Search This Blog

Sunday, July 24, 2022

KIROBA CHEUSI

   


MTUNZI : LAURA PETTIE


PALISHAKUCHA.

Pakuche mara ngapi?

Ni vile tu huyu Morena alilala chakari. Asubuhi hii ya saa nne, kwake ilikuwa ingali liamba. Alilala kifudifudi. Fofofo..

Ghafla, kuna mtu alimtoa katika ule ufofofo. Akamkera. Alimkera hasa!

Kivivu, aliinua shingo yake, akakigeuzia kichwa chake upande mwingine. Akasonya

Angali na mawenge ya usingizi. Si hayo tu, bali pia uvivu ulimjaa. Vikampa hali ya kutaka kuendelea kubadili uchago kila dakika, licha ya jua la asubuhi kuhanikiza nuru ya kutosha mle chumbani mwake.

Akilini, aliutaka utulivu kwa gharama yoyote ile. Japo apate kukimalizia hicho kipande cha usingizi. Wala hakujua kingekwisha saa ngapi. Alitaka kulala. Kulala tu mpaka pale mwili wake utakapomruhusu kutalikiana na kitanda.

Aliyemkera, akamkera tena.

“Eeh mchicha matembele majani ya kundeee… eeh mchicha tembeleee… eeh mchicha tembele majani ya mabogaaa”

Huyu muuza mboga ndiye aliyemgutua toka usingizini, kwani alikuwa akichuuza biashara yake ya mboga za majani karibu na dirisha la Morena. Dirisha lililokuwa upande wenye kichochoro kilichopakanisha chumba alichokuwemo na nyumba ya jirani.

Mchuuza mboga alisimama hapo kichochoroni pamoja na wateja wake waliokuwa wakichagua mboga toka kwenye tenga. Wakafanyiana mizaha ya hapa na pale iliyosindikizwa kwa vicheko vya juu na chini.

Kelele zao zikamfanya Morena ajihisi kama mtu anayepigiwa zumari sikioni. Akasonya tena. Msonyo mrefu uliobeba uzito wa makumi ya maneno. Maneno aliyotamani yawasilishe hisia zake kwa sauti ya kuhutubia umati. Alichefukwa.

Naam! Ikawa kama vile huo msonyo wake ulimuhimiza mchuuza mboga akolezee tena kibwagizo chake maradufu. Akamvumilia kidogo huku akiinua tena shingo yake na kuzisikiliza sauti za wateja wake. Akaitambua moja, ya mtoto wa mpangaji mwenzake.

“Somoe! We Somoe!” akaita kwa sauti ya kukaripia na Somoe mwenyewe akaginiza kwa sauti ya juu.

“Abeee!”

“Embu niondoshee huo mnada wenu hapo dirishani”

Morena akatoa amri yake kwa sauti ya chini kidogo huku akiyabana mate yaliyomjia ghafla kinywani. Hakuona pa kutemea. Akakunja ndita kadhaa usoni. Kwanza alikereka kwa kule kugutuliwa usingizini; pili, ile adha ya kujaa mate ilimkalfisha nafsi. Na mwisho, ombi lake kwa Somoe lilipita kimya kimya kama kivuli.

Muuza mboga naye kama mtu aliyefinywa alianza tena kuchuuza biashara yake kwa sauti. Safari hii Morena hakusubiri mbivu ziwe mbovu. Alitoka kitandani. Akasimama na kuikaza khanga yake kifuani. Ngoja nikamshikishe adabu! Akajiapiza.

Alipita katikati ya chumba chake, akivipamia vitu vilivyotupwa sakafuni shaghalabaghala; hapa nguo, pale viatu na makorokoro yake mengine chungu nzima.

Alihangaika na kitasa kwa takribani robo dakika wakati akiufungua mlango ambao ni dhahiri ulikuwa mbovu. Pale nje ya mlango wa chumba chake aliitafuta ndala yake moja na asiione, akaivaa hiyo moja iliyokuwepo na kuanza safari ya kuelekea nje.

Alimpungia mkono mpangaji mwenzake aliyepishana naye, akishindwa hata kuijibu sawasawa salamu aliyopewa, kwa kule kuyakonga mate kinywani. Aliukusanya mdomo wake akautanguliza mbele mithili ya mdomo wa bata.

Akatoka nje na kuyatema upenuni mwa nyumba. Akayafukia kwa mguu uliokuwa peku.

Haikuleta maana; kuivaa ile ndala moja na kisha kwenda kuyafukia mate kwa mguu uliopeku. Ila ndiyo falsafa ya maisha, kupata na kukosa; wanaokosa ndio wenye kutumika na kusulubika.

Twaibu! Morena aliiongoza miguu yake kuelekea ule upande wenye uchochoro. Alimfungia kibwebwe muuza mboga kana kwamba alitaka tena kwenda kulala akishamfukuzia mbali.

Alipoifikia ile kona inayoelekea uchochoroni, akausikia mlio wa bodaboda, mlio uliomgeuza shingo. Aliyemuona akamfanya ayasahau yote yaliyomtoa nje. Akakigeuza kiwiliwili kizima kumtazama mgeni aliyewasili.

Alikuwa rafikiye, Fatumata Mzinga. Somo yake wa kufa na kuzikana.

Alitulia akimtazama namna anavyoshuka toka kwenye bodaboda, mwili wake tipwatipwa uliogawanyika kike kisawasawa ukitibwirika. Na mshukaji nwenyewe akaongeza sifa za mkwezi kuudandia mnazi. Aliujaza madoido ule mtibwiriko!

Wanaume waliokuwa upande wa pili wa barabara palipo na karakana ya fenicha wakameza mate ya tamaa, wengine walijikohoza na wengine walikaribia kuviranda vidole. Umbile lake lilileta hali ya kubahashika pasi hiyari.

Wakaingia ndani, Morena akitangulia na Fatumata akimfuatia. Mle ndani Fatumata akayaanzisha maongezi mara tu baada ya kuufunga mlango na kwenda kuketi kitandani.

“Nilijua nikifika kwa Mzee Hizza n’takuta wanatembeza daftari la rambirambi” akazungumza akimtaja baba mwenye nyumba aliyopanga Morena.

“Aaah! kwa lipi?” Morena akauliza huku akiumba uso wa mshangao.

“Yale mapombe makali makali uliyogida jana. Mwanamke unakunywa kiama” Akampigia saluti. “Nikajua utaunguza hadi utumbo maana ile mijibaba jana ilikuvulia kofia ujue! Chupa ya tisa jicho kodo!... kope zimekusimama kama miiba ya nungunungu” Fatumata aliongea akitoa macho na kuchezesha mikono kuyasindikiza maneno yake.

Morena akacheka. Alicheka vile mwenzake alivyomsifu na kumsagua kwa pamoja.

“Tena mbona ungenikuta nimelala kama si muuza mboga mmoja mpuuzi alonikatishia usingizi wangu” Morena akalalamika akiutafuta mswaki wake kwenye stuli pana iliyokuwa na vitu vya kila aina; vipodozi, misumari, kalamu mbovu, dawa zilizokwisha muda wake mpaka karatasi za vocha zilizotumika. Stuli ilijaa hobelahobela!

Akaupata mswaki.

Pasipo dawa aliuchomeka mdomoni na kutoka nje. Alimuacha Fatumata anapitisha macho kwenye kipande cha gazeti kilichotumika kufungia dagaa mchele waliokwishaliwa tangu juzi.

Dakika moja Morena alirejea ndani, akautupia mswaki wake juu ya ile stuli.

“Kwanza nambie jana uliondoka na nani kwani… hukuokota garasa kweli?” Fatumata akamdodosa Morena aliyekuwa anaukagua uso wake kwenye kipande cha kioo.

Kioo kilichokuwa kimetundikwa kwenye msumari ukutani. Aliutazama uso wake, akazitazama nywele zake ndefu zilizopakwa rangi mbili tatu tofauti kiasi cha kufanana na mtu aliyejitwika jogoo kichwani.

Morena akacheka kwanza, kama ilivyo haiba yake. Alicheka akigeuka na kumtazama Fatumata kwa bashasha.

“Mimi huyu, niliyenyonyeshwa mataputapu. Nikalewe zile bia zenu za mafungu” akasonya. “Bia ya tisa nikikurembulia jua nimekuhurumia saaana”

“Kijukuu cha mwana harashi wewe!” Fatumata akashadidia akifinyanga kile kipande cha gazeti na kumtupia Morena, huku akitoka kitandani na kuketi sakafuni. Akatandaza miguu yake huu mashariki ule magharibi.

“Hizi kazi zetu ukijifanya unajua kulewa utakopesha kiuno hicho kila siku” akamjibu na kuendelea “Nimeingia kulala humu saa moja asubuhi” Morena akaachana na kioo na kukifuata kitanda.

“Eh! Nipe… nipe… michapo” Fatumata akasherehesha akipunga mikono hewani.

“Kitu Bokilo” Morena akatamka kwa mbwembwe akinyanyuka na kuketi sawa pale kitandani huku akilitaja jina la mwanaume aliyeondoka naye usiku uliopita.

“Yule Bokilo Mzaire?” Fatumata akauliza kishabiki, akitenga mikono kiunoni.

“Mzaire dada, mutu ya vitenge na bazee” Morena akafanya mbwembwe zake tena akipaza sauti.

“Pedeshee la Bukavu, Kinshasa na kati ya Lubumbashi, mutu ya suruali pande sita” Fatumata akaumalizia utambulisho.

“Kwani zile ni suruali? Kwa upana ule tuyaite mashuka tu dada”

Kikafuata kicheko kirefu cha kugongesha mikono, kisha wakarejea kwenye mjadala wao.

“Alikupeleka wapi? Maana wangu yule majinuni na akili zake za kuhesabu alijua kuninywesha tu. Tumefika kule Bondeni loji kwenye mbuyu akalala puh!”

“Ndani puh!” ikawa zamu ya Morena kushangaa.

“Puh! Nilitamani kumchumia mikwaju nimtandike fimbo za kitambi anijue mie nani” Fatumata hakusemea utani, alimaanisha kiasi cha kumchekesha mwenzake.

“Pole mwaya, mie kwanza alinipeleka gesti moja nzuri balaa maeneo ya Kigogo. Akanianzia na ahadi za mtaji wa biashara, nikaongeza bakora… chapa! chapa!” akakung’uta vidole. “Akaniahidi nyumba nzima. Dada upo?” Morena akalivuta neno la mwisho kwa mikogo mingi, Fatumata akiwa bado amemtumbulia macho.

“Nyumba nzima! Bokilo Mzaire huyo? Ulimvalia na njinjili?” Fatumata akauliza kwa midadi akijishikashika kiuno kumaanisha shanga zivaliwazo na wanawake kiunoni.

“Mie tena, nilimfungia hizi” akafunga dole gumba na kuviacha vinne hewani. “Sio watoto wa siku hizi wanaovamia fani na zigo la shanga ka’ fundo la msuli” Morena akamfanya Fatumata acheke mpaka machozi.

“Asubuhi kaacha elfu 50 kasema baadaye atan’tumia bajaji tukale kuku sekela mahali”

“Usinambie!” Fatumata akamaka. “Ngekewa hiyo dada. Mungu akitaka kukupa-” Fatumata akatamka akikomea njiani kwanza kisha kwa pamoja wakamalizia.

“Hakuandikii barua” wakamalizia kwa sauti za kuimbia irabu.

Wakacheka cheko lingine refu kisha wakatulia, wakiyaanza maongezi mengine.

Ilikuwa kawaida yao, kukutana namna hii na kuzungumzia maisha yao ya ukahaba almaarufu kama uchangudoa. Wangetambiana juu ya wanaume waliowaopoa, pesa walizopata na pengine hata ahadi hewa za hiki ama kile. Lakini pia, mara nyingine ingekuwa huzuni tupu, wangekutana kufutana machozi, kupeana pole na kusaidiana kwa suluba na madhila waliyokumbana nayo.

“Embu kaoge tutoke kwanza, twende mahali nikakupe akili za maisha leo” Fatumata sasa akaweka umakini kwenye mazungumzo yao.

“Kuna nini tena?”

“Kaoge tutoke mwe! hii mijumba yenu isiyo na silingibodi mtu akijamba hapa panya wa chumba cha tatu kule anasikia” Fatumata aliposema hivi Morena alicheka, na wapangaji waliokuwa nje nao wakasikika wakicheka. Dongo lile kuhusu nyumba walilisikia kama walivyoyasikia maongezi mengine yote.

“Kwako kuna nini?”Morena akasaili akinyanyuka toka kitandani.

“Hivi sijakwambia, baada ya ile harusi ya binamu, nyumba imejaa watu kama soko”

“Usinambie!” Morena akamtolea macho.

“Mwenzangu, ukipita nje utasema kuna meza ya muuza mitumba ndani… embu kaoge tutoke bwana” Fatumata akalijibu swali na kumuhimiza tena Morena ajihimu.

Alipotoka kuoga Morena alirejea chumbani kwake. Pasi kujali uwepo wa rafiki yake, akaitupilia mbali ile khanga moja iliyokuwa imesitiri maungo yake na kuanza kuranda mle chumbani akijipaka mafuta, akitafuta nguo ili mradi alikuwa na hekaheka za hapa na pale.

Morena alikuwa mrefu wa kadiri, ungemtazama kwa haraka haraka ungedhani ni mwanamke wa kisomali. Vile alivyojaaliwa nywele ndefu laini na wajihi mwembamba kiasi wenye pua iliyonyooka. Watu wengi walihisi Morena alikuwa na usomali ndani yake.

“Haya shanga ushatupa kule, kwanza huo mkufu kiunoni hauchuji?” Fatumata alimtupia swali mwenzake akimtazama vile alivyokuwa akimkatishia mtupu kama mwanga, huku akiuvaa huo mkufu wake.

“Dhahabu yenye gramu zake hii sio cheni zenu za vyuma chakavu ukinunua leo mtondogoo kutu imekutoa mapunye” Morena akajibu akianza kuvaa nguo zake.

“Hivi ulidunduliza miezi mingapi? halafu umenikumbusha Bintuni na cheni lake la kuhongwa”

“Yule nusura tumpeleke India kwa matibabu, sijui aliuokota wapi mcheni mzito kama mnyonyoro wa geti” Alidakia Morena na kuzua kicheko kingine mpaka kwa wapangaji waliokuwa koridoni wakidoea mazungumzo yao.

Morena alipomaliza kuvaa na kujipara, akajipulizia manukato yake. Manukato ghali kidogo kulinganisha na kipato chake cha kuungaunga.

Pamoja na uduni wa maisha yake na uzito wa majukumu aliyokuwa nayo, Morena hakuacha kujitafutia vitu alivyovipenda kwa dhati. Hata kwa kudunduliza senti moja kila siku, angeweka bila kusita wala kuchoka, aliamini haba na haba hujaza kibaba. Morena alipenda vidani vya dhahabu, na aliyapenda manukato.

Akamgeukia Fatumata.

“Haya twen’zetu sasa” akatamka huku akiufuata mkoba wake na kuweka sawa baadhi ya vitu vyake.

Wakatoka pamoja mpaka nje ambako walianza kutembea pole pole huku wakishauriana pa kwenda. Papo hapo, Fatumata akichombezea hizo akili za maisha alizotaka kumgawia mwenzake. Aliuremba mpango wake kiasi cha kumtia kiwewe mwenzake.

“Hili dili lililonifungisha safari likitiki… tutaununua huu mtaa mzima somo!” Fatumata akamfanya Morena adondoshe mguno.

“Ngoja tufike basi Kha!” akamtoa papara huku akijiandaa kuvuka barabara kuelekea mahali ziliposimama bodaboda.

Taratibu wakakaza mwendo kuwahi kupeana hizo akili za maisha. Wasijue tu namna ambavyo akili hizo zingekuja kuigharimu furaha yao maishani.

2

JUA la saba mchana liliwaka hasa!

Liliwakutia mgahawa maarufu wa Vitukoutata, maeneo ya Vingunguti. Kila mmoja alikwishaagiza chakula chake. Wakakishambulia chakula hicho haraka haraka, kana kwamba walikuwa wamekikamia.

Morena alikuwa wa kwanza kumaliza kula. Akamwita mhudumu amletee maji ya kunawa. Maana, mchuzi wa kongoro ulikwishamganda mikononi. Ikawa kero kwake. Wakati mhudumu anafika na beseni lake mkononi, Fatumata naye akawa amemaliza chakula chake. Akajiunga kwenye kunawa.

“Shing’ ngapi?” Fatumata aliuliza huku akikimbilia kutoa kijiti cha meno kwenye kichupa chake mara tu baada ya kumaliza kunawa.

Morena yeye alihangaika kuyachokonoa magego yake kwa ulimi.

“Vishalipiwa mbona!” Yule mhudumu alijibu akitabasamu, akiufurahia pia mshangao wa wanawake wawili mbele yake.

Wakatazamana kwa bashasha. Wakaendelea na mambo yao pasipo hata kusaili ni nani aliyewalipia. Nyakati zingine ofa kama hizi zilikuwa za kawaida kwao, hasa akiwepo Fatumata Mzinga. Wangelipiwa chakula, nauli na huenda wangepata ahadi za kupelekwa huku na kule kisha kuzungumza biashara.

Wateja wao walikuja kwa njia mbalimbali.

“Tawire! Haya leta habari habibti” Morena alijiweka sawa tayari kumsikiliza rafiki yake.

“Unamkumbuka yule bwana alonileteaga dili ya mawese?” Fatumata akaianzia mbali habari yake. Akakitupa kando kijiti cha meno.

“Bwana we hayo ya nani anafanya nini utanichanganya tu, hao mabwana zako wauza mawese nawajua kumi na…” Morena akajibu, akimfanya Fatumata amtukanie ukoo wake, akaliunga na tusi lingine la nguoni na Morena asijali.

“Kimboka” Fatumata alipolitaja jina Morena akadakia.

“Yule mpuuzi. Haya kafanyaje?” akauliza kwa sauti ya mkwara.

“Hujasamehe tu!”

“Muuza mawese yule aliyetaka kutulaza ndani kwa bia zake za mafungu.” Akasonya.

Uso wa Morena haukuwa na masihara hata kidogo. Alimpindishia mwenzake midomo.

“Tukio la mwaka juzi bado linakupandisha mavi ya kifua tu! Punguzaga vinyongo unenepe shaa!… embu sikia, Kimboka ana dili la mamilioni somo!”

Akayatumbua macho kimbeya.

Aliianza tena habari yake kwa madaha. Akimfanya Morena aukunje uso na kumeza mate mithili ya mtu aliyelambishwa kitu kichachu.

“La kuuza mawese yake?” Akauliza kwa dharau akibetua midomo.

“Sio mawese jamani!”

“Kumbe!?”

“Madini!” Alilitamka neno madini kwa sauti ya chini akikisogeza kichwa chake mbele zaidi ili Morena amsikie vizuri pamoja na kule kunong’ona.

Morena alitoa macho kana kwamba alichotamka Fatumata kilikuwa kitu cha kutisha mno. Akauliza kwa sauti ya mshangao. “Madini?”

“Mdomo huo mwanamke, shiii!” Fatumata akamuwahi, akimtaka apunguze sauti.

Morena akafunga mdomo wake wa kiganja chake cha kuume huku bado jicho likiwa limemtoka pima. Taratibu akamtazama mwenzake kama zumbukuku.

“Jela unaijua lakini Fatumata?”

“Jela ya nini?”

“Jela hizi za Segerea, Ukonga sijui Butimba?”

“Mie nilimsikia anaongelea biashara ya madini, sasa jela inahusikaje?”

“Mmh! Madini mwenzake utapeli Fatu, lakini haya! Kila la kheri kwenye huo mpango wako. Mie n’taendelea kuibia wanaume kwa mtaji huu chini mpaka siku yangu ikifika.” Alizungumza akiutazama huo mtaji wake.

“We huzitaki pesa?”

“Nazitaka ndio, ila hizo mishe mishe za lala apache alolo amka Bakhresa, Bongo hii, haya!”

“Mbona unan’tisha na sijamaliza, unajua nimekuita sababu kuna lingine na ndio hilo linaloniumiza kichwa?” Fatumata alimtazama mwenzake kwa uso mkavu usio hata na chembe ya utani.

Morena naye akamtazama kwa umakini kidogo, moyo ukimtokota. Alishaingia woga ghafla. Akauliza mboni za macho zikicheza kulia na kushoto kwa kasi ya ajabu. “Kitu gani?”

“Kuna kiroba cheusi hicho tukishikamana tunatoka huku uswazi”

“Eeeh!”

“Punguza mchecheto basi!”

“Haya niambie kuna nini kwenye hicho kiroba?” Morena akajiweka sawa, akitazama huku na kule kana kwamba alihofia watu wangewasikia wakiongelea mambo ya viroba.

“Ndio maana n’kakutoa kule kwenu.” Fatumata alimzodoa mwenzake, akiucheka ule mchecheto wa Morena. Huku akitaka kuziweka sawa akili za mwenzake, Fatumata aliendelea. “Sikia, wiki iliyopita, siku ile tuliyokesha Kiwalani sijui unaikumbua…”

“Tunakesha mara ngapi uko Kiwalani? We n’ambie moja mbili tatu basi!” Morena aliona anachelewa kuijua habari yenyewe.

“Haya twende, nililala kwa Kimboka pale, unajua tena kusikia mamilioni kidogo niingie wehu, sasa vile jasiri haachi asili….” Fatumata hakumalizia, Morena akamdaka.

“Ukaiba?”

“Hebu bwana we kha!” Fatumata alianza kukerwa na kule kukatishwa katishwa kila mara.

“Sikuiba, nilikuwa nafanya doria, nikatokezea stoo moja uchwara umo ndani. Na hapo ndio paliponifanya nikuite hapa n’kupe akili za maisha.” Alijieleza huku mwenzake akiitikia tu chapuchapu. Kichwa kikienda juu chini juu chini mara kadhaa.

“Nilikuta viroba hivi…” Alivikutanisha vidole vyake vya mikono yote kwa pamoja akimaanisha kumi.

“Enhee!” Morena akaendelea kuitikia.

“Nikafungua kimoja kidogo dogo. Nilichokiona sasa aaah!” Fatumata akanesa nesa akifuatisha maneno aliyoyatamka kwa kupanda na kushuka.

Morena hakumdaka, alimfuata kwa macho alivyonesa kulia na kushoto akingoja kuisikia habari kamili.

“Almasi!” Fatumata alimalizia mithili ya mtu aliyeubwaga mzigo mzito kupitiliza.

“Almasi!? Unazijua almasi wewe au unazisikia tu? Ukute uliona vipande vya chupa ukajua almasi.” Morena hakumwamini kabisa.

“Nimekuja mjini na lori za mpunga huku waitukei inatikisa dunia naanzaje kutoijua almasi? Mungu na Mtume vile ni almasi pyuwa!” Fatumata alisisitiza, akipitisha kidole cha shahada shingoni na kukinyooshea juu kuapia.

“Sasa?” Morena akaomba dira ya mwito.

“Nataka n’kitaifishe kimoja, tunakimbilia zetu Zambia au Msumbiji hapo, tunakula maisha huku tunasikilizia kwanza, kisha tunarejea kulijenga taifa. Naamini hata hela ya kumlipa tutakuwa tumepata.”

Morena alimtazama mwenzake kama vile alikuwa anaisoma hiyo ramani ya kufika Zambia usoni pa somoye. Kisha, akaguna akipiga kofi moja hafifu hewani.

“Shosti hebu tuagize bia ya baridi kwanza, hiki unachoongea ni kama vile koo limekukauka sana mwenzangu. Ukurupuke na kiroba cha watu uko, ukimbie nacho wapi sijui, ujifiche siku mbili tatu, urudi kuishi maisha ya kawaida? Narudia tena na tena hivi unaijua jela wewe? Unaijua almasi?” Morena hakuelekea kukubaliana na mwenzake.

“Umaskini matusi somo! Mie nimeuchoka. Na tatizo lako uoga umekuzidi pia. Hapo ulipo, umri unaenda bado umebanana mule kwenye chumba kimoja chenye dirisha moja. Mwili unaporomoka huo hata gari ya mtumba huna!” Fatumata aliuongea ukweli unaochoma nafsi.

“Kwa hiyo?” Morena akabweta.

Maneno ya Fatumata yalimkwangua roho. Hata hivyo, wazo la kukiiba kiroba halikumwingia.

“Maisha ukitaka kuyapatia lazima kuna mbilinge upitie.” Akamshawishi tena.

Mwenzake wala hakumsikiliza. Aliangaza huku na kule kama mtu anayetafuta kitu.

“Psiiiii! We kaka!” Morena alimwita mhudumu aliyepita karibu yao. Akamwagiza. “Niletee maji madogo ya baridi.”

Naye Fatumata akadandia. “Na mie niletee.”

Mhudumu alipoondoka wakatazamana tena.

“Kwa hiyo?” ikawa zamu ya Fatumata. Akiutafuta msimamo wa mwenzake.

“Wahenga walisema, mchuma janga….” Morena hakumalizia.

Fatumata naye alimkatisha. “Umeanza mambo yako, Kiswahili chenyewe ulipata mswaki huko shule. Ungewaelewa sana hao wahenga ungekuwa na mijidigriii leo. Si wanasemaga elimu ndio ufunguo wa maisha?”

Akamsuta mwenzake, akimpindishia midomo upande.

Morena akacheka.

Akili za rafiki yake zilikuwa za mafungu mafungu kama zake tu, ingawa kidogo yeye alimzidi mwenzake wepesi wa kuelewa. Aliwaza. Fatumata na umbole sheshe alilokuwa nalo, ungempa karatasi akuandikie hata hilo jina lake la Fatumata, si ajabu ungeitisha umati wa Mtume ukusaidie kusoma! Katu, asingekosea kama angeamua kumuita shogaye mbumbumbu mzungu wa reli.

“Kimboka anajua ulikiona hicho kiroba?” Morena aliuliza. Wakati huo, mhudumu alirejea na chano chenye chupa za maji na bilauri. Walipokaribishw

a, waliendelea na maongezi yao.

“Kimboka anajua?” Morena akalirudia swali lake.

“Angekuwa anajua nisingekuja hapa. Najua hajui na mle ndani mwake anaingiza dazeni kwa dazeni ya wanawake. Hivyo, anaweza asijue kabisa nani kamkwapulia. Huoni godeni chansi hiyo?” Fatumata akasisitiza.

“Naona na kizungu cha kuongelea uko Zambia ushajifunza tayari. Mambo ya golden chance, sijui good morning – how are you teacher – I am fine – thank you au siyo eeeh?” Morena alitamka akiigiza lafudhi ya Kizungu.

Wakaangua kicheko, wakigonga viganja vyao.




****

PAKA ndiye wa kumpa sumu. Kumpa mbuzi ni kumdhulumu.

Swadakta! Morena alikuwa kama mbuzi aliyekabidhiwa sumu. Fatumata alimdabika kisawasawa na ile habari ya kuiba kiroba cha almasi kwa Kimboka.

Hakuyazoea mambo haya. Hakuwa na mkono mrefu. Haikuwa haiba yake kuchukua ambacho si chake. Kisebusebu. Roho ilimchonyota. Pesa aliitaka. Aliitaka sana tu na ushawishi wa Fatumata ulivyomvika nguvu, Morena akayavua mashaka na kuamua kujitosa.

Siku ile, walizunguka mjini kama watalii. Baadaye, walikwenda kula nyamachoma na bia za ofa kwa Bokilo, mteja wa Morena. Walipotoka huko, walirudi Vingunguti, kwa Morena. Wakalala hapo. Senti mbili tatu alizoshika toka kwa Bokilo zilimpa jeuri ya kuupumzisha mwili kwa siku hiyo.

Morena Malizozo alikuwa msichana wa miaka ishirini na saba tu. Lakini, kwa sababu ya pombe na hekaheka za kujiuza ili aweze kuyamudu maisha, ungeweza kusema alikuwa anaikimbilia miaka arobaini tangu alione jua.

Waama, shida zilimkongoroa. Ila, hazikuufuchama uzuri wake wa asili. Katikati ya dhiki zake, ulimbwende wake uliwaka kama kandili hafifu gizani. Isingehitajika darubini kung’amua ni wapi uzuri wake ulikopotelea. Ni dhahiri, maisha yalimpigisha kwata.

Utoto wake ulidhulumiwa na majukumu mazito aliyobebeshwa angali mtoto. Akiwa binti mdogo, asiyejua lila wala fila ya ulimwengu. Usichana wake ulishambuliwa na utu uzima uliomjia ukiwa umevikwa koti la umasikini.

Morena hakuwa na elimu wala ujuzi wowote wa maana. Angeupata wapi na ufakiri uliung’ang’ania ukosi wa maisha machungu aliyoyavaa tangu angali tumboni. Elimu ya darasa la saba aliyokuwa nayo, aliimaliza kwa mbinde, ikimuachia uwezo wa kusoma, kuhesabu na kuandika tu.

Alikuwa na kesi za shule kila siku; utoro, uchafu, ujinga, kukosa pesa ya michango ya hiki na kile. Shule aliiona chungu, mawio hadi machweo.

Alipozaliwa, Morena aliwakuta ndugu zake watatu waliomtangulia. Akawashuhudia wengine watatu waliozaliwa baada yake. Kila mtu na baba yake. Wakakua wakijifunza kujitunza na kujiongoza.

Mama yao aliyekuwa muuza pombe za kienyeji, aliwaletea baba tofauti kila uchao. Mwishowe, wakazoea kuita baba kila mwanaume aliyezama chumbani kwa mama yao. Neno baba likakosa thamani mbele yao. Likapungua uzito. Hatimaye, kupoteza maana.

Hakuyapenda yale maisha yao hata kidogo, lakini ndiyo vile mtu hajichagulii pa kuzaliwa. Maisha ni kama chakula kilichofunikwa na kawa. Hujui ni chakula gani hadi kawa lifunuliwe; hujui kina ladha gani mpaka uchote ukionje. Unayafunua maisha ukishazaliwa, unayaonja ukianza kuyaishi!

Basi angesoma ili ajikwamue, lakini angejikwamuaje na kilabu cha pombe kilimsubiri kila alipotoka shule. Kama si kilabu, basi angepewa chano kubwa la mahindi ya kuchemsha akalitembeze stendi ya mabasi. Angerudi akiwa hoi, hoi bin taabani. Mwili wote ukiushtakia uchovu wa kutwa nzima. Angejiunga na mama yake kuuza pombe mpaka usiku mnene. Dakika mbili tatu za kuinamia daftari ili apate kujisomea, angesinzia, angetopea usingizi mpaka adhana ya alfajiri.

Mzunguko wa maisha yake, ukawa hivi kila iitwapo leo.

Kuna wakati alitamani kuyakimbia maisha yale. Alitafakari kwa kina katika ule umri wa miaka tisa. Akaona pengine amtafute baba yake mzazi, huyo Mzee Malizozo. Aliwaza, labda angeliiona ahueni katikati ya ile dhiki.

Kama ambavyo mlilala handingwa handingwa mwenye macho haambiwi kula, ndivyo ilivyokuwa kwa Morena kusubiri mama yake amueleze mwenyewe alipo baba yake. Haikutokea!

Usiku mmoja, baada ya kufunga hesabu za pombe, akajitosa. Akamwuliza mama yake, mahali alipo baba yake. Alichojibiwa, kilimkalfisha.

Mama yake mzazi alimporomoshea matusi ya nguoni. Akamtukana kiasi cha kutosha. Akitishia kumpa laana ya maisha endapo angemsaili tena kuhusu baba yake. Morena akalala usiku ule akiutazama ukuta machozi yakimtiririka. Hakuliona kosa lake. Akalazimika kuzibana hata kwikwi za kilio akichelea kuambulia kipigo toka kwa mama yake.

Aliumia zaidi kwa kuwa hata ndugu wachache aliowafahamu upande wa mama yake, ilisemekana si ndugu wa damu. Hakujua alikotokea mama yake, naye hakutaka kusailiwa juu ya hilo. Alisononeka zaidi, kujua yeye pia angefuruka na kuzeeka pasi kujua asili wala fasili yake.

Lahaula!

Ikawa mwanzo na mwisho wa Morena kumfikiria baba yake. Hakuthubutu tena kumuulizia fakaifa kumtaja kwa bahati mbaya. Maisha yakaendelea.

Morena alivunja ungo alipofikia miaka kumi na miwili. Matiti machanga yalianza kusimama. Umbile la kuvutia likaanza kuchomoza. Miluzi ya hapa na pale ikamsindikiza. Walevi kilabuni wakaanza kumshikashika.

Alijua amekua!

Mabadiliko aliyoyaona hakuyaelewaelewa. Lakini sasa, nani angemweka kitako amweleweshe? Hakuna. Alipambana nayo mwenyewe alivyojua, kimya kimya.

Maisha nayo yalimpiga danadana. Hakuwa na hakika ya sare ya shule, wala mahitaji mengine muhimu. Alibangaiza kwa kudokoa kidogo pesa za mama yake. Mama mwenyewe, wala hakuwa na habari na shule. Kitu pekee alichokifanya, kilikuwa kumwandikisha Morena shuleni. Mengine, atajuana nayo Morena mwenyewe.

Mara moja moja sana, mama yake angekumbuka kumpa mafuta ya mgando ya kujipaka mwilini. Tena ambayo, mara zote ni kwenye chupa iliyo mbioni kubakia tupu. Morena angeikwangua hadi mgando wa mwisho. Kukwangua kwenyewe kungeambatana na maumivu ya viganja vyake, kuingiza vidole hadi kwenye sakafu ya chupa ya mafuta. Chupa yenyewe, aliyopewa kwa masimango.

Si kwamba mama yake hakumudu gharama za hapa na pale katika kumhudumia. Hata kidogo. Aliingiza kipato japo kidogo, kupitia biashara yake ya pombe. Ila sasa, alitumia kipato hicho kuwahonga vijana kadha wa kadha pale kijijini. Aliwahitaji, wamtimizie haja za mwili wake.

Jambo hili lilimuumiza vilivyo Morena. Afanyeje sasa, ilhali huyo ndiye mama yake? Afadhali basi, Morena aliwaza, walau angewafahamu ndugu wengine wa mama yake. Hao wachache aliowafahamu, kila mmoja alitingwa na hamsini zake. Hivyo, Morena aliendelea kuwaza, mkono asioweza kuukata, yampasa aendelee kuubusu.

Kuna nyakati, Morena aliikosa hata pesa ya sabuni. Shule nayo, haikumweka salama dhidi ya viboko kila alipokwenda akiwa na nguo chafu. Si tu uchafu, bali pia, uchakavu. Viboko vikawa sehemu ya maisha yake ya shule. Leo, angekula vya viatu vichafu na vichakavu. Kesho, vya kukosa ada ya mtihani. Keshokutwa, kwa kukosa kalamu na madaftari. Mtondo, kwa kukosa vitabu alivyoagizwa na walimu kuvinunua. Mtondogoo, kwa kusinzia darasani kutokana na kukesha akimsaidia mama yake kuuza pombe kilabuni.

Angelala kwa saa mbili tatu tu baada ya pilika za kutosha kuhangaishana na wateja walevi kilabuni. Jumlisha adha za hapa na pale alizokabiliana nazo kila siku. Kuamka alfajiri, kutafuta kuni za kuchemshia chai iliyonyweka mara moja moja sana. Zaidi, angechemsha uji, na kuutia chumvi. Angeunywa kabla ya kwenda shule.

Pamoja na mchakamchaka huo wa maisha, Morena alimaliza elimu ya msingi. Hakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari. Hilo alilitegemea. Alifahamu fika, kufaulu kwake kungekuwa miujiza.

Akaendelea na maisha yasiyokuwa na muamana juu yake.

Siku moja yakamkuta!

“Umeshakuwa mtu mzima sasa mwanangu na wewe tafuta hela ya matumizi tusaidiane majukumu. ” Mama yake alimtolea uvivu siku aliyomwomba pesa ya kununulia gagulo mnadani.

Alimuelewa. Roho ikamuuma hasa. Alijua alichopaswa kukifanya ili kusaidia hayo majukumu mle ndani. Mama yake akasitisha rasmi kumpatia hata ile pesa ndogo ya mafuta.

Tayari alikwishatimu miaka kumi na nne. Chuchu za kisichana zikachomoza kifuani. Waama, zikitishia kuitoboa fulana hohe-hahe aliyoivaa. Mama anamwambia atafute pesa zake. Azipate wapi sasa? Njia moja rahisi ya kujiingizia kipato ikamjia kichwani.

Kulala na wanaume, apate wake ujira.

Alianza taratibu. Siku za mwanzo zilikuwa za maumivu makubwa kwenye viungo vyake. Hakuwa na namna. Baada ya shughuli, alijibanza maliwatoni akijikanda. Machozi yalimdondoka pasi ajizi. Akajikaza. Alifahamu anapaswa kukomaa. Akakomaa kweli, akazowea. Ikafikia wakati, alimudu kulala na wanaume zaidi ya watatu, usiku mmoja!

Nyakati zingine, alisononeka. Ah! Mungu wangu mpaka lini? Nyakati zingine angejiuliza kwa nini hakuzaliwa kwenye familia zenye ahueni kama wenzake? Kwa nini maisha yalikuwa hivi kwake? Hakukuwa na wa kumpa majibu, fakaifa hata wa kumpa maneno ya kumtia moyo wa kupambana na madhila yale peke yake. Hakuwepo! Pepo kwake ilikuwa nyeusi ti!

Kipindi hicho, mama yake alikwishaanza kuumwa hiki na kile. Akawa mtu wa kuuguzwa. Wakahisi ameukwaa UKIMWI. La hasha! Walipima na kupima. Hawakuona walichokihisi. Aliendelea kuugua tu. Mara alalamike mgongo, mara miguu, ama kichwa. Ili mradi, hakuna magharibi iliyopita asiwe katika hali ya kunung’unikia maumivu.

Ikasemwa mitaani amefanyiwa ushirikina. Tabibu mmoja akawaambia, kinachomsumbua zaidi, ni msongo mkali wa mawazo. Hili la msongo hawakulimaizi. Walichagua kuamini katika ushirikina. Ilikuwa rahisi kwao kulielewa hilo kuliko kuambiwa mawazo yakizidi huleta ugonjwa. Potelea mbali! Ikabaki kusemekana mpaka leo hii, usiku huu. Morena alipokuwa ameitumbulia macho dari pasipo kuitambua akilini. Mama yake huko alikokuwa alikuwa mgonjwa wa kuchechemea.

Alifanya yote aliyoyafanya hapa mjini, ili kila wiki atume pesa kidogo nyumbani kwao. Wadogo zake wajikimu na walio shuleni wasome. Kamwe, hakutaka na wao waishie alikoishia yeye. Aliifanya kazi yake dhalili katika mazingira magumu mno, aliifanya kazi ngumu iliyomuondolea utu na heshima kwa jamii ili tu wadogo zake wapate elimu.

Elimu aliyoamini ingewakomboa toka katika lindi la ufakiri.

Morena alilengwa na machozi wakati alipokumbuka alipotoka na kutazama pale alipokuwa sasa. Akajikuta tu tamaa ya kushirikiana na Fatumata kuiiba hiyo almasi ikimtekenya kupitiliza huku ujasiri ukimpapasa mbavu polepole. Aliuchoka ufakiri, naye akataka kuijaribu bahati yake.

Akiamini tu, huenda ni kweli mgagaa na upwa hali wali mkavu!

Laiti tu angejua!



3

MORENA alibadili uchago na kujilaza kiubavu. Huko alikogeukia alilala akimtazama Fatumata aliyekua ametopea usingizini. Alimtazama tu na kutabasamu. Huyu alikuwa ni rafikiye wa utotoni mpaka sasa utu uzimani.

Mwenzake ahueni ndogo ya maisha ilishamtembelea, alitangulia kuja mjini. Lile umbile lake murua walau lilimjalia kupata wa kumpa vya kumuwezesha hata kupanga upande mzima wa vyumba vya uani, ila kichwani ndiyo vile alikuwa mtupu kuliko mtungi uliotoboka.

Mungu hakupi vyote!

Usiku ule alilala usingizi wa kuvizia. Ilipotimu alfajiri ya saa kumi na moja akawa wa kwanza kudamka. Akaketi kitandani huku moyo wake ukiwa bado unamsokota. Alichotaka kukifanya hakikuwa sahihi, lakini mangapi yasiyo sahihi amekwishayafanya hadi sasa? Hata leo hii aliogope hili la kuiba? Akawaza, akawazua!

Aligeuza shingo polepole na kulitazama dirisha. Akalitanua pazia na kulitazama anga la Karima. Kwa dakika zile alizoketi pale aliushuhudia ulimwengu ukipambazuka na ule utusitusi wa alfajiri ukikimbizwa na ujio wa siku mpya. Alijikuta tu akitamani maisha yake yabadilike kirahisi namna ile, kama pambazuko lile.

****

Pilika pilika za kuashiria kumekucha zilikwishaanza. Sauti za wapangaji jumlisha na miburuzo ya viatu, achilia mbali honi za pikipiki kwa baiskeli vilifanya utulivu ufungashe virago na kwenda masafa ya mbali zaidi.

Morena alikuwa bado kitandani kwake pale pale. Safari hii akiwa peke yake. Fatumata alikwishaamka na kuelekea msalani. Mlango ukafunguliwa na Fatumata akaingia akirusharusha miguu huku mikono ikiwa imekikamata kibofu chake kana kwamba kilitaka kuchomoka. Alizunguka kama tiara.

Akaenda, akarudi, akapunga mikono hewani na kukishikilia tena kibofu chake. Alilalamikia haja ndogo iliyokuwa imembana kupitiliza.

“Ah! Kwani chooni kuna nini!?” Morena alimwuliza, akimshangaa. Papo hapo akijisikia kucheka kwa namna ule mwili wa Fatumata ulivyokuwa ukitikisika. Ufundi wa Mungu ulidhihirika.

“Kuna foleni na mtu ‘uko ndani sijui anajisaidia kamba… basi aah!” Aling’aka.

Morena aliinyoosha shingo mbele. Akachungulia kule mlangoni. Kwa vile mlango ulikuwa wazi, alimwona mpangaji mwenzake aliyekuwa akizoa taka mlangoni pake.

“Mama Sara eti chooni kuna nani jamani?” Morena aliuliza akisotesha matako ili kuteremsha miguu sakafuni.

“Sinasudi huyo na bwana yake wanakoshana uko masaa… Si unajua kuna watu wanajikuta wazungu kila mwisho wa mwezi!” Mama Sara alijibu akiwa amegeuka kabisa kumtazama Morena ambaye sasa alishateremka toka kitandani na kwenda kusimama karibu na mlango.

“Wazungu wako Masaki ’uko wanakogea masinki, sasa maji ya kujaa kisadolini nayo ya kukogeshana?” Alisonya akimgeukia Fatumata. “Chukua kopo chini ya uvungu hapo ujisaidie!”

Morena alitoka pale mlangoni. Aliikamata korido akielekea huko msalani. Aliwakuta wapangaji wenzake wamefura. Kila mtu akisema lake, huku misonyo ikiwamba eneo zima.

Aliutazama mlango wa msalani. Khanga na taulo vilining’inia mlangoni hapo.

“We Sinasudi hebu toa basi hicho kikaragosi chako humo ndani watu waoge bwana!” Morena aligomba kwa sauti ya juu hasa, ikipokea ushirikiano mkubwa toka kwa wale wapangaji wengine pale nje. Walishambulia kwa maneno na wengine wakifanya mizaha iliyowavunja mbavu.

Zikapita dakika kadhaa, ile khanga ikavutwa kwa ndani, na lile taulo likafuatia. Watu wote waliukodolea macho mlango. Sinasudi alitangulia kutoka, akifuatiwa na mwanaume nyuma yake. Hakusemezana na mtu licha ya wapangaji wenzie kumsindikiza na maneno ya kukera.

Ni kama hakuwasikia, nao wakaachana naye na kuendelea na shughuli zao. Haikuwa mara ya kwanza kwa Sinasudi kuwakera wenzake namna hii kila mpenzi wake alipomtembelea. Kero kama hizi zilikuwa sehemu ya maisha yao katika nyumba yao ya kupanga ambayo choo na bafu vilikuwa sehemu moja.

Zilikuwepo kero zingine kedekede. Leo, wangesutana kwa umbeya. Siku nyingine, wangeshikana mashati na kutoleana maneno makali wakigombea foleni ya kukinga maji bombani ama zamu za kununua umeme. Wakati mwingine wangeamka na ugomvi wa zamu za kusafisha choo chao kiasi cha watu kuapizana kutozikana. Na baada ya siku mbili tatu ungewakuta wakisogoa na kuteta kama si wao.

Morena alirudi chumbani kwake huku koridoni wachache wakiendelea kuzoza.

“Mmemalizana?” Fatumata akamsaili wakati akiingia chumbani.

“Tushamsuuza na bwana’ake huyo mwenye komwe ka’ kifuu cha kutwangia dawa, akija hatuhemi dada!” Alisonya akimfanya Fatumata acheke wakati akiliweka uvunguni lile kopo lenye mkojo.

Morena alikifuata kitanda. Akaketi hapo, mwayo ukimvamia na kumtangazia njaa.

“Sasa inakuwaje?” Aliuliza akipiga mwayo mwingine kiasi cha kumletea cheche za machozi machoni.

“Tunywe hata chai kwanza, kisha ndio nikupe mpango mkakati.” Fatumata naye akapiga mwayo alioubembeleza kwa kupiga piga mdomo wake kwa kiganja.

“Ila wasiwasi wangu ni mambo yakienda kombo! Mie n’na mama mgonjwa mwenzio, nikipotea miezi tu nitaiua familia kwa njaa.” Alijitetea Morena.

“Kwahiyo ukifa na wao watakufa? Wadogo zako washakuwa watu wazima wale nao waanze kukata viuno sasa msaidiane majukumu!” Fatumata alimjibu kimasihara na asijue kauli kama hiyo ndiyo iliyomfikisha mwenzake kwenye maisha haya aliyonayo.

Morena akatikisa kichwa kwa masikitiko huku akinyanyuka toka pale kitandani. Akaenda zake kutafuta staftahi.

Jioni ya siku ile, Kimboka, mpenzi wa Fatumata aliwapigia simu akiwataka waende Wanyama Hotel, Sinza. Wakati wakijikwatua, Fatumata akaamua kumweleza Morena mpango mzima utakavyokuwa. Waliongea kwa sauti ya chini kidogo kuepuka kusikika hadi nje.

“Mmh! Daudi Chochoro? Yule anaweza kukaa na siri kweli?” Morena alionyesha shaka mara tu alipotajiwa huyo dereva teksi ambaye wangemtumia katika shughuli nzima.

“Sasa nani mwingine wa kumtumia? Daudi mtu poa sana, tutamkatia jiwe ili aogope kusema maana atajua akijichanganya tu tutasombwa wote.” Fatumata alijaribu kumtoa hofu.

“Kwa hiyo ukinibeep tu ndio nizunguke ukirushe au ukibeep itamaanisha umeshakirusha?” Morena aliachana na kazi ya kupaka wanja akamgeukia mwenzake, akiuliza maswali aliyotaka yamtulizie nafsi yake.

“Nitakuwa nimeshakirusha yaani wewe na Chochoro mkisikia ndindili ndindili…” Aliuigiza mlio wa simu, akaendelea. “Wewe zunguka nyuma chukua kiroba kimbilia teksi ya Daudi na yeye aondoe gari moto… Hakuna kusimama mpaka muwe na uhakika mko salama. Ikibidi mzunguke kidogo mjini kupoteza maboya kama kuna mtu anawafuatilia.” Fatumata aliongea kwa ujasiri.

“Hatariii! Kama muvi la misukosuko vile!” Morena alihisi matumbo yakimcheza.

“Yaani msikosee Morena, mi n’tahakikisha siachi alama yoyote na nyie ndio kabisa mhakikishe mmetoka salama.” Fatumata alisisitiza akizidi kumtia mwenzake hali ya mshawasha.

Walipomaliza kujipara, waliita bajaji tayari kwa safari yao.



Walianzia starehe zao Wanyama Hotel. Wakati wengine wakiburudika, kwa Morena havikulika vikashuka. Alikuwa na wahaka uliompeleka msalani kila dakika. Alijisikia kuhara, wala asihare fakaifa kushuta tu. Moyo haukudunda kawaida tena, ulikwenda mara mbili ya mshale wa sekunde. Ta! Ta! Ta! Ta!

Alichachatika! Wizi haukuwa hulka yake abadani. Pombe zilizotapakaa mezani aliziona kama chupa za sumu. Hazikunyweka!

Usiku wa saa sita kasoro vichapo kadhaa, starehe zao zilifikia ukingoni. Kimboka alikuwa anayumba kwa ulevi huku akiwa na mpenzi wake ubavuni. Kwa mahaba ya uongo na kweli, alioneshwa mpaka sehemu za kukanyaga wakati akilifuata gari lake. Morena yeye alizuga kuaga kuwa anarejea kwake Vingunguti.

Marafiki wa Kimboka nao walinyanyuka. Baadhi yao, kwa safari za kurudi makwao na wengine wakiwa na nia ya kuhamia kiwanja kingine cha starehe. Kila mmoja alikuwa anaondoka eneo lile. Fatumata alimtazama Morena akimkazia macho. Macho ya kusisitizia mipango waliyoongea.

Moyo wa Morena ulidunda dabali, ni kama vile aliyahisi matatizo, na kuzinusa dalili mbaya; hakuwa huru nafsini hata kidogo. Ujasiri mdogo aliokuwa nao ulimwezesha kutembea japo kwa kujikanyaga kanyaga kana kwamba alihisi kuna watu walioyaona mawazo yake.

Alikwenda kujibanza mahali, akitaka kuhakikisha kwanza watu wote aliokuwa nao wameondoka. Kisha taratibu alijichomoa toka kwenye eneo alilokuwa amejibanza. Akasimama kwenye njia iliyopita nyuma ya ile hoteli.

Ukimya mkubwa uliotamalaki eneo hilo ulimdabua kidogo. Ulikuwa ukimya uliomfanya akiogope hata kivuli chake. Aliangaza huku na kule akiitarajia teksi aliyokuwa anaisubiri. Walikwishakubaliana mawasiliano pekee yawe ile beep na kwamba dereva teksi, Daudi Chochoro, angepita saa sita kamili kumchukua Morena hapo alipokuwa. Waende sehemu waliyopanga kujibanza.

Morena aliitazama tena simu yake kwa minajili ya kujua muda.

00:47 pm

Maandishi ya saa yake kwenye simu yalimfanya azidi kupungukiwa subira. Zilikwishapita dakika arobaini na tangu muda wa makubaliano. Kulikuwa na tatizo gani? Akawaza mamoja kwa makumi ndani ya muda huo mfupi.

Ni vipi kama Daudi Chochoro amebadili mawazo? Akawaza tena ilhali hofu nayo ikizidi kumtomasa maungoni na kumchachafya.

Wakati akiangaza huku na kule, miguu nayo ilianza kumwuma. Alishasimama pale kwa muda mrefu wa kutosha kutembea hata nusu kilometa. Alipotaka kuchutama alimwona mtu akija upande ule aliokuwa amesimama. Mtu huyo alikuwa peke yake. Alikuja kwa mwendo wa taratibu. Mavazi na umbile lake vilimjulisha kuwa ni mwanaume, tena kipande cha mtu.

Morena alimeza mate kwa nguvu mno mithili ya mtu anayejaribu kuimeza sarafu ya shilingi hamsini. Ghafla tu, vinyweleo vilimsimama. Alighairisha hata zoezi la kuchutama. Alihisi baridi ya hofu ikipenya hadi kwenye mifupa. Alipomwona mtu yule akihama upande wa njia aliyokuwepo na kuja upande huo aliokuwa amesimama yeye, aliuhama huo upande huku akigeuka nyuma mara kadhaa kutazama alikotoka.

Alionekana kama mtu aliyekuwa akivizia jambo!

Hili lilimwongezea mashaka zaidi Morena. Alitamani kupiga yowe na sauti yake ikamsaliti. Kwa nini apige yowe? Akili ilimhoji na kumtia ganzi. Akayafinya macho yake na kuyapunguza upana wake wakati akiyakaza yamtazame vema yule jamaa aliyekuwa anazidi kumkaribia. Bado alikuwa na ule mwendo wa kuvizia, mwendo uliomfanya Morena amuone yule jamaa na kivuli chake kama watu wawili tofauti!

Nafsi yake ilimtuma kupiga hatua moja kurudi nyuma. Hiyo hatua moja ikazaa hatua zingine za pole pole. Hatua za minyato. Mapigo ya moyo yakikimbia kwa kasi ya ajabu. Alihisi yalikaribia kukitoboa kifua na kuchanja mbuga nje ya mwili wake.

Afanaleki!

Alitishika. Alitishika si kidogo.

Hapana huyu si mtu mzuri! Morena alijiambia kwa sauti ya kichwani huku akimtazama jamaa kwa wasiwasi. Wakati huo, alikwishagotea kwenye ukuta wa nyumba iliyotazamana na ile hoteli.

Alimwona yule jamaa akichomoa mkono toka kwenye mfuko wa jaketi kubwa alilokuwa amevaa. Morena hakusubiri kuona kilichochomolewa. Aliinama haraka. Akavua viatu vyake. Akatimua mbio.

Alikimbia kwa kasi ndogo. Mara moja aligeuka kutazama nyuma. Pengine alitaka kuhakiki kama uamuzi wake wa kukimbia ulikuwa sahihi. Akashuhudia mwendo wa yule jamaa nao ukiwa umebadilika toka mwendo wa pole pole na kuwa mchaka mchaka. Morena alihamanika.

Anakimbizwa, uwii!

Hakugeuka tena. Alikimbia kwa kadiri miguu yake ilivyonyonga, akitamani kuiuliza kama aliwahi kula chochote na kuinyima. Alikimbia hadi alipoifikia njia panda iliyogawanyika mara nne; ile aliyotokea, iliyoelekea mbele yake na mbili zilizokuwa kushoto na kulia kwake. Akapiga breki za ghafla akiwa anahema na asijue ashike njia ipi.

Aliweweseka kwa hofu lakini ikamlazimu kuuvaa ujasiri wa kukopa. Akageuka kutazama kwanza kule alikotoka. Patupu!

Hakukuwa mtu tena wala kivuli. Kaenda wapi? Akachoka. Hii kwake haikuwa ishara njema kwenye mpango wao. Aliliona bwawa la mikakati yao likinyemelewa na ruba.

Alihamanika. Alipepesa macho kutazama kule alikotoka. Pamoja na kuwepo kwa mwanga wa taa toka nyumba hii na ile. Bado giza dogo lililokuwepo katikati ya barabara hii iliyokuwa kimya, lilimchezesha kwata. Ujasiri wa kurudi alikotoka ulichanja mbuga na kutokomea.

Sasa?



4

MORENA alikata shauri kusonga mbele. Kwa wahaka aliokuwa nao, asingeweza kurudi pale alipokuwa amesimama mwanzo. Aliangaza akizitazama zile njia nne kwa awamu. Kibaridi cha usiku nacho kilimpuliza na kuiparaza ngozi mpaka utumbo. Kuna majuto yalipita haraka kichwani mwake, yalipita kwa kasi mno kiasi cha kumtaja Mungu na asimweleze alilotaka amfanyie.

Akaamua tu kukamata njia iliyokuwa mbele yake, akiwa amejikumbatia, mkono wa kulia ukiwa na viatu vyake huku ule wa kushoto ukiwa na simu yake. Akaivuka njia panda, akiwa yeye na kivuli chake. Alitembea tu na asijue aendako.

Si kwamba hakuzoea kuwa nje usiku kama huu. La hasha! Katika mikikimikiki yake ya kujiuza alikwishazunguka nje usiku mnene zaidi ya huu.

Vingunguti, Buguruni, Yombo ama Kariakoo hii saa saba kasorobo usiku, pilika pilika za hapa na pale zingetosha kumfanya akae mahali aagize hata mchemsho wa miguu ya kuku kusukumia wasaa. Ila huu mtaa alioibukia ulikuwa kimya mno, kimya kupitiliza.

Hatua kadhaa mbele akamwona mtu kwenye moja ya mageti yaliyokuwa mbele yake. Kwa haraka haraka akahisi ni mlinzi. Mkombozi!

Alimkimbilia. Akasimama mbele yake wakati mlinzi yule naye akiacha kuingia ndani na kusimama kizingitini. Alimtazama Morena juu chini.

“Kaka yangu n’na shida!” Alianza kujieleza.

Ile hali ya kuhema ilifanya mabega yake yapande na kushuka kiasi cha kuonekana wazi kuwa alikuwa katika hali ya taharuki. Yule mwanaume getini, alimtazama Morena kwa mashaka kisha akatazama kule alikotokea. Ni dhahiri alitaka kuhakiki kwanza kama Morena alikuwa yu mtu mwema, ama pengine kujiridhisha kuwa hakuwa ameongozana na mtu mwingine yeyote.

Morena alimeza mate kwa taabu akiwa kimya. Huenda aliomba dua amri ya kuendelea kujieleza itoke na kumhakikishia usalama wake. Yule mwanaume akamkunjia uso.

“Shida gani?” Alisaili kwa sauti kali. Alifunga geti, akasimama kumwelekea bibie.

Morena aliomba hifadhi ya muda hata pale ndani ya geti ili aweze kuwasiliana na ndugu yake kwa usalama.

Yule mwanaume hakumwelewa. Alimtandika maswali ya haraka haraka ambayo Morena alijitahidi kuyajibu ili tu apate hifadhi aliyoihitaji. Uongo na ukweli vikichanganywa kuitafuta huruma. Akaipata.

Alipopewa stuli ili aketi hapo getini kwa ndani, Morena alipata amani ya kumpigia simu Fatumata. Ghadhabu na hofu vilikumbatiana wakati akisubiri simu yake ipokelewe.

Simu iliita hadi kukatika. Aliitoa sikioni. Akaitazama kwa hasira.

Yule mwanaume alimtazama kana kwamba alitaka kuthibitisha kuwa Morena hakuwa mwongo. Akaipiga tena simu ya Fatumata safari hii akimwomba Mungu simu ipokelewe. Ikaita kwa sekunde tatu nne.

Kimya!

Alisubiri kidogo tena.

Kimya!

Alihisi ile ilikuwa siku ya kufa nyani, kila mti pruuu mpaka maka. Akainua macho. Alimtazama yule mlinzi, ambaye naye alikuwa anamtazama kwa umakini.

“Hapokei simu!” Alitamka kwa huzuni akinyanyua mabega juu na kuyashusha.

“Sasa?” Mlinzi alimtupia swali kwa sauti ya kuhimiza jibu.

Morena akatapatapa. Kwa nini? Hakuwa na pesa yoyote ya maana zaidi ya shilingi elfu mbili alizokuwa amezitia kwenye sidiria. Makubaliano yao yalikuwa teksi ije impitie pale alipokuwa akiisubiri mwanzo kisha impeleke huko pa kusubiria kuuchukua mzigo halafu imrudishe nyumbani. Si hivi mambo yalivyoonekana kuparaganyika ghafla!

Hasira zilimshika maradufu. Hakuwa na namba ya Daudi Chochoro ambaye pengine angemsaidia kujua kinachoendelea. Akahisi kudhalilika na kusumbuka kwa tamaa ya pesa za haraka. Wakati akiwaza cha kumjibu yule mlinzi. Simu yake ikaita, alikuwa Fatumata.

Moyo ukafunguka haraka, hata kabla ya mwito wa simu ile kuchanganyia akaipokea.

“Mpuuzi wewe na huyo Uchochoro wako!” Alisonya. “Hivi mnadhani mie kipande cha mti kukaa hapa nawangojea kiama na msiniambie mko wapi?”

Morena hakuwa na muda wa kumsikiliza Fatumata aliyekuwa akiongea wakati Morena akigomba. “Mie mgeni huku halafu hamnambii kinachoendelea mkitegemea nini? Nimekoswa koswa kisu cha utumbo we’ unalalana tu uko…”

Alisonya msonyo mrefu zaidi wa kilo za kutosha kiasi cha kumfanya mlinzi atabasamu.

“Sipajui hapa… niendeje?... Mwenzangu mwisho usiku huu nitokezee Matombo Morogoro bure kwa kukatiza katiza… Kwa hiyo?” Morena aliuliza akiinama kidogo na kuanza kuvaa viatu vyake. Ni kama vile sasa alipata suluhisho la namna ya kuondoka pale.

Alipomaliza kuongea na Fatumata, alinyanyuka. Alimshukuru yule mlinzi. Aliitoa ile elfu mbili yake aliyokuwa nayo. Alimpatia mlinzi. Kwa uungwana wake, mlinzi akaikataa akidai kumsitiri pale ilikuwa ihsani tu.

Huenda alishikwa na imani vile alivyoitoa hela pekee toka kwenye kitambaa kidogo kilichokuwa kwenye sidiria. Wakazungumza mawili matatu. Mlinzi akavunja kanuni za ulinzi. Alimsindikiza Morena mpaka karibu na ile njia panda. Dakika tatu tu, mwanga wa gari ukaonekana ukikata kona kuja eneo lile.

Morena akashukuru. Wakaagana.

“Unajua una mishe ya hatari halafu unachukua gari bovu, la kazi gani mzee?” Morena alinung’unika wakati akiingia kwenye teksi ya Daudi Chochoro baada ya kuelezwa sababu ya kuchelewa kwake.

Daudi alikuwa mtu mzima wa makamo. Mvi lukuki zilizompatia shikamoo nyingi za hiari. Huo utu uzima wake ndiyo uliopelekea Morena amfanyie staha ya kutomporomoshea maneno ya shombo. Vinginevyo, njia nzima angeipata pata.

Kwa ule umri wake, ilimpasa kuwa nyumbani akiogelea kwenye bahari ya usingizi wa raha. Tena, baada ya uchovu wa kucheza na wajukuu kutwa nzima. Lakini, uhalisia wa maisha ulimpiga ngwara matata sana. Nazo shida za dunia hii zikampora yote yampasayo.

Alikuwa barabarani usiku huu akitafuta senti za ziada. Senti za kupeleka mkono kinywani kwake na kwa familia yake kubwa ya wana na wajukuu. Familia iliyomtegemea yeye kwa kila kitu.

“Magari hayana muamana mwanangu!” Mzee Daudi alijitetea akitabasamu. Tabasamu lililovaa uchovu wa kutwa nzima. Mwendo wa gari ukaongezeka.




****

Fatumata Mzinga alinyanyua kichwa chake. Alimtazama Kimboka usoni. Akapunga punga kiganja cha mkono wake wa kulia juu ya uso wa Kimboka kuyakinisha kama alikuwa amekwishatopea usingizini. Akajifanya kugeuka kwa fujo kidogo akiutupa mwili wake mteketeke huku na kule ili kuhakiki tena uzito wa mwenzake usingizini.

Chaga za kitanda zikalalamika, wakati mwenye kitanda hata kutingishika hakutingishika.

Fatumata alijisogeza taratibu, kwa tahadhari kubwa, akiondoa shuka juu yake na kukikaza kifuani kitenge alichokuwa amekivaa. Kwa mwendo wa kunyata akatembea taratibu akiunyatia mlango.

Alikwishaweka kitambaa tangu mwanzo ili mlango usijifunge vizuri akichelea kunyongwa kwa kitasa kungemshtua Kimboka. Akauvuta mlango na kutoka chumbani. Korido ndefu kidogo ikamkodolea macho. Kulikuwa na giza japo si totoro.

Alinyata huku akiushikilia ukuta kama nguzo yake. Chumba cha pili, akakishika kitasa. Alikinyonga kiuangalifu. Mara kadhaa, alitazama nyuma kuhakiki usalama wake. Akaiuma midomo kwa ndani wakati akiusukuma mlango kwa mbele, akitanguliza kichwa kuchungulia ndani.

Giza lingine jepesi lilimfanya atamani kuiwasha taa.

Mlango wa stoo iliyokuwa ndani ya chumba hicho ulikuwa kulia. Hatua tatu nne toka mlangoni. Aliufuata. Akalitazama kufuli lililoning’inia hapo.

Alilitarajia.

Mikono yake ikazama kwenye kichwa chake. Akapekenyua fundo la rasta lililofungiwa kiustadi katikati ya kichwa mithili ya mdomo wa chungu. Akatoa ufunguo. Akauzamisha kwenye kufuli. Sekunde tu, kufuli likaachia. Akahangaika na mlango wa chuma mpaka nao ukafunguka.

Akaubusu ule ufunguo malaya, akiushukuru kwa kazi uliyomfanyia. Kuufungua ule mlango wa stoo ilikuwa kama kuufungua mlango wa neema ya maisha.

Kwa uangalifu na umakini mkubwa, akaingia mle stoo. Kama mtu aliyejipanga tangu mwanzo, akahesabu kwa kichwa na kidole cha shahada zikitetembea hewani kufuatiza mtikisiko wa kichwa; akahesabu kiroba cha kwanza hadi cha sita, kulikuwa na vingine vingi, vingefika hata 10. Alishafanyia uchunguzi na kujua kile cha sita ndicho kilichokuwa na mchanga ambao chini kidogo ndiyo kulikuwa na hizo almasi.

Alikifuata kwa kasi. Akakikwapua. Uzito wa kiroba ulimfanya atumie mikono miwili kukitia begani. Mkono mwingine ukijaribu kusawazisha nafasi iliyobaki baada ya kukiondoa kiroba. Aliporidhika, alitoka haraka. Akalifunga lile lango la chuma. Akafunga kufuli. Alitoka nje ya chumba kwa haraka sana.

Kiroba kikiwa begani!

Ufunguo wake ukarudi kwenye fundo la nywele. Hakutazama kokote. Alitoka kwa mwendo wa kuunga hatua. Mwendo wa mbeba zege kazini. Mwendo wa haraka. Alilifuata eneo la jiko ambalo nalo alishaliandalia mazingira kwa kusindika milango bila kuufunga itakiwavyo.

Alitoka nje ambako kulikuwa na ukimya mkubwa. Alinyata kwa tahadhari akichungulia upande aliokaa mlinzi. Mlinzi ambaye alikuwa amejipumzisha kibandani kwake bila shaka lolote. Akazunguka nyuma kidogo ambako ndiko alikopanga kukipitisha kile kiroba.

Ukuta ulikuwa na nafasi kwa juu, nafasi iliyotokana na urembo uliokuwa kama sehemu ya ukuta. Kulikuwa na meza ya mbao iliyoonekana kutumiwa na mafundi wapaka rangi, lakini kwa usiku huo ilikuwa mahsusi kwa kazi iliyotaka kuifanyika.

Akapanda kwa shida. Akasimama juu ya ile meza akihisi pia kuyumba nayo, pengine kutokana na uzito wake. Mungu nisaidie! Akamkumbuka Manani katikati ya ujahili wake.

Alikiinua kiroba na kukining’iniza kwa nje. Akakiachia taratibu ili kisitoe kishindo kikubwa. Akafanikiwa. Kilitua puh! Akashuka na kuondoa ile meza kwa taabu nyingi akiisogeza mbali. Akachomoka kwa mwendo wa haraka kurudi ndani.

Dakika tatu zilimtosha Fatumata kurudi chumbani kwa Kimboka. Alimkuta kama alivyomwacha.

Usingizini. Fofofo!

Aliketi kitandani na kuitafuta simu yake. Aliziona missed calls za Morena. Akampigia kumjulisha mambo yalikuwa tayari. Kazi ilikuwa imeisha.

Utajiri ulikuwa mlangoni, ukiwagongea hodi.

****

Asubuhi.

Kama kawaida kutaradadika kulishaanza mapema kabisa mle ndani kwenye nyumba aliyopanga Morena. Huko nje mashine ya kuranda mbao na honi za pikipiki kwa baiskeli vilikazana kuukimbizia mbali utulivu. Harufu ya vitafunwa mbalimbali vikiandaliwa kwa ajili ya staftahi ilipenya kila kona. Ikiyaungurumisha matumbo ya waja.

Hekaheka ya kutarazaki ilikamata kasi.

Morena alijigeuza kitandani kwa minajili ya kubadili uchago lakini mwanga wa jua aliokumbana nao huko alipogeukia ulimfanya afinye uso. Akafumbua macho. Mwayo ulimtoka.

Alikiinua kichwa tu huku kiwiliwili kikiwa na uzito uliomfanya atamani kikurudisha kichwa mchagoni. Mwayo mwingine ukafuata wakati akijitutumua kuukwepa ule mwanga wa jua na kugeukia upande mwingine.

Macho yake yakatua kwenye kiroba cheusi.

Kiroba alichokuja nacho usiku wa manane. Alikitazama kwa muda kana kwamba ndiyo kwanza alikuwa anakitia machoni. Uzito wa kiroba hicho ndiyo uliomletea hali ya kuuhisi uzito mwilini. Alipokiokota pale kiliporushwa, alikitia begani na kukimbia nacho nusu ya miguu kuchomoka. Akatabasamu alipokumbuka mbio alizochapa usiku uliopita.

Udadisi pia ukamtomasa taratibu. Uzito wa kiroba ulimfanya atake kujua ujazo wa hiyo almasi. Atake kuiona almasi yenyewe mikononi mwake. Tamaa pia ikimuingia kiasi cha kuwaza kuiba jiwe moja na kulificha. Wizi ulianza kumkolea polepole.

Kwani Fatumata alizihesabu hizo almasi? Akajiuliza.

Alijiinua kivivu na kuketi kitandani. Alikitazama kile kiroba akitabasamu kwa mbali. Kwa hesabu za haraka tu, alijiona akiwa na milioni kadhaa kibindoni. Atapanga nyumba nzuri. Atanunua shamba kijijini kwao. Atalipa karo za wadogo zake. Halafu, ataifungulia familia yake biashara yoyote. Atafanya hiki, atafanya kile. Mawazo yakapangana kama ngazi ya mnara wa babeli.

Alinyanyuka toka pale kitandani. Akakifuata kiroba. Akakinyanyua kwa mkono mmoja akitumia jitihada zote. Akarudi nacho kuketi kitandani, akitawanya miguu kile kiroba kikiwa katikati.

Alihangaika kukifungua. Hatimaye, akafanikiwa. Alipokitanua kile kiroba. Akakunja uso.

Mchanga uliokuwa ndani ya kiroba ulimfanya agune.

“Mwe! Mbona kuna mchanga!” Alistaajabu huku akitumbukiza mkono kuuchambua ule mchanga kwa kuhisi almasi yenyewe ilikuwa amefukiwa chini zaidi.

Akapekenyua mchanga akisikilizia.

Ghafla, akahisi kukamata kitu. Akahisi kugusa kitu ambacho hakukitarajia. Haraka akauchomoa mkono kwa kasi ya ajabu, moyo ukipiga mkambi!

Macho yalimtoka. Aliruka toka kitandani kwa kasi ya mchomoko wa risasi. Alisimama mbali na kile kiroba. Akili ilicheza segemnege. Alisimama hapo kwa muda mikono ikiwa kifuani kabla ya kuamua kuuvuta mfuko wa ‘salfeti’ uliokuwa na nembo ya unga wa ngano. Akauvuta toka uvunguni. Akautandaza chini. Alikinyanyua kile kiroba haraka. Akakimimina juu ya salfeti kwa tahadhari.

Afanaleki!

Morena alipiga ukunga wa hofu.

“Uwiii! Mungu wangu! Mungu wangu! Mamaaaa!” Aliruka tena kurudi nyuma. Akala mweleka chini. Alisota kwa matako kurudi nyuma. Tena, kwa kasi zaidi. Alipiga mayowe ya fadhaa. Haikuwa almasi, ama walau vipande vya kioo afananishie na almasi.

***Kumbe ni nini tena Morena jamaniii!!?




Ulikuwa mkono wa mtu. Sehemu ya kiwiko hadi kiganja. Mkono uliokuwa na saa yake. Mkono wa binadamu mweusi ti. Kulikuwa na korodani na dhakari yake. Kulikuwa na vingine vidogo vidogo ambavyo Morena hakuvitambua haraka kama ule mkono na zile sehemu za siri.

Alitetemeka kuliko mwanzo. Alijitahidi kuufumba mdomo wake kwa mikono yake ili asipaze zaidi sauti ya ule mshtuko wake.

“We Morena vipi? Mbona mayowe? Hebu fungua!” Alimsikia mpangaji mwenzake akimhoji, papo hapo akitingisha kitasa kuashiria kutaka kufunguliwa.

Aliuinua uso wake kukitazama kile kitasa kilivyokuwa kikipanda na kushuka kwa kule kunyongwa na yule mpangaji kule nje. Sababu ya ubovu wake kilitoa sauti iliyomwewesesha Morena. Je, mlango ukifunguka pasipo yeye kuufungua? Alikitazama kitasa kwa uoga mno, macho yakiwa yamejaa wahaka wa kutosha.

Aliyasikia maneno mengine ya mpangaji mwenzake na wala asiyaelewe. Mshtuko uliomkung’uta ghafla uliivuruga milango ya fahamu zake.

Akayatoa macho yake toka kwenye kitasa na kukitazama tena kile kifurushi cha mchanga chenye mazagazaga ya ajabu. Akachoka mwili na roho.

Alikitazama tu kama mtu asiyeamini usiku kucha alikuwa amelala na vitu vile pasipo kujua. Kwamba usiku ule wa manane alipokikwanyua kiroba kile na kukimbia nacho kwa mbio za kuruka viunzi, alikuwa amebeba sehemu za siri za mtu na mkono wake, na si almasi.

Morena alisisimka!

5

MORENA hakuweza kusota kurudi nyuma zaidi japo kwa hatua moja. Aliendelea kuketi pale chini kwa fadhaa kama punguani, akiingoja akili yake irudi toka ilikokimbilia na kumwamrisha cha kufanya. Alikuwa kama binadamu mwenye debe na si kichwa tena.

Alikuwa mtupu akilini!

“We mwanamke vipi jamani? We Morena! Morena!” Yule mpangaji kule mlangoni alimng’ang’ania kana kwamba alishajua kuna mauzauza huko ndani.

Baada ya dakika kukatika, Morena alipiga moyo konde. Alisimama kwa taabu, asijali sana zile kelele za yule mpangaji. Alipoinuka ndiyo akagundua kulikuwa kuna watu pia kule dirishani. Akatoa macho kwa nguvu zote naye akiwashangaa.

“Niko gengeni uko nasikia mayowe dada vipi?” Alisikia sauti toka pale dirishani.

Kwa kuwa nyavu za dirisha zilikuwa na vumbi la kutosha, hawakuweza kuyaona sawa sawa yaliyokuwemo ndani. Isitoshe kile kifurushi kilikuwa kimezibwa na ukingo wa kitanda. Ikawa salama yake.

Katikati ya ile fadhaa, Morea alitamani kucheka namna ule umati kule dirishani ulivyominyana barabara kutaka kujua kulikoni.

“Wapigieni mashilawadu waambieni kuna vioja huku. Mtu kapiga yowe ndani mwake halafu wala hasemi kuna nini!” Alimsikia mmoja akiwaambia wenzake. Kicheko kikubwa kikazuka hapo nje ya dirisha.

“Hakuna kitu jamani!” Morena alijitutumua kuwajibu, moyo ukimuenda hobelahobela.

“Kuna usalama?” Mwingine alimwuliza haraka.

“Nimeteleza tu nikaanguka!” Alitaka kuwatawanya toka dirishani kwa kuwa sasa wengine walianza kulipangusa lile vumbi ili wapate kusogeza macho vizuri.

Dakika mbili tatu, dirisha likawa tupu.

Aligeuka kuutazama mlango. Nao ulikuwa kimya. Akahisi aliyekuwa amekishika kitasa alizunguka kuungana na wenzake kule dirishani. Akapumua!

Alikifuata kitanda kwa tahadhari mno. Alikivuta kipande cha khanga kilichokuwa hapo kitandani. Alikifunika kile kifurushi kwa mtindo wa kurushia. Akasimama mikono kiunoni, akiutafuta ujasiri kidogo wa kupunguza midundo ya moyo. Alihisi kama vile moyo wake ulikaribia kudundia utosini. Akapapasa chini ya mto akiitafuta simu yake. Akaipata.

Mikono yake ilikuwa inatetemeka wakati akiiwasha simu. Ilipowaka tu meseji ikaingia. Akaifungua uso ukiwa na ndita kadhaa. Pumzi zilizotoka hazikulingana na zile zilizoingia. Damu ilimchachawa!

Za kumka.yapo.mawe magapi?ntaka niazedarari wa madni tufanyeyetu

Aliusoma ule ujumbe wa Fatumata kwa taabu kidogo ila alimuelewa.

Fatumata alikuwa anataka kutafuta dalali wa madini. Nafsini alijua kwa meseji ile inawezekana alitumia dakika nzima kuiandika baada ya kumkosa hewani. Akataka kutabasamu ila mshtuko aliokuwa nao ukampiga roba.

Ujumbe wa maneno ungemchelewesha kufikisha taarifa za kiroba chao.

Alizitafuta namba. Akamwendea hewani mwenzake. Mitambo ilipomjulisha kuwa hakuwa na salio la kutosha, akasonya. Msonyo mfupi mzito wa kukereka.

Alishusha pumzi akiwa ameipakata simu yake kama kopo tu. Macho yake yakirudia kukitazama kile kifurushi kilichositiriwa na khanga. Alisisimka tena mwili. Akawaza cha kufanya. Hakupata, zaidi ya kuamua kumsubiri Fatumata kwanza.

Na namna alivyomjua rafiki yake, si ajabu angetoka huko aliko na kupita madukani kumaliza pesa yake yote ya akiba akijua kuna almasi ya kumuingizia mamilioni.

Akaona aende kuisaka vocha dukani, ili ampigie Fatumata aje ajionee mwenyewe. Akalifuata kapu la nguo lililokuwa limejaa pomoni. Akavuta dera na kulivaa, akalifuata dirisha na kusogeza pazia kuliziba dirisha lote.

Akatoka.

Wapangaji waliokuwa koridoni walimshangaa. Wapo waliomsemesha wakati akifunga mlango kwa ufunguo na wapo walioishia kucheka kwanza. Akatabasamu tu kama zumbukuku. Hakuwasikiliza, nguvu ya kusikiliza angeitoa wapi. Alikuwa na yake elfu kwa laki kichwani.

Akatoka varandani. Alinyoosha njia kulifuata duka. Kila aliyepishana naye alimkodolea macho katika namna iliyomfanya naye awatazame kwa viulizo kisha kuendelea na safari yake. Dukani hakukuta watu wengi. Wawili watatu aliowakuta walimtazama kwa macho ya kumuajabia.

Akanunua vocha na kutoka pale dukani, akiiongoza miguu yake mpaka kwenye kijimsingi kidogo cha pagale mbali na makundi ya watu. Akakaa hapo na kuanza kuingiza namba za vocha kwenye simu. Sasa ndiyo akagundua alikuwa amevaa dera chakavu ambalo hulitumia kufutia viatu au vumbi linapozidi ndani mwake.

Akacheka!

Lilikuwa kuukuu mno. Hata mwendawazimu asingejisumbua kulitazama sembuse kuliokota. Mbali na hayo alikuwa ameligeuza ndani nje, mbele nyuma. Akacheka akisikitika. Hakuyaona haya yote wakati akilivaa, wakati akikatiza mtaa.

Simu ya Fatumata iliita kwa sekunde mbili tu ikapokelewa.

“Shoga niko kwenye bajaji naenda Tandika mara moja.” Alipokea akijieleza.

“Njoo kwanza huku kwangu!” Morena alitaka kumkatishia safari yake.

“Heheheee! Unaona kama unachelewa kuyashika mamilioni yako eh… Pesa tamu asikwambie mtu!” Fatumata alitamba.

“We njoo kwanza, yaani vunja safari zako zote uje kwanza huku!” Mwenzake alimsisitiza.

“Kwani kuna nini somo?” Fatumata aliuliza akianza kuingiwa na mashaka.

“Ukiitwa nenda! Mbona unakuwa kama msungo? Nasisitiza vunja safari zako za wapi sijui ‘uko uje kwanza!” Morena hakuonyesha masihara.

Fatumata sasa hakutaka kubishana tena, akamwomba dereva wa bajaji amshushe kituo cha basi mbele, achukue daladala.

Morena hakurudi kwake.

***Mnh! Majanga!! Yeshakuwa mauzauza sasa...nini kitafuata?




Alikaa kwenye msingi ule akitazama wanaoenda na kurudi pengine asiwatambue akilini. Alikaa hapo kwa takribani nusu saa nzima akimsubiri rafiki yake.

Dakika ishirini zaidi baadaye akamwona akija juu ya pikipiki.

Hakungoja hata amfikie. Akashuka toka kwenye msingi na kusimama.

“Umen’shtua somo yaani njia nzima nawaza na kuwazua, haya vipi?” Fatumata alizungumza wakati akishuka kwenye pikipiki.

“Twende kwanza nyumbani.” Alitamka kiunyonge akianza kuchapua hatua wakati Fatumata akimalizana na yule dereva wa pikipiki.

“Na umevaa nini hiki leo?” Fatumata alimshangaa mwenzake aliyeishia kutikisa kichwa kulia kushoto. Hakumweleza masaibu yaliyomkuta. Asingeyaelewa kwa nadharia tupu maana cha kusikia si cha kuona.

Wakafika. Morena aliufungua mlango.

Wakaingia ndani.

Fatumata alikifuata kitanda na kujitupa hapo akimtazama Morena aliyekuwa amesimama karibu na mlango.

“Haya vipi?” Alidodosa.

“Dada. Daaada we mmh!” Alipiga kofi hewani na kujishika kiuno.

“Kwani vipi?” Fatumata alikaza uso sasa akisemea sauti ya chini kama aliyoitumia mwenzake. Kwa sauti aliyotumia Morena, Fatumata alijua mwenzake hakutaka mazungumzo yao yafike hata hapo koridoni.

“Kwanza jua hapa ukikohoa hata mara tatu, watu watajaa dirishani hapo kukuuliza unatumia dawa gani?” Alizungumza kichinichini, akionyesha msisitizo kwa kulisonta dirisha.

Asteaste, akamshuhudia Fatumata akipoteza nuru usoni na wasiwasi kuupamba uso wake. Kabla hata ya kuambiwa habari yenyewe tayari alishapeleka mikono kifuani na kuiacha hapo. Mashaka!

“Funua khanga hiyo!” Alimpa maelekezo huku akikinyooshea kidole kiroba mahali kilipokuwa.

Fatumata akasita, alimtazama Morena kana kwamba yaliyokuwa chini ya khanga ile yangeonekana usoni pa Morena.

“Funua!” Alimsisitizia kwa sauti ya kuvuta.

Fatumata aliupeleka mkono. Akaishika ile khanga kwa ncha za vidole. Akaiinua taratibu huku akiinama na kuchungulia.

Aliiogopa hata khanga yenyewe.

Aliuona mchanga. Akaona vitu kadhaa ambavyo hakuvielewa. Akaendelea tu kuifunua khanga yote polepole. Aliyoyaona yakamfanya apeleke mkono mdomoni, aufumbe mdomo kwa nguvu zote alizojaaliwa wakati akitoa macho kwa kadiri ya upana wake.

Alijiondoa kitandani kwa Kiwewe. Kiwewe hicho kikamfanya aivamie ndoo ya maji iliyokuwa pembeni na kuanguka kwa kishindo, hakuyajali hata yale maumivu ya kuanguka, alisota akaushika mguu wa meza kwa nguvu zote akiwa bado na lile hamaniko. Nguvu zake zikamfanya achomoke na ule mguu wa meza.

Meza nayo ikakosa uwiano na kuanguka. Parakacha! Ilianguka upande sambamba na vitu vyote vilivyokuwa juu ya hiyo meza. Kelele za kishindo cha meza, kupasuka kwa vyombo na kelele za vikombe vya bati vilisimamisha watu kule koridoni.

Fatumata aliinuka. Alimkimbilia Morena ambaye aliduwazwa pia na ile mikikimikiki ya Fatumata. Wakashikana wakitetemeka.

Unga wa ugali uliokuwa juu ya meza uliishia kichwani mwa Fatumata, vile alivyokuwa amesimama akitetemeka, na ule unga kichwani mpaka usoni,alitisha na kuchekesha kwa wakati mmoja.

Kwanza walisogeza shingo mbele kuangalia vizuri kile walichokiona muda ule. Ni kama vile hawakuyaamini macho yao. Waliona kama vile ule mkono wenye saa unatikisika, vidole vikacheza kana kwamba bado vilikuwa na uhai. Kitendo kile kilipojirudia tena hakuna aliyesubiri adhana wala kengele ya kanisani. Waligeuka. Wakaugombea mlango kwa fujo nusu ya kuling’oa bawaba. Walipiga mayowe mchanganyiko.

. Walikuwa tayari kufa wakiugombea mlango na si kufa wakiyashuhudia mauzauza kama yale.

Mlango ulipofunguka kila mtu alishika njia yake. Hata wapangaji waliokuwa wakisikilizia mayowe yao mlangoni kila mmoja alichomoka na njia yake pasipo kujua hata kilichowakimbiza wenzao.

Mtawanyiko wa watu kuelekea nje uliiacha nyumba ikiwa nyeupe ndani ya dakika.

Hakuna aliyekaa. Hakuna aliyesubiri. Hata waliokuwa msalani nyumba jirani na yao, kwa zile pukurukushani na mayowe walitoka na makopo mkononi na mapovu ya sabuni kichwani. Zikasikika sauti za redio na runinga tu zilizokuwa hewani muda huo.

Kule nje watu toka sehemu zingine nao wakaacha shughuli zao na kusimama nje ya nyumba zao wima wima, wakiitizama ile nyumba ya Mzee Hizza.

Wakaulizana. Hakuna aliyepata jibu la ni nini hasa kilikaribia kuwategua miguu. Morena alikuwa mbali mno, kwenye kibaraza cha fundi cherehani akiwa ameinama. Alihema mithili ya mwanariadha aliyemaliza mbio za masafa.

Aliinama akiwa kayashikilia magoti yake, uso ukitazama kule alikotokea pengine akistaajabu aliwezaje kufika pale kwa zile sekunde chache tu alizochomoka toka mle ndani. Fundi cherehani alimsemesha, lakini ndiyo vile alikuwa amemgeuzia mgongo, akili na mwili vikiwa kule alikotoka. Aliutazama umati uliozidi kujazana umbali mfupi tu toka ilipo varanda ya nyumba yao.

Fatumata ndiye aliyekuwa karibu kidogo na eneo la tukio.

Alitokea uchochoroni huku akiyakagua magoti yake mara mbili mbili, kwani alianguka mara kadhaa mpaka kufika huko uchochoroni. Alipotokezea tu, watu wazima wakamdaka.

Akatulia kwanza. Aliipa akili yake nafasi ya kuchanganua ni nini aseme na nini asiseme. Ilikuwa halahala kidole na jicho! Akahema tu akinyoosha mkono kuelekea kule ndani na asiongee kitu. Alitikisa kichwa katika hali ya kutoamini.

Watu nao walimkodolea macho wakingojea atamke lolote la kuwapa pa kuanzia. Wengine huko nyuma wakiucheka ule uso na zile nywele zilizokuwa zimetapakaa unga licha ya mwenyewe kujaribu kuupunguza usoni.

Alikuwa kama mcheza ngoma za jadi aliyeanguka jukwaani.

“Tumeona mkono!” Alisema katikati ya zile pumzi.

“Mkono!? Mkono wa mtu… mkono wa birika ama mkono wa nini hasa?” Sinasudi yule mwanadada aliyesubirisha watu bafuni asubuhi iliyopita akauliza. Yeye akiwa mbele kabisa kama kiongozi, huku wananchi wenzake nyuma yake wakiitikia kukubaliana na swali lake.

“Mkono wa mtu!” Fatumata alijibu, mwenyewe akiwa na hali ya kutoamini alichokiona.

“Astaghfirullah!” Mzee mmoja aliyekuwa na kibandiko kichwani alistaajabia maneno ya Fatumata.

Wengine, kila mtu akaweka mshtuko wake kwa staili yake.

Upesi upesi, wanaume wachache wakajitoa mhanga kwenda kujua kulikoni huko ndani. Ni wakati huo huo Morena naye alifika pale kwenye ule umati. Naye akaanza kuhojiwa kama kweli walichokiona ni mkono wa binadamu.

Alipokiri ni kweli, hamaniko likaongezeka. Wakasubiri kwa hamu kujua watakachokiona hao walioingia ndani.

Dakika mbili tatu wakatoka.

“Mbona hamna kitu?” Alitamka mmoja aliyetangulia kutoka, akipukutisha mikono yake

Fatumata na Morena walitazamana.

Wale walioingia hawakujua tu ni kiasi gani walizichemsha akili za wanawake hawa wawili kwa lile tamko lao. Kama walioambizana wakatoka kwa pamoja kuelekea ndani, umati mdogo nao ukiwafuata nyuma. Fatumata akawa wa kwanza kufika mlangoni.

Macho yakamtoka pima!

6

FATUMATA alipiga hatua za kunyata huku akiangaza kwa juhudi kama mtu anayetafuta kitu kwa hadhari kubwa. Aliiona ile khanga aliyoifunua ikiwa pale pale sakafuni. Akauona ule mfuko wa salfeti uliotandazwa chini, lakini kiroba cheusi hakikuwepo!

Wala vile vilivyokuwemo ndani yake!

Mazingazi haya!

Morena yeye alikomea mlangoni tu. Aliizungusha shingo yake mithili ya mtu mwenye degedege akiweweseka nusu ya kufa. Alimeza mate mpaka akahisi kinywa kinamkauka. Lile dera kuukuu mwilini aliliona kama vazi la chuma, vazi la vita ya karne ya kumi.

Alipiga hatua chache tu na kuingia ndani mwake.akiendelea kuangaza. Na yeye aliyaona aliyoyaona Fatumata.

Kasheshe bin balaa!

Watu waliokuwa kule nje kila mtu alinena lake.

“Hapa aitwe Shekhe Kombo afanye kisomo tu kwa kweli. Hivi hivi tutazikana humu ndani jamani!” Mpangaji mmoja alitoa wazo lake. Wazo lilikubaliwa na wengi walioitikia kwa sauti za chini chini na kutikisa vichwa juu chini.

“Unacheza wewe, labda aje afanye kisomo chumba hicho tu, kwingine huku kuna watu wametoka kwa fundi juzi tu. Tutaumbuana hapa oh!” Sinasudi akamjibu mtoa wazo.

“Wa kwanza kuumbuka wewe, unamkogesha madawa mbaba wa watu pesa yote ya masafa ya malori anaimalizia kwako!” Mtu mmoja aliyekuwa nyuma kabisa akamjibu Sinasudi kwa jazba kana kwamba kile kijembe cha watu kwenda kwa mganga kilimhusu yeye.

“Hajaitwa huyo Shekhe mshaanza kugugumia mtajibeba mbona… Haya nyie wendawazimu humo ndani jana mlivuta bangi ya wapi? Na jua hili la utosi bangi bila kula mtaacha kuona mguu wa kitanda kama mkono wa mtu?” Sinasudi akaongea haraka haraka.

Watu walivunjika mbavu na kupunguza kidogo ile hali ya kutaharuki.

Watu wazima wakaingilia kati, kuwadodosa tena akina Fatumata kama kweli walichokiona ni mkono. Wakakiri walichokiona ndicho walichokisema, wakijiapiza kwa miungu ya babu zao. Lakini, habari ya wapi walikotoka na hicho kiroba wakaimezea.

“Mpigieni Mzee Hizza uko Tanga mumwambie. Maana kuna yule mpangaji aliondokaga hapa kwa msuguano wa makumbi na mashushu, ukute ndio anarudi kwa staili hii.” Kijana aliyekuwa na mashine ya kuranda mbao mkononi alitoa maoni yake.

“Kabisaa! Mwezi tu baada ya kuhama, mke wa Hizza alianguka bafuni akafa.” Mpangaji wa Mzee Hizza akadakia.

“Halafu kweli.” Mwingine aliyekuwa na kibao cha mbuzi kichwani na isijulikane alikotoka nacho alikubaliana na mpangaji wa Hizza.

“Hatukulia tukanyamaza mtoto wa mama Shaibu akafiwa na mwanaye. Hamuoni kitu hapo?” Mpangaji aliendelea kutema sumu.

“Na kweli.” Walikubaliana naye.

“Atakuwa ni baba Muni tu. Mshirikina kama nini. Yule mtoto aliharisha safari ngapi sijui eti chwaaa kafa! Haya sasa mikono hiyo inaifuata nyumba… Mwambieni Mzee Hizza aongee na wataalamu.”

“Ikibidi tuchangishane hapa tumwite profesa Mtindiga aufunge mtaa.” Watu walitoa maoni yao wakimsema mpangaji aliyehama kipindi cha nyuma kwa ugomvi mkubwa na mwenye nyumba.

Kila mtu alisema lake.

***DAH, Uswahilini kuna vituko! Ila vinavyowakuta Morena na shogaye ni kiboko ya vyote! Watatokaje?


“Unajua unaweza ona mambo hayakuendei, chapati hazitoki, biashara haziendi kumbe kuna mikono ya watu inazuia riziki yako!” Mwingine akaongeza.

Ilikuwa dhahiri kuwa watu wengi pale waliamini matatizo yao mengi yalisababishwa na ushirikina. Fatumata alishakamata khanga na kuanza kujipangusa vizuri. Morena aliivuta stuli. Akaketi akiitazama ile meza yake ilivyolala upande na makorokoro yote chini.

Saa moja baadaye, watu walirudi katika shughuli zao. Mtaa mzima gumzo lilikuwa huo mkono uliosadikiwa kuonekana asubuhi hiyo. Kule chumbani walifunga mlango wakabaki wawili. Akili zilichemka nusu ya vichwa kupasuka.

Wakati wakiongea, Fatumata akagandisha macho mbele akiwa kayatoa ndi! Akaufumba mdomo haraka na kunyoosha kidole kumtaka Morena atazame kule alikotazama yeye.

Kiroba cheusi!

Morena aliruka akitaka kukimbia lakini mbio zake zikaishia mlangoni. Alisimama hapo akitetemeka. Alikitazama kile kiroba kwa wahaka. Mwenzake alinyanyuka taratibu kama mtu ambaye hakutaka hata ile sauti ya kunesa kwa kitanda ikishtue kile kiroba.

Kilikuwa vile vile kama kilivyomwagwa na Morena.

Mazingara!

Fatumata alinyata mpaka alipo Morena. Wakasimama sambamba wakikitazama kile kiroba na wasiamini kilikuwa pale tena. Kimerudije? Nani kakirudisha pale? Kilienda wapi?

“Tuondoke hapa, twende kule kwangu kwanza halafu tutajua cha kufanya.” Fatumata aliongea, pumzi zikikimbizana puani kiasi cha kumletea shida ya kuhema sawasawa. Kuendelea kuwa pale kungemfanya apige nduru na kualika tena umati uliokwisha tawanyika.

Morena hakujibu. Aliitikia tu huku akianza kufungua mlango kwa tahadhari. Aliuchomoa ufunguo mlangoni. Wakatoka na kuufunga mlango kwa nje.

Wakaondoka vile vile wakiwa kituko kila walikopita.

****

Siku hiyo, kwao ilikuwa ndefu kuliko karne. Walikodi teksi mpaka nyumbani kwa Fatumata. Pesa ya kulipia wakaitafutia ndani. Baada ya kuoga, wakaketi chumbani. Fadhaa iliyowakaba koo ilionekana kwenye nyuso zao kama pembe la ng’ombe. Haikufichika!

“Shoga tumeuvaa mkenge. Hiki kiroba ulikikwapua wapi na ilikuwaje?” Morena aliuliza mara tu baada ya kuketi chini.

“Sielewi, unajua kabla ya yote nilikifungua, n’kahakikisha ni almasi na n’kakiweka cha sita ili kisinipotee, sijui imekuwaje mwenzangu sijui kwa kweli” Fatumata alisawijika.

“Sasa tunafanyaje? Maana kama ni kuharibu ndio hivi tumeshamong’onyoa. Tuchimbe mahali tukizike au tukirudishe tulipokitoa ama tukakitupe tu?” Morena aliuliza maswali mfululizo.

Fatumata hakujibu. Angejibu nini? Hakuwa na jibu hata la kuzugia muda ule. Wakati wakitazamana kama mbuzi wa kafara, mlio wa hodi ukasikika, kisha mlango ukafunguliwa. Wote wakageuza shingo zao. Wakautazama mlango.

“Kuna mgeni wako Fatu.” Mama yake Fatumata akatumia kichwa kumuonyesha alipo huyo mgeni.

Fatumata na Morena wakatazamana tena. Mama alipoufunga mlango tu, wakasimama kama watu walioambizana na kukimbilia dirishani. Wakaliona gari la mtu wanayemjua fika.

Gari la Kimboka. Mmiliki wa kiroba.

Taharuki nyingine iliwafanya wakaribie kuumeza ulimi wakati wakiyameza mate ya mshtuko. Kwa nini kamfuata kwao, tena pasipo kumpigia simu?

Fatumata alijiuliza. Haikuwa kawaida yao kufuatana namna ile. Alimtazama Morena kama vile alitaka amjibie yale maswali aliyojiuliza kimoyomoyo. Lakini Morena alikuwa bado amesimama pale dirishani, akimkagua Kimboka kwa macho ilhali akiitafuna kwa bidii kucha ya kidole cha shahada.

Alimtazama namna alivyoiminya minya simu yake ya mkononi na kuiweka sikioni. Sekunde tu akaitoa na kuonyesha kufadhaika. Pale mbele ya gari hakutulia, alikwenda kushoto akaenda kulia akarudi kusimama katikati. Alionyesha kuuvaa mfadhaiko.

Fatumata akamvuta Morena ili kumtoa pale dirishani.

“Sasa?” Alimwuliza Morena kana kwamba Morena alikuwa ameisoma akili yake.

“Kuhusu?”

Fatumata alishusha pumzi. Hata maneno ya kujieleza vizuri yalipotelea kusikojulikana. Akamtumbulia macho Morena ambaye naye alimtazama tu. Kisha kama watu waliougutuka wakatoleana macho.

“Simu!” Walitamka kwa pamoja.

Kila mtu akaitafuta simu yake na asiione. Wakakumbuka ule mwendo wa arubii waliotoka nao kule ndani kwa Morena, haukuwapa hata nafasi ya kuchana nywele fakaifa kuzikumbuka simu zao.

Wakapata jibu.

Kimboka alikuwa amemtafuta Fatumata kwa simu na kumkosa na ndiyo maana alikuwa pale. Hakukuwa na ujanja mwingine wa nyongeza zaidi ya kujitokeza tu.

“Akiuliza kuhusu kiroba?” Fatumata alihoji wakati akiufuata mlango.

“Kwani alikuona wakati unakichukua?” Morena alimkunjia uso.

“Sidhani. Sasa kaja kufanya nini?” Fatumata hakujiamini.

“Kama amejua bora umwambie tu ukweli. Hili kasheshe mpaka sasa ni kitendawili, na mteguzi ni yeye. Bora tumwambie tu kama ameshtukia.”

“Kwamba?” Fatumata hakumuelewa.

Muda ule akili ya kuelewa kitu haraka ilikuwa likizo.

“Heri kichane cha shari kuliko mkungu mzima” Morena aliongea akianza kumsukuma mwenzake aende huko aitwako.

Fatumata alitoka barazani. Mikono imelikamata dera lake refu barabara, ili japo lisiburuzike chini lakini pia limsaidie kuficha kule kutetemeka kwa mikono. Alitabasamu akimfuata Kimboka.

Kule ndani Morena aliendelea kuwachungulia.

Walisalimiana. Wivu ukipita kwanza kwa Kimboka kuhoji sababu ya simu zake kutokupokelewa. Fatumata akajitetea na mara kadhaa akiuma midomo yake kwa ndani na kuikakamaza mishipa ya shingo kuutuliza wasiwasi aliokuwa nao.

“Tutoke hapa kuna kitu nataka tuongee.”

Kimboka aliongea kwa msisitizo. Moyo wa Fatumata ulipiga msamba wa hofu.

“Nimetoka kufua mpenzi. Nmechoka. Kwa nini tusiongelee hata chini ya mti pale?” Fatumata alijaribu kukwepa kwenda mbali na pale. Wasiwasi ulimfanya amuogope hata Kimboka.

“Ah! Fatu, sisi ni wa kuongelea chini ya mti? Hebu jikoki kitu cha maana chapchap tusogee mbele hapo.” Kimboka akalikataa wazo la Fatumata na kumuongezea mashaka.

“Nipe dakika tano basi.” Fatumata alijibu akijiondoa pale nje. Alirudi ndani mbio mbio. Alitembea kwa hatua za kupimia shamba.

Chumbani mle, Morena bado alikuwa amesimama dirishani. Alimtazama Kimboka utadhani alitarajia naye angegeuka kuwa kiroba. Aliposikia mlango ukifunguliwa, aligeuka. Alimtazama Fatumata aliyefikia sandukuni na kuchakura chakura akitafuta nguo ya kuvaa.

“Kasemaje?” Morena alimsemesha mwenzake huku akiwa bado ameganda pale pale pembeni ya dirisha.

“Anataka tuongee.” Fatuama alijibu pasipo kugeuka. Alimfanya Morena atoke pale dirishani sasa. Akakifuata kitanda. Akaketi hapo akimtazama Fatumata anavyobadili nguo.

Ukimya ukawapitia.

Dakika tano mbele, Fatumata alikuwa amesimama na kioo dirishani akiihakiki ile poda aliyopaka haraka haraka, na mara kadhaa akitupa jicho kule alikosimama Kimboka.

Pamoja na fadhaa aliyokuwa nayo bado alipata akili ya kujipara kwa kulipua ili kuificha kidogo hali halisi. Hali ya mchachatiko. Akahangaika huku na kule mwisho akatulia na kumtazama rafiki yake.

“Naenda somo! Fanya kuvumilia hapa nikayajue ya uko.” Fatumata alimuaga mwenzake.

Morena hakujibu kitu. Aliishia kuguna. Akamtazama mwenzake alivyoishia.

***Kimenuka!!





Walitoka. Walikwenda kwenye mgahawa uliokuwa umbali mrefu kiasi toka pale kwa Fatumata. Hakukuwa na watu wengi muda huo. Waliokuwepo, walihesabika.

Kimboka aliegesha gari eneo maalumu la maegesho. Hakushuka. Alighairi wazo la kuzungumza huku wakipata staftahi. Alihisi hakuna ambacho kingepita kooni salama hata kwa kujilazimisha pasipo kutoa dukuduku lake kwanza.

Alitulia garini. Aliufyatua mkanda wa kiti. Akajiweka sawa. Kabla ya kuongea, alishusha pumzi iliyoashiria kujiandaa kulitoa la moyoni.

“Fatumata kuna kitu kimetokea mpenzi… Na sijui hata nianzie wapi kukwambia...” Kimboka alitamka taratibu. Akimakinika hasa. Alihakikisha kila neno linamfikia Fatumata ambaye alimkodolea macho mwenzake misuli ya tumbo ikimcheza.

“Kuna kitu kimepotea nyumbani pale.” Aliendelea kuongea.

Fatumata aliukunja uso wake. Moyoni, alijikaza.

“Kwa hiyo unahisi mie ndio nimekichukua?” Alijihami macho yakipepesuka, akijigusa kifuani kwa kidole cha shahada.

“Hapana... Hapana mama! Sijasema wewe ndio umekichukua. Lakini hadi nimekufuata hapa ni kwamba mimi na wewe ndio tumelala mle ndani. Yawezekana ulisikia chochote kinachoweza kunisaidia kujua pa kuanzia.” Kimboka alizungumza pasipo kumtazama Fatumata.

Ikachangia kumpa pumzi za ujasiri mwanamke huyu.

“Mh! Kwanza nini hicho kimepotea?” Fatumata alijifaragua.

“Dah! Sijui naanzia wapi…” Kimboka aliweka mikono yote kichwani akionesha kuhamanika.

“Sema sasa yawezekana naweza kukusaidia.” Fatmata alijifaragua zaidi, pumzi zikimjaa kifuani.

Kwa asilimia mia na zaidi alishapata uhakika kuwa yeye hakuwa mtuhumiwa. Kimboka aliuinamia usukani kama mtu aliyeelemewa na mzigo mzito wa mawazo. Alitulia hivyo kwa sekunde za kutosha mpaka alipokusanya nguvu. Akakiinua kichwa. Akamgeukia mpenzi wake akitikisa kichwa kulia na kushoto.

“Kuna mambo f’lani… unajua tena hizi ishu zangu mpya za machimbo, kuna dawa nilipewa nikanuizie… Sasa kabla hata sijaizika kwenye kazi… Ghafla siioni na masharti yake ilikuwa ndani ya saa 72 niwe nimeizika hiyo dawa.” Alijieleza kwa kigugumizi cha hapa na pale.

“Eeh!” Fatumata alihamanika.

“La sivyo kuna hatari ya kuondoka mimi, au mama yangu, ama wewe!”

“Kuondoka kivipi yaani… nani aondoke? Mimi niondokeje sijaelewa” Fatumata alitaharuki kiasi kwamba alijikuta anazungumza kwa sauti kubwa mithili ya mtu anayehubiria umati.

“Fatu, we’ ni mtu mzima mama, unajua kafara zinavyokuwa. Mpaka nimekwambia nina maana yangu Fatumata kwa sasa nipe hata akili nijue pa kuanzia. Tunusurike mpenzi mengine tutaongea tukishanusuru uhai.” Akatikisa kichwa tena. Akaendelea. “Yaani nikimjua mshenzi anayenipa hii homa ya ghafla nitamkata vidole nivizike na mzigo. Tangu nigundue dawa haipo mle ndani nimeshazunguka nusu ya mji huu kama kichaa!”

Kimboka akamfanya Fatumata amtolee macho zaidi.

Ulimi uling’ang’ania kinywa. Katika vyote alivyopata kufikiria kuhusu kiroba, wazo la kifo kinachomhusu yeye halikupita kichwani kabisa hata kwa bahati mbaya. Hii ilikuwa taarifa mpya kwake, tena yenye kuupeleka mtima wake msobemsobe.

“Si… sasa… kwani… mwe! Mungu wangu!” Fatumata alishindwa hata kupangilia sentensi zake katika mtindo unaoeleweka.

Alihema kwa nguvu kiasi cha kufanya matiti yake yainuke na kifua kila alipohema. Aligundua alichokifanya kilikuwa ni zaidi ya hatari. Zaidi ya kumpigia hodi Izraili!

Misuli ya tumbo ilimcheza dabali.

Simu ya Kimboka iliita. Mwito ukauondoa ule ukimya kati yao. Akaipokea. Alipomaliza kuzungumza simuni, Kimboka alilala upande. Alitoa pochi yake. Alichomoa noti mbili za elfu kumi. Akampatia Fatumata aliyeona taabu hata kuzipokea.

Kichwa kilishavurugwa. Hakutarajia harakati zake zingekuja kutaalaki na mambo ya kishirikina namna hii. Tena, yakawa makubwa kwa kiwango hiki.

“Naenda Temeke kuna mtu nadhani anaweza kunisaidia kujua kilipo… chukua bajaji hapo urudi nyumbani.” Kimboka alimpa maelezo ambayo yalipita sikio la kulia na kutokea kushoto.

“Fatu!” Kimboka alimshtua kwa kumtikisa pajani.

Ile nguvu ya kupiga hatua tu kuzifuata bajaji hakuwa nayo. Alihisi dunia ilikuwa imekwenda mbele kwa kasi ya ajabu na kumuacha nje ya ulimwengu huu.

Aliposhuka garini, alisimama kikuku akiwa kama mbuzi aliyepotezana na wenzake. Aliangaza huku na kule, akizitazama zile bajaji kule kwenye lango la kuingilia hapo mgahawani na wala asizitambue akilini. Alizitazama tu kama urembo akili ikiwa imemruka kwa muda.

Uhai ni mtamu, na hauna kipuri. Alilotenda lilikuwa kama linajiandaa kumrudi.

Alijitumbukiza kwenye kisima alichokichimba mwenyewe! Aliiona tamaa aliyojivika ikimvuka na uhai. Ikimwacha pale aliposimama kama jifu!

Balaa!

***Tena si dogo!



DEREVA teksi, Daudi Chochoro alisimamisha gari lake nje ya nyumba ya Mzee Hizza kwa mara ya tatu. Alisabahiana na wapangaji aliowakuta varandani.

Akamuulizia tena Morena.

“Baba naona leo una ruti za hapa kutwa mara tatu kama dozi ya panado… Hajarudi huyo!” Mwanamke aliyekuwa amesimama na beseni la mihogo kichwani alimjibu.

“Huyo kurudi mpaka kesho baba.” Mwingine aliyekuwa ameupakata ungo wenye mihogo, alitia msisitizo.

Majibu haya yaliupiga mtama moyo wake. Morena hakuwa amerejea tangu alipoondoka. Mzee Daudi alisononeka.

Ni jana tu, wakati alipokuwa akimrudisha Morena hapo kwa Mzee Hizza, tena usiku wa manane wakiwa na kiroba cha almasi, walikubaliana adhuhuri ya siku hiyo apite kuchukua jiwe lake. Asubuhi hiyo akampigia simu Fatumata na kuuulizia mgao wake. Fatumata akamwambia angeenda kuuchukua kwa Morena kama walivyokubaliana. Hivyo, akawa na uhakika mgao wake ulikuwepo.

Na sasa ndiyo hivi, alishachoma mafuta mara tatu kuufuata mgao wake. Alishapiga simu kama opareta na asiwapate wote wawili.

Alilaani akihisi kusumbuliwa na kutumika. Alidamka akiwa na msururu wa mawazo. Alishawaza utatuzi wa mamoja kwa makumi ya shida zake. Akapanga usiku kucha namna ambavyo analala maskini na kuamka tajiri. Kititi! Mipango yote ilikuwa inataka kuyeya kama moshi angani.

Aliiondoa teksi yake akijiapiza kuwashikisha adabu mabinti hawa waliotaka kujifanya wajanja wa mji, baada ya kupata hizo almasi. Alisahau tu ya kuwa mchakacho ujao haulengwi kwa jiwe.

Ilikwishapita saa nzima na vichapo kadhaa. Morena aliuona ule muda wa dakika sitini kama miaka hamsa. Hakutulia, aliingia msalani akatoka. Alikwenda ukumbini akatoka. Akashika hiki akashika kile. Kuna wasaa hata baiskeli ilipokatiza alisimama na kukimbilia dirishani.

Alimngoja Fatumata kuliko anavyomngoja Israfili.

Katika muda ambao hakutarajia, Fatumata alirejea. Alishukia mbali kidogo na asijue kwa nini alishukia mbali kote kule na kujipa adhabu ya kutembea. Alifika kimya kimya.

“Enhe!” Alilakiwa na mwitiko wa bashasha ya kujuzwa.

“Morena!” Fatumata aliita akivua nguo, pengine uzito wa mambo kichwani ulimfanya ajihisi amevaa magome ya miti.

“Kasemaje kwani?” Morena aliuliza akimsindikiza mwenzie kwa macho wakati akitupia nguo zake kitandani na kubaki na nguo za ndani. Alisimama nusu mtupu vile vile akiwa kashika kiuno.

“Mmmh… mmmh!” Aliguna kwa hatua akitikisa kichwa chake kufuatiza ile miguno yake iliyopishana kwa sekunde.

“Dada sema basi, kasemaje Kimboka?” Morena alichoka kusubiri.

Fatumata hakumjibu. Aligeuka. Akaitafuta khanga yake. Akajisitiri kwanza. Kisha, akaketi kitandani akimtazama mwenzake.

“Tumechukua mazindiko ya watu somo!”

“Manini?”

Morena alisogeza uso mbele akimtolea macho mwenzake. Alimsikia, ila hakumwelewa.

“Mazindiko” Alirudia jibu akiwa na hali ya uchovu kupitiliza.

“Hebu nipe a-be-che-de kwanza. Maana naona tu unaongea mie hata moja sina” Morena aliongea akivua fulana aliyokuwa amevaa. Akajipepea.

Mshtuko ulimtekenya makwapa.

“Kasema ndani ya saa sabini na ngapi sijui kiwe kimezikwa, sijui anasema ni dawa za machimbo sijui nini na nini. Mara kisipozikwa sijui mimi na mama yake na watu gani uko tunaondoka.” Fatumata alitupa mikono kiunoni.

Aliongea tu ili mradi sauti inatoka ila mpangilio wa namna ya kuwasilisha taarifa yake ulimgomea.

“Kuondoka? Kuondokaje?”

“Kufa. Kwamba kisipozikwa ndani ya masaa hayo mmoja hapo anawekewa matanga.” Alifafanua akivuta maneno kwa hasira kwa kule kuona Morena anachelewa kumwelewa kwa kila kitu anachoongea.

“Na mie nakufa?” Morena aliuliza safari hii macho yakimtoka nusu yamdondoke

“Sijui shosti! Hapa nahisi kichwa kinavanga vanga, tutoke tu hapa mbio mbio tukapange mipango ya wapi tunakizika usiku huu.” Fatumata alitoa wazo.

“Ungemwambia basi, ungemwambia tu ukweli” Morena alitaka kuleta lawama.

“Ningeanzaje kwanza? Namna alivyoniingia hata pozi la kuungama likapotea. Tuvae ujasiri tu tukizike sie wenyewe.”

Morena aliacha kujipepea, akatikisa kichwa akiwa na mengi kichwani. Vurugu tupu.

“Hili likipita mie utajiri basi.” Morena aliapa.

“Tutoke muda huu tukapange ya kupanga, saa sabini na mbili si kesho kutwa tu hapo!” Fatumata alimhimiza mwenzake yeye akinyanyuka.

Saa kumi na mbili jioni, wakawa wamerudi Vingunguti kwa Morena. Wakapewa ujumbe ya kuwa dereva teksi, Daudi Chochoro alipita hapo kuwaulizia mara tatu.

“Angejua basi yalotukuta maskini, asingechoma mafuta kufukuzia hewa” Fatumata alisikitika.

“Mpigie tu umwambie yaliyomo, tutabeba lawama za bure. Mwambie tu na ikibidi umlete aone vioja vya dunia.” Morena alijibu akionyeshea kidole kile kiroba kilichokuwa pale pale walipokiacha.

Fatumata hakujibu.

Kuna vitu vingi vilipita akilini mwake. Alikumbuka siri ikiingia mtu wa tatu sio siri tena. Ni taarifa. Lakini, ndiyo wafanyeje katika hali kama ile. Maji yalikuwa yanazidi unga.

Jioni ile, Fatumata na Morena walikaza roho wakalishika lile salfeti lenye mchanga na mengineyo na kumimina kila kilichokuwemo juu yake, ndani ya kiroba. Wakakirudishia kama kilivyokuwa wakati walipokiiba. Wakatoka na kuzunguka zunguka maeneo ya mtaani kwao wakitafuta pa kukizika. Mitaa haikuwa salama, kila sehemu waliyodhani ingefaa walikuta mushkeli mbili tatu za kutia mashaka.

Walizunguka sana mpaka kutokea makaburini. Wakasimama hapo wakitazamana kana kwamba waliwaza jambo moja.

“Tukizike hapa?” Fatumata alimwuliza Morena ambaye aliyakodolea macho makaburi akipepesa macho kutafuta eneo ambalo lingefaa.

“Mh! Lakini sasa kukibeba mpaka huku Fatu? Tena usiku mzito… Ndio ghafla tunafumwa makaburini humu. Mtaa utakalika huu? Watu na shida zao watasema sisi ndio vigagula tunaologa watu mtaani.” Morena alieleza wasiwasi wake.

“Haya tutakizika wapi sasa? Maana kila n’nakokuonyesha unatia zohali. Sema basi wewe unafikiria nini?” Fatumata aliongea kwa hasira kidogo. Aliona kama mwenzake mchecheto ulikuwa nyuzi joto sifuri kwa vile maisha yake hayakuwa hatarini.

Morena alimtazama Fatumata kwa jicho pembe. Akamtazama tu kwa sekunde kadhaa akitafuta cha kumwambia na akakosa. Hawakuzungumza tena.

Waligeuza njia kurudi walikotoka. Njia nzima wakiwa kimya mpaka nyumbani. Wakaketi kitandani wakikitazama kile kiroba.

Maji ya shingo!

Magharibi yao ikapita kwa mbinde. Walipanga na kupangua. Walilaumiana na kupeana moyo hadi saa saba usiku, Fatumata alipotoka kuangaza nje kupeleleza usalama. Utulivu aliokuwa anautaka hakuupata kwa wakati alioutaka. Alitoka kwa kunyata akarudi kwa kunyata kama mwizi wa bata.

Saa nane usiku kukawa kumetulia mle ndani. Kidogo iliwapa matumaini kuwa hata nje kungekuwa na utulivu wa kutosha kuikamilishia kazi yao. Walishakubaliana kukizika nyuma ya mtaa kulikokuwa na pagale iliyojengwa na kuishia kati. Ndani ya pagale kulikuwa na kichaka.

Fatumata akajitanda khanga akilificha jembe walilonunua duka la pembejeo jioni ya siku hiyo. Mwili wake mkubwa ukishiriki kulisitiri. Akatoka tena kwa mwendo wa kunyata akichukua tahadhari zote na kutoka salama nje ya nyumba.

Mtaa ulikuwa kimya kiasi. Alizisikia kelele mbili tatu mita kadhaa toka pale alipokuwa. Akawasikia vyura nao wakipokezana kuuharibu utulivu. Krooo krooo! Mbalamwezi ilimmulika kiasi cha kumsisimua. Alikiogopa hata kivuli chake kila alipopiga hatua.

Hofu ilimtambalia mwilini vibaya mno. Akabana pumzi. Alijipa ujasiri wa kuanza kuchapua hatua kuelekea kwenye lile pagale. Kilichomtisha zaidi ni kile alichokuwa anaelekea kukifanya. Wala, si ukimya wa eneo lile. Alimwomba Mungu kila sekunde asikutane na kundi la wahuni yakatokea ya kutokea na kuwaharibia mipango.

Alinyata haraka haraka. Akazunguka nyuma. Alikatiza kile kichochoro kinachopita dirishani kwa Morena. Humo ndani ya pagale, kulikuwa na nyasi za kufikia kiunoni pamoja na mlima mdogo wa takataka. Akainama pembeni ya hizo takataka. Akaanza kuchimba akitafuta sehemu laini zaidi ya kuikwatua.

Alichimba kwa hadhari mno. Mara kadhaa alilazimika kuzibana pumzi kila aliposikia chochote kilichoashiria uwepo wa mtu kupita karibu na pale. Sala zilimtoka kila alipolikita jembe ardhini. Tii! Alikita jembe ardhini. Mungu wangu! Alitamka kuusindikiza mkito. Masikio yakiwa dede kunasa mawimbi ya kilometa mbili toka pale.

Aliporidhika na shimo alilochimba, aliinuka. Akaliacha jembe pembeni.

Alisogea kando. Akaitoa simu yake akiifunika funika kwa khanga ili kuzuia mwanga wa simu usimletee balaa. Akampigia Morena.

Hii ilikuwa ishara yao kuwa shimo lilikuwa tayari na Morena alipaswa kutoka na ule mzigo. Hawakutaka kutoka pamoja wakihofia kukamatwa na kile kifurushi. Ilimpasa mmoja wao kuhakiki mazingira kwanza.

Shughuli ikawa kwa Morena.

Alikinyanyua kile kiroba na uzito wake ukamfanya aongeze nguvu zaidi wakati wa kukipachika begani. Akayumba nacho kidogo akistaajabia ule uzito ambao alihisi umeongezeka. Akabana pumzi na kukiweka sawa begani, akitumia mkono wa kushoto kushikilia eneo la juu la kiroba kilicholala begani na ule mkono wa kulia ukinyonga kitasa.

Alipouvuta mlango ili kuufungua, taa ya koridoni ikawaka na hivyo ikamlazimu kukiachia kitasa na kutulia ili kusikilizia. Alishtuka.

Hatua za mtu aliyevaa kandambili na kutembea akiburuza miguu zikasikika zikielekea mlango mkubwa wa kutokea nje ya nyumba. Morena alijikuta anaurudishia mlango wake taratibu na kukitua kiroba chini. Alirudi nyuma msamba mmoja.

Yule mwenye hatua aliufuata mlango wa kutokea, akamsikia akisemezana na mtu hapo mlangoni. Morena akanyata na kutega sikio lake mlangoni, macho yakiwa yanapepesa gizani.

“Mpaka siku watoto wa mbwa mwitu na panya rodi watuvamie humu ndani ndio tutatia akili, mlango uko wazi kama pango saa nane yote hii.” Alimsikia yule mpangaji mwenzake akiongea kwa sauti huku sauti ya kiume ikimjibu. Akatulia kwa kutaka kuzitambua sauti.

Hakuelewa saa nane ile mwanaume alikuwa akitokea wapi lakini ndiyo vile walikuwa wanauchelewesha mpango wao. Simu yake ikatoa mwanga kitandani, akajua Fatumata alikuwa akimngoja kule nyuma kwenye pagale.

Lakini sasa, angetokaje?

***Pagumu hapo!!


MWISHO


0 comments:

Post a Comment

Blog