Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

JINSI JINI LILIVYONITUMA KUMWAGA DAMU

  

MTUNZI: JUMA HIZA


Ulikuwa ni usiku wa manane, usiku ambao nilijikuta nipo makaburini peke yangu huku nikiwa sina nguo hata moja. Nilikuwa uchi wa mnyama. Niliitazama maiti iliyokuwa mbele yangu juu ya kaburi moja ambalo sikuweza kulifahamu kuwa lilikuwa ni kaburi la nani. Kutokana na uchakavu wake, yawezekana muhusika alizikwa miaka mingi iliyopita.

Maiti ile Ilikuwa ni ya mwanamke nisiyemfahamu aliyeonekana kujeruhiwa vibaya kwa kukatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili wake. Ile damu iliyokuwa ikiendelea kuchirizika mahali pale iliweza kunithibitishia kuwa muuaji aliyefanya mauaji yale bila shaka aliyafanya muda mfupi uliopita.

Hofu kubwa ikaanza kunitawala moyoni na kila nilipojaribu kuyakwepesha macho yangu yasiendelee kuishuhudia maiti ile nilishangaa kuona macho yakiendelea kuishangaa tu bila kutoka.

Ghafla! Mingurumo pamoja na sauti za ajabu zikaanza kusikika mahali pale. Sikujua sauti zile za kutisha zilikuwa zinatokea wapi ila kwa uwoga wangu nikajikuta nimeketi chini huku nikijaribu kuyaziba masikio yangu yasiendelee kuzisikia sauti zile za ajabu.

Lahaula!

Haikuwa kama nilivyotegemea, badala ya masikio yangu kuyazuia yasiweze kuzisikia sauti zile za ajabu sasa ikawa kama ndiyo nimezikaribisha sauti zile walau ziweze kusema chochote.

“Haaa! Haaa! Haaa! Haaa!” nilizisikia sauti za watu zikicheka huku zikiwa zinajirudiarudia masikioni mwangu.

Ghafla! Nikaanza kukisikia kishindo cha mtu ambaye alikuwa akitembea kuja mahali nilipokuwepo. Nilipogeuka kumtazama huyo mtu aliyekuwa ananifuata ajabu sikumuona. Nikazidi kuogopa mno! Kijasho chembamba kikaanza kunitoka huku nikitetemeka kwa hofu.

Sikujua nilikuwa mahali pale kwa lengo gani na ni kwa nini nilikuwa nikiishuhudia ile maiti ikiwa juu ya kaburi huku ikiwa inachirizika damu.

Wakati nilipokuwa nikishangaa kuwepo mahali pale hasa katika nyakati kama zile za usiku mara nikamuona kwa mbali mwanamke mmoja ambaye alikuwa akinifuata huku akiwa amevaa sanda iliyokuwa imeufunika mwili wake kasoro sehemu ya uso wake tu. Alitisha mno kutazama hasa katika giza lile.

Nikatamani kukimbia lakini kila nilipojaribu kufanya hivyo nilishindwa. Aliponikaribia, aliniita jina langu kisha akaanza kucheka huku sauti ya kicheko chake ikijirudiarudia kama sauti ya mwang’wi.

“Wewe ni nani na umenijuaje jina langu?” nilimuuliza kwa sauti ya hofu huku nikimsihi asinidhuru.

“Haaa! Haaa! Haaa! Haaa! naitwa Mulhaty,” alijitambulisha kisha akaunyoosha mkono wake wa kulia kuielekezea ile maiti iliyokuwa imelala juu ya kaburi halafu akawa kama kuna maneno anayanena kwa sauti ya chini ambayo sikuweza kujua ni maneno gani.

Niliushuhudia mwanga mkali ukitokea katika mkono wa Mulhaty ukielekea mahali maiti ilipo. Ni kama kitendo cha dakika mbili nikashuhudia maajabu mengine tena. Ile maiti ikatoweka juu ya lile kaburi.

Sikumbuki ni nini kilitokea ila nilijikuta nikitokea sehemu nyingine kabisa tofauti na pale makaburini tulipokuwa. Nikabaki kinywa wazi huku nikiendelea kuishangaa miujiza ambayo katika maisha yangu sikuwahi kuwaza au kutegemea kama kuna siku nitakuja kuishuhudia kwa macho yangu.

Nilimtazama Mulhaty kwa wakati huo alikuwa katika hali ya utulivu kabisa.

“Uliwahi kuua katika maisha yako?” aliniuliza Mulhaty.

“Hapana,” nilimjibu kwa sauti iliyojaa hofu.

“Yasri nataka umwage damu.”

“Nimwage damu?”

“Ndiyo nataka nikutumie katika kumwaga damu.”

“Kumwaga damu ya nani?”

“Damu ya binadamu, nataka uue Yasri.”

“Niue?”

“Ndiyo.”

“Sasa nimuue nani, amefanya kosa gani na kwa nini nimuue?” nilijiuliza kimoyomoyo lakini kabla sijaunyanyua mdomo wangu ili kusudi nimuulize ghafla nikapokea majibu ya maswali yangu yote. Ni kama vile alikuwa ndani ya nafsi yangu kwa wakati ule.

“Nitakurudisha duniani,” aliniambia Mulhaty maneno ambayo yakanifanya nijiulize kuwa kwa wakati ule nilikuwa wapi hasa.

Sikutaka kusubiri jibu la kimiujiza tena kutoka kwake safari hii nikaamua kumuuliza.

“Kwani hapa tupo wapi?” nilimuuliza huku moyo wangu ukiwa umetawaliwa na hofu.

“Hapa ni kuzimu,” alinijibu kisha akacheka kama ilivyokuwa kawaida yake.

Nilizidi kuogopa mno hapa ni baada ya kufahamu kuwa pale nilipokuwa ni kuzimu.

****

Niliamka katika ndoto ile ya kutisha. Nilikuwa nikitetemeka huku kijasho chembamba kikinitoka. Nikaitazama saa ya ukutani ilikuwa ni majira ya saa kumi usiku. Sikutaka kuamini kile nilichokuwa nakishuhudia kule makaburini kuwa ilikuwa ni ndoto, ndoto ya kutisha.

Wakati nilipokuwa nikiendelea kuitafakari ile ndoto ya ajabu na juu ya yule mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Mulhaty ghafla! simu yangu ikawa inaita. Haraka niliipokea hapa ni baada ya kuliona jina la mpenzi wangu aliyejulikana kwa a Salha bint Hassan ambaye nilimuandika kwa jina la ‘My futer wife’ (Mke wangu wa baadae).

“Salha mpenzi wangu kuna nini mbona unanipigia simu usiku huu?” nilimuuliza huku nikitegemea majibu ya maswali yangu lakini chakushangaza badala ya kujibiwa nilipokewa na sauti ya kilio kwa upande wa pili. Ilikuwa ni sauti ya mpenzi wangu Salha ambaye mpaka kufikia wakati huo nilikuwa sijui ni kipi hasa kilichokuwa kinamliza.

“Salha,” nilimuita.

(Kimya) kilichosindikizwa na sauti ya kilio.

“Salha mpenzi wangu unalia nini mbona sasa husemi?” nilisema huku nikianza kujiwa na hofu kubwa moyoni. Sikujua ni nini kilichokuwa kimetokea mpaka kumfanya Salha awe katika hali ile.

“Yasri..Ma..mama,” aliniambia Salha huku akilia kwa sauti ya kwikwi.

“Mama! amefanyaje kwani, kuna nini niambie basi?” nilimuuliza.

“Ameanguka tu ghafla! na muda huu ninavyoongea na wewe tupo hospital hali yake si nzuri,” aliniambia Salha maneno ambayo yalinishtua sana. Nilijikuta nikiinuka kitandani kisha nikaanza kutembea huku na kule mule chumbani kwangu kama mwendawazimu.

“Unasema?” nilijikuta nikimuuliza swali la kizembe kana kwamba mwanzoni sikumsikia vizuri akinielezea hali ya mama yake ilivyokuwa.

“Hali ya mama sio nzuri mpenzi,”alinijibu.

“Upo hospitali gani?” nilimuuliza.

“KCMC.”

“Ok nakuja,” nilijibu kisha nikaichukua suruali niliyokua nimeining’iniza nyuma ya mlango pamoja na shati langu kisha nikaanza kuzivaa huku nikionekana kuwa mwingi wa haraka mno. Sikutaka jina la muda hata kidogo kwa wakati ule.

Nilipomaliza kuvaa nilimpigia simu dereva teksi mwenzangu ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Deo. Alipopokea nilimuelezea kwa kifupi tatizo lililokuwa limetokea kwa wakati ule, alionekana kuwa muelewa sana.




Baada ya dakika kama kumi Deo aliweza kunifuata nyumbani kwangu maeneo ya Bomambuzi na safari ya kuelekea hospitalini ikaanzia hapo. Barabarani akili yangu ilikuwa ikimfikiria mama yake Salha ambaye mpaka kufikia wakati ule sikujua alikuwa anasumbuliwa na nini. Nilimuomba Deo akimbize gari ili niwahi kufika hospitali. Niliamini kwa kuwahi kwangu kufika hospitalini pengine hali ya mama yake Salha ingeweza kubadilika na kupata nafuu lakini haikuwa kama mategemeo yangu.

Baada ya muda mfupi hatimaye tukawa tumefika nje ya hospitali ya mkoa iliyokuwa ikijulikana kwa jina la KILIMANJARO CHRISTIAN MEDICAL CENTER (KCMC). Nikazamisha mkono mfukoni mwangu kisha nikaibuka na waleti ambayo niliifungua nikatoa kiasi kidogo cha pesa, nilitaka kumlipa Deo. Ajabu Deo hakuweza kuipokea pesa yangu, nikajaribu kumsihi apokee jasho lake lakini alikataa katakata.

“Kwanini Deo?” nilimuuliza.

“Yasri pesa si kitu kuliko utu wa mwanadamu nenda kamwangalie mama mkwe wako mtarajiwa na kama tatizo ni hiyo pesa basi kanunue chochote kwa ajili yake. Sisi ni madereva najua hali uliyokuwa nayo kwa sasa nenda kamsaidie mama kwanza,” alinijibu Deo majibu ambayo yakanifanya nimuone kuwa binadamu wa tofauti sana, ndiyo alikuwa ni dereva mwenzangu lakini sikupaswa kumfanyisha kazi bila malipo, nafsi yangu ilikuwa inikinisuta.

Yani nimemuamsha katika usiku kama ule halafu nikamuomba anipeleke hospitalini kwa taksi yake ambayo ndiyo muhimili wa maisha yake lakini bado hakuweza kuhitaji hata senti moja kutoka kwangu.

Kuna muda nilihisi wenda alikuwa yupo katika utani lakini haikuwa hivyo alikuwa akimaanisha kile alichokuwa akikizungumza kwa wakati ule. Nikashuka kwenye taksi yake kisha nikaanza kujongea haraka kuelekea ndani ya hospitali ile huku akili yangu ikiendelea kumfikiria mama yake Salha ambaye alikuwa ni mama mkwe wangu mtarajiwa.

Niliamua kumpigia simu Salha na kumuuliza kuwa alikuwa wodi namba ngapi. Hapa ilikuwa tayari nimeshaingia ndani ya hospitali.

“Yasri nipo huku theatre bado madaktari wanajaribu kuyaok……..” kabla hajamaliza kuzungumza nilimsikia akianza kulia huku akilalamika kwa sauti iliyojaa uchungu, uchungu wa mama yake mzazi.

Nilikifahamu vyema chumba kile cha upasuwaji, haraka nikatembea mpaka eneo hilo. Macho yangu yalikutana na Salha mpenzi wangu ambaye alikuwa amejiegesha pembeni mwa mlango wa chumba kile cha upasuaji huku machozi yakimtoka mfululizo bila kukoma. Aliponiona aliinuka kisha akaja kunikumbatia, kumbato ambalo likazidi kuniweka karibu naye kihisia.

“Yasri…Mama yangu…Mama,” aliniambia huku akilia wakati nilipokuwa nimekumbatiana naye.

“Salha embu tulia kwanza, Mama atakuwa sawa umesikia?” nilimwambia katika hali ya kumpa matumaini lakini ilikuwa ni kama vile nimemwambia azidishe kulia. Alizidi kulia mno kama mtoto mdogo.

Machozi yake yaliyokuwa yakidondoka katika shati langu yalinifanya nizidi kujisikia vibaya sana, nikajikuta nadondokwa na machozi ila niliwahi kuyafuta ili nisionekane dhaifu hasa mbele ya mtu niliyekuwa nampenda kuliko kitu chochote kile katika hii dunia iliyojaa kila aina ya jema na shari.

“Usilie basi utaniumiza na mimi,” nilimwambia katika hali ya kumtuliza huku nikimpigapiga mgongoni kwa utulivu wa hali ya juu.

Niliamini kwa vyovyote vile ni lazima mama yake angeweza kuwa salama lakini imani yangu ilianza kupotea hapa ni baada ya kumuona daktari mmoja aliyetoka katika chumba kile cha upasuaji huku sura yake ikionekana kupoteza furaha kabisa, alionekana kutawaliwa na mawazo.

Haraka tukamkimbilia kwa lengo la kutaka kumuuliza hali ya mgonjwa kwa wakati ule ilikuwa inaendeleaje? lakini daktari alionekana kuwa mzito wa kutupa majibu, hilo likazidi kuniweka katika wasiwasi mkubwa.

“Dokta Dokta imekuaje?” nilimuuliza daktari yule lakini badala ya kunijibu alianza kunipigapiga begani ishara kama alikuwa akinipooza machungu fulani. Kwa kitendo kile sikuweza kumuelewa kabisa nikajikuta najiuliza alikuwa akimaanisha nini Lakini sikuweza kupata jibu kabisa badala yake ndiyo kwanza nilizidi kubaki njia panda nisijue ni kitu gani kilichokuwa kimetokea mule ndani.

“Dokta Mama yangu anaendeleaje?” sauti ya Salha iliyokuwa ikimuuliza daktari aliyekuwa amesimama mbele yetu kwa wakati ule ndiyo iliyoweza kunishtua kutoka katika dimbwi la mawazo.

“Tumejitahidi sana kwa kila hali katika kujaribu kuyaokoa maisha ya Mama yenu kipenzi lakini nasikitika kuwaambia kuwa amefariki dunia,” alijibu daktari majibu ambayo yalitushtua mno. Ni hapo ambapo nilimshuhudia mpenzi wangu Salha akianguka chini na kupoteza fahamu.

MUNGU WANGU!

Salha alizinduka siku tatu baada ya mazishi ya Mama yake mzazi kupita, tukio hilo la kuzinduka siku tatu baada ya mazishi ya mama yake liliwashangaza watu wengi sana. Miongoni mwa watu ambao walishtuka walikuwa ni wale waliyohudhuria siku ya msiba wa Mama yake Salha, hawakutaka kuamini.

Kwa kweli si tu kwa wale ambao walihudhuria siku ya msiba bali hata mimi pia nilikuwa miongoni mwao, nilishangazwa sana na tukio lile.

“Salha mpenzi wangu umeamka?” nilimuuliza Salha hapa ni pale alipoyafumbua macho yake kwa kuyapepesapepesa.

“Sal…..” kabla sijamaliza kumuita jina lake ghafla! Nikakutana na swali zito.

“Yasri Mama yuko wapi?” aliniuliza huku akionekana kutokukumbuka chochote kilichokuwa kimetokea.

Ndugu msomaji nilijikuta nikiwa katika wakati mgumu sana hasa ya kumueleza Salha juu ya kifo cha Mama yake. Mama ambaye alikuwa ni kila kitu katika maisha yake, hakika nilipagawa. Machozi yakashika hatamu yake, yakaanza kunidondoka mashavuni mwangu bila hata kujitambua.

Hakika nilikuwa katika wakati mgumu sana, wakati wa kurudia kuiwasilisha taarifa ya msiba kwa mtu ambaye alionekana kusahau kila kitu.

“Yasri mbona unalia?” sauti ya Salha ndiyo iliyonishtua kutoka katika dimbwi la mawazo kwa wakati ule na kunirejesha tena katika swali lililokuwa likihitaji jibu, jibu la Mama yake alipo.

“Mbona simuoni mama yangu yuko wapi?” aliniuliza huku akinitazama usoni.

Kitendo cha kunitazama nikapata wasaa wa kuitazama sura yake vyema. Alikuwa na uso uliotawaliwa na uzuri wa kipekee ambapo mara zote nilikuwa nikipenda kumsifu kuwa alikuwa mrembo sana na kwa urembo aliyokuwa amejaaliwa hakustahili kabisa kuruhusu kuyadondosha machozi yake na kama ingetokea akathubutu kufanya hivyo basi urembo wake ungetoweka asilani.

Looh!

Ona sasa nilikuwa naenda kumfanya ayadondoshe machozi yake kwa mara ya nyingine tangu alipowahi kuyadondosha katika msiba wa baba yake aliyefariki kwa ajali ya gari. Nilikuwa naenda kumtonesha jeraha kubwa lililopo ndani mwa moyo wake.

Watu waliyokuwa wakija kwa lengo la kumpa pole, walizidi kumshtua sana.

“Nini kwani kimetokea, Mama yangu yuko wapi, mbona Yasri hunijibu lolote?”aliniuliza Salha huku akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa sana.

“Tulia binti Yasri atakueleza kila kitu ila ulikuwa umepoteza fahamu kikubwa unatakiwa upumzike,” ilikuwa ni sauti ya mwanamke mmoja ambaye alikuwa akijaribu kumtuliza Salha. Mpaka kufikia wakati huo alikuwa hajui nini kilichokuwa kinaendelea.

Kwa kweli sikujua ni nini nifanye au nitumie lugha ipi ili kusudi mpenzi wangu aweze kunielewa kwa wakati ule kuwa Mama yake alikufa na tayari alishazikwa. Hilo likazidi kuniumiza sana akili yangu, nikajaribu kuutunga uongo wa kumdanganya lakini nafsi yangu ilinisuta kufanya hivyo na kwanini nimdanganye sasa wakati ukweli ulikuwepo.

“ Salha ,” nilimuita katika hali ya utulivu kabisa huku nikimtazama.

“Abee,” aliitika.

“Naomba unielewe kwa hiki ninachokwenda kuukuambia,” nilimwambia huku nikiwa nimejikaza kiume, sikutaka kuogopa lolote.

“Sawa niambie kuna nini?” aliniuliza.

“Ni kuhusu habari ya Mama yako,” nilimwambia.

“Mama yangu?”

“Ndiyo.”

“Amefanyaje?”

“Salha Mama yako amefariki dunia, daktari alipokuwa anatueleza habari za kifo chake ulipoteza fahamu na umekuja kuzinduka siku tatu baada ya mazishi yake,” nilimuambia huku nikijikaza machozi yasinitoke.

Nilipomaliza kuzungumza nikaanza kuyaona machozi yakimdondoka mashavuni mwake. Hakutaka kuamini kama kweli mama yake alikuwa amefariki dunia.



Ilinibidi nikamthibitishie kwa kwenda kumuonyesha kaburi la Mama yake mzazi. Machozi yalikuwa yakimtiririka mfululizo bila kukoma. Niilifahamu fika ni maumivu kiasi gani ambayo alikuwa akiyapata kwa wakati ule hasa alipokuwa akilitazama kaburi la Mama yake mzazi.

“Mama kwanini umeniacha, kwanini umewahi kuondoka kipindi ambacho bado nakuhitaji?”alisema Salha kwa sauti iliyosindikizwa na kilio cha kwikwi.

Alilia kama mtoto mdogo juu ya kaburi, hakutaka kuamini kile alichokuwa akikiona mbele yake, alihisi wenda ulikuwa ni mchezo wa maigizo ambapo muda wote ungeweza kufika mwisho lakini haikuwa hivyo kila sekunde na dakika zilizokuwa zikijongea hali haikuweza kubadilika.

“Basi mpenzi inatosha usilie sana utajiumiza,” nilimwambia katika hali ya kumbembeleza lakini haikuweza kusaidia lolote.

“Niache nilie Yasri, niache niumie siwezi kuvumilia machungu haya,”aliniambia Salha huku machozi yakiendelea kumdondoka, kiukweli kila nilipokuwa nikiyashuhudia machozi yake yalizidi kuniumiza sana moyoni, nilijihisi kuwa kama kuna kitu kinanitafuna na kuniacha na maumivu makili sana ambayo siwezi kuyasimulia.

“Najua mpenzi lakini kuna wakati inabidi ukubaliane na hali halisi iliyotokea,” nilimwambia hapa ni baada ya kujikaza kiume, sikutaka kuyadondosha machozi yangu. hakika iliniwia vigumu mno.

“Nimeumia sana kwa kumpoteza mama yangu, mama upo wapi?” aliuliza katika namna ya kukufuru huku akiwa amelala juu ya kaburi la Mama yake. Tukio hilo lilizidi kuniumiza sana moyoni mwangu, kiukweli niliumia sana ndugu msomaji.

Ama kwa hakika msiba usikie kwa mwenzio tu! Ila usiuombe ukakukuta, utahisi dunia nzima imekuelemea halafu hakuna wa kukupa msaada wowote, kila mtu atabaki akikushangaa tu! huku pole zikikutawala kila kona.

“Usiseme hivyo unakufuru mpenzi,” nilimwambia huku nikimtoa pale juu ya kaburi.

“Niache Yasri, niache Yaasri nikufuru,” alisema huku akiendelea kulia.

“Binafsi nimeumia pia ila jikaze basi mpenzi wangu, naomba tuondoke eneo hili,” nilisema huku nikimlazimisha kuondoka naye eneo lile kwani kwa kuendelea kukaa pale isingeweza kubadili ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea. Alikubali kisha tukaondoka eneo lile la makaburi.

****

Nilifanya kila niwezalo ili nihakikishe kuwa Salha anarudi kuwa katika hali yake ya kawaida. Kuhusu hilo niilifanikiwa na ilifikiwa wakati hata yale mawazo ya kuhusu Mama yake yakafutika kabisa, tukaufungua ukurasa wa maisha mengine kabisa.

Niliamua kumuamishia Salha nyumbani kwangu maeneo ya Bomambuzi ambapo ndipo nilikuwa nimepanga chumba kimoja, ilikuwa ni nyumba ambayo ilikuwa na mazingira mazuri ya wapangaji wake. Mahitaji yote muhimu yalikuwepo kama vile maji na umeme, hakukuwa na shida yoyote.

Nilikuwa nikifanya kazi ya udereva teksi, kazi ambayo ndiyo ilikuwa ikiniweka mjini. Kwa kifupi nilikuwa nikiyaendesha maisha yangu kupitia kazi yangu hiyo. Deo huyu alikuwa ni dereva mwenzangu katika kazi hii ya udereva teksi. Kijiwe chetu kilikuwa kipo maeneo ya stand ya mkoa ya Moshi mjini.

Tulikuwa tukiishi maisha ya amani yaliyogubikwa na upendo wa hali ya juu lakini kuna kitu kimoja kilikuwa kikinisumbua sana, kila siku haikuweza kupita bila kunisumbua.

****

Nilikuwa katikati ya msitu nisioufahamu, mvua kubwa ilikuwa ikinyesha kwa wakati huo. Mingurumo ya radi pamoja na upepo uliokuwa ukivuma mahali hapo vilizidi kuniweka katika hofu kubwa. Mbele yangu alikuwa amesimama bibi kizee ambaye alionekana kuwa na hasira iliyodhihirishwa na sura yake ya makunyanzi. Alinitazama usoni halafu mara akaanza kunguruma mithili ya simba. Haikuchukua sekunde chache mara nikaushuhudia muujiza mwengine tena. Yule bibi kizee alianza kutetemeka kama mtu ambaye alikuwa akihisi baridi kali sana ghafla! akaanza kubadilika. Ngozi yake iliyojikunja ikaanza kupotea taratibu na kuja ngozi nyingine. Kilikuwa ni kitendo kama cha dakika moja ambapo nikamuona mtu mwingine kabisa tofauti na yule bibi aliyekuwa amesimama mbele yangu. Alikuwa ni msichana mrembo sana lakini nilipomtazama sura yake haikuwa ngeni machoni mwangu. Nikajaribu kumkumbuka.

Naam!

Hatimaye nikamkumbuka, alikuwa ni Mulhaty yule mwanamke niliyewahi kumuona kule makaburini kupitia ndoto niliyowahi kuiota hapo kabla.

“Nataka umwage damu Yasri,” aliniambia huku akinitazama kwa namna ya kutisha, macho yake yalikuwa yakionekana mithili ya macho paka.

“Nimwage damu?” niliuliza huku nikitetemeka.

“Ndiyo.”

“Siwezi kuua.”

“Kwanini?”

“Naogopa.”

“Hutakiwi kuogopa chochote, nitakulinda?”

“Sijawahi kuua katika maisha yangu.”

“Hiyo isiwe sababu ninachotaka ni umwage damu.”

“Siwezi Mulhaty.”

“Nimesema ni lazima umwage damu.”

“Siwezi Mulhaty.”

“Huo ndiyo mkataba wetu.”

“Mkataba wetu?”

“Ndiyo.”

“Mkataba gani?”

“Mkataba wa kumwaga damu.”

“Mbona sifahamu lolote?”

“Kwaheri,” aliniambia Mulhaty kisha upepo mkali ukaanza kuvuma eneo lile, haikuchukua sekunde kadhaa akatoweka mahali pale.

“Mulhaty! Mulhaty! Mulhaty!” nilijaribu kumuita kwa kuipaza sauti yanngu ili aweze kurudi lakini haikuwezekana. **** Niliamka katika ndoto ile ya ajabu ambayo ilikuwa ni kama muendelezo wa ndoto niliyowahi kuiota hapo kabla juu ya yule mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Mulhaty. Alikuwa akinitaka nimwage damu. Nikazidi kujiuliza maswali mengi kuwa ndoto ile ilikuwa ina maana gani na kama ni ndoto tu sasa ni kwanini ijirudie katika hali ile ile ya kusisitiziwa nimwage damu.

Nilizidi kuchanganyikiwa, Sikujua ni nini kilichokuwa kinakwenda kutokea katika maisha yangu kwani kila nililokuwa naliwaza kwa wakati ule sikuweza kulipatia jibu. Niliamua kumueleza Salha kila kitu juu ya zile ndoto zilizokuwa zikinitokea mara kwa mara lakini alionekana kutoziamini kabisa.

Alizichukulia kuwa kama ndoto ambazo zisingeweza kutokea katika maisha ya kawaida.

“Yasri hivi kweli unaamini ndoto?” aliniuliza.

“Kwa ndoto ninazoziota sinabudi kuamini kuwa zina maana,” nilimjibu.

“Mpenzi wangu hutakiwi kuamini ndoto hata mara moja,” aliniambia.

“Hii sio mara ya kwanza kuota, nimekuwa nikiota ndoto ileile tena imekuwa kama inaendelea kila siku.”

“Hizo ni ndoto tu kama zilivyo ndoto nyingine usiziamini.”

“Salha yule mwanamke ananisumbua sana ndotoni.”

“Anakusumbulia nini?”

“Ananilazimisha nimwage damu.” nilimwambia kisha nikapokelewa na kicheko, alinicheka huku akionekana kutoamini kabisa.

“Mbona unanicheka?” nilimuuliza.

“Hapana sicheki.”

“Ila.”

“Unajua unanishanga sana na hizo ndoto zako.”

“Nakushangaza tena.”

“Kwani huyo mwanamke ulishawahi kumuona hapo kabla?”

“Hapana.”

“Sasa utawezaje kuiamini hiyo ndoto?”

“Yaani hata sielewi mpenzi wangu,” nilimwambia.

Kwa kweli mpaka kufikia wakati ule nilijikuta nikianza kuiamini ile ndoto. Kuna muda nilikuwa nikiwaza kuwa Mulhaty amenitokea na akawa anataka kuniua kwasababu sikufanya kama alivyoniagiza. Wazo hilo liliponitoka likanijia lingine kuwa nimeshakufa kisha naungana na wafu wenzangu kuzimu. Hofu ikazidi kunitawala.

Kila mtu niliyekuwa nikijaribu kumuelezea tatizo langu la kusumbuliwa na ndoto ya aina moja kila siku alikuwa haniamini kabisa. Wengi wao waliniambia kuwa ndoto kamwe haiwezi kuwa maisha ya kweli hivyo nisiendelee kuiamini ndoto.




Sikutaka kuiamini tena ndoto, nikaendelea kufanya kazi yangu ya udereva teksi, kila siku nikawa napata wateja. Hatimaye lile tatizo langu la kusumbuliwa na ndoto likanitoka kabisa, nikawa nalala vizuri bila matatizo yoyote. Nikasahau kabisa kuhusu ndoto ambayo ilikuwa inanisumbua.

Niliamua kumueleza mpenzi wangu Salha kuhusu habari zile, hakika zilionekana kuwa habari zilizomfurahisha sana. Upendo ukaongezeka ndani ya nyumba.

Japo sikuwa nimemuoa Salha lakini nilikuwa nikiishi naye kama mke wangu wa ndoa, nilikuwa nikimpenda sana.

“Yani siku hizi nalala usingizi mzuri kabisa, sisumbuliwi na zile ndoto za ajabuajabu tena,” nilimwambia Salha huku furaha ikiwa imenitawala.

“Mimi nilikwambia zile ni ndoto lakini hukutaka kunisikia,” aliniambia Salha.

Kwa kweli nilianza kuyaona maisha yangu yakirudi kuwa na amani kwani ilikwishaanza kupotea kutokana na ndoto zilizokuwa zikinisumbua. Nilihisi kuna mtu alikuwa akinichezea akili yangu.

Sikutaka kumficha Deo, niliamua kumueleza kila kitu kilichokuwa kimetokea na mara baada ya kumuelezea alinicheka sana.

“Sasa mbona unanicheka?” nilimuuliza.

“Tatizo lako wewe ni muoga sana,” aliniambia Deo.

“Uwoga wangu ni upi sasa?” nilimuuliza.

“Yani na ujanja wako wote ukaamini kabisa ndoto,” alinijibu kisha akacheka tena.

“Wewe unazungumza kwasababu hayajakukuta,” nilimwambia.

“Sinaga desturi ya kuogopaogopa kizembe.”

“Haya bhana ila hayo ndiyo yaliyonikuta,” nilimwambia.

Deo alikuwa ni mtu wa kupuuzia sana mambo, hakuwa akiamini kabisa mambo ya kishirikina kila nilipokuwa nikimuelezea matatizo yangu yaliyokuwa yakinisumbua alikuwa akipenda kuniambia kuwa nisiwe mtu wa kuamini kila kitu.

“Yasri embu acha kuwa mjinga kiasi hicho vitu vingine usiviamini vipuuzie,” aliniambia Deo huku akionekana kujiamini sana.

Maisha yaliendelea mpaka pale siku moja majira ya usiku nilipokutana na msichana mmoja maeneo ya Kindoroko akiwa hoi bin taabani, alionekana kuwa kama anayekimbizwa na watu ambao sikubahatika kuwaona mpaka leo ninapokusimulia mkasa huu.

“Samahani kaka yangu naomba unisaidie kuna watu wanataka kuniua,” aliniambia yule msichana, nilipomtazama alionekana kuwa katika mavazi yaliyokuwa machafu sana.

Licha ya mavazi yake kuwa machafu lakini alionekana kuwa mrembo sana, kitendo cha kumtazama mara moja pamoja na maneno yake aliyoniambia kuwa alikuwa akihitaji msaada wangu, sikutaka kujiuliza mara mbilimbili, nikaamua kumsaidia.

“Ingia ndani ya gari,” nilimwambia huku nikiendelea kumtazama kwa macho ya kujiibaiba. Wakati huo yaalikuwa ni majira ya saa sita za usiku muda ambao nilikuwa narudi nyumbani kwangu Bomambuzi.

“Asante sana kaka yangu Mungu atakubariki,” aliniambia huku akionekana kuwa mtu mwenye wasiwasi mkubwa sana.

“Usijali,” nilimwambia kisha nikanyamaza kidogo halafu nikaendelea kuzungumza.

“Kwani unaelekea wapi?” nilimuuliza huku nikimtazama.

“Nyumbani,” alinijibu.

“Nyumbani ni wapi?” nilimuuliza.

“Pasua,” alinijibu.

“Pasua sehemu gani?”

“Sembeti.”

“Kwahiyo nikikufikisha Sembeti utakuwa umeshafika nyumbani?”

“Ndiyo.”

“Basi sawa ngoja nikupeleke,” nilimwambia kisha nikawasha gari tukaondoka eneo lile huku ukimya ukiwa umetutawala kati yetu.

Tulipofika Mbuyuni niliamua kuuvunja ule ukimya, nikaanza kwa kumuuliza jina lake lakini kabla hajanijibu akatabasamu.

“Naitwa Hytham,” alijitambulisha huku macho yake akiwa ameyaelekezea chini, alionekana kuwa mwenye aibu sana.

“Ok mimi naitwa Yasri,” nilijitambulisha kisha kama kawaida yangu nikanyamaza kidogo usawa kama wa kumeza fundo la mate halafu nikaendelea kuzungumza.

“Nashukuru kukufahamu hivi nani tena?” nilimuuliza kichokozi.

“Hytham,” alijibu kisha akacheka.

“Jina lako zuri sana,” nilimwambia.

“Hata jina lako zuri pia,” aliniambia.

“Mimi siamini hilo.”

“Amini.”

“Sawa itabidi niamini kwa kuwa umenilazimisha,” nilimwambia Hytham.

Haikuchukua dakika nyingi hatimaye nilikuwa nimeshafika Sembeti, nikafunga breki.

“Nadhani tayari nimeshakufikisha nyumbani?” nilimuuliza Hytham.

“Ndiyo,” alinijibu kisha akanishukuru sana, akashuka kisha taratibu akaanza kujongea kuvuka upande wa pili wa barabara.

Kitendo cha kufumba na kufumbua macho nikajikuta nikishikwa na bumbuwazi mara baada ya Hytham kunitoweka katika mazingira ya kutatanisha, sikutaka kujiuliza maswali mengi sana. Nikayatazama yale makaburi yaliyokuwa pembezoni mwa barabara lakini sikutaka kuhisi lolote. Nikawasha gari kisha nikatoweka eneo lile, moyoni nilikuwa mwenye furaha sana hasa baada ya kukutana na Hytham msichana niliyeamua kumsaidia.

Nilikumbuka jinsi ambavyo alikuja kuniomba msaada lakini sikumbuki kama nilimuuliza kuhusu watu ambao walikuwa wakimkimbiza na kwa nini walikuwa wanamkimbiza. Hilo nilisahau kumuuliza lakini nililokuwa nalikumbuka ni jina lake.




Hakukuwa na kitu kingine nilichokuwa nikikifikiria kwa wakati huo zaidi ya Hytham, sijui hata ni kwanini lakini nilijikuta nikimuwaza tu! bila sababu

Nilipofika nyumbani kwangu mara baada ya kupaki gari sehemu nzuri niliugonga mlango huku nikiamini muda huo mpenzi wangu Salha alikuwa amelala hivyo nilimuita lakini haikuwa kama nilivyowaza, nilipougonga mlango haikuchukua dakika ukafunguliwa, ni kama vile alikuwa akinisubiria.

“Mbona umechelewa sana mpenzi?” aliniuliza mara baada ya kunikaribisha ndani kisha akanipa pole kutokana na mihangaiko yangu ya siku ile.

“Kuna matatizo yalitokea ndiyo yakafanya nichelewe,” nilimjibu kwa kumdanganya, nilikuwa nikimfahamu sana, alikuwa ni msichana mwenye wivu na kama ningemwambia ukweli kuwa nilimsaidia mwanamke kwa kumpa lift hakika angeweza kuninunia.

“Matatizo gani tena hayo Yasri na kwanini usiniambie?” aliniuliza tena huku akionekana kuingiwa na uwoga.

“Hapana nilihisi nitakusumbua hata hivyo usiwe na wasiwasi ni gari ilizingua barabarani,” nilimjibu huku nikiweka msisitizo.

“Sawa mpenzi ila uko salama?”

“Ndiyo nipo salama kabisa,” nilimjibu huku nikitabasamu.

Sikutaka kumueleza ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea, niliamua kufanya hivyo huku nikijaribu kulinda penzi langu. Nilifahamu Salha alikuwa ni msichana wa aina gani hivyo kama ningeamua kumueleza ukweli ningeweza kuihatarisha amani ya penzi langu hasa katika usiku kama ule.

Nilikuwa nimechoka sana hata mpenzi wangu Salha alilitambua hilo, aliamua kuniandalia maji bafuni kisha nikaenda kuoga, nilipomaliza akaandaa chakula tukala kwa pamoja.

Tulipokuwa tunakula hakuacha kuniuliza juu ya siku yangu iliendaje. Sikutaka kuweka mazungumzo marefu.

“Imeenda vizuri,” nilimjibu.

Baada ya kumaliza kula chakula nilimshukuru kwa chakula kitamu alichokuwa amepika kisha tukaenda kulala.

Kwa kweli taswira ya Hytham bado iliendelea kunijia akilini, sikuweza kupata usingizi kabisa kwa wakati ule, nilikuwa nikimfikiria muda wote huo, sikujua alipatwa na nini mpaka akawa anakimbizwa kiasi cha kuja kuniomba msaada nimsaidie. Ajabu sasa kwa uzembe niliyoufanya eti nilisahau kumuuliza kilichokuwa kimemsibu. Kha!

Bado akili yangu iliendelea kumfikiria msichana huyo ambaye nilikutana naye masaa machache yaliyopita.

“Hytham,” nilijikuta nikilitaja jina lake kwa sauti bila kutarajia, wakati huo Salha alikuwa bado hajapitiwa na usingizi, akanisikia kisha hapohapo akakurupuka na kuniuliza kuwa Hytham ni nani.

“Aaaah aaaamm ni abiria,” nilijiumauma kisha nikajibu jina la kizembe kabisa.

“Abiria?” aliniuliza kwa ghadhabu.

“Ndiyo ni abiria ila,” nilimwambia kisha kabla sijamaliza kuzungumza akanikata kauli.

“Ila nini?” akaniuliza swali ambalo likatuingiza katika mgogoro, Salha hakutaka kuelewa chochote kile nilichokuwa nikimueleza, alihisi kuwa nilikuwa nikimsaliti na tena huyo Hytham ndiyo msichana ambaye nilikuwa nikitoka naye.

“Yani Yasri kumbe unanisaliti kweli,” aliniambia Salha kwa sauti iliyokosa uvumilivu, alianza kulia, machozi yake yakazidi kunifanya nibaki katika mshangao yani kwa dakika chache tayari alikuwa akibubujikwa na machozi.

“Salha mbona unakuwa hivyo lakini mpenzi, nimekwambia hakuna chochote kinachoendelea na huyo Hytham ni abiria tu kama walivyo abiria wengine,” nilimwambia huku nikajaribu kumuweka sawa, hakutaka kunielewa, alizidi kulia.

“Mpenzi.”

“Nini.”

“Embu jaribu kunielewa basi.”

“Nikuelewe nini, nikuelewe nini Yasri na hao wanawake zako.”

“Wanawake gani?”

Salha hakutaka kunielewa kabisa, alikuwa akilia muda wote na ni hapo ambapo usingizi uliweza kunipotea kabisa, sikuwa na lepe hata moja la usingizi.

“Kwanini imekuwa hivi?” nilijiuliza swali ambalo sikuweza kupata jibu. Wakati huo Salha alikuwa ameninunia, hakutaka kuzungumza na mimi lolote, nilibaki nikimtazama bila kusema lolote kwa muda mrefu.

Sikumbuki ni nini kilitokea mara baada ya ule ugomvi uliyozuka ghafla! pale kitandani ila nilichokuja kushuhudia ni kuamka katika asubuhi ya siku iliyofuata, ilikuwa ni miongoni kati ya asubuhi ya siku mbaya sana kuwahi kutokea katika maisha yangu.




Niliamka katika siku iliyokuwa na matatizo ambayo sikuyatarajia kwa kweli. Kwanza mpenzi wangu Salha alikuwa bado ameninunia, hakutaka kabisa kusemezana lolote na mimi, uso wake aliyokuwa ameukunja ulitengeneza makunyanzi yaliyoonekana kuwa mithili ya bibi aliyejaaliwa kuishi miaka mingi hapa duniani.

Sikutaka kuliwazia hilo sana, niliamini zilikuwa ni hasira za muda tu! na kuna muda ungeweza kufika zingeweza kuisha. Niliamua kujiandaa vyema kisha nikamuaga Salha kuwa nilikuwa natoka kama ilivyokuwa kawaida yangu, hakunijibu lolote, alibaki akinitazama mithili ya sanamu lisiloweza kusema. Hilo nalo sikutaka kulitilia maanani, nikatoka zangu nje kuielekea teksi yangu kisha nikapanda, kabla sijaamua kuondoka eneo lile ghafla! simu yangu ya mkononi ikawa inaita, haraka nikaitoa mfukoni na kutazama ni nani ambaye alikuwa akinipigia kwa wakati huo, alikuwa ni Mzee Mabula ambaye ndiye aliyeniajiri kibarua kile cha udereva teksi. Haikuwa kawaida yake kunipigia hasa katika nyakati kama zile kwani kama ni hesabu zake nakumbuka nilikuwa nikimtumia kwa njia ya huduma za kifedha za simu, sasa kuna nini? Nilijiuliza bila kupata jibu.

Nilihisi kulikuwa na tatizo na mimi sikutaka kupoteza muda, niliipokea.

“Yasri uko wapi?” sauti ya ukali ya Mzee Mabula ilinipokea kwa kuniuliza swali, sauti yake ilionyesha kuwa na jazba za waziwazi.

“Nipo nyumbani hapa ndiyo natoka hivyo kuelekea kibaruani,” nilimjibu huku nikijifanya kujichekesha na kujikoholesha.

“Teksi yangu ipo salama?” aliniuliza.

“Ndiyo iko salama kabisa wala hakuna tatizo mkuu,” nilimjibu huku nikianza kuwa na wasiwasi, nilihisi kulikuwa na tatizo, niliamua kumuuliza.

“Kwani kuna nini?” nilimuuliza huku nikiwa nimeyakodoa macho kodo.

“Usiniulize kuna nini wewe sasa sikia nimepata dereva mwingine hivyo naomba uirudishe teksi yangu hapa nyumbani haraka sana, naona hujui kufanya kazi ngoja niweke mtu mwingine anayejua kupiga kazi,” aliniambia maneno ambayo yalinichanganya sana. Mpaka kufikia wakati huo sikuwa nikifahamu lolote lile lililokuwa limetokea, nikabaki njia panda na hakukuwa na mtu mwingine wakumuuliza zaidi ya Mzee Mabula ambaye alikuwa akibwata kwa wakati huo, alifika mbali mpaka akawa ananitukana matusi ya nguoni. Kwa kweli nilishindwa kuyastahimili matusi yale aliyokuwa akinitukana.

“Mzee Mabula hivi nimekukosea nini mpaka unaamua kunitukana asubuhi yote hii au tatizo ni hii teksi yako?” nilimuuliza huku hasira zikianza kunipanda.

“Sitaki maneno mengi na wewe mpumbavu wa akili, nimesema naomba unirudishie teksi yangu na kama ni mkataba wako nauvunja sitaki tena mkataba na wewe,” aliniambia maneno yaliyozidi kuniweka katika hasira kali mno.

“Sawa mzee nimekuelewa ila ungeniambia basi tatizo ni nini mpaka umeamua kufanya hivyo maana hapa unaniacha njia panda,” nilimwambia katika mtindo wa kumuuliza.

“Kijana hivi huelewi Kiswahili au?”

“Nakielewa vizuri.”

“Nimesemaje?”

“Unaitaka teksi yako.”

“Ok basi fanya kama ulivyoelewa maana nilihisi labda utakuwa hujaelewa,” aliniambia Mzee Mabula maneno yaliyokuwa na kejeli ndani yake.

Niliamua kufanya kama alivyoniambia, nilimrudishia teksi yake na katika hali ya kushangaza akaamua kuuvunja mkataba wangu na yeye. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wangu wa kufanya kazi kama dereva teksi, Mzee Mabula alidhamiria kuniachisha kazi. Awali nilihisi wenda alikuwa katika utani lakini haikuwa hivyo, alimaanisha kila kitu.

Niliamua kumfuata Deo na kumuelezea kile kilichokuwa kimetokea kwa Mzee Mabula mpaka akaamua kunifukuza kazi.

“Aisee unasema kweli?” aliniuliza huku akionekana kushangazwa na taarifa zile.

“Yani mpaka sielewi ni nini nifanye ndugu yangu,” nilimjibu huku nikiwa katika hali ya huzuni kwa wakati huo.

“Sasa utafanyaje?”

“Sijui ndugu yangu nahisi kuwa na mikosi tu!”

“Hapana usiseme hivyo.”

“Huo ndiyo ukweli halafu shemeji yako naye ameshaanza kisirani chake na hili nalo nikimwambia anaweza akanibwaga kabisa.”

“Kafanyaje tena shemeji wewe nawe umezidi majanga.”

“Amna tu! ni wivu wake tu eti anahisi namsaliti na ni jana tu nimetoka kugombana naye leo naachishwa kazi.”

“Duh! Pole sana ndugu yangu.”

“Asante,” nilimjibu.

Katika maisha yangu sikubahatika kuwekeza katika biashara yoyote ambayo ingeweza kunisaidia kuyaendesha maisha yangu. Kwa kweli sikuwa sawa kabisa naweza kusema hivyo, nilihisi kuchanganyikiwa.

Niliporudi nyumbani kwangu na kumueleza habari zile Salha hakuweza kunielewa kabisa, aliniambia umalaya wangu ndiyo uliyosababisha mpaka nikafukuzwa kazi. Muda wote alikuwa akilitaja jina la Hytham na aliniambia alikuwa akimchukia kupita kawaida.

“Haya nenda kwa Hytham sasa,” aliniambia Salha maneno yaliyochanganyika na wivu. Wivu ndiyo ulikuwa ukimsumbua.

“Hytham kafanyaje tena mpenzi wangu?” nilimuuliza.

“Nani mpenzi wako?” aliniuliza kwa sauti ya ukali.





Salha hakutaka kunielewa kabisa kwa kile kilichokuwa kimetokea, nilijitahidi kuzungumza naye kila aina ya mazungumzo huku nikimuelewesha lakini hakutaka kunielewa, alizidi kunilaumu na ni hapo machozi yalianza kumdondoka.

“Yasri haya yote umeyataka mwenyewe,” aliniambia huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake.

“Hakuna kitu nilichokifanya mpenzi wangu kwanini hutaki kuniamini?” nilimuuliza huku nikizidi kushangazwa na machozi yake, alikuwa akilia bila sababu yani wivu wake ndiyo ulikuwa unamsumbua kwa wakati huo wala hakukuwa na kingine.

Sasa kwanini alie? Nilijiuliza bila kupata jibu, nikazidi kumtazama tu bila kusema lolote.

Mpaka kufikia wakati huo nilikuwa katika kizungumkuti, sikujua ni nini kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia mpaka kikasababisha nikafukuzwa kazi na Mzee Mabula. Mawazo yakazidi kunizonga na kila nilipokuwa nikiwaza na kuwazua ugomvi kati yangu na Salha uliingilia kati na kunivuruga kila kitu. Siku hiyo ilipita huku tukilala katika ugomvi.

Tukaamka siku nyingine ya muendelezo wa ugomvi uleule wa siku iliyopita, hakukuwa na amani tena ndani ya nyuma, lawama za Salha kuwa nilikuwa nikimsaliti zilizidi kuniweka katika wakati mgumu mno, sikujua ni nini nilitakiwa kumjibu ili aweze kuniamini.

“Umalaya wako umefanya mpaka unafukuzwa kazi Yasri ona sasa tutaishi vipi?” aliniambia maneno ambayo naweza kuyaita ni ya kipuuzi kisha akaniuliza swali la kipumbavu.

Yani nimefukuzwa kazi wala sina kitegea uchumi chochote halafu bado ananiuliza tutaishi vipi. Kha! Bila shaka alikuwa akinikejeli.

Sikumjibu lolote nikaamua kukaa kimya kuepusha maneno lakini kwa kufanya hivyo napo ilikuwa ni kosa, akacharuka na kuanza kuniambia kuwa nilikuwa nikimdharau ati! Kwa kuwa nilikuwa na mwanamke mwingine nje basi ndiyo sababu nilikuwa nikimdharau kiasi kile.

Nikajikuta natokwa na kicheko cha bila kukitarajia huku moyoni kikisindikizwa na maumivu makali mno, nilikuwa nikiumia hasa kwa kuendelea kuhukumiwa kwa kesi ambayo haikuwa yangu, kesi ya usaliti.

Baada ya kuona maneno yamezidi asubuhi ile niliamua kuondoka nyumbani, akili yangu haikuwa sawa hata kidogo wala sikuwa najua ni kitu gani nilikuwa nikikifanya kwa wakati ule. Kila uamuzi ambao niliuchukua, niliuchukua kwa kukurupuka.

****

Baada ya matatizo kuzidi kunizonga, niliamua kwenda nyumbani kwa Deo maeneo ya Pasua mshana alipokuwa amepangisha, nilienda kumuomba msaada. Alionekana kunihurumia sana na kila kitu nilichokuwa nikimuelezea kilikuwa kikimgusa.

“Unajua sisi binadamu matatizo tumeumbiwa na yakitokea hatutakiwi kuyakimbia isipokuwa inabidi tupambane mpaka tuhakikishe tunayamaliza,” aliniambia Deo huku akijiweka vizuri kwenye kochi dogo alilokuwa amekalia.

“Ni kweli Deo lakini nahisi kama kuna sehemu nimekosea mbona matatizo yananiandama kila siku,” nilimwambia.

“Hapana inabidi umuamini Mungu kwa imani yako, yeye ndiye ambaye anaweza kukusaidia kuondokana na matatizo haya yaliyokusibu,” aliniambia huku akionyesha msisitizo wa kauli yake.

“Sawa ila nahisi kuchanganyikiwa yani sielewi nini nifanye mpaka muda huu,” nilimwambia kisha nikamuona akiingiza mkono mfukoni akatoa shilingi elfu elfu thelathini.

“Chukua hii pesa itakusaidia kumaliza matatizo madogomadogo,” aliniambia kisha akanikabidhi.

Nilimshukuru sana Deo kwani alikuwa amenisaidia sana lakini hakunitaka nifanye hivyo, aliniambia kuwa aliamua kufanya vile kama sehemu moja wapo ya ubinadamu. Kwa kweli nilizidi kumshukuru sana.

Nilirudi nyumbani majira ya usiku, nikamkuta Salha akiwa amejilaza kitandani, sikutaka kumsemesha lolote zaidi ya kumpa salamu ambayo hata hakuijibu.

Kabla hata sijakaa chini nikapumzika ghafla! Salha alikuruka na kunipa taarifa nyingine iliyochukua sura mpya akilini mwangu. Aliniambia kuhusu ujio wa baba mwenye nyumba ambaye alikuwa anahitaji kodi ya chumba chake, taarifa hiyo hiyo ikazidi kunipa wakati mwingine wa mawazo, nikajiona kuwa mkosaji.

Kichwa kilianza kuniuma nikaamua kwenda bafuni kuoga, niliporudi sikutaka kuulizia chakula wala kitu chochote, moja kwa moja nikajitupa mzobemzobe kitandani na hapo sikuweza kuchukua dakika nyingi usingizi ukaweza kunipitia.

****

Nilishtuka kutoka usingizini, hakukuwa na kitu kingine kilichonishtua zaidi ya simu yangu iliyokuwa ikiita kwa wakati huo, nikamtazama mpenzi wangu Salha alikuwa bado amelala kisha nikaitazama saa iliyosomeka kwenye kioo cha simu yangu, ilikuwa ni majira ya saa nane za usiku.

Niliitazama ile namba iliyokuwa ikinipigia huku usingizi ukiwa bado umenitawala, ilikuwa ni namba ngeni na kila nilipojaribu kuitafakari ilikuwa ni namba ya nani sikuweza kupata jibu mwisho nikaamua kuipokea.

“Yasri habari yako,” sauti ya kike nyororo ilinipokea kwa kunisalimu.

“Nzuri tu,” nilimjibu.

“Pole kwa matatizo yaliyokukuta,” aliniambia.

“Asante ila sijui nazungumza na nani?” nilimuuliza.

“Jamani umenisahau mara hii wakati tumetoka kuonana juzi na tena ukanipatia namba yako ya simu,” aliniambia kisha nikajaribu kukumbuka kama juzi niliweza kukutana na msichana ambaye nilizungumza naye mpaka nikafikia hatua ya kumpa namba yangu ya simu, kumbukumbuku hiyo ilikataa kunijia kichwani, nikabaki nimeyakodoa macho nikiendelea kumsikiliza.

“Umenisahau?” aliniuliza.

“Ndiyo, nikumbushe,” nilimjibu kisha nikapokewa na sauti ya kicheko kikali.

“Unaitwa nani?” nilimuuliza huku nikiwa na shahuku ya kutaka kumfahamu kwa jina.

“Naitwa Hytham,” alijitambulisha kisha akakata simu.

Kumbukumbu iliyonijia ghafla! ilikuwa ni ile ya usiku mmoja ambapo nilikutana na Hytham Kindoroko alipokuwa akiniomba msaada kutokana na watu aliyodai kuwa walikuwa wakimkimbiza, nilikumbuka matukio yote yaliyotokea usiku ule lakini sikukumbuka kama niliweza kumpa namba yangu ya simu.

Nikajaribu kumpigia simu kwa wakati ule ambapo aliweza kukata ajabu namba yake ilikuwa haitambuliki, nikajaribu kuitazama namba yake kwa umakini ndipo hapo nilipokutana na maajabu mengine, namba zake hazikutimia namba kumi, zilikuwa zimeishia nane.



MWISHO






0 comments:

Post a Comment

Blog