa wakiongozana na Annakova pamoja.

Annakova alimsalimu, “Mzee, habari.”

“Usiongee na mimi.”

“Hata salamu?”

“Ni asubuhi, muda wa tafakari-kimya kikuu.”

Mzee aliongea

huku macho akiwa ameyakaza mbele. Hakumuangalia machoni.

Alikaza uso kama gumegume.

Dhamira yake kuu ilikuwa ni kuchukua tahadhari; kuchukua

tahadhari toka kwa watu asiowafahamu. Katika kazi yake alitambua:

mazoea yana tabu. Kutoa nafasi ya mtu kukuzoea huku ukiwa huna hakika na historia yake wala mipaka yake ya mazoea kuna madhara makubwa.

Kipindi cha nyuma , kwenye kazi kama hii, alifanya kumzoea

binti aliyekabidhiwa kumficha mpaka kwa wahusika wasafirishaji.

Aliponea chupuchupu ya kifo baada ya binti kutaka kumchoma

koromeo, ilivyo bahati, aliinama ghafla, kisu kikachoma kidevu

badala ya koromeo. Binti alikuwa na maagizo maalum ya kummaliza

alikuwa ni adui aliyepandikizwa. Hakutaka kurudia makosa; alijiepusha kuongea na Annakova huku akichukua tahadhari kubwa.

Annakova aliamua kukaa kimya na kuendelea kumfuata mzee.

Walifika eneo la wazi.

Mzee akamuangalia Annakova, na kisha akageuza kichwa

kuangalia gari lenye muundo wa daladala-hiace lililokuwa limeegeshwa

pembeni. Eneo lilikuwa kimya. Lisilo na watu. Ni kiwanda cha zamani kilichotelekezwa baada ya kushindwa kutengeneza faida

kwenye uchumi wa kibepari.

Ndani ya gari walishuka vijana wawili warefu waliovaa miwani.

Mzee alianza kuondoka.

Annakova alijongea kuelekea wapokuwa vijana.

“Habari zenu,” aliwasalimia.

Hawakumjibu, badala yake walimwonyesha kiti kwenye gari.

Aliingia na kukaa.

Kisha mmojawapo wa vijana alipanda mbele na kuketi kiti cha

dereva. Wa pili alikaa na Annakova kiti kimoja, wote wakiangalia

mbele.

Bila matarajio, Annakova alipokea kipigo cha kiwiko cha

shingo. Nuru ilipotea mbele ya macho yake. Ghafla alihisi usingizi mzito. Alikuwa anapoteza fahamu.

*****

*****

Baxter alisimama bila ruhusa. Utaratibu uliwataka wajumbe

wote kusimama baada ya kuruhusiwa na mwenyekiti wa kikao.

Wajumbe wote walikuwa kimya.

Baxter alifanya kitenda cha namna hii nadra na kama alikuwa na

hoja ya msingi ya kuongea. Ni mjumbe aliyeheshimika na wajumbe

wenzake kwa mawazo yake machache; yenye uzito na ambayo

mara nyingi yaliwatoa wajumbe kwenye mtanzuko. Baxter alikuwa

na nguvu ya kubadili ulekeo wa mijadala iliyosababisha mitanziko

ndani ya bodi.

Urefu wake ulimfanya awaangalie wajumbe wote kana kwamba

wamepiga magoti huku yeye akisimama. Alitua miwani yake, na kisha

mkono wake ukaelekea kwenye pua yake yake ili kuondoa alama

zilizowekwa na miwani. Kisha alishika nywele zake na kuzirudisha

nyuma.

“Ndugu zangu wajumbe,” alianza kuongea, akiruhusu meno

yake yaliyofubaa kwa kahawa kali kuonekana, “tunapoteza muda

bure wakati jibu tayari tunalo.”

Kisha alimgeukia mjumbe namba mbili, “Kinachotakiwa hapa

ni kuona kama tunakubaliana kwenye jibu husika ama la… hilo

ndilo suala la msingi.”

“Unamaanisha?” Mjumbe namba moja alihoji.

“Yawezekana Weusi Kusini wasiwe na pesa ya kulipa lakini

wana almasi, dhahabu, gesi asilia, urani, zebaki, cobati, makaa ya

mawe, na mbuga za wanyama!”

Kisha alinyoosha kidole chake cha shahada, na kujigusa

kichwani, karibu kabisa na sikio lake huku akisema, “Tumia akili

ndogo tu, utaona kuwa kuna manufaa makubwa kuwapa kuliko

kuwanyima mkopo.”

Baadhi ya wajumbe walielewa, huku wengine wakibaki kukunja

nyuso; nyuso zenye maswali, ziliakisi wasiwasi.



MWISHO






0 comments:

Post a Comment

Blog